USIFE KWANZA MPENZI WANGU....EPISODE.35
Deo yupo kitandani Muhimbili, matukio yote katika maisha yake ya kimapenzi na Levina yanaonekana kama sinema. Anakumbuka siku Levina alipogundua rasmi kwamba anatoka kimapenzi na Cleopatra.
Levina akiwa mezani na mama yake wakipata chakula cha usiku, mama yake anagundua tofauti ambayo mtoto wake anayo. Anajaribu kumuuliza lakini hasemi kitu.
SASA ENDELEA...
MAMA Levina akaacha chakula na kumwangalia mwanaye vizuri machoni, ambaye alionekana wazi kuwa na jambo zito linalomsumbua. Alitaka kujua namna ambavyo angeweza kumsaidia.
“Levina, lazima uniambie ukweli!”
“Unataka ukweli gani mama?”
“Nataka kujua nini kinakusumbua, maana naona haupo sawa. Kuna jambo linakutatiza. Lazima.”
“Hapana mama.”
“Wewe ni mwanangu, nimekuzaa na kukulea mwenyewe, sijasaidiwa na mtu, hivyo nakujua ulivyo. Hapo una tatizo lakini hutaki kusema. Hebu kuwa wazi, mama una nini?”
“Nothing mom, niamini.”
“Wewe utakuwa na mimba!”
“Mama!”
“Mama what? You must have a pregnant!”
“Hapana mama, sina mimba. Kwa nini unanifikiria hivyo?”
“Sasa nifikirie nini?”
“Mama ni kweli nina tatizo, lakini si mimba.”
“Ok! Niambie, ni nini kinakusumbua?”
“Ni Deo mama.”
“Deo? Tena?!”
“Mama nampenda, lazima niwe mkweli bado niliendelea kuwa na uhusiano naye na nilimsaidia sana lakini sasa hivi amenisaliti mama, anatoka na bosi wake ambaye ni rafiki yangu!” Levina akasema kwa uchungu sana akikaribia kudondosha machozi.
Mama yake akaumia sana, moyo wake ukaingiwa na ganzi, pamoja na kwamba mwanaye alimuudhi kwa kukaidi maagizo yao lakini bado aliona ana kila sababu kama mama kumsaidia mwanaye katika hali aliyokuwa nayo.
“Lakini mwanangu, kumbuka kwamba hapa tunatakiwa kujadili kuhusu wewe na siyo huyo Deo tena.”
“Kivipi mama?”
“Wewe unazungumzia juu ya mwanaume unayempenda lakini yeye hakupendi, unajua kama ingekuwa ni kesi ya wewe kumpenda na yeye kukupenda, yaani mkapendana, halafu kukawa na tatizo fulani, basi ingekuwa rahisi lakini hapa ni kinyume chake.
“Kifupi Levina binti yangu unatakiwa kufahamu kwamba huyo mwanaume hana mapenzi na wewe, huna haja ya kuendelea kumuweka moyoni mtu ambaye hakupendi. Najua ni kiasi gani unateseka na kuumia. Najua kwa sababu hata mimi nimepita huko lakini huyo Deo si mwanaume sahihi kwako!” Mama yake aliongea kwa sauti ya chini sana akihitaji usikivu wa mwanaye.
“Kweli mama?”
“Ndiyo hivyo mwanangu, si mwanaume atakayeweza kuyashika maisha yako sawasawa, bado una muda wa kusubiri mwanangu!”
“Mama!” Levina akaita.
“Mwanangu!”
“Nitajua mwenyewe cha kufanya!”
“Angalia isiwe kuwa na madhara kwako lakini!”
“Nipo makini kwa kila ninachokifanya mama. Naamini unanifahamu nilivyo, nakupenda na sitakwenda kinyume!”
“Nenda kapumzike mwanangu, kabla hujalala hakikisha unasali. Tuliza kichwa chako mwanangu, usiwe na mawazo sana!”
“Nimekuelewa mama, nakupenda sana.”
“Nakupenda pia binti yangu.”
Levina akaondoka na kwenda chumbani kwake kulala, kichwa chake kilikuwa kizito kuliko kawaida.
***
Deo alikuwa mezani kwake, akiendelea na kazi kama kawaida, simu yake ikaanza kuita, alipoangalia kwenye kioo cha simu, akagundua ni Levina ndiye alikuwa akimpigia. Deo akashtuka sana!
Ilikuwa ni wiki mbili baada ya Levina kumfuma akiwa na Cleopatra nyumbani kwake, ni siku hiyo ndiyo aliyoamua kuweka ukweli hadharani kwamba yupo na Cleopatra kimapenzi. Pamoja na ujeuri na maneno makali, dhamira iliendelea kumsuta Deo kwa kitendo alichomfanyia Levina.
Hakumtendea sawa, hilo hata moyo wake ulimdhibitishia. Aliiangalia ile simu ikiendelea kuita kwa muda mrefu bila kupokea.
