Simulizi ya kweli: Niliolewa na Jini bila kutarajia

Simulizi ya kweli: Niliolewa na Jini bila kutarajia

SEHEMU YA 11


Nilipogeuka ili kuondoka tu akanishika mkono na mkono wake ulikuwa wa baridi sana.
Ubaridi ule ulipenya kwenye mwili wangu hata nilihisi baridi na mimi, Carlos akaniangalia kwa makini kana kwamba anayasoma mawazo yangu.
"Mbona unaniogopa Sabrina? Mimi ni binadamu wa kawaida kama wengine jamani."
Nilibaki nikimuangalia tu, bila ya kumjibu kitu chochote.
"Kwani mimi nina pembe jamani? Au natisha? Kwanini uniogope Sabrina?"
Nikazidi kumuangalia na kuanza kumuuliza maswali na mimi.
"Kwani wewe ulijuaje kama simu yangu ilianguka?"
"Kwahiyo hicho ndio kinafanya uniogope?"
"Na je namba yangu uliitoa wapi?"
"Sikia Sabrina, siku niliyochukua simu ya Sam kuweka namba yangu ndio nikachukua namba yako humo. Halafu siku ile niliyokupigia nilijua tu umeshtushwa na simu yangu kwani nikasikia kama simu imeanguka na gafla ukapotea hewani ndipo nilipogundua kuwa simu yako imeanguka na kuharibika. Roho ikaniuma sana kwani mimi ndiye niliyesababisha ndiomana nikaamua kwenda kukununulia simu nyingine kama ishara ya kuomba samahani. Tafadhari Sabrina pokea simu hii"
Ingawa nimeyaelewa maelezo ambayo Carlos ameyatoa ila bado iliniwia vigumu kupokea ile simu.
Mara mama akatoka ndani na kunikuta nimesimama na Carlos pale nje.
"Yani Sabrina muda wote umesimama na mgeni hapo nje? Kwanini usiingie nae ndani mwanangu! Haya karibu ndani baba."
Nikajua mama ameshapagawa na lile gari la Carlos pale nje, ikabidi nimkaribishe Carlos ndani ingawa sikuwa na imani nae.

Tukiwa tumekaa pale sebleni, mama akaanza kumuuliza maswali mawili matatu Carlos.
"Kwani wewe ni mwenyeji wa wapi baba?"
"Mimi ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma"
"Wazazi wako wako wapi?"
"Wazazi wapo Kigoma ila nina ndugu zangu baadhi hapa na wazazi nao watakuja tu maana wamekaa sana kule na wameshapachoka"
Carlos aliongea mambo mengi sana na mama, hadi kumwambia kuhusu simu aliyoniletea.
Mama nae akaanza kunilazimisha kuwa nichukue simu ile niliyoletewa na Carlos.
"Yani mama, mi sina nia mbaya kabisa kumletea Sabrina simu. Nimefanya hivi kama ishara ya urafiki wetu tu."
"Ndio namshangaa hapa kinachomfanya akatae, labda anahisi utamdai."
"Siwezi kumdai mama, nimemletea hii simu kwa hiyari yangu mwenyewe"
Mama akaendelea kunisisitiza kuwa niichukue, ikabidi niichukue ile simu na kumuuliza swali ambalo lilinitatiza bado.
"Mbona mikono yako ni ya baridi sana?"
"Hutokea tu ila si mara zote, nadhani nina upungufu wa madini flani mwilini"
Mama akaanza kucheka kisha Carlos akaaga na kuondoka.

Nilitafakari vitu vingi sana bila ya kupata jibu, kwakweli huyu Carlos alinifikirisha sana tena sana, hata nikashangaa kuwa mama amewezaje kumuamini Carlos kwa muda mfupi kiasi kile.
Mama akaja na kuanza kuniambia,
"Maskini jeuri wewe, simu unaitaka halafu unavunga! Kaka wa watu kajitokea mbali kwaajili yako eti wewe unavunga loh"
"Ila mimi simuamini yule kaka kabisa"
"Kwanini humuamini? Mbona ni mtu wa kawaida tu mwanangu!"
"Mi simuamini tu jamani"
Kwakweli sikumuamini kabisa Carlos niliona ni majanga tu.

Usiku ulipofika, mama alikuja kutembelewa na rafiki yake mama Salome.
Mama akaanza kumuelezea kuhusiana na matatizo yangu ya kuogopa ndani.
Nilikuwa kimya kwenye kochi nikijifanya nimesinzia ila nilisikia yote waliyozungumza.
"Sasa mama Penina, kama mtoto anawehuka hivyo wakati wa kulala kwanini msifanye maombi?"
"Hapo ndio hadi mi mwenyewe najishangaa mama Salome, yani Sabrina akianza kuwehuka huwa sikumbuki kabisa kusali hata sijui kwanini?"
"Dunia imechafuka sana ndugu yangu, shetani ana jeshi lake kubwa humu duniani inatakiwa mkumbuke kusali kwani sala ni nguzo imara ya kumpinga shetani."
"Asante mama Salome nitafanyia kazi ulichosema"
"Tena kwa ushauri wa bure, ita familia yako tulia nayo mnaomba pamoja halafu mnalala"
"Nimekuelewa ndugu yangu"
Mama Salome akaaga na kuondoka kwani alikuja kumwambia mama habari za kikundi chao ila mazungumzo haya mengine yaliingilia kati tu.

Dada akarudi nyumbani, kwakweli leo alichelewa sana kurudi na alitukuta tunakula ilibidi mama amuulize sababu ya kuchelewa.
"Kuna mambo ya Fatuma namsaidia kushughulikia, nadhani kesho au keshokutwa tunaweza kufanikisha"
"Mambo gani hayo?"
"Nikiyasema sasa hivi kuna shoga yangu hapa atasema namtisha asilale, nitawaambia kesho kama nikirudi mchana"
Nikajua tu hayo mambo lazima yatakuwa yanahusiana na majini tu ndiomana hajayaongelea kwani anajua kuwa mimi naogopa sana mambo hayo.

Muda wa kulala ukafika, mama akainuka kwenda kulala na kuniacha na dada pale sebleni. Nikakumbuka maneno ya mama Salome kuwa tupende kusali kabla ya kulala, nikamfata mama na kumwambia kuwa amesahau maagizo aliyosema kwa mama Salome kuwa atayatelekeza.
Nikamkumbusha mama kusali naye akakumbuka, akarudi sebleni na kumwambia dada Penina kuwa tunatakiwa kusali kabla ya kulala.
"Mama, kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe, maswala ya kulazimishana kusali mimi hata siyapendi"
Dada Penina akawa anapinga kabisa ikabidi mama amuombe na kumlazimisha kuwa ni vyema tukifanya ibada ya pamoja, badae akakubali.
Kama familia tukaamua kufanya ibada kabla ya kulala.

Wakati wa ibada hiyo hakuna aliyeelewa nini kiliendelea kwani kila mmoja alijikuta yupo chumbani kwake asubuhi, na mama ndiye aliyekuwa wa kwanza kuja chumbani kwangu.
"Hivi muda ule tuliosema tunafanya ibada ilikuwaje?"
"Hata sielewi mama, maana sina kumbukumbu za ibada hiyo."
"Mmh ya leo kali!"
Dada Penina nae aliamka na kuja chumbani kwangu.
"Leo nimechelewa hadi kwenda kazini sijui hata ni usingizi wa aina gani!"
"Kila mmoja anashangaa hapa maana mara ya mwisho tulipanga kufanya ibada"
"Au tulifanya ibada na kwenda kulala?"
"Labda ila hakuna mwenye kumbukumbu yoyote."
Mimi nilikuwa natafakari tu na nikatambua kuwa yote yanafanywa na yule mkaka wa ndotoni tu kwani tuo afanyaye mambo ya ajabu.

Mchana nikampigia simu Sam, ambaye alikuwa na mawazo ya kupotelewa na pesa ya ofisi.
"Yani nimechanganyikiwa Sabrina, hata sijui pesa ya ofini nitaipatia wapi tena jamani mmh!"
Nikajaribu kumpa moyo na kumwambia maneno mazuri ambayo najua hayakumfariji hata kidogo kwani alikuwa ameshachanganyikiwa.

Nikapigiwa simu na rafiki yangu Suzy ambaye alianza tena kuniuliza kuhusu Carlos.
"Sabrina, unamuonaje Carlos?"
"Namuona ni mtu wa kawaida tu, kwani wewe unamuonaje?"
"Ngoja kwanza, nikimaliza uchunguzi wangu nitakwambia"
Suzy akakata simu, nikajiuliza maswali kuwa kwanini Suzy ana wasiwasi juu ya Carlos.
Mama akaniita na kuniambia kuwa ameongea na kaka na amesema kwamba hivi karibuni atanihitaji kwake ili nikabadilishe mazingira kidogo, kwakweli nilifurahi sana, hata dada aliporudi aliona jinsi nilivyofurahi.

Wakati wa kula dada akaamua kunitani,
"Naona umefurahi kuepukana na stori zangu za kutisha."
Mama akadakia,
"Lazima afurahi, anavyoogopa majini na watu waliofufuka huyu balaa"
Yani wanavyosema watu waliofufuka mie mwenzao ndio nazidi kupatwa na uoga wa mawazo.
"Anaogomba mazombie mdogo wangu jamani, ila mama yanatisha kweli yale usiombe ukutane nao"
"Majini yako je hayatishi?"
"Mama wee usiniambie habari za majini, kilichompata Fatuma ni balaa"
"Mmeshaanza stori zenu sasa, mi mnanikera sana"
Ikabidi wanyamaze na tuendelee kula kama kawaida.

Usiku mawazo yangu yalikuwa ni kwenda kwa kaka tu, sikuwa na mawazo mengine zaidi ya hayo na sikutaka kukaribisha mawazo ya zaidi.
Wakati wa kulala ulipofika, nilikwenda chumbani na kulala moja kwa moja hata simu sikuongea nayo usiku.

Nikamuona Sam akihangaika sana, mara nikamuona akifunga ndoa na Lucy halafu tena nikamuona akitokwa na majipu mwili mzima. Nikashtuka kutoka kwenye ile ndoto na kujikuta nikianza kuogopa mule nyumbani, kwani wakati nimeshtuka nilikuwa nahisi kama mtu akitembea tembea mara avute kiti mara avute meza halafu sauti ikasika,
"Mbona umeamka kabla ya wakati Sabrina?"
Uoga ukanijaa, nikakumbuka maneno ya mama Salome kuwa natakiwa kusali.
Nikashuka kitandani na kupiga magoti, kabla sijafanya chochote taa ya chumbani ikazimwa halafu mikono ya baridi ikawa inagusa miguu yangu.
Kwakweli nilitetemeka kiasi cha kupoteza fahamu, sikupenda kutazama mbele na mara taa zikawashwa tena hapo nilizidi kutetemeka na hakuna maombi tena niliyoweza kuyafanya.
Nilijikunyata ukutani bila ya kujua cha kufanya, ile sauti ikajirudia tena.
"Mbona umeamka mapema Sabrina"
Kwakweli huu usiku ningeweza kuubadilisha basi ningeubadilisha jamani, jasho jingi lilinitoka na wakati nilikuwa natetemeka kwa baridi la uoga.
"Usiogope Sabrina, nipo nje ya chumba chako bado sijaingia ndani ila karibia nitaingia"
Mara gafla nikaona mlango wa chumba changu ukifunguliwa, muda huohuo mkojo ulinitoka bila ya hodi.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 12



Mara gafla nikaona mlango wa chumba changu ukifunguliwa, muda huo huo mkojo ulinitoka bila ya hodi.
Nilikuwa nangoja kuona huyo mtu wa ajabu atakayeingia ndani kwani nilijua kuwa kwa vyovyote vile siwezi kumkwepa.
Mlango wangu ulikuwa unafunguliwa polepole, ujasiri ukaniisha na kujifunika sura kwani sikuweza tena kutazama kitu kitakachoingia, mara nikashikwa kichwani na hapo nikapiga ukelele uliomuamsha hadi mama.
Mama akafika chumbani kwangu wakati mimi nikiwa bado nimeinama na kujikunyata.
"Vipi mwanangu jamani? Umepatwa na nini tena? Eti Penina, mdogo wako amepatwa na nini?"
Mama alimuuliza dada Penina ambaye naye alikuwa chumbani kwangu.
"Hata mimi namshangaa jamani, mi nilikuja chumbani kwake huku na nikafungua mlango taratibu ili nisimsumbue, shida yangu ilikuwa ni ile pochi ndogo. Nimeshangaa kumkuta hapo chini amejikunyata na kujiinamia nikaamua kumshika kichwani ili kumuangalia ana tatizo gani ila ile kumshika tu ndio akapiga makelele yote hayo."
Mama akaniangalia kwa makini,
"Kwani una nini Sabrina? Au kuna mambo ulikuwa unayawaza?"
Kitu cha kwanza kuwauliza ilikuwa ni muda,
"Kwani saa ngapi saizi?"
"Kumekucha mwanangu na dada yako ndio huyu amejiandaa kwenda kazini"
Nikabaki nashangaa tu na sikuelewa chochote, mama akaangalia chini na kuona yale majimaji ya mkoje.
"Kheee! Hadi umejikojolea Sabrina!! Ulikuwa unaogopa nini mwanangu?"
"Amejikojolea kweli loh"
Dada akaanza kucheka, kisha akachukua alichosema na kuondoka.
Nikabaki na mama tu pale ndani.

Kulipokucha vizuri nilikuwa nimeshaoga na kutafakari ya usiku kwakweli hakuna ambacho nilikuwa nakielewa. Nikaenda kwa mama jikoni kumuuliza,
"Nitaenda lini kwa kaka Deo mama?"
"Sabrina mwanangu, umeanza uoga hadi wa kufikia kujikojolea si utaenda kutia aibu tu huko kwa kaka yako? Sidhani kama wifi yako atavumilia hali hiyo!"
"Mama yani bahati mbaya ya siku moja ndio unaihesabia kama siku zote? Mimi nataka kwenda kwa kaka haijalishi nini wala nini"
"Utaenda ila ndio hivyo utatutia aibu kama ukiendeleza hiyo tabia"
Nikamsikiliza mama ila moyoni bado nilitaka kwenda kwa kaka tu ili nibahatike kubadilisha mazingira kidogo.

Mchana nikajilaza sebleni kwani macho yangu yalikuwa mazito sana na kujawa na usingizi.
Mama akanishtua kuwa nimepata ugeni, kuamka nikamkuta ni Carlos ambapo mama alimkaribisha sebleni tayari.
Kisha mama akaenda chumbani kuendelea na mambo yake mengine, Carlos akaanza kujiongelesha pale.
"Mbona umechukia Sabrina? Hujaupenda ujio wangu?"
"Hapana, ila mbona umekuja bila taarifa?"
"Nimekuja kuangalia unaendeleaje Sabrina, nakujali sana mama angu. Nikwambie kitu Sabr."
"Niambie tu hakuna tatizo"
"Sabrina, wewe kweli ni binti mzuri na mrembo yani ingawa umetoka kulala ila bado unapendeza na kuvutia. Sura yako ina mvuto wa hali ya juu Sabrina, na umbo lako ni zuri sana ila samahani kama sifa zangu zimevuka mipaka."
Nikacheka na kumuangalia vizuri huyu Carlos ambaye leo alikuja na staili ya kunisifia.
Nikaamua kumuuliza swali Carlos,
"Mbona umeamua kunisifu kiasi hicho?"
"Anayestahili sifa acha apewe sifa yangu, kwakweli Sabrina hadi nimekupenda yani."
Nikashtuka na kumuuliza tena,
"Si unajua kama mimi nipo na Sam halafu tunapendana sana?"
"Tatizo lenu wasichana ndio hilo, mtu akitamka nakupenda basi wewe ushapelekea kwenye maana nyingine. Mimi nakupenda Sabrina kama Sabrina na si vinginevyo."
Nikabaki kimya kwani alinishushua, akaongea mambo mengine kisha akaondoka.
Nikawa naitafakari ile kauli ya Carlos ya kusema kuwa ananipenda Sabrina kama Sabrina na si vinginevyo, kauli yake bado ilikuwa na utata sana kichwani mwangu ila sikupenda kuijadili zaidi.

Jioni yake Carlos akanipigia simu na kuniuliza.
"Unapenda chocolate Sabrina?"
"Ndio nazipenda."
"Nikuletee?"
Nikasita kuitikia nikawa kimya tu na simu sikioni,
"Basi nakuletea"
Halafu akakata simu, nikawa nashangaa tu kwani bado sikuwa na imani nzuri na Carlos.
Haikuchukua muda nikamsikia Carlos akizungumza na mama.
"Mimi sio mkaaji mama, nimemletea Sabrina mzigo wake huu."
Kisha nikamsikia akiaga, baada ya muda kidogo mama akaniita huku akiufungua ule mzigo.
"Mmh kumbe chocolate, huyu ndio mkwe bwana sio huyo Sam wako."
Akafungua moja wapo na kuanza kula huku akinikabidhi ule mfuko, ila mimi nikakataa na kumuachia mama.
Dada yangu Penina nae aliporudi wakaungana na mama kula zile chokleti. Na mimi nikatumia mwanya huo kumchombeza mama,
"Leo mama tutalala wote eeh!!"
"Hakuna shida mwanangu tutalala tu, ila masharti yale yale kuongea na simu usiku sitaki."
"Sawa mama hakuna tatizo"
Nikatulia pale sebleni na kuwaangalia tu walivyokuwa wakisakamia zile chokleti huku wakisifu kuwa ni tamu sana.

Usiku ulipowadia, nilijipanga kulala na mama ila nilimkumbuka sana Sam nikaamua kumpigia simu kabla ya kulala ila haikupatikana.
Mawasiliano yangu na Sam yamekuwa yakisuasua sana kwa siku mbili tatu hizi hata nikishindwa kuelewa kuwa Sam atakuwa amepatwa na tatizo gani jingine.

Nikaenda kulala chumbani kwa mama ambaye alinisihi kuwa nisiwe muoga, kitu cha ajabu kwetu ilikuwa tunakumbuka vyote ila si kusali tena mara nyingine kukishakucha mama ndio anakumbuka kuwa hakufanya ibada.
Niliongea na mama pale mambo mawili matatu na kisha kulala.

Kama kawaida yule mkaka wa ndotoni alinitokea na kunifata mahali ambapo nilikuwa nimekaa katikati ya nyasi laini na nyororo, yule mkaka akaanza kusema.
"Nikupe kitu gani Sabrina ili ujue kama nakupenda? Nikuonyeshe ishara gani ili utambue upendo wangu kwako?"
Nikawa namuangalia tu bila ya kumjibu chochote kile.
"Ninauwezo mkubwa sana wa kukufanya mke wangu hata kama hutaka ila mimi nahitaji ukubali kwa hiyari yako mwenyewe"
Akaanza kuongea maneno ambayo yalifanana na aliyoongea Carlos mchana.
"Sabrina, wewe ni binti mzuri na mrembo. Una sura ya kuvutia na umbo."
Kisha akamalizia kuwa,
"Anayestahili sifa apewe sifa yake"
Nikashtuka kutoka usingizini na kuhema juu juu.
Nikaanza kumfikiria Carlos, sura yake ikatembea mawazoni mwangu na ule ubaridi wa mikono yake nikaanza kuuhisi mwilini mwangu hadi kuanza kutetemeka.
Nikajiuliza maswali mengi sana juu ya Carlos, mara nikaona kivuli cha mtu mule chumbani kwa mama hapo sasa uoga ukanishika na kuanza kutetemeka, kile kivuli kikawa kinanisogelea taratibu yani kinakuwa kirefu nikawa nimemkumbatia mama na mara ikasogea hdi usoni kwangu na kunichekea.
Hapo sasa nikaanza kumuamsha mama kinguu ila mama alikuwa hoi kabisa hata hajitambui na hakuamka kabisa ikawa kama vile niko peke yangu mule chumbani.
Ikaanza sauti ya paka kama ile ambayo uwa inasikika chumbani kwangu, hapo nikazidi kutetemeka na kuzidi kumkumbatia mama.
Kwakweli leo nilimshangaa mama kwani hakushtuka hata kidogo tofauti na siku zingine, na gafla umeme ukakatika hapo ndipo uoga ulipozidi na kuendelea kumuamsha mama ambaye aliamka na kuongea kama mlevi kisha kulala tena.
Katika hali ile ya uoga nikapitiwa na usingizi palepale.

Yule mkaka wa ndotoni alikuwa anacheka sasa tena akicheka sana sana, kisha akaniambia nimpe mkono wangu nikasita kumpa na kukataa kabisa, akaniambia.
"Nakupenda Sabrina"
Nikamuangalia tu, akawa analazimisha kuwa nimwambie nampenda nikagoma akawa anataka kunichukua kwa nguvu.
Nikashtuka na kupiga kelele,
"Nampenda Sam"
Hapo mama nae akashtuka na kuniangalia kwa jicho kali sana.
"Yani wewe asubuhi Sam, mchana, jioni khee hadi ndotoni? Huyo Sam kakupa nini mwanangu?"
Akiuliza hayo, alikuwa akiangalia mwanga uliokuwemo chumbani na kugundua kuwa kumeshakucha teyari, akastaajabu sana kuona amepitiliza kulala kiasi kile.
Nikaenda kumuangalia na dada Penina ambaye nae alikuwa hoi na usingizi, nikamuamsha naye alishangaa kuona kumekucha kuasi kile.
"Mmh nimelala kama mlevi leo jamani"
Nadhani na wao hawakujielewa kama mimi niotaye ndoto za ajabu tu.

Siku ya leo kila mtu alikuwa na mawazo nyumbani kwetu, sijui na wao walipatwa na mandoto ya ajabu kama yangu. Nikawa nimetulia na kutafakari, ikaingia simu kuangalia mpigaji ni Lucy. Ile kupokea tu akanipachika swali,
"Sam unampenda humpendi?"
"Swali gani hilo la kuniuliza Lucy?"
"Kila swali ni swali na linahitaji majibu, jibu swali nililokuuliza."
"Unajua wazi jinsi gani nampenda Sam"
"Kama unampenda mbona unamsababishia majanga?"
"Majanga? Majanga gani?"
Lucy akakata simu, nikajaribu kumpigia Sam hakupatikana.
Nikampigia tena Lucy naye hakupatikana na kujikuta nikiwaza vitu vingi mno.

Nikafikiria sana na kukosa jibu, nikaamua kuvaa ili niende kwa Sam.
Kwavile ilikuwa ni jioni sana yani karibia na usiku, mama akanikatalia kutoka. Nikajikuta nikiwa na mawazo sana na roho kuniuma, muda wote nilimjaribisha hewani Sam alikuwa hapatikani wala Lucy nae hapatikani.
Siku hiyo nilikaa na dada kwenye luninga huku nikiwa na mawazo tu, ila badae dada alienda kulala na kuniacha mwenyewe pale sebleni. Saa sita usiku nikaamua kumtafuta tena Sam hewani na muda huu simu yake ikaita nikafurahi sana ili niweze kuongea naye na kupunguza mawazo yangu ila cha kushangaza hakupokea Sam bali ilipokelewa na Lucy.
"Sema shida yako haraka tunataka kupumzika bhana."
Niliiweka ile simu sikioni huku nikiwaza kuwa huyu ni Lucy kweli au yule jamaa wa kujigeuza. Mara nikashikwa bega na ile mikono ya baridi.

Itaendelea
 
Ilikuwa kwenye mida ya saa mbili usiku wakati tumekaaa kwaajili ya chakula cha usiku.
Wakati nakula simu yangu ikaita kuangalia mpigaji ni mpenzi wangu Sam ila nikashindwa kunyanyuka kwenda kupokea kwani mama alikuwa ananiangalia sana ikabidi nibonyeze kitufye cha kimya (silence).
Johayna Abdallah! SIJASAHAU, ulichonifanyia kipindi unajiita MJUKUU WA CHIFU!
Narudia tena SIJASAHAU HATA KIDOGO.
 
SEHEMU YA 13

Niliiweka ile simu sikioni huku nikiwaza kuwa huyu ni Lucy kweli au yule jamaa wa kujigeuza. Mara nikashikwa bega na ile mikono ya baridi.
Kiukweli mikono ile ilikuwa inanipa wazimu kila inaponishika na kufanya nijiulize maswali mengi bila ya majibu.
Nikatulia kuisikilizia ile mikono kwani niliogopa kugeuka na kukutana na kitu cha ajabu.
Ile mikono ikaacha kunigusa ni hapo nilipokimbilia chumbani kwa mama na kumkumbatia wala sikukumbuka tena kuzungumza na ile simu, mama nae akashtuka.
"Nini tena usiku huu?"
"Hamna kitu mama."
"Unaogopa?"
"Ndio naogopa mama."
Mama akainuka pale kitandani na kuniangalia kisha akaniambia.
"Punguza uoga mwanangu."
Akalala chali na kuchukua kichwa changu na kukiweka kifuani mwake kisha akanikumbatia na kusema.
"Tulale mwanangu, usiogope chochote ukiwa na mimi mama yako"
Nililala kama mtoto mdogo hadi asubuhi.

Asubuhi na mapema nikaoga na kuvaa lengo langu ni kwenda kwa Sam nikajue mbivu na mbichi kama kumfumania au la.
"Mapema sana, unaenda wapi Sabrina?"
"Suzy ameniomba nimsindikize mahali, natakiwa kuwahi kwenda ili niwahi kurudi."
Tofauti na siku zingine, leo mama alinikubalia kwenda kwa moyo mweupe kabisa na nauli akanipa yeye mwenyewe, nikatoka na kuelekea kwa Sam.

Kufika kwa Sam nikawa nayasoma mazingira kwanza, nikafika chumbani kwake na kunyonga kitasa mlango ulikuwa wazi, nikaingia na kumkuta Sam amelala bado ila ilikuwa saa mbili asubuhi.
Muonekano wa chumba nilihisi kuwa kuna mtu wa ziada alilala mule, nikamshika mgongoni Sam na kumuamsha ambapo kabla hajaamka vizuri akaniuliza swali.
"Mbona umerudi wakati ulisema unataka kuwahi?"
Swali hili lilinipa mashaka kichwani mwangu kuwa Sam anamaanisha mtu gani.
"Unamaana gani kusema hivyo?"
Hapo akashtuka na kufikicha macho huku akishangaa kuona kuwa ni mimi.
"Khee Sabrina! Umefika muda gani? Umekutana na nanii? Ooh samahani mpenzi wangu?"
Bado alinishangaza, nikamkazia macho Sam.
"Unamaana gani? Unamzungumzia nani? Niambie Sam"
"Samahani bhana ni maruweruwe ya usingizi tu."
"Maruweruwe saa mbili hii Sam? Hebu niambie ukweli, unanificha kitu gani?"
"Hakuna cha kukuficha Sabrina ni maruweruwe tu."
Akainuka na kwenda kuoga, nikawa namngoja kwa hamu ili aniambie kuhusu Lucy kuwa kwanini apokee simu yake ule usiku.

Wakati Sam yupo bafuni, nikaona bahasha mezani kwake nikaifata na kuichungulia nikaikuta ina pesa nyingi tu yani kwa kuzikadilia ni kama milioni mbili, nikawa najiuliza kuwa mbona Sam aliniambia kuwa hana pesa na hizi ni kitu gani? Bado sikupata jibu nikamngoja atoke bafuni nimuulize.
Alipotoka bafuni wakati anavaa nikamwambia kitu ili nisikie jibu lake.
"Sam, nina shida na hela kidogo. Vipi utanisaidia mpenzi?"
"Sabrina mpenzi wangu nilipokwambia kuwa nimeibiwa hukunielewa ama ni nini? Mimi sina hela kabisa yani pangu pakavu tia mchuzi"
Nikamuangalia sana Sam kwa yale maneno, nikamngoja amalize kuvaa ili nizungumze nae vizuri.

Alipokuja kukaa nikamuuliza tena,
"Sasa usiponisaidia wewe mpenzi wangu anisaidie nani?"
"Sabrina, kwanini unakuwa mgumu kuelewa? Swali gani hilo unaniuliza? Unataka nikujibu kuwa ukajiuze au?"
Sam aliongea kwa ukali sana hadi nikaogopa.
"Mbona umebadilika sana mpenzi?"
Hapo Sam akanywea kidogo nilipomuuliza kuwa kwanini amebadilika, akaniangalia kwa makini kisha akasema.
"Nisamehe mpenzi wangu, si unajua tena matatizo ya kukosa pesa yalivyoniathiri. Nisamehe sana Sabrina, hata mi sijajisikia poa kukujibu kwa ukali kiasi hiki."
"Sawa, ila je ni kweli huna pesa?"
Sam akakataa kusema kwamba ana pesa ndani, ikabidi mimi nimuonyeshe bahasha niliyoikuta mezani kwake.
"Na hii ni nini?"
Sam kwa mshangao akaivuta ile bahasha na kuangalia.
"Umeitoa wapi Sabrina?"
"Hapo mezani kwako"
"Hivi unajua kwamba hii pesa ndio niliyokwambia nimeibiwa? Imefikaje sasa hapo mezani?"
Akamwaga zile pesa na kuhesabu.
"Tena ziko vilevile milioni tatu, inamaana nilisahau nilipoweka au ni nini?"
Sam alikuwa na maswali mengi ambayo mimi sikuweza kumjibu kwakweli kwani sikuwa na majibu yake, sasa nikaamua kumuingizia lile swala la Lucy.
"Na mbona jana usiku simu yako imepokelewa na mwanamke?"
"Aah mpenzi, achana na habari hizo bhana inatakiwa tufurahie kuzipata hizi pesa. Eeh unataka kiasi gani nikupe baby wangu?"
"Sitaki chochote Sam naona unajipumbaza tu hapa."
"Kujipumbaza ndio nini mpenzi?"
"Unajifanya huelewi ninachoongelea, nataka kujua Lucy alikuwa anafanya nini hapa kwako usiku?"
"Lucy wa kazi gani mamii, tuongelee mapenzi yetu kwanza. Inuka twende benki nikaweke hizi pesa zisije zikapotea tena."
Ikabidi niinuke tu kwani alijifanya kuwa na haraka ya kupeleka zile pesa benki.

Tulivyofika benki sikuweza kuvumilia kukaa kwani nilikuwa na mawazo sana, nikaamua kumuaga Sam kuwa nataka kurudi nyumbani.
"Mbona mapema sana Sabrina? Basi ngoja niweke pesa hapa benki ili nikupeleke."
"Usijari, mi narudi tu mwenyewe."
"Ila si ulesema kuwa una shida na pesa, sema basi nikupe ngapi?"
"Hata sina shida ya pesa zako."
Nikaondoka pale benki na safari yangu nilienda moja kwa moja nyumbani kwa kina Suzy.

Nilifika na kumueleza Suzy kila kitu kuhusu Lucy na hali niliyomkuta nayo Sam.
"Anaogopa tu kukwambia ukweli inaelekea Lucy alilala hapo."
"Hata mimi nahisi hivyo."
"Ila za mwizi ni arobaini, utambamba tu shoga yangu ila unatakiwa ukaze moyo."
"Yani Lucy kweli ni wa kunifanyia hivi?"
"Si nilikwambia lakini, Lucy ni gumegume na akipangia kumpata mwanaume basi lazima ampate. Ila kaza moyo hili swala tutalipatia ufumbuzi tu."
Ikabidi niingizie na habari za Carlos hapo hapo ili kujua Suzy amegundua nini kuhusu Carlos.
"Yule mkaka simuamini ila nadhani anakutaka Sabrina."
"Kwanini humuamini?"
"Hayupo kawaida kama wengine, akikushika lazima utasisimka halafu kama vile ana sumaku mkononi."
"Unamaana gani Suzy? Inamaana Carlos si binadamu?"
"Hapana ila ana uwezo wa ziada kuliko binadamu mwingine. Pengine ndio wale huitwa mageneous maana ana uwezo hata wa kutambua mawazo yako mara nyingine."
"Mmh! Umemjuaje kwa wepesi kiasi hiko?"
"Sikuile aliyonileta nyumbani nilizungumza nae mambo mengi sana, halafu akanipa namba yake ya simu na nimeweza kumjua sana ndiomana nakwambia ndio wale huitwa mageneous ila cha muhimu kwa sasa ni kuijua familia yake kwanza yani wazazi na ndugu zake ili tuweze kujiridhisha kama ni mtu kweli au la."
Nikaongea mengi na Suzy na kupanga namna ya kumuingia Carlos ili tuweze kutambua familia yake.

Nilirudi nyumbani huku mawazo juu ya Sam yakinichanganya sana sana ila nikajikaza tu kama wengine.
Nikatembelewa na mgeni naye alikuwa ni Carlos, nikamkaribisha na alinikuta nje naye akaketi hapo hapo nje akanisalimia kwa kunishika mkono ila leo mikono yake haikuwa ya baridi.
"Mbona leo mikono yako sio ya baridi?"
"Kwasababu leo nina furaha, sina hasira kabisa kila kitu kwangu kimeenda sawa na hakuna aliyenikera"
Nikamuangalia sana Carlos kwani kauli yake ya leo ilikuwa tofauti na siku niliyomuuliza kuwa kwanini mikono yake ya baridi.
Leo aliongea kwa furaha sana tofauti na siku zote na badae akaaga na kuondoka.

Usiku ukawa umeingia, mawazo juu ya Sam na Lucy hayakunitoka kichwani. Nikamuuliza dada,
"Hivi ukiona kuwa kuna kila dalili ya kusalitiwa na mpenzi wako unatakiwa ufanyaje?"
"Hutakiwi kuwa na hasira ila mjengee mpenzi wako mazingira ya kumfumania, nenda mahali alipo kwa kumshtukiza. Unapohisi kusalitiwa hutakiwi kuchukua maamuzi ya haraka."
Nikafikiria sana, wazo lingine likanijia kuwa natakiwa kwenda kwa Sam asubuhi na mapema ili nimshtukize, wazo lingine likaniambia kuwa nimpigie Lucy simu ili kumuuliza ila kwavile nilitaka Lucy apokee simu yangu upesi nikaamua kutumia simu ya dada ambayo haijui namba yake.

Ilikuwa ni saa tano usiku wakati nampigia Lucy simu kwa namba ya dada, upande wa pili ikapokea sauti ya kiume.
"Hallow, nani mwenzangu?"
Kuisikilizia kwa makini ni sauti ya Sam, hapo nguvu ziliniisha na kukata simu kwani sikuweza kuzungumza kabisa.
Niliona machozi yakinitoka na moyo kudunda dunda kwani hakuna kitu kibaya kama kuhisi unasalitiwa halafu upige simu na sauti ya mpokeaji ikupe mashaka zaidi.
Nilijaribu kujikaza ila nikashindwa, nikachukua simu yangu na kumpigia Sam ila simu iliita bila ya kupokelewa, nilipiga mara nyingi niwezavyo simu yangu haikupokelewa, mawazo mengi yakatawala kichwa changu na nikakosa raha kabisa.

