Simulizi ya kweli: Niliishi kuzimu siku saba

Simulizi ya kweli: Niliishi kuzimu siku saba

SEHEMU YA 50
ILIPOISHIA:
“Ndiyo,” nilisema kwa kujiamini, akanitazama usoni kisha akaenda mlangoni na kufungua, akawaita Raya na Firyaal, wakaingia ndani na tukakaa tena kama tulivyokuwa tumekaa mwanzo, kazi ikaanza upya huku akinisisitiza kuwa makini na kuishinda hofu ndani ya moyo wangu, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye.
SASA ENDELEA…
Kazi ilianza upya, akatusisitiza kila mmoja awe anavuta pumzi ndefu kwa kutumia tumbo na siyo kifua kama wengi tunavyopumua, pia akatutaka kuhakikisha kila mmoja akili yake aielekeza eneo la tukio.
Muda mfupi baadaye, ile hali ilianza kunitokea tena, nikawa najihisi kama naelea angani huku mwili mwingine ukiwa palepale tulipokuwa tumekaa. Hofu ilianza kunijia tena lakini nilipokumbuka maneno ya yule mwanamke, nilijitahidi kuishinda hofu.
Nikaendelea kutuliza kichwa na kufumba na kufumbua, nilijikuta nikiwa pale hospitalini nilipokuwa nimelazwa. Niliweza kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea, wagonjwa waliokuwa wakiingia na kutoka, manesi na madaktari waliokuwa wakikimbizana huku na kule kuelekea kwenye ukumbi wa mikutano.
Upande wa Kaskazini kulikuwa na magari matatu ya polisi yaliyokuwa yamepaki huku askari wengi wenye silaha wakirandaranda huku na kule.
“Kumetokea nini kwani leo hapa?”
“Nasikia kuna wagonjwa wametoroshwa usiku sasa ndiyo polisi wamekuja kutafuta wahusika.”
“Mh! Yaani wagonjwa kutoroshwa tu ndiyo zije difenda kibao na askari utafikiri kuna vita?”
“Nasikia huyo mgonjwa mmoja ni mtoto wa kigogo mmoja mkubwa ndiyo maana unaona hali ipo hivi,” niliwasikia watu wawili wakihojiana, wakiwa wamesimama chini ya kivuli cha mti.
Ghafla nikasikia vishindo vya mtu akitembea kwa kasi nyuma yangu, nikageuka, katika mazingira ambayo sikutegemea, nilimuona askari mmoja mwenye bunduki, akiwa ananifuata pale nilipokuwa nimesimama, nikajua ameshaniona na kunitambua, nikawa natetemeka.
Cha ajabu, ni kwamba alinipita akiwa ni kama hajaniona na kuwafuata wale watu waliokuwa wakiendelea na majadiliano pale chini ya mti, nikamsikia akiwapa amri kwamba hatakiwi mtu yeyote asiyekuwa na shughuli maalum kuonekana ndani ya hospitali hiyo, akawataka watoke nje ya geti na kwenda nje kabisa.
Kidogo nilishusha pumzi kwani nilikumbuka mara nyingi ninapokuwa kwenye hali kama ile, huwa siwezi kuonekana kwa macho ya kawaida. Harakaharaka nikawa nawafuata wale manesi na madaktari kule walikokuwa wanaelekea kwa lengo la kwenda kuona kinachojadiliwa.
Cha ajabu zaidi, nilipofika kwenye mlango wa kuingilia kwenye ule ukumbi, nilimkuta yule mwanamke, mama yake mdogo Shamila naye akiwa ameshafika, nikamtazama nikiamini yeye hawezi kuniona. Cha ajabu na yeye aligeuka haraka na kunikazia macho, tukawa tunatazamana.
Nilijifunza kitu kingine kwamba kumbe ukiwa katika hali ambayo huwezi kuonekana kwa macho ya kawaida, akija mtu mwingine ambaye naye anakuwa kwenye hali kama yako, mnaweza kuonana vizuri, yaani yeye akakuona na wewe ukamuona ingawa watu wengine wa pembeni wanakua hawana uwezo wa kumuona yeyote kati yenu.
Alinisogelea na kunigusa, kingine cha ajabu ni kwamba nilihisi kabisa kwamba nimeguswa na mtu, akanivutia pembeni na kuanza kuzungumza na mimi kwa sauti ya chini, akaniambia Shamila yuko ndani na amewekwa chini ya ulinzi, amejaribu kumtorosha lakini ameshindwa peke yake, akaniomba tukaunganishe nguvu ili tumtoe haraka iwezekanavyo.
“Sasa tutafanyaje” nilimuuliza huku hofu ikianza kuniingia kwani kwa mbali niliwaona askari wengine wawili wenye silaha wakija, akaniambia tukiingia niwe namfuatisha kila anachokifanya, nikatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye. Akaniminya mkono na kunitazama usoni, akaniambia natakiwa niishinde hofu ndani ya moyo wangu. Nadhani aliniona jinsi nilivyoanza kuingiwa na wasiwasi, nikatingisha tena kichwa.
Pale kwenye geti la kuingilia, alinionesha ishara kwamba tunatakiwa kuingia kinyumenyume, tukafanya hivyo na muda mfupi baadaye tayari tulikuwa ndani. Madaktari na manesi walikuwa tayari wameshakaa kwenye nafasi zao huku wengine wakiendelea kuingia.
Mbele kabisa kulikuwa na meza kuu ambako walikuwa wamekaa watu walioonesha kuwa viongozi wa juu wa hospitali hiyo pamoja na askari aliyekuwa na nyota nyingi mabegani, nadhani alikuwa ni kiongozi wa polisi.
Upande wa kushoto, alikuwa amekaa Shamila huku amezungukwa na askari wawili wa kike, mmoja kila upande. Pembeni kidogo, walikuwa wamekaa wale walinzi tuliowapita getini usiku wakati tukitoroka, ambao nao ilionesha wamewekwa chini ya ulinzi. Tulipita mpaka mbele kabisa huku mtu yeyote akiwa hatuoni.
Akanipa ishara kwamba tunatakiwa kuwazunguka wale askari waliokuwa wamemuweka chini ya ulinzi Shamila mara saba kwa uelekeo tofauti, yaani mimi nianzie kulia kwenda kushoto na yeye kushoto kwenda kulia.
Tulianza kufanya kazi hiyo huku kukiwa hakuna mtu yeyote aliyekuwa akielewa kinachoendelea. Tulizunguka mzunguko wa kwanza, wa pili na hatimaye mizunguko saba ilitimia, akanionesha ishara kwamba inatakiwa tuwaguse vichwani wale askari, kweli tulifanya hivyo.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa kuwaona wale askari wawili wa kike, wote wakishikwa na usingizi wa ghafla, Shamila naye akawageukia mmoja baada ya mwingine, akashangaa akiwa haelewi chochote kinachoendelea.
Wakati hayo yakiendelea, pale meza kuu daktari mmoja alikuwa akizungumza kwa kutumia kipaza sauti, akielezea jinsi tukio la kutoroshwa wagonjwa wawili lilivyofanyika usiku.
Hatukuwa na muda wa kupoteza, alionesha ishara kwamba tukamshike Shamila, mmoja kwenye bega la kushoto na mwingine bega la kulia, tukafanya hivyo kisha akanionesha ishara kwamba akihesabu mpaka tatu, tupige mguu wa kushoto chini kwa nguvu na kufumba macho na nisifumbue mpaka atakaponiambia.
Akaanza kuhesabu, moja! Mbili! Taaatu, nikakanyaga mguu wangu wa kushoto chini kwa nguvu, sawasawa na yeye, mara umeme ukakatika jengo zima, nikafumba macho kama alivyoniambia huku nikiwa nimemshikilia Shamila kwa nguvu, nikahisi kama tumezolewa na kimbunga chenye nguvu kubwa.
“Fumbua macho,” alisema, nilipofumbua macho, sikuamini nilichokiona. Tulikuwa tumerejea ndani ya kile chumba tulichokuwemo mwanzo lakini tofauti na awali, safari hii kila mmoja alikuwa amelala sakafuni, kuanzia mimi, yule mwanamke, Raya na Firyaal huku akiwa ameongezeka mtu mwingine kati yetu, Shamila.
Bado wale wenzetu wote walikuwa kama wamepitiwa na usingizi mzito isipokuwa mimi na yule mwanamke pekee, nikajivutavuta na kuinuka pale nilipokuwa nimelala, nikashangaa mwili wangu ukiwa umechoka kupita kiasi huku viungo vyote vikiniuma.
Yule mwanamke naye aliinuka na kukaa kwa kujiegemeza ukutani, naye akionesha kuchoka kuliko kawaida.
“Kweli wewe ni mwanaume wa shoka, njoo nikupongeze,” alisema kwa sauti ya kichovu, nikajikokota na kusimama, nikasogea mpaka pale alipokuwa amekaa, akanionesha ishara kwamba nikae chini pembeni yake, nikafanya hivyo huku sote macho yetu yakiwa kwa Shamila.
“Sikuwahi kudhani kwamba unaweza kuwa na nguvu kubwa kiasi hicho, hongera sana, utanifaa sana wewe,” alisema huku akipitisha mkono wake mmoja begani kwangu kichovu kisha akanigeukia, tukawa tunatazamana. Katika hali ambayo sikuitegemea hata kidogo, nilishangaa yule mwanamke akinibusu, tena mdomoni, nikashtuka mno.
“Hongera sana, ila inabidi upunguze mambo ya wanawake, utakuwa na nguvu zaidi ya hizi ulizonazo,” aliniambia huku akinitazama usoni.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue
 
SEHEMU YA 51

ILIPOISHIA:
“Sikuwahi kudhani kwamba unaweza kuwa na nguvu kubwa kiasi hicho, hongera sana, utanifaa sana wewe,” alisema huku akipitisha mkono wake mmoja begani kwangu kichovu kisha akanigeukia, tukawa tunatazamana. Katika hali ambayo sikuitegemea hata kidogo, nilishangaa yule mwanamke akinibusu, tena mdomoni, nikashtuka mno.
“Hongera sana, ila inabidi upunguze mambo ya wanawake, utakuwa na nguvu zaidi ya hizi ulizonazo,” aliniambia huku akinitazama usoni.
SASA ENDELEA…
“Sijakuelewa,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kukaa vizuri pale juu ya zulia. Bado si Raya, Shamila wala Firyaal waliokuwa wamezinduka.
“Utanielewa tu,” inabidi kwanza tukaoge kuondoa uchovu halafu tuwasaidie na hawa nao warudi kwenye hali yao ya kawaida, tuna kazi nyingine ya kumsaidia Shenaiza, ni lazima arudiwe na fahamu zake, tena ikiwezekana haraka iwezekanavyo,” alisema mwanamke huyo kisha akapiga miayo mfululizo na kujinyoosha.
“Kwa kawaida, kila binadamu huwa anazalisha nguvu, nadhani hilo nilishakueleza kutoka mwanzo ingawa ni wachache sana wanaolitambua hili.
“Yaani ni kama kupepesa kope, unajua ni mpaka mtu akukumbushe kwamba muda wote macho yako yanapepesa kope ndiyo unakumbuka?” alisema, nikawa sioni chochote kipya kwenye mazungumzo yake kwa sababu ni jambo ambalo nilikuwa nimeshalisikia sana maishani mwangu kwamba kila binadamu anazalisha nguvu zisizoonekana.
“Nguvu tunazozalisha huwa zinatengeneza kitu kinachoitwa aura ambacho wengine huwa wanakiita ni mwili usioonekana juu ya mwili unaoonekana. Sasa kwa mtu mwenye utambuzi wa nguvu hizi, anao uwezo wa kuuona mwili huu.
“Kwa mtu ambaye anaishi maisha ya kitakatifu, yaani hanywi pombe, havuti sigara, hafanyi zinaa, hawasemi vibaya watu wengine, hana wivu wala kinyongo, ana upendo wa dhati kwa watu wote na ambaye moyo wake uko safi, hii aura huwa na kawaida ya kung’aa sana. Mtu akikutazama tu anaiona nguvu inayokuzunguka.
“Lakini vilevile kama mtu anaishi maisha ya hovyo, pengine ni mlevi sana, anafanya ngono hovyohovyo, ana wivu, hasira, vinyongo na tabia mbayambaya, kwa kawaida huwa aura yake inafifia sana na kama una utambuzi wa nguvu hizi, ukimtazama tu unamjua ndiyo maana nilikwambia vile,” alisema yule mwanamke na kuzidi kunishangaza.
Kitu alichokisema sikuwa nimewahi kukisikia sehemu yoyote, nikabaki nimepigwa na butwaa, akaendelea:
“Japokuwa watu wengi huwa hawaelewi kuhusu aura kwa hiyo hawajui umuhimu wa kuishi kitakatifu hata kama huna dini, siyo kitu cha mchezomchezo. Aura ya mtu huanza kuishi kabla mtu hajazaliwa na huendelea pia mpaka mtu anapokufa. Ndiyo maana mtoto anapokaribia kuzaliwa, tafiti zinaonesha kwamba huwa ana uwezo wa kuelewa kinachoendelea kwenye ulimwengu wa nje.
“Hii ni kwa sababu tayari mwili wake ambao hauonekani unakuwa umeshaingia kwenye ulimwengu wa kawaida. Akishazaliwa, huwa inatakiwa mwili wake halisi uungane na hii aura na hiyo hufanyika katika kipindi cha siku arobaini tangu mtoto azaliwe ndiyo maana kuna tamaduni nyingi kwamba mtoto anatakiwa kuanza kutolewa nje baada ya siku arobaini kwani pale inakuwa tayari aura yake na mwili halisi vinakuwa vimeungana hivyo anakuwa na kinga dhidi ya mambo mabaya yasiyoonekana kwenye ulimwengu wa kaiwada.
“Hiyo pia hutokea pale mtu anapokufa ambapo nafsi inapotengana na mwili, aura huwa inaendelea kuishi mpaka baada ya siku arobaini ndiyo nayo hutoweka, ndiyo maana pia huwa kuna tamaduni za kufanya arobaini ya marehemu kwani pale ndiyo uhai huwa unakuwa umefikia mwisho.”
Maelezo hayo yalinifanya nikune kichwa kwani siyo siri yalikuwa yamenichanganya sana akili. Ni mambo ambayo sikuwahi kuyasikia kabla lakini kwa jinsi alivyokuwa akiyafafanua, ilionesha dhahiri kwamba ni kweli. Hata mimi sikuwahi kupata jibu la kwa nini mtoto anatakiwa atolewe nje baada ya siku arobaini tangu azaliwe na kwa nini mtu akifa, msiba huwa unahitimishwa baada ya siku arobaini.
“Lakini mamdogo…”
“Usiniite mamdogo, ningependa zaidi uniite kwa jina langu halisi ambalo ni watu wachache huwa wanalijua. Nina majina mengi lakini jina langu halisi ni Junaitha,” alisema huku akiinuka pale alipokuwa amekaa.
“Hakuna cha lakini… punguza wanawake ili aura yako ing’ae na kukuongezea nguvu, mimi sijui nina mwaka wa ngapi simjui mwanaume,” alisema huku tayari akiwa amesimama, akanipa mkono kama ishara ya kutaka anisaidie kuinuka.
Nilibaki kumtazama tu usoni, mambo mengi yalikuwa yakipita ndani ya kichwa changu.
“Mbona unanitumbulia macho? Amka twende ukaoge, bado kuna kazi kubwa leo,” alisema yule mwanamke, nikampa mkono, akanishika na kunivuta kidogo, nikasimama.
“Halafu inatakiwa pia uwe makini na vyakula unavyokula, inaonesha mwili wako hauna uzito unaotakiwa, hata hao wanawake unaotembea nao hovyo huwa unawaridhisha kweli? Wanaume wa siku hizi wana tatizo kubwa la upungufu wa nguvu za kiume, na wewe usije kuwa miongoni mwao,” alisema huku akitabasamu.
Japokuwa mwenyewe alichukulia kama masihara lakini kwa hulka za kiume, niliona kama amenidharau sana. Maneno yake ni kama yalikuwa yakihitaji nifanye kitu fulani kumthibitishia kwamba sikuwa mtu wa mchezomchezo bali mwanaume niliyekamilika.
Nilipounganisha na tukio la yeye kunibusu kwenye midomo yangu wakati akinipongeza, akili nyingine zilianza kupita ndani ya kichwa changu.
“Kwa hiyo unaishije bila mume?”
“Kwani wewe unapata faida gani kubadilishabadilisha wanawake?” aliniuliza swali juu ya swali ambalo lilinifanya nijiulize sana kwa nini alikuwa akinikomalia kuhusu suala la mimi kuwa na wanawake wengi. Elimu aliyonipa ilikuwa imetosha kunifanya nijitambue lakini kwa nini alikuwa akiendelea kuulizauliza kuhusu mimi kuwa na wanawake? Sikupata majibu.
“Mbona unakuwa mkali sana kwangu Junaitha? Au kuna kitu nimekuudhi?”
“Ndiyo umeniudhi, kwa nini kijana mtanashati kama wewe usitafute mwanamke mmoja tu anayejitambua ukatulia naye?” nilijikuta nikishindwa kujizuia, nikaangua kicheko kwani tayari nilishaanza kupata picha ya kilichokuwa kikiendelea ndani ya kichwa chake.
“Kwa hiyo unanidharau si ndiyo? Yaani mi naongea mambo ya maana wewe unacheka,” alisema, akatoka na kuniacha nimesimama palepale, nikiwaangalia wale waliokuwa wamelala juu ya zulia, kila mmoja akiwa hajitambui kwa uchovu.
“Hebu njoo huku,” nilisikia sauti ya Junaitha ikitokea chumbani kwake, harakaharaka nikatoka pale na kuelekea kule sauti ilikokuwa inatokea.
“Ingia tu mlango upo wazi,” alisema, nikageuka huku na kule kwanza kwa sababu sikuona kama ni heshima kwa mtoto wa kiume kuingia chumbani kwake, hasa ukizingatia ukweli kwamba alikuwa amenizidi sana umri. Nikapiga moyo konde na kuingia ndani ya chumba hicho cha kisasa kilichokuwa na vitu vingi vya thamani.
“Chukua taulo pale kabatini ingia bafuni ukaoge,” alisema akiwa amekaa juu ya kitanda kikubwa cha kisasa akihangaika kufungua zipu ya gauni alilokuwa amevaa, nikaelekea pale kwenye kabati aliponielekeza, nikachukua taulo na kuanza kuelekea kwenye lile bafu la ndani kwa ndani kule chumbani kwake.
Nililazimika kuingia na nguo zote bafuni kwani nilikuwa naona aibu kuvua hata shati mbele ya macho yake.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
 
SEHEMU YA 52


ILIPOISHIA:
“Chukua taulo pale kabatini ingia bafuni ukaoge,” alisema akiwa amekaa juu ya kitanda kikubwa cha kisasa akihangaika kufungua zipu ya gauni alilokuwa amevaa, nikaelekea pale kwenye kabati aliponielekeza, nikachukua taulo na kuanza kuelekea kwenye lile bafu la ndani kwa ndani kule chumbani kwake.
Nililazimika kuingia na nguo zote bafuni kwani nilikuwa naona aibu kuvua hata shati mbele ya macho yake.
SASA ENDELEA...
“Sasa utaingiaje bafuni na nguo? Hebu toa ushamba wako hapa,” alisema Junaitha huku akicheka, nikajikuta nikiwa kwenye wakati mgumu sana. Japokuwa nilikuwa nimeshaingia, ilibidi nitoke, nikajikaza kisabuni na kuvua fulana niliyokuwa nimeivaa, bandeji iliyofungwa juu ya jeraha langu ikaonekana vizuri.
“Mh! Kumbe uliumia kiasi hicho, hebu njoo nikuangalie,” alisema, nikavungavunga kwa aibu mwishowe nikasogea mpaka pale kitandani alipokuwa amekaa. Akanisogelea na kuanza kunitazama vizuri pale kifuani.
“Unajisikiaje kwani?” aliniuliza huku akiligusa jeraha langu kwa juujuu.
“Sasa hivi nina afadhali kubwa,” nilimjibu, akaendelea kulitazama jeraha hilo kwa muda kisha akaniambia nisiwe na wasiwasi, kuna dawa atanipaka ambayo itanifanya nipone haraka kuliko kawaida, niliitikia kwa kutingisha kichwa.
“Halafu mbona kama unaniogopa? Kwani nina tofauti gani na hao wanawake zako unaotoka nao? Au unaniona mimi mzee?” alisema huku mkono wake mmoja akiwa amenishika shingoni kwa upole. Kiukweli nilikuwa najisikia aibu sana kiasi kwamba sikuweza hata kumtazama usoni.
“Haya malizia kuvua nguo zako ukaoge na mimi nataka kuoga,” alisema huku akiniachia, nikashusha pumzi ndefu na kusogea pembeni ambapo niligeukia pembeni, nikalifunga lile taulo juu ya suruali kisha nikavua juu kwa juu, nikamsikia akiangua kicheko kutokana na ujanja nilioutumia.
“Mbona mimi sijishtukii kama wewe? Hebu niangalie,” alisema, nikageuka na kumtazama, nikamuona akilishusha gauni lake kwa maringo ya kikekike, macho yangu yakatua kwenye kifua chake, japokuwa alikuwa mtu mzima, alikuwa na kifua kama kigori. ‘Braa’ ya rangi ya zambarau iliyahifadhi vizuri maembe bolibo mawili yaliyokuwa yamejaa vizuri kama mtu ambaye hajawahi hata kuwa na mtoto.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilimuona akimalizia kulitoa gauni lake lote, nilichokiona kilinifanya nipoteze ‘network’ kwa sekunde kadhaa, akaifungua na ile ‘braa’ aliyokuwa ameivaa, akabakia na nguo ya mwisho tu, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida, nikameza funda la mate kama fisi aliyeona mfupa.
Japokuwa kwa nje alikuwa akionekana kama mtu mzima flani hivi, ndani Junaitha alikuwa tofauti kabisa, kwa makusudi kabisa akageuka kama anayetafuta kitu fulani, macho yangu yakatua kwenye mlima mkubwa uliokuwa upande wa nyuma, nikashusha pumzi ndefu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka.
Ni kama alishaona kwamba ndege mjanja nimenasa kwenye tundu bovu kwani alisimama na kuanza kutembea kama wanamitindo wanavyotembea jukwaani, akanisogelea mpaka pale nilipokuwa nimesimama, akaipitisha mikono yake nyuma ya shingo yangu, tukagusanisha ndimi huku mikono yangu ikiwa bado haijui ishike wapi.
“Sitaki uniogope, mimi ndiyo mtu sahihi unayepaswa kuwa naye, nitakulinda na kukuepusha na matatizo yote unayoweza kuyapata kwa kubadili wanawake ovyo,” alisema kwa sauti ya kunong’ona, mdomo wake ukiwa sentimita chache kutoka kwenye sikio langu, sauti yake ikapenya hadi kwenye ngoma zangu na kuniongezea msisimko wa kipekee.
Nikajikuta mikono yangu imeenda kushikilia mlima wake, nikashtushwa na jinsi alivyokuwa na ngozi laini, nikamuona naye akishtuka kidogo kisha akaachia tabasamu pana, akaniachia shingoni na kunishika mkono, akawa ananivuta kama kondoo anayepelekwa machinjioni, nikawa namfuata, safari yetu ikaishia kwenye kitanda kikubwa cha kifahari.
Sikuelewa kilichoendelea mpaka nilipokuja kushtuka muda mfupi baadaye na kujikuta nikiwa kama nilivyokuja duniani, naye akiwa katika hali hiyohiyo, ‘Jamal’ wangu akiwa amechachamaa kupita kawaida. Kilichoendelea baada ya hapo, ilikuwa ni ‘experience’ nyingine mpya kabisa maishani mwangu.
Waliosema usidharau kitabu kwa kutazama kava lake hawakukosea, japokuwa kwa mwonekano Junaitha alikuwa akionekana mtu mzima flani hivi, alikuwa ‘fit’ mno, mpaka chombo kinatia nanga kwenye bahari ya huba kuashiria kufika mwisho wa safari, nilikuwa sijitambui, ukichanganya na ule uchovu wa kazi ya kumuokoa Shamila, nilijikuta nikipitiwa na usingizi mzito ambao nikiri kuwa sijawahi kuupata tangu nizaliwe.
Nilikuja kuzinduka baadaye na kujikuta nikiwa nimelala juu ya kitanda kilichotandikwa shuka jeupe na juu yake karatasi laini la nailoni, nikiwa nimefungwa taulo kubwa jeupe huku Junaitha naye akiwa amevaa nguo kama ya kulalia hivi, yenye rangi nyeupe.
Nilitaka kuinuka lakini akaniwahi na kunituliza, akaniambia ananisafisha kidonda changu na kunipaka dawa kama alivyoniambia, nikatulia. Nilimuona akichanganya dawa fulani kama mafuta hivi, akaja kuinyunyiza juu ya ile bandeji, muda mfupi baadaye akaitoa taratibu. Wala sikuhisi maumivu yoyote kama ilivyokuwa hospitali au wakati Shamila akinisaidia.
“Ungechelewa sana kupona kwa dawa za hospitali, inaonekana hili jeraha lilimaanishwa kuyakatisha maisha yako,” alisema huku akinimwagia dawa nyingine juu ya jeraha langu na kuanza kunichua taratibu, nikakosa cha kujibu zaidi ya kuwa namtazama tu usoni, kumbukumbu za yote yaliyotokea zikirudi kwa kasi kichwani mwangu.
“Nisamehe kwa kutangulia kukudharau, kumbe wewe siyo wa mchezomchezo,” alisema Junaitha, nikaachia tabasamu pana, aliendelea kunitibu lile jeraha na baada ya muda, aliniambia niinuke.
“Mbona hunifungi bandeji?” nilimuuliza huku nikijitazama pale kifuani.
“Wala hakuna haja, kitapona chenyewe, nakupa siku mbili tu lazima kiwe kimekauka ila inabidi upate muda wa kutosha wa kupumzika,” alisema, akaniongoza mpaka bafuni ambako kwa umakini mkubwa aliniogesha kama mtoto mdogo huku akizingatia maji yasiguse jeraha langu.
“Wameshaamka?”
“Ndiyo, ila ilibidi niwadanganye kwamba ulizidiwa tukiwa kule kwenye kazi kwa hiyo ndiyo nipo kukutibu, nakuomba sana uitunze hii siri, si unajua Shamila mimi ni mwanangu japokuwa sijamzaa mwenyewe, akijua itakuwa fedheha sana kwangu,” aliniambia, nikamtoa wasiwasi huku nikitaka kujua kwa nini tendo la mimi na yeye lilikuwa tofauti sana?
“Ni kama nguvu chanya na chanya zimekutana, hata mimi kuna mambo yamenitokea ambayo hayajawahi kunitokea tangu nipate akili zangu,” alisema Junaitha huku safari hii yeye ndiyo akiwa ananionea aibu, akishindwa hata kunitazama usoni mara mbili.
“Wewe ni mwanaume wa shoka,” alisema huku akinibusu kwenye paji la uso wangu, tukarudi chumbani ambapo nilivaa nguo zangu, akanishika mkono na kuniambia natakiwa ‘kuekti’ kama nasikia maumivu makali, akanitoa mpaka sebuleni ambako niliwakuta Shamila, Firyaal na Raya wakiwa wanatazama runinga kubwa ya ukutani.
Waliponiona tu, wote waliinuka haraka na kunikimbilia, kila mmoja akitaka awe wa kwanza kunifikia, nikamuona Junaitha akinitazama kwa macho yaliyoonesha kuwa na viulizo vingi, akawawahi:
“Bado hajapona, msimkumbatie kwa nguvu mtamtonesha!” Nikaona wote wameishiwa pozi, wakaishia kunishika mikono tu huku wakinitazama usoni, kila mmoja alionesha kuguswa mno na hali yangu, hakuna aliyekuwa anajua kwamba nilikuwa ‘nikiwaektia’, Junaitha ambaye pale ndiyo alikuwa mkubwa kuliko sisi wote, akawa ananitazama kama anayenisisitiza nisije nikaharibu.
Nikaenda kukaa kwenye sofa la peke yangu, wote wakanipa pole na nikawahakikishia kwamba nitakuwa sawa. Tukaanza kuulizana maana ya kile kilichofanyika mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila ambapo Junaitha alianza kutufundisha mambo ambayo hakuna aliyekuwa akiyajua kati yetu, ambayo kama hujui ungeweza kusema ni uchawi wa hali ya juu.
“Hata ukitaka kuingia benki na kuchukua kiwango chochote cha fedha unachotaka, inawezekana, mbona rahisi tu, nitawafundisha,” alisema.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 53


ILIPOISHIA:
Tukaanza kuulizana maana ya kile kilichofanyika mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila ambapo Junaitha alianza kutufundisha mambo ambayo hakuna aliyekuwa akiyajua kati yetu, ambayo kama hujui ungeweza kusema ni uchawi wa hali ya juu.
“Hata ukitaka kuingia benki na kuchukua kiwango chochote cha fedha unachotaka, inawezekana, mbona rahisi tu, nitawafundisha,” alisema.
SASA ENDELEA...
“Mh!” niliguna kama ishara ya kutoamini kile alichokisema, akanigeukia na kuniambia hakuna kitu kisichowezekana chini ya jua. Alianza kutufafanulia jinsi nguvu zisizoonekana kwa macho zilivyo na uwezo wa kufanya chochote na kikatimia.
“Hujawahi kuona mtu anakunja kijiko kwa kukitazama tu au mtu anahamisha glasi ya maji kwa kuitazama tu?” alisema. Nilishawahi kusikia habari hizo lakini sikutaka kabisa kuziamini mpaka nishuhudie mwenyewe.
“Kabla ya yote nataka kujua nini kilichotokea mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila?” niliuliza, nikamgeukia Shamila ambaye muda wote alikuwa kimya kabisa, akionesha bado kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
“Eti kwani wewe ulihisi nini wakati tumekuja kukuokoa?”
“Yaani hata sielewi kilichotokea, nakumbuka nilikuwa nimewekwa chini ya ulinzi, tena mambo yakiwa yamenikalia kooni kwelikweli kwa sababu jambo la kwanza nilitakiwa kulipa bili za matibabu za wewe na Shenaiza ambazo kimsingi ni kubwa sana kisha baada ya hapo ndiyo taratibu za kisheria zingefuatia.
“Nilishaanza kuwasikia wakisema kwamba kwa jinsi tukio lenyewe lilivyokuwa limenikalia vibaya, ningeenda kufungwa, tena si kifungo cha chini ya miaka saba,” alisema Shamila, akaendelea:
“Nikiwa nimekaa pale ndani ghafla nikaanza kuhisi kama upepo hivi unavuma, mara wale askari waliokuwa wakinilinda wakapitiwa na usingizi mzito na kufumba na kufumbua, nilishangaa nikisombwa na kimbunga kikali na sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipozinduka na kujikuta humu ndani. Kwani ilikuwaje?” Shamila naye alinigeuzia mimi swali.
“Labda tumuulize mama mdogo,” na mimi nililikwepa swali, wote tukamgeukia Junaitha ambaye alishusha pumzi ndefu kisha akatuambia hawezi kueleza kilichotokea kwa maneno machache tukamuelewa, tunahitaji kukaa darasani na kupata muda wa kutosha kujifunza.
“Ila kwa kifupi kilichotokea ni uthibitisho wa jinsi kila mmoja wetu hapa alivyo na nguvu kubwa ndani yake ambayo iwe anajua au hajui, ina uwezo wa kufanya mambo makubwa sana. Na tukiunganisha nguvu hiyo ndiyo tunaweza kufanya mambo makubwa yakautingisha ulimwengu wote.
“Ukishajua kucheza na nguvu hizi unao uwezo hata wa kwenda kuzimu na kurudi, yaani roho ikatengana na mwili kabisa na kila mmoja akaamini kwamba umekufa kisha baada ya muda ukazinduka tena na kuwa hai,” alisema Junaitha huku akinitazama, nikajua alikuwa akinilenga mimi jambo fulani ingawa sikuwa na uhakika.
“Hayo tutaendelea nayo baadaye lakini niwape onyo, kama kuna yeyote anayeshiriki mapenzi nje ya ndoa aache kwa sababu hiyo ni sumu kubwa sana katika udhibiti wa nguvu za ndani na najua hakuna aliyeoa au kuolewa kati yenu. Tuna kazi ya kumzindua Shenaiza kwa hiyo lazima kila mmoja ajitahidi mwili wake kuwa msafi vinginevyo hakuna kitakachofanyika,” alisema Junaitha.
Akilini mwangu nilielewa kwa nini ameyasema maneno hayo, ndani ya kichwa chake alishahisi kwamba miongoni mwa wale wasichana lazima kuna ambaye natoka naye kimapenzi na kwa sababu tayari nilishamuonjesha asali, alikuwa tayari kuchonga mzinga ila hakutaka mtu mwingine yeyote aendelee kuchangia naye.
Aliposema hivyo niliwaona wote watatu, Shamila, Raya na Firyaal wakinitazama kwa macho ya chinichini kama wanaosema ‘potelea mbali’. Alituchukua wote na kutupeleka kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza akiwa hana fahamu.
“Roho yake imekwenda mbali kabisa na mwili, tunatakiwa kuivuta mpaka irudi mahali pake na hilo likifanyika tu, atazinduka. Tutakuwa na kazi kubwa kwa sababu licha ya kuwa roho yake imekwenda mbali, pia nguvu za ubongo wake zimevurugwa na madawa makali aliyokuwa anachomwa kule hospitalini, haitakuwa kazi nyepesi,” alisema Junaitha kwa msisitizo.
Wote tukawa kimya kabisa tukisubiri maelekezo yake, akatuambia kwamba itabidi wenye nguvu kati yetu ndiyo watoke kuifuata roho yake mahali ilipo na wale wengine wajazie nguvu zao kwetu.
“Narudia tena, haitakuwa kazi nyepesi na pengine tutachoka kuliko hata ilivyokuwa mwanzo,” alisema, sote tukashusha pumzi ndefu na kuendelea kumsikiliza. Akatuambia kabla ya yote, kila mmoja anatakiwa kwenda kuoga kwa maji mengi na kuhakikisha amevaa nguo safi, akatuambia kama hatukuwa na nguo safi tusijali atatupa mavazi maalum ambayo huwa anayatumia kwenye shughuli kama hizo.
“Shughuli kama hizi? Zipi?”
“Za kusaidia watu wenye matatizo kama wewe,” alijibu Junaitha huku akinitazama kwa macho ambayo yalimaanisha yupo kikazi zaidi. Kwa kututazama, usingeweza kuamini kwamba ndiyo sisi ambao muda mfupi uliopita tulikuwa tukisakata kabumbu kwenye uwanja wa fundi seremala. Tofauti na wanawake wengine, Junaitha alionesha kuwa na uwezo mkubwa wa kuzimudu vyema hisia zake.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, harakaharaka tulienda kuoga, kwa kuwa karibu kila chumba kilikuwa na bafu la ndani, muda mfupi tu baadaye tayari wote tulikuwa tumeshaoga, ingawa ilibidi mimi nijitenge peke yangu ili kuzuia mtafaruku unaoweza kutokea.
Muda mfupi baadaye wote tulikuwa tumevalia mavazi maalum kama yale yanayotumika kwenye hoteli kubwakubwa kwa ajili ya kulalia, yote yakiwa na rangi nyeupe.
“Hamuoni mmependeza?” alisema Junaitha, wote tukacheka, tukarudi kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza. Ilibidi tusaidiane kumshusha kutoka pale kitandani mpaka chini kwenye jamvi, kisha na sisi tukakaa mkao maalum wa kukunja miguu na kutengeneza duara kumzunguka Shenaiza ambaye hakuwa akielewa chochote.
“Tunafanya kama tulivyofanya wakati wa kumuokoa Shamila,” alisema Junaitha, kwa sababu wote tulikuwa tunakumbuka tulichokifanya, tulishikana mikono na kufumba macho, kila mmoja akaanza kuvuta hewa kwa utaratibu maalum na kuiachia, haikuchukua muda eneo lote likatawaliwa na utulivu wa hali ya juu.
Ile hali ilianza tena kunirudia kama mwanzo, nikaanza kuhisi kama napaa huku nikishuhudia jinsi mwili wangu usioonekana ulivyokuwa ukiachana na huu unaoonekana. Tofauti na mwanzo ambapo nilikuwa nahisi hofu kubwa ndani ya moyo wangu, safari hii nilikuwa najisikia ku-relax sana.
Kuna muda nilitamani hata maisha yangu ya kila siku niwe kwenye ulimwengu huo mwingine. Hata hivyo, hali niliyokuwa naisikia ilikuwa ya muda, ghafla nikaanza kuhisi mtikisiko mkubwa, ukasikika mlio mkali wa radi na mandhari yakabadilika hapohapo.
Kelele za vyuma vingi vilivyokuwa vikigongana, pamoja na muungurumo wa kutisha sambamba na moshi mwingi mweusi unaopalia kooni vikanizingira kila upande.
“Mbona kama nimewahi kufika kwenye haya mazingira?” niliwaza lakini cha ajabu nikasikia sauti ya kile nilichokuwa nakiwaza ikijirudia kama mwangwi mkali, nikajua kazi imeanza.
Nilipogeuka huku na kule, nilijikuta nimekaa kwenye kiti cha chuma kilichokuwa na kutu nyingi, nikageuka tena na kutazama huku na kule, nikagundua kwamba nipo kwenye lile treni ambalo siku ile nilipojeruhiwa na kupoteza fahamu kisha kuhamia kwenye ulimwengu mwingine, nililipanda.
Kwa mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo usingizini. Kasi ya treni ilizidi kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga mbele, milio ya ajabu ilianza kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa treni lile la ajabu, na giza totoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 54


ILIPOISHIA:
Kwa mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo usingizini. Kasi ya treni ilizidi kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga mbele, milio ya ajabu ilianza kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa treni lile la ajabu, na giza totoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
SASA ENDELEA...
“Poooh! Pooh!” honi kali ya treni ilisikika ikifuatiwa na msuguano mkali wa vyuma, nikaona watu wote waliokuwa mle ndani ya treni la ajabu wakirushwa upande wa mbele. Nilijishikilia kwa nguvu, treni likajisugua juu ya reli na kusababisha cheche nyingi ziruke, eneo lote likawa kama karakana ya kutengenezea vifaa vya chuma.
Treni liliposimama, nilishtukia nimeshashuka, hata sikumbuki nilipitia mlango gani, macho yangu yakatua kwenye kitu kilichosababisha treni hiyo ifunge breki za ghafla kiasi kile. Msichana mmoja, aliyekuwa na macho yanayong’ara kama paka awapo gizani, nywele ndefu zilizokosa matunzo na kucha kama mnyama wa porini alikuwa amekaa katikati ya reli huku akinguruma kama mnyama wa kutisha.
Sijui nilipata wapi ujasiri wa kumsogelea, kadiri nilivyokuwa nasogea mbele ndivyo msichana yule alivyozidi kutoa mlio wa kunguruma na kusababisha nipatwe na hofu kubwa mwilini. Lakini cha ajabu, eti muda huohuo nilikuwa nasikia sauti ya Junaitha ikiniambia napaswa kuishinda hofu yangu, nikazidi kumsogelea.
Kwa msaada wa taa moja kubwa iliyokuwa mbele ya lile treni, kufumba na kufumbua, nilishangaa yule niliyekuwa namuona kama msichana akibadilika na kuwa jibwa lenye meno na kucha ndefu, likaanza kubweka kwa nguvu huku likitokwa na mate mengi mdomoni.
Kiukweli nafsi yangu ilielemewa na hofu lakini eti cha ajabu sauti ya Junaitha ikawa inaendelea kusikika ndani ya moyo wangu ikiniambia sipaswi kuogopa chochote, nikapiga hatua moja mbele na sasa tukawa tumekaribiana sana na jibwa hilo ambalo lilikuwa likiendelea kubweka kwa hasira lakini lilipoona sishtuki, liligeuka na kuanza kutimua mbio huku likiendelea kubweka.
Nikasikia sauti ikiniambia nianze kulifukuza jibwa lile, bila hata kuuliza nikaanza kukimbia kuelekea kule lilikokimbilia, huku nyuma nikasikia lile treni likianza kunguruma tena kwa kasi, moshi mwingi ukatanda eneo lote kisha likaanza kuondoka.
Nilifunga breki za ghafla na kugeuka nyuma, nilishindwa kuelewa kama lile treni linaondoka mimi nitaondokaje kwenye mazingira yale ambayo kwanza sikuwa najua ni wapi halafu yalikuwa yakitisha sana?
“Mkimbize Jamal, utakosa vyote,” ilisikika sauti ya Junaitha, nikaachana na treni hilo na kuanza kutimua mbio, lile jibwa lilikuwa likikimbia na kufika mbali kidogo, linasimama na kugeuka kunitazama, likawa linaendelea kubweka kwa nguvu na likiniona nakuja, linaanza tena kukimbia.
Japokuwa kulikuwa na giza nene, niliweza kuyatambua mazingira hayo kuwa ilikuwa ni katikati ya msitu mkubwa wenye miti iliyofungana kwani hata nilipojaribu kutazama juu, sikuona mwezi wala nyota, kila sehemu kulikuwa na giza. Kilichosaidia niweze kuelewa jibwa lile lilikokimbilia, ilikuwa ni mwanga wa macho ya lile jibwa, ambayo sasa yalikuwa yaking’aa sana.
Niliendelea kukimbia, mara nikajikuta nimetokezea sehemu iliyokuwa na majimaji, nikawa kila nikipiga hatua nakanyaga kwenye matope, sikupunguza mwendo, niliendelea kutimua mbio, nikawa najikwaa kwenye visiki, wakati mwingine nakanyaga miiba lakini sikuchoka, mara tukatokezea kwenye sehemu ambayo hakukuwa na giza kama kule tulikotoka.
Giza lake lilikuwa ni kama katikati ya usiku wa manane na mapambazuko, kwamba kunakuwa na giza lakini siyo totoro na kwa mbali kuna mwanga unaonekana. Hali hiyo ilifanya niweze kuona vizuri mazingira yote, nikawa pia na uwezo wa kuliona vizuri jibwa lile ambalo liliendelea kutimua mbio huku likibweka kwa hasira.
“Huyo siyo mbwa, ni binadamu, mganga wa baba yake Shenaiza, anajua siri nyingi sana kumhusu na ndiye atakayetusaidia kuiona nafsi ya Shenaiza ilikofungiwa, jitahidi uishike ile kamba yake ya shingoni, usijali hata kama litakurarua,” sauti ya Junaitha ilisikika tena ingawa sikuwa na uwezo wa kumuona. Kauli hiyo ilinitisha sana, nikaanza kuamini kwamba kumbe zile stori nilizokuwa nazisikia tangu kitambo, kwamba kuna binadamu wanaoweza kubadilika na kuwa mbwa, zilikuwa za kweli.
Nilipiga moyo konde, nikaongeza mwendo na hatimaye nikawa nimelikaribia kabisa lile jibwa ambalo sasa lilipoona naelekea kulizidi mbio, liligeuka kwa hasira na kutaka kunirukia, likiwa limetoa makucha yake. Nilifanya kama nilivyoagizwa na ile sauti, mkono mmoja nikautumia kuibana miguu yake ya mbele iliyokuwa na nguvu kubwa, likadondoka chini kama mzigo.
Kwa bahati mbaya sikuweza kuidhibiti miguu ya nyuma, likaitumia kunirarua mapajani mwangu ambapo kama isingekuwa uzito wa ile nguo niliyokuwa nimevaa, huenda lingenijeruhi zaidi ya vile.
Japokuwa nilisikia maumivu makali, sikujali, nikalishika shingoni ambapo lilikuwa limefungwa kwa kamba iliyokuwa na mafundofundo kadhaa.
“Unaniuaaaa, nisamehe unaniuaaa,” nilishangaa mno kuona jibwa lile likibadilika na kuwa mtu ambaye alianza kupiga kelele akiniomba msamaha. Bado nilijihisi kama nipo ndotoni, nikawa nimekodoa macho nikiwa ni kama siamini.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilishangaa Junaitha naye akidondoka kutoka kusikojulikana kama mzigo, harakaharaka akainuka na kujikung’uta, akasogea pale nilipokuwa nimelikaba lile jibwa ambalo sasa lilibadilika na kuwa mwanamke, tena mzee tofauti na msichana ambaye nilimuona pale treni liliposimama ghafla.
“Nilikwambia nitakupata tu ukabisha, sasa yako wapi?” nilimsikia Junaitha akisema wakati akinisaidia kumfunga mwanamke yule ambaye bado alikuwa akiendelea kupiga kelele huku akifurukuta. Nilishangaa kugundua kwamba kumbe Junaitha alikuwa akifahamiana na yule mtu wa maajabu.
Nikawa najiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, Junaitha alipomaliza kumfunga mikono kwa kutumia kamba za miti, alihamia miguuni. Akamfunga na kumgeuza, akamburuza na kumkalisha akiwa ameegamia kisiki cha mti.
“Unaona ulivyomuumiza? Haya nataka umtibu sasa hivi, vinginevyo nitakufunza adabu,” alisema Junaitha kwa hasira huku akimshika nywele na kumtingisha, kwa msaada wa mwanga hafifu nikawa namshangaa yule mwanamke jinsi alivyoumbwa usoni.
Alikuwa na masikio makubwa, pua nene ya duara na meno yaliyochongoka pembeni. Ama kwa hakika alikuwa akitisha. Baada ya Junaitha kumwambia vile, huku akitetemeka alitoa ishara kwamba nifunue lile eneo alilokuwa amenijeruhi, akatoa ulimi wake na kunipa ishara kwamba nisogeze majeraha yangu anilambe, jambo ambalo nilisita.
“Sogea tu hawezi kukufanya chochote, si unaona nimeshamvua kamba yake ya shingoni,” alisema Junaitha huku akinionesha kamba iliyokuwa na mafundo kadhaa aliyokuwa ameishika mkononi. Nikasogeza mapaja yangu ambapo alitoa ulimi wake mrefu na kuanza kunilamba damu zilizokuwa zinachuruzika.
Ulimi wake ulikuwa mgumu na unaokwangua kama wa mnyama mkali, nikashangaa maumivu niliyokuwa nikiyasikia yakiyeyuka ghafla, Junaitha akanihakikishia kwamba nitapona baada ya muda mfupi, nikawa bado nimepigwa na butwaa.
“Ukitaka kuendelea kuishi, kazi ni moja tu, tunataka utuoneshe Shenaiza alipo na pia utuambie mbinu zote za kishirikina ulizomfanyia baba yake alipokuja kwako kuomba kinga ya kufanikisha mambo yake ya kishetani,” alisema Junaitha, mwanamke huyo akaanza upya kulia huku akitingisha kichwa chake, hali iliyozidi kunifanya nikose majibu.
Aliendelea kulia na mara akaanza tena kutoa muungurumo kama mnyama mkali wa porini, akawa anafurukuta kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 55


ILIPOISHIA:
“Ukitaka kuendelea kuishi, kazi ni moja tu, tunataka utuoneshe Shenaiza alipo na pia utuambie mbinu zote za kishirikina ulizomfanyia baba yake alipokuja kwako kuomba kinga ya kufanikisha mambo yake ya kishetani,” alisema Junaitha, mwanamke huyo akaanza upya kulia huku akitingisha kichwa chake, hali iliyozidi kunifanya nikose majibu. Aliendelea kulia na mara akaanza tena kutoa muungurumo kama mnyama mkali wa porini, akawa anafurukuta kwa nguvu.
SASA ENDELEA...
“Usitake kututisha hapa na ukiendelea na upuuzi wako nitakuua kwa mikono yangu mwenyewe, unajua ni kwa kiasi gani nina hasira na wewe?” alisema Junaitha kwa sauti nzito ya kunguruma, ambayo sikuwahi kumsikia hata siku moja, yule mwanamke mzee akanywea na kurudi kwenye hali yake ya kawaida lakini bado alikuwa akilia huku akitingisha kichwa, akionesha hayupo tayari kuzungumza kitu chochote.
“Wala sikulazimishi, uchaguzi ni wako, ukitaka kuendelea kuishi ni lazima uzungumze na ukitaka kufa endelea kukataa.”
“Hata nikizungumza nitakufa tu, hawezi kuniacha, ataniua.”
“Nani, unamzungumzia nani?”
Badala ya kujibu, yule mwanamke alionesha kwa ishara, Junaitha na mimi tukageuka kutazama kule alikokuwa anaonesha.
“Mungu wangu,” nilijikuta nimetamka wa sauti kubwa, Junaitha akaniwahi na kuniziba mdomo.
“Huku huwa hatumtaji ovyo Mungu, si unajua kuna amri katika vitaabu vitakatifu ambayo inasema usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako?” alisema Junaitha kwa sauti ya kunong’ona, nikatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana naye lakini bado moyoni nilikuwa nimepatwa na hofu kubwa mno.
