Serikali yapiga marufuku masomo ya ziada
Bongo5Jun 22, 2021Soma halisi
Serikali imepiga marufuku masomo ya ziada kwa shule za Serikali na hasa wakati wa likizo, kwa kubainisha kuwa yanaongeza gharama zisizo za lazima kwa wazazi na ni kinyume na waraka wa elimu namba tatu wa mwaka 2016,ambao unataka wanafunzi wapate likizo ama muda wa kupumzika.
Hayo yamesemwa bungeni na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia , Prof. Joyce Ndalichako wakati akitoa taarifa kwa mbunge wa Bukoba Vijijini Mh.Jasson Rweikiza aliyetaka ufafanuzi kwa waraka uliotolewa na kamishna kutoka Wizara ya Elimu uliotaka shule zote zifungwe wakati wa likizo.
Waziri Ndalichako amesema kuna baadhi ya shule za Serikali zinalazimisha wanafunzi na wazazi kuchangia gharama kwa kipindi chote cha likizo ambacho wao wanatumia kufundishwa.Hiyo si sawa na inakiuka lengo la Serikali la kutoa Elimu bila malipo kwa Wananchi.Na hii imekua ni uchochoro wa watu kujipatia pesa.Na hizi tozo zimekua kama gharama ya Elimu zinarudishwa kwa sura nyingine.
“Serikali imeweka mfumo wa kwenda likizo kwa sababu akili ya binadamu inachoka, siku 194 za masomo ambazo zimewekwa kwa mwanafunzi kusoma zinatosha, wanafunzi wanahitaji kupumzika, kukaa na familia zao na kufanya shughuli nyingine, mfano wanafunzi wa kidato cha nne wamefungua shule Januari 13,na wanatarajia kuanza mitihani yao ya kumaliza mwezi wa 11,ukisema mtoto asifunge shule mwezi wa sita sio sawa.Sisi kama serikali bado tunaona na tunatambua umuhimu wa likizo”amefafanua Waziri Ndalichako.
Vile vile Waziri Ndalichako amewaelekeza maafisa Elimu Wilaya na Mikoa, kuacha kupoka mamlaka ya kuweka Sera kwa kuwa Serikali imebaini maeneo mengi shule zinafungwa kwa maagizo ya Maafisa Elimu, bila ya Waziri wa Elimu wala Tamisemi kuwa na taarifa.