Dk. Slaa awakaanga Kikwete, Spika Sitta
Asema Sitta si saizi yake, asijitafutie umaarufu asiostahili
MGOMBEA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amewarushia kombora Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea urais wa chama hicho, Jakaya Kikwete na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuwa ni wabadhirifu na wapenda anasa, ndiyo maana hawaamini kama elimu inaweza kutolewa bure.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana mjini Arusha alipokuwa akizungumza kwenye mikutano yake ya kampeni, ambapo alisema kuwa nchi ina fedha nyingi lakini kwa sababu ya ubadhirifu wa viongozi ambao wanapenda anasa, fedha hizo zimekuwa zikitumika kwa manufaa ya wachache.
Alisema Rais Kikwete na Sitta, kamwe hawawezi kuelewa au kuikubali sera ya elimu ya bure inayonadiwa na CHADEMA kwa sababu wamezoea kuzitafuna rasilimali za umma huku wakiwaacha wananchi wakiishi maisha ya tabu.
Hawa viongozi (Sitta na Kikwete) ni wabadhirifu, mioyo yao imejaa mambo ya anasa, ndiyo maana wanaposikia CHADEMA tunaweza kutoa elimu bure wanashangaa na kukataa kuwa hatuwezi kutekeleza, sisi tutaitoa elimu bure, kwa sababu tunajali masilahi ya walio wengi, alisema.
Dk. Slaa alitumia nafasi hiyo kupuuza ombi la Sitta ambaye alitaka mdahalo naye kujadili sera ya kutoa elimu bure, ambapo alisema spika huyo aliyemaliza muda wake si saizi yake, bali anafaa kupambanishwa na mgombea ubunge wa CHADEMA katika Jimbo la Urambo Mashariki, Msafiri Mtemelewa.
Hoja hizo za Dk. Slaa zimetokana na Rais Kikwete kumtaka aachane na sera ya kutoa elimu bure, kwa sababu ni jambo lisilowezekana na hata kama analisema hivi sasa ni katika lengo la kutafuta kura za wananchi.
Kauli hiyo ya Kikwete ilishabihishwa na Spika Sitta, ambaye alisema kuwa sera hiyo haitekelezeki na kama Dk. Slaa anabisha uitishwe mdahalo baina yao wawili wajadili hoja hiyo.
Dk. Slaa alisema serikali yake itatoa elimu bure kwa watoto wote wa Tanzania, kutoka chekechea hadi kidato cha sita, kwa sababu anajua fedha za kufanya hivyo zipo, isipokuwa zinatapanywa na viongozi wasiojali masilahi ya umma.
Alitoa mfano wa matumizi mabaya ya fedha za umma yaliyofanywa na Sitta akiwa spika, akasema wakati gharama ya ujenzi wa ofisi ya mbunge ni kati ya sh milioni 40 na 50, Sitta alitumia sh milioni 500 kujenga jengo la ofisi ya spika katika Jimbo la Urambo, kana kwamba kuna vikao vya Bunge vinavyofanyikia Urambo.
Utadhani Sitta anajiandaa kuwa spika wa maisha. Huu si ubadhirifu wa fedha za umma. Nimefanya hesabu, kiasi hicho cha pesa kinatosha kujenga zahanati 10 zilizokamilika na kinaweza kujenga madarasa 71 yaliyokamilika, alisema Dk. Slaa.
Sitoi takwimu hizo kwa kubahatisha ndugu zangu
ninazo nyaraka ambazo zinaonyesha namna fedha hizi zilivyotumika, kampuni zilizopewa tenda za ujenzi huo, sasa kama Sitta atasema ninasema uongo anijibu, alisema Dk. Slaa.
Alisema serikali ya Kikwete imekuwa ya anasa, kiasi cha kutenga bajeti ya sh bilioni 30 kwa ajili ya chai na vitafunio, pesa ambazo zingeweza kutumika kwenye masuala ya maendeleo.
Kama hakuna pesa, mbona wanajitengea sh bilioni 30 kwa ajili ya chai. Si wangezielekeza kwenye elimu na afya? Hawafanyi hivyo kwa sababu wanajua hawatafanya ubadhirifu wala kuendelea na maisha yao ya anasa, alisema.
Alisema kwa kuonyesha kuwa viongozi wetu ni wafujaji wa rasilimali za taifa, Rais Kikwete alikodi ndege mbili kwenda Urambo kufungua jengo la spika ambalo liligharimu mamilioni ya fedha za walipa kodi.
Alibainisha kuwa samani (fenicha) zilizowekwa katika jengo hilo zina thamani ya sh milioni 155, kiasi ambacho ni kikubwa mno, na kwamba hizo ni katika ofisi moja tu ya spika, bado ofisi nyingine za umma ambazo kila kukicha zimekuwa zikisifika kwa kununua samani za bei ghali.
Alisisitiza kuwa kama fedha hizo zingeokolewa na kutumika katika huduma, zingeweza kutumika kulipia huduma nyingine za kijamii.
Dk. Slaa aliwasisitizia wakazi wa Arusha kuwa elimu bure na afya bure ni mambo yanayowezekana, na CHADEMA imeamua kutoa vipaumbele kwa sekta hizo, kwa sababu zinagusa moja kwa moja masilahi ya wananchi wengi.
Aliongeza kuwa Sitta na Kikwete hawapaswi kuzungumza kuwa kutoa elimu bure haiwezekani, kwa sababu wao walipata elimu bure wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, lakini wanasahau jambo hilo na kuwa kikwazo cha kutoa elimu hiyo.
Alibainisha kuwa kwa serikali makini yenye kujali masilahi ya wananchi ambao ndio walipa kodi, ni jambo la lazima kuangalia matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi badala ya kutafuta sababu za kushindwa kutimiza wajibu.
Nataka nimwite Sitta kuwa ni mnafiki wa wazi, kwa kuwa anatumia fedha ya wananchi bila huruma, wakati yeye mwenyewe pamoja na wanaodai kuwa elimu bure haitawezekana walisoma katika serikali ya CCM wakati huo ikiongozwa na Mwalimu Nyerere bure, alisema.
Dk. Slaa alipata mapokezi makubwa wakati anaelekea uwanja wa Mbauda, ambapo alilakiwa na wananchi walioacha kazi zao na kuzuia msafara wake, wakaandamana kumsindikiza hadi uwanjani hapo kwa kulisukuma gari lake.
Katika mkutano wa jioni uliofanyika katika viwanja vya Kimandolu - Tindigani, maelfu ya wananchi yaliandamana kumsindikiza uwanjani, huku akiwa anasindikizwa na magari, pikipiki na watembea kwa miguu chini ya ulinzi wa polisi.
Dk. Slaa pia alisema mishahara minonno ya wabunge inachangia umaskini wa Watanzania, ambapo alitoa mfano wa posho na mshahara wa mbunge mmoja anavyolipwa katika vikao vyake kwa mwaka ni sawa na mishahara ya miaka 50 ya askari polisi au mishahara ya miaka 70 ya hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.
Mimi naona mgombea mwenzangu wa CCM - Kikwete hana sababu ya kuendelea kuzunguka, kwa kuwa ahadi ambazo anazisema kwa wananchi hajawahi kuzitekeleza hata moja.
Wakati nazindua kampeni zangu Jangwani, nilizungumza kuhusu fedha zilizochotwa na CCM katika mfuko wa matumizi ya kawaida (Other Charges) kwa ajili ya kufanyia kampeni zirudishwe, vinginevyo suala hili nitalilipua
lakini nashukuru kwamba agizo langu limetekelezwa, kwani fedha zote zimerejeshwa hata kabla sijaingia Ikulu, alisema.
source Tanzania daima
Hii imekaa vizuri sana wadau
Dk. Slaa pia alisema mishahara minonno ya wabunge inachangia umaskini wa Watanzania, ambapo alitoa mfano wa posho na mshahara wa mbunge mmoja anavyolipwa katika vikao vyake kwa mwaka ni sawa na mishahara ya miaka 50 ya askari polisi au mishahara ya miaka 70 ya hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.