Joka kubwa lililokuwa limesimamia mkia na kujiinua, likiwa na macho mekundu yanayowaka huku ulimi wake mrefu wenye ncha mbili ukichezacheza, lilikuwa likitutazama, mita chache kutoka pale tulipokuwa tumembananisha yule mwanamke mzee.
“Huyu ni nani?”
“Mkuu.”
“Anahusikaje katika hili?”
“Maagano yote wanayoyafanya watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuzimu hupitia kwake na yeye ndiye anayeidhinisha.”
“Anataka nini?”
“Anataka mniachie niende zangu,” alisema yule mwanamke huku akitetemeka. Muda wote huo, macho yangu yalikuwa yameganda kwenye lile joka, kuna wakati nilihisi kama haja ndogo inanitoka kwa hofu. Likawa linageuza kichwa huku na kule, likiendelea kuchezesha ulimi huku likitutazama.
Mara likaanza kuteleza taratibu likitusogelea, Junaitha akanipa ishara kwamba nisogee tusaidiane kumshika yule mwanamke, nikafanya hivyo. Ndani ya dakika sifuri tayari tulikuwa tumemshika yule mwanamke, mimi upande wa kulia na Junaitha upande wa kushoto.
“Inabidi tuondoke, fuatisha ninachokifanya,” alisema Junaitha, akapiga mguu wa kushoto chini, na mimi nikafanya hivyo, akapiga tena, na mimi nikapiga mpaka mara tatu kisha akanionesha ishara kwamba tunatakiwa kuanza kuzunguka kutengeneza duara, tukifuata uelekeo wa kinyume na mshale wa saa au kwa Kizungu wanaita Anti-Clockwise, yaani kutoka kulia kwenda kushoto.
Tulipozunguka mara moja tu, ghafla upepo mkali ulianza kuvuma, Junaitha akanionesha ishara kwamba tuendelee kuzunguka kwa kasi zaidi, kufumba na kufumbua kikaibuka kimbunga kikali na kutuzoa, kwa mbali nikawa nasikia sauti ya lile joka likinguruma kwa hasira, sauti zikafifia masikioni mwangu na ikafika mahali nikawa sijitambui tena.
Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta nikiwa nimelala kwenye zulia, ndani ya kile chumba tulichokuwa tumekaa mimi, Junaitha, Raya, Shamila na Firyaal. Kama ilivyokuwa mara ya kwanza tulipotoka kumuokoa Shamila, mwili wangu ulikuwa umechoka mno, karibu kila kiungo kikiniuma.
Nilipofumbua macho, nilimuona Junaitha akiwa anasumbuana na yule mwanamke mzee, ilivyoonesha ni kama alikuwa akitaka kujifungua kamba tulizomfunga, akamzabua kibao kwa nguvu na kumtaka atulie.
Nilijikakamua na kusimama, japo kwa taabu, miguu yangu ikiwa inatetemeka kwani sikuwa na nguvu kabisa.
“Hebu njoo tukamfungie huyu mshenzi naona anataka kushindana na mimi,” Junaitha alisema, kijasho chembamba kikimtoka. Kwa kuwa mle ndani kulikuwa na mwanga tofauti na kule kwenye ulimwengu mwingine tulikotoka, niliweza kumtazama vizuri yule mwanamke. Ama kwa hakika alikuwa anatisha.
Ngozi yake ilikuwa imeweka utando mweusi juu yake, kuonesha kwamba ulipita muda mrefu sana bila kuoga au kugusa maji, kucha zake nazo zilikuwa ndefu, zilizojaa uchafu, huku kichwani nako akiwa na nywele ndefu, chafu, zilizonyonyoka na mdomoni alikuwa na meno machafu, yaliyochongoka kama ya mnyama wa porini.
“Mbona unashangaa? Shika tumpeleke ndani,” alisema Junaitha, akawa ni kama amenizindua kutoka kwenye lindi la mawazo ya kutisha. Nilimshika yule mwanamke japo kwa woga, nikamuona akinitazama na kunikazia macho.
“Sura yako siyo ngeni, tumewahi kukutana mahali,” alisema yule mwanamke huku akiendelea kunitazama kwa kunikazia macho. Alipozungumza, harufu mbaya ilimtoka mdomoni na kusababisha hali ya hewa ichafuke, sikumjibu kitu, akawa anaendelea kunitazama.
Sikuwahi kumuona kabla wala sikuwahi kukutana na kiumbe cha mfano wake, nilishangaa ananiambia sura yangu siyo ngeni, nikahisi anataka kunichezea mchezo wa kunirubuni.
“Donda lako la kifuani lilishapona?” aliniuliza swali lingine lililonishtua mno. Ni kweli nilikuwa na kidonda kifuani ambacho kilinitesa kwa kipindi kirefu lakini alijuaje? Nikajikuta nikiwa kwenye mtihani mgumu uliokosa majibu. Nilimtazama Junaitha lakini alifanya kama vile kunipotezea fulani hivi, akijifanya hajasikia kilichozungumzwa na yule mwanamke.
“Hukupaswa kuwepo hapa leo, ulimwengu huu siyo sehemu yako, unatakiwa kuwa sehemu nyingine sasa hivi,” alizidi kusema yule mwanamke wakati tukimkokota kuelekea kwenye chumba cha ndani kabisa ambacho Junaitha hakuwa akiruhusu mtu yeyote kuingia.
“Naongea na wewe, unajifanya hunisikii si ndiyo?” alifoka yule mwanamke baada ya kuona nimemchunia, akawa anatishia kama anataka kuning’ata na meno yake kama mnyama wa porini, Junaitha akamzibua kibao kingine cha uso, akatoa ukelele kuonesha kilikuwa kimemkolea.
“Kanisubiri chumbani kwangu,” alisema Junaitha, akawa amenizuia kijanja kuingia kwenye kile chumba chake cha siri ambacho hakuna aliyekuwa anajua ndani yake kuna nini kwa sababu hakuna aliyewahi kuingia. Hata Shamila mwenyewe, alinidokeza kwamba hakuwahi kuingia hata mara moja.
Alimuingiza yule mwanamke kisha akafunga kwa ndani, nikamsikia yule mwanamke mzee akitoa sauti ya kuugulia, sikujua nini kilichokuwa nikaendelea humo ndani. Nilijivuta na kuelekea chumbani kwa Junaitha kama alivyioniambia.
Kila kitu kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa mno kiasi cha kunifanya nijihisi kama nipo kwenye ndoto za kutisha. Nilirudi mpaka kwenye kile chumba nilichowaacha akina Shamila, bado walikuwa wamelala fofofo kama mizigo, nikarudisha mlango taratibu na kuelekea chumbani kwa Junaitha lakini kabla sijafika, nikiwa napita kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza, nilimsikia akikohoa.
Harakaharaka nikafungua mlango nikiwa ni kama siamini nilichokisikia, nikamkuta Shenaiza akihangaika kujigeuza, jambo ambalo hakuwa amelifanya kwa kipndi kirefu tangu akiwa kule hospitalini.
“Shenaiza! Shenaiza,” nilisema huku nikipiga magoti pembeni ya kitanda chake. Bado hakuwa amefumbua macho yake.
Je, nini kitafuatia?
 
Back
Top Bottom