MGOMBEA Urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chadema, Dk Wilbrod Slaam, amesema ubinafsi wa viongozi wa Serikali ya CCM, umekwamisha uchimbaji wa mafuta katika visiwa vya Zanzibar.
Kwa mujibu wa Dk Slaam, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), liliwahi kuwasilisha bungeni, sampuli ya mafuta yaliyotafitiwa katika visiwa vya Zanzibar.
Alisema hata hivyo Serikali ya CCM haijachukua hatua kuchimba mafuta hayo na kwamba hiyo inatokana na ubinafsi wa viongozi wa CCM.
Viongozi wa Serikali ya CCM, wameshindwa kuchimba mafuta yaliyoko Zanzibar kwa sababu ya ubinafsi wao wakihofu kuwa yatachukuliwa, alisema Dk Slaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wake wa kampeni, uliofanyika katika Jimbo la Mtoni katika Wilaya ya Mjini Magharibi.
Alisema hata hivyo kama atachaguliwa katika uchaguzi mkuu unatorajiwa kufanyika Jumapili ijayo, serikali atakayoiunda, itahakikisha kuwa mafuta ya Zanzibar, yanachimbwa.
Mafuta ya Zanzibar yatachimbwa na hayatakuwa katika mambo yaliyoko katika orodha ya Muungano na badala yake, yatatumika kuendeleza Zanzibar, kama ilivyo kwa gesi inayopatikana Mtwara, ambayo inatumika kuinufaisha Tanzania bara pekee, alisema Dk Slaa
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na mikutano mingine ambayo mgombea huyo amekuwa akikusanya umati mkubwa wa watu, alisema akichaguliwa pia ataimarisha Muungano.
Alisema yeye ni mmoja wa waumini wakubwa wa Muungano na kwa hiyo atauimarisha lakini ukiwa na mfumo wa serikali tatu na si serikali mbili kama ulivyo sasa.
Hali kadhalika alisema kama atachaguliwa, atachukua hatua za kuunda upya katiba ya Jamhuri ya .Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, ili zikidhi matakwa ya wananchi.
Dk Slaa alisema katiba hizo zitaundwa kwa kuwashirikisha wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa.
Katiba zilizopo sasa hazina sifa ya kuitwa katiba za wananchi kwa sababu hazikuwashirikisha wananchi. Tutaunda katiba zitakazotokana na mapendekezo na maoni ya wananchi, alisema mgombea huyo.
Dk Slaa pia alisema serikali atakayoiunda kama atachaguliwa, itahakikisha kuwa rasimali za Zanzibar zitatumika kikamilifu
ili kuvifanya visiwa hivyo kuwa lulu na dhahabu.
Zanzibar ni lulu na dhahabu ambayo hata hivyo haijatumika na hii ni kwa sababu, rasilimali zake haijatumika kikamilifu na kuifanya ipige hatua kubwa za kimaendeleo, alisisitiza.