URUSI NA UKRAINE; BABA NA MTOTO ANAYEGOMBANISHWA NA MZIMU WA "NATO".
Na. Comred Mbwana Allyamtu (CMCA)
Wednesday-23/02/2022
Marangu, Kilimanjaro, Tanzania
Mapema juzi Raisi wa Urusi Vladimir Putin alitangaza kuyatambua maeneo mawili ya miji ya Luhansk na Donetski kuwa Jamuhuri mpya ambazo zimetangaza kijitenga na nchi ya Ukraine.
Mgogoro huo wa ukanda wa Donbass umefatia baada ya kuwepo mivutano mikali baina ya Urusi na Ukraine kwa miaka 7 sasa, jambo ambalo linatishia kuwepo kwa vita kamili kati ya Urusi na Ukraine.
Hii Donbass ni nini hasa?.....
Nadhani tuanzie hapa, Donbass ni eneo la kihistoria, kitamaduni na kiuchumi kusini-mashariki mwa Ukraine, Neno Donbass linatokana na Bonde la Donets, na mto Donets, pia neno Donbass linatumika kulejelea mji wa Donetski ambao ndio mji mkubwa ukanda huo ambao ni mji wa tano kwa ukubwa nchini Ukraine.
Hivyo mji uliojitenga wa Donetski unawakilisha ukanda muhimu kiuchumi nchini Ukraine, ukiachilia mbali mji mwenza wa Luhansk ambao nao upo ndani ya bonde la Donets, kwaiyo unaposema Donbass unarejerea miji ya Donetski na Luhansk ambayo yote imo ndani ya bonde la Donets yani ndani ya ukanda wa Donbass.
Hivyo sasa.....
Ukanda huu wa Donbass una undwa na miji mikubwa miwili ya Donetski na Luhansk ambayo yote kwa pamoja ina migodi mikubwa ya makaa ya mawe ya Donets, hivyo maeneo hayo kwa namna yoyote ile ni muhimu kiuchumi kwa Ukraine.
Kwa muongo sasa maeneo hayo yalikuwa na vuguvugu la kujitenga, huku yakiungwa mkononi na Urusi, duru za kisiasa hudai kuwa vikundi hivyo ni vikundi vilivyo pachikwa na Urusi kufatia kuwepo kwa tishio la Ukraine kutaka kujiunga na NATO.
Hivyo, mapema juzi makundi yanayokalia eneo hilo la Donbass yametangaza kujitenga na kutangaza kuanzisha Jamhuri ya Watu wa Donetsk na Jamhuri ya watu wa Luhansk.
Lakini maswali ya kujiuliza hapa ni kwanini Urusi anachochea mgogoro wa ndani wa Ukraine na eneo la Donbass (Donetsk na Luhansk) ? Swali la kujiuliza zaidi ni kwanin Urusi anataka kuivamia Ukraine?
Maswali haya ndio yatatupa majibu ya kuujua kiundani mgogoro huu wa Ukraine na Urusi na kufahamu Kwanini Urusi ana lazimisha kusogeza mpaka wake wa Urusi ndani ya nchi ya Ukraine, jibu jepesi hapa ni NATO, yes NATO ndio sababu ya haya yote yanayo endelea huko Donbass.
Kwanini ni NATO?...........
Kwanza tuifahamu NATO, hii NATO hufahamika kama umoja wa kujihami wa nchi za magharibi, kwa kimombo hufahamika kama "The North Atlantic Treaty Organization", lakini pia hufahamika kama "North Atlantic Alliance", ni jumuia ya ushirikiano kijeshi baina ya nchi 27 za Ulaya na nchi 2 za America ya kaskazini na nchi moja ya Ulaya ya kati, jumuia hii iliweka mkataba wa kusaidiana kijeshi iwapo nchi moja wapo itavamiwa.
Jumuia hii ya NATO ilianzishwa mnamo tarehe 4 April 1949 kufatia kumalizika kwa vita ya pili ya dunia na kuibuka kwa vita baridi dhidi ya tishio la Umoja wa Usoviet USSR, hii Soviet Union ilikuwa tisho duniani dhidi ya mataifa ya kibepari huko Ulaya magharibi.
Kufatia hilo wakaona waunde jumuia ya kujihami ili wawe salama, tutaliona hilo kwa undani zaidi baadae kwenye makala hii ntakapo lielezea.
Ila kwa sasa tuangazie swali letu la kwanini Urusi anachochea mgogoro wa ndani wa Ukraine na eneo la Donbass (Donetsk na Luhansk), na pia tutafute majibu ya undani juu ya Swali la kwanin pia Urusi anataka kuivamia Ukraine?
Kwanza tuanze na mtego ambao Putin kawawekea NATO na nchi za G8, mtego huo NATO na Marekani wamenasa, maana wao waliwekeza nguvu kubwa dhidi ya Urusi kuivamia Ukraine, lakini imekuwa ni kinyume chake cha Putin kutumia akili kubwa ya kuisabaratisha Ukraine yenyewe ndani kwa ndani kupitia kanuni ya Divide et Impera, ntalieleza hili baadae.
Hapa unaweza kusema kuwa Putin ana akili sana, lakini jibu lingeni ukasema hapana ni mfumo thabiti uliojengwa Urusi, majibu yote yanaweza kuwa "Ndio" au "Hapana", ili kuelewa hizo Ndio au Hapana itakuitaji ufatilie nachoelezea then uunganishe na swali letu la msingi kuhusu huu mgogoro wa Urusi na Ukraine.
Majibu yako haya yote utayapata humu ndani ya makala hii, ni kwanini Urusi imeinuka kutoka mavumbini hadi kufika hapa leo, na ni kwanini Putin kawa tishio kwa mataifa ya magharibi, na hasa Kwanini Urusi na Ukraine zitake kuchapana?
Unaweza kudharau haya ninayosema lakini huu ndiyo ukweli na wala haukimbiliki, Sidhani kama Ujasusi wa Vladmir Putin ndiyo umeifanya Urusi kufika hapo ilipofika leo, Labda ngoja nikukumbushe.
Iko hivi.........
Urusi mwaka 1982 mpaka mwaka 1984 wakati ile iliyoitwa Soviet Union ikielekea kuanguka Urusi iliwahi kutawaliwa na raisi aliyeitwa Yuri Andropov ambaye huyu bwana alikuwa bosi wa KGB kwa miaka 15 lakini bado hali ya nchi ilikuwa mbaya sana hasa kwenye mtikisiko wa kusambaratika na Uchumi.
Mathalani, George Bush alishawahi kuwa Jasusi mkubwa (Mkurugenzi Mkuu) katika idara ya CIA lakini alitawala kwa miaka 4 na utawala wake una historia ya kuwa na sera mbovu sana nchini humo kuwahi kutokea.
Deng Xiaoping hana historia yoyote ya Ujasusi lakini utawala wake wa mwaka 1978-1989 ndiyo umeifanya nchi ya Uchina kuwa imara hivi ilivyo leo kwa...
-Mfumo Imara wa Soko la kimataifa,
-Mfumo Imara wa kiuchumi,
-Mfumo Imara wa Siasa ya Chama Kimoja,
-Mfumo Imara na mitaala bora kabisa ya Elimu na
-Mifumo Imara ya Kiulinzi na Usalama (Kuanzia Ujasusi, Ulinzi wa mipaka, Ulinzi wa tamaduni na Udhibiti mzuri wa mali za Umma)
Japo Majasusi wengi wana nafasi kubwa ya kuwa viongozi wazuri kwenye nchi endapo tu akiwa na kipawa na vinasaba vya Uongozi thabiti.
Sasa turudi Urusi kuangazia Chimbuko la Mgogoro Wenyewe........
Uongozi wa Vladmir Putin umekuwa na mafanikio makubwa sana na wenye urahisi kwasababu ya mifumo iliyojengwa na watawala wa Urusi kabla yake, Kwenye suala zima la Sayansi na Teknolojia Putin amekuta Urusi imeendelea sana, yeye kazi yake ilikuwa ni kusimamia na kuendeleza kwa uthabiti.
