Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Kwa upande mwingine, shule nyingi zimekuwa zikijitangaza kwa matokeo mazuri ya mitihani, wakati suala la malezi na stadi za maisha likipewa uzito mdogo.
Stadi za maisha ni uwezo wa mtoto kujitambua, kutatua matatizo binafsi, kuwasiliana kwa ufanisi, na kushirikiana na wengine katika jamii.
Utafiti unaojulikana kama Tathmini ya Stadi za Maisha na Maadili Afrika Mashariki (ALiVE) umebaini kuwa licha ya juhudi za serikali za Afrika Mashariki kufanya maboresho katika sera za elimu na mitaala, bado kuna pengo kubwa la stadi muhimu za maisha miongoni mwa vijana. Hali hii inazua wasiwasi kuhusu uwezo wa mifumo ya elimu kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za maisha halisi.
Soma: Ripoti mpya: Vijana Afrika Mashariki wana upungufu wa Stadi za maisha licha ya mabadiliko ya mitaala
Utafiti huo ulihusisha zaidi ya vijana 45,000 wenye umri kati ya miaka 13 hadi 17 kutoka Kenya, Tanzania na Uganda, ukipima ujuzi kama utatuzi wa matatizo, kujitambua, ushirikiano na heshima.
Juhudi za mashirika
Kutokana na changamoto hiyo, mashirika mbalimbali yameanzisha programu za kusaidia watoto kupata stadi za maisha. Moja ya mashirika hayo ni Sawa Wanawake Tanzania, ambalo limekuwa mstari wa mbele kuwawezesha watoto wa rika mbalimbali kupata ujuzi huo muhimu.
Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1996 na kusajiliwa mwaka 1998 chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kabla ya kusajiliwa tena mwaka 2019 chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii.
Akizungumza hivi karibuni mjini Morogoro, yalipo makao makuu ya shirika hilo, Mkurugenzi wake, Hellen Nkalang’ango, amesema lengo kuu ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu sawa bila kujali hali zao za kiuchumi.
“Tulianza kwa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata elimu. Ndipo tukaanzisha Shule ya Msingi Leena katika Manispaa ya Morogoro, inayochukua watoto wenye mahitaji maalum pamoja na wengine,” amesema.
Ameongeza kuwa baadaye walipanua wigo wa shughuli zao katika wilaya za Morogoro Manispaa, Mvomero na Iringa.
Hellen, ambaye pia ni mmoja wa waanzilishi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), amesema shule hiyo inayotumia lugha ya Kiingereza kufundishia ina wanafunzi 279, na inalenga kuwasaidia watoto kujitambua sambamba na kupata elimu ya darasani.
“Tunawachanganya wanafunzi wenye mahitaji maalum na wale wa kawaida ili kuwajengea uwezo wa kushirikiana na kujifunza kwa pamoja. Ingawa hatuna wataalamu wa kutosha, wanafunzi wenzao wanawasaidia kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Shule hiyo ilijengwa kwa msaada wa shirika la Social Teachers Association (STA) na ilianza masomo mwaka 2001, huku darasa la kwanza la saba likihitimu mwaka 2007.
Kwa mujibu wa Hellen, ufaulu wa shule hiyo ni mzuri, ambapo wanafunzi wengi hupata daraja la juu katika mitihani ya kitaifa.
Usalama wa watoto nao wapewa kipaumbele
Mbali na elimu ya darasani, shirika hilo pia linaweka mkazo katika usalama wa wanafunzi, hasa wasichana.
“Tulibaini baadhi ya watoto wa kike wanatembea umbali mrefu hadi kilometa saba au nane kwenda na kurudi shule. Hivyo, tulishirikiana na jamii kujenga hosteli,” amesema.
Hadi sasa, hosteli tano zimejengwa—nne zikiwa Wilaya ya Mvomero na moja Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Shirika hilo pia limeshirikiana na wadau mbalimbali kama ChildFund Korea pamoja na serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Kuwawezesha wazazi kuinua elimu ya watoto
Katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora ya stadi za maisha, shirika hilo pia limejikita kuwawezesha kiuchumi wazazi, hususan wanawake.
“Tumewawezesha wanawake 550 kwa kuwapa mafunzo na mitaji kupitia vikundi 19, ambapo kila kikundi kimepata Sh5 milioni tangu mwaka 2019,” amesema Hellen.
Utekelezaji kupitia jamii
Mdhibiti Ubora wa Elimu wa shirika hilo, Mahmoud Ngamange, amesema wanatekeleza programu hizo kupitia mtandao wa Regional Education and Learning Initiative (RELI).
Kwa sasa, shirika linahudumia shule 14 nchini, zikiwamo shule za Msingi Msasani, Mela na Vianzi katika Wilaya ya Mvomero, ambapo wameboresha miundombinu ya kujifunzia.
Ngamange amesema wanatumia mbinu ya kuwajengea uwezo viongozi wa jamii, ambao hueneza elimu hiyo kwa familia na jamii kupitia vikundi vya kijamii kama Vicoba.
Wasichana wanufaika zaidi
Ofisa Habari wa Sawa Wanawake, Mary Abel, amesema wanatoa mafunzo ya stadi za maisha kwa wasichana katika shule za sekondari za Wami, Mvomero na Doma.
“Tunawafundisha kujiamini, kuwasiliana, kushirikiana na kutatua matatizo yao. Mara nyingi ujuzi huu haufundishwi nyumbani wala darasani,” amesema.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yameleta mabadiliko makubwa kwa wanafunzi.
“Awali, baadhi ya watoto walikuwa hawawezi hata kujieleza. Lakini baada ya mafunzo, wana uwezo wa kujieleza, kushirikiana na wenzao na kutatua changamoto zao,” amesema.
Wazemavyo wazazi
Lina Chuma - mkazi wa Wami Dakawa wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro.
Mathayo Chimanyi - Mwenyekiti wa kamati ya Shule ya Msingi Msasani Wami Dakawa- Mvomero.