“Nitamwambia nini?” Akawaza akiangalia simu iliyoanza kuita tena kwa mara ya pili.
Levina alikuwa msaada mkubwa katika maisha yake, ni yeye ndiye aliyemtoa kwenye dhiki na shida. Aliyemsomesha na kumtafutia kazi. Kwa hakika hakupaswa kumtenda. Alijishauri sana lakini mwisho wake akaamua kupoikea...
“Haloo!” Sauti ya Deo ilisikika ikionekana dhahiri kuwa na woga ndani yake.
“Deo!”
“Yes!”
“Kwa nini umenitenda hivyo? Kwa nini lakini Deo? Ni kweli nastahili kufanyiwa yote hayo? Wema wangu wote kwako, malipo yake ndiyo haya?”
“Najua nimekukosea Levina, tena nimekosea sana lakini unatakiwa kufahamu kwamba, sikufanya hayo kwa makusudi Levina.”
“Unamaanisha nini unaposema hukukusudia?”
“Namaanisha kwamba hayakuwa makusudi yangu mpenzi.”
“Kumbe ni nani amefanya hayo.”
“Ni mimi lakini kwa shinikizo.”
“Shinikizo la nani?”
“Cleopatra.”
“Kwa hiyo huyo Cleopatra ndiyo amebeba moyo wako, yeye ndiye anakuamulia mambo yako?”
“Sina maana hiyo lakini nilihofia kupoteza kazi.”
“Lakini hiyo kazi si mimi ndiye niliyekutafutia? Kwani ningeshindwa vipi kukutafutia nyingine ili uendelee kuwa wangu?”
“Lakini nilijua kabisa hizo fedha zako za mawazo, mwisho wake ungekuwa mbaya. Levina hata kama umenisaidia unanisimanga sana, bila shaka ungeendelea kunisimanga haya ningekuoa. Kifupi nimeamua kuwa na Cleopatra, haya ni maamuzi yangu na moyo wangu, hayawezi kubadilishwa na mtu yeyote. Nimemaliza!” Akasema Deo kwa hasira na kukata simu.
Levina alijaribu kumpigia kwa mara nyingine, akawa anaiangalia simu bila kupokea. Baadaye akaamua kuzima kabisa.
***
Macho ya Deo yalikuwa yananyemelewa na machozi, moyo wake ulikuwa unapingana kabisa na kitu kilichokuwa mbele yake. Ulikuwa unapingana kabisa na ndoa. Alihisi kumkosea sana Levina ambaye hakuwa na hatia kwa aliyofanyiwa.
Akiwa kwenye kumbukumbu za mawazo hayo, Cleopatra anatokea, tabasamu lake linayeyuka baada ya kuona wekundu katika macho ya Deo. Anakimbia haraka hadi kitandani.
“Kuna nini?” Akauliza.
“Hakuna kitu.”
“Hapana mpenzi, kwa nini unajiumiza? Dokta ameshakuruhusu, tafadhali naomba utulize moyo wako, turudi nyumbani.”
“Sawa.”
“Lakini kuna jambo moja muhimu, nimezungumza na mama kuhusu hali yako, amesema ni vizuri ukapumzike nyumbani kwanza hadi utapopata nafuu, hali yako haikuruhusu kukaa peke yako. Lazima uwe chini ya uangalizi wa karibu.”
“Sawa.”
Taratibu zote muhimu zikafanyika, Deo akaruhusiwa. Cleopatra akamshika mkono hadi kwenye gari, akamwingiza taratibu na kufunga mlango. Akaendesha gari mpaka nyumbani kwao Mikocheni.
Deo alipokelewa kwa upendo mkubwa, akafikia kwenye moja ya vyumba vya wageni. Cleopatra alikuwa na wasiwasi sana, alitamani mpenzi wake apone haraka ili waweze kupanda madhabahuni kufunga ndoa yao.
***
Mipango yote ilikuwa tayari, Deo alikuwa na hali nzuri zilibaki siku tano tu, kabla ya ndoa. Deo akiwa mwenye mawazo sana, asubuhi ya Jumatatu aliamka akiwa mchovu zaidi kuliko siku zote. Cleopatra alipokwenda kumsalimia chumbani kwake, akashangaa kumkuta Deo katika hali ile.
Hakuwa na furaha, uso wake ulionekana wazi kuwa na jambo zito sana. Cleopatra akakaa kitako kitandani na kumtulizia macho yake usoni.
“Vipi mpenzi wangu? Nahisi kama kuna tatizo.”
“Ni kweli kuna tatizo.”
“Ni nini?”
“NAJUA HUKUTARAJIA KUSIKIA MANENO HAYA, LAKINI SINA JINSI, LAZIMA NIKUAMBIE. NIMEFIKIRIA KWA MUDA MREFU SANA JUU YA NDOA YETU, NIMEAMUA TUSITISHE. SITAKI KUFUNGA NDOA TENA NA WEWE! SITAKI...” Deo akasema kwa kumaanisha.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua