USIFE KWANZA MPENZI WANGU....
EPISODE.5.
“Samahani Deo, naweza kupata namba zako za simu?” Levina akamwuliza.
“Simu?”.
“Ndiyo!”
“Mimi sina, labda nikupe namba za nyumbani!”
“Hapana, nataka namba zako mwenyewe!”
“Sina.”
“Kwanini?”
“Maisha Levina!”
“Ok! basi chukua zangu...ukimaliza kazi zako nipigie kwenye kibanda cha simu, nahitaji kuzungumza na wewe!” Levina akasema akiandika namba na kumkabidhi Deo akiambatanisha na noti ya elfu tano.
“Ahsante sana Levina, nitakupigia!”
“Usiache tafadhali, ni muhimu sana!”
“Sawa.”
ANZA SASA KUISOMA....
DEO alibaki na maswali mengi sana kichwani mwake bila kuwa na majibu, bado kitu kikubwa kilichokuwa kinamsumbua ni kwamba, ni kweli hisia zake zilikuwa sawa kwamba Levina alikuwa anampenda au zilikuwa hisia zake mwenyewe?
Hakujua hakika!
Lilikuwa suala gumu sana kichwani mwake kupitishwa moja kwa moja kuwa Levina alikuwa anampenda, hata hivyo ndani ya moyo wake alijua wazi kuwa kabisa yeye alimpenda sana Levina.
“Nitampataje jamani huyu msichana? Nahisi kabisa moyo wangu unaniambia kuna kitu fulani, ni kweli nampenda sana Levina,” akawaza Deo.
Siku nzima alishinda akiwa na mawazo, alitamani sana kumpigia simu Levina ili amsikilize alichokuwa akitaka kumwambia, lakini kwa sababu alikuwa na wateja wengi alishindwa kufanya hivyo,
lakini kubwa zaidi kelele za pale sokoni zilimfanya ashindwe kumpigia kwakuwa alifahamu kwamba hawataweza kuelewana vyema!
Jioni alifunga biashara yake na kuanza kurudi zake nyumbani, kwakuwa alipewa pesa na Levina na pia alikuwa na haraka ya kuwahi kumpigia simu, akaona bora apande daladala.
Akachepuka kutoka sokoni Tandale hadi Manzese ya Agerntina, pale akapanda daladala iliyompeleka mpaka Magomeni ya Mwembechai, akashuka na kutafuta kibanda cha simu..
“Habari yako dada?” Deo akamsalimia mhudumu wa kibanda cha simu.
“Salama, karibu kaka’ngu!”
“Nahitaji kupiga simu.”
“Sawa, naomba namba.”
Deo akamtajia.
Yule dada akabonyeza zile namba kwenye simu, kisha akaweka saa yake ya kuhesabu muda tayari na kumpatia Deo simu.
“Hallow,” sauti laini ya kike ilisikika upande wa pili, baada ya kupokelewa.
“Hallow, habari yako?”
“Nzuri, bila shaka ni Deo?”
“Umejuaje?”
“Kwanza sauti yako, lakini pia wengi wanaonipigia simu namba zao nimezi-save!”
“Niambie Levina.”
“Poa!”
“Nimekupigia kama ulivyoniambia.”
“Hujakosea kitu Deo, tena umefanya vizuri sana, maana nilikuwa nawaza namna ya kukupata kama usingenipigia.”
“Sawa...sawa...nini kipya?” Deo akauliza.
Kimsingi hakuonekana kuwa na jambo lolote la kuzungumza zaidi ya kusubiri kumsikiliza Levina.
“Sikia Deo, kuna kitu cha muhimu sana nilitaka kuzungumza na wewe, lakini naona kama mazingira hayafanani kabisa.”
“Kivipi?”
“Nahisi upo kwenye kelele sana, kiasi kwamba hata hutakuwa na usikilizaji na uelewa mzuri wa nitakayokuambia.”
“Kwani unataka kuniambia nini?”
“Subiri Deo, usiwe na haraka kiasi hicho, huwezi kupata muda nikazungumza na wewe nje ya kazini kwako?”
“Kama lini?”
“Wewe off yako ni lini?”
“Jumapili, ingawa si mapumziko ya moja kwa moja!”
“Kivipi?”
“Huwa siendi sokoni, lakini kazi nyingine za nyumbani zinaendelea kama kawaida.”
“Sasa?”
“Naweza kujaribu kutoka mara moja, lini unataka tuonane?”
“Itakuwa Jumapili, lakini kesho nitakuja tena kuzungumza na wewe zaidi!”
“Sawa.”
“Haya usiku mwema mwaya Deo!”
“Ahsante,nawe pia ulale salama.”
Wakakata simu zao.
Deo akalipa na kuanza kutembea kwa miguu akienda Mburahati, nyumbani kwa bosi wake. Ndani ya moyo wake alijihakikishia kumpenda Levina, lakini ufukara wake ulimfanya ashindwe kuelewa namna ambavyo angeweza kumfanya Levina awe wake.
Alifika nyumbani nusu baadaye, kwanza alikabidhi mahesabu, akaingia bafuni kuoga. Aliporudi alifikia mezani kupata chakula cha usiku, kabla ya kwenda jikoni kuanza kazi ya kufunga mifuko ya barafu kama ilivyo kawaida yake.
***
Kama ni mateka, alikuwa mateka asiye na hali, ambaye pamoja na kutekwa kwenyewe, alikuwa tayari kufanywa mateka. Levina alijishangaa sana jinsi alivyotokea kumpenda Deo.
Hakika hakuwa hadhi ya mwanaume wa kuwa naye, uwezo wao kifamilia, heshima waliyonayo wazazi wake ni kati ya mambo ambayo yalimchanganya sana na kumfanya ashindwe kuwa na maamuzi ya moja kwa moja ya nini cha kufanya kwa ajili ya Deo.
Pamoja na yote hayo, moyo wake ulikuwa na kitu kimoja tu...
Mapenzi!
Alimpenda sana Deo, lakini alikuwa na changamoto nyingi sana kichwani mwake.
Kwanza aliwaza juu ya wazazi wake...hakujua kama wangekubaliana na wazo lake la kuolewa na Deo, kijana fukara ambaye hana mbele wala nyuma.
Hilo lilimchanganya sana kichwa chake, lakini alijipa moyo kwamba siku moja lazima Deo angekuwa mikononi mwake, yeye akiwa mama na Deo akiwa baba.
“Hilo nitahakikisha nalitimiza, maadamu nimempenda, hayo mengine nitajua baadaye!” Akawaza Levina.
***
“Mambo Deo,” alikuwa ni Levina akimsalimia Deo, asubuhi ya siku iliyofuata alipokwenda sokoni.
“Poa, za nyumbani?”
“Salama.”
“Kilo ngapi?”
“Hapana, leo sihitaji mchele, nimekuletea zawadi yako,” akasema Levina akimkabidhi bahasha ya khaki.
Deo akapokea...
“Hiyo ni simu Deo, imebidi nikununulie ili kurahisha mawasiliano yetu.”
“Mh! Ahsante sana jamani, lakini kwanini umeamua kufanya hivi?”
“Kwa sababu sisi ni marafiki, unajua tunatakiwa kudumisha urafiki wetu kwa kuwasiliana mara kwa mara, au wewe hupendi tukiwa marafiki?”
“Napenda sana, nashukuru sana!”
“Usijali, line imo humo humo ndani, tayari nimeshakuwekea vocha za elfu ishirini, zikiisha nijulishe nikuongeze nyingine.”
“Ahsante sana,” Deo akashukuru tena.
Haikuwa rahisi kuamini jambo hilo, zawadi ile kwa Deo ilikuwa zaidi ya zawadi,ule ulikuwa uthibitisho tosha kwamba Levina alikuwa anampenda.
Levina hakukaa muda mrefu sana, akaaga na kuondoka.
***
Siku zilivyozidi kwenda na kuwasiliana, mapenzi kati ya wawili hawa yalizidi kuchipuka kwa kasi, lakini si Deo wala Levina aliyekuwa tayari kueleza hisia zilizokuwa ndani ya moyo wake.
Wote waliishi na siri nzito za mapenzi ndani ya nafsi zao, lakini leo Levina amepata wazo la kufanya ili aweze kumnasa Deo.
Alitumia kila njia kumuonesha kwamba anampenda na alichokuwa akikisubiri siku zote ni Deo kumtamkia kwamba anampenda, lakini hilo halikutokea.
Deo naye alishangazwa na jinsi Levina alivyopenda kuwa naye karibu na kumsaidia mambo mbalimbali, lakini aliogopa kumwambia kwamba anampenda, akihofia kupoteza urafiki wao ambao kwake ulikuwa na manufaa makubwa sana.
Levina ameshapata njia za kumsogeza karibu Deo ili iwe rahisi kwake kutamka kwamba anampenda. Alipanga mpango hatari, haukuwa mwingine zaidi ya kufanya jitihada mfanyakazi wao wa kiume wa nyumbani atimuliwe ili amfanyie Deo mipango ya kupata kazi nyumbani kwao.
Hapo ndipo angempata Deo kwa urahisi zaidi, maana angekuwa anammiliki. Hilo alijihakikishia kulifanya.
Je, nini kitatokea?
Levina atafanikiwa kumpata Deo?
Usikose kufuatilia ..........