Leo sikwenda kulala chumbani kwa mama, nilienda kulala chumbani kwangu kwani hata usingizi sikuwa nao niliona kama dunia ikizunguka hovyohovyo na kila nikifikiria machozi yananitiririka tu sikuwa na raha wala furaha.
Nilitamani yawe ni mawazo tu na sio kweli kwani Sam ni mwanaume nimpendaye sana, roho iliniuma na kuzidi kukosa raha moyoni mwangu na hapa ndipo mtu anayajua maumivu ya kusalitiwa yalivyo. Wakati nawaza hayo usingizi wa gafla ukanichukua.

Nikamuona Sam akiwa na Lucy halafu mimi niko pembeni nikiwatizama huku roho ikiniuma sana, mara nikawaona wakiwa wamelala pamoja hapohapo nilitamani hata kupasua mtu ndotoni halafu akatokea yule mkaka wa ndotoni na kunicheka.
Nikashtuka, sikutaka kulala tena, nikaanzalia saa ilikuwa ni saa kumi na nusu.
Nikaenda kuoga na kuvaa, nikaenda chumbani kwa mama kuchukua funguo kwani siku hizi alikuwa analala na funguo tangia lile tukio la mimi kutaka kutoka usiku.
Nilifurahi kuona nimechukua funguo bila ya mama kushtuka kwani sikutaka kumuaga, nilijua lazima atanirudisha tu.
Safari ilikuwa ni nyumbani kwa Sam moja kwa moja.

Sikuogopa chochote njiani kwa kifupi nilikuwa nimevurugwa na mapenzi jamani na nilishajipanga kwa lolote, yani liwalo na liwe kama kufa au kupona ila mbivu na mbichi lazima nizijue na nilikuwa kishari haswaa, nikaenda hadi nyumbani kwa Sam na nilifika mapema sana kama saa kumi na moja na nusu nilikuwa tayari nimefika.
Ile kufika tu nikamuona Lucy akiwa na ndoo mkononi inaonyesha alitoka kuoga kwani alikuwa amejifunga khanga moja kifuani halafu ilikuwa na maji maji.
Nikamsogelea na kumuita, naye akageuka kuniangalia.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 14


Ile kufika tu nikamuona Lucy akiwa na ndoo mkononi inaonyesha alitoka kuoga kwani alikuwa amejifunga khanga moja kifuani halafu ilikuwa na majimaji.
Nikamsogelea na kumuita, naye akageuka kuniangalia.
Nikamsogelea karibu tena bila ya kufikiri zaidi, nikamzaba kibao kilichofanya aangushe hadi ile ndoo aliyoibeba kisha akakimbilia chumbani kwa Sam.
Nikamfata hukohuko, Lucy alipiga kelele zilizomuamsha Sam. Nilienda kumshika koo Lucy na kumkaba, yani nilikuwa na hasira za kuua mtu siku hiyo.
Kufumania kubaya sana haswaa kwa mtu mwenye hasira unawezajikuta umepata kesi ya mauaji bila kutarajia.
Sam aliinuka na kunishika huku akinisihi kuwa nisimtende vibaya Lucy, Sam alinishika kwa nguvu na kufanya Lucy apate nafasi ya kukimbia.
Kibao kikageukia kwa Sam sasa, hasira zangu zote zikahamia kwake. Nilijikuta nikivurugua kila kitu kwenye kile chumba ingawa Sam alikuwa akinizuia.
"Tulia mpenzi wangu Sabrina nikueleze."
"Unieleze nini? Unieleze nini mwasherati mkubwa wewe."
Nilikuwa naongea kwa hasira tena bila ya nukta.
Sam alijitahidi kunibembeleze ila alishindwa nilikuwa na hasira iliyopitiliza hadi kuhisi mishipa ya fahamu inanyofoka.

Nilikaa chini na kuanza kulia kama vile mtoto mdogo.
"Sam nimekukosea nini mimi? Kitu gani kwangu hupati hadi kunichanganya na rafiki yangu kweli? Kwanini umenifanyia hivi Sam."
"Punguza hasira Sabrina nikueleze ilivyokuwa, unachofikiria sio kabisa mpenzi."
Maneno yake yakawa yananiliza zaidi kwani niliona kuwa ana mpango wa kuniongopea wakati ukweli wote nimeushuhudia kwa macho yangu.
"Au kwavile unajua siwezi kuja kwako usiku ndiomana unatumia nafasi hiyo kuingiza wanawake utakao! Vingapi nimefanya kwaajili yako Sam? Yani leo ndio unanitenda hivi!"
Sam akanishika huku akinibembeleza na kunisihi nimsikilize kwanza.
"Sitaki Sam, nimesema sitaki. Sitaki kusikiliza huo upuuzi wako, leo nimeamini kuwa ni kweli wanaume wote ni nyoka. Usinieleze chochote Sam, hakuna utakachoniambia nikakuelewa."
Nikainuka na kutoka nje kisha kuondoka kabisa, Sam alijaribu kuniita ila ilishindikana na sikujua pa kwenda kwakweli.

Nikaamua kwenda ufukweni ili nikawaze huko na kulia nitakavyo, nilienda fukwe iliyotulia ambayo huwa haitembelewi sana na watu ili tu niwe mwenyewe. Sikutamani kurudi nyumbani na sikutamani chochote duniani.
Nilitamani nitupwe dunia nyingine nikajifiche huko kwani mapenzi ambayo nimekuwa nikijivunia nayo kila siku yaliingia doa tena doa lisilotoka.
Kila nikifikiria jinsi nilivyokuwa najitapa kwa rafiki zangu kuhusu mapenzi yangu na Sam roho iliniuma sana, jinsi nilivyokuwa nikiwaeleza kuwa hakuna cha kunitenga na Sam, jinsi ambavyo nilimsifia Sam kuwa mwanaume wa kipekee na tofauti na wanaume wengine. Mwanaume mpole na mwaminifu, leo kanisaliti tena na rafiki yangu kipenzi machozi yalinitoka kama maji.

Wakati nalia pale na kuomboleza, nilihisi mtu akinishika bega kumtazama alikuwa ni Carlos, nilimuangalia tu kwani kichwa chote kilikuwa kinaniuma sababu ya kulia sana.
"Umejuaje kama niko hapa?"
"Nimehisi tu Sabrina, tafadhari turudi nyumbani. Naomba nikurudishe kwenu Sabrina."
Niliendelea kutoa machozi huku Carlos akinibembeleza.
"Sitamani kurudi nyumbani Carlos bora nikae hukuhuku hadi nife."
"Tatizo ni nini Sabrina?"
"Wanaume ni watu wabaya sana, wanaume ni mashetani siamini kama Sam angeweza kunifanyia hivi, yani kunisaliti na rafiki yangu siamini."
Carlos aliendelea kunibembeleza pale na kunisihi nirudi naye nyumbani, nilipokubali akaenda kunipakiza kwenye gari yake na kunipeleka kwetu.

Kufika nyumbani, mama akamshukuru sana Carlos kwa kunirudisha. Sikuweza kuongea chochote na mama kwani kichwa kilinigonga sana sababu ya kulia.
Nilienda moja kwa moja chumbani kwangu na kujitupa kitandani huku nikifikiria mengi kumuhusu Sam.

Nikakumbuka jinsi nilivyoanza mahusiano na Sam, alikuwa bado anaishi kwao na wazazi wake. Ndugu zake walikuwa wakimsema sana kuwa atategemea wazazi hadi lini wakati ameshakua, Sam alikuwa analalamika kwangu kwani hakujua cha kufanya.
Mimi ndio nikamshauri apange chumba na vitu vingi ndani alinunua kwaajili yangu, nilikuwa nachukua pesa nyumbani na kumpelekea ya matumizi kipindi baba yupo kwani ndiye aliyekuwa na pesa nyingi kutokana na kazi yake tofauti na sasa hayupo na tumeanza kufilisika.
Na kazi anayofanya sasa ni kwa msaada wangu kwani waajiri wake walitaka atoe kitu kidogo (Rushwa) kwanza ila Sam hakuwa na pesa kipindi hicho, nikachukua pesa ya ada na kumpelekea halafu nyumbani nikasema nimeibiwa. Mama alinisema sana na kulalamika sana lakini sikujali kitu ilimradi Sam afanikiwe tu, na kweli Sam alifanikiwa na kupata kazi ya kuajiriwa tena ajira ya kudumu.
Halafu leo hii ananisaliti kwa rafiki yangu kipenzi! Iliniuma sana, kwani sikutarajia kabisa kuwa ipo siku Sam angefanya alivyofanya.
Wakati nawaza, Sam naye akawa anapiga simu yangu sikuipokea na nikaizima kabisa kwani sikutaka kuongea nae.

Nililia usiku kucha kwani sikuweza kulala kabisa, kila nikigeuka usingizi ola haukuwepo kabisa.
Asubuhi macho yangu yalikuwa yamevimba sana.
Dada yangu Penina alikuja chumbani kwangu kuniuliza, nikamuelezea kila kitu kilivyokuwa.
"Hutakiwi kuwa na hasira hivyo mdogo wangu, utajiumiza bure. Naimani Sam anakupenda sana na kama hicho kitu kimetokea kweli basi kuna sababu. Huwezi jua labda alilazimishwa"
Sikuweza kuchangia neno kwani niliona dada nae akinichanganya tu.
"Punguza hasira mdogo wangu, badae kuna mahali tutaenda kutembea. Acha kulia tafadhari, usiwaze sana kuhusu Sam. Nipo mimi na yupo mama tunakupenda sana Sabrina."
Nikamuomba kitu kimoja tu dada kuwa asimwambie mama ukweli kwani najua mambo yake.

Mchana nilitoka na dada, akanizungusha sehemu mbali mbali ili tu nifurahi na badae tukarudi nyumbani.
"Kesho tena tutaenda kutembea kuanzia asubuhi hadi jioni. Sawa mdogo wangu"
"Sawa"
Ila mawazo yangu yalikuwa kwa Sam tu bado.
Nikaenda kuwasha simu yangu kwani tangia nilivyoizima usiku wa jana.
Zikaingia meseji mfululizo kutoka kwa Sam, zingine akiniomba msamaha, zingine akitaka tuonane ili anieleze ilivyokuwa.
Nikajifikiria sana kuwa Sam ana nini cha kunieleza, uongo gani anataka kuutunga hapo na wala sikupata jibu na sikuzijibu zile meseji zake wala nini na alipopiga sikupokea.
Leo nilipokaa kitandani nikapitiwa na usingizi.

Nikamuona yule mkaka wa ndotoni akifurahi na kucheza sana, huku pembeni Sam akiwa analia na kunisihi nimsamehe kwani hajafanya kosa lolote.
Nikashtuka usingizini, nikachukua simu na kutaka kumpigia simu mara ile simu ikaonyesha kuwa haina chaji na kuzima, nikainuka ili niichomeke kwenye chaji kwanza.
Wakati naichomeka kuna mkono wa baridi ukagusa mkono wangu na kufanya nishtuke na nisifanye chochote, nikajisemea kimoyomoyo.
"Wewe ni nani?"
Mara nikasikia sauti ya kiume ikicheka tena ikicheka sana, hapo nikaanza kujawa na uoga tena. Sauti Ile ikanyamaza, mara gafla simu nayo ikawaka ikiwa mkononi mwangu na kujionyesha kuwa chaji imejaa, nikawa naogopa na simu ikaanza kuita kuangalia namba ni tofauti na ya ajabu sijawahi kuona namba kama ile, nikaitupia kitandani huku hofu na uoga vikinitawala.
Niliiacha iite hadi ikatike, nikatamani nitoke chumbani kwangu na kukimbilia kwa mama ila niliogopa kwavile nilisikia sauti za watu nisiowafahamu zikizungumza sebleni, nikawa nimejikunyata bila ya kujua cha kufanya. Sauti ikasikika,
"Kwanini unapenda kujitaabisha Sabrina?"
Nikawa natetemeka, nikaona mtu akishuka toka dalini taratibu na kiti kirefu huku yeye akiwa amekaa nikapiga kelele huku nimejiziba sura.
"Mamaaaaaaaaaa.........."
Mama na dada walikuja chumbani kwangu na kunikuta nimejikunyata, mama akanichukua na kwenda kulala chumbani kwake.
Huko nikalala hadi asubuhi.

Dada alinihimiza nijiandae ili twende ile safari, nikajiandaa na kuondoka na dada pale nyumbani.
Kama kawaida yake ya kupenda ofa, akanipeleka sehemu ambayo ameitwa kwaajili ya ofa na huko akanywa sana huku akifurahia maisha ya aina ile.
Nikaaga kuwa naenda chooni, ile kufika mlango wa choo nikamuona mtu kama Sam akiwa amesimama. Nikashtuka sana kuwa Sam anafanya nini pale, nikamuita "Sam"
Akageuka na kuniangalia kisha akaondoka, nikabaki nashangaa na kurudi alipo dada.
Kwavile muda ulikuwa umeenda sana nikamuomba dada kuwa turudi nyumbani kwani sikuweza kuendelea kubaki eneo lile, nilitaka nifike nyumbani ili nimpigie simu Sam na kumuuliza kuwa alikuwa anafanya nini pale.

Tukapanda daladala na dada ili tuweze kurudi, wakati tumekaa nilimuona tena Sam akiwa kiti cha mbele nikajiuliza kuwa Sam ananifatilia au ni kitu gani kwani alikuwa na nguo zile zile nilizomuona nazo mwanzo.
Nikasogea hadi alipokaa na kumshtua kwa nyuma "Sam"
Akageuka na kuniangalia, alikuwa ni Sam kabisa ila hakusema chochote na kushuka gari iliposimama, nikashangaa sana kuona Sam amekuwa vile yani kukosea akosee yeye na kununa anune yeye.
Tulipnfika kituoni mi na dada tukashuka na kuelekea nyumbani, huku mawazo mengi yakinitawala kichwani.
Kufika nyumbani tukamkuta Sam akiwa amelala mlangoni kwetu, mama akatoka ndani na kusema.
"Yani huyu kijana kaniletea malimwengu leo maana tangia asubuhi yupo hapohapo hataki hata kuondoka."
Nilipatwa na mshangao wa hali ya juu kwani nguo alizovaa ndio zilezile nilizomuona nazo.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 15


Nikapatwa na mshangao wa hali ya juu kwani nguo alizovaa ndio zilezile nilizomuona nazo mwanzo.
Nikawa namuangalia kwa makini zaidi na kujisemea,
"Jamani huyu sio Sam"
"Kama sio Sam ni nani sasa?"
Sam akaamka pale chini na kutaka kunisogelea huku sura yake ikiwa imejawa na simanzi, alikuwa ananisogelea huku akipepesuka nikamkwepa nae akaanguka chini.
"Nisamehe Sabrina, nahitaji kuzungumza nawe mamangu."
Nikakimbilia ndani kwani sikutaka kuamini kabisa kama yule ni Sam, nilihisi yule mkaka wa ndotoni akinifanyia mchezo.

Dada akanifata ndani ambako nilikuwa nimejiinamia.
"Sabrina, nenda ukamsikilize mwenzio huwezi jua ana kipi cha kukueleza."
"Dada, wewe hujui tu kinachoendelea. Nakwambia mimi yule sio Sam."
"Sasa kama sio Sam ni nani?"
"Sijui ila yule sio Sam na mwambieni aondoke kabisa hapa nyumbani sitaki kumuona."
Sikukubaliana na moyo wangu kabisa kama yule ni Sam, najua Sam ananipenda sana ila sio yule na haiwezekani nikutane na Sam watatu kwa siku moja.
Nikamshangaa mama nae akija kunibembeleza kwa mara ya kwanza kuhusu Sam.
"Sabrina mwanangu, kwakweli mimi ni namba moja kumchukia Sam humu ndani ila anatia huruma pale nje tafadhari nenda ukamsikilize."
"Mama sikia, yule sio Sam kwanini hamtaki kunielewa jamani!"
Ikabidi niwe mkali sasa kwani walikuwa hawanielewi kuwa ninamaanisha nini.

Sikutaka kutoka nje tena, mama na dada nao wakaingia ndani huku wakidai kuwa wamemuacha Sam nje.
Roho ya huruma ilinitembelea ila bado nikapingana na moyo wangu kuwa yule sio Sam ninayemjua mimi. Dada akaniuliza tena.
"Inamaana Sabrina humpendi tena Sam?"
"Sam nampenda sana tena sana ila yule wa nje sio Sam"
Ikabidi dada aniache niamini kama ninavyoamini.

Tukaenda kulala, leo niliamua kulala na mama kwani niliogopa yale mauzauza ya kumuona Sam mahali tofauti.
Mama alilala hoi kabisa ila mimi nilikuwa macho, sikupata usingizi hata kidogo kwani mawazo mengi yalinitawala.
Nilikuwa nikimuwaza sana Sam, nikasikia sauti ya Sam akilia nje ile sauti ilikuja na kuingia hadi masikioni mwangu nilihisi ikinikera sana.
Nikaamua kuinuka ili nikamwambie aondoke pale nje.
Nilipofungua mlango, sikumuona Sam tena na ile sauti ikakatika gafla akatokea paka mweusi sana mwenye macho makali kama taa ya gari alikuwa akinisogelea, uoga na hofu vikanijaa na kubamiza ule mlango huku natetemeka.
Nilipogeuka ili kurudi chumbani, nikamuona tena yule paka mbele yangu hapo ndipo ujanja ulinishinda. Nilitamani kupenya kwenye mlango, nilihisi kuchanganyikiwa kabisa. Nikaanza kupiga kelele za kumuita mama.
"Maaamaaaaaa........."
Mama alikuja mbio,
"Kuna nini mwanangu kuna nini?"
Alinikuta nikitetemeka sana na yule paka alitoweka, nikamkimbilia mama na kumkumbatia.
"Ulikuwa unatoka kumuangalia Sam?"
Mama akataka kwenda kufungua mlango tena, nikamzuia na kumsihi turudi chumbani.
Kufika chumbani nikamuomba mama tusali kwanza, tukashikana mikono ili kufanya maombi ila gafla kila mmoja alikuwa kitandani amelala.

