WABUNGE wa kiume wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambao bado hawajatahiriwa, wametakiwa kutekeleza zoezi hilo mapema, ili kusaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa ukimwi kwa kuwa tohara kwa wanaume ndiyo njia mojawapo ya kupunguza maambukizi mapya.
Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM), alitoa wito huo bungeni, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza bungeni na kudai kuwa, viongozi wanapaswa kuongoza kwa mifano, hivyo kabla ya kuhamasisha wananchi, ni vema zoezi hilo lianzie kwa wabunge.
Alisema iwapo wabunge watatekeleza zoezi hilo, watakuwa mfano mzuri ambao utaigwa, na kutolea mfano wa Rais Jakaya Kikwete aliyeonyesha mfano wa kupima ukimwi kwa lengo la kuhamasisha upimaji kwa hiari na kwamba zoezi hilo lilifanikiwa.
Sanjari na swali hilo, mbunge huyo pia aliitaka serikali kuwachukulia hatua kali wale wote ambao wanaambukiza virusi vya ukimwi kwa makusudi na kusababisha kuendelea kuwapo kwa maambukizi mapya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda, alitoa wito kwa wanaume wote ambao wanaguswa na kitendo hicho kufanya tohara, ili kupunguza maambukizi hayo kwa kuwa suna kwa wanaume, inasaidia kupunguza maambukizi ya ukimwi.
Kuhusu kuwachukulia hatua za kisheria wote ambao wanaambukiza virusi vya ukimwi kwa makusudi, Dk. Kigoda alisema tayari Bunge limeshapitisha sheria ambayo itawabana wanaofanya hivyo.
Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Dk. Kigoda alisema kutokana na matokeo ya tafiti zilizofanyika Afrika Kusini, Kenya na Uganda hivi karibuni, imethibitika kuwa tohara kwa wanaume inapunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya ukimwi (VVU).
Dk. Kigoda alisema kutokana na ukweli huo, serikali inaandaa mkakati maalum wa kuhamasisha tohara kwa wanaume kote nchini kwa kutumia huduma zilizopo, ikiwa ni pamoja na kutumia sehemu za huduma za afya na za kiutamaduni.
Alisema msisitizo utalenga kