Simulizi ya kweli: Niliolewa na Jini bila kutarajia

Simulizi ya kweli: Niliolewa na Jini bila kutarajia

SEHEMU YA 26


Nikamkuta Carlos akiwa amesimama huku akitabasamu.
Nikashtuka sana kwani sikumtegemea Carlos kwa wakati ule kabisa.
Ikabidi nimuulize kwanza kabla ya kumkaribisha ndani.
"Khee Carlos mbona gafla! Halafu umekuja moja kwa moja nyumbani"
"Kwani ni vibaya kukutembelea Sabrina?"
"Si vibaya ila ungekuja kwa taarifa kamili kuliko kunishtukiza kama hivi"
"Usijali Sabrina, nilikuwa napita hapa nje kwenu nikaona itakuwa vyema kama nikija kuwasalimia kwanza"
"Kwahiyo leo humwogopi wifi?"
"Sina kawaida ya kumwogopa mtu na nimekuja kwa lengo la kumwonyesha wifi yako kuwa mimi ni binadamu wa kawaida tu kama wengine."
Ikabidi nimkaribishe Carlos ndani kabisa kwani alijitoa kututembelea.
Kuingia ndani, tulimkuta wifi akiwa amekaa tena na mawazo sana.
Ile kumuona tu Carlos akiingia ndani kabisa, wifi akainuka na kuanza kuongea kwa hasira.
"Sabrina, kwanini umemkaribisha huyu mtu ndani?"
"Amekuja kututembelea wifi"
Wifi akamwangalia Carlos na kuanza kusema.
"Wewe shetani toka kwenye nyumba yangu"
Carlos akaanza kucheka tena kwa furaha kabisa.
"Unaniita shetani sababu nazijua siri zako! Au niziseme zingine hapa mbele ya Sabrina?"
Wifi akanywea kwanza na kusema.
"Najua unataka kunipunguzia imani kwavile umeona kuwa mimi ni mcha Mungu"
Carlos akacheka tena na kusema.
"Tatizo lako kubwa ni kuniita mimi shetani ndio useme sasa ushetani wangu uko wapi?"
Nikamuona wifi akiwa kimya kabisa na kukosa cha kujibu kwakweli. Wifi alikuwa akimuangalia Carlos kwa uoga tu.
"Unapokuwa mtu mwema jaribu kusema yote unayoyafanya siri ili uaminike. Wewe mwanamke, umeweka siri ngapi hadi leo? Niziseme kwa Sabrina?"
Wifi alitulia kimya kabisa na kushindwa kusema chochote, nilimuona akikaa kitini kwa uoga.
Carlos akamsogelea wifi na kumnong'oneza kitu sikioni kisha akanifata na kuniaga huku akitaka nimsindikize, kwakweli nilikuwa nimetulia kimya muda wote nikiangalia mabishano ya Carlos na wifi yangu.
Nikaongozana na Carlos hadi nje, akapanda kwenye gari yake na kuniambia.
"Nitakuja badae kukutembelea"
"Badae ya muda gani? Maana muda umeisha!"
"Ooh samahani, namaanisha kesho"
Kisha Carlos akaondoka.
Nikiwa bado pale nje nikaona gari ya kaka ikiwasili, naye akaingiza gari na kushuka kisha nikaongozana nae kuingia sebleni.
Tukamkuta wifi ametoa mimacho kama mtu anayeugua, kaka akamshtua wifi nae wifi aliposhtuka moja kwa moja akataja "James" kaka akadakia.
"Kafanyaje mtoto wetu James?"
Nadhani ni hapo wifi akarudiwa na ufahamu wa kawaida.
"Hajafanya kitu mume wangu"
"Mbona ulikuwa umetoa mimacho hapa?"
"Ni uchovu tu mume wangu"
Basi kaka akaongea pale mawili matatu na kupumzika kwa uchovu pale sebleni.
Muda wa kula ulipofika, tulienda kula.
Baada ya kupumzika nikainuka ili niende kulala, wifi akaninong'oneza
"Kuwa makini usiku wa leo Sabrina"
Nikamuitikia wifi na kwenda kulala huku nikiyatafakari maneno yake ila usingizi nao ukanipitia.
Wakati nimelala nikamuona yule kijana wa ndotoni akiwa mahali na mimi kwa mazungumzo.
"Unapenda kuumia Sabrina?"
Nikatingisha kichwa nikiashiria kuwa sipendi.
"Je, unapenda kuutesa moyo wako kwa maumivu?"
Nikakataa pia.
"Basi kama hupendi rudi nyumbani kwenu"
Hapo nikashangaa na kushtuka, ile sauti ikawa inapiga kama mwangwi mule chumbani.
"Rudi kwenu Sabrina, rudi nyumbani"
Nikaanza kuogopa na kutetemeka kwani mambo ya ajabu yalinianya tena, nikabahatika kuinuka pale kitandani na kukimbilia sebleni.
Nikamkuta wifi akimbembeleza mtoto wake aliyekuwa analia sana usiku ule, ila nae aliponiona akaniambia.
"Rudi nyumbani Sabrina"
Nikaogopa na kumuuliza vizuri.
"Unasemaje wifi?"
Wifi nae akajibu kwa mshangao.
"Kwani nimesemaje?"
"Inamaana hujui ulichokisema?"
"Sijasema chochote Sabrina, si unaona mwenyewe nahangaika na mtoto hapa hataki hata kulala"
"Mmh wifi! Umeniambia nirudi nyumbani"
Ni hapo ambapo wifi alishtuka na kuniuliza kwa makini nami nikarudia nilichosema.
"Kuna kitu Sabrina, kuna kitu kipo ndani humu. Siwezi kukwambia hivyo hata mara moja. Ona mtoto anavyolia hataki hata kutulia. Nipe mikono yako Sabrina"
Wifi akanishika mikono na kuanza kuomba, haikupita muda sana hali ikawa shwari kabisa ila sikujisikia tena kulala.
Niliongea na wifi pale hadi mtoto akalala, halafu mimi na wifi tukalala pale pale.
Kulipokucha tuliendelea na kazi kama kawaida kisha wifi akaniuliza kuhusu usiku uliopita.
"Hivi ni kweli ulinisikia mimi usiku nikiongea ulivyosema?"
"Ndio wifi, wewe ndio ulisema"
"Mimi siwezi kukwambia hayo maneno Sabrina, huyo ni shetani na lazima tumuaibishe"
"Kivipi wifi?"
"Lazima shetani aaibike, wewe huendi popote utabaki hapa hapa na kesho nitakupeleka kwa mchungaji akakufanyie maombi kamili"
"Sawa wifi yangu, nitafurahi ikiwa hivyo ili na mimi niweze kuwa huru"
"Najua hilo Sabrina, amekufanya kuwa mtumwa wake na lazima ashindwe"
Mara nikapigiwa simu muda huo huo na Carlos.
Nikapokea ili kumsikia anachotaka kuniambia.
"Naomba tuonane Sabrina"
"Tuonane wapi?"
"Palepale pa siku zote"
Sikuwa na pingamizi kwavile nimekuwa nikikutana nae mara nyingi tu.
Nikamuaga wifi kuwa naenda dukani, nae hakunizuia kwavile hakujua niendako.
Nilimkuta Carlos mahali pale akiwa na hasira sana hadi nikashangaa kwani sijawahi kumuona Carlos akiwa na hasira kiasi kile.
"Mbona umechukia hivyo Carlos?"
"Kuna watu wanataka niwaonyeshe kuwa nina uwezo wa kiasi gani na mimi ni mtu wa aina gani"
"Kwanini?"
Akaniangalia sana na kuniuliza.
"Unaniamini Sabrina?"
"Ndio nakuamini kwani vipi?"
"Vizuri sana kama unaniamini, nakuahidi kuwa nitakufanyia mambo mengi sana"
"Kama yapi?"
"Tulia utauona uwezo wangu niliopewa na Mungu"
Nikamuangalia tu bila ya kuelewa chochote, kisha akasema.
"Unajua kwanini wifi yako alishindwa kutoa ile mimba?"
"Mi sijui ila nadhani ni kwavile imani yake haimruhusu"
"Imani yake haimruhusu! Unajua ni mimba ngapi alitoa hapo kabla?"
Nikazidi kumshangaa Carlos, kisha akaniambia kuwa nikamuulize kuwa ni mimba ngapi alitoa kabla na kusema atakuja badae kunitembelea tena. Nikaondoka na kurudi nyumbani bila kuelewa nia na dhumuni la Carlos ni nini kwenye maisha ya wifi yangu.
Nilipofika nyumbani wifi alikuwa ametulia kama kawaida yake na aliponiona akafurahi kurudi kwangu.
"Bora umerudi wifi yangu"
"Kuna kitu nataka nikuulize wifi"
"Uliza tu"
"Ushawahi kutoa mimba?"
"Swali gani hilo Sabrina? Unajua wazi kutoa mimba ni dhambi, haina tofauti na kuua. Kwani umepata mimba mdogo wangu?"
"Hapana, sina mimba wifi"
"Mbona umeniuliza kuhusu kutoa mimba? Unataka nikwambie maumivu yake? Kama una mimba Sabrina usithubutu kuitoa, ni dhambi sana mbele za Mungu wetu"
"Sawa wifi nimekuelewa"
Ila hakujibu swali langu kama amewahi kutoa mimba au la.
Nikiwa nazungumza na wifi, nikapigiwa simu na Sam.
Ile kupokea tu akaanza kuongea moja kwa moja.
"Hata kama tumegombana Sabrina, si vizuri kunitumia ujumbe wa kunitusi kiasi hiki"
"Ujumbe wa kukutusi? Nimekutumia saa ngapi? Umechanganyikiwa wewe"
"Sabrina, asante sana hata kama unasema kuwa nimechanganyikiwa asante sana ila kunitusi si vizuri. Kukupenda sio kosa Sabrina"
Halafu akakata simu, nikabaki nashangaa tu. Mara kidogo ukaingia ujumbe kwenye simu yangu kutoka kwa Sam.
"Poa tu Sabrina kwa kunikatia simu"
Hapo nikahisi ni wazi Sam hajielewi kwa sasa na kudhani labda amechanganywa na Lucy, sasa hasira zake ndio anamalizia kwangu.
Na ubaya simu yangu haikuwa na salio hivyo nikashindwa kumpigia wala kujibu ujumbe wake kwahiyo nikawa kimya kabisa huku nikitafakari na kushangaa tu kuwa kwanini Sam amekuwa vile alivyokuwa.
Ila haukupita muda sana nikapigiwa simu na Carlos kisha akaomba kuzungumza na wifi yangu, nikamuwekea wifi ile simu sikioni ila baada ya dakika chache niliona wifi akishusha ile simu taratibu tena bila ya kusema chochote, nikamuuliza.
"Amekwambiaje kwani?"
Wifi alinitazama tu bila ya kunijibu, ikabidi nikaendelee na kazi zangu za jioni hadi pale kaka aliporudi toka kwenye kazi yake.
Nikamsalimia na kuendelea na mambo mengine, nikaandaa chakula mezani lakini hawakuja kula ikabidi nile na kwenda chumbani kwangu kupumzika kwani wifi hakunijibu chochote tangu muda alioongea na Carlos.
Usiku wa leo ulikuwa wa ajabu sana, nilikosa raha kabisa nikiwa mule chumbani ukizingatia hata chakula nilichopika hakikuliwa na wifi pamoja na kaka kwahiyo nikawa najiuliza nini tatizo mpaka inakuwa hivi.
Sikupata jibu lolote kwakweli, nikaamua tena kwenda sebleni kuona kama wifi na kaka wameenda kulala, ila niliwakuta pale pale tena kaka akiwa amelala kwa kujinyoosha kwenye kitu kitendo ambacho kilinichanganya.
Wifi alikuwa amekaa na mtoto mikononi, nikaamua kumsogelea na kumuuliza kuhusu kaka ili amwamshe akalale, na muda huu wifi alinijibu kila nilichomuuliza pale.
"Wifi mbona hivyo, mwamshe kaka akalale ndani"
"Mwangalie kaka yako alivyo Sabrina"
Moyo wangu ukalia paaa kwa uoga, na kuuliza kwa taharuki.
"Kwani ana nini?"
"Wee msogelee tu umwangalie"
Nikamsogelea kaka kwa uoga na kumwangalia kwa makini huku na uoga ukiniandama ila nilimuona kuwa yupo sawa.
"Mbona yupo sawa wifi!"
"Mwangalie vizuri Sabrina"
Huku wifi machozi yakimlengalenga nami hofu ikanizidi na kujaribu kumuamsha kaka ila hakushtuka wala kutingishika alikuwa kama vile mtu aliyekufa, uoga ukanijaa zaidi.
Itaendelea…!!
 
SEHEMU YA 27



Nikajaribu kumuamsha kaka ila hakushtuka wala kutingishika alikuwa kama vile mtu aliyekufa, uoga ukanijaa zaidi.
Nikamuangalia vizuri kaka Deo na kumuuliza wifi.
"Mbona kaka haamki?"
Machozi yalikuwa yakimtoka wifi, huku akinijibu.
"Sijui Sabrina, sijui kwanini mume wangu haamki"
"Na mbona umekaa tu bila kufanya chochote?"
"Chochote kipi? Unafikiri ni hali ya kawaida hiyo? Akipelekwa hospitali ujue wanaenda kummalizia"
Maneno ya wifi yakaijaza hofu zaidi moyoni mwangu, nikaanza kukumbuka jinsi Carlos alivyosema kuwa ataenda kumuokoa rafiki yangu Suzy, wazo la haraka likanijia tena bila kufikiria zaidi. Nikaenda chumbani kwangu na kumpigia simu Carlos ili kama kunauwezekano basi aje atusaidie.
Ile simu haikuchukua muda sana kupokelewa, na Carlos nae hakuchukua muda sana kuwasili hadi nikajiuliza kuwa huyu Carlos anaishi nje kwetu kama jirani au! Mbona amefika muda huo huo baada ya kumpigia simu. Jibu nilikosa.
Carlos aliingia ndani kwetu kwa uhuru kabisa bila ya kuogopa kitu chochote kile, alipokuwa ndani ndio akaniuliza kuwa tatizo ni nini.
"Mtazame kaka yangu hapo"
"Huyu mwacheni nimpeleke hospitali"
Nikamuangalia wifi aliyekuwa kimya kabisa, Carlos akambeba kaka yeye mwenyewe bila msaada wowote na kumpakia kwenye gari yake kisha kuondoka nae, baada ya nusu saa Carlos na kaka walirudi nyumbani huku kaka akiwa mzima kabisa, nikashangaa sana hata wifi nae akashangaa hakuwa na la kufanya zaidi ya kuongea vizuri na Carlos kwani amemsaidia mumewe kurudi kwenye hali ya kawaida kama aliyokuwa nayo zamani.
Kaka alikuwa akimshukuru tu Carlos na kuona kuwa Carlos ni mtu mwema.
"Pole sana mtu wa watu, wamekusumbua usiku wote huu"
"Hata msijali jamani, mimi mwenyewe nilimwambia Sabrina kuwa endapo atakuwa na tatizo lolote lile basi asisite kuniambia"
"Basi ni vizuri kama ni hivyo"
Carlos nae akaanza kuzungumza yake kwani alijuwa wazi kuwa ni lazima atasikilizwa tu.
"Halafu huyu Sabrina kuna kitu kinamsumbua sana"
Kaka akadakia.
"Kitu gani?"
"Huenda ikawa mizimu ya kwenu, kinamtaka arudi nyumbani. Mimi naona ni bora mkamruhusu kuwa arudi tu kabla mambo hayajaharibika"
Kaka hakuwa na pingamizi lolote kwa Carlos, nadhani alishaiteka akili ya kaka kwahiyo imekuwa rahisi kumkubalia, wifi nae alishapumbazika.
"Ila kwa mwezi huu niko busy sana, hakuna wa kumrudisha nyumbani"
Mara hii nilicheka kwani niletwe na kurudishwa nimekuwa mtoto mdogo au! Carlos akamjibu kaka,
"Usijali kwa hilo, mimi nipo na nitahakikisha nampeleka hadi nyumbani kwenu. Mwenyewe utafurahi"
Waliongea mengi bila kujali kuwa ni usiku na watu karibia wote wamelala kasoro sisi, kaka akamkubalia Carlos kuwa aje anichukue na kunirudisha nyumbani, badae wakaagana nae bila ya kumuuliza kuwa na yeye je anaishi wapi maana anapoishi hata hapajulikani.
Alipoondoka kila mmoja akaenda kulala hadi kulipokucha.
Kulipokucha, nikiwa chumbani kwangu nikamsikia wifi akiniita.
"Hivi usiku kulikuwa na nini?"
"Inamaana hujui wifi kama kulikuwa na nini!"
"Hivi ilikuwa ni kweli au ni ndoto?"
Nikamshangaa wifi, tulikuwa wote halafu anashindwa kutambua kama ilikuwa ni kweli au ni ndoto.
"Wifi, inamaana huelewi chochote hapo ulipo? Ilikuwa ni kweli na wala sio ndoto wifi yangu"
"Mmh! Halafu mimi nikashindwa hata kukemea mdogo wangu! Inawezekana kweli? Labda kuna mtu alinipumbaza, sio bure kwakweli. Nakosa hata jibu."
"Pole wifi ila ndio ilivyokuwa"
"Ila si nilikwambia kuwa leo tutaenda kwa mchungaji, itabidi tufanyiwe maombezi"
"Hapana wifi, leo narudi nyumbani"
Wifi akabaki kushangaa bila ya kuelewa chochote kinachoendelea.
Mchana wa siku hiyo nilimsikia wifi akiongea na kaka, nikasikia akibishana nae kuhusu kuondoka kwangu pale na kurudi nyumbani kwetu.
Baada ya kukata simu akaniita na kuniuliza.
"Kaka yako nae kapatwa na nini? Yani amekubali kabisa wewe uondoke!"
"Ndio amekubali, mbona na wewe ulikubali wifi"
"Hapana, mi sijakubali bado nakuhitaji hapa"
"Ila mimi nikiendelea kukaa hapa nitamwambia kaka ukweli kuhusu huyo mtoto, unakubaliana na mimi!"
"Yanatokea wapi sasa hayo jamani Sabrina?"
"Kwasababu sitaweza kukaa kimya kwa kipindi kirefu, kumbuka mumeo ni kaka yangu wa damu. Acha tu nirudi nyumbani wifi"
"Nakuomba ombi moja mdogo wangu"
"Lipi hilo?"
"Ukienda huko kwenu usimwambie hata mama yako ukweli, nitaumbuka mimi jamani"
"Mmmh hadi mama!! Nitaweza kweli? Ungekuwa wewe wifi ungeweza kumficha mama yako mzazi kuhusu hili?"
"Nakuomba Sabrina, kama ulivyonyamaza kwa kaka yako fanya hivyo na huko. Fanya kamavile hakuna lililowahi kutokea. Nisaidie mimi wifi yangu."
"Nitajaribu wifi, je hiyo ndio sababu pekee ya kunizuia mimi kurudi nyumbani?"
"Hapana, nakuhurumia pia na maisha yako, nayahurumia na maisha yangu pia. Sijui kwanini siri hii inanitesa hivi!"
"Usijali kuhusu hiyo siri wifi ila matumaini yangu ni kuwa ipo siku utamwambia kaka yangu ukweli kuhusu huyo mtoto"
Nikaamua kufanya mambo yangu mengine, huku nikimsubiri huyo Carlos aje kunichukua ili niweze kurudi nyumbani.
Nikiwa chumbani kwangu huku nikitafakari baadhi ya mambo yanayoendelea, wifi akaniita tena nikaamua kumuuliza,
"Mbona unakuwa kama mtu mwenye mashaka sana wifi yangu?"
"Hata hujakosea, ni kweli nina mashaka sana"
"Nini unaogopa wifi? Bado unahofu na siri yako?"
"Aaah! Hapana, ila ni kuhusu zile picha hebu kaniletee tena"
"Zile ulizoniambia kuwa si za kawaida?"
"Ndio, hizohizo naomba uniletee"
Ikabidi nikazipekue tena kwani nilishaziweka kwenye begi, nikazichukua na kumpelekea. Akaziangalia kwa makini sana, na kuishika picha moja wapo na kuniuliza.
"Umesema kuna nani na nani hapa?"
"Mpenzi wangu na rafiki yangu"
"Una hakika kuwa huyu ni mpenzi wako?"
Nikaitikia kwa kichwa kuwa nina uhakika, wifi akaniangalia kwa umakini sana na kusema.
"Yani picha anaonekana kaka yako na mwanamke halafu wewe unasema mpenzi wako na rafiki yako! Ndiomana nilikwambia kuwa hizi picha si za kawaida, namuamini sana Deo hawezi kunisaliti kiasi hiki cha kupiga picha na mwanamke mwingine"
Nikamshangaa sana wifi kwani zile picha ziliwaonyesha Sam na Lucy wakiwa pamoja halafu yeye anadai ni kaka Deo na mwanamke, nikamuuliza tena wifi,
"Utakuwa umechanganyikiwa wifi, kaka Deo yuko wapi hapo?"
"Wewe ndio umechanganyikiwa Sabrina, huyu ni kaka yako na mwanamke halafu wewe unasema ni mpenzi wako! Wewe Sabrina umechanganyikiwa kweli kabisa nakwambia"
Nikamuangalia tu wifi ambaye nilikuwa nikimshangaa muda wote, akachukua zile picha zote na kuzichana chana vipande vipande huku akisema.
"Siamini kabisa kama Deo anaweza kunisaliti, hata siku ile ya kwanza uliponionyesha zile picha sikuamini. Ila za mwizi arobaini, kama kweli kaka yako ananisaliti basi nitajua tu"
"Usiwe na hasira sana wifi, kwani hata mimi sielewi unachosema"
Nilitulia tu na kuona kuwa ni wazi mimi na wifi tumevurugwa ila hakuna la kufanya na kueleweka kwa urahisi zaidi.
Nikiwa nimetulia ndani, Carlos akanipigia simu na kusema kuwa yupo njiani kuja kwa kaka kunifata.
Sam nae akanipigia simu.
"Hivi Sabrina, huko ulipo sasa na huku kuna umbali upi?"
"Kwanini umeuliza hivyo Sam?"
"Nijibu kwanza"
"Kwakweli ni mbali, yani kama masaa mawili au matatu kufika kama barabara haina foleni"
"Na Carlos je anaishi wapi?"
Hapa sasa ikawa kamavile Sam kanizindua akili yangu kwani hata mi mwenyewe sikujua mahali ambako Carlos anaishi.
"Kwakweli sijui"
"Basi muulize, akikupa jibu niambie halafu nitakwambia jambo fulani"
Sam akakata simu na kuniacha nikiwa na maswali mengi sana kwenye kichwa changu kuhusu Carlos, nikaanza kujiuliza sasa.
"Carlos anaishi wapi? Nilipokuwa kwetu alikuwa anakuja mara kwa mara, nipo huku napo anakuja kila siku. Je, anaishi wapi?"
Ni maswali yaliyokosa majibu kichwani mwangu ila nikajipanga kumuuliza Carlos atakapokuja kunichukua wakati wa kuondoka.
Muda ukapita kidogo na Carlos akawasili pale nyumbani kwa kaka.
Wifi alimuangalia Carlos kwa macho ya ghadhabu sana, kisha nikamsikia Carlos akimwambia wifi yangu.
"Na bado, utagundua mengi sana Joy"
Ila wifi hakujibu kitu chochote, alimuangalia tu.
Kaka nae akawasili muda uleule na kutukuta pale ndani pamoja na Carlos, baada ya salamu akaanza kuuliza.
"Nilifikiri mtakuwa mmeshaondoka, mbona mpaka sasa bado?"
Carlos akamjibu kaka.
"Mkeo hayupo tayari kuwa Sabrina aondoke, ndio tunangoja ruhusa kutoka kwake"
Mimi na wifi tukamshangaa sana Carlos kwa maneno yale, kaka akamuangalia wifi na kumuuliza.
"Eti hujawaruhusu? Si tulishaongea kwenye simu tayari!"
Wifi alizidi kuwa kimya, Carlos nae akaongezea maneno mengine.
"Tatizo ni kwamba Sabrina ana siri nyingi sana za wifi yake, sasa ......"
Kabla Carlos hajaendelea wifi alidakia kwa haraka sana.
"Mbona niliwapa ruhusa muda mrefu sana, nyie nendeni tu kwa amani"
Carlos akatabasamu na kuinuka ili tuianze safari ila kaka nae akauliza.
"Kwani hizo siri ni siri gani?"
"Hakuna cha siri mume wangu, huyo kijana ameongea yake tu"
Carlos alikuwa tayari ameshatoka nje.
Wifi akanifata na kuniambia kwa taratibu.
"Keshokutwa nitakuja hukohuko nyumbani na tutaongea vizuri ila kuwa makini sana huyo sio mtu"
Nikamuitikia na kwenda kupanda gari ya Carlos kwaajili ya safari.
Tukiwa ndani ya gari Carlos akaniuliza,
"Unataka tuwahi kufika au tuchelewe?"
"Kila mtu anapenda kuwahi kwakweli, hakuna anayependa kuchelewa"
"Wewe je unapenda lipi?"
"Napenda tuwahi ila itategemea na foleni barabarani"
Na tulipofika barabara kuu ni kweli kulikuwa na foleni sana hata yale matumaini ya kufika mapema yakapotea kabisa, nikamuangalia Carlos na kumwambia.
"Hatuwezi kuwahi tena kwani foleni ni kubwa sana"
"Ila bado kuna uwezekano mkubwa wa kuwahi"
"Upi huo"
"Fumba macho mpaka nikwambie fumbua, utaona mwenyewe"
Nikafumba macho ila kauli ya mwisho ya wifi ikatembea tena kichwani kuwa Carlos si mtu, nikajikuta natamani kufumbua macho ili nijue afanyacho hapohapo nikafumbua macho.
Nikaona lile gari tulilopanda limepaa angani kama ndege.
Nikaanza kupiga kelele kwa uoga.
Itaendelea muda sio mrefu…!!
 
SEHEMU YA 28



Nikaona lile gari tulilopanda limepaa angani kama ndege.
Nikaanza kupiga kelele kwa uoga.
Hofu ikatanda moyoni mwangu, kwa kelele nilizopiga nadhani hata ndege angani walinisikia.
Nikamuona Carlos akiniangalia kwa macho makali sana na gafla nikalala usingizi mzito na sikujua chochote kilichoendelea tena mahali pale.
Carlos akanishtua toka usingizini, jambo ambalo lilinishtua sana.
"Mbona unashtuka hivyo Sabrina? Tumeshafika nyumbani kwenu"
Nikawa nashangaa kamavile mtu aliyepoteza kumbukumbu zake za maana, nikamuangalia Carlos kwa makini na kukumbuka kuwa mara ya mwisho tulikuwa tunapaa angani.
"Tumefika? Mbona tulikuwa tunapaa?"
Carlos nae akashangaa,
"Tunapaa! Muda gani huo?"
"Muda uliponiambia nifumbe macho, nikafumbua na kuona gari inapaa"
Carlos akacheka sana na kusema.
"Kweli Sabrina wewe una maruweruwe, hebu twende huko ndani kwenu nikakueleweshe vizuri"
Ikabidi tuingie ndani kwanza.
Ila hakuwepo mama wala dada Penina na mlango ulikuwa umerudishiwa tu, sikushangaa sana kwavile sikuwapa taarifa kama narudi leo.
Kwahiyo nikakaa pale sebleni na Carlos.
"Haya sasa nieleweshe nisichoelewa"
"Sikia Sabrina, nilikwambia ufumbe macho ili ulale na siku zote mtu anayelala wakati wa safari hushtukia tu wakati ameshafika, hilo ndio lilikuwa lengo langu kwako.
"Na mbona gari ilipaa?"
Niliuliza kwa ujasiri ila moyoni uoga ulinijaa kwavile sikuwa na amani kabisa na Carlos.
"Sabrina ulikuwa umelala, hizo ni ndoto tu. Tangu lini gari likapaa?"
Nikawa kimya nikimuangalia huku nikitafakari kama kweli ni ndoto.
"Ila nilifumbua macho kabisa"
"Hizo ni ndoto tu Sabrina usipende kuzitilia umakini sana"
Mama nae akawa amerudi na kutukuta mule ndani.
"Kheee Sabrina! Umerudi bila hata taarifa?"
Nikainuka na kumkumbatia mama kisha kumsalimia.
Halafu mama akasalimiana na Carlos aliyeanza kuaga na kusema kuwa atakuja kesho, kisha akaondoka.
Mama akaniuliza,
"Penina kaenda wapi?"
"Sijui ila nimekuta mlango umerudishiwa tu"
"Na bora umerudi maana huyu Penina atafanya tuibiwe humu ndani, vipi maruweruwe yako siku hizi yamepungua?"
"Ndio yamepungua mama"
Tuliongea na mama pale hadi aliporudi dada Penina, moja kwa moja mama akamuanzia na maswali.
"Ulienda wapi Penina na kuacha mlango wazi?"
"Khee mama, ngoja nimsalimie mdogo wangu kwanza"
Nikasalimiana pale na dada Penina.
"Nimemuona Carlos hapo njiani, nilikuwa na rafiki yangu basi alipomuona Carlos katoka nduki, sijui hata ana matatizo gani yule shoga yangu?"
Mama akamuuliza,
"Sasa vipi ulimfatilia?"
"Nimfatilie wa kazi gani wakati kajitia uwehu mwenyewe. Atajijua huko"
"Mmh! Roho mbaya hiyo Penina, ungemfatilia kwani huwezi jua matatizo yake hivyo hivyo bila ya kumfatilia"
Dada Penina hakujali na kuendeleza stori zingine anazojua yeye hadi muda wa kula na kulala ulipofika.
Nilienda kulala chumbani kwangu na nililala vizuri leo bila tatizo lolote hadi kunakucha.
Asubuhi yake nikapigiwa simu na Suzy.
"Bado upo kwa kaka yako Sabrina?"
"Hapana, nimesharudi nyumbani"
"Basi kesho nitakuja kwenu, nina mengi ya kuzungumza na wewe Sabrina"
"Hakuna tatizo Suzy, utanikuta tu"
Sikujua mazungumzo ya Suzy yatamuhusu Sam au Carlos maana wote wanahusika kati yetu.
Nikatulia kungoja hiyo kesho kuona nini Suzy ataniambia.
Nilitoka nje na kumkuta mama akiendelea na kazi.
"Sijataka kukusumbua leo maana hukawii wewe kusema kuwa mama ana roho mbaya"
Nikacheka tu na kumsalimia kisha kumsaidia kazi za hapa na pale.
Nikasikia simu yangu ikiita, nikaenda kupokea.
"Nasikia umesharudi nyumbani kwenu Sabrina!"
"Ndio nipo nyumbani"
"Ulimuuliza Carlos nilichokwambia?"
Hapo ndio nikakumbuka na kumjibu Sam kuwa sijamuuliza ila nitamuuliza iwapo nikionana nae. Sam akaniomba tukutane jioni ya leo ili aniambie baadhi ya mambo yanayompa mashaka, nami nikakubali wito wake.
Nikarudi jikoni ili kuendelea na kazi.
Jioni ilipofika nilijiandaa ili niweze kwenda kuonana na Sam, kabla sijatoka nikafikiwa na ugeni naye alikuwa ni Carlos aliyeongozana na kijana flani hivi ambaye sikumfahamu, ikabidi niwakaribishe ndani.
Mama nae akaja kusalimiana nao, ambapo Carlos alitutambulisha kuwa kijana yule ni ndugu yake.
Nikashindwa kutoka tena, ila nadhani Carlos alikuwa anajua kama mimi nataka kutoka, kwahiyo akasema,
"Nenda tu Sabrina uendako, sisi nia yetu hapa ni kuzungumza na mama yako tu"
Mama akashtuka na kuuliza
"Kwani Sabrina unataka kwenda wapi?"
Nikajiumauma kwani sikuwa na maelezo ya kueleweka, Carlos akasema tena.
"Mwache aende tu mama, akirudi atakwambia alipotoka"
Mama hakuwa na pingamizi, nae akaniruhusu niende hadi nikashangaa. Niliondoka huku nikijiuliza kuwa Carlos anataka kuzungumza nini na mama yangu na huyo ndugu yake hata sikuelewa kwakweli.
Nilienda moja kwa moja mpaka eneo nililoahidiana na Sam, nikamkuta Sam ananingoja.
"Pole sana, umenisubiri muda mrefu eeh!"
"Ndio salamu hiyo Sabrina?"
"Samahani, mambo vipi?"
Huku nikivuta kiti na kukaa.
"Yani hatujaonana kwa siku nyingi na salamu inaishia mambo vipi tu!"
"Aaah! Mada ya salamu imeisha bhana, tuongee mambo ya muhimu sasa"
Ikabidi Sam nae akae maana aliona kuwa sipo kama alivyonifahamu zamani.
"Nia yangu kubwa ni kumuongelea Carlos"
"Kafanyaje?"
"Carlos amekuja katika maisha yetu kwa lengo moja tu"
"Lengo gani hilo?"
"Anataka kuharibu maisha yetu na pia kuvuruga amani, halafu kikubwa zaidi anataka kututenganisha"
"Atutenganishe kwa lipi na kwanini?"
"Carlos anakutaka Sabrina, anataka uwe mpenzi wake. Tangia amekuja katika maisha yetu tumekuwa tukigombana kila siku. Nimejaribu kuchunguza na kugundua kuwa chanzo cha yote haya katika maisha yetu ni Carlos. Si mtu mzuri yule"
Nikajisikia kucheka kwani sikujua kama Carlos anaweza akanitaka na asiniambie siku zote hizo ambazo huwa nakuwa nae.
"Acha wivu Sam, Carlos ni rafiki tu wala hakuna chochote kinachoendelea kati yangu na yake. Tofauti kabisa na wewe ukiwa na Lucy wako"
"Kwanza Sabrina naomba utambue kuwa hakuna mahusiano yoyote kati yangu na Lucy, hata sisi wenyewe tunajishangaa"
Nikajua hapo Sam anatafuta njia ya kujitetea tu wakati kila siku nambamba akiwa na Lucy.
Sam akaendelea kuongea kuhusu Carlos.
"Halafu kitu kingine, Carlos sio mtu wa kawaida"
"Kama sio mtu wa kawaida ni nani? Na kwanini useme kuwa sio mtu wa kawaida?"
"Nitakwambia kilichotokea wakati Suzy amepatwa na matatizo, ndiomana nasema kuwa Carlos sio mtu wa kawaida"
"Niambie basi nielewe"
Sam akaanza kunielezea kuhusu Suzy, siku aliyopata matatizo na hapo kwa mbali nikaelewa kwanini Carlos alinikataza kupiga sinu kwakina Suzy kwani alijua lazima ningeshtuka tu.
"Siku ambayo Suzy alipatwa na matatizo, mimi na Lucy tulikuwa nyumbani kwao"
Hapo alipotaja jina la Lucy nilihisi kuchefuka moyoni ila nikaendelea kumsikiliza tu.
"Eeh ikawaje?"
"Kwakweli Suzy alikuwa na hali mbaya sana, hivyo tulikuwa kwenye harakati za kumsaidia"
"Ngoja nikukatishe kwanza, kwani Suzy alipatwa na nini?"
"Alikutana na watu wakampiga sana, halafu wakamtegeshea nyoka aliyemng'ata Suzy ila ukikutana nae atakusimulia vizuri zaidi, ngoja mimi niendelee na habari za Carlos"
"Haya endelea"
"Muda ule mama Suzy anakupigia simu wote tulikuwepo pale, alipokata tu haikupita hata dakika mbili Carlos aliwasili eneo la tukio na kusema amepewa taarifa na wewe kwahiyo amekuja kutusaidia. Swali langu sasa, hiyo taarifa ulimpa saa ngapi? Na je lile eneo ambalo Suzy alipatia matatizo amelijuaje wakati hata mama Suzy hakukutajia wewe?"
Hapo nikamkatisha Sam kwani nilikumbuka kuwa Sam alinipigia simu kuhusu Suzy.
"Kama ulikuwepo eneo la tukio mbona ukanipigia simu kuulizia hali ya Suzy?"
"Nia yangu nilitaka upige simu kwa kina Suzy na uweze kumtambua Carlos ni mtu wa aina gani! Hajulikani anapoishi wala hana ndugu, sasa huyo ni mtu gani?"
Hapo nikakumbuka kuwa leo Carlos amekuja na ndugu yake nyumbani kwetu.
"Kuhusu swala la ndugu, Carlos ana ndugu zake bhana. Leo alikuja na ndugu yake nyumbani kwetu"
"Tatizo lako Sabrina hutaki kukubali ukweli. Haya tuongelee mapenzi yetu sasa"
Nikatulia kwa makini ili nimsikilize hoja zake kuhusu mapenzi yetu, ingawa moyo wangu ukaniambia kuwa atakayoyasema Sam yote ni uongo tu kwani kashampenda mtu mwingine.
"Unajua Sabrina nakupenda sana, halafu...."
Kabla hajaendelea, alikuja Lucy na kusimama nyuma ya Sam kisha kuingilia yale maongezi huku akiwa amemuinamia Sam na mikono yake ikazunguka kwenye kifua cha Sam, huku akiongea sauti ya taratibu kama mtu anayenong'oneza sikioni kwa Sam.
"Halafu nini?"
Nikapatwa na hasira kwani muonekano wa Lucy kwa Sam ulinikela sana, kilichoniudhi zaidi ni kumuona Sam ametulia kama sanamu bila ya kufanya chochote hata kumzuia Lucy na mikoo yake iliyokuwa ikimpapasa hakumzuia.
Hasira ikanizidia na kuona cha msingi ni kupambana na Lucy tu kwani amezoea kunifatilia na mpenzi wangu.
Nikainuka kwa ghadhabu huku hasira zikiwa zimenijaa kooni tena bila hata ya kufikiria mara mbili, nikachukua chupa ya soda niliyokuwa nakunywa na kumpiga nayo Lucy kichwani.
Hapohapo, Lucy akaanguka huku damu zikimtoka puani na mdomoni.
Itaendelea…!!
 
SEHEMU YA 29



Lucy akaanguka huku damu zikimtoka puani na mdomoni.Uoga ukanijaa na akili yangu ikasema haraka sana kuwa "Umeuwaaa" moja kwa moja nikawaza kifungo cha maisha au kuhukumiwa adhabu ya kifo, sikufikiria zaidi na kuanza kukimbia.
Nilikimbia sana bila ya kuangalia nyuma wala nini na hakuna aliyenikimbiza.
Nikapishana na gari ya Carlos njiani, nadhani walitoka nyumbani kwetu. Ingawa ilisimama ila sikulisogelea hata kidogo na kuendelea kukimbia, hatua ya kwanza ilikuwa ni nyumbani kwetu huku nikihema kwa nguvu kama jibwa koko.
Mama akaniona wakati naingia ndani huku nikihema juu juu na kuniuliza.
"Una nini Sabrina, mbona hivyo?"
"Mama nimeuaaa"
Hapo hapo nikaanguka chini na kuzimia kwani nguvu zote ziliniisha na sikuelewa tena kilichoendelea baadae.
Nilipozinduka, nilijikuta chumbani kwangu.
Nikainuka na kuanza kurudisha kumbukumbu nyuma, hapohapo nikakumbuka kuwa tukio la mwisho ni kumpiga Lucy kwa chupa ya soda kichwani. Nikakumbuka jinsi damu zilivyokuwa zikimtoka Lucy na jinsi nilivyokimbia huku nikiwaza kukamatwa.
Wazo jingine likanijia kuwa kwanini nilikimbia wakati makosa ni yangu na ilitakiwa mimi ndio nimsaidie rafiki yangu, ila nitamsaidiaje zaidi ya kukamatwa na kushtakiwa? Na je kukimbilia nyumbani ndio suluhisho? Wakati Sam anapajua kwetu na ataweza kuwaleta maaskari muda wowote ule, wazo likanijia kuwa hata kukaa nyumbani napo si salama.
Mara mlango wa chumbani kwangu ukafunguliwa, nikashtuka sana ila ni mama ndiye aliyeingia.
"Sabrina mwanangu umeamka? Eeh bora, kumbe Carlos alinipa ushauri mzuri"
Nikataka kuuliza kuwa ni ushauri gani ila kabla sijauliza ikasikika hodi toka nje, hapo pia nikashtuka na hofu kunitanda moyoni.
Mama akatoka kwenda kumkaribisha mgongaji, nikatamani hata kuingia uvunguni ili nijifiche.
Mara mama akaniita, nilitoka kwa uoga hadi sebleni na kumkuta mgeni mwenyewe kuwa ni Carlos, na moja kwa moja akaniuliza.
"Unaendeleaje Sabrina?"
Nikawa namjibu kwa wasiwasi huku uoga na hofu vikizidi kunitawala.
"Naendelea vizuri"
"Usijali kwa ulichokifanya, mimi nitashughulikia na kukusaidia"
Mama akadakia,
"Kwani amefanyaje?"
"Sabrina amegombana na rafiki yake huko baa, halafu amempiga mwenzie na chupa kichwani."
Mama akashtuka sana na kuniuliza kwa hamaki.
"Umeanza lini kupigana Sabrina?"
"Nisamehe mama, sikudhamilia"
Huku machozi yakinilengalenga.
"Hukudhamilia nini? Yani unampiga mtu na chupa kichwani? Unajua madhara yake kweli? Kwanza mmegombania nini hadi kupigana hivyo?"
Carlos akadakia,
"Walikuwa wanamgombea Sam, yule mpenzi wa Sabrina sasa siku hizi amekuwa na mahusiano na Lucy. Hapo ndipo ugomvi wao ulipoanzia"
Mama akapandisha hasira zaidi.
"Yani Sabrina unafikia hatua ya kumpiga na chupa rafiki yako mpenzi Lucy sababu ya huyo paka Sam! Mara ngapi nimekukataza kuwa na hiko kidubwasha? Mara ngapi? Wewe mtoto wewe utaniua mimi jamani"
"Nisamehe mama"
"Msamaha wako utasaidia nini wakati mwenzako anahangamia huko! Nitaiweka sura yangu wapi mimi nikikutana na mama Lucy? Mungu wangu, mtoto wewe umeniadhirisha jamani. Bora ungebaki hukohuko kwa kaka yako. Yani kujifanya unaharaka hapa walivyokuja Carlos na nduguye kumbe ndio ulikuwa unaenda kufanya huo upuuzi!"
Mama akainuka kwa hasira na kuanza kunipiga ila Carlos akamzuia mama na kusema.
"Usimpige, alikuwa na hasira tu. Hakudhamilia kumpiga rafiki yake ila imetokea kwa bahati mbaya tu na nitamsaidia kwa hilo. Lucy atapona na atakuwa mzima kabisa, msijali kitu kuhusu hilo"
Mama akamuuliza Carlos.
"Ila baba, si watakuwa wanamtafuta Sabrina kwa hilo kosa?"
"Ni kweli watamtafuta ila mimi nitashughulikia, hili swala niachieni mimi maana hata Sabrina alipokimbia, mimi ndio nilienda pale kuwasaidia. Jambo la muhimu kwasasa ni moja tu"
Mimi na mama tukajikuta tukisema kwa pamoja.
"Jambo gani hilo?"
"Sabrina unatakiwa kuwa makini kwasasa, usiwasiliane na Lucy wala Sam hadi mambo yatakapokuwa shwari. Na wala usitoke toke hovyo hapa nyumbani kwenu, tulia hapa hapa halafu kila kitu nitasawazisha"
Mama akaanza kumshukuru Carlos.
"Asante sana baba, endelea na moyo huo huo jamani. Kwasasa Sabrina yupo chini yangu, hatoenda popote. Tusaidie tu baba hatuna cha kukulipa"
Carlos akaaga huku akiendelea kunisisitiza jambo moja tu kuwa nisiwasiliane na Sam wala Lucy halafu nisitoke toke nyumbani. Mama nae aliendelea kumshukuru hadi alipoondoka.
Niliingia chumbani na kujifikiria sana bila hata ya kupata majibu, yani ni jana tu ndio nilifika nyumbani halafu leo nimeenda kufanya mambo makubwa kama yale. Kwakweli moyo uliniuma na kukosa majibu ya niwazacho. Nikajiuliza je huyo Carlos ananisaidia kwa namna gani? Sikujua ila ninachojua ni kuwa ananisaidia tu, naona maisha yangu yanaelekea pabaya kwani kila kitu kinanitesa, mawazo ya mapenzi, mawazo ya maisha vyote hivi vinanitesa sana na wala sikuelewa ni nini kinaendelea kwangu, nikatamani kuwa na kazi ya kufanya ila sikuwa na kazi, nalo likawa ni tatizo pia katika maisha yangu.
Mawazo yalikuwa mengi sana kwangu bila hata ya majibu.
Nikamsikia dada Penina akiongea na mama sebleni na kugundua kuwa dada amerudi.
Akaja chumbani kwangu,
"Pole mdogo wangu kwa matatizo, mbona hujawahi kuniambia kama wewe na Lucy mnatembea na Sam?"
"Nilikwambia dada, labda umesahau tu"
"Pole sana, bora hata Carlos alikuwepo kukusaidia mdogo wangu"
Nilimuangalia tu dada bila ya kusema chochote cha zaidi, tukaongea pale hadi muda wa kula.
Tukaenda kula, kisha nikarudi chumbani mwangu kwaajili ya kulala.
Nilipokuwa chumbani, mawazo mengi sana yalinitawala hadi nikakosa usingizi.
Nikawaza hali ya Lucy kuwa anaendeleaje, nikajilaumu sana kwa kuamua kumpiga rafiki yangu sababu ya mwanaume, nikajisemea.
"Kama hanipendi hanipendi tu, kupigana sio suluhisho. Ama kweli hasira hasara"
Sikuwa na uwezo wa kuonana tena na Sam wala Lucy, halafu nitakuwa ndani kama mfungwa. Nimepata hasara kweli kwani sikuwa na amani tena. Nikatamani kumpigia simu Sam ila moyo wangu ukasita, mara simu yangu ikaita kuangalia alikuwa ni Carlos anayenipigia.
"Umelala Sabrina?"
"Nipo macho"
"Vipi, bado una mashaka?"
"Kiasi, lazima mashaka niwe nayo"
"Ondoa hofu Sabrina, muda wote tambua kwamba Carlos yupo kwaajili yako. Nitakusaidia kwa chochote na kwa lolote, usijali kitu chochote"
"Sawa nimekuelewa, asante"
"Lala kwa amani, nitakutembelea ndotoni mwako"
Nikacheka kwani nilijua ni maneno ya utani kwavile si rahisi mtu kuamua kutembelea ndotoni kwa mwenzie, nikaishia kumjibu.
"Haya karibu"
Nikaagana nae na kulala sasa.
Nikajiona nipo kwenye bustani nzuri sana, yenye upepo mzuri unaopepea kwa utaratibu unaopendeza.
Nikakaa chini ya mti mmoja wa matunda, halafu akaja yule kijana wa ndotoni mbele yangu akaita,
"Hawa"
Nikamjibu, "Mimi sio Hawa"
Akacheka na kuniuliza,
"Kwanini wewe sio Hawa?"
"Mimi naitwa Sabrina"
Akacheka tena, leo ikawa mara ya kwanza kwangu kuongea vizuri na huyu mkaka wa ndotoni kwenye ndoto.
Kisha akaniuliza,
"Kwanini ulitaka kumuua mwenzio?"
Hapo nikachukia sasa, naye akaendelea kuongea.
"Najua yote sababu ya mapenzi, kwanini uangamie sababu ya mtu mmoja? Je huoni mimi ninavyokupenda?
Na lazima nikuoe Sabrina"
Nikajibu kwa ukali,
"Huwezi kunioa"
Akacheka tena na kusema,
"Ndiomana nimekuita Hawa"
Akaendelea kucheka, nami hasira zikanizidi kwani sikujua ni kwanini ameniita Hawa na kwanini ang'ang'anie kuwa atanioa. Nikajibu kwa nguvu sasa,
"Huwezi kunioa"
Nikashtuka toka usingizini na kuhisi harufu ya marashi mazuri ikiwa imetapakaa chumbani kwangu, hapo uoga ukanishika na kuhisi mauzauza yanaanza kujirudia tena ila sikuona chochote zaidi ya ile harufu ya marashi iliyotapakaa chumbani kwangu.
Ila kabla sijafanya chochote tena, usingizi ulinichukua nikalala hadi kunakucha.
Nilipoamka asubuhi nikaenda kufanya kazi zangu kama kawaida, leo sikutaka kushurutishwa na nikakumbuka kuwa wifi alisema atakuja leo, pia rafiki yangu Suzy nae alisema kuwa atakuja leo kunipa habari kamili kuhusu Carlos.
Ujio wa wifi sikumwambia mama nilitaka ashtukizwe tu kwani najua ni kitu ambacho hajakitegemea, na leo dada yangu Penina nae alikuwa nyumbani kwani ilikuwa ni mwisho wa wiki.
"Nakuona Sabrina unajishughulisha sana leo"
Dada alinitania, halafu mama nae akadakia
"Mwache ajishughulishe, hapo alipo hana pa kwenda kwa mauza uza yake aliyoyafanya"
Ila dada akanipa moyo,
"Usijali Sabrina, yote yataisha"
Tulifanya kazi zote za asubuhi na kumaliza, mchana wake tukafikiwa na mgeni ambaye ni wifi Joy, mama akafurahi sana.
"Bora umemleta mjukuu wangu nyumbani kwa bibi na babu yake jamani"
Mama akampokea mtoto kwa furaha sana huku wakiongea mengi ya hapa na pale.
Dada Penina nae alikuja kumsalimia wifi ingawa anavisa nae vya muda mrefu sana.
"Karibu Joy, na bora umekuja mwenyewe maana sikuwa hata na mpango wa kuja huko"
"Ndio maneno gani hayo Penina?"
"Mmh mama, nimeongea tu kusafisha koo"
Maongezi mengine yakaendelea, wifi akaniambia kuwa kuna jambo muhimu sana lililomleta leo kuzungumza na mimi.
Wakati mama amembeba mtoto na kucheza cheza nae, mimi na wifi tukaingia chumbani kwangu ili tuongee kwanza.
"Sikia Sabrina mdogo wangu, kuna jambo kubwa sana nimeligundua kuhusu Carlos"
"Jambo gani hilo wifi?"
Kabla hajanijibu tukasikia mlango wa chumbani kwangu ukifunguliwa halafu akaingia Suzy, nadhani mama alimwambia kuwa aingie moja kwa moja chumbani kwangu. Ila alivyoingia tu, mara gafla nikamuona wifi akiinuka na kumtazama kwa makini Suzy kisha akamzaba kibao.
Itaendelea muda sio mrefu…!!
 
SEHEMU YA 30


Mara gafla nikamuona wifi akiinuka na kumtazama kwa makini Suzy kisha akamzaba kibao.
Nikashangaa kwavile sikujua kwanini wifi kamzaba kibao Suzy, kisha akamkunja.
Ikabidi niingilie kati,
"Kwani kuna nini wifi? Huyu ni rafiki yangu."
Wifi akaongea kwa hasira
"Huyu rafiki yako hafai, ni kahaba huyu. Anatembea na mume wangu"
Kwakweli hapo nikaduwaa na kushangaa, wifi aliendelea kumkunja Suzy ambaye hata kujitetea alishindwa. Ikabidi nimuite mama ili aje kusuluhisha, mama nae akaja kuuliza.
"Kwani vipi hapa?"
Wifi akiongea kwa hasira tena,
"Huyu mtoto anatembea na mume wangu"
"Yani Suzy akatembee na mwanangu Deo! Si kama kaka yake yule jamani! Eti Suzy ya kweli haya?"
Suzy alicki akijiuma uma tu kwa maneno wala hakueleweka, ikabidi wote tutoke twende sebleni tukaongee vizuri.
Mama akamuuliza wifi,
"Unaushahidi lakini Joy?"
"Ndio ushahidi ninao, si unaona anashindwa hata kujibu kwa aibu"
Kwakweli sikuelewa, yani mume wa mtu anayetembea nae Suzy ndio kaka yangu Deo! Sikuelewa kabisa.
Mabishano yalikuwa makubwa sana kwani wifi hakukubali kumwachia Suzy, alitaka kumkomesha.
Nikajaribu kumpooza wifi ila ilikuwa ngumu huku akidai kuwa mume anauma. Nami nikajisemea kimoyo moyo kuwa hata mpenzi anauma ndiomana mi mwenyewe nimemuumiza Lucy bila ya kutarajia.
Ikabidi itumike njia nyingine ya kumuondoa Suzy pale nyumbani kwani wifi alikuwa na hasira sana tena sana.
Suzy alipoondoka, wifi nae hakukaa sana akaaga na kuondoka nadhani hasira ilimzidia halafu akahisi labda na sisi tunajua kitu kuhusu Suzy na kaka Deo ndiomana tukamruhusu Suzy kukimbia, kumbe na sisi hatujui chochote ndio kwanza tumemsikia yeye.
Ikabidi mama ndio amsindikize wifi kituoni kupanda gari sababu mimi sikuruhusiwa kutoka kwenda mbali sababu ya mkasa nilioufanya jana.
Wifi alipoondoka nilikaa na kutafakari, au wifi kamuona Suzy kwenye zile picha alizosema? Ila yule hakuwa Suzy bali ni Sam na Lucy. Ni nini hiki, mbona mambo ya ajabu sana! Sikufikiria kama mume wa mtu anayetembea na Suzy ni kaka yangu Deo. Inamaana Suzy hamjui kaka Deo au kaka Deo hamjui Suzy hadi wakawa pamoja?
Niliwaza sana bila ya kupata jibu la maana mpaka pale mama aliporudi. Naye akaendelea kuzungumzia jambo hilo hilo,
"Hivi ni kweli kabisa Suzy yupo na Deo? Hata siamini jamani"
Dada Penina akaja na yeye,
"Kwakweli mimi nafurahi kusikia kaka Deo ana mwanamke nje sababu Joy anajishauwa sana ila kwanini mwanamke huyo awe huyo Suzy? Nilikuwa chumbani nikiwasikiliza tu, kwakweli hii ni fedheha kubwa sana"
Mama akamuuliza dada
"Kwahiyo wewe unaona sawa tu Deo kuwa na mwanamke mwingine?"
"Ndio naona sawa kwani hata rafiki yangu alipinduliwa na Joy ila sijapenda kusikia mwanamke mwenyewe ni Suzy. Yani kaka Deo kaacha wanawake wa maana na kwenda kwa kale katoto! Si udhalilishaji huu, sijapenda kwakweli. Suzy nae hafai tena hana adabu kabisa, mtoto mdogo kuparamia waume za watu ndio nini? Ndiomana kipindi kile alidundwa hivyo hivyo"
Mimi na mama tulikaa kimya na kuendelea kushangaa kwani hatukuwahi kuwaza hata mara moja kuwa Suzy anaweza kuwa na mahusiano na kaka Deo, ilikuwa ni kitu cha kustaajabisha sana.
Jioni ya leo hali haikuwa shwari kama siku zote sababu familia ilikumbwa na maswahibu mchana wake.
Nikaenda jikoni kwaajili ya maandalizi ya chakula cha usiku kwani nikiendekeza mawazo nayo huwa hayaishi bora nimalizie kazi kwanza.
Wakati naandaa chakula cha usiku, nikapigiwa simu na Carlos,
"Hallow, unafanya nini muda huu Sabrina?"
"Nipo kupika chakula cha usiku"
"Wow, natumaini leo utanialika na mimi kuja kula usiku"
"Hata usijali, karibu sana. Muda ukifika wewe njoo tu ujumuike nasi"
"Asante Sabrina, nakutakia mapishi mema"
"Asante"
Nikakata simu na kuendelea kupika kama kawaida hadi nilipomaliza, kisha nikaenda chumbani kwangu kupumzika kwanza na kutuliza akili.
Nilitulia ndani nikitafakari mambo yanavyokwenda kwani sikuelewa hata moja na sikujua kwanini imekuwa kama ilivyokuwa ila sina la kufanya ukizingatia na mimi nishafanya mabaya ambayo hayajaipendeza familia yangu.
Muda wa kula ulipofika wote tulikaa pamoja kama kawaida na kupata mlo wa usiku, nilitoka mezani nikiwa na shibe ya kutosha ila nilivyoenda kitandani nilianza kuhisi njaa, nikawa kama vile mtu ambaye hajala kabisa, yani njaa ilinipata sana tumbo lilikuwa tupu kabisa kama sijala kumbe nimekula.
Nikatamani kwenda kuchukua chakula kingine ila nikahofia kuwa mama akijua atasema nina minyoo kumbe sivyo.
Wakati njaa ikinisumbua nikapata ujumbe toka kwa Carlos.
"Asante kwa kunikaribisha mlo wa usiku leo, nimeshiba sana"
Nikashangaa bila ya kumjibu huo ujumbe huku nikijiuliza mara mbili mbili, inamaana amekula chakula changu kweli? Na kama amekula basi amekulaje wakati sijamuona!
Hofu ikanijaa moyoni na muda huohuo Carlos akanipigia simu.
"Hujalala hadi saizi unangoja nini?"
"Hakuna kitu, mawazo tu"
"Pole kwa mawazo, ila mimi nipo nitakuliwaza wakati wote utakaonihitaji"
"Asante"
"Je, nikaribie kwenye ndoto zako pia?"
Hapo nikajiumauma bila ya kutoa jibu, kisha Carlos akasema
"Nitakutembelea ndotoni"
Na kukata simu, maneno ya Carlos yakaanza kunitisha na kuniogopesha ila swali langu likawa, mbona Carlos hafanani na yule mkaka wa ndotoni? Au hii kitu inamaana gani katika maisha yangu?
Sikuelewa kitu na kuamua kulala tu.
Nikiwa ndani ya usingizi mzito, nikajiona tena nipo kwenye bustani yenye maua mazuri ila leo kulikuwa na utofauti kidogo kwani paliwekwa meza na viti viwili mahali pale tofauti na siku zingine ambazo huwa nakaa chini ya mti, halafu akaja yule kaka wa ndotoni mbele yangu kisha akaanza kuongea.
"Hujapenda nilivyoweka leo?"
Nikawa kimya tu,
"Mbona hukai?"
Kisha akanishika mkono na kusogeza kiti kimoja wapo na kuniambia nikae, nami nikakaa na kuendelea kumsikiliza.
"Leo umenikaribisha kwenu, umenipa chakula kitamu sana ulichopika. Unajua nini Sabrina! Nilikula chakula chote ulichoandaa ndiomana nimeshiba sana. Sasa na mimi nimekuandalia chakula kizuri sana muda huu kama asante yangu"
Kisha akanyoosha mkono, mara nikaona chakula kimewekwa mezani, kilikuwa na harufu nzuri sana.
Nikatulia tu huku nikimuangalia yule mkaka, akasema tena.
"Karibu ule Sabrina"
Nikasita ila gafla nikajikuta nikila kile chakula huku nikionyesha kukifurahia tu.
Nilipomaliza, yule mkaka akatabasamu na kusema.
"Nitakualika tena katika kufurahia kitu kizuri katika maisha yetu"
Nilikuwa kimya kabisa, sikuweza kumjibu chochote kile labda leo nilizibwa mdomo.
"Muda wa kukurudisha umefika, nitakuja tena badae kukutembelea nyumbani kwenu"
Halafu akanikumbatia, na gafla nikashtuka toka usingizini na kugundua kuwa kumekuchwa, kichwa changu kilikuwa kizito sana.
Simu yangu ikaingia ujumbe mfupi, nikachukua na kuangalia ulikuwa umetoka kwa Carlos ukisema kuwa,
"Badae nitakuja kwenu kukutembelea Sabrina"
Nikashtuka sana na kuanza kukumbuka matukio ya ndoto, kisha nikaoanisha matukio ya ndoto na Carlos nikaanza kuhisi kuwa huenda yule mkaka wa ndotoni akawa ni Carlos, nikawaza bila jibu ila nikajipanga kumuuliza huo muda atakaokuja ili nijue mbivu na mbichi.
Nikainuka na kwenda jikoni huku kichwa changu kikizungukwa na mawazo ya kila aina, nikahisi kama mkono wangu wa kulia unanata kwenye kiganja, nikaangalia na kuunusa nikapata ile harufu ya chakula kwenye ndoto halafu tumbo langu lilikuwa limeshiba sana, nikajiuliza je nilikuwa nakula kweli? Na kama ni kweli kwanini inakuwa ndotoni? Sikupata majibu kwakweli.
Wakati nipo jikoni dada Penina akarudi na nikajua moja kwa moja kuwa ametoka dukani, kisha akaenda mezani na kuandaa chai.
"Mbona leo mapema sana dada?"
"Yani wee acha tu, njaa inaniuma kamavile usiku sijala, ndiomana nimedamkia kwa mama muuza chapati kwanza ili ninywe chaji nipooze tumbo kwanza"
Mama nae akatoka chumbani kwake na kunikuta na dada tukiulizana pale.
"Khee jamani hata mimi njaa inaniuma sana yani kamavile sikula usiku wa jana, sijui chakula kimeyuyuka mdomoni!"
Dada akacheka kisha tukamsalimia mama, halafu dada akaendelea kuongea.
"Itabidi tumuulize Sabrina vizuri labda jana katupikia hewa"
Mama akacheka na kujiunga na dada mezani katika kunywa chai halafu mimi nikaendelea na kazi jikoni huku nikijiuliza maswali mengimengi, je huyo Carlos kama jana ndio alikaribia kwetu kwa chakula cha usiku ndio ale chote peke yake kweli? Hata sikuelewa kwakweli na maswali yangu yalikosa majibu, nikajiandb kwa maswali mengi sana muda atakaofika Carlos nyumbani.
Mchana wa leo nilijikuta nikimkumbuka sana Sam wangu, nikatamani kuwasiliana nae ila maneno ya Carlos yakanifanya nisite kwa muda, ila baada ya kutafakari zaidi nikaona si kosa kumpigia simu Sam na kumsalimia tu.
Nikachukua simu ili kumpigia ila hakupatikana, nikamtumia ujumbe ili atakapopatikana basi anitafute kwanza.
Mawazo juu ya Sam yalinitawala sana huku nikijiuliza kuwa atakuwa wapi na anafanya nini kwa muda huu, ni kweli nampenda sana Sam na moyo unaniuma sana kuona penzi letu limeingia madoa, ila kwasasa nilikuwa tayari kurudiana na Sam ili tujaribu kufungua ukurasa mpya wa mapenzi kwani nadhani kuwa Sam kashajifunza vya kutosha huku nikijipa moyo kuwa, kutenda kosa si kosa bali kurudia kosa.
Mama alikuja na kunishtua katika yale mawazo ambapo nikaropoka,
"Kutenda kosa si kosa bali kurudia kosa"
Mama akaikanusha kauli yangu na kusema,
"Hapana, kutenda kosa ni kosa ila kurudia kosa ni kosa kubwa"
Nikamuangalia tu mama na kutabasamu ili asiweze kugundua ninachowaza kwa muda huo.
"Nina maswali matatu ya kukuuliza Sabrina"
"Maswali gani hayo mama?"
"Muda bado ila muda ukifika nitakuuliza maswali yangu"
Hapohapo nikakumbuka kuhusu mama Salome ambaye sijaiulizia hali yake tangu siku niliyorudi nyumbani.
"Eeh mama, mama Salome anaendeleaje?"
"Anaendelea vizuri, ila si nilikwambia wewe kuwa mama Salome amepararaizi! Kwakweli anitia huruma sana, hawezi fanya chochote hadi afanyiwe"
"Mmh pole yake, ngoja haya mambo yaishe kwanza ili niweze kumuona"
"Itakuwa vizuri ukienda, ngoja hali itulie mwanangu"
Tukakubaliana na mama pale, kisha akaja dada Penina.
"Nimekutana na Suzy, yani kanywea kweli aliponiona. Anatembea na Deo kweli yule atakuwa ndomana anaona aibu"
Sikutaka kuzungumzia habari ya Suzy, hivyo nikainuka na kwenda chumbani na kumuacha mama azungumze mwenyewe na dada Penina.
Ila baada ya muda wakaniita kuwa kuna mgeni wangu nikajua tu kuwa ni lazima atakuwa Carlos, nami nikatoka huku nikijiandaa na maswali yangu kichwani.
Nikafika sebleni, wakaniambia kuwa yupo nje ananingoja.
Nikatoka nje na kumkuta Carlos akiwa amesimama kwa kuegemea ukuta akiningoja.
Moja kwa moja nikamuuliza,
"Mbona leo hujaingia ndani?"
"Aaah nimepapenda hapa nje leo, nadhani patanifaa"
"Basi ngoja nikalete viti"
"Acha tu, mi sio mkaaji sana nimekuja kukuangalia tu"
Nikajua anataka kukwepa maswali yangu, sikutaka kupoteza muda nikaanza kumuuliza hapohapo.
"Samahani Carlos, hivi wewe ni nani na unamaana gani kwenye maisha yangu?"
"Kivipi Sabrina?"
"Jana umekuja kimazingara, umekula chakula chetu chote. Halafu usiku umenijia ndotoni na kunilisha mavyakula yako ya ajabu. Niambie ukweli Carlos, wewe ndio yule kijana anayenitokeaga kwenye ndo....."
Kabla sijamalizia, nikaona sura ya Carlos ikibadilika na kuwa sura ya yule kijana wa ndotoni.
Itaendelea…!!
 
SEHEMU YA 31


Kabla sijamalizia, nikaona sura ya Carlos ikibadilika na kuwa sura ya yule kijana wa ndotoni. Nikaanza kuogopa na kupiga makelele hadi mama na Dada Penina wakatoka nje kuja kushuhudia kuwa kuna nini. Mama akauliza kwa mshangao,
"Kuna nini hapa?"
Nikiwa nimejiziba uso kwa kiganja changu nikamsikia Carlos akimjibu mama.
"Hata Mimi mwenyewe namshangaa Sabrina, sijui ana matatizo gani maana
gafla tu kaanza kupiga makelele"
Mama akasogea karibu ili anitoe mikono machoni na aweze kuona Kuwa nina tatizo gani. Sikutaka kuangalia tena, nikaamua kukimbilia ndani kwa uoga niliokuwa nao. Nikawaacha mama na dada wakiongea na Carlos pale nje.
Nilipokimbilia ndani nikaishia sebleni kwani chumbani nako niliogopa kwenda, baada ya muda kidogo mama, dada Penina na Carlos nao wakaja pale sebleni kitendo kilichofanya uoga unishike zaidi na kusema kwa nguvu,
"Jamani, huyo Carlos sio mtu"
Mama akaniuliza,
"Sasa kama sio mtu ni nani?"
"Sijui ila sio mtu"
"Umeshaanza maruweruwe yako mwanangu"
Kisha mama akamgeukia Carlos na kumwambia,
"Msamehe mwanangu, anamatatizo sana
tumehangaika nae bila jibu. Ndio anakuwaga hivyohivyo maruweruwe yakimuanza. Msamehe sana"
"Usijali mama, hata mimi naelewa kama Sabrina ana matatizo ila kila nikimuuliza anakataa. Ila mimi naweza kumsaidia na hayo matatizo yakamuondoka kabisa"
Nikaropoka hapohapo,
"Unisaidie nini wewe wakati wewe ndio tatizo"
Kisha nikakimbilia chumbani kwangu kwani uoga ulishanitoka kwa kutambua kwamba dawa ya tatizo ujue kwanza chanzo cha tatizo, nikawaacha pale sebleni wakiendelea kuongea. Moja kwa moja nikaenda kukaa kitandani kwangu, mara gafla nikasikia sauti ikipenya masikioni mwangu huku ikiita kama kwa kunong'oneza,
"Sabrina, Sabrina, Sabrina"
Ile sauti ilikuwa kama ikigongwa gongwa na mwangwi na kujirudia rudia, nikaanza kuogopa tena na kupiga makelele nadhani hata watu wa mbali waliweza kusikia ila hawakuelewa kuwa kuna nini.
Mama, dada Penina na Carlos wakaja chumbani kwangu ila sikutaka kumuona Carlos wala kuongea nae ikabidi aage na kusema.
"Kama mtahitaji msaada wangu msisite kunipigia simu. Nitakuja kuwasaidia"
Kisha akaondoka, halafu tukatoka sebleni ili tuweze kuongea vizuri.
"Kwani una matatizo gani mwanangu?"
"Sijui na hata sielewi"
"Elezea kidogo ili tupate kukusaidia"
"Hata sijui jinsi ya kuelezea mama"
"Jaribu mwanangu"
Nikataka kuwaelezea tangu mauzauza yalipoanza hadi hapa yalipofikia, ila mdomo ukawa mzito gafla, sikuweza kutamka neno lolote lile, mama akabaki kushangaa. Ikabidi dada aulize,
"Mbona kimya cha gafla?"
Nikawa nataoa machozi tu, mama akaona nitazidiwa akaamua kunipa dawa ya usingizi ili nipunguze maruweruwe, na muda huo huo nikalala kweli. Nilipoamka nilijikuta nipo chumbani kwangu, nadhani
mama alinipeleka chumbani muda nilipoanza kulala.
Ilikuwa ni usiku, nikachukua simu yangu kuangalia muda nikaona ni saa saba usiku. Nikajiuliza kama nimekula usiku wa leo na kupata jibu kuwa sijala. Mara nikasikia sauti ikiniambia.
"Usijali Sabrina, chakula nimekuwekea mezani hapo"
Nikashtuka sana na kujiuliza ni mawazo au ni kitu gani, ila nilipoangalia mezani nikaona kuna sahani na juu imefunikwa, nikaogopa.
Nikatoka chumbani kwangu na kukimbilia chumbani kwa mama ambaye alikuwa amelala, nikamtingisha ili kumwamsha na kumuuliza.
"Eti mama umeniwekea chakula mezani kwangu chumbani?"
"Ndio, nilijua ukiamka lazima utakuwa na njaa ndiomana nikakuwekea"
Nikapumua kidogo na kuona kuwa ile mwanzo
yalikuwa mawazo yananisumbua tu. Mama akaniambia tena,
"Nenda ukale tu mwanangu, usiogope"
Nikatoka chumbani kwa mama na kurudi chumbani kwangu. Nikasogea pale mezani kuona mama ameniwekea chakula gani, nikafunua sahani ya juu na kukuta ni chips kuku, nikashangaa na kujiuliza. Inamaana leo kwetu wamepika chips kuku au mama ameamua kuninunulia tu, nikajisemea kuwa nitamuuliza kesho na kuanza kula. Nilipomaliza kula, nikaenda jikoni kuchukua maji ya kunywa. Kisha nikarudi chumbani kwangu na glasi ya maji mkononi, nikashangaa kuona soda mezani na kujiuliza nani kaiweka, sauti ikaja.
"Nimeweka mimi Sabrina"
Nikaanza kuogopa na kutaka kukimbia, sauti ile ikasema tena
"Unaogopa nini sasa mbona chips zangu na kuku umekula!"
Nikahisi kuchanganyikiwa kwakweli na kutaka kupiga makelele ila ikashindikana, nikahisi kama kuna kitu kinanigusa na kujikuta nimeanguka chini na kupoteza fahamu.
Nilipozinduka ilikuwa kumekucha na nilijikuta kitandani, hapo nikaogopa pia na kukimbilia sebleni ambako nilikutana na mama.
"Nani kaniweka kitandani?"
"Khee, kwahiyo wewe uliona raha kabisa kulala pale chini!"
Nikamuangalia mama na kumuuliza tena,
"Chakula ulichoniwekea jana ni chips kuku?"
"Chips kuku? Kwa lipi haswaa? Nilikuwekea wali, maharage na mchicha kwani hujala?"
Majibu ya mama nayo aliyajua mwenyewe, hapo nikajifikiria na kuona kuwa zile chips kuku niliwekewa na lile jitu lililokuwa linaongea usiku, nikatamani hata kujitapisha lakini ilishindikana. Nikiwa nashangaa shangaa pale sebleni, mama akaenda chumbani kwangu na kutoka na sahani na chupa ya soda. Kisha akasema,
"Ona sasa, chakula nilichokuwekea hujala hata
kidogo. Bora hata usiku ule wakati unaniuliza
ungekiweka kweje friji, kitakuwa kimechacha tayari"
Huku akikinusa kile chakula, nikawa naangalia kama
mtu nisiyeelewa na kujiuliza kuwa mbona usiku
sikukiona zaidi ya zile chips kuku!
Nikamuuliza mama,
"Na hiyo chupa je?"
"Unauliza nini wakati unaona ni chupa ya soda! Au
unaona kingine mwenzetu?"
Nikatulia na kujiona kweli nina matatizo na ninahitaji
msaada wa hali ya juu saa, nikakaa kwenye kochi
pale sebleni huku nikitafakari mambo
yanavyokwenda katika maisha yangu kwani nilikuwa
sielewi hata moja nipo kama sipo.
Mchana nilitulia ndani nikiangalia video. Nikapata
ujumbe toka kwenye namba mpya ukisema.
"Una tabia mbaya sana wewe, sikutegemea kama
Sabrina utakuja kuwa na tabia kama hii"
Nikajiuliza ni tabia gani? Na nani kanitumia ule
ujumbe?
Nikajaribu kuipiga ile namba, naambiwa.
"Namba ya simu unayopiga haipo"
Basi nikazidi kuchukia kuwa kwanini iwe hivyo na
wakati amenitumia ujumbe jamani!
Mama akaja kukaa sebleni ili kuzungumza nami.
"Mwanangu una matatizo"
"Ndio nina matatizo mama"
"Unaonaje kama tukimuomba Carlos atusaidie maana
kasema kuwa anaweza kutusaidia"
"Mama, sitaki msaada wa Carlos sio mtu yule"
"Kwanini sio mtu?"
"Mtu gani, hana ndugu na wala hajulikani anapokaa!
Mimi simtaki kwakweli, sitaki kabisa anisaidie"
sana hadi tukamshangaa pale nyumbani.
Mama akamuuliza,
"Mbona mapema leo Penina?"
"Mmh! Nitakusimulia tu mama"
Akaja kwangu na kunikabidhi bahasha.
"Mzigo wako huo, kuna mtu kanipatia"
Kisha akaondoka zake, nikajiuliza ni nini na kufungua
ile bahasha.
Nikakuta kadi yenye rangi nyekundu ndani yake
imeandikwa,
"NAKUPENDA"
Ndani yake kulikuwa na pete ya dhahabu yenye jiwe
linalong'aa sana katikati nikahisi itakuwa ni almasi.
Nikajiuliza kuwa inatoka wapi maana ni vitu vya
ajabu.
Nikabeba ile bahasha na kwenda nayo chumbani kwa
dada kumuuliza kuwa kaitoa wapi.
"Dada, mbona sielewi hii bahasha! Umeitoa wapi?"
"Kwani haijaandikwa ilipotoka?"
"Haijaandikwa ndio, ila vilivyomo ndani yake sielewi"
"Ina nini kwani?"
"Kuna kadi nyekundu na pete"
"Acha masikhara Sabrina, hebu ilete tuone"
Nikampa dada, akaifungua.
"Kadi na pete viko wapi sasa? Mbona kuna barua tu!
Unajua nilipoitoa hii bahasha Sabrina?"
"Sijui"
"Nimepewa na Suzy, hebu angalia hapa ameandika
sijui mkutane wapi"
Nikashangaa na kuichukua tena, kuangalia ni kweli
ilikuwa barua. Sikutaka hata kuisoma kwani nilipatwa
na mashaka tayari.
Nikaichana na kwenda kuitupa nje, kisha nikarudi
sebleni huku nikijiuliza kuwa haya ni mambo gani. Dada akaniuliza Kuwa mbona nimeichana nikamjibu kuwa siiamini.
Muda mfupi kidogo nikapigiwa simu na Suzy.
"Bora nimekupata, maana kila nikikupigia haupatikani
ndiomana nikaandika ujumbe na kumpa dada yako ila
kaniambia umeuchana kwanini? Au ujumbe wangu
hauna maana?"
"Samahani Suzy, labda ungeniambia tu sasa hivi"
Simu yake ikakatika, nikajaribu kumpigia lakini
haikupatikana basi ikabidi niachane nayo.
Usiku ulipofika nilijikuta nikikosa hamu ya kula,
sikutamani chakula chochote kabisa hata mama na
dada walipokuwa wanakula sikujumuika nao.
"Naona umeshiba mwenzetu"
"Hapana mama, ila sijisikii kula tu"
"Kwanini wakati hata mchana hujala?"
Dada akadakia,
"Siku hizi mwanao anafanya diet, asubuhi nimeingia
chumbani kwake nimekuta soda mezani akasema
yeye hataki basi mimi nikainywa"
"Kumbe ndio ile chupa niliyoitoa asubuhi!"
Mama akanigeukia na kuniuliza,
"Kwani ulinunua muda gani soda?"
Dada akajibu,
"Aliletewa na Carlos halafu mimi nikampelekea
chumbani kwake"
"Unapendwa na Carlos mwanangu, tatizo lako
hupendeki"
Nilikuwa kimya kabisa nikiendelea kutafakari maneno
yao, kuwa snda alileta Carlos na usiku ule nikasikia
sauti ya ajabu. Huenda kweli Carlos akawa ndio lile
jitu la ndotoni.
Niliinuka pale sebleni na kwenda chumbani ili nijaribu
kulala maana ndio kazi niliyofanya, kula, kulala na
kuzunguka ndani ukizingatia bado naogopa kwenda
nje kuzurula.
Nikiwa chumbani nikapata ujumbe kwenye simu
kutoka kwa Carlos.
"Unanionea tu Sabrina, mimi sio mtu mbaya na nina
nia nzuri na wewe. Nipe nafasi nikusaidie na mambo
yako yote yataenda sawa. Ukiwa karibu na mimi
hakika utafurahia maisha. Usinitenge Sabrina, nipo
tayari kukusaidia kwa kila hali. Ukiwa na tatizo lolote
usisite kuniambia"
Nikaweka simu pembeni kwani ujumbe wake
haukuwa na maana yoyote kwangu.
Nikatulia na kuangalia mezani nikaona ile kadi
nyekundu na pete juu yake, nikashindwa kuelewa
maana hata ile barua niliichana muda ule ule sasa ile
kadi imetoka wapi tena, nikaogopa kusogelea na
kutoka nje. Nilipofika sebleni nikamvuta dada mkono
ili nae aone nilichokiona.
Nikafika nae chumbani ila ile kadi haikuwepo.
"Mbona hakuna kitu Sabrina?"
Nikatoa mimacho tu,
"Unajua wewe Sabrina una matatizo sana, kwanza
kilichokuleta kulala mapema yote hii ni nini? Twende
sebleni tukaangalie video"
Nikatoka na dada kwenda kuangalia video ila
sikuelewa chochote hadi muda ambao dada alichoka
na kwenda kulala ndipo na mimi nikainuka na kwenda
tena chumbani kwa lengo la kuchukua simu yangu
kisha niende kulala kwa mama kwani nilishapata uoga
wa kulala
chumbani kwangu.
Nikiwa chumbani, nikachukua simu ili nitoke.
Nikasikia sauti ikisema,
"Huwezi kunikimbia Sabrina"
Uoga ukanijaa na kusogelea mlango, kabla
sijaufungua ule mlango ukafunguliwa halafu akaingia
yule kijana wa ndotoni.
Itaendelea
 
SEHEMU YA 32



Kabla sijaufungua ule mlango ukafunguliwa halafu akaingia yule kijana wa ndotoni.
Nikawa natetemeka pale karibu na mlango huku nimejiziba sura yangu kwa mkono, nikahisi yule mtu akinishika mkono wangu ili autoe mara nikasikia sauti ya mama karibu yangu.
"Wee Sabrina una nini?"
Nikatoa mkono wangu na kumuona mama mbele yangu, nikakimbilia sebleni halafu mama akanisogelea.
"Una nini wewe mtoto?"
Sikutaka kumtazama mama usoni na kumwambia.
"Wewe sio mama, sitaki"
"Sasa mimi kama sio mama ni nani sasa?"
Dada Penina nae akaja kutuangalia,
"Kuna nini hapa?"
"Namshangaa mdogo wako eti anasema mimi sio mama"
"Mama, huyu Sabrina ana mapepo si unaona jana kasema kuwa Carlos sio mtu! Halafu leo kachana barua aliyopewa na rafiki yake, ukimuuliza anasema sio barua. Itabidi asaidiwe huyu mama"
Mama akamwambia dada,
"Hebu mpigie Carlos simu aje atusaidie kwa hili maana hata sielewi"
Nilijiziba tu macho huku nikiogopa na machozi kunitoka.
Dada akamwambia mama nadhani baada ya kumpigia Carlos simu.
"Carlos kasema tumpe dawa ya usingizi alale halafu kesho atakuja na ufumbuzi wa hili tatizo"
Mama akachukua dawa na kunipa, nilikunywa vilevile nimejiziba sura kwa mkono.
Mama akanishika mkono hadi chumbani kwake na huko ndio nikaenda kulala hadi kunakucha.
Nilichelewa sana kuamka, nikatoka hadi sebleni kuangalia mida kwenye saa ya ukutani.
Ilikuwa ni saa nne asubuhi, na macho yangu yalikuwa mazito yani yalihitaji kuendelea kulala.
Nikaenda jikoni na kumkuta mama yupo makini na mapishi yake.
"Kheee umeamka mziwanda wangu! Njoo, mwanangu. Njoo uonje ninachopika"
Nikamshangaa sana mama kuchangamka kiasi kile, ila nikamwambia asubiri kwanza nikaoge na kuondoa uchovu wa usingizi ndio niende kuonja.
Nikiwa bafuni, nikaguswa mgongoni kugeuka nyuma hakuna kitu.
Nikaendelea kuoga huku nikiimbaimba ili kukatisha mawazo ya uoga, mara nikaona kitu cheusi kikiingia chini ya mlango wa choo.
Kuangalia vizuri ni nyoka, nikaanza kupiga makelele.
"Nyokaaa, nyokaaa. Nakufa jamani nakufa"
Yule nyoka akawa anatoa toa ulimi wake nje, hapo ndio uoga ukanizidi na kutoka bafuni siwezi maana yupo mlangoni.
Alifika mama na Carlos, kisha Carlos akampiga yule nyoka na kumuua nami nikakimbilia ndani huku nikitetemeka kwa uoga.
Carlos akaanza kunicheka.
"Kweli Sabrina muoga jamani, yani umetoka na mapovu duh!"
"Na wewe umefika saa ngapi?"
Mama akadakia,
"Si ushukuru amefika, mwenye ujasiri wa kuua huyo nyoka humu ndani nani? Mbona ingekuwa balaa, ila huyo nyoka katokea wapi jamani wakati hakuna hata nyasi kwenye uzio wangu?"
Mama alijiuliza swali sawa na nilivyojiuliza mimi kuwa huyo nyoka katokea wapi.
"Nenda kamalizie kuoga choo cha ndani mwanangu"
Nikaenda kuoga choo cha ndani ila bado fikra za nyoka zilitembea kichwani mwangu na kunifanya niwe na wasiwasi muda wote.
Nikajimwagia haraka haraka na kutoka kwenda kuvaa, kisha nikaenda sebleni kukaa ambako kulikuwa na mama na Carlos ukizingatia siwezi kupakimbia kwetu, nitaenda wapi? Bora nivumilie tu.
"Tulimuomba Carlos aje atusaidie mwanangu kwa tatizo lako, kwahiyo usichukie"
Nilitulia kimya kabisa nikiwasikiliza, kisha Carlos akaanza kuongea,
"Unajua mama, huyu Sabrina ananishutumu kuwa mimi sio mtu wa kawaida kwa sababu kuu mbili"
"Zipi hizo?"
"Moja, najua siri nyingi sana za watu wake wa karibu na pili sababu hawajui ndugu zangu. Ila mimi nakuahidi mama, nitawaleta baba na mama yangu hapa muwafahamu na mahali wanapoishi mtapafahamu pia. Huwa sipendi mtu anifikirie sivyo"
Mama nae akasema,
"Mimi nakuelewa baba yangu, ila ningependa kufahamu hizo siri unazofahamu za watu wa karibu na Sabrina"
"Kwanza kabisa najua kuhusu rafiki yake Suzy, na pia kuhusu wifi yake Joy. Yule Joy yule....."
Nikamkatisha na kumkonyeza, huku mama akiwa makini kusikiliza.
Nikaamua kusema neno la kubadilisha mada.
"Nipo tayari kusaidiwa na wewe Carlos"
"Kweli Sabrina! Upo tayari? Basi vizuri sana"
"Nipo tayari ndio"
Mama akafurahi sana kusikia nipo tayari. Sikupenda siri ya wifi ivuje kwani nilimuonea huruma sana ndiomana nikaamua kubadili mada.
Nikaingiza mada zingine za namna ya kunisaidia, mara dada Penina akawa amerudi na leo ndio aliwahi kurudi zaidi kushinda jana. Mama akamuuliza,
"Mbona mapema sana?"
"Majanga mama"
"Yapi hayo?"
"Kuna mauzauza ofisini kwetu siku hizi, tunakimbia ofisi sijui nini tatizo" Carlos akadakia,
"Mimi najua tatizo"
"Ni nini sasa?"
"Pale ofisini kwenu kuna mtu anaomba sana, huyo ndio tatizo"
Mama akamuuliza dada,
"Unamjua huyo?"
"Ndio, ni Salome mwenye tabia hiyo hadi ofisini"
Kisha wakamuuliza tena Carlos,
"Kwani kuomba sana ni tatizo?"
"Kuomba sana si tatizo ila yule binti ni mchawi sana na ndio anawatesa, pale ofisini jaribu kufatilia mambo yake" "Mmh tutafanyaje sasa?"
"Labda afukuzwe kazi"
Mama akamuuliza tena dada Penina,
"Huyo Salome si ndio yule wa mama Salome aliyepata ajali?"
"Ndio huyo huyo mama, nipo nae ofisi moja ni mtu wa dini sana hadi anakera" "Ila mbona haelekei na hayo mambo ya uchawi?"
Dada Penina akajibu,
"Mchawi huwezi kumjua kwa macho mama"
Kisha Carlos akaendelea kusema.
"Ni kweli, mchawi hauwezi kumjua kwa macho. Kama yule rafiki yako yule naye ni mchawi" Dada Penina akauliza,
"Yupi huyo?"
"Yule wa kuitwa Zuhura"
"Mmmh! Mbona ni mtu wa ibada sana huyo!"
"Hao watu wanaojifanya wa ibada waogope sana hawafai kwani wengi wao hutumia ibada kuficha makucha yao ila mimi nawaona" Nikamuuliza,
"Wewe unawamaje sasa au mmoja wao?"
"Hapana ila mimi nilichanjiwa na babu yangu nikiwa mdogo sana ndiomana naona na kugundua vitu vingi" Mama na dada waliamini kila alichoongea Carlos ila mimi imani yangu ilikuwa nusu nusu juu yake. Akaongea na kusema kuwa kesho anakuja na ufumbuzi wa swala langu, kisha akaaga na kuondoka zake.
Muda kidogo tukasikia mtu anagonga mlango, nikamchungulia kuwa ni nani. Dada akaniuliza,
"Ni nani kwani?"
"Rafiki yako da' Zuhura"
"Kafata nini na yeye na uwanga wake"
Mama akatufata kuwa tukamfungulie mtu, nikainuka na kwenda kumfungulia kisha nikamkaribisha ndani.
Dada akamsalimia kiunafki tu kuonyesha kuwa hapendezewi naye, mama akaja nae kumsalimia ili tumuone na uchawi wake leo maana hakuna hata mmoja aliyejua leo kafata nini ukizingatia ni kipindi kirefu sana hajafika kwetu.
"Najua leo mnanishangaa sana na kuona ajabu mimi kuwa hapa"
Dada akadakia,
"Lazima tukushangae maana huna kawaida ya kuja kwetu, zaidi ya mimi kuja kwenu"
"Rafiki yangu Penina, sio kwamba mimi sipendi kuja hapa. Mbona zamani nilikuwa nakuja hujiulizi hilo?"
"Haya, niambie sasa kwanini huwa hufiki hapa? Na leo umekuja kwanini?"
"Kwanza kabisa nimekuja kuwasalimia"
Wote tukaguna
"mmmh!!"
"Halafu kuna jambo kubwa sana lililonileta hapa"
"Jambo gani?"
"Ni kuhusu Sabrina, nimekuwa nikimuotea ndoto mbaya sana"
Mama aliyekuwa kimya kabisa tangu da' Zuhura anaongea akamkatisha sasa.
"Wewe Zuhura wewe usituletee uchawi wako hapa, tafadhari ondoka nyumbani kwangu na hizo ndoto mbaya nenda ukawaotee ndugu zako mwanga mkubwa wewe"
"Samahani mama kama nimekosea"
"Hakuna cha samahani hapa, nenda kawaombe msamaha wanga wenzio. Ondoka kwangu sasa hivi usiniletee mapepo na uchawi wako hapa"
Dada Zuhura akainuka na kuanza kuondoka huku akisema,
"Ila mimi nilitaka kuwasaidia tu, Mwenyezi Mungu awarehemu"
"Akurehemu wewe na uchawi wako, mwanga mkubwa wewe"
Alipoondoka, mama akaanza kumtania dada.
"Humsindikizi shoga yako?"
"Nani amsindikize mwanga? Loh! Ndoto mbaya, ndoto mbaya anajua maana ya ndoto mbaya au shobo tu. Na leo umemuweza kweli mama"
"Aende zake huko, siku zote hafiki hapa kaona tumemgundua ndio anakuja kujineng'enesha. Mwendawazimu kweli yule mtoto"
"Umenifurahisha sana mama yangu leo, bado hiko kisalome nacho kitajileta tu"
Mama na dada wakacheka sana ila mimi nilikuwa kimya kabisa nikitafakari mambo yangu kichwani maana yananichanganya sana.
Usiku ulipofika, dada aliandaa chakula ili tuweze kula.
Tulikaa na kula kile chakula, kilikuwa ni kitamu sana kupita kawaida.
Wakati tunakula, tukasikia sauti ya kitu kama kimeanguka chini kwa nje kwetu.
Kila mmoja akashtuka na kuambizana kwenda nje kuangalia nini ila ujasiri uliondoka sababu ya uoga na mimi ndio niliongoza kwa kukosa ujasiri, ikabidi mama ajitoe muhanga kwenda kuangalia ni nini ila hakuona chochote na kurudi ndani.
"Hakuna chochote"
"Mmh mama wakati wote tumesikia!"
"Ndio, ila hakuna kitu tuendeleeni kula tu"
Tukakaa ili tule, tukasikia kishindo tena na kushtuka.
"Mmh mama kuna kitu huko nje sio bure"
"Labda kweli kuna kitu, itabidi wote twendeni tukaangalie"
Mimi nikagoma kwenda na kumuacha mama na dada kwenda peke yao kuangalia.
Nikiwa pale ndani, nikasikia muungurumo kama vile wa simba, hapo ndipo uoga ukanizidi na kuinuka huku nikijaribu kutoka nje ila mama na dada wakarudi muda huo huo ndani na kusema kuwa nje hakuna chochote.
"Ila mimi nimesikia muungurumo kama wa simba humu ndani"
"Acha miujiza sasa, huyo simba atafute nini humu ndani kwetu Sabrina?"
Dada penina akakumbuka kitu na kuuliza,
"Au wale wachawi aliosema Carlos ndio wameanza kazi yao?"
"Hebu mpigie simu atusaidie"
Dada akampigia simu Carlos aliyesema anakuja, na baada ya dakika kadhaa alikuwa nyumbani kwetu.
Kisha akaanza kusema nasi,
"Leo alikuja mdada kajitanda ushungi eeh"
Dada akajibu,
"Ndio, ni Zuhura huyo"
"Basi ndio anawatupia makombora yake ila mimi nitawasaidia"
Mama akamuuliza,
"Kwani wewe ni mganga?"
"Hapana, mimi si mganga na wala siwaamini waganga hawafai ila mimi ninauwezo niliopewa na Mungu"
"Ila ulisema umechanjiwa"
"Ndio nimechanjiwa ili watu wabaya wasinipate"
Tukamuangalia tu Carlos, ambaye alichukua maji nakujifanya kama anayaombea kisha akayamwagia nyumba yetu yote.
Mama akamshukuru sana, kisha akatuaga na kusema kuwa atakuja tena kesho.
Ikabidi dada Penina amsindikize Carlos kidogo kwani mimi na mama tulibaki ndani.
Dada alilazimisha kumsindikiza Carlos nje ingawa Carlos alikataa ila dada akatoka nae.
Mara gafla tukasikia dada akipiga kelele huko nje.
Itaendelea
 
SEHEMU YA 33



Mara gafla tukasikia dada akipiga kelele huko nje.
Tukapatwa na mashaka, na kuinuka ili twende nje
tukaangalie kuwa kuna nini. Ila kabla ya kutoka nje,
Carlos alikuwa amerudi huku amemshika dada mkono
ambapo mkono mwingine alijiziba sura. Mama
akauliza, "Kuna nini tena?"
"Kuna vitu nje vimemtisha, mwacheni akapumzike
kwanza halafu nitakuja kesho kuongea vizuri" Ikabidi
mama amshike dada mkono na kumpeleka chumbani
kwake kisha mimi na mama tukaenda chumbani kwa
mama kulala kwani na leo nikaogopa kulala chumbani
kwangu.
Nikiwa chumbani na mama, akaanza kuniuliza
maswali kuhusu Carlos.
"Unamuonaje Carlos mwanangu?"
"Kwakweli mama sina la kusema maana hata
nikisema sidhani kama utanielewa"
"Kivipi mwanangu? Nieleze tu nitaelewa"
"Nimuonavyo mimi ni kama kijana wa kwenye ndoto
zangu"
"Kivipi mwanangu? Au unatamani awe mumeo?"
"Hapana mama, simpendi name ndiomana
nimekwambia Kuwa huwezi kunielewa hata kama
nitakuelezaje"
"Haya niambie basi unaonaje anaweza kutusaidia
kweli?"
"Sijui mama, kwa kifupi simjui Carlos tofauti na
unavyofikiria"
"Sawa mwanangu kesho nitafanya kitu fulani, nadhati
kitakuwa kizuri kwetu na maisha yetu"
Halafu tukalala. Leo mambo ya ajabu hayakutokea
kabisa usiku hadi kunakucha ilikuwa shwari kabisa.
Asubuhi ya leo kama kawaida Dada alijiandaa na
kwenda kazini, akasahau yote yaliyotokea Jana yake.
Nikabaki Mimi na mama ila mama nae akajiandaa na
kutoka, akaniacha pekeyangu nyumbani nikaamua
kuangalia luninga ili kujisahaulisha baadhi ya mambo.
Nikapatwa na ugeni leo alikuwa ni dada Salome,
nikamkaribisha ndani bila ya kuhofia uchawi wake
ambao nimeambiwa.
"Asante kwa kunikaribisha mdogo wangu, Nina mengi
ya kuzungumza na wewe"
"Usijari Dada, kuwa huru tu kuniambia chochote"
"Kwanza kabisa ni kuhusu maisha yako, hivi hujioni
kuwa umebadilika?"
"Mi sijijui Dada, bora uniambie nilivyo"
"Umejibu vyema Sabrina ni kweli kabisa hujijui wewe
wala hujitambui kwa sasa, pia napenda nizungumze
nawe kuhusu yule kijana uliyekuwa nae hospitali siku
ile"
"Nani huyo? Carlos?"
"Nadhani ndio huyo huyo, yule kijana yule ni......"
Mama alikuwa karudi akiambatana na rafiki yake
mwingine, aliyeitwa mama Semeni na kukatisha
mazungumzo ya mimi na dada Salome maana mama
alimvamia Salome kwa maneno.
"Eeeh kilichokuleta na wewe?"
"Kwani vibaya mama?"
"Mara yako ya mwisho kuja hapa lini ?"
"Mwaka Jana"
"Mwaka huu umefata nini"
Dada Salome akabaki kimya.
"Haya, kama ulivyokuja naomba uondoke hivyohivyo"
Nikajaribu kumtetea,
"Lakini mama...."
"Hakuna cha lakini hapa, huyu binadamu simtaki
nyumbani kwangu"
Ikabidi dada Salome aondoke, nami nikaenda
chumbani kwangu kwani sikutaka maswali zaidi toka
kwa mama.
Baada ya muda kidogo mama akaniita, nikaamua
kutoka na kuwafata pale sebleni. "Kilichokukimbiza
ndani ni nini? Hujui kama yote haya nafanya kwaajili
yako?"
Nikabaki kimya tu huku nikimuangalia mama,
"Haya njoo ukae hapa"
Nikasogea na kukaa karibu yao ili kuwasikiliza.
"Huyu hapa mama Semeni kasema atatusaidia pia"
"Atatusaidiaje?"
"Atatupeleka kwa mtaalam"
"Mtaalam??"
Nikajua sasa mama ameanza na mambo yake ya imani za kishirikina.
"Sasa unashangaa nini?"
"Mmh mama! Huo ni ushirikina"
Mama Semeni akaongea sasa.
"Sio ushirikina Sabrina, yote haya ni katika kukusaidia
wewe na maisha yako" "Basi kama ni vya kunisaidia
mimi msinilazimishe kwanza, acheni nifikirie halafu
nitawajulisha" Mama akachukia sana,
"Huyu Sabrina kashaanza utahira wake"
"Mwache tu Mama Penina, akiwa tayari atasema
mimi nipo wakati wote nitawapeleka" Nikarudi
chumbani kwangu na kuwaacha na mazungumzo yao.
Nikawaza sana nikiwa chumbani kuwa mama ana
maana gani kutaka twende kwenye mambo ya
kishirikina ila sikupata jibu. Baada ya muda nikasikia
kuwa mama Semeni kaondoka, nikaamua kwenda
kumuuliza mama maswali yangu.
Nikamkuta ametulia kabisa akiangalia video, ila kabla
sijamuuliza alifika dada Penina akiwa ameongoza na
Carlos.
Tukashangaa kuwaona pamoja, mama akawa wa
kwanza kuuliza.
"Mmekutana wapi nyie leo?"
Dada Penina akaanza kuelezea,
"Yani huwezi amini mama jinsi Carlos alivyotusaidia
ofisini yani mpaka Salome akaondoka mwenyewe"
"Basi ndio akaja huku kutuletea mauzauza yake"
"Khee! Alikuja huku mama?"
"Ndio, nimemkuta akiongea na Sabrina.
Nimemtimuaje"
"Umefanya vizuri sana mama, huyu Sabrina ni mjinga
na hajielewi hata kidogo. Kwakweli tumshukuru sana
Carlos kwa moyo wake wa kusaidia watu"
Carlos alikuwa akitabasamu tu kufurahia sifa
alizopewa, dada Penina akaenda kupika kwa lengo
kuwa leo jioni Carlos apate kula kwetu.
Carlos aliongea kidogo na mama na kuahidi kuwa
atarudi hiyo jioni.
Kitu hiki kwa Carlos huwa kinanichanganya pia kwani
sio mtu wa kusema utakaa nae muda mrefu kuongea,
yeye akikaa kidogo tu huwa anaaga na kuondoka na
hapo hufanya nizidi kupatwa na maswali mengi zaidi
juu yake.
Tulipokuwa tunaandaa chakula cha usiku ndio muda
huohuo Carlos nae alifika tena.
"Nimekuja kutimiza ahadi yangu ya kula hapa leo"
"Bora umekuja maana kesho tungekulaumu sana"
Sikuongea neno lolote, nilikuwa kimya kabisa.
Tukaanza kula, kila mmoja na sahani yake. Wakati
nakula, Carlos alikuwa akiniangalia na kunikonyeza,
nikaishia kutabasamu tu.
Niliposhusha macho kwenye sahani yangu nikaona
kumejaa mchanga na mawe wakati kulikuwa na wali
nyama, nikasogeza sahani pembeni na kupiga kelele.
Mama akaniuliza,
"Nini wewe? Una kichaa?"
"Hapana mama, ona"
"Nione nini?"
Namuonyeshea sahani yangu,
"Si wali huu na nyama! Au ni nini?"
"Ni mchanga na mawe mama"
Mama na dada wakacheka,
"Kweli unawazimu wewe, yani wali nyama unasema
mchanga na mawe!"
"Kweli mama ni mchanga na mawe"
Carlos akainuka huku akitabasamu na kusogea
mahali nilipokuwa nimesimama, akanishika bega na
kunikalisha kwenye kitu kisha akanisogezea ile
sahani yangu ya chakula ambayo nimelalamikia kuwa
ni mchanga ili nile.
Akasogea na yeye na kula karibu yangu, nikajikuta
nikila kile chakula bila mashaka tena yani kamavile
sio mimi niliyelalamika kuwa kile chakula ni mchanga.
Tulipomaliza Carlos aliaga kuwa anaondoka, mama
hakuacha kumshukuru Carlos.
Carlos akaniangalia na kuniambia kuwa,
"Hunifikishi mlangoni Sabrina?"
Mama akadakia,
"Inuka Sabrina umsindikize mwenzio"
Nikainuka na kumfikisha mlangoni, kisha akaniambia.
"Nitakusaidia kila kitu endapo utakubali kitu kimoja tu
kutoka kwangu"
"Kitu gani hicho?"
Hakuniambia ila akaondoka na kuniacha nimesimama
pale mlangoni, kisha nikarudi ndani na kumkuta
mama na dada wakijadili kuhusu Carlos.
"Unaona mama, Carlos ndio anafaa kwa Sabrina.
Atamsaidia huyu na uchizi wake"
"Kweli kabisa maana alivyoanza pale kwenye chakula
kuwa ni mchanga sijui ingekuwaje, bora Carlos
alikuwepo"
Nikawaangalia tu na kwenda chumbani kwangu kwani
leo nilijisikia kulala kwenye chumba changu.
Nilipokuwa chumbani ile kauli ya Carlos ikanirudia
kichwani kuwa nimkubalie jambo moja tu, nikajiuliza
tena.
"Litakuwa jambo gani hilo?"
Mara nikasikia sauti kama ikininong'oneza,
"Olewa na mimi"
Nikashtuka sana na kuangalia kila mahali kuwa ni
nani anaongea, nikajijibu mwenyewe kuwa,
"Sitaki kuolewa na wewe"
Sauti ile ikasema tena,
"Lazima nikuoe Sabrina"
Uoga ukanijaa kuwa ni huyuhuyu Carlos au ni nani
maana sikujielewa kabisa.
Mara nikajiona kama nimelala halafu naota ila
nilikuwa macho kama mtu aliyepumbazika, nikaona
mbele yangu vitu vingi vya kifahari huku ile sauti
ikijirudia ndani.
"Lazima uolewe na mimi, lazima uolewe na mimi
Sabrina"
Nikajiona tena nimekuwa mwanafunzi, nimevaa sale
za shule nimesimama barabarani nikiomba lifti.
Ikaja gari na kusimama mbele yangu nikapanda,
kwenye uskani alikaa dereva, nilipomuangalia ni yule
mkaka wa ndotoni akitabasamu na kusema.
"Lazima uolewe Sabrina"
Hapo ndipo niliposhtuka kutoka kupumbazika kwangu
na kushangaa nikiwa chumbani kwangu tena
kitandani huku nimekaa bila hata ya kujielewa kwani
uoga ulikatika gafla na kujikuta nikikumbuka matukio
ya nyuma wakati nasoma.
Nakumbuka nilipenda sana kusimamisha magari ya
watu kwaajili ya lifti ila sikumbuki kama kuna siku
yoyote niliyowahi kukutana na mtu wa ajabu.
Hapohapo nikapatwa na usingizi na kulala hadi
panakucha.
Mama ndiye aliyekuja kunishtua siku ya leo.
"Khee Sabrina, umelala hadi muda huu?"
Nikaamka na kumsalimia mama,
"Leo ni siku njema mwanangu, kuna habari njema
zinakuja"
"Zipi hizo mama?"
"Sijui ila nimeoteshwa tu mwanangu"
"Sawa mama, na ziwe njema kweli"
Nikaenda kujisafisha mwili na kuendelea kufanyakazi
za ndani kama kawaida.
"Ila mama natamani kweli kwenda kuwatembelea
rafiki zangu"
"Sabrina mwanangu usitake kuniletea makubwa hapa,
hebu tulia ndani. Ngoja mambo yawe shwari utaenda,
kama umewakumbuka sana wasiliana nao kwa simu
tu"
"Hawapatikani mama, natamani sana kujua hali zao
ila siwapati"
"Usijali mwanangu, muda upo utawatembelea hadi
uchoke"
Kwakweli kukaa nyumbani kwa muda nilichoka tena
nilichoka sana
Tulipomaliza kazi na mama tulienda kupumzika sasa.
Nikaenda chumbani kwangu na kujaribu tena
kuwapigia simu rafiki zangu haswaa Sam,
nilimkumbuka sana ingawa mengi yalitokea kati yetu
ila sikuacha kumkumbuka ila hakupatikana hewani.
Rafiki zangu wote hawakupatikana hewani hadi
nikaona ni uchafu tu kuwa na simu isiyokuwa na
maana yoyote ile kwani ilikuwa ikikaa bila kupigwa
wala kutuma ujumbe, nikajisemea iwe isiwe lazima
kesho niende kumtembelea Sam.
Mawazo yalikuwa mengi sana, nikaamua kulala
ilikupunguza mawazo.
Wakati nimelala, nikawaona watu wengi sana
wamekuja nyumbani wakiwa wameambatana na yule
kaka wa ndotoni halafu mimi nilikuwa pembeni
nikishangaa.
Nikamvuta mkono dada Penina na kumuuliza.
"Kuna nini kwani?"
"Wamekuja kutoa mahari, mdogo wangu unaolewa"
Nikauliza kwa mshangao,
"Naolewa! Na nani?"
"Si yule kijana pale"
Akimuonyeshea yule kijana wa ndotoni.
Nikashangaa na kusema.
"Simtaki yule"
"Khee! Humtaki mchumba wako?"
"Sio mchumba wangu yale"
"Awe mchumba wako asiwe mchumba wako lazima
akuoe maana mahali yake ishakubaliwa"
Nikaanza kulia na kusema kuwa kuwa sitaki kuolewa,
dada akasema.
"Usilie mdogo wangu, furahia ndoa. Ndoa ni furaha"
Nikazidi kulia na kulia sana.
Kushtuka pale kitandani, mahali nilipolaza kichwa
pote palijaa machozi, hapo nikagundua kuwa nilikuwa
nalia kweli wakati naota.
Nikainuka na kukaa kitandani huku nikitafakari ile
ndoto, ila nikasikia kama kuna watu wakizungumza
sebleni nikaamua kujifuta machozi na michirizi ya
usingizi ili nikawaone kuwa ni wakina nani.
Nikatoka hadi sebleni na kuona watu kadhaa kabla
sijawatambua vizuri, mama akainuka na kuanza
kunipigia vigelegele.
Itaendelea muda sio mrefu…!!
 
SEHEMU YA 34


Nikatoka hadi sebleni na kuona watu kadhaa kabla
sijawatambua vizuri, mama akainuka na kuanza
kunipigia vigelegele.
Hapo ndipo nikahisi kuwa huenda ile ndoto ni ya kweli
na kuanza kulia tena huku nikisema kwa nguvu kuwa,
"Sitaki kuolewa, nimesema sitaki kuolewa"
Mama akanishika mkono na kusema,
"Wewe mtoto una nini wewe? Mbona wanifedhehesha
kwa wageni?"
"Nimesema sitaki kuolewa mama"
Huku nikizidi kulia,
"Kwani nani anataka kukuoa hapa jamani!"
"Hao waliokuja kutoa mahari, nimesema sitaki
kuolewa"
Niliwaangalia wale wababa huku sura yangu ikiwa
imejaa machozi na kuwaambia.
"Sitaki kuolewa, ondokeni na mahari zenu sitaki mie
siwataki nimesema sitakiii"
Mama akaanza kunituliza, huku akisema,
"Mwanangu jamani una nini wewe? Unanitia aibu ujue!
Hebu waombe radhi wageni"
Nikaona mama ndio ananichanganya kabisa, nikaenda
jikoni na kuchukua kisu huku usoni nikiwa na
machozi.
Nikawafata wale wababa mbele,
"Ondokeni hapa sasa hivi, kama hamuondoki
najichoma kisu"
"Wewe Sabrina mwanangu wewe, usifanye hivyo
mama. Nakupenda mwanangu"
Ikabidi wale wababa wainuke na kutoka, bado
niliendelea kuongea neno moja tu.
"Sitaki kuolewa"
Na machozi kunitoka zaidi, mama akanisihi kuwa
niachie kile kisu, kisha nikamkabidhi na kukimbilia
chumbani kwangu huku nikiendelea kulia kwa
uchungu sana hadi nikapatwa tena na usingizi.
Nikiwa ndani ya usingizi mzito sana, nikamuona yule
kaka wa ndotoni akicheka sana na kufurahi huku
akinionyeshea alama ya dole gumba yani kamavile
mtu aliyekipenda kitu.
Nikashtuka sasa na usiku ulikuwa umeshaingia,
nikakaa kitandani na kujiuliza kwanini yule mkaka wa
ndotoni alionyesha kufurahi, au alifurahia nilichofanya
kwa ndugu zake au kuna kitu gani kikubwa
alichofurahia, hapo nikakosa jibu.
Ila sasa hivi nilikuwa na hali nzuri kidogo nilipoamka
tofauti na wakati ule nilipowatimua wale wababa
sebleni.
Nilitoka chumbani na kumkuta mama na dada wakiwa
sebleni ila mama hakuniuliza chochote zaidi ya
kuniangalia na kutikisa kichwa kama vile mtu
anayenisikitikia.
Nikaenda kula na kisha kurudi tena chumbani kwangu
kwaajili ya kulala.
Haikuchukua muda sana nikawa nimelala, kama
kawaida ya yule kijana wa ndotoni na leo akaja tena
ndotoni kwangu.
Akaniangalia na kutabasamu kisha akasema,
"Sabrina, wewe ni binti mwenye akili sana tena sana.
Kwakweli leo umenifurahisha sana, kesho nitakupa
zawadi yako kwa hakika utaipenda"
Nikamuangalia tu huku akiendelea kuongea,
"Na ukiendelea kufanya kama ulivyofanya leo, kwa
hakika utafurahi daima"
Sikuwa na uwezo wa kumsemesha wala kumjibu
nilikuwa namsikiliza tu na alinisifia muda wote kwa
nilichofanya leo hadi kunakucha.
Asubuhi ya leo niliwahi kuamka kupita siku zote, wote
ndani ya nyumba yetu walikuwa bado kuamka.
Nikaanza kufanya usafi, hata dada alipoamka na
kujiandaa kwenda kazini alinishangaa sana.
"Naona leo mapepo yako yamepungua"
"Sina mapepo bhana"
Dada akacheka na kuniambia,
"Yani wewe Sabrina wewe, maisha yako yana tabu
sana"
Nikamuangalia tu, naye akaondoka kwenda kwenye
kazi yake.
Mama alipoamka alinikuta nikiangalia video na kazi
zote za asubuhi nimezimaliza, nikamsalimia pale
mama kisha nae akaanza kusema yake.
"Naona leo amani imetawala mwanangu"
"Mbona siku zote ni amani mama"
"Mmh wewe mtoto wewe, aibu uliyonipa jana sitokaa
niisahau"
"Aibu gani mama?"
"Inamaana huelewi ulichofanya jana? Ngoja nikaoge
kwanza ndio nije nikwambie mauzauza yako"
Mama akaenda kuoga na kuniacha nikiwa na mawazo
sasa maana mimi mwenyewe sikuona kama kile
nilichofanya jana ni kitendo cha aibu ukizingatia
kuolewa ni hiyari ya mtu na sio kulazimishwa,
kwahiyo mimi niliona ni sawa kabisa kuwatimua wale
wababa nyumbani kwetu.
Wakati nawaza hayo, simu yangu ya mkononi ikaita,
kuangalia ni Suzy anapiga.
"Niambie mwanampotevu Suzy"
"Wewe ndio mwanampotevu Sabrina, sijui hata kama
unajua yanayoendelea kwasasa"
"Yapi hayo?"
"Sam yuko wapi?"
"Sijui, niambie wewe"
"Ona sasa Sabrina hadi mpenzi wako alipo hujui,
nakuachia kazi wewe mwenyewe ukatafute Sam alipo
ndio utapata jibu"
"Jamani Suzy si uniambie tu"
"Nikwambie kitu gani wakati barua yangu umeichana
Sabrina, unajua niliandika vitu gani? Au ulisoma na
kuipuuzia? Sasa kazi kwako kujua Sam alipo."
"Jamani Suzy, tafadhari rafiki yangu nisaidie. Mimi
nitajuaje alipo Sam kwasasa?"
"Nilikuwa na moyo wa kukusaidia sana ila
umeuvunja, inaonyesha wazi msaada wangu huutaki.
Sam unapajua kwao kwahiyo utaenda kumuulizia"
Kisha akakata simu na kuniacha na mawazo kichwani
kuwa Sam atakuwa wapi, au atakuwa na Lucy
kumfariji kwa lile tukio nililofanya! Sikupata jibu.
Nilitulia pale nikiwa na mawazo, mama ndiye
akanishtua tena.
"Haya sasa mwanangu nimerudi"
"Eeh mama niambie hiyo aibu niliyokupa jana"
"Hivi wewe unaona kufukuza wageni kama vile ni
jambo zuri?"
Hapo nikawa mkali kidogo sasa,
"Kwani mama kuolewa lazima? Mi sikotayari
kuolewa"
"Aliyekwambia unataka kuolewa nani?"
"Si wale wageni mama walikuja kutoa mahari"
"Una akili wewe? Uliona wapi mahali inatolewa na
kupokelewa bila ya muhusika kukubali? Uliona wapi?"
"Sijawahi ona"
"Na hiyo mahari yako ni mahari gani hadi niipokee
mwenyewe? Huna baba wadogo wewe? Huna
wajomba? Mbona unataka kuniletea balaa mtoto! Na
huyo wa kukuoa ni nani?"
Ikabidi niwe mpole sasa,
"Kwani wale wajana walifata nini?"
"Kwa mawazo yako wewe wale wababa wanataka
kukuoa? Hebu uwe na adabu mwanangu, wale ni
kama baba zako tena wana wake zao, watoto wao
kama wewe na familia zao. Yani umenitia aibu sana,
unajua walichofata wale?"
"Sijui mama"
"Wale ni rafiki wa marehemu baba yako, walikuwa
wakifanya nae kazi sehemu moja. Tena walikuja na
habari nzuri sana ya kwako ila uchizi wako
umevuruga kila kitu"
"Habari gani mama?"
"Sikia mwanangu, kipindi upo kwa kaka yako nilienda
ofisini kwa wale maana nilikuonea huruma sana
kukaa nyumbani wakati mwanangu umesoma.
Nikaenda kuwalalamikia na kuwaomba kuwa endapo
ikitokea nafasi wakuingize na wewe mwanangu,
sikupendezewa kukaa kwako nyumbani hapa.
Sasa jana walivyokuja, walikuja kutusalimia kwanza
na pili waliniambia kuwa kuna nafasi ofisini kwao
kwahiyo unatakiwa wewe ukafanye interview
wakuweke"
Hapohapo nikashtuka na kumuuliza mama,
"Na mbona nilipotoka ndani uliponiona tu ukaanza
kunipigia vigelegele?"
"Furaha mwanangu, unajua furaha wewe? Nilikuwa na
furaha iliyopitiliza mwanangu kuwa ombi langu
limejibiwa, ndiomana nikapiga vigelegele. Kwahiyo
kwamaana yako wewe vigelegele vinapigwa kwenye
ndoa tu au mahari tu?"
"Sijui mama, nilichanganyikiwa"
"Uchanganyikiwe na nini mwanangu, hata kama
wangekuwa watu wa kuoa ulitakiwa uulize kwanza
maana humu ndani wa kuolewa hauko peke yako.
Kumbuka hata dada yako Penina hajaolewa"
"Sasa mama itakuwaje?"
"Unadhani itakuwaje kwa yale uliyoyafanya jana?
Hakuna cha kazi tena, nani atapenda kuajiri chizi
kwenye kampuni yake?"
"Ila mimi sio chizi mama"
"Kwa ulichofanya jana ni chizi, umenitia aibu ya
mwaka mwanangu hata sijui nitawaangaliaje wale
wababa tena! Kwakweli umeniumiza sana Sabrina"
"Nisamehe mama"
"Nisamehe yako haina muhimu tena mwanangu, hii ni
aibu na fedheha"
Nikajisikia vibaya sana, nikatamani siku irudishwe
nyuma ili nirekebishe nilichokosea ila ndio hivyo, maji
yakimwagika hayazoleki. Machozi yakanitoka na
kujilaumu kwa uchizi ambao nimeufanya kwa wageni
wa muhimu kama wale.
Nikakumbuka kuwa ndiomana yule mkaka wa ndotoni
alikuwa akinisifia usiku kucha.
Nilikuwa na mawazo sana leo na sikujua cha kufanya
moja kwa moja, kila kitu kilinichanganya.
Nikifikiria kuhusu kazi na jinsi nilivyowatimua wababa
wa jana, nikifikiria kuhusu Sam niliumia sana.
Nikaona kuwa itakuwa vyema kama nikifatilia kuhusu
Sam kwanza ila je nitatokaje nyumbani wakati mama
yupo? Nitamuaga vipi wakati nimekatazwa kutoka?
Huo ukawa mtihani kwangu na maswali pasipo
majibu, ila nikatulia kwanza ili nipate njia rahisi ya
kutoka hapa nyumbani.
Wakati nawaza nikapigiwa simu na Carlos.
"Nina zawadi yako Sabrina"
"Zawadi gani?"
"Utaiona nikiileta"
"Utaileta muda gani?"
"Nitakuja jioni"
"Poa karibu"
Alipokata simu nikaendelea kutafakari njia ya
kuondokea na nikaona hiyohiyo ya kuhusu Carlos ndio
itafaa.
Nikaenda kuongea na mama kwanza ili nimvute
kimawazo,
"Carlos kanipigia simu kasema ana zawadi yangu"
"Zawadi gani hiyo? Carlos anakupenda sana
mwanangu"
"Sijui ni zawadi gani, ila kasema ataileta au
ataniambia nikaichukue"
"Leo leo?"
"Ndio ni leo mama"
"Basi hakuna tatizo mwanangu"
Nikatulia na kujigelesha kufanya kazi ndogo ndogo,
zilizobaki.
Muda wa mchana nikaenda chumbani kwangu na
kuandaa nguo za kuvaa kabisa, kisha nikategesha
simu yangu kuwa ipigwe baada ya robo saa ili mama
ajue kuwa napigiwa halafu nikaenda kukaa sebleni
karibu na alipokaa mama kisha simu nikaiweka
mezani na kuendelea na maongezi mengine na mama.
Baada ya robo saa simu ikaanza kuita, mama
akaangalia pale mezani na kuona kuwa Carlos
ananipigia hakujua kama ni ya kudanganya yani (fake
call), akanishtua na kusema,
"Si unapigiwa na Carlos hapo, mbona hupokei?"
Nikajigelesha kuwa sikuisikia kisha nikaichukua na
kuipokea huku nikiongea kwa nguvu na pale pale ili
mama anisikie kuwa kweli nimeitwa.
"Hallow.... Ndio.... Nije muda huu?.... Sawa nakuja....
Nipe dakika tano tu nitakuwa nimefika hapo"
Nikakata simu na kumwambia mama,
"Carlos kaniambia niende stendi mara moja
kuichukua ile zawadi"
"Kuhusu watu je?"
"Nadhani hakuna tatizo maana kaniita mwenyewe"
"Sawa basi nenda uwahi kurudi"
Nikaenda chumbani na kuvaa haraka haraka nguo
zangu nilizoandaa kisha nikatoka na kumuaga mama
kuwa nitarudi muda sio mrefu halafu nikaondoka.
Mwendo ulikuwa moja kwa moja hadi kituo cha
madaladala na kwenda nyumbani kwa Sam.
Kufika pale nikakuta kufuli kwenye mlango wake,
ikabidi nimgongee jirani wa chumba cha pili
kumuuliza, alitoka mdada. Nikamsalimia na kuanza
kumuuliza.
"Samahani dada, eti Sam ulimuona alipotoka?"
"Kwakweli huyo Sam sijamuona wiki ya pili sasa,
hayupo kabisa. Hiko chumba kipo hivyo hivyo kila
siku na kufuli lake"
"Kwahiyo hajulikani alipo?"
"Hilo ndio jibu maana hatujui kama amesafiri au yuko
wapi"
Basi nikamshukuru yule dada kwa taarifa na
kuondoka pale, huku nikifanya safari ya kwenda
nyumbani kwao kabisa na Sam.
Nilipofika kwao sikumkuta mtu yoyote nje, hivyo
nikagonga.
Alikuja mama Sam na kunifungulia mlango, nilikuwa
natabasamu ila yule mama alikuwa amechukizwa
sana na sikujua ni nini kilichomchukiza.
Aliniangalia kwa hasira sana, halafu akanizaba kibao.
Itaendelea…!!
 
SEHEMU YA 35


Aliniangalia kwa hasira sana, halafu akanizaba kibao.
Nikabaki kuugulia kibao nilichopigwa bila ya kujua
sababu ya kupigiwa haswaa na mama Sam ambaye
nilikuwa naongea nae vizuri sana zamani.
Yule mama baada ya kunizaba kibao akaanza
kuongea maneno ambayo alitaka kuongea.
"Mtoto mbaya sana wewe sitaki hata kukuona"
"Kwani nimefanya nini mama?"
Akaiga kwa kubana sauti,
"Kwani nimefanya nini mama? Hujui ulichokifanya
wewe mbwa?"
Nikawa nimeduwaa kuwa leo nimeshakuwa mbwa.
"Tena wewe ni shetani mwenye mapembe, hufai hata
kidogo. Mtoto umenichefua wewe halafu bila haya
unaleta ngwala zako hapa"
"Ila mama sijui kosa langu"
"Kosa lako kawaulize wazazi wako kwanini walikuzaa
maana hilo ndio kosa kwao kumzaa shetani kama
wewe"
Machozi yakaanza kunitoka kwani sikuelewa kwanini
nafokewa kiasi kile,
"Nisamehe mama"
"Tena unipishe mtoto wa kike, sina mtoto shetani
kama wewe na uondoke hapa nyumbani kwangu sasa
hivi"
"Kwani kosa langu lipi?"
"Nimekwambia uondoke na ole wako siku nikukute na
mwanangu Sam nitakukata hiyo miguu yako. Ondoka
sasa hivi usitake nitende zambi hapa"
"Ila Sam nampenda mama"
"Umpende kitu gani? Unajua kupenda wewe?
Kumtesa mwanangu tu na ushetani wako. Unaujua
uchungu wa Sam wewe? Nimekwambia uishie
hukohuko kwenu, nikikukuta siku nakukata miguu
hiyo."
Nikajaribu kujitetea, akasema kwa nguvu.
"Nimesema tokaaaaa"
Ikabidi niondoke huku machozi yakinitoka kwani
sikujua kosa langu ni nini kuwa vile.
Nikaamua kwenda kwa dada wa Sam ambaye alikuwa
akiishi sio mbali na hapo.
Kufika nilimkuta ila nae alikuwa na hasira na mimi,
nikamueleza kilichonileta kwake na jinsi nilivyopigwa
kibao na kutimuliwa na mama yao.
"Tena hicho kibao hata hakitoshi ilibidi akutwange
kabisa"
"Ila kosa langu ni nini?"
"Kwani hujui?"
"Sijui, naomba uniambie"
"Mara ya mwisho Sam umemuacha wapi?"
Nikashindwa kujieleza na kujiumauma tu.
"Unaona hata kujieleza unashindwa sababu ya maovu
yako, basi kwa taarifa yako Sam ameswekwa jela
sababu yako. Mdogo wangu anahenyeka tu huko na
wewe hata kwenda kumjulia hali umeshindwa halafu
leo unajileta bila aibu!"
Na yeye akanizaba kibao na kusema,
"Hiyo ni haki yako na uondoke hapa hata mimi sitaki
kukuona"
Nikaendelea kutoa machozi kwani hata sikujua pa
kuelekea, nikaulizia kituo alichopelekwa ila yule dada
alinitimua bila ya kusema chochote.
Nikawaza pa kuelekea ila sikuwa na pa kwenda,
mawazo yalinijaa tele bila ya majibu hata kurudi
nyumbani nikaona itakuwa kazi bure tu.
Nikafanya maamuzi ya haraka haraka na kuamua
kwenda nyumbani kwakina Suzy.
Nilipofika sikumkuta Suzy ila niliwakuta wadogo zake
na mama yao ambapo walinikaribisha vizuri sana,
kwahiyo nikakaa sebleni kwao kumngoja Suzy. Mara
usingizi wa gafla ukanipitia.
Wakati nimelala pale, nikamuona Sam amewashiwa
moto mbele halafu wanamsukuma ili wakamchome.
Nikashtuka na kupiga kelele,
"Msimchomeeeee...."
Kumbe nilikuwa naota, nikaona aibu sana pale
wadogo zake Suzy walipokuwa wakinishangaa na
kucheka, kisha mama Suzy akaniuliza.
"Nini tena mwanangu?"
"Ndoto tu mama"
"Pole sana"
Muda huo Suzy nae akawa amewasili pale kwao,
akafurahi kuniona na kuanza kuzungumza nae.
"Bora umekuja Sabrina, nimekuwaza sana. Haya
inuka twende maana nikikaa hatutaweza kwenda"
Nikainuka na kuaga kisha kufuatana na Suzy tena bila
ya kujua tunapoelekea.
Kufika nje Suzy akaanza kuongea,
"Unajua rafiki yangu, Sam ana wiki ya pili sasa yupo
ndani. Siku ile nimekutumia ujumbe ili twende ila
ukapuuzia, mi sijali shoga yangu. Kwenu siwezi kuja
kwa yale mabalaa. Ila leo nilienda kituoni kumuangalia
Sam, anatia huruma kwakweli na anahitaji sana
kukuona hivyo nimeshukuru kweli kukukuta hapa
nyumbani. Twende haraka haraka tuwahi kurudi"
Nilikuwa kimya kabisa nikimsikiliza tu Suzy maana
sikuwa na cha kusema kabisa.
Wakati tupo kituo cha madaladala tukisubiri usafiri wa
kwenda huko nikaamua kumuuliza Suzy.
"Kwani ni sababu gani iliyofanya Sam afungwe?"
"Inasemekana kuwa Sam amempiga sana Lucy
kwasababu yako, halafu akammalizia kwa kumbonda
na chupa ya soda kichwani. Hivi ninavyokwambia
hadi leo Lucy yupo hospitali na Sam yupo polisi,
ndugu wa Lucy wamesema asiachiwe hadi Lucy
atakapopona"
Nikaishia kuguna tu na kushangaa kuwa iweje
aambiwe Sam wakati ni mimi niliyempiga Lucy kwa
chupa? Hapa ndipo palinishangaza zaidi.
Sikutaka kumueleza Suzy ilivyokuwa ila nilijiamulia
moyoni mwangu kuwa nikifika huko polisi nitasema
ukweli ili wamuache Sam huru, ila je Sam nae
alishindwa kujielezea kuwa ilikuwaje? Au ameamua
kutumikia kifungo kwaajili yangu? Sikupata jibu.
Gari iliposimama tukapanda na Suzy na kuanza safari
ya huko kwenye kituo cha polisi alipopelekwa Sam.
Wakati lile gari lipo kwenye mwendo kuna kitu
kikaniambia ndani yangu,
"Shuka Sabrina, usiendelee na hiyo safari"
Ila nikapuuzika na kuendelea, kituo cha mbele yake
abiria wengi kwenye ile gari wakashuka nikabaki mimi
na Suzy na abiria wengine wawili ambao sikuwajua,
daladala ikaendelea na safari yake.
Kufika njiani ile daladala ikapoteza uelekeo na kuanza
kwenda hovyohovyo, mimi na Suzy tukaanza
kuogopa.
Ile gari ikafika mahali na kusimama kwa gafla, Suzy
na wale abiria wengine wakafanikiwa kushuka ila
wakati mimi nataka kushuka ile daladala ikaondoka
na haikuwa na abiria wala konda wala dereva,
nadhani wote walishuka.
Nikapiga makelele lakini hakuna aliyenisikia, niliogopa
sana na nikajua ndio mwisho wangu.
Kweli kwenye matatizo hata kama hujui kuomba
utaomba tu, nilijikuta nikisema.
"Mungu naomba unisaidie, naomba unisamehe
dhambi zangu zote"
Nilijikuta nikitubu mara nyingi niwezavyo, kweli kifo ni
kifo tu wanadamu huwa tunapenda kusema bora nife
ila kiukweli tunaogopa kifo ingawa tunajua kipo na
lazima kitupate.
Uoga ulizidi zaidi pale lile gari lilipokuwa
likiyumbayumba kila upande, nilijisemea kuwa
mwisho wangu umewadia sasa, mwisho wa Sabrina
na mauzauza yake umefikia.
Niliziba uso wangu kwa mikono ili nisione
kitakachotokea mbele yangu.
Mara nikasikia lile gari likigonga kitu, hata kama
nilifumba macho sasa nilifumbua kwa uoga, ile gari
iligonga mti na ikawa inafuka moshi. Hapo ndipo
nikatokea dirishani na kujitahidi kukimbia ila kabla
sijafika mbali sana nikasikia mlio kama wa bomu
ulionirusha na kuniangusha chini, kuangalia kwenye
lile gari palikuwa na moto mkubwa ukiwaka
ikionyesha kuwa lile gari lililipuka.
Nilikuwa pale chini kama mtu nisiyejielewa, sikuona
mtu yeyote eneo lile nilikuwa mwenyewe. Nikawa
najitazama vizuri na kujiuliza,
"Hivi mimi mzima kweli au nimekufa? Eneo gani hili
lisilokuwa na watu?"
Nikajaribu kujitingisha na kujifinya finya nione kama
nitapata maumivu yoyote, nikajigundua kuwa mimi ni
mzima ila nipo mahali ambako sipatambui kuwa
nitaanzia wapi na nitaishia wapi.
Nikaanza kujikongoja ili niweze kutoka kwenye lile
eneo. Nikasikia sauti ikiniambia,
"Kiburi chako ndio kinachokuponza hapo"
Nikijaribu kuifatilia hiyo sauti najikuta sina uwezo wa
kuifatilia zaidi ya ninavyoisikia.
Cha kushangaza sasa, licha ya misukosuko yote hiyo
simu yangu bado nilikuwa nayo kwenye mfuko wa
suruali niliyovaa siku hiyo.
Nilipojipapasa na kuikuta nilishangaa sana na kufurahi
pia, nikaichukua na kumpigia Suzy hakupatikana,
nikampigia mama na dada hawakupatikana yani wote
niliojaribu kuwapigia muda huo hawakupatikana na
wakati giza lilishaanza kuingia, sikuwa na la kufanya,
nikaamua kutembea hovyohovyo ili hata nikiwakuta
wenyeji wa eneo lile niwaulize vizuri ili wapate
kunielekeza.
Nilitembea sana hadi giza ilishaingia vizuri, nikakosa
matumaini na sikujua cha kufanya.
Kwa bahati nikakutana na kijana, sijui hata alikuwa
ametokea wapi na anaenda wapi, nikajaribu
kumsalimia ila yeye aliongea maneno mengine, kila
nilichosema yeye alijibu vingine hapo nikagundua
kuwa yule kijana hajui kiswahili, sasa tutaelewana
vipi ikiwa na mimi sielewi anachosema?
Kwavile ni mimi mwenye shida nikaamua kumfatilia
nyuma nyuma hadi anapoenda.
Akafika sehemu moja kuna nyumba ya nyasi tena iko
peke yake wala hakuna nyumba ya karibu jirani yake.
Wakatoka watoto wawili wakike kwa kuwakadilia
kama wana miaka kumi hivi, wakampokea yule
kijana.
Kwavile na mimi nilianza kuogopa giza nikaamua
kuwafata hivyohivyo huku uoga ukiwa umenijaa
moyoni, niliogopa sana.
Nikajaribu kuwaongelesha ila wakanijibu kwa kilugha
chao, nikaamua kukaa hivyohivyo hata kama
hatuelewani.
Wakatenga chakula na kuniita kwa ishara ya mkono
kuwa nijumuike nao, ingawa njaa ilikuwa inaniuma ila
nilisita kujumuika nao ukizingatia hata chakula
chenyewe sikukielewa, nilichokitaka hapo ni mahali
pa kulala tu kwa usiku huo ukizingatia maeneo
yenyewe hapakuwa na watu zaidi ya hao.
Walipomaliza kula, wakanionyesha mahali nikajilaza.
Wakati nimelala nikamuona mtu ameshika kisu
anataka kunichoma nikashtuka na kupiga makelele.
"Nakufaaaaa....."
Kitu ambacho kiliwashtua mule ndani, nikashangaa
yule kijana akija kwa hasira na kunivutia nje, nilikaa
pale nje na kulia hadi panakucha.
Asubuhi yake nikaanza kuondoka lile eneo huku sauti
ikitembea kichwani mwangu,
"Yote hayo yataisha ukikubali kuolewa na mimi"
Nikawa naumia sana hukunikichukia kuwa ni mambo
gani haya yanayoiandama akili yangu.
Nilikuwa nimechoka sana muda huo, mara simu
yangu ikaita kuangalia ni Carlos aliyekuwa akipiga ile
simu nikaipokea huku ninalia.
"Njoo unisaidie Carlos njoo"
"Nakuja Sabrina"
Nilichoka sana na njaa ilikuwa inaniuma, hata sikuwa
na muda wa kumuuliza Carlos kuwa atafika vipi
mahali ambako sijamtajia maana hata mimi
mwenyewe sikujua nilipo.
Nilikaa chini, kiu na njaa vilinisumbua sana maana
hapakuwa na maji hata kidogo wala miti ya matunda
nayo haikuwepo.
Nikakaa chini ya mti mmoja na usingizi kunipitia
palepale, akatokea mkaka wa ndotoni akitabasamu
na kusema.
"Yote yataisha ukiolewa na mimi"
Nikashtuka na kusema,
"Sitaki kuolewa na wewe"
Simu yangu ikaita tena, ni Carlos aliyepiga na
kuniambia kuwa yupo maeneo ya karibu na nilipo
kwahiyo niinuke kumfata.
Nikaamua tena kutembea taratibu, mbele yangu
nikaona gari yake ambapo alishuka na kunifata nilipo,
kisha akasema.
"Napenda sana kukusaidia Sabrina ila unatakiwa
kukubaliana na mimi jambo moja tu"
"Lipi hilo?"
"Olewa na mimi"
Nikabaki nimeduwaa tu na kukosa cha kujibu.
Itaendelea muda mrefu…!!
 
SEHEMU YA 36


Nikabaki nimeduwaa tu na kukosa cha kujibu.
Nikamuangalia kwa makini Carlos na kupata jibu la
haraka kumjibu.
"Naomba unitoe kwanza eneo hili halafu hayo
mengine tutazungumza badae"
"Hakuna tatizo Sabrina, najua unanihitaji kupita
unavyofikiria"
Kisha akaniongeza hadi kwenye gari yake nikapanda,
kwavile nilikuwa nimechoka sana na usingizi kunizidia
nikajikuta nimelala.

Kuja kushtuka tayari tulikuwa tumefika nyumbani
kwetu, mama akafurahi sana kuniona huku
akimshukuru Carlos.
"Nilikwambia mama usijali nitamtafuta Sabrina hadi
nimpate, huyo hapo sasa"
"Nimefurahi sana, asante baba angu"
Tukaingia ndani na mama kisha Carlos akaenda zake.
Mama akaanza kuniuliza sasa,
"Ulikuwa wapi mwanangu?"
"Sijui mama, sijui"
"Utaniua mama yako wewe, utaniua kwa presha. Hivi
huyo Sam wako atanizalia Sabrina mwingine mimi?
Mbona unanitesa hivyo mwanangu?"
"Nisamehe mama"
"Na huo msamaha ungeombea kaburini nani
angekusikia mwanangu? Unajua utaniua wewe mtoto!
Kilichokupeleka kwa wakina Sam sijui ni kitu gani,
nadhani unaombea hata mimi nife ila ubaki na Sam
jinsi ambavyo umekosa akili wewe mtoto"
Nikakaa kimya kabisa kwani sikupenda kubishana na
mama na vilevile sikujua ni nani aliyemwambia kama
nilienda kwa wakina Sam.
Mama alipomaliza kusema yake nikaenda zangu
kuoga ili kupata nguvu kidogo, kisha nikala chakula
ambacho mama aliniandalia bila hata ya kujua kama
mwenzie nimelala maporini usiku wote wa jana.
Nilipomaliza kula, nilienda chumbani kwangu kwa
lengo la kupumzika kidogo.

Nikiwa nimetulia chumbani, nikaona mfuko wa rambo.
Nikainuka na kwenda kufungua, nikakuta viatu vizuri
sana vipo ndani yake. Nikabeba ule mfuko na kwenda
kumuuliza mama.
"Nani kaweka mfuko huu chumbani kwangu?"
"Ni mimi nimeweka, ni zawadi yako hiyo uliyoletewa
na Carlos halafu ukanidanganya kuwa unakwenda
kuifata"
"Nisamehe mama"
"Nishakwambia kuwa msamaha wako hauna maana
kwa sasa. Sema lingine tu"
Nikaviweka vile viatu chini na kuvijaribisha, kwakweli
vilikuwa vizuri na vilinipendeza sana.
Nikaanza kujaribu kuvitembelea maana vilikuwa
virefu kiasi,
"Amekupatia sana Carlos, viatu vimekupendeza sana
mwanangu"
Nikawa natabasamu huku nazunguka navyo ndani
kisha nikarudi chumbani kwangu, nikakaa kitandani ili
nivivue niweze kupumzika.
Nikavivua, mara gafla miguu ikawa kama inawaka
moto halafu inauma sana sikujua tatizo ila kuna roho
ikaniambia kuwa sababu nimevua vile viatu kwahiyo
nikavivaa tena na ile miguu ikaacha kuuma na kuwa
kama inawaka moto.
Nikajiuliza mahusiano ya kile kiatu na mguu wangu ni
nini nikakosa jibu, nikajaribu tena kuvivua nione napo
miguu ikaanza tena kupwita, nikavivaa tena na
kujiuliza nitalala na viatu miguuni leo? Ila sikuwa na
jinsi kwani nilichoka sana na kuamua kulala navyo.
Dada ndiye aliyekuja kunishtua pale kitandani.
"Sabrina, Sabrina hebu amka tuongee"
Nikaamka na kukaa, kisha nikamsalimia na
kumsikiliza.
"Ulikuwa wapi jana?"
"Sijui dada"
"Mmh Sabrina! Nasikia ulienda kwa wakina Sam
umedundwa huko hadi umekoma"
Nikawa kimya tu nikimsikiliza.
"Viatu vizuri hivyo kakununulia nani?"
"Nimevikuta humu ndani, mama kasema nimeletewa
na Carlos"
"Eeh vimekupendeza! Hadi unalala navyo duh!"
Kisha akainuka na kutoka chumbani kwangu.
Nikajitazama tena miguuni na vile viatu, nikajaribu
kuvivua hali ikawa kama ya mwanzo. Nikajiuliza ni
kwanini? Ila nikajisemea kuwa lazima Carlos anajua
sababu, nikachukua simu na kumpigia ila
hakupatikana hewani.
Nikatoka sebleni.
"Naona viatu havibanduki miguuni leo mwanangu"
Dada Penina akadakia,
"Chezea kitu kipya wewe"
Wote wakacheka, nikatamani kuwaambia
ninavyojisikia nikikivua ila mdomo ulikuwa mzito
kusema chochote kuhusu kiatu.
Nikatulia pale sebleni na kusikiliza mazungumzo ya
mama na dada ambayo yalinivutia sana, nikajisemea
kuwa badae nitamfata dada chumbani kwake ili
kumuuliza vizuri.

Usiku ulipoingia kama kawaida ya dada yangu
alikuwa yupo chumbani kwake akicheza na kompyuta
yake ya mezani, nikamfata alipo ili anijibu maswali
yangu.
"Eeh niambie mwali wa viatu vipya"
Nikacheka tu na kumwambia,
"Nimekuja kukuuliza kitu dada"
"Kitu gani hicho? Uliza tu kuwa huru"
"Ni kuhusu mazungumzo yako na mama, umesema
yule rafiki yako dada Fatuma alikuwa akisumbuliwa
na matatizo gani hadi akaachana na mchumba
wake?"
"Aah! Kumbe, alikuwa akisumbuliwa na jini mahaba
yule"
"Jini mahaba? Ndio yukoje huyo jini mahaba?"
"Kwakweli mdogo wangu sijui ila itakuwa vyema
kama hayo maswali ukienda kumuuliza Fatuma moja
kwa moja, nadhani yeye atakuwa anajua maana ndio
alikuwa nalo na likamsumbua sana"
"Ila je hilo jini lilimuachanisha vipi na mpenzi wake?"
"Nasikia lile jini likikupata huwa linataka likutawale
lenyewe tu, utashangaa gafla huna maelewano na
mpenzi wako mara unaona hakupendi mara anahisi
hakuridhishi au hakufai tena na mengineyo hadi
unafikia uamuzi wa kuachana nae"
"Sasa suluhisho ni lipi hapo?"
"Suluhisho ni kwenda kulitoa kama ukigundua unalo,
je wewe unahisi kuwa na hilo jini?"
"Sijui dada ila ninahitaji kufahamu zaidi"
"Basi nitakukutanisha na Fatuma uongee nae na
akuelezee vizuri"
"Lini sasa?"
"Hata kesho"
"Mi nataka iwe kesho dada"
Nikakubaliana na dada kuwa kesho yake atanipeleka
kwenda kukutana na Fatuma nipate kuzungumza nae.
"Nitawahi kurudi kesho halafu nitakupeleka"
"Sawa dada, utakuta nimeshajiandaa"
Akacheka kisha tukainuka na kwenda kula halafu
kulala huku nikifikiria hayo mambo ya kesho na viatu
vyangu mguuni ambavyo kuvivua sikuweza.

Nikiwa nimelala, yule mkaka wa ndotoni akanijia
kwenye ndoto kama kawaida na kusema.
"Natumaini umeifurahia zawadi yangu"
Nikashtuka na kujitazama miguuni ambako nimevaa
vile viatu kisha nikavivua kwa hasira ila maumivu
niliyoyapata sikuweza hata kusogea na kuamua
kuvivaa tena maana sikuwa na la kufanya kwakweli.
Nilipovivaa tena nikalala vizuri hadi panakucha na
kuamka huku nikifanya kazi za hapa na pale.
Mama kuniona tena na vile viatu akaanza kunitania,
"Nadhani leo utaoga navyo hivyo viatu maana
havivuliwi"
Sikujibu kitu maana hawakujua jinsi ninavyoteseka na
kile kiatu mguuni.
Nilipomaliza kazi, nikaenda kuoga.
Nilipofika bafuni nikajaribu kuvua kile kiatu ili nioge,
nikakivua na wala miguu haikuniuma ila nilipomaliza tu
kuoga ilianza kuniuma tena na kuamua nivae tena vile
viatu wakati natoka bafuni.
Nikaenda chumbani na kujiandaa ili kumngoja dada
arudi na niende nae huko kwa rafiki yake.

Dada aliporudi akapumzika kidogo kisha tukamuaga
mama na kuondoka huku vile viatu vyangu vikiwa
miguuni,
"Naona umevipenda sana hivyo viatu Sabrina"
"Ndio nimevipenda dada"
Tulipofika kwa rafiki yake na dada, tulimkuta ametulia
tu ndaki akisikiliza muziki.
Dada akaongea nae kidogo pale na kutuaga kuwa
kuna mahali anaenda mara moja akitoka huko ndio
atapitia tena hapa.
"Naona umeniletea Sabrina leo"
"Ana maswali yake huyo atakuuliza mwenyewe"
Kisha dada akaondoka na kuniacha na rafiki yake
dada Fatuma pale.
"Kuwa huru Sabrina, niulize chochote nitakujibu"
"Jana nilimsikia mama na dada wakiongelea maswala
ya jini mahaba na kusema kuwa hata wewe limewahi
kukurumbua"
"Kwahiyo unahitaji kujua kuhusu jini mahaba?"
Nikatikisa kichwa kuonyesha kwamba nahitaji kujua.
"Jini mahaba ni kiumbe mwenye tabia ya kukuingilia
kimwili bila ridhaa yako, mara nyingi huja wakati
umelala. Unakuwa unahisi kama unaota vile kuwa
unaingiliwa na mtu, ukija kushtuka mara nyingine
unajikuta umechafuka kwa mbegu za kiume, hapo
utakuwa na jini mahaba tena aliyekubuhu"
"Je mwanadamu wa kawaida anaweza kufanya
mambo kama afanyayo jini mahaba"
"Si rahisi ila akiwa mchawi anaweza maana
atakupumbaza wakati umelala kama huna kinga
thabiti dhidi ya watu wabaya"
"Unaweza kumuona jini na kuongea nae kama
binadamu wa kawaida?"
"Majini ni viumbe wa ajabu sana, kwanza wanatisha
huwezi kustahimili ukikutana nao. Halafu wananamna
nyingi za kutembea na kusafiri, anaweza kujigeuza
upepo au hata mdudu mdogo kabisa. Hata ukiwa
katika shule zenye majini utashangaa gafla upepo
mkali unapita, wanaojua watakwambia jini kapita"
"Kwahiyo huwezi ukaonana nae kabisa yani"
"Nakwambia huwezi kustahimili kumtazama jini,
kwani hujawahi kusikia watu wakisema kuwa majini
wanakwato za ng'ombe miguuni mwao, au kusikia
kuwa majini ni warefu sana hata ukikutana nao
lazima uchanganyikiwe. Si rahisi kukaa na
kuzungumza na jini mdogo wangu"
"Je wewe ukimuona jini utamjua?"
"Inategemea ila kiukweli nawaogopa majini sitaki hata
kukutana nayo nahisi nitakufa kabisa"
"Nasikia jini mahaba alifanya uachane na mpenzi
wako!"
"Ndio, unajua sifa kubwa ya jini mahaba ni wivu. Huyu
jini anawivu sana na huwa anataka akumiliki peke
yake hivyo atakufanyia visa hadi uachane na
unayempenda"
"Sasa ulifanyaje wewe ulipogundua unae?"
"Nilitafuta mtaalamu, kipindi kile nazunguka sana na
Penina tukapata mtaalamu huko mbali, yeye ndio
akatusaidia. Kwani unajihisi kuwa na jini mahaba
wewe?"
"Sielewi dada, maana nimejikuta mambo yangu
yakienda sivyo na mpenzi wangu nae nimeachana
nae. Basi nisaidie dada yangu, nipeleke kwa huyo
mtaalamu"
"Hayupo hapa kwa sasa, yupo mkoani ndio anafanyia
shughuli zake. Akirudi nitakwambia twende mdogo
wangu hata usijari"
"Sawa dada, ila ni kweli kabisa huweza kumuona
jini?"
"Wanatisha mdogo wangu, sio kama sisi tulivyo wao
ni viumbe wa ajabu."
Nilikuwa nauliza kwa makini huku moyoni mwangu
nikipima kuwa Carlos atakuwa ni mtu wa aina gani.
Dada aliporudi, tuliaga mahali pale na kurudi
nyumbani na giza lilishaingia.

Nikiwa nyumbani nikatafakari sana na kuona kuwa
yule wa ndotoni atakuwa jini mahaba tu, nikahisi
mpaka atakaporudi huyo mtaalamu wa dada Fatuma
nitakuwa nishateseka sana na kuolewa na Carlos
sikutaka maana sikumuamini na yeye, nilihisi ni
mchawi.
Nikapata wazo la kwenda kuongea na mama kuhusu
mama Semeni maana alisema yupo tayari kunipeleka.
Nikamwambia mama kuwa nipo tayari, akafurahi
sana na kumpigia mama Semeni simu muda huo huo
ambapo akasema nijiandae kesho ili twende.
"Ila mwanangu umekuwa mzungu wewe? Viatu
umezurula navyo huko na bado upo navyo ndani"
Dada akadakia tena,
"Kipya kinyemi mama"
Sikusema chochote huku nikiamini kuwa majibu ya
maswali yangu yote yatapatikana kwa huyo mtaalamu
kesho.
Nikaenda kuoga ikawa kama asubuhi, nikiwa bafuni
navivua na kuoga ila kutoka miguu inauma hadi
nivivae.
Nikazunguka vile vile na viatu hadi usiku wakati wa
kulala ila leo nililala vizuri tu wala sikupatwa na ndoto
yoyote ya kutisha hadi panakucha.

Asubuhi na mapema, mama Semeni aliwasili
nyumbani na kukuta mimi na mama tumeshajiandaa
tayari.
Safari ikaanza ya kwenda kwa huyo mtaalamu,
ilikuwa mbali kweli ila tukavumilia hadi kufika.
Ilikuwa ni kibanda cha nyasi, mama na mama Semeni
waliingia nikabaki mimi nje kwani kila nikitaka kuingia
mtaalamu ananiambia
"Vua viatu"
Vile viatu muda huu havikutaka kutoka miguuni
kabisa, kila nilipojaribu kuvua ilishindikana.
Nikamwambia yule mtaalamu,
"Havitaki kuvuka"
Yule mtaalamu akafanya dawa zake kisha akanifata
yeye mwenyewe, akainama na kushika viatu vyangu.
Mara gafla akarushwa kamavile mtu aliyepigwa na
shoti ya umeme.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 37


Yule mtaalamu akafanya dawa zake kisha akanifata
yeye mwenyewe, akainama na kushika viatu vyangu.
Mara gafla akarushwa kamavile mtu aliyepigwa na
shoti ya umeme.
Akaanguka na kuzirai jambo ambalo lilitushangaza
sana.
Msaidizi wa mganga alituangalia kwa hasira na
kuanza kutufukuza,
"Ondokeni, nyie ni watu wabaya sana"
Mama Semeni akajaribu kumbembeleza ila
ilishindikana, tukaondoka pale na kumuacha yule
mganga akiwa vile vile kazimia.
Tulitembea njia nzima bila ya kusema chochote hadi
tulipofika nyumbani, mama Semeni hakutaka hata
kuingia ndani akaondoka huku akimwambia mama.
"Hii ni aibu ndugu yangu, mwanao hafai"
Nikaingia ndani na kumuacha mama aliyekuwa
amemsindikiza kidogo mama Semeni.
Baada ya muda kidogo mama akarudi ndani na
kuanza kuniuliza,
"Hivi hivyo viatu vina nini mwanangu? Kwanini hutaki
kuvivua jamani?"
"Havitaki kuvuka mama"
"Unamaana gani? Si umeletewa na Carlos hivyo!"
"Ndio mama ila havitaki kuvuka"
"Kwahiyo ukienda kuoga unaogaje?"
"Navivua naweka pembeni, nikimaliza kuoga navivaa
tena"
"Wewe Sabrina ni mwehu sana tena sana, ngoja
nimpigie simu huyo Carlos anipe maana ya hivyo
viatu ambavyo havivuliki"
Mama akajaribu kumpigia Carlos kisha akanipa jibu
kuwa hapatikani.
Ikabidi kuendelea na mambo mengine tu kwani
kilichotakiwa kufanyika kimeshindikana.

Dada Penina aliporudi akaanza kumuuliza mama,
"Mbona mmewahi sana kurudi? Nilijua sitawakuta"
"Mwenzangu kiatu hicho"
Huku akinyooshea kidole kwenye kiatu changu,
"Kimefanyeje?"
"Mwambie akivue"
Dada akacheka na kuniangalia kisha akaninyooshea
kidole na kuwa kama anataka kuimba na kusema,
"Hicho kiatu kivue"
Mama nae akacheka huku akitingisha kichwa kama
ishara ya kusikitika na kusema,
"Kiatu kimetuzulia mambo hicho leo"
Dada akatulia kwa makini, kisha mama akaanza
kumsimulia kilichotokea leo.
"Sasa mganga wa watu anaendeleaje?"
"Sijui maana msaidizi wake alitufukuza na
kusema......."
Nikinuka na kwenda zangu chumbani kwangu na
kuwaacha na mazungumzo yao.
Nikiwa chumbani nilijitafakarisha sana na kukosa jibu
kabisa, sikujielewa hata kidogo.
Muda kidogo dada nae akanifata chumbani kwangu
na kukaa karibu yangu ili tuzungumze.
"Nasikia hicho kiatu uliletewa na Carlos, sasa
ukimuuliza kuhusu hayo mauzauza anakwambiaje?"
"Carlos hapatikani dada"
Dada nae akachukua simu yake kujaribisha kisha
akanipa jibu kuwa hapatikani kweli na kusema.
"Inamaana kakupa hivyo viatu kwaajili ya kukukomoa
au?"
"Hata sijui dada"
"Ngoja, tutafanya kitu lazima tupate ufumbuzi wa hilo
swala"
Kisha akatoka na kwenda chumbani kwake. Nikabaki
mwenyewe sasa na kuendelea na mawazo yangu.
Nikakumbuka tena kuhusu Sam, na roho ya kuhitaji
kujua anavyoendelea ilinisumbua sana na kujisemea
kuwa lazima nikamtafute. Pia nikakumbuka tena
kuhusu Suzy ambaye sijawasiliana nae kabisa tangu
siku niliyopata matatizo, nikajaribu kumtafuta ila
hakupatikana.
Nikajaribu kumtafuta na Sam nione kama nitampata,
kwa bahati simu yake ikaita hadi nikashangaa
nikatulia kwa makini ila haikupokelewa, nikajaribu
tena na tena haikupokelewa nikakata tamaa na
kujilaza kwa mawazo.
Wakati nimelala nikashtuka kusikia simu yangu inaita,
ila nilipotaka kuipokea ikakatika na kugungua kuwa
alikuwa anabeep halafu namba ilikuwa ngeni machoni
pangu.
Nikaamua kumpigia,
"Hallow, nani mwenzangu"
"Mimi ni Sam"
Nikafurahi sana,
"Jamani Sam wangu uko wapi?"
"Nateseka Sabrina, naumia ila bado nakupenda sana"
Machozi yalinidondoka, nilihisi maumivu moyoni
mwangu.
"Niambie ulipo Sam"
Sam hakusema chochote zaidi ya kukata simu, roho
ilizidi kuniuma nikajaribu tena kuipiga ile namba lakini
haikupatikana.
Baada ya muda kidogo nikapokea ujumbe kutoka
kwenye ile namba.
"Nakupenda Sabrina, haya ni mapito tu ila ipo siku
yataisha. Sitaki kukwambia nilipo maana najua
utateseka kulijua hilo, ila tambua nakupenda sana na
upendo wangu kwako hauwezi kufa kamwe.
Nakupenda sana Sabrina"
Roho ilizidi kuniuma, nikajaribu tena na tena kuipiga
ile namba sikuipata hewani.
Nikajiinamia kitandani kwa uchungu nilionao muda
huo huku nikijiuliza alipo Sam maana nilitamani kweli
kuonana nae.
Nikapata wazo la kwenda kwa kina Suzy tena
kuangalia hali ya Suzy na kumuuliza alipo Sam ili
niende mwenyewe.
Wazo la kwenda kwakina Suzy lilikuwa kwa kasi
sana na sikutaka kupoteza muda tena, nikatoka
chumbani kwangu na kwenda nje bila ya kuaga
nikaondoka. Nyumbani hawakuwa na mashaka kuwa
naenda mbali, kumbe mwenzao sipo kabisa maeneo
ya nyumbani.
Kufika kwa wakina Suzy nikamkuta mama yake nje,
baada ya salamu akaniambia.
"Nakupenda Sabrina ila sitapenda uongozane na
mwanangu tena"
"Kwanini mama?"
"Hakuna cha kwanini, fanya nilichosema.Namaanisha
uondoke hapa kwangu, matatizo unayompatia
mwanangu yanatosha kwa sasa"
"Lakini mama....."
"Hakuna cha lakini Sabrina, nilikuamini sana na
kukuona kuwa ni mtoto mwema na mzuri, sikujua
kama wewe ni mtoto mbaya kiasi hiki"
"Ila sijui kosa langu mama!"
"Nishakwambia, sitaki kukuona ukiongozana tena na
mwanangu Suzy"
"Sawa mama, ila ningependa kumuuliza Suzy jambo
moja"
"Niulize mimi nitakujibu"
"Samahani mama, naulizia mahali ambapo Sam
amepelekwa"
"Nenda kituo cha kati"
"Ndio kipi hiko?"
Akanipa maelekezo na kusema kuwa niondoke.
Niliondoka bila ya kujua nini kosa langu hadi mama
Suzy kunichukia.

Nikafika kituo cha polisi na kuwaomba kuzungumza
na Sam, mwanzoni walinikatalia ila baada ya
kuwaomba sana wakaniruhusu kuongea nae.
Wakamuita Sam aliyekuwa amekonda sana, roho
ikaniuma na kuhisi kuwa kama Sam ataendelea
kuwekwa kwenye kile kichumba cha giza atakufa.
Niliona machozi yakinitiririka, Sam alinikumbatia
akilia huku akiniambia nikaze moyo.
"Ila ni mimi Sam ninayestahili hukumu hii"
"Sioni tatizo kuteseka kwaajili yako Sabrina, najua hii
ni njia mojawapo ya kuniamini jinsi ninavyokupenda"
"Sam nahitaji kukusaidia"
"Ila usijitoe thamani yako kwaajili yangu, haya ni
mapito tu"
"Ila mbona wewe umeitoa thamani yako kwaajili
yangu? Lazima na mimi nijitoe Sam"
"Usifanye hivyo tafadhari utaniumiza zaidi, napata
ndoto mbaya sana juu yako. Halafu nasikia
ulimsukuma Suzy toka ndani ya gari na....."
Askari akakatisha mazungumzo yetu na kusema
muda umekwisha halafu akamchukua Sam na kumrudisha rumande,
nililia sana huku nikijiuliza maswali mengi bila ya
majibu.
Kwanini inakuwa hivi kwangu, maana hata Suzy
sikujua nilichomfanya na huko kumsukuma
nilimsukuma muda gani? Kwakweli mengi
nilisingiziwa na kuchukiwa na watu walionizunguka tu.
Sikuwa na jinsi zaidi ya kurudi nyumbani.
Kufika ndani nikajua nitapata lawama nyingi sana
kutoka kwa mama sababu nimeondoka bila kuaga na
niliporudi giza lilishaingia.
Nilimkuta mama sebleni ila hakuniuliza chochote
kuhusu kutoka kwangu, nilikaa kwa kusitasita mama
akasema.
"Na wewe mwanangu unalala sana, sijui hata usiku
utalala usingizi gani"
Nikastaajabu sana, yani muda wote ule niliotoka
mama anajua nimelala ndani! Au kuna Sabrina
mwingine ndani kwetu? Nikajiuliza na kukosa jibu ila
kumuuliza mama nikashindwa, kisha nikainuka na
kwenda chumbani.
Nilipakuta vilevile kama nilivyopaacha, muda kidogo
dada akaja chumbani kwangu.
"Khee ushaamka?"
"Kwani ulikuja muda gani ambao ukaniona nimelala?"
"Muda sio mrefu nilikuja chumbani kwako nikakukuta
umelala, tena hoi kabisa ila bora umeamka twende
ukanisaidie kitu chumbani kwangu"
Nikashangaa tu kuona kuwa wote ndani walijua
nimelala, kisha nikainuka na kufatana na dada hadi
chumbani kwake.
"Ile picha imerudi tena kwenye kompyuta yangu,
niondolee Sabrina"
Nikakaa na kuiangalia kwa makini na kugundua kuwa
ni ileile picha ya kijana wa ndotoni ila dada huwa
anaitoa wapi?
Wakati najiuliza ile picha ikatabasamu, nikashtuka na
kuacha kufanya ninachofanya huku nikimshtua dada
nae aweze kuona.
Ila dada alipoangalia nae akatabasamu na kusema.
"Asante Sabrina kwa kunitolea ile picha maana
ilikuwa inanikera sana"
Nikashindwa cha
kusema sababu ile picha sikuweza kuitoa lakini ilitoka
yenyewe.
"Ila dada huwa unaitoa wapi hiyo picha?"
"Sijui, labda kwenye mitandao hii mdogo wangu
maana hata sijui ilipotoka kwakweli"
Nikaachana na dada pale na kwenda sebleni
kuzungumza na mama aliyekuwa akiniita.
"Nasikia kuna tukio ulifanya majuzi"
"Tukio gani tena?"
"Ulivyonidanganya hapa nyumbani kumbe ulienda
kwa kina Suzy, haya kilichokufanya umsukume
mwenzio kutoka kwenye gari ni nini?"
"Sijamsukuma Suzy mama na siwezi kufanya hivyo"
"Shauri yako, utaua wenzio wewe. Lucy umempiga
sababu ya mwanaume, Suzy umemsukuma bila
sababu. Sina pesa ya kusimamia kesi zako mie,
shauri yako"
Kwakweli lawama kuhusu Suzy iliniuma sana, hata
kuhusu Lucy niliumia pia ukizingatia Sam anateseka
rumande kwaajili yangu.
Sikuwa hata na hamu ya kula leo kwani matatizo
yalikuwa mengi na kunikosesha raha kabisa, niliamua
kwenda kulala tu.
"Huli leo?"
"Nimeshiba mama"
"Njoo ule kidogo mwanangu"
Dada akadakia,
"Si ameshasema kuwa kashiba! Mwache akalale tena
tu maana chakula chake kinapatikana usingizini"
Huku akicheka nami nikaingia chumbani kwangu.

Kwakweli nilikuwa nimechoka sana kwahiyo
haikuchukua muda sana nikawa nimelala tayari.
Wakati nipo usingizini, akatokea yule mkaka wa
ndotoni na sahani ya chakula mkononi akanipa nile
nami nikala chakula chote kisha akaanza kusema.
"Asante kwa kula chakula changu Sabrina, nakupenda
sana ndiomana nakujali. Si unaona leo umeondoka
kwenu bila kuaga ila nyumbani kwenu hawakujua
sababu nilikuja mimi na kulala kwenye kitanda chako
kwahiyo wakajua ni wewe. Nimekuepushia lawama
Sabrina sababu nakupenda. Nielewe Sabrina na
ukubali kuolewa na mimi"
Nilikuwa kimya kabisa nikimsikiliza, mara akasema.
"Naomba busu lako Sabrina"
Nikashtuka toka usingizini, nikakuta picha kitandani
kwangu kuangalia ni ya yule kijana wa ndotoni
nikaanza kuogopa na kuitupa. Nikasikia sauti,
"Usiogope Sabrina siwezi kukudhuru"
Huku nikitetemeka, nikamuuliza.
"Wewe ni nani kwani?"
"Mimi ni jini"
Nilitamani nisingesikia hiyo kauli kuwa yeye ni jini
kwani niliogopa sana na kutetemeka, aliendelea
kuongea.
"Naweza fanya chochote nitakacho ila sitaki
kukuumiza, nataka ukubali kwa hiyari yako kuolewa
na mimi"
Ile sauti ilikuwa inaniogopesha sana, nikakimbilia
mlango ili niweze kutoka lakini haukufunguka na
kufanya uoga unizidi.
Gafla sauti ile ikatoweka na kujikuta nikihema kwa
nguvu sana kama mtu niliyekimbia sana.
Nikatulia sasa huku uoga nao ukiendelea kunitawala,
gafla nikasikia sauti ikipiga kama mwangwi na
kusema,
"Carlos, Carlos, Carlos"
Nikajikuta nikilia kwa nguvu sana ila hakuna
aliyenisikia, halafu nikapitiwa na usingizi pale pale
mlangoni.

Kulipokucha nilijikuta kitandani ila sikujua ni nani
aliyeniweka kitandani.
Nikaamka na kupatwa na wazo moja tu kwenda
kumtazama Lucy ili niwaambie wazazi wake kama
mimi ndio nahusika na wamuachie Sam wangu huru
bora nikafungwe mimi mwenyewe muhusika wa yote.
Nikaoga na kujiandaa kisha nikatoka bila hata ya
kumuaga mama kwani najua atanikataza tu.
Safari ilikuwa moja kwa moja kwakina Lucy, kufika
pale mama yake alinikaribisha vizuri sana.
"Umekuja kumuona mwenzio, karibu sana"
"Asante mama"
"Za tangu juzi?"
Nikashangaa kuwa hiyo juzi ni juzi gani wakati nina
miezi sijafika kwakina Lucy, na mara ya mwisho
ilikuwa ni siku niliyoenda na Suzy halafu Lucy akaja
na Sam basi.
Sasa hiyo juzi anayoisema huyu mama ni juzi gani?
Ikabidi niitikie kwa kujigelesha,
"Nzuri tu mama"
"Mwenzio yupo ndani na yule daktari uliyetuletea,
kwakweli anaendelea vizuri sana tunashukuru kwa
hilo"
Hapo ndio akazidi kunichanganya kabisa yani maana
sikumjua huyo daktari anayemuongelea na je ni muda
gani niliompeleka huyo daktari? Sikujua kwakweli,
nikawa nimeduwaa ila mama Lucy akaniambia niingie
ndani baada ya kuona nimesimama tu pale nje.
"Ingia tu, nenda moja kwa moja chumbani kwake
utamkuta na mdogo wake Maria yupo huko huko"
Nikaongoza hadi chumba cha Lucy, nikapishana na
Maria mlangoni ambaye alinifurahia na kunikaribisha
ndani halafu yeye akatoka.
Nikaingia mule chumbani na kumuona Lucy amelala
kwenye kitanda halafu mtu mwingine mwenye koti la
kidaktari akiwa amesimama na kumpimapima,
nikasogea hadi pale.
Yule daktari akaniangalia, nikashtuka sana kwani
alikuwa ni Carlos.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 38


Yule daktari akaniangalia, nikashtuka sana kwani
alikuwa ni Carlos.
Nikashangaa kuwa Carlos ni daktari tokea lini? Na
vipi waseme kuwa nimemleta mimi?
Nikawa namuangalia Carlos kwa uoga, nikatamani
kupiga makelele ila nikashindwa kwani mdomo wangu
ulikuwa mzito kupiga kelele. Nikajikuta nikimuuliza tu,
"Wewe Carlos umeanza lini kuwa daktari?"
Maria nae akarudi muda huo huo mule ndani na
kuongea na mimi,
"Huyu dokta wako ametusaidia sana dada Sabrina,
maana dada Lucy anaweza hata kukaa na kula
kwasasa tofauti na mwanzoni. Kwakweli
tunakushukuru sana maana hapo amebakiza
kurudisha kumbukumbu tu"
Carlos akamuangalia Maria akitabasamu na kusema.
"Msijali, kumbukumbu zake zitarudi tu"
Kisha akaaga na kuondoka, Lucy alikuwa amelala
kwasasa.
Mama Lucy naye akaingia wakati Carlos akiondoka
na kuendelea kumshukuru kwa sana Carlos huku
akimsindikiza.
Nilibaki pale na Maria bila ya kujua cha kusema wala
cha kujielezea, je ni nani atanielewa? Sikujua kabisa.
Muda kidogo mama Lucy alikuja mule ndani na
kuniambia,
"Daktari anakuita hapo nje Sabrina"
Sikuwa na la kufanya zaidi ya kutoka na kwenda
kumsikiliza Carlos, cha kushangaza leo vile viatu
niliingia navyo hadi ndani kwa kina Lucy ila mama
Lucy hakushangazwa wala kuniuliza.
Nikamfata Carlos pale nje na kumwambia.
"Nimekuja kukusikiliza Carlos halafu nina maswali
yangu kadhaa nataka kukuuliza"
"Najua kama una maswali ndiomana nikakuita"
"Sasa nianze kukuuliza?"
"Hapana, nenda ukaage halafu twende mahali
ukaniulize"
Nikarudi
ndani kwa wakina Lucy na kumuaga mama Lucy
kisha nikaondoka na Carlos, akanipeleka mahali
ambako pametulia sana kisha kabla ya kumuuliza
akaanza yeye kuniuliza.
"Unampenda Sam?"
"Ndio nampenda"
"Kama unampenda basi hutopenda kuona anateseka
si ndio?"
"Ndio, roho inaniuma sana kuona Sam wangu
anateseka vile"
"Uhuru wa Sam unao wewe, unatakiwa kuamua moja
kama unapenda Sam awe huru hata leo"
"Natakiwa kuamua lipi?"
"Suluhisho ni kukubali kuolewa na mimi"
"Siwezi Carlos siwezi, kwanza sikuamini kama wewe
ni mwanadamu"
"Sasa mimi ni nani?"
Nikajibu kumwambia kuwa yeye ni jini ila mdomo
wangu ukasita na kusema,
"Sijui tu"
"Na kwanini sasa useme kuwa mimi sio binadamu?"
"Hueleweki Carlos hata wazazi sijui kama unao"
"Nia yako ni kuwaona wazazi wangu kumbe!!
Nikupeleke sasa hivi?"
Nikasita, kwani nikikumbuka zile stori kuhusu majini
nikahofia ikinitokea mimi.
"Naona unashaka na mimi, basi nitawaleta wazazi
wangu nyumbani kwenu"
"Eeh na huyo Sam atatokaje?"
"Nimekwambia kuwa unatakiwa kukubali kuolewa na
mimi halafu Sam atakuwa huru hata sasa"
"Kweli?"
"Sina tabia ya kudanganya"
"Sawa basi niko tayari, mwachie Sam huru"
"Upo tayari kweli Sabrina?"
"Ndio, nipo tayari kwaajili ya Sam"
"Utapata majibu yako muda mfupi ujao"
"Haya niambie na hivi viatu ambavyo umenipa mbona
ni vya ajabu"
"Tatizo lake ni nini kwani?"
"Havitaki kuvuka"
"Kweli havitaki kuvuka Sabrina?"
"Ndio havitaki kabisa"
"Hebu tuone"
Nikainua mguu wa kwanza, Carlos akanivua kile kiatu
kwenye ule mguu na kuniuliza.
"Unajisikiaje?"
"Najisikia vizuri tu"
"Nipe na huo mguu mwingine"
Nikauinua na kumwekea nao akanivua, kabla
hajasema chochote nilijishtukia nipo nyumbani.
Tena kitandani nimekaa, nikajitazama miguuni vile
viatu havikuwepo tena.
Akaja mama chumbani,
"Leo unaamka na kulala, unaamka na kulala sijui una
matatizo gani mwanangu?"
Nikamuangalia tu mama na kuinuka, nikatoka hadi
sebleni ili kujiona kama kweli nipo macho au nimelala
maana sikujielewa kabisa, ilikuwa kama ndoto vile
lakini ilikuwa ni kweli yani sikuamini kabisa haya
mambo kwakweli.

Jioni nikiwa nimekaa na mama sebleni akaanza kuniuliza,
"Mbona viatu ulivyosema havivuki leo umevua?"
"Ni Carlos huyo mama"
"Carlos kafanyaje?"
Mara akaingia dada Penina ndani na kukatisha mazungumzo yetu.
"Kuna mgeni wako nje Sabrina"
"Nani huyo?"
"Toka ukamuangalie"
Nikatoka hadi nje na kukuta mgeni wangu ni Sam, niliruka na kumkumbatia kwa furaha. Kwakweli nilifurahi sana kumuona Sam wangu tena akiwa huru kabisa.
Sam nae alinikumbatia huku akisema,
"Nipo huru mpenzi wangu Sabrina, nipo huru sasa"
Nilimkumbatia zaidi na kumkaribisha ndani ila Sam alikataa na kusema ni bora tukae palepale nje, nikaona haina tatizo.
Nikaenda ndani kutoa viti kisha kukaa na Sam ili tuzungumze yaliyojiri.
"Kwanza kabisa nimefurahi sana kukuona Sam wangu upo huru. Umetolewa lini kwani?"
"Leo leo, alikuja baba Lucy kunitoa. Nilipofika nyumbani sikukaa sana nikaona nije kukushukuru"
"Embu kwanza niambie, ilikuwaje hadi ukashikiliwa wewe wakati muhusika ni mimi?"
"Kwanza hata mimi mwenyewe nashangaa, unajua lile tendo lilikuwa la kushtukiza sana. Yani muda huo huo umempiga Lucy kwa chupa watu wengi wakajaa eneo lile, mara wakaja mapolisi halafu watu wote wa pale wakasema kuwa wameniona mimi nikimpiga Lucy ngumi kisha kumponda kwa chupa. Kwakweli ni jambo la kushangaza sana, kisha nikakamatwa na kupelekwa polisi yani haikuchukua muda wakafika ndugu wa Lucy na kusema nikae ndani hadi nishike adabu na si unajua tena wakina Lucy wana hela! Basi wakatumia pesa yao hata dhamana nikakataliwa"
"Sasa wewe hukuwaambia kama huhusiki?"
"Nani angenisikia na kunielewa Sabrina? Wakati watu wote pale wamesema kuwa wameshuhudia mimi nikifanya hivyo. Yani wewe hukutajwa kabisa kamavile mtu ambaye hukuwepo kabisa eneo la tukio"
Nikaishia kuguna maana mambo ni ya ajabu sana, Sam akaendelea kunielezea
"Ndugu zangu niliwaambia ukweli, wakaniomba sana nieleze kwa maaskari ukweli huo ila sikutaka kwamaana ningekuangamiza wewe wakati nakupenda siku zote"
"Pole sana Sam"
"Asante, ila cha muhimu nipo huru kwasasa. Asante sana Sabrina"
"Asante ya nini sasa?"
"Ya kunisaidia kutoka jela"
Hapo nikashangaa sasa na kuuliza,
"Nimekusaidiaje kwani?"
"Baba Lucy alipokuja kunitoa akasema amefanya hivyo sababu yako. Eeh na huyo Lucy anaendeleaje?"
Kwanza nilikuwa nikijiuliza maswali maana sikuelewa, huyo baba Lucy nimeonana nae muda gani hadi kuongea kuhusu Sam? Hapo maswali yakanichanganya kwakweli.
Sam akanistua kwenye hayo mawazo.
"Mbona hunijibu Sabrina au bado una hasira kuhusu Lucy?"
"Hapana Sam, Lucy anaendelea vizuri na wala sina hasira nae tena"
"Sasa mbona upo hivyo? Hujafurahi kutoka kwangu mpenzi?"
"Nimefurahi sana, hii ni furaha iliyopitiliza"
Halafu tukaendelea na maongezi pale nje, mara mama akatoka ndani na kunikuta na Sam pale nje nikajua atafoka sana lakini alikuwa tofauti sana leo. Kwani aliposalimiwa na Sam akaitikia vizuri sana hadi tukashangaa, kisha akasema,
"Mbona umeishia na mgeni hapo nje Sabrina? Hebu ingia nae ndani"
Sam akajibu kuwa pale nje panatosha.
Tukaendelea na maongezi pale mara mvua ikaanza kunyesha ikabidi tukimbilie ndani na giza nalo lilishaanza kuingia. Nikatamani hata kumkumbatia Sam ila tatizo tulikuwa nyumbani.
Kwenye mida ya saa tatu usiku ndio ile mvua ikakatika na hali kuwa shwari, Sam nae akaaga.
Dada akaniambia kuwa tumsindikize Sam kituoni.
Kufika kituoni, Sam akapata gari muda uleule.
Wakati tunarudi nyumbani tukakutana na gari ya Carlos, ikapita mbele yetu. Dada akaisimamisha lakini haikusimama, dada akaniuliza
"Si Carlos yule?"
"Ndio ni yeye"
"Mbona hajasimama sasa au umegombana nae?"
"Hapana"
Kabla hatujafika nyumbani mvua ikaanza tena ikabidi tujibanze mahali ili ipungue kidogo ila ile mvua haikupungua iliendelea kunyesha tu na radi kupiga, mimi na dada tukaanza kuogopa kwani umeme ulikatika muda huohuo baada ya mvua kuwa kali sana, hatukuwa na la kufanya zaidi ya kumkumbatia dada tu na kwa uoga nilionao nikaanza kulia maana tulikuwa tumesimama kwenye ubaraza tu wa duka ambalo lilikuwa limefungwa.
"Tuondoke dada"
"Tutaondokaje? Ngoja ipite gari tuombe lifti"
Mara gari ya Carlos ikapita tena, dada akaisimamisha, ikasimama na tukapanda. Dada akaanza kumuuliza,
"Mbona mwanzo umepita kama hutuoni?"
"Sikuwaona kweli ndiomana nikapita"
Basi Carlos akatufikisha nyumbani, kisha akamnong'oneza kitu dada ambapo sikuelewa ni kitu gani.
Kisha akanifata mimi kuniaga na kusema.
"Msaada wangu kwako wewe hauepukiki na huwezi ukastahimili bila kuhitaji msaada wangu, hili la leo ni somo tu"
Kisha akaondoka zake na kuniacha na msongo wa mawazo ila leo hakuingia ndani kwetu.
Kwavile muda ulikuwa umeenda ikabidi twende kulala tu maana chakula tulishakula, na umeme ukarudi muda huo huo ambao tulikuwa tukijiandaa kulala.

Usiku wakati nimelala nikajiona nipo mahali halafu
karibu yake kuna bonde kubwa sana tena la kutisha,
uoga ukanijaa kulitazama.
Kuangalia upande wa pili wa bonde nikamuona Sam
akiwa amefungwa kamba mwili mzima, nikatamani
kwenda kumfungua ila nitamfunguaje wakati kuna
bonde kati yetu. Nikaanza kuhangaika pale kwa lengo
la kumsaidia Sam ila ikaahindikana, pembeni yangu
akatokea yule kijana wa ndotoni huku akitabasamu na
kusema,
"Najua huwezi fanya chochote Sabrina bila ya
msaada wangu, unahitaji msaada niambie nikusaidie"
Nikamwambia,
"Nisaidie kumuokoa Sam"
Akanyoosha mkono kisha Sam akaletwa karibu yangu
na kusema
"Nimemuokoa tayari Sabrina, sasa wewe ni wangu"
"Hapana mimi si wako"
"Wewe ni wangu Sabrina na lazima nitakuoa na
utakuwa mke wangu"
"Siwezi kuolewa na wewe siwezi kuolewa na jini
kamwe"
Akacheka sana, nikamuangalia tu na kuongea maneno
mengimengi maana leo niliachiwa kuongea.
"Hivi karibuni nitakuja kukuvisha pete ya uchumba
kwahiyo jiandae mpenzi"
"Sitaki nimesema sitaki na siwezi kuolewa na wewe"
Nikashtuka toka usingizini na kukuta giza limetanda
chumbani wangu kumbe umeme ulikatika, na hapo
ndipo uoga ukanijaa kwa lile giza.
Mara nikasikia mtu akicheka sana kwenye chumba
changu, uoga ukanijaa na kujikuta nikiuliza na Leo.
"Wewe ni nani?"
Sauti ikaaikika,
"Unataka kila siku nijitambulishe?"
Nikabaki kimya nikitetemeka, kisha akacheka tena na
kusema
"Mimi ni jini"
Kwakweli hili neno la jini lilikuwa linanitisha sana
ukizingatia umeme umekatika Leo basi nikazidi
kutetemeka.
Mara nikasikia kama mtu akinikuna mgongoni hapo
nikashtuka sana na kutetemeka.
Nikaogopa kuongea chochote huku moyo wangu
ukiwa umejaa hofu tupu, muda huo huo umeme
ukarudi ikawa bora kwangu maana ningekufa kwa
presha ya giza.
Ile hali ya kukunwa mgongoni ikatoweka muda huo,
nikajipanga kwenda kumalizia usingizi kwa mama
lakini kabla sikainuka nikapatwa na usingizi pale pale
na kulala.

Kulipokucha alikuja mama kuniamsha,
"Kheee umelala sana mwanangu hebu amka kuna
kazi nyingi Leo"
Nikaamka na kujiandaa kwa hizo kazi, Kisha
nikamfata mama anipangie.
"Unajua hatujafua siku nyingi sana na nguo chafu
zimejaa, angalia pale"
Akanionyesha, kulikuwa na furushi la nguo chafu na
hapo nikakumbuka kuwa tuna wiki kama tatu
hatujafua.
"Mmmh mama tutamaliza leo kweli?"
"Tutamaliza tu mwanangu ila ndio tutafua siku nzima"
Mama akatoa zile nguo zote nje na kuniambia mimi
nianze kufua wakati yeye anamalizia kupika ili
tukimaliza kufua tule.
"Uwe unafua hapo, nikimaliza tu nakuja tusaidiane"
Kwakweli nguo zilikuwa nyingi sana maana ni nguo za
familia nzima.
Wakati naanza kufua nikasikia sauti,
"Nikusaidie kufua Sabrina?"
Kabla sijajibu chochote nikashangaa ndani ya dakika
mbili nguo zote zimeanikwa kwenye kamba na pale
chini hapakuwa na nguo tena.
Nikaogopa sana na kukimbilia ndani, mama
akanishangaa na kuniuliza.
"Vipi mbona umeacha kufua na kukimbilia ndani?"
Nilikuwa kimya nikitetemeka, mama akachungulia
dirishani, na kuuliza kwa mshangao
"Inamaana umemaliza kufua Sabrina??"
Mama hakuamini akaenda nje kuangalia, Mara sauti
ikaniambia tena
"Au nizikaushe kabisa na kuzikunja?"
Nikaanza kutetemeka sasa.

Itaendelea
 
Back
Top Bottom