Makampuni karibia yote makubwa ya Urusi Vladmir Putin ameyakuta yameshaanzishwa, mfano mzuri ni,
- Gazprom (Kampuni kubwa ya gesi Urusi) imeanzishwa mwaka 1989 kwenye utawala wa Mikhail Gorbachev.
- Rosneft (Kampuni ya mafuta) imeanzishwa mwaka 1993 kwenye utawala wa Boris Yeltsin.
- Ularvagonzavod UVZ (Kampuni ya mashine na silaha) imeanzishwa mwaka 1936 na Joseph Stalin.
- Tupolev TU (Kampuni ya ndege) imeanzishwa mwaka 1922 kipindi cha Utawala ya Vladmir Lenin.
- JSC Kalashnikov Concern (Kampuni ya silaha) imeanzishwa mwaka 1807 na mfalme Alexander.
Hapa nadhani unanielewa sasa....
Namaanisha hivi......
Kuwa ukimsoma mwandishi maarufu duniani Milan Kundera kwenye Riwaya yake ya "IGNORANCE" anasema kwamba Urusi ni tofauti sana na mataifa ya kifashisti kwasababu mafanikio yake yameunganishwa na tamaduni yao, dini zao na historia yao, Hivyo tofauti na Ujerumani, Italia au Japan ambapo Ufashisti ulikufa mara tu baada ya viongozi kama Adolf Hitler, Benitho Mussolini na Hedaki Tojo kufariki.
Mfano mwingine hai kabisa ni nchi ya Marekani, ambapo Maraisi wengi wamefanikiwa kutokana na mifumo ambayo ilijengwa hata kabla wao hawajazaliwa au kuwepo Madarakani, Mfano Ronald Reagan ndiye raisi aliyefanikiwa sana kwenye historia ya Marekani tangu Vita ya Pili ya dunia kuisha mwaka 1945, Lakini vitu vyote vizuri alivikuta vimeshajengwa muda mrefu sana na yeye kazi yake ikawa ni kusimamia kwa kupitia sera yake ya "REAGANOMICS", mfano mzuri tu ni hasa...
1. C.I.A ilikuwa na nguvu sana kipindi cha Ronald Reagan lakini ilianzishwa mwaka 1947 na raisi Harry S Truman.
2. Mifumo bora kabisa ya Kiutawala hapa duniani (Demokrasia, Utawala wa Katiba na sheria, Uhuru wa mahakama na mgawanyo wa madaraka) alivikuta vimeanzishwa na wakina George Washington, Thomas Jefferson, James Monroe, John Adams na Benjamin Franklin kuanzia mwaka 1776 wanapata uhuru hadi mwaka 1787 wanaandika katiba na mwaka 1789 wanaanzisha Jamuhuri.
3. Nguvu kubwa ya kijeshi (Military Industrial Complex) imeanza kipindi cha utawala wa Franklin Delano Roosevelt 1933 mpaka mwaka 1945 na kuendelea na Harry S Truman mpaka leo.
4. Mifumo na Mitaala bora kabisa ya Elimu ameikuta (Vyuo kama Harvard, Yale na Stanford vilikuwepo) alichofanya ni kuboresha tu, ikumbukwe kuwa Mwaka 1985 Marekani na Japan waliiga mtaala wa Elimu wa nchi ya Urusi ya Kisovieti na kuuboresha kuweza kukidhi mahitaji ya nchi zao.
Sasa hili linalotokea sasa la Urusi kuiadabisha NATO inatokana na uzembe wa mataifa ya Magharibi yenyewe ndiyo yameifanya Urusi kurudi kwa nguvu, na kutafuta enzi yake upya.
Hii imetokeaje? OK imetokea hivi......
Wakati Urusi inakaribia kuanguka miaka ya themanini mwishoni na tisini mwanzoni kulikuwa na makubaliano baina ya Serikali ya Mikhaili Gorbachev na George Bush kwamba Urusi ingesitisha vita na kuzipa Uhuru nchi kama Poland, Latvia, Estonia, Ukraine na zinginezo ambazo zingependa kujitoa kwenye Jamhuri ya Kisovyeti, Lakini haya yangefanyika tu endapo umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi NATO hautajitanua tu hata kwa Inchi moja wala Sentimeta moja kuelekea Ulaya Mashariki kwenye nchi ambazo bado zina maslahi na Urusi.
Kwa bahati zaidi Mikhaili Gorbachev kwa kipindi hicho alikuwa akihudhuria kwenye vikao vya G7 mnamo siku za mwisho za Jamhuri ya Kisovieti na alikuwa akiomba mkopo kwa mataifa hayo ili kunusuru uchumi wa Urusi, lakini tofauti na Ufaransa hakuna taifa lililokubali kumpa mkopo wakati tayari alikuwa ameshakubali kufanya matakwa yao ya kuiuganisha Ujerumani kwa Kuvunja Ukuta wa Berlin.
Utawala wa William Jefferson Clinton (Bill Clinton) ulikiuka masharti na kuamua kufanya ubabe kwa kuanza kuitanua NATO kwa kasi kuielekea nchi ya Urusi ambayo ilikuwa imeshakubali kuweka silaha chini na kutafuta amani.
Unakumbuka walivyoanza kuilipua Yugoslavia ambayo kwenye Historia Warusi wanaichukulia SLAVS kama ndugu zao wa damu, na ikumbukwe kwamba chanzo cha vita ya kwanza ya dunia ni pale ambapo Urusi hakukubali kuona Ujerumani na AUSTRIA-HUNGARY wanaipa masharti nchi ya Serbia.
Ambapo mwaka 1914 Austria ilivyoitangazia vita Serbia kwa kushindwa kuwapelekea wauaji wa Arch-Duke Ferdinand basi Urusi chini ya Mfalme Nicholas Ramanov waliitangazia vita Austria na yakatoe yaliyotokea mpaka mwaka 1917, vita ilipo koma.
Lakini William Jefferson Clinton na Madeline Albright waliipuuza hii historia na kuanza kuvunja makubaliano waliyowahi kufanya na Gorbachev kwenye "mkataba wa Minsk".
Mwaka 1999 nchi za Czech, Poland na Hungary zikajiunga na NATO kuwa wanachama waangalizi, na watu wengi walililamika sana akiwemo Gorbachev na Boris Yeltsin lakini Marekami wakawapuuza, Warusi walichukulia hili kama Usaliti hasahasa pale ambapo NATO miaka ya 1990's ikiongozwa na Marekani iliamua kufanya uvamizi dhidi ya Jamhuri za Yugoslavia na kuanza kuilipua Kosovo ambayo ni sehemu yenye maslahi makubwa na Urusi pia ndiyo sehemu iliyomfanya Mrusi aingie kwenye Vita ya Kwanza ya dunia mwaka 1914.
Hili jambo la Marekani kuingia Kosovo lililalamikiwa sana na Urusi hadi kijarida cha National Interest walilaani kwa kusema kwamba haya yalikuwa ni makosa ya kiufundi kwa Utawala wa William, unaweza kujisomea mwenyewe hapa "How Bill Clinton Made America More Ambitious—and Dangerous"
George Bush Mdogo naye akaendelea kufanya ujinga, kaitoa Marekani kwenye mkataba wa ABM (Anti-Ballistic Missile Treaty 1972) na kuamua kutengeneza makombora ya masafa Marefu, Walipoulizwa na Urusi kuhusu hili wakasema na nyinyi tengenezeni kama mnaweza sisi hatuna tatizo.
Mwaka 2000 PENTAGON ilipeleka ripoti ya Uchambuzi wa Ulinzi kwa raisi George Bush kwamba serikali ya Urusi hasa jeshi lake lipo hoi, Nchi imechoka na rushwa, utawala mbovu, vita ya Chechenya na Ugaidi, Kama ikiendelea hivyo basi kufika mwaka 2004 Jeshi la Urusi na nchi inaweza isiwepo kabisa hapa duniani kwasababu itakuwa imeshasambaratika zaidi.
Serikali ya Marekani wakiongozwa na Media zao wakayaamini haya na kuanza kujifanyia wanayotaka, Nyuma ya pazia Warusi wakaanza kujipanga na kuungana hasa hasa baada ya kujua kwamba Marekani anataka kuwafutilia mbali ya uso wa dunia.
George Bush baada ya kuona Urusi imeanza kuwa na nguvu, Vita za Afghanistani na Iraq zimeenda vibaya na wakati huo huo Uchina anachuana naye sana kibiashara akachanganyikiwa hadi mwaka 2004 bila hata kufikiria madhara yake, akaamua kuziingiza nchi saba zilizo jirani na Urusi kwenye Umoja wa kujihami wa NATO.
Marekani akavuta mipaka zaidi baada ya kusogea karibu kabisa na Urusi kupitia Georgia mwaka 2008 na tunakumbuka wote nini ambacho Vladmir Putin alimfanya Mikhail Sakhasvilli ambaye alikuwa raisi wa Georgia.
Mjaluo wetu Barack Obama huyo naye akaingia kichwa kichwa huko Ukraine na Syria sehemu zenye maslahi makubwa ya Urusi, Kumbe hakujua kwamba anazidi kuwafanya Warusi wapate sababu ya kujijenga kijeshi mpaka leo hii Marekani inapigwa mikwara na Kremlin.
Ni kweli Urusi siyo taifa kubwa hapa duniani kiuchumi, lakini kafanyia kazi makosa yake, Henry Kissinger aliwahi kusema kama Marekani itataka kumshinda Uchina basi ni lazima iunde urafiki na Urusi, na hii ndiyo njia pekee (Hakuna njia mbadala), Hii inamaanisha hata Ujuio na zile sera za Donald Trump ni mipango ya wakubwa hapa duniani, maana ukiona mtu kama Henry Kissinger anasema Trump anaweza kuijenga Marekani basi Ujue la mgambo limelia, lakini tayari walikuwa wamesha chelewa Putin alihakikisha Trump apiti.
Hivyo Vladmir Putin kufika hapa alipo pia ni Ujinga wa mataifa ya Ulaya umechangia kwa kiasi kikubwa na kusababisha Warusi wamuunge mkono Putin na kuona kama ni mwokozi wao kwa wakati kama huu.
Sasa basi........
Marekani anazidi kumfanya Vladmir Putin na Urusi wawe na nguvu ya zaidi ya hapa walipo kwasababu hana jinsi nyingine ya kumshinda Mchina isipokuwa kupitia ushawishi wa Urusi tu.
Hii sera kwenye Sayansi ya Siasa inaitwa "Divide et Impera" ambapo taifa moja linawagawa mataifa mawili au zaidi na kusababisha chuki baina yao ili liwatawale vizuri, Imetumika sana hii sera hapa duniani hasa hasa kwetu Afrika kipindi cha Ukoloni au Ujerumani mwenyewe aliitumia hii sera sana kipindi cha Chancellor Otto Von Bismarck ambapo mataifa mengi yalipandikiziwa chuki ili yatawaliwe kirahisi na nchi ya Prussia ambayo ilikuja kuwa Ujerumani.
Kibaya zaidi hii sera Henry Kissinger mwenyewe aliitumia kuwafarakanisha Warusi na Wachina kipindi cha Vita Baridi na bila Warusi kufikiria vizuri wakaingia mkenge na mwishowe sera ikazaa matunda mazuri sana, ikumbukwe kuwa Mwaka 1960's Urusi alianza kuzozana na Uchina na hatimaye mwaka 1969 serikali ya Leonid Brezhnev alifikiri hadi kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Uchina, ambapo aliwauliza Wamarekani ambao walikuwa hawampendi Mchina kwamba tukimpiga Uchina ninyi msiingilie.
Wamarekani wakakataa na kuamua kutumia mwanya kumvuta Uchina Upande wake ili kumzorotesha Urusi na Mwishowe kikatokea kitu kilichokuja kuitwa "SINO-SOVIET SPLIT".
Mwaka 1972 raisi Richard Nixon akaenda hadi Uchina kutembelea Great Wall (ukuta mkuu wa China) ambapo alifanya kikao na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Zhou Enlai pamoja na baadae raisi wa nchi hiyo Mao Zedong.
Walikubaliana kuanza mikataba ya kibiashara na kufungua masoko yote hii kumkomoa Urusi, hii ndio inaitwa divide et Impera, nadhani sasa unaanza kuelewa mgogoro huu ulipotokea.
Lakini pia......
Ikumbukwe kipindi hiki sera maarufu ya Uchina moja ( ONE CHINA POLICY) ndiyo ilizaliwa, Nataka uone namna Marekani ilivyotumia Sera ya divide et Impera, Ili kumkomoa Urusi serikali ya Marekani ikaamua kutambua kwamba Taiwan ni jimbo halali la Uchina japo linajitawala lenyewe.
Ukikumbuka vizuri mwaka huo huo Uchina ilikuwa haina kiti katika baraza la Ulinzi na Usalama la Umoja wa mataifa na hivyo Taiwan ndiyo ilikalia hicho kiti pamoja na kupewa kura ya VETO, Lakini mwaka huo kwa mara ya kwanza serikali ya Marekani ikaitambua serikali ya Kikomunisti ya Uchina kama Serikali halali ya nchi hiyo.
Ghafla mwaka huo huo Uchina ikarudishwa kwenye Baraza la Ulinzi la Umoja wa Mataifa na kupewa kura ya VETO huku Taiwan ikitolewa, Marekani kamfungulia Masoko Uchina na kuanza kuwasomesha Wachina bure huku Wachina wakianza kukua kwa haraka sana kiuchumi.
Matokea ya hii sera Uchina akaanza kupingana na Urusi sehemu nyingi hapa duniani hadi kupelekea ushawishi wa Urusi kupungua kwa kasi hasa barani Afrika kuanzia miaka ya 1970.
Mfano mzuri Uchina alimuunga mkono Muingereza nchini Angola dhidi ya taifa la Urusi na Cuba, kwenye kuvamia Afghanistani Wachina walikuwa upande wa Marekani kinyume kabisa na Urusi tofauti na ilivyokuwa kwenye vita ya Vietnam hivyo kupelekea Urusi kushindwa kujitanua kwa kasi, Mwisho wa haya ni kwamba Urusi ilididimia hadi kufika mwaka 1991 huku Uchina ikikua kwa haraka sana.
Sasa Marekani amekuwa mkubwa na Ukomunisti na Jamhuri ya Kisovieti haipo, adui mkubwa kwa Uchumi wa Marekani akageuka kuwa ni Uchina, hivyo basi kipindi hiki Henry Kissinger na wataalamu wengine wakapendekeza kwamba Watumia sera hiyo hiyo ya Divide et Impera na kutengeneza THE SECOND SINO-SOVIET SPLIT.
Matokeo yake ni kwamba Urusi lazima itakuwa na nguvu sana kwasababu Marekani hatampinga sana kwasababu Muungano wa Uchina na Urusi kutokea mwaka 2014-2016 umeleta madhara makubwa kwa Marekani hivyo ni bora hawa wasiwe wote.
Ndio maana kipindi cha utawala wa Donald Trump aliwachukia sana Wachina na Kuwakumbatia Warusi, yote hii ni mikakati kwasababu yeye aliamini kuwa Wamarekani huwa wanafanya sana hesabu ya hatua zao hata kama ni za hovyo.
Putin alilijua hilo mapema ndio maana akawekeza nguvu kuifanya Urusi wazidi kuwa na nguvu sana, na pia kuhakikisha Putin anacheza karata yake vizuri ndio maana sasahivi anatumia akili sana kuliko nguvu kwanza.
Mpaka sasa Urusi hana cha kupoteza kabisa kwasababu mataifa yote ulaya umtegemea pakubwa, hii ni kwasababu 43% ya gesi yote ulaya inatokea Urusi, huku 20% ya technology ya silaha nzito kutia ndani mabomu ya nyukria duniani inamilikiwa na Urusi, hivyo kwa vyovyote vile Marekani na Ulaya wanahitaji Ushawishi wa Moscow katika kutafuta ustawi na amani ya ulaya.
Kwa mantiki hii Sasa.....
Ni kwamba Unaweza kuona ni Kwanini Urusi Kaamua kuingia kwenye vita ya akili na ulaya na Marekani huku ikienda mbele zaidi kuingia kwenye vita ya kimkakati na Ukraine, sababu kubwa ni NATO kukiuka mashariti ya mkataba wa Minsk "Minsk agreement" kwa mataifa ya Marekani kujitanua kwa kuidhibiti Urusi.
Kinachofanyika sasa ni Urusi kuzuia yale mataifa yake ya zamani (USSR) kutokujiunga na NATO, maana Urusi anaamini kwamba kitendo cha Ukraine kujiunga na NATO ni kuwasogeza Maadui mlangoni, hivyo Putin anazuia makosa yaliyofanyika awali mpaka kupelekea kuvunjika kwa Soviet Union yasijirudie tena.
Ndio maana Moscow haiko Tayari kuona maeneo ya mipaka yake na nchi za ulaya kati haipotezi ushawishi wake, kwa kutambua hilo ndio maana kaamua kuzuia NATO kujipenyeza kwenye mataifa yote ya Ukraine, Lithuania, Belarus na ukanda mzima wa Urusi magharibi.
Hata hivyo mpaka sasa Urusi imeshawekewa vikwazo na mataifa kazaa duniani ikiwemo Ujerumani ambayo tayari imesha tangaza kusitisha mpango wake wa bomba la gesi na Urusi, "Nord Stream 2"
Pia Marekani wametangaza vikwazo kwanza kwa miji ya Donesk na Luhansk na kwa Urusi, vikwazo hivyo zimewekewa Benki mbili za urusi ambazo zinafanya biashara za kifedha Marekani.
Pia Canada imeiwekea vikwazo Urusi na meeneo ya Donbass, pamoja na katazo la wakanada kufanya miamala na donesk na luhansk, na katazo la kununua Russian sovereign debt bonds kwenye mabenk mawili yanayomilikiwa na serikali ya Urusi.
Kwa Japan imeiwekea vikwazo Urusi ikifuata nyayo za Marekani na washirika wake, Japan inasema vikwazo ni pamoja na kupiga marufuku bima ya mipaka ya Urusi nchini Japani na kufungia mali za watu wa Urusi, hii Inamaana kuwa Japan Wametaifisha mali za Maafisa kadhaa wa Urusi Pia wamewakataza maafisa wa juu wa Urusi kusafiri kwenda Japan.
Kwa Australia wao wamewawekea watu 8 wa baraza la usalama la Urusi vikwazo na Benki kadhaa pamoja na taasisi kadha za uchukuzi na mawasiliano.
Msimamo wa Urusi kwenye mgogoro huu na Ukraine ni kwamba, ili Ukraine iwe salama inapaswa kuachana na mpango wake wa kujiunga NATO, la sivyo Kiev itarudi Moscow.
Je nani ataibuka mshindi kwenye mgogoro huu! Ni Urusi au NATO? Ngoja tuone mwisho wake...
.
[emoji419] Kwa kupata makala Zaidi wasiliana na Mimi WhatsApp 0679555526 uungwe group la Maktaba Kuu kwa gharama ya Tsh 3000/=.
[emoji117][emoji420] Ukinakili kazi zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
[emoji2400]Wako Mjoli wa Historia na diplomasia ya ulimwengu.
Ndimi: Comred Mbwana Allyamtu
[emoji2398] Copyrights of this article reserved
[emoji2400]written by Comred Mbwana Allyamtu
•Napatika Kwa mawasliano
[emoji769]Comred Mbwana Allyamtu
Kwa Tanzania
+255679555526 (WhatsApp).
+255765026057.
Email-
mbwanaallyamtu990@gmail.com
[emoji2398] Copyright 2022, All Rights Reserved.
[emoji420]Maktaba Kuu.
View attachment 2130977View attachment 2130976View attachment 2130981View attachment 2130978View attachment 2130979View attachment 2130982View attachment 2130980View attachment 2130983