Kulipokucha, mimi nilijikuta chumbani kwangu nimelala. Hapo nikaamka na kutoka ambapo nilimkuta mama sebleni.
Mama akaanza kuniuliza maswali kwani na yeye alishapatwa na mashaka.
"Hivi kwanini tukitaka kusali tunajikuta tumelala?"
"Hata mimi sielewi ni kwanini mama."
"Haya mambo ni makubwa jamani tena ni makubwa sana, hata sielewi kwanini inakuwa hivi. Itabidi nitafute ufumbuzi juu ya hili swala"
"Itakuwa vizuri mama."
Nilishukuru kuona mama nae amepatwa na mashaka juu ya yanayotokea nyumbani kwetu.

Mchana wa leo nilitembelewa na Suzy, nilifurahi sana kupata wa kumueleza kilichonisibu.
Nilikaa nae na kuongea mambo mengi sana, nikamueleza mambo ambayo Lucy amenifanyia. Suzy akanionea huruma sana.
"Ila mimi nilikwambia Sabrina kuwa Lucy si mtu mzuri wewe hukunielewa"
"Sasa nimekuelewa Suzy ila sijui la kufanya kwani Sam bado nampenda."
Suzy akanishauri kuwa twende nyumbani kwakina Lucy ili tukaongee nae.
"Unadhani nitaweza kuongea na Lucy baada ya yote yale?"
"Usijali Sabrina, mimi ndio nitaongea nae. Lucy ni wa kusemwa, bila ya hivyo hawezi kuacha yule. Ni rafiki yetu na lazima tumseme kwa tabia yake mbaya."
Swala la kumuona Sam kwa utatanisho sikumwambia Suzy kwani sikutaka ashtuke.
Suzy akaniombea ruhusa kwa mama kuwa tunatoka kidogo kisha tukaondoka na safari ilikuwa ni kwakina Lucy.

Kufika kwa kina Lucy, tulifunguliwa mlango na mdogo wake Lucy aliyeitwa Maria naye akatuambia kuwa Lucy ametoka kidogo. Suzy akampachika swali,
"Ameenda wapi?"
"Kuna mgeni wake ameenda kumpokea."
Tukaona vyema tukae pale nje kumngoja, Maria akatutolea viti na tukakaa.
"Sabrina wewe usiwe na wasiwasi wowote ilimradi upo na mimi kila kitu kitaenda sawa bhana."
Nikaitikia kwa kichwa kuonyesha kuwa nimeelewa, wakati naendelea kuongea na Suzy nikajikuta nikitazama njia inayokuja kwakina Lucy, nikamuona Lucy ameongozana na Sam wanakuja.
Kwakweli moyo wangu ukalia paaa, nilipatwa na ugonjwa wa tumbo gafla kwani sikuweza kuamini kama Sam bado anaendeleza mahusiano na Lucy.
Nikamwambia Suzy awaangalie, Suzy aliwatizama kisha akaniangalia mimi kwa huruma.
Wakazidi kusogea pale tulipokuwa, nikajikuta nikisimama yani nilijihisi kama vile nimechukua msumari wa moto na kuushindilia kwenye kidonda changu kibichi.
Walipofika, nami nikaanza kuondoka. Suzy akanirudisha nikagoma, Sam nae akanikimbilia.
"Sabrina usifikirie unachofikiria tafadhari, hakuna chochote kati yangu na Lucy"
Sikutaka kusikia na kuondoka kabisa, kufika kituoni ikapita gari ya mtu anayenijua na kusimama kisha akaniita niende kupanda, kuangalia alikuwa ni Carlos nami nikapanda ile gari.
"Umetokea wapi na unaelekea wapi Sabrina?"
"Naelekea nyumbani."
Nilijibu huku machozi yakinitoka, Carlos akatoa leso na kunikabidhi kuwa nifutie machozi.

Carlos alinipeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwetu kisha akaniambia.
"Ukiwa na tatizo usisite kunipigia simu, niambie nami nitakutatulia."
Halafu akaondoka zake na kuniacha mimi nikiingia ndani.
Simu yangu ikaanza kuita, kuangalia mpigaji ni Suzy.
"Sabrina mbona unakuwa na hasira kiasi hiko?"
"Hujui maumivu yangu Suzy na ndiomana unauliza hivyo."
"Acha mawazo finyu Sabrina, unatakiwa kukaa chini na Sam ili uzungumze nae."
"Sitaki kuzungumza nae kwakweli"
"Tafadhali Sabrina, kesho nitaandaa mahali ya wewe kuweza kuzungumza na Sam."
Nilimuitikia tu ila sikuafiki hata kidogo kuhusu hilo swala la mimi kuzungumza na Sam wala nini nikafikiriaa mambo mengi huku nikitawaliwa na mawazo mengi zaidi.

Usiku wa leo pia nilienda kulala kwa mama kwani niliona kwangu kukiwa na maumivu zaidi na mambo mengi ya kunitia uoga.
Wakati tumelala, nikahisi kama mtu akiniamsha kwa kunishika mgongoni kisha nikashtuka wala nisielewe kinachoendelea, mara nikaona matone ya maji yakinirukia kama vile kuna mvua au mtu ananimwagia.
Tukio hili likanipa uoga sana, nilitamani kufanya maombi ila kuna roho nyingine imekazana kunizuia kufanya maombi ya aina yoyote ile.
Yale maji maji yakaacha kunimwagikia gafla ila nikahisi mtu akigonga chumbani kwa mama, nikajua kwa vyovyote vile ni yale mambo ya ajabu tu, mara nikaanza kumsikia mtu akicheka tena anacheka kama vile kuna kitu anafurahishwa nacho sana.
Nikamuamsha mama na kumwambia kuwa na yeye asikie ile sauti ya kucheka ila yeye alijibu kuwa hasikii chochote.
"Punguza maruweruwe mwanangu, ila yote haya yana mwisho wake usijali"
Mama akalala, nami nikajaribu kufumba macho nikamuona yule paka mweusi wa jana kwenye mlango wa mama.
Nikapiga tena kelele, mama akaamua kuamka kabisa ingawa yeye hakuona kile nilichokiona. Akaamua kuanza maongezi na mimi ingawa ilikuwa ni usiku nikaongea nae hadi kunakucha.

Mawazo hayakuacha kutawala kichwa changu, Suzy akanipigia simu na kuniambia kuwa ni siku hiyo natakiwa kuonana na Sam kisha akanitajia mahali pa kukutana nae ili niweze kuzungumza nae kuhusu tofauti zetu,
"Je na wewe utakuwepo?"
"Ndio nitakuwepo hata usijali, nakuomba uwahi tafadhari."
Nilikubali kishingo upande tu kwani moyo wangu ulikuwa mzito sana kuhusu hiyo safari.

Nikamuaga mama na kuondoka nyumbani, kufika njiani yani kabla sijafanya chochote alipita Carlos na gari yake na kunipa lifti, humo akaniuliza maswali kadhaa nami nikamjibu kuwa naenda kuonana na Sam.
"Yani kwa mambo yote yale aliyokutenda bado una moyo wa kuonana nae? Kweli unampenda jamani."
Nilimuangalia tu Carlos bila ya kumjibu chochote, kufika karibu naeneo nililotajiwa nikamuomba Carlos anishushe.
Niliposhuka nikaanza kuelekea mahali nilipoambiwa huku nikitarajia kumuona Suzy na Sam eneo lile.
Kufika pale nikapatwa na mshtuko kwani Sam walikuwa wawili na walisimama mbele yangu, mmoja alinuna na mwingine alitabasamu.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 16


Niliposhuka nikaanza kuelekea mahali nilipoambiwa huku nikitarajia kumuona Suzy na Sam eneo lile. Kufika pale nikapatwa na mshtuko kwani Sam walikuwa wawili na walisimama mbele yangu, mmoja alinuna na mwingine alitabasamu.

Nilipatwa na mshtuko wa hali ya juu kwani sikutarajia hata kidogo. Nikajikuta nikitetemeka na hofu kunitawala zaidi, mara yule Sam aliyekuwa akitabasamu akaninyooshea mkono kama ishara ya kuniita kwakweli hapo uoga ulinishika zaidi nikatamani iwe ni ndoto lakini ilikuwa ni kitu cha kweli kabisa kuwa Sam walikuwa wawili na mmoja wapo aliniita, nikageuka nyuma ili nianze kukimbia ile nageuka tu namuona Sam mwingine aliyekuwa nyuma yangu, nilitetemeka sana na kuanguka chali kichwa changu kiligonga kitu kama godoro nikashangaa kuwa godoro limetokea wapi mahali pale, nikajigeuza kuangalia na kuona kwamba nilikuwa nimemuangukia Sam, nikazidi kutetemeka kwani mtu gani awezae kudinyadinya kama godoro na ubaya zaidi ni mpenzi wangu Sam ambaye namjua sana kupita maelezo ya kawaida, niliinuka gafla na kukimbilia kusikojulikana ila nilijikuta nikitokea stendi huku nikihema sana na jasho jingi kunitoka. Wakati nimesimama pale stendi kuna mtu akanishika bega, nikaogopa hata kugeuka na kumuangalia usoni kwani nilijua wazi kuwa ndio yale mauzauza. Yule mtu akaja mbele yangu, kumbe alikuwa ni dada yangu Penina na hapo nikapumua kidogo.
"Mbona unahema hivyo Sabrina? Unatokea wapi?"
Hata kumjibu nilishindwa na dada akatambua kama nimepoteza dira, hivyo akanishika mkono huku tukisubiri usafiri wa kurudi nyumbani. Ikaja gari na kusimama karibu yetu, nikaijua mapema kama ni gari ya Carlos kwani imekuwa ikinibeba mara nyingi sana. Carlos alishuka kwenye gari na kutuomba tupande ili atupeleke tuendako na hakukuwa na swali la kumuuliza zaidi ya kupanda lile gari.
Carlos aliendesha lile gari hadi nyumbani kwetu, hapo mi na dada tukashuka kisha nikaingia ndani bila kusema chochote na kumuacha dada akimuaga Carlos pale nje. Kuingia ndani mama alikuwa sebleni ila hakuniuliza chochote, nami nikapitiliza hadi chumbani kwangu moja kwa moja kitandani na kulala ili kuipumzisha akili yangu kwani ilishapoteza dira.

Nilipoamka, giza lilikuwa limeshaingia tayari nikaamua kutoka nje ili nikanawe japo uso na kujinyoosha. Nikamkuta mama na mama Salome wapo sebleni, baada ya salamu mama akaniomba nikae na kuniambia kuwa mama Salome ana maongezi na mimi. Nikakaa kumsikiliza kuwa ana lipi jipya naye akaanza kuzungumza nami.
"Sabrina"
"Abee"
"Kwakweli wewe Sabrina ni kama mwanangu, niwaonavyo wakina Salome nawe nakuona hivyohivyo. Kwajinsi unavyoteseka mimi kama mzazi naumia sana wakati njia za kukusaidia zipo."
Hapo nikadakia kwa haraka ili nijue,
"Njia gani hizo?"
"Njia kubwa ni moja tu mwanangu, nayo ni maombi" "Mmmh!!"
Nikaguna hapo, naye akaniuliza.
"Mbona unaguna Sabrina?"
"Naguna hayo maombi, mara nyingi huwa tukitaka kusali na mama hujikuta tumelala."
Mama nae akaingilia kati.
"Ndio maana mama Salome amekwambia kuwa una tatizo na inahitajika maombi kwahiyo msikilize kwanza."
Nikaendelea kumsikiliza mama Salome na zile habari zake. "Kesho nitakuja kukufata na kukupeleka kanisani kwetu, mchungaji wetu ni muombeaji mzuri sana na tatizo lako litaishia hapo."
Ikabidi niitikie na kukubaliana nae kwani hata kama ningekataa nisingeweza kumkatalia mama na pia ingeonekana kuwa lile tatizo nalipenda wakati silipendi. Baada ya muda kidogo mama Salome akaaga na kuondoka, nami nikabaki na mama huku nikianza kumuuliza.
"Mama, si ulisema kuwa makanisa ya ajabu ajabu huyataki? Sasa mbona umemkubalia mama Salome?"
"Nakuhurumia wewe mwanangu, yote haya ni kwaajili yako unavyoteseka wewe mi naumia mwanangu."
Basi tukaongea mawili matatu na mama kisha kula na kwenda kulala.

Nilipokuwa nimelala nikamuona mama Salome akivuka barabara mara kuna gari ilikuwa ikimfata kwa kasi sana kisha ikamgonga, kumuangalia dereva ni yule mkaka wa ndotoni ila gari ilifanana na ile ambayo Carlos huwa anaiendesha kisha yule mkaka akaniangalia na kutabasamu, nikawa nimesimama na kushikwa na bumbuwazi kisha watu wakajaa pale alipogongwa mama Salome na yule mkaka akashuka kwenye ile gari ila akawa na sura nyingine kabisa si ile ya ndotoni wala Carlos nikawa nashangaa tu na sikuweza kusogea eneo la tukio, nikiwa nashangaa yule mkaka aliyegonga akageuka kwangu na kuanza kunifata kisha akanishika bega na mara sura yake ikageuka na kuwa yule mkaka wa ndotoni halafu akatabasamu na kuanza kunitingisha hapo ndipo niliposhtuka vibaya sana kwani nilihisi kuna mtu ananitingisha kweli. Nikaamka na kukuta ni dada Penina anayenitingisha nikaropoka palepale.
"Mama Salome kapata ajali"
Dada akawa ananishangaa kwa kile nilichokisema.
"Unamatatizo gani wewe Sabrina?"
Nikamuangalia tu dada yangu Penina kwani sikujielewa na ile ndoto, dada akaendelea kuongea.
"Nimekuja kukuamsha maana umelala sana hadi unaanza kuwaotea watu mambo mabaya. Haya amka hapo twende kufanya kazi."
Nikainuka huku nikijisemea mwenyewe kuwa ndio tabu ya dada asipoenda kazini anapenda kumshurutisha mtu tu.
Nikamkuta mama sebleni, nikamsalimia na kwenda jikoni alipo dada halafu mama nae akatufata jikoni mara mlango ukagongwa halafu akaingia mkaka flani ambaye ni ndugu wa mama Salome, alifika akiwa anahema sana tena bila salamu akasema.
"Mama Salome amepata ajali"
Dada Penina aliyekuwa anapanga vyombe aliacha na kunitazama kisha nami nikamtazama halafu akasema.
"Umeona sasa Sabrina?"
Mama akatushangaa na kuuliza,
"Kuona nini tena?"
Sikujibu chochote bali niliwaacha na kwenda chumbani kwangu huku maswali mengi yakinitawala, nilijikuta nikisema "Mungu wangu msaidie mama Salome asife"
Nilikosa amani kwani nilijihisi mkosaji na nilijiona kamavile mimi ndio chanzo cha yote.
Mama alienda alipoambiwa kuhusu mama Salome kisha dada akaja chumbani kwangu na kuniuliza.
"Ulikuwa na maana gani uliponiambia asubuhi kuwa mama Salome kapata ajali na halafu ni kweli? Je unajua chanzo cha ajali yake?" "Sijui chochote dada"
"Kuwa makini na maneno yako Sabrina"
Kisha akainuka na kutoka chumbani kwangu, maneno ya dada nayo yalikuwa yakinichanganya tu kwani sikumuelewa ni umakini gani anaouongelea.
Nikiwa bado nimetulia chumbani, simu yangu ikaita kuangalia ni Suzy anapiga ila sikupokea, mara akanitumia ujumbe mfupi, "Niko njiani na Lucy tunakuja kwenu"
Pia sikujibu huo ujumbe, nikaangalia tu na kuupuuzia kisha nikaendelea na mawazo yangu mara nikasikia sauti ya mama akiita kwa nguvu sana.
"Wee Sabrina wee"
Ikabidi nitoke na kwenda kumsikiliza.
"Jiandae haraka haraka twende hospitali kumuona mama Salome huko maana njia nzima anakutaja wewe."
Ikabidi nijiandae bila kuuliza chochote na kuanza kuongozana na mama kwa safari ya kwenda huko hospitali aliposema.


