SoC04 Suluhisho la tatizo la ukosefu wa ajira rasmi kwa vijana

SoC04 Suluhisho la tatizo la ukosefu wa ajira rasmi kwa vijana

Tanzania Tuitakayo competition threads

Frajoo

Member
Joined
May 28, 2024
Posts
12
Reaction score
3
SULUHISHO LA TATIZO LA UKOSEFU WA AJIRA RASMI KWA VIJANA NCHINI TANZANIA.

Ndoto ya kila mzazi au mlezi ni kuona kijana anapata ajira rasmi mara tu anapohitimu masomo yake.Huku ajira ya serikalini ndio lengo kuu.Pia inachochea maendeleo kwa taifa kuajiri vijana wenye ufahamu wa ujuzi mpya kulingana na changamoto zilizopo.

Lakini sote tunafahamu ulimwenguni kote hakuna taifa ambalo limefanikiwa asilimia mia moja kutoa nafasi za kazi kwa wananchi wote wenye ujuzi mbalimbali, hapo kuna nafasi ya sekta binafsi na ajira binafsi (Wananchi kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine pia.)

Taifa letu lina changamoto nyingi ukiacha na hili la ajira rasmi, kuna maswala kama raia wake kukosa ufahamu zaidi kuhusu ajira mbadala yaani kutokuwa tegemezi kwa ajira za serikali,pia kuna maswala ya kutofanikiwa kwenye mipango-mikakati ya kuondoa tatizo hili la ukosefu wa kazi, na kuna swala la usimamizi mbovu wa rasilimali zilizopo nchini,ambao kimsingi zingeweza kuwa mrobaini wa changamoto hii na mwisho nimeangazia swala la ubinafsi au ufisadi au kukosa hisia za kujali wengine wenye changamoto za uchumi na maswala yote hayo ni majukumu ya viongozi waliopo mada ramani na hata wastaafu kwa ushirikiano mzuri kati ya Serikali na Wananchi.

Hayati Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa aliwahi kusema kwamba Tatizo la ajira ni bomu ambalo ipo siku litalipuka na hakuna atakayeweza kulizima.Ilikua ni kama wito kwa viongozi katika kukazia fikira zao ili kutatua tatizo hili mapema.Na sasa hali iliopo ni kama bomu limeshalipuka na sioni jitihada za kulizima mapema kabla maafa zaidi kutokea.Hasa tukiangalia Uwiano kati ya wahitimu kwenye taasisi mbalimbali za elimu na idadi ya nafasi za kazi zinazotolewa.Hakika hali si shwari!

Kama mzalendo kwa nchi yangu Tanzania,ninayo maono juu ya Tanzania ninayoitaka kuiona ili nijivunie zaidi kuwa Mtanzania na kujivunia Viongozi wa taifa hili kwa ngazi zote.

Mapendekezo yangu yameegemea zaidi kwenye kutengeneza mfumo mpya wa kuwapatia vijana kazi.Ni mkakati wa dharula wenye malengo endelevu.Naona fursa kwenye rasilimali tulizonazo pamoja na utekelezaji wa dira ya taifa kwanzia kwenye Vitongoji,kata, vijiji mpaka halmashauri za jiji.

USIMAMIZI WA RASILIMALI.

Kuna vyanzo vingi vya mapato katika kila wilaya, kuna ushuru kwenye minada na masoko,vituo vya ukaguzi wa mazao na zaidi. Hapa nadhani uwepo mpango maalumu wa kusaidia vijana kupata kazi rasmi za kufanya,kwa kuwapatia mitaji yenye lengo la kuwainua wao ili na wengine pia watakaofuata.Sote tunafahamu kwamba kuna mikopo inatolewa kwenye halmashauri, lakini changamoto ni urasimu pia biashara huwa zinagoma hupelekea vikundi kukimbia pasi na kurejesha fedha.

Huu ni mpango maalumu utakao ambatana na mafunzo ya ujasiriamali kwa kila aina ya biashara.Waalimu watakua wahitimu wasio na ajira walisomea maswala hayo ya ujasiriamali,biashara,masoko na usimamizi wa fedha.Na wao watapata ujira wao.

Hii itasaidia pia vijana kuchagua kuishi maeneo waliozaliwa ambapo wanafahamika,kwakua itakua ni kigezo mojawapo ni lazima kijana atambulike kwamba ni mwenyeji kwa uthibitisho wa Serikali za mitaa, hivyo itapunguza msongamano wa watu maeneo mijini na kuacha wazee vijijini ambao kimsingi hawawezi kuleta mabadiliko chanya.

Hatua ya awali itakua vijana kusaidia utekelezaji wa majukumu kulingana na fani husika na kupitia kujitoa kwao huko ndipo watakapopata gawiwo na elimu ya uwekezaji au ubunifu,kilimo biashara na zaidi .Dhamira kuu ni kusimamia rasilimali hizo au tuseme kufanya kazi kwenye makusanyo ya ushuru na kuhamasisha wananchi kufuata taratibu za serikali kama kulipa kodi kwa wakati, kusajiri biashara Brela ili kutambulika,hapo ndugu zangu waliosoma masomo ya kodi na ushauri wa uwekezaji hawatasita kujitoa kwa taifa lao hasa wanapojua kwamba kuna gawiwo litatoka kwa asilimia kubwa kwaajili ya vijana. Kwavile ni mkakati serikali itajua namna ya kufanya kwaajili ya matumizi ya Pato hilo kwa miaka yote, yaani kama ilikua ndio fedha za barabara au chochote.

Pili kuna maeneo tumeshindwa kutumia vyema rasilimali au utajiri tulionao.Kwa mfano sekta ya utalii inakua kwa kasi na tunaona juhudi za Ndugu Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii wetu duniani kote. Wengi tukisikia utalii tunawaza Wanyama ,mlima Kilimanjaro, Zanzibar na misitu tu.Lakini tunasahau utalii wa kitamaduni .(Cultural Tourism.)Ni moja ya utambulisho wenye nguvu kwa kila taifa.Watalii wanapokuja wanatamani kuonja vyakula vyetu vya asili ,kuona namna tunaandaa vyakula,kuona na kusikia ngoma zetu pamoja na kuelewa ujumbe kwenye nyimbo zetu,ushairi wetu,ngano zetu, misemo na busara za wahenga wetu, wanapenda kuona mitindo yetu ya maisha ya kilasiku, yaani tunavyoishi na familia zetu tunavyochangamana na majirani,wanapenda kujua jinsi utamaduni wetu ulivyochanganywa na tamaduni za mataifa mengine kwasababu za kihistoria na utandawazi, wanapenda kujua tiba zetu za asili na historia za makabila yetu na mashujaa wetu.

Ikumbukwe Tanzania ina zaidi ya makabila mia moja na ishirini, na kila kabila lina utamaduni wake na lugha yake na historia tofauti na jamii nyingine.Watalii hulipia ziara za utalii wa kitamaduni si chini ya elfu hamsini kwa mtu mmoja.Na wakati mwingine ni zaidi ya hapo hasa kama watahitaji kutembelea kivutio kilichopo kwenye jamii husika ili kujifunza historia ya eneo hilo.

Mikoa ya kaskazini ilishachangamkia fursa hio na tayari kuna maendeleo yanayoonekana yaliyoletwa na utalii wa kitamaduni.

Sasa basi kila kabila likianzisha vituo vya kijamii kwaajili ya huduma hii ya utalii nadhani ni hatua kubwa, sote tunakubaliana kila kabila lina upekee wake ambao ndio bidhaa yenyewe kwenye utalii inayoleta fedha zakigeni, watalii wanahitaji kujifunza makabila mengine zaidi ya Wamasai.

Vijana wetu watapata ajira za kuongoza watalii,akina mama watapata pesa kupitia vyakula na ngoma za asili na hata babu na bibi zetu watanufaika na historia walizonazo.

Mwaka 2017 Serikali iliona fursa hii na walianza jitihada za kuhamasisha kwa Mikoa ya nyanda za juu kusini.Lakini hili jambo ni lenye tija kwa mikoa yote.Kinachohitajika ni vijana kufanya masoko kwa njia ya mtandao ili sasa vijiji vyetu viwekwe kwenye ratiba za ziara za utalii , asitokee mtu aseme kuna umbali kufika baadhi ya maeneo wakati serikali yetu imetengeneza barabara kuunganisha Mikoa yote kwa kiwango cha lami, pia sasa kuna garimoshi la Umeme kuna ndege pia hivyo sio jambo lisilowezekana .

Japo sijaelezea kwa mifano mingi kuhusu kusimamia mapato ili kuwainua vijana na kuwapa elimu ya ujasiriamali,lakini kwa viongozi hapa wanapata Mwanga juu ya kile ninachomanisha.Na hii itakua ni muunganiko wa sekta zote kwenye uitikio wa mkakati huu.(Cross Sector Collaboration.) Yaani mfano kwenye madini itafahamika kuna gawiwo la vijana kwavile utakua ni mkakati wa nchi basi zile tozo au kuanzishwa kwa mfuko maalumu kwaajili ya vijana.Fikiria fedha zinazokusanywa na askari wa barabarani kwa makosa ya madereva kukianzishwa mfuko maalumu itasaidia vijana..Tena kila kijana atasaidika kupitia taaluma aliyonayo kwaio wale wa JKT na wengine fungu Lao na mafunzo watayapata kwenye eneo husika.Kama ni mwalimu anapata gawiwo lake shule atayokuwa akijitolea sambamba na elimu ya ujasiriamali kwakuwa kimfumo anatambulika,lakini kwa kuzingatia maeneo waliozaliwa au tuseme mkoa aliozaliwa,japo tutapata wachache ambao taaluma zao hazina ofisi ndani ya mikoa waliozaliwa pia suluhisho halitakosekana.

Kuna fedha za maendeleo ya majimbo ambazo Wabunge hupewa nazo zitaingia humo kwenye mfumo kwa kipindi flani hadi pale tutapoleta mabadiliko ya kifikra kwa Wananchi juu ya swala la ajira rasmi na kiuchumi pia.Hata wahisani wetu wakijua mkakati wa nchi kwa miaka hiyo inaweza ikawa ni miaka mitano ,ni rahisi kupata misaada ya ki fedha na ujuzi kupitia international Volunteers japo tutaanza wenyewe kama taifa na utajiri wetu.Lengo lingine ni kusimamia kwa weledi rasilimali na kutekeleza majukumu ya kiuongozi na kuwapandikiza Wananchi mtazamo mpya .

Kwa kuhitimisha nadhani tatizo la ajira linahitaji suluhisho la kimkakati na maamuzi magumu ya Rais.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom