Klabu ya Singida Black Stars imemfuta kazi Kocha Mkuu, Patrick Aussems, kutokana na matokeo yasiyoridhisha. Hadi kufikia hatua hii, timu hiyo imecheza mechi 11 za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ikishinda mechi 7, kutoka sare 3, na kupoteza mechi 1.
Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji, alijiunga na Singida Black Stars kabla ya kuanza kwa msimu wa 2024/2025, akilenga kuipa timu hiyo mafanikio makubwa. Hata hivyo, licha ya rekodi ya ushindi katika mechi nyingi, uongozi wa klabu umeamua kumaliza mkataba wake kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa timu.
Kabla ya kujiunga na Singida Black Stars, Aussems aliwahi kuifundisha Simba SC na AFC Leopards ya Kenya. Alipokuwa Simba, alifanikiwa kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.