Tukiwa njiani kuelekea hospitali ilipita gari ya Carlos na kutupa lifti kama kawaida yake, akatupeleka hadi hospitali alipolazwa mama Salome. Kwakweli hali ya mama Salome ilikuwa mbaya sana ila bado alihitaji kuzungumza na mimi, nikamsogelea karibu kisha nikainama kumsikiliza naye akaongea kwa shida sana sababu ya maumivu.
"Mapambano ni makali sana mwanangu unatakiwa....." Akaanza kupiga makelele kwa maumivu, daktari akaja na kutuamuru kuwa tutoke nje ili wamuhudumie. Bado nilijiona kuwa mimi ndio chanzo cha mambo yote, mama akaniambia. "Usiwaze sana mwanangu hii ni mipango ya Mungu tu na huwezi jua kwanini imekuwa hivi. Je mama Salome alikuwa anakwambia nini?"
"Kaniambia kuwa mapambano ni makali sana, kwakweli mama mi naogopa jamani hata sielewi kitu" "Usijari mwanangu yote haya yataisha"
Wakati naongea na mama pale akatufata Carlos na kudai kuwa ana mazungumzo nami kidogo. Nikamfata kwenda kumsikiliza.
"Kwakweli Sabrina una matatizo na unahitaji msaada wa hali ya juu"
"Ni kweli nina matatizo ila wewe umejuaje?"
"Nimejua tu Sabrina, na kama utahitaji msaada wangu basi usisite kuniambia"
Mara akaja Salome yani mtoto wa mama Salome kisha akatusalimia pale na hapo hapo Carlos nae akaaga na kuondoka kisha Salome akaanza kuniuliza.
"Huyu mkaka aliyetoka hapa ni nani yako?"
"Ni rafiki yangu tu dada"
"Unamjua vizuri?"
"Kiasi tu dada, kwani vipi?"
"Mmmh!?" "Mbona unaguna dada?"
"Hamna kitu mdogo wangu ila simuamini kwakweli"
"Kwanini humuamini dada?"
Mara mama akaja kuniita na kuniambia kuwa twende tukamuage mama Salome na kurudi nyumbani.

Tukaongozana na mama hadi kwenye wodi aliyolazwa mama Salome, kufika mlango nesi akatuzuia kuingia.
"Jamani ustaarabu ni kitu muhimu sana, muda wa kuona wagonjwa umeisha na kama muonavyo hakuna hata mtu mmoja wa kuona wagonjwa wodini, naomba muende na mrudi tena kesho"
Mama akajaribu kujitetea ili waturuhusu.
"Tunataka kumuaga tu mgonjwa wetu, tafadhari nesi"
"Hata kama, muda wa kuona wagonjwa umeisha, mimi nafata taratibu za kazi tafadhari naomba muende"
Ikabidi tukubaliane na nesi na kuanza kuondoka, tulipokaribia kutoka nje kabisa ya hospitali tukamsikia yule nesi akituita kwa nguvu, tukasimama na kisha akauliza.
"Kuna Sabrina kati yenu hapo?"
Nikaitika, ndio mimi hapa.
"Samahani, mgonjwa anaomba kuzungumza na wewe kidogo" Mama akauliza,
"Si ulisema muda umeisha wewe! Vipi tena?"
"Aah! Samahani mama, hii ni kwa taadhari tu."
Ikabidi niongozane na mama ambaye aliishia nje ya wodi akiongea na yule nesi na kuniacha mimi niingie mwenyewe wodini. Nikaingia na kwenda hadi alipo mama Salome ila kufika pale nilishtuka sana na kuanza kupiga makelele kwa uoga.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 17


Nikaingia na kwenda hadi alipo mama Salome ila kufika pale nilishtuka sana na kuanza kupiga makelele kwa uoga kwani nilimuona yule mkaka wa ndotoni amesimama karibu na kitanda cha mama Salome halafu akaanza kunifata huku sura yake ikiwa inatisha sana leo.
Kelele zile zilimshtua kila mtu aliyekuwepo eneo lile kiasi kwamba kila mmoja alishtushwa na kuanza kuja eneo la tukio ila mimi nilikuwa nakimbia na kutoka wodini kama vile chizi.
Mama akanidaka mlangoni, jasho jingi lilinitoka na kuanguka palepale aliponidaka mama na kuzimia.

Nilipozinduka nilijikuta nikiwa kwenye chumba cha daktari na mama, ambapo mama aliandikiwa dawa ambazo nilitakiwa niende kuzitumia nyumbani kisha mama akanishika mkono na kuanza kuondoka eneo lile la hospitali.
Kufika nyumbani, mama akaanza kumuhadithia dada Penina mambo yaliyojiri hospitali.
"Mwenzangu, mdogo wako leo ule uchizi wake si umemuanzia hospitali loh ilikuwa balaa nakwambia"
"Huyu anahitaji tiba mama maana hali yake inasikitisha"
Mama akamwambia dada kila kilichotokea kule hospitali.
"Hivi ninavyokwambia, Sabrina amezuiliwa kwenda tena kumuona mgonjwa kwahayo yaliyotokea."
Nilikuwa kimya kabisa kamavile siwasikilizi ila moyoni mwangu iliniuma sana.
Muda wa kulala ulipowadia tulienda kulala na hapo nikalala na mama kwani niliogopa mauzauza yale ya hospitali.

Nikiwa nimelala na mama, nikasikia sauti toka sebleni ikiita jina langu.
"Sabrina, Sabrina"
Nikaanza kuogopa maana kwetu wote tulikuwa tumelala, sasa ni nani awezaye kuniita vile usiku ule.
Ile sauti ilianza taratibu ila badae ikawa inaita kwa nguvu hadi kunishtua zaidi, nilipoisikilizia kwa makini nikajua ni sauti ya Sam hapo ndio hofu ilizidi ukizingatia huyu Sam nimekuwa nikimuona mara mbilimbili.
Mara mlango wa chumbani kwa mama ukafunguliwa, na hapo ndipo nikaanza kupiga kelele za uoga huku nikimuamsha mama.
Mama aliposhtuka nilimueleza kuwa kuna mtu ananiita, mama akainuka na kuwasha taa kisha akaenda kuangalia sebleni akiwa ameongozana na mimi ila sebleni hapakuwa na chochote kile.
"Acha uoga mwanangu, si unaona mwenyewe hakuna chochote huku ni maruweruwe yako tu. Twende tukalale halafu kesho tutajua cha kufanya"
Nilikubaliana na mama huku uoga bado ukiwa umenitawala sana moyoni mwangu.
Asubuhi na mapema nikaamka wakati huo ambapo mama nae alikuwa ameamka, dada Penina alikuwa nyumbani na leo kwani ilikuwa ni mapumziko.
Tukafanya kazi za hapa na pale kisha dada akaniuliza.
"Mbona una roho mbaya kiasi hicho Sabrina?"
"Nimefanyaje kwani dada?"
"Yani wewe jana marafiki zako walikwambia watakuja hata kuwajibu loh! Na ulivyo na makusudi ukaondoka na kuacha simu hapa nyumbani ili wasikutafute, tabia mbaya hiyo."
Hapo ndio nikakumbuka kuwa Suzy alinitumia ujumbe kuwa yeye na Lucy wanakuja nyumbani.
"Kwahiyo walikuja dada?"
"Kama wasingekuja ningejuaje miadi yenu? Walikuja hapa, wakangoja hadi kuchoka na kuamua kuondoka. Tabia mbaya hiyo mdogo wangu, utakosa marafiki wazuri kwa upumbavu wako. Na ubaya ni kuwa kila wakipiga simu yako tukasikia ikiitia ndani na kujua kuwa uliiacha, itakuwa ulifanya kusudi wewe."
Hapo nikajifikiria sana na kukumbuka kuwa kweli simu niliiacha chumbani kwangu, hivyo nikaenda kuichukua nione.

Nikakuta ujumbe wa kutosha toka kwa Suzy na wote ukibeba lawama mwanzo mwisho, nikawaza cha kujitetea kwa haraka na nikaona ni bora kuwaeleza kuwa hata ule ujumbe wa mwanzo sikuuona nilikuwa tayari nimeshaenda huko hospitali.
Nikamtumia ujumbe Suzy kisha nikampigia simu kumuomba msamaha.
"Kwakweli Sabrina umenikera sana, hata hujui tulikuwa tunakuja kwasababu ipi jamani. Ilikuwa ni mambo ya kukusaidia wewe mwenyewe lakini umetupuuzia. Poa bwana, sie tushakusamehe."
Msamaha wa Suzy ulitoka ilimradi tu ili yaishe.
Mchana wake alikuwa kaka Deo ambapo alitukuta mimi na dada Penina kwani mama alienda hospitali kumuona mama Salome.
Tulifurahi sana kumuona kaka Deo na kuongea nae mambo mengi sana.
"Nia yangu kubwa ni kumchukua Sabrina tu maana wifi yake anamuulizia balaa"
Dada Penina akadakia.
"Inamaana wifi haniulizii mimi jamani!"
"Sio hivyo Penina, ila anajua wewe upo busy na kazi na huwezi kubali kuishi kule mbali na kazini kwako."
"Sawa nimekuelewa kaka, ila utamchukuaje Sabrina wakati mama hayupo?"
"Hilo ndio tatizo ila hakuna shida hata kesho naweza kumfata maana kuna project nafatilia inafanyika maeneo ya hukuhuku. Halafu kuna habari njema, sijui mama hajawaambia?"
"Habari gani hiyo kaka?"
"Wifi yenu ni mjamzito"
Kwakweli mi na dada tulifurahi sana kwa habari ile kwani ilikuwa njema kweli. Dada Penina alimpa sana hongera kaka Deo na mimi nikamwambia kaka.
"Yani kaka nina hamu kweli ya kubeba mtoto mchanga loh nitamleaje"
Dada Penina akadakia.
"Zaa wako na wewe"
Tukabaki kucheka tu huku tukimpongeza kaka, nikawa na hamu ya kumuona wifi na hiyo mimba yake. Dada Penina akasema,
"Natamani sana kumuona Joy na hiyo mimba loh sijui anafananaje jamani hahaha"
"Tena ina miezi saba kwasasa, mjiandae tu kuitwa na mashangazi na mama yenu kuwe bibi"
"Na wewe kuwa baba, Joy kuwa mama"
Wote tukacheka na kufurahi kisha kaka akatuga na kuondoka.
Mama aliporudi tukamuelezea uwepo wa kaka muda mfupi uliopita na kumwambia kuwa amesema atakuja kunichukua mimi kesho yake.
"Itakuwa vizuri maana hata mauzauza utayapunguza"
Dada Penina akadakia
"Atapunguza mauzauza? Wakati mwanao kawa mtabiri siku hizi."
"Mtabiri? Kivipi?"
"Unakupa siku mama Salome alipopata ajali?"
Mama akaitikia anakumbuka na hapo nikajua kuwa dada anataka kumwambia mama kuhusu nilivyomwambia kabla ya taarifa ya msiba.
"Basi mama, ile siku nilienda chumbani kwa mwanao kumuamsha moja kwa moja akaniambia kuwa mama Salome kapata ajali kabla hata ya taarifa kuletwa. Mwanao amekuwa mtabiri huyo."
Mama aliniangalia sana nadhani alikuwa akiyapima maneno ya dada, kisha akaniuliza.
"Eeh Sabrina mwanangu, ulijuaje"
Nikainama chini na kumjibu mama kuwa niliota tu.
"Kuotea watu mabaya si vizuri mwanangu, unaweza shikwa uchawi bila ya kutarajia"
"Kivipi mama?"
"Watu wanaweza kukushika uchawi bure mwanangu wakati hata uchawi kwetu haupo jamani"
Nikamsikiliza mama kwa makini na kumuelewa, kisha tukamuuliza habari za hospitali.
"Unajua jana muda umeenda kiajabu ajabu sana Sabrina, hata sijui ilikuwaje hadi muda wa kuona wagonjwa jioni ile ukatupita mmh!"
"Na nyie mna mauzauza sana, mtaua wagonjwa wa watu bila ya kutarajia?"
"Maneno gani hayo Penina?"
"Basi yaishe, tupe habari za mgonjwa anaendeleaje?"
"Anaendelea vizuri ila aliulizia sana uwepo wa Sabrina, sijui hata anataka kusema maneno gani ila ndo hivyo Sabrina kazuiliwa kwenda kule kwa muda."
Tukamgea mengi na kumuuliza mama kuhusu ujauzito wa wifi kuwa mbona hajatujulisha mapema.
"Mbaya kaka yenu, mi kama mama yake alitakiwa kuniambia mapema eti majuzi ndo ananipigia simu kunitaarifu kuwa mkewe ni mjamzito tena mimba kuwa kabisa ya miezi saba ila hata hivyo nilisahau kuwaambia."
"Hata huyo Joy nae ana tabia mbaya, kilichomfanya kushindwa kututembelea siku zote hizo nini?"
"Penina, usimlaumu sana maana hujui makubaliano yake na mumewe"
Ikabidi dada awe mpole kwani alishapoozwa na mama.

Mama akaniambia kuwa nianze kujiandaa kwaajili ya safari ya kwenda na kaka huko nyumbani kwake, nami sikusita nikaenda chumbani kwangu na kupanga baadhi ya nguo ambazo nitaondoka nazo na kwenda huko kwa kaka Deo.
Nikiwa chumbani napanga nguo, mara simu yangu ya mkononi ikaita kuangalia mpigaji alikuwa ni Sam, nikashtuka sana kwani Sam alikaa siku nyingi kidogo bila ya kunipigia simu.
Nikaamua kupokea ili kujua anachotaka kusema.
"Tafadhari Sabrina naomba tuonane"
"Sina muda huo Sam"
"Usinifanyie hivyo Sabrina, kumbuka wapi tumetoka, kumbuka jinsi gani nakupenda, kumbuka tunavyopendana Sabrana. Tafadhari nakuomba tuonane mpenzi."
Maneno ya Sam yaliniingia sana ila bado nikawa na mashaka na yale mambo ya kuwaona Sam wawili wawili.
"Kwanza nihakikishie kuwa Sam ninayeongea nae sasa ndiye Sam wa siku zote"
"Ni mimi Sabrina, kwani una Sam wangapi siku hizi? Inamaana hata sauti yangu umeisahau mpenzi? Tafadhari nielewe Sabrina"
"Poa, njoo karibu na maeneo ya nyumbani halafu utanishtua nitakuja ulipo."

Nikamaliza kuongoa nae na kuendelea na upangaji wa nguo zangu, baada ya muda kidogo Sam akanipigia simu na kunielekeza maeneo alipo na ilikuwa karibu na nyumbani kwetu.
"Upo mwenyewe au na mtu mwingine?"
"Nipo mwenyewe Sabrina, njoo utaniona mwenyewe"
Nikakata simu na kujiandaa kutoka pale nyumbani, nikamuaga mama kuwa naenda dukani mara moja.
"Usichelewe sana Sabrina, si unaona giza linakaribia kuingia!"
"Sawa mama sitachelewa"
Nikaondoka na kwenda eneo ambalo Sam amenielekeza kuwa yupo.
Nikiwa natokea nyumbani nikamuona Sam kwa mbali mahali alipo, mara nikamuona Lucy akitokea upande mwingine, nikaamua kujibanza kidogo ili niangalie picha itakwendaje.
Lucy alifika hadi mahali alipo Sam kisha wakakumbatiana, moyo wangu ulilia paaa kwa wivu kwani wivu ulinishika kupita kiasi ukizingatia si utamaduni wetu kuona mdada na mkaka wasiojuana kiundani zaidi wakikumbatiana.
Roho ikaniuma sana, Lucy akaongeza na mbwembwe zake pale kwani alimbusu Sam shavuni kwakweli nilitamani nikawatimue kwa viboko mahali pale.

Nikajitokeza na kuwafata ili wajue kama nimewaona, Sam aliponiona akamsukumia Lucy kwa pembeni kidogo.
"Unamsukuma wa nini? Nimeyaona yote mliyoyafanya hapo"
Sam akataka kuanza kujitete ila nikamkatisha.
"Subiri nikueleze ilivyokuwa Sabrina, ni...."
"Hakuna cha kunieleza Sam, kila kitu nakifahamu na hii leo umeamua kunithibitishia tu kuwa ni kweli mna mahusiano"
Lucy nae akataka kujieleza.
"Ila Sabrina na...."
"Tena wewe ndio unyamaze kabisa na umalaya wako, yani Sam katika wanawake wote ukaona bora unichanganye na huyu Lucy? Halafu leo ooh tuje tujadili mpenzi sijui nini na nini kumbe unafki tu"
"Jamani Sabrina usiseme hivyo!"
"Nisiseme hivyo kitu gani? Wakati wewe umeona ni vyema kuja kunionyesha kabisa kama upo na huyo malaya wako. Watazame sura zao zilivyo loh! Hamuoni haya wala kujihisi vibaya"
Kwakweli niliongea sana kwani hasira ilikuwa imenikaa kooni nikatamani hata kupigana na Lucy ila nikaona itakuwa ni ujinga tu.
Nikaamua kugeuza ili niondoke na kurudi kwetu, Sam akasogea na kunizuia kwa kunishika mkono ndio akawa kamavile ananipandisha mashetani kwajinsi nilivyoongea kwa ukari.
"Sam, niache! Nenda zako huko na Lucy wako, na usithubutu kunifatilia tena mjaa laana wewe usojua vibaya. Niache nakwambia."
Ikabidi Sam aniache kwani nilibadilika sana kwa wakati huo.
Nikatembea bila hata ya kugeuka nyuma kwa hasira, nilifika nyumbani na kujipangusa machozi kwanza kabla ya kuingia ndani ili mama asiweze kuniona kama nalia.
Niliingia ndani na kwenda chumbani kwangu moja kwa moja kwani uchungu niliopata ulikuwa ni wa kutonesha kidonda changu ambacho nilianza kukisahau maumivu yake yalivyo.

Nilikaa kitandani na kulia sana, nikaiona ile leso niliyopewa na Carlos kujifutia machozi, nikaichukua na kujifuta.
Ujumbe ukaingia kwenye simu yangu, kuangalia umetoka kwa Carlos.
"Ukiwa na tatizo lolote Sabrina usisite kuniambia. Nitakusaidia"
Nikausoma huo ujumbe mara mbili na kuuona hauna manufaa yoyote kwa sasa kwangu kwani moyo ulikuwa unaniuma sana kuhusu Sam na Lucy.
Mama akaniita kula ila nikamjibu kuwa nimeshiba, ukweli ni kwamba sikuwa na hamu ya chakula kabisa.
Usingizi ulinipitia mule mule chumbani kwangu, usiku wa manane nikasikia mtu akiniita toka sebleni na ikawa kama nilivyosikia jana yake. Uoga ukanishika sasa, mara mlango wa chumbani kwangu ukafunguliwa ila aliyeingia hakuonekana na mara nikaona ukifungwa.
Sauti ikaanza kusikika karibu sasa kuwa naitwa ila muitaji sikumuona, uoga ukanizidi.
Ile sauti ikasogea karibu na sikio langu na kusema.
"Sabrina si nakuita wewe mbona huitiki?"
Nikawa natetemeka kama nimewekewa barafu, mara nikaguswa na kitu kama mkono.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 18


Nikawa natetemeka kama nimewekewa barafu, mara nikaguswa na kitu kama mkono.
Hapo nilitamani hata kuzimia huku natetemeka kwa uoga zaidi na sikuweza hata kugeuka nyuma, mara simu yangu ikaanza kuita kwakweli nilishtuka sana na kutamani hata kukimbia.
Yale mauzauza ya uwepo wa mtu ndani yakapotea na kukawa shwari kabisa, kuangalia mpigaji ni Carlos nami nikapokea.
"Niambie Sabrina, nimelala nikaota kuwa una matatizo ndiomana nimekupigia"
"Ni kweli nina matatizo Carlos"
"Ila mimi najua jinsi ya kukusaidia, kama ukihitaji msaada wangu utaniambia."
Hapo ndipo Carlos alipokuwa akinichosha maana kama anajua cha kunisaidia si angenisaidia tu, yani yeye anangoja hadi nitake msaada ndipo anisaidie.
Nikaongea nae mambo mengi tu usiku ule na kuniambia kuwa kesho yake atakuja kunitembelea kwetu.
Baada ya maongezi na Carlos nikalala vizuri hadi kunakucha.
Maswali mengi nilijiuliza kuhusu Carlos kuwa ni mtu wa aina gani na ana maana gani kwenye maisha yangu.

Asubuhi niliamka na kuwa kama vile mtu nisiye na tatizo lolote lile.
Mama akaanza kunipa wosia wake.
"Ukienda huko kwa kaka yako upunguze mawenge mwanangu halafu uvivu acha"
"Mmh jamani mama, kwani mi mvivu!"
"Ndio, wewe ni mvivu mwanangu. Kumbuka wifi yako huko ni mjamzito inatakiwa wewe ndio umsaidie sio yeye akufanyie kazi zako"
"Sawa mama, nimekuelewa"
"Unielewe na ufate nisemacho, uwe unawahi kuamka huko sio unalala hadi saa tatu saa nne mtoto wa kike na usaidie kazi najua wataogopa kukusema ila nitakuwa nawauliza kama utaendeleza uvivu wako"
"Mmh! Umeanza sasa mama, nitagoma kwenda mimi."
"Basi mwanangu, ila ndio hivyo"
Dada Penina leo hakuwepo kwani aliakuwa ameshaenda kazini kwake.
Wakati naongea na mama, nikapata ugeni naye alikuwa ni Suzy.
Nilikaa na Suzy na kuongea nae kiasi.
"Na wewe Suzy asubuhi yote hii upo kwetu?"
"Ndio, maana nikichelewa sikukuti"
"Na usingenikuta kweli, una bahati sana"
Nikamuacha Suzy na kwenda kuoga ili nirudi kuongea nae vizuri zaidi.

Nilipokuwa bafuni naoga nikasikia sauti ikiniuliza.
"Hivi wewe ni mtu wa aina gani Sabrina"
Nilishtuka sana baada ya kutajwa jina langu mwishoni na kujua kuwa ni mimi ndiye ninayeulizwa.
Nikajimwagia maji haraka ili nitoke, wakati natoka sauti ile ikaja kwa nyuma yangu.
"Madai yako unakimbia?"
Na kweli hapo nilikimbia hadi sebleni huku nikihema, Suzy akacheka kuniona na kuniuliza.
"Vipi wewe, au ndio kuoga fastafasta huko"
Nilitabasamu kwa tabasamu la uongo lakini ukweli wa nikimbiacho niliujua mimi na hata kama nikisema wataniona mzushi tu au mawenge, hivyo nikawa kimya na kwenda ndani kuvaa kisha kumfata Suzy alipo.
"Kwanza niambie Sabrina, ulikuwa unakimbia nini kutoka bafuni?"
"Mmh! Wee acha tu Suzy"
"Au ndio yale maruweruwe yako anayoyasemaga mamako?"
"Achana na hayo bwana Suzy"
"Niachane nayo kivipi wakati umerudi na povu sikioni!"
Hapo nikashtuka na kujishika masikio kweli yalikuwa na povu, nikainuka na kuchukua maji na kwenda nje kunawa kwenye masikio yangu.

Nilipomaliza kunawa nikamuona mtu amesimama karibia na kwetu, kumuangalia vizuri alikuwa ni Sam, nadhani alikuwa anataka kuja kwetu ika alikuwa kama anasita. Nami nikampuuzia kama vile sijamuona ingawa mcho yangu na yake yaligongana. Kisha nikaingia ndani na kwenda kuendelea kuongea na Suzy na wala sikumwambia kama nimemuona Sam nje kwetu.
Suzy akaanza kuniambia kilichomleta,
"Sabrina rafiki yangu, nimekuja kuongea nawe hapa kuhusu mambo matatu."
Nikawa namsikiliza kwa makini ili nijue mambo hayo ni nini.
"La kwanza ni kuhusu wewe mwenyewe, la pili ni kuhusu Carlos na la tatu ni kuhusu Sam"
"Nakusikiliza Suzy"
"Sabrina rafiki yangu una matatizo, tena unahitaji msaada wa karibu sana."
"Ni kweli nina matatizo shoga yangu, eeh niambie kuhusu huo msaada wa kunipa"
"Sabrina, sio mambo ya masikhara hapa. Na usifikirie kila aliyekuwepo mbele yako ataweza kukusaidia. Mengi ufikiriayo kuhusu sisi marafiki zako na mpenzi wako Sam ni kati ya matatizo uliyonayo Sabrina"
Nikaendelea kumsikiliza Suzy ili nijue alichonacho cha maana.
"Halafu kuhusu Carlos, napenda kukutahadharisha kuhuyu huyu mtu rafiki yangu. Carlos ni....." Kabla Suzy hajamalizia, alikuja mama na kukatisha mazungumzo yetu. "Sabrina, mgeni wako huyo amekuja"
Kumuangalia alikuwa ni Carlos, ikabidi nimkaribishe tu na hapo rafiki yangu Suzy akasita kunieleza kuhusu Carlos kisha akasema. "Cha tatu, nilifika na Sam yupo nje anahitaji kuzungumza na wewe Sabrina" Nilimuangalia tu Suzy aliyekuwa akiongea kwa uoga muda huu tofauti na alivyokuwa akizungumza mwanzoni kwa kujiamini.

Suzy akainuka ila kunipeleka alipo Sam, nami nikamfuata Suzy kumbe Carlos naye aliinuka kutufuata.
Akafika mahali pale nje na kutuangalia tukiwa tunaelekea alipo Sam, tulimkuta akiwa amekaa chini ya ule mti nadhani ni baada ya kuchoka kusimama, na alikuwa amesinzia pale pale ndipo Suzy alipomshtua na aliposhtuka tu akasema.
"Lucy!!"
Nikamuangalia sana Sam.
"Yani inaonyesha jinsi gani Lucy alivyokukaa katika akili yako loh! Hadi ndoto za mchana unamuota!"
Sam alibaki kunitazama tu mi na Suzy. Nikamgeukia Suzy na kumwambia.
"Yani mtu mwenyewe uliyetaka nizungumze naye ndio huyu! Amekaa hapo na kumuwaza mwanamke mwingine halafu unataka nijipe imani kuwa bado ananipenda mimi. Sikiliza Suzy, sina muda wa kuzungumza na Sam, nyie nendeni tu na mambo yenu"
Nikageuka na kuanza kuondoka, ingawa waliniita nikawasikilize lakini sikugeuka nyuma.
Nikaenda hadi aliposimama Carlos na kuongea nae.
"Mmh na wewe ni mmbea loh! Hadi umeamua kutufata ushuhudie kinachoendelea"
Carlos aliniangalia tu na kucheka kisha tukarudi ndaniIla hakukaa sana na wala hakusema chochote cha maana ila aliaga na kuondoka na kusema kuwa atakuja badae na wala sikumwambia kama anaweza asinikute kwakuwa sikutaka ajue kama badae nitaondoka na kaka Deo.
Akaniomba nimsindikize kwani siku hiyo hakuja na gari yake, wakati namsindikiza nikamuuliza kuwa gari ameiacha wapi kwani.
"Ina matatizo kwahiyo ipo garage"
Mi nikashangaa.
"Kheee ina matatizo!"
"Ndio, mbona unashangaa? Kwani mimi gari yangu haiwezi kupata matatizo?"
"Aah hapana nimeshangaa tu."
Akaendelea kuongea mambo mbali mbali na huku akijaribu kuniambia kitu kuhusu Suzy.
"Unajua kwanini rafiki yako Suzy aliponiona alishtuka?"
"Eeh kwanini?"
"Kwanza kabisa pale alikuwa ananisema mimi, pili kuna siri yake nimeijua"
"Siri gani hiyo?"
"Rafiki yako anatembea na mume wa mtu, mwambie awe makini sana kwani itamletea matatizo badae"
Nikashangaa na kutaka kumuuliza Carlos kuwa amejuaje, ila daladala ilifika akapanda na kuniaga kwahiyo sikuweza kumuuliza tena.
Nikarudi nyumbani nikijiuliza kuwa je ni kweli kwa nilichoambiwa na Carlos kuhusu Suzy, na mbona Suzy amenificha hilo wakati huwa ananieleza mambo yake mengi tu.
Ikabidi nichukue simu na kumuuliza Suzy kuhusu hilo swala.
"Nasikia una mahusiano na mume wa mtu Suzy!"
"Nani kakwambia?"
"Nijibu kwanza ni kweli au sio kweli?"
"Fanya yako, yangu hayakuhusu."
Kisha akakata ile simu, kwa mara ya kwanza leo namsikia Suzy akinijibu majibu ya mkato na kukatisha tamaa kiasi hicho. Nikabaki kumshangaa na kujiuliza kuwa kwanini amechukizwa na nilichomuuliza.
Ikabidi tu niendelee na mambo yangu kwamaana nilishashushuliwa, nikaenda chumbani kwangu kuweka vitu sawa huku nikimngoja kaka afike tuondoke.
Mama akaniaga kuwa anaenda hospitali kumtazama mama Salome kwahiyo ilitakiwa nimngoje hadi atakaporudi.
"Kaka yako akija mwambie mnisubiri kwanza"
"Sawa mama"
Kisha akaondoka na kuniacha mwenyewe pale nyumbani ila kwa uoga niliamua kwenda kukaa nje kumngoja kwani ndani kwetu kulinipa sana mashaka ya kukaa.

Nikiwa pale nje nimejilaza, akaja Sam na kukaa karibu yangu. Hapo nikainuka na kumuuliza.
"Yani hujaondoka tu?"
"Siwezi kuondoka Sabrina, nahitaji sana kuongea na wewe"
"Sikia Sam, umeshaniumiza vya kutosha hivyobasi sitaki tena kuumizwa na wewe."
"Inamaana Sabrina hunipendi tena?"
"Kukupenda nakupenda tena sana tu ila wewe ndio hunipendi"
"Nakupenda Sabrina"
"Kama ungenipenda usingenichanganya na wasichana wengine haswaa kunichanganya na rafiki yangu kipenzi, kwakweli imeniuma sana Sam"
"Sikia Sabrina, hakuna chochote kinachoendelea kati yangu na Lucy. Mimi nakupenda wewe, mambo yote uyaonayo kwangu hata mwenyewe siyaelewi ila Lucy si mpenzi wangu na hakuna chochote cha zaidi kati yetu"
Sam aliendelea kunieleza kwa makini sana ila gafla kichwa kikaanza kuniuma ikawa kamavile mtu ananigongagonga na nyundo hata Sam akanishangaa kuwa nina tatizo gani, ikabidi anisaidie kunipa huduma ya kwanza na kunipeleka ndani.
Nilikaa nae sebleni ambapo tulikaa kwenye kochi na akaweka kichwa changu kwenye mapaja yake.Muda kidogo kaka Deo alikuwa amewasili pale nyumbani na kunikuta mimi usingizi umenipitia nikiwa vilevile nimelaza kichwa changu kwenye mapaja ya Sam, huku Sam nae akinibembeleze kwa kunishika kichwani.
Kaka alitushtua sana pale ndani hadi niliamka na kukaa.
"Ndio mambo gani haya Sabrina? Mama yuko wapi? Na huyo ni nani yako?"
"Mmh kaka hata salamu?"
"Salamu ya kazi gani? Ni picha gani hii unanionyesha kaka yako? Sema, mama yuko wapi?"
Akawa anaita "Mama, mama"
"Mama hayupo kaenda hospitali kumuangalia mgonjwa."
"Kwahiyo mama kama hayupo ndio wewe unatumia nafasi hiyo kufanya upuuzi wako humu ndani?"
Kisha akamuangalia Sam kwa jicho la ukali sana.
"Wewe kijana toka humu ndani na upotee kabisa kabla sijakuharibu haribu"
Ikabidi Sam aondoke kwani kaka alionekana kuwa na hasira sana.
Baada ya Sam kuondoka nikajaribu kumuelewesha kaka lakini hakutaka kunielewa hata kidogo, aliendelea kuamini alichoamini tu.

Mama aliporudi, alisalimiana na kaka na kuongea nae mawili matatu kisha akamruhusu kuondoka na mimi.
"Kwakweli mama bora nikakae kidogo na huyu Sabrina ili akili yake iwe sawa"
"Ni kweli kabisa mwanangu, na mkifika huko mnipe taarifa kama mmefika"
"Hakuna tatizo mama"
Safari ya mimi na kaka ikaanza, nikapakia begi langu kwenye gari yake aliyokuja nayo na kuondoka.
Safari ilikuwa ni ndefu kiasi kwani kaka alikaa mbali kidogo na nyumbani.
Tulipokuwa tunakaribia kufika, kaka akagundua kuwa kuna mtu anatufatilia tangia tumeanza safari, akaniita na kunionyesha kwenye kioo cha gari na hapo nikashtuka sana.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 19


Tulipokuwa tunakaribia kufika, kaka akagundua kuwa kuna mtu anatufatilia tangia tumeanza safari, akaniita na kunionyesha kwenye kioo cha gari na hapo nikashtuka sana.
"Huyo mtu amekuwa akitufatilia tangia tumeanza safari. Je unamjua?"
Nikasita kujibu kwani ile gari iliyokuwa ikitufatilia ilikuwa ni gari ya Carlos.
"Mbona hunijibu Sabrina, je unamjua?"
"Hapana kaka simjui"
Ikabidi kaka asimamishe gari ili amuulize yule mtu ni nani.
Gari ya kaka iliposimama na ile gari nyingine nayo pia ilisimama. Kaka akashuka ili amfate kumuuliza, wakati kaka anaikaribia ile gari, yule mtu akashusha kioo akaniangalia halafu akawasha gari na kuondoka kabla hata kaka hajalifikia.
Nilishtuka sana kwani hakuwa Carlos kama nilivyodhani bali alikuwa ni yule kaka wa ndotoni.
Nikajikuta nikitetemeka hata kaka aliporudi ndani ya gari alitambua kama nimeshikwa na uoga.
"Vipi na wewe una matatizo gani?"
"Sina tatizo kaka"
"Mtu mwenyewe namfata pale kaondoka, labda alikuwa kibaka yule."Nikaitikia kwa kichwa nikiashiria kwamba nakubaliana na maneno ya kaka na safari ikaendelea.
Kidogo tu, tulifika nyumbani kwa kaka na wifi akatupokea vizuri sana na kutukaribisha ndani.
Nilifurahiana na wifi yangu na kuongea nae mambo mengi ila giza lilishaingia kwahiyo mengine kupanga kuongea kesho yake.
Nilimzoea sana wifi kwavile aliwahi kuishi nyumbani kwetu kipindi ambacho kaka alikuwa safarini kwa muda mrefu kidogo, kwahiyo tulikuwa tumeshazoeana.
Baada ya chakula cha usiku, wifi akanionyesha chumba cha kulala nami nikaenda huko kulala.
Nikawaza mambo mengi sana haswaa kuhusiana na kufatiliwa na yule jamaa wa ndotoni, nikawaza kama je na huku kwa kaka itakuwa vilevile kama nyumbani au itakuwaje.
Niliwaza na kupitiwa na usingizi na nililala hadi asubuhi bila ya tatizo lolote wala kuota ndoto za ajabu ajabu.
Kulipokucha nilifurahi sana na kuona kuwa huku ndio kunanifaa kuishi na sio kule kwetu ambako nakumbana na mauzauza ya kila siku.Niliamka nikiwa na uchovu kiasi, wifi ndiye aliyenishtua kwani mimba yake ilikuwa ikimfanya awahi sana kuamka. "Umeamka muda mrefu eeh!"
"Ndio mdogo wangu si unajua tena"
"Mmh huyo mtoto atakayezaliwa naona atakuwa janja sana, maana anawahi kukuamsha balaa" Tukakaa na wifi tu kwani kaka alikuwa ameshaenda kwenye kazi zake. Wifi alikuwa akiisifu sana mimba aliyobeba kwani haikumpa uvivu kama watu wengine wanavyopataga shida na mimba zao. "Yani huwezi amini wifi, hii mimba na ukubwa wake bado naimba kwaya tena nakuwa namba moja kuwahi mazoezini, sina uvivu kabisa yani" "Mimba yako inaraha basi, yani bado nguvu ya kuimba unayo na tumbo lote hilo duh!" "Mmh! Huyu mtoto nitakayemzaa atakuwa mtundu sana na kama nikimzaa wa kike najua atafanana na wewe na nitamuita Sabrina." "Mmh! Akiwa wakiume je?"
"Atakuwa wakike bwana, sidhani kama ni wakiume"
Wifi alichangamka sana hadi nikaona raha kuishi nae kwani alinipa furaha na amani, pia nilikuwa huru kwa chochote kile.

Mchana wa siku hiyo wifi akaniomba kuwa nimsindikize kwenye mazoezi ya kwaya kanisani kwao, hakupenda kuniacha mwenyewe ndiomana akaniomba niende nae.
Tulipofika nilikuwa kimya sana nikiangalia mambo yanayoendelea kwenye ile kwaya, nilikb na mdada mmoja aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Jack ila hakujua kama mimi ni wifi yake na Joy kwahiyo akawa anaongea mambo mengi sana kwa uhuru tu.
"Yani hiyo kwaya usione hivyo, humo kumejaa unafki tupu."
"Kwanini?""Yani huyo Joy na mtumbo wote huo lakini anapendelewa na James balaa, kila siku anaanzisha yeye nadhani wanaajenda yao ya siri"
Nikacheka kidogo na kuuliza tena, "Kwani James ndio nani?"
"Si yule mwalimu wa kwaya, yani wengine hata hatuonekani. Anayeonekana ni Joy tu, mara amsifie sijui ana sauti nzuri sijui nini na nini yani unafki mtupu"
Nilicheka na kujiambia moyoni kuwa huyu dada anasumbuliwa na wivu kwani ndio kawaida ya watu katika kundi lolote lile kutawaliwa na wivu, chuki na husda ila nami nikawa makini ili nione kama kweli huyo mwalimu wa kwaya anampendelea wifi yangu, ila kabla ya yote nikamuuliza swali la kizushi huyu Jack.
"Je ameanza kumpendelea baada ya ujauzito au kabla ya hapo?"
"Hata kabla ya ujauzito alikuwa akimpendelea ila saivi ndio amezidisha jamani loh kama kambebea ile mimba yeye!"Nikacheka sana na kumuuliza, "Kivipi?"
"Kwani wewe hujui mtu akikubebea mimba anavyokuwa? Yani unatokea kumpenda na unapenda kila afanyacho na kumuona mara zote hata yeye inakuwa hivyo. Kuna mwingine mimba yako itampenda na mwingine itamchukia ila kwa Joy na James imezidi sasa."
Nikamuangalia sana Jack aliyeonyesha kuchukizwa sana na kupendelewa kwa wifi yangu, badae wakainuka kwenda kuimba na baada ya hapo tukaondoka.
Nilimuona yule Jack akijisikia vibaya sana kuona nimeongozana na wifi Joy kuondoka kwani alijua yote aliyoniambia yatamfikia.
Nilipokuwa na wifi naye nilimuuliza kwa uzushi tu.
"Nasikia wifi yangu unapendelewa kweli na mwalimu wa kwaya eti kila siku unaanzisha wewe"
"Ile kwaya ni wanafki wifi, yani kuna chuki mule balaa mengine nikikuelezea hata utashangaa ila huwa tunakaa kimya tu na kuyaacha yapite mdogo wangu. Watu wanawivu mule, chuki binafsi na kila kitu"
Nilimuangalia wifi na kukubaliana na maneno yake kwani hata mimi niliona kuwa ni wivu ndio uliowasumbua watu wa aina ile ya Jack.Mara kuna kijana akatufata, kisha wifi akanitambulisha kwa yule kijana kuwa ndiye mwalimu wao wa kwaya hapohapo nikaelewa kuwa yule ndio James anayezungumziwa na yule Jack, nikasalimiana nae kisha akatuambia tumngoje ili twende wote kwahiyo mimi na wifi tukasimama mahali kumngoja.
Alipoondoka kidogo nikamuuliza wifi yangu,
"Kwani na yeye tunaenda nae njia moja?"
"Ndio, ila yeye tutamuacha njiani halafu sisi tutaendelea"
"Huwa unaongozana nae mara kwa mara?"
"Ndio, tena huwa ananisindikiza hadi nyumbani ingawa kwake ni nyuma. Yani huyu mkaka anaupendo sana wifi yangu"
"Kweli, anaonyesha kuwa na upendo"
Yule James akarudi na safari ya kuondoka ikaendelea, kufika njiani James akamnunulia wifi matunda na kumkabidhi kisha akamwambia.
"Kumbuka ulivyoambiwa kliniki, kula matunda kwa wingi na mboga za majani"
"Natambua hilo James hata usijali"
Tukaendelea na safari kisha yule James akatusindikiza hadi nyumbani.
Swali nililojiuliza ni kuwa huyu mwalimu wa kwaya anaelewa nini juu ya ushauri anaopewa wifi kliniki.Ila sikuuliza chochote tena nikawa kimya tu, naye wifi alifata ushauri kwani alipofika tu akaanza kula yale matunda ambayo kwakweli ni mazuri kwa afya na kunipa baadhi mimi.
Kaka aliporudi alitukuta tukiwa tumekaa na wifi huku tukisimuliana mambo mbali mbali.
"Naona mtu na wifiye, leo amani tupu humu ndani"
Wifi akawa anacheka, nami nikauliza.
"Kwani siku zingine amani hakuna?"
"Muulize wifi yako akujibu"
Kaka akaenda chumbani na wifi akaendelea kucheka tu kisha akasema.
"Amani ipo wifi ila kaka yako si unajua tena na ubize wake, yani muda wote amechoka sina hata mtu wa kuongea naye humu ndani. Ngoja huyu mtoto aje achangamshe nyumba tu"
"Na sisi tunamngoja kwa hamu huyo mtoto pia, akaiwa wa kike kweli nitakuwa namsuka vinywele vyake"
"Ndio unachowaza Sabrina, (wifi akacheka) na ndiomana nasema nitamuita Sabrina maana napenda mwanangu awe mcheshi na mpole kama wewe"
"Na kama wakiume basi afanane na kaka"
Wifi akacheka na kuuliza.
"Asipofanana nae je?"
"Namaanisha afanane nae upole maana kwetu wote wapole"
"Na je ataitwa jina gani?"
"Ataitwa James"
Wifi akashtuka sana nilipotaja hilo jina na kuuliza.
"Kwanini?"
"Ili awe na moyo wa upendo kama mwalimu wenu wa kwaya"
Nikamuona wifi akipumua kiasi na kusema.
"Aah kumbe!"
"Ndio, mbona ukashtuka ulidhani nini?"
"Hamna kitu wifi, nadhani itakuwa vyema kama tukienda kula"
Ikabidi tuinuke na kuandaa chakula kisha wifi akamuita kaka ili tule pamoja. Wakati tunakula simu yangu ikaita kwa nguvu sana kwani nilikuwa nayo mezani ukizingatia tangia asubuhi hakuna aliyenipigia. Kaka aliniangalia na kusema,
"Nani anayekupigia muda huu? Au ndio kale kajamaa kaka ka siku ile" Nilikaa kimya tu kwani ni kweli mpigaji alikuwa Sam, ikabidi niizime kwa muda ili kaka asiingee tena. "Mbona hujaipokea sasa?"
Wifi akajaribu kunitetea.
"Mmh! Muda wa kula huu sio wa kuulizana maswali Deo, utamkosesha raha mdogo wako" Mi nikatulia tu na kuendelea kula, nikahisi kuwa huenda kaka aliambiwa na mama kuhusu Sam na ndiomana amekuwa mkali kwangu na kuniuliza maswali mengi mengi.Nilipomaliza kula nilienda chumbani na kuwasha simu na jambo la kwanza ikawa ni kumpigia Sam. "Kweli nimeamini kuwa Sabrina hunipendi tena, yani unaondoka kwenu hata bila ya kunipa taarifa! Kwanini lakini?" "Niliamua tu sababu siku hizi wewe una watu wako unaowajali hata ningekwambia usingeona umuhimu wake" "Hivi Sabrina, nifanye nini ili uamini nakupenda?"
Nikamsikia wifi akiniita huku akigonga mlango wangu, ikabidi nimwambieSam kuwa nitampigia badae na kwenda mlangoni kuongea na wifi.
"Kakako anakuita"
Nikatoka na kumfata kaka alipo ili nikazungumze nae.
"Yani mdogo wangu kumaliza kula tu unakimbilia chumbani au uliogopa nilivyokusema wakati wa kula?"
"Hapana kaka"
"Nisamehe Sabrina maana si vizuri kumsema mtu wakati wa kula"
"Usijali kaka, nami nisamehe kwa kukaa na simu mezani wakati wa kula"
"Sawa mdogo wangu usijali, kuwa huru mama. Sawa eeh!"
Nikamuitikia kaka na kujigeresha kidogo kisha nikaenda tena chumbani ili nikaongee na simu.
Kufika chumbani, nikaiona simu yangu ikiwaka waka mwanga wa ajabu nikaogopa kuishika na kujiuliza au mauzauza yamenianza tena na kwenye ile nyumba ila nikakumbuka maneno ya wifi yangu kuwa niwe nasali kabla ya kulala, nikaamua kukaa mbali na ile simu ili niombe kwamba na kama ikiendelea vile nikamwambie kaka.
Nikapiga magoti na kuinama ila sikuelewa kilichoendelea kwani nilimsikia wifi tu akifungua mlango wangu na kuniambia.
"Mmh Sabrina unafanya nini?"Nikashtuka sana na kumuuliza.
"Kwani nini?"
"Unakoroma sana duh! Ndio mlalo gani huo?"
Nami nikawa najishangaa kwani nilikuwa vilevile nimeinama, kwakweli sikuamini kama nimelala vile muda wote.
"Kwani saa ngapi muda huu?"
"Ni saa mbili na nusu asubuhi"
Nikazidi kushangaa, wifi akaniambia kuwa alikuja kuniamsha ili nikapate kifungua kinywa.
Baada ya yote, wifi alitaka twende sokoni ili kununua baadhi ya mahitaji. Nikabeba simu yangu ambayo ilikuwa kawaida kabisa leo wala haikuonyesha tatizo lolote.
Tukiwa njiani nikapigiwa simu na Carlos aliyeniuliza nilipo nikamtajia naye akasema anakuja.
Baada ya muda tu kidogo Carlos aliwasili na kukuta nimesimama na wifi njiani, nikamuonyeshea ishara naye akafika mahali alipo.
Wakati Carlos alipokuwa anamsalimia wifi alimpa mkono, mara gafla wifi akapiga kelele.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 20


Wakati Carlos alipokuwa akimsalimia wifi alimpa mkono, mara gafla wifi akapiga kelele na kuuachia mkono wa Carlos huku Carlos akionekana kutabasamu.

Kwakweli kitendo hiki kilinishtua sana kwani wifi alijawa na uoga uliopitiliza wakati Carlos alikuwa kawaida huku akitabasamu tu, sikujua Carlos alimfanya nini wifi yangu wakati wanasalimiana.
Nikajikuta nikiuliza,
"Kwani vipi jamani? Mbona sielewi!"
Wifi akanishika mkono huku akinivuta kuwa tuondoke.
"Tuondoke Sabrina, huyo mkaka sio mtu mzuri"
Nikazidi kushangaa kuwa wifi atamsemaje mtu kuwa sio mzuri wakati hamjui, wifi alizidi kunivuta kwahiyo ikabidi tuondoke hata safari ya kwenda sokoni ikaghairishwa na tukarudi nyumbani.
Nilimuona wifi akijiinamia huku akiwa na mawazo sana, kisha akaniambia kuwa anaenda kufanya maombi kwanza.
Alienda chumbani kwao na mimi nilibaki pale sebleni nikitafakari yale mambo kwani yalinichanganya tayari huku nikiwa na maswali mengi sana ya kumuuliza wifi atakapotoka kusali.

Baada ya muda, wifi alirudi pale sebleni nami nikafurahi ili niweze kumuuliza maswali yangu.
"Mmh afadhali sasa nina amani kidogo"
"Kwanini?"
"Kwasababu nimeomba, unajua Sabrina maombi ndio silaha kubwa na ya pekee katika mambo ya khatari"
"Sawa wifi nimekuelewa, ila kwanini umesema kuwa yule sio mtu mzuri?"
"Sabrina mdogo wangu, nakupenda sana yule sio mtu kabisa sijui hata umemtolea wapi?"
"Sio mtu kivipi wifi? Mbona unanitisha?"
"Yule sio mtu mdogo wangu, huenda akawa ni mchawi tena wa kuzimu"
"Mmh niambie vizuri wifi"
"Aliponipa mkono kunisalimia, ubaridi ulipenya katika mwili wangu wote halafu mtoto wa tumboni mwangu alishtuka sana. Umeyatizama kwa makini macho ya yule kaka?"
"Kwani yana nini mbona mi huwa naongea nae na kumtizama kila siku?"
"Mdogo wangu umefungwa hata huoni, macho ya yule kijana si ya kawaida"
"Ila kuhusu ubaridi ndio alivyo yule siku zote"
"Acha kutetea kitu usichokijua kwa undani zaidi, ila mimi nakwambia ukweli kwamba yule sio mtu wifi yangu. Kuwa makini sana"
Nikamsikiliza wifi ila bado sababu zake za kutaka niamini kuwa Carlos si mtu wa kawaida hazikuniingia akilini kwani Carlos nilishaanza kumzoea kwa sasa, ikabidi nijiweke katika mazingira ya kumchunguza Carlos kabla ya kuwa tatizo kubwa.
Tuliendelea na wifi katika kazi mbili tatu na kufanya mambo mengine ila wifi hakutaka tena kwenda sokoni.

Wakati tunakula chakula cha mchana, Sam akanipigia tena simu na haikuwa tatizo kuipokea kwani kaka hakuwepo.
"Naomba kuonana na wewe Sabrina, tafadhari sana"
"Nipo kwa kaka na sitaweza kuonana nawe na wala sina muda huo"
"Tafadhari Sabrina, kumbuka nakupenda"
"Hata kama, sitaki kuonana na wewe"
Nikakata ile simu na kuendelea kula, kumbe wifi alinisikiliza kwa makini sana.
Tulipomaliza kula akaniuliza,
"Ulikuwa unaongea na nani wakati ule?"
"Ni rafiki yangu tu"
"Mpenzi wako eeh"
Nikacheka kidogo na kuitikia kuwa ni kweli mpenzi wangu, wifi nae akacheka na kuniuliza.
"Sasa mbona hutaki kuongea nae wala kuonana nae kwanini? Humpendi au ni nini?"
Niliinama kidogo kama nafikiria jambo, kisha nikamjibu wifi.
"Kumpenda nampenda tena sana tu, tatizo amenisaliti tena kwa my best friend"
"Mmh! Umeshuhudia au umeambiwa?"
Ikabidi nimueleze kwa kifupi wifi ilivyokuwa, nikamueleza mengi ila sikumueleza kuhusu mauzauza yangu.
"Pole sana, ila kama anahitaji kuongea nawe bado ni lazima anakitu cha kukwambia"
"Ila mimi sijisikii kabisa kuzungumza nae, kwakweli ananiumiza sana na kila siku ananiongezea maumivu"
"Ila ndio mapenzi yalivyo, uvumilivu unahitajika sana. Me ningependa uzungumze nae, tena ikiwezekana aje hapa nyumbani"
"Mmh labda kaka asiwepo"
"Usijali Sabrina, huwa sipendi kuona mtu anakosa muafaka kwa kitu apendacho. Usikubali mtu wa mbali kuvunja mahusiano yenu, mtu mnayependana nae ndio anastahili kuwa naye katika ndoa ingawa mara nyingi huwa haiwi hivyo?"
"Je, wewe unapendana na kaka Deo?"
Wifi akacheka sana na kuniambia.
"Ndoa ni uvumilivu na kabla hujaolewa unatakiwa kuwa makini na mtu anayetaka kukuoa ili usijekujutia mbele ya safari"
Nilimuangalia wifi na kutafakari maneno yake aliyoyasema kwani hakunijibu swali langu kama anapendana na kaka Deo au la. Nikamuuliza tena,
"Kwani ni kitu gani kinaweza kufanya mtu uamini kuwa unapendwa?"
"Siku zote mtu anayekupenda anakuwa karibu yako, anakujali na kuwa bega kwa bega na wewe katika huzuni na furaha"
"Utajuaje sasa kama Sam bado ananipenda?"
"Atakuwa anakupenda ndiomana hakati tamaa kwako, usiache kumsikiliza maana watu wenye kupenda kweli siku hizi wamepotea"
Tukaongea mambo mengi sana na wifi yangu.
"Unaonaje swala la mwanamke kutembea na mume wa mtu au mke wa mtu?"
"Si vizuri kwakweli, kwanza kabisa fikiria je ukiwa ni wewe unafanyiwa kitendo hicho je utajisikiaje? Yani wewe ndio uwe mke halafu mumeo anamwanamke nje utajisikiaje? Kwakweli inauma sana tena sana"
"Na vipi mwanaume kutembea na mke wa mtu?"
"Nayo inauma pia kama ya mwanzo tu ila je umefikiria nini kuniuliza hivyo?"
"Hakuna kitu nimeuliza tu wifi yangu"
Muda wa kwenda kwenye kwaya ukawadia ila leo wifi hakujisikia kwenda, sikujua ni kwanini ila hakujisikia.

Jioni yake tukatembelewa na mgeni ambaye alikuwa ni James, mwalimu wa kwaya anayoimba wifi. Baada ya salamu akaanza kumtania wifi
"Sijakuona mazoezini leo nini tatizo au hali imeanza kuwa mbaya?"
Huku akishika shika tumbo la wifi lililokuwa kubwa sana sababu ya ujauzito, wifi nae alikuwa akitabasamu na kufurahi.
"Nimepatwa na uvivu leo, na wewe kutokuniona siku moja tu ndio hadi uje kuniulizia?"
"Ndio, lazima nije ili nijue hali yako ndio mapendo yalivyo"
Wifi alionekana mwenyefuraha sana kuzungumza na James hadi pale alipoaga na kuondoka.

Kaka aliporudi alikuta wifi ameshalala kwani kaka alichelewa sana leo, na mimi nikaenda kulala baada ya kumsalimia.
Nilipokuwa chumbani nikapata wazo la kumpigia Suzy simu ila kumuuliza vizuri kwani nilihisi huenda hasira zake zimepungua.
"Suzy shoga yangu, sikuwa na nia mbaya kukuuliza kama kweli unatembea na mume wa mtu"
"Nia yako ni nini sas?"
"Nia yangu ni kukutahadharisha tu, mume wa mtu sumu jihadhari sana shoga yangu sipendi kukuona ukiumia jamani!"
"Aliyekwambia kuwa nitaumia ni nani? Mi ni mtu mzima Sabrina najua jema na baya kwahiyo usiwe na shaka kuhusu mimi"
"Ila kama mimi ningekuwa ni wewe basi ningeachana na huyo mbaba"
"Simwachi ng'ooo ananisaidia sana, kwanza familia yake hainihusu yeye ndio ananihusu"
"Mmmh haya shoga yangu ila kuwa makini sana"
"Kuwa makini wewe na mambo yako, me acha nifurahie maisha"
Akakata simu, nikatambua kuwa Suzy hapendi kuongelea zile habari za mume wa mtu kwahiyo nikaachana nae na kulala kwani sikupenda malumbano katika mambo yasiyonihusu.

Nilipokuwa nimelala nikajiwa na ndoto kuhusu Suzy.
Nikamuona Suzy yupo baa na mbaba flani, baada ya muda wakainuka na kwenda nyumba ya kulala wageni wakachukua chumba kimoja chenye kila kitu ndani, ilikuwa kamavile naangalia video jinsi nilivyokuwa nawaona kwenye ndoto.
Wakiwa kwenye kile chumba, mara kuna watu wakagonga hodi halafu yule mbaba akaenda kufungua gafla wakaingia wamama watatu waliojazia sana wakamsukuma yule baba pembeni na kumfata Suzy aliyekuwa kitandani kisha wakampiga mfululizo na kumvuta hadi nje, nikamuona mama mmoja akichukua gongo na kutaka kumbamiza nalo Suzy kichwani.
Nikastuka na kupiga kelele,
"Usimpigeeeeeee...."
Kelele zile ziliwashtua wifi na kaka ambao walikuja haraka chumbani kwangu kuniulizia kuna nini na kunikuta machozi yakinitoka kama mimi vile niliyekuwa napigwa kwenye ndoto, hata sikujielewa.
Wifi akafanyakazi ya kunipooza kuwa ni ndoto tu na haina maana yoyote ile kwenye maisha yangu kwahiyo nisiwe na wasiwasi wala mashaka yoyote kuwa itatokea kwani ni ndoto tu.
Baada ya kutulia wifi akaondoka na mimi nikarudi tena kulala, safari hii nikamuona Suzy akiwa hospitali amelazwa huku akionekana kuwa na majeraha mwili mzima, wakati namshangaa na kusikitika kuhusu Suzy akatokea Carlos pembeni yangu huku akitabasamu na kuniambia.
"Nilikwambia Sabrina, mwambie rafiki yako ajihadhari si unaona sasa!"
Nikastuka tena na kujiuliza, kwani hii ni kweli au ndoto tu? Mbona matukio yake yananitisha, nikatafakari sana mara mlio wa ujumbe mfupi ukaita kwenye simu yangu, kuangalia umetoka kwa Carlos.
"Naomba badae tuonane, kuna kitu muhimu nataka kukwambia"
Nikashangaa kuona Carlos kanitumia ujumbe usiku ule, kuangalia saa ilikuwa tayari kumekucha kwani ilikuwa ni saa mbili asubuhi, ikabidi tu niamke na kutoka chumbani ili nikamsaidie wifi baadhi ya kazi kidogo.
Niliporudi tena chumbani kwangu, nikachukua simu na kumpigia Suzy ili kujua hali yake ila simu haikupokelewa, nikaamua kumpigia mama ili kujua hali ya mama Salome hospitali kuwa anaendeleaje maana tangu nilipoondoka sijaulizia.
"Kwakweli anaendelea vizuri tunamshukuru Mungu kwa hilo, tatizo amepararaizi upande mmoja"
"Hivi aliyemgonga mlimpata kweli?"
"Nasikia alikimbia na hata hajulikani alipo"
Nikaishia kuguna tu, ujumbe tena ukaingia kwenye simu yangu na alikuwa Carlos tena aliyenielekeza pa kumkuta.
Nikawa napanga jinsi ya kumuaga wifi, ila kwa bahati wifi akatembelewa tena na mwalimu wa kwaya ila leo aliongozana na mwanakwaya mwingine nikatumia nafasi hiyo kumuaga wifi kuwa kuna mahali naenda mara moja ila sikumwambia kama naenda kuonana na Carlos.

Nilifika eneo alilonielekeza Carlos na kumkuta, baada ya salamu nikaanza kuzungumza nae.
"Unakumbuka nilipokwambia kuhusu rafiki yako Suzy na mume wa mtu?"
"Ndio nakumbuka?"
"Je, ulichukua hatua gani?"
Nikamueleza jinsi nilivyomuuliza Suzy na yote niliyomwambia.
"Unajua kwanini wifi yako anasema kuwa mimi sio mtu wa kawaida?"
"Sijui"
"Kwasababu naijua siri yake, kuna siri kubwa sana katika ujauzito alionao"
Nikaanza kujiuliza kuwa ni siri gani hiyo, kisha nikamuuliza ili anijibu.
Ila kabla hajanijibu simu yangu ikaanza kuita, kuangalia mpigaji ni mama yake Suzy. Nikashtuka kwani hana kawaida ya kunipigia.
Nikaipokea ile simu, mama Suzy alikuwa anaongea kwa kilio kikubwa.
"Sabrina, Sabrina rafiki yako mwanangu mimi mwanangu...."
Kilio cha mama Suzy kilipasua moyo wangu kwa uoga wa kupewa habari mbaya.

Itaendelea kesho...
 
Ilikuwa kwenye mida ya saa mbili usiku wakati tumekaaa kwaajili ya chakula cha usiku.
Wakati nakula simu yangu ikaita kuangalia mpigaji ni mpenzi wangu Sam ila nikashindwa kunyanyuka kwenda kupokea kwani mama alikuwa ananiangalia sana ikabidi nibonyeze kitufye cha kimya (silence).
Mama kumbe alisikia wakati inaita akauliza,
"Nani anakupigia wakati wa kula?"
"Hakuna mtu mama, ni alarm tu"
"Unadhani sijasikia wakati inaita? Umeanza uongo eeh!!"
"Hapana mama ni Sam"
"Nilijua tu, anakupigia wakati wa kula amekununulia hiyo simu? Anaijua bei yake?"
Ikabidi nikae kimya, mama yangu alikuwa anamchukia sana Sam. Hakupenda kabisa mahusiano ya mimi na Sam ingawa tulipendana sana.

Tulipomaliza kula tulikuwa tumekaa sebleni, nikatamani kuinuka kwenda chumbani nikazungumze kidogo na Sam na kumwambia kuwa muda aliokuwa anapiga nilikuwa nakula.
Nikawa nainuka, mama akaanza kuongea kabla hata sijaanza kutembea.
"Unaenda wapi Sabrina?"
"Naenda chumbani mara moja mama"
"Kuongea na simu eeh!! Amekupa nini huyo Sam jamani? Yani unashindwa kukaa hapa kuzungumza na mama yako na chakula kitulie, wewe macho juu juu kukimbilia ndani kuongea na Sam. Amekuwa mzazi wako huyo? Sipendi hiyo tabia, haya kaa tuzungumze ya maana hapa"
Ikabidi nikae ila mawazo yangu yote yalikuwa ni kwa Sam tu hata maneno ambayo mama alizungumza sikumuelewa hata kidogo, nikaona anapiga kelele tu.
Nadhani pale aliyekuwa anamsikiliza ni dada yangu Penina tu maana ndio waliokuwa wakijibishana.
Mama akaniomba simu yangu na kupigia ndugu zake, akaongea wee hadi muda wa maongezi ulipokata ndio akanirudishia. Nikabakiwa na ujumbe mfupi tu bila ya muda wa maongezi.

Mama aliponyanyuka nami nikanyanyuka kuelekea chumbani, kisha nikamtumia ujumbe mfupi Sam kuwa anipigia. Naye hakusita kunipigia ila alinipa lawama mwanzo mwisho.
"Sabrina una dharau sana, yani simu yangu hupokei. Nangoja kidogo kupiga namba inatumika yani kuna watu unawaona wanathamani sana kushinda mimi. Poa tu Sabrina"
"Jamani Sam mpenzi wangu, tafadhari nisamehe"
"Umefanya makusudi wewe, poa tu mi nalala saivi"
Halafu akakata simu, nikajisikia vibaya sana ikabidi nimtumie ujumbe wa kumuomba msamaha ila Sam hakupiga wala kujibu ujumbe wangu.
Sikuweza kumwambia Sam kama mama yangu anamchukia kwani nilijua wazi kuwa akijua tu lazima atajisikha vibaya ukizingatia kwao mama yake ananipenda sana mimi.

Asubuhi na mapema nikapata ujumbe toka kwa Sam.
"Yani wewe Sabrina una dharau sana, sijui kwavile umejua nakupenda sana. Yani umeshindwa hata kunipigia simu upooze mawazo yangu umekazana na ujumbe tu!! Najua muda wote wa maongezi umemaliza kwa watu wako ila poa tu. Mimi nitaendelea kukupenda Sabrina"
Nikaamua kuamka na kwenda kununua vocha ili nipate kuzungumza na Sam.
Ila maduka yalikuwa bado hayajafunguliwa, nikaamua kuanza kufanya kazi mbalimbali za pale nyumbani ili niwahi kumaliza na niweze kwenda kwa Sam kwani nililuwa nimemkumbuka na pia nilitaka nikamweleweshe ya jana.
Baada ya kazi nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea rafiki yangu Suzy, mama hakuwa na pingamizi akaniruhusu niende nami nikaenda moja kwa moja kwa Sam ila sikumkuta na mlango wake ulikuwa na kufuri.
Ikabidi niende duka la karibu kununua vocha kisha nikampigia ila hakupokea nikajua tu kisirani kimempanda.
Nikaamua kuondoka na kwenda kweli kwa kina Suzy ili badae nipate kurudi tena kumuangalia.

Nilikaa sana kwa kina Suzy ila sikumueleza Suzy jambo lolote lile kuhusu Sam, badae nikaaga na kwenda tena kwa Sam nikawa namngoja kuwa pengine ameenda kazini ila ilikuwa ni mwisho wa wiki ndiomana nilijiamini na kwenda.
Nilimngoja sana Sam bila ya kutokea, nilikata tamaa na moyo kuniuma sana kuwa kwanini Sam amenifanyia vile kwa kosa dogo kiasi kile.
Nikajaribu kuwauliza na majirani ambao walisema kuwa Sam ameondoka asubuhi sana, nikajiuliza kuwa labda ameenda kwao ila kwanini asipokee simu? Nikaona kuwa Sam ananifanyia kusudi, hisia mbaya zikanitawala kuwa Sam atakuwa kwa mwanamke mwingine tu hapo roho ikaniuma sana.
Muda ulizidi kwenda, ikabidi nirudi nyumbani.

Nilifika nyumbani kwenye mida ya saa tatu usiku, nikamkuta mama na dada wakifanya maongezi ya hapa na pale.
Nikawasalimia na kwenda kuoga kisha kula chakula.
Dada akaanza kuzungumza,
"Halafu wewe Sabrina, kupenda kwako huko kutembea usiku usiku ipo siku utakumbana na majini huko njiani"
Nikashtuka sana na kumuuliza dada,
"Majini? Una maana gani dada?"
"Usiku ni mida ya majini, yakikukumba huko usituletee balaa hapa"
"Kwani majini yakoje?"
"Ukikutana nayo lazima nywele zisisimke, halafu ni marefu sana mara nyingine huwezi ona mwisho wa urefu wao"
"Mbona unanitisha dada?"
"Sikutishi ila huo ndio ukweli, unatakiwa kuwa makini sana. Majini hayana masikhara, likikuvaa ndio limekuvaa utakula nalo, kulala nalo na kuamka nalo bila ya kutarajia"
Nikaanza kuingiwa na uoga, mama nae akaanza kuchangia hoja zake.
"Unakumbuka kule makaburini wakati wanamzika yule dada mwenye mashetani kilichotokea?"
Dada akajibu,
"Ndio nakumbuka mama, yani majini hayataki mchezo"
Ikabidi niulize tena,
"Kwani majini yanafanana na kitu gani"
"Majini yanatisha mdogo wangu usiombe ukutane nayo njiani unaweza usilale siku mbili unaweweseka tu."
"Inamaana yanaweza kutokea wakati mtu amelala?"
"Ndio, unaweza ukashangaa umelala na jini pembeni yako"
Niliogopa sana na kuwaza kwanini nimesikiliza habari za majini usiku.
Mama akaongezea kitu kingine ambacho kilifanya niende chumbani kumtafuta Sam.
"Ila leo umenifurahisha kitu kimoja, kwenda kweli kwa Suzy maana huyo Sam wako amekuwa hapa siku nzima kukungoja"
Nikagundua kuwa, wakati mimi namngoja Sam kule kwake kumbe na yeye alikuwa kwetu kuningoja ila kwanini hakutaka kupokea simu yangu.

Nikaenda zangu chumbani kwa lengo la kumpigia tena Sam simu.
Ila nikasita kwani nikaona Sam nae ananifanyia kusudi, kama kweli alikuwa kwetu kuningoja kitu gani kimemfanya asipokee simu yangu. Mara dada akaniita na kufanya yale mawazo yangu juu ya Sam yakatike.
"Vipi Sabrina ndio unataka kulala muda huu?"
"Ndio dada, nataka kulala"
"Njoo mara moja, kuna kitu nataka unisaidie huku chumbani kwangu"
Nikatoka na kufatana na dada hadi chumbani kwake.
"Kuna kitu kinanichanganya hapa kwenye computer yangu, naomba uniondolee hii picha"
Mimi nikaitazama ile picha, ilikuwa ni ya mwanaume mzuri sana. Nikamuuliza dada kuwa kwanini anataka kuifuta,
"Kwanini uifute dada? Mbona picha yenyewe ni nzuri?"
"Hata sielewi nimeidownload vipi hiyo picha hadi imekaa hapo, nitolee bhana mipicha mingine inaweza kuwa ya majini"
"Mbona unapenda sana story za majini dada?"
"Yapo na ndiomana nayaongelea, usishangae siku ukitokewa na jini"
"Basi yaishe, mi sitaki tena hizo habari nisije kushindwa kulala bure"
Nikafanya ninachojua kuifuta ile picha kisha nikamuaga dada usiku mwema na kuondoka.

Nikarudi chumbani na kuendelea kuwaza kuhusu Sam wangu. Wakati nikiwaza juu ya Sam, wazo la majini likanijia tena kichwani nikajikuta naanza kuogopa chumbani halafu ile picha ambayo dada aliniomba kuwa nimsaidie kufuta ikawa inatembea kichwani mwangu.
Niliona chumba kimekuwa kikubwa sana, nilipokaa kitandani nilihisi kama vile kuna mtu pembeni yangu nikaanza kuogopa zaidi huku nikijilaumu kuwa kwanini nimesikiliza stori za kutisha muda wa kulala.
Nikachukua tena simu na kuamua kumpigia Sam ili kujiliwaza kidogo ila kabla sijapiga nikapitiwa na usingizi.

Mwanaume mzuri sana na mtanashati alikuwa mbele yangu, asili yake kama mwarabu hivi au muhindi.
Alikuwa anatabasamu na kusogea taratibu kuja mahali ambako mimi nipo.
Nilikuwa namwangalia kwa jicho la mshangao tu.
Alipofika karibu yangu, akanivuta mkono kisha akatoa kitu cha ajabu kilichofanya nishtuke.

Itaendelea
Duh
 
Back
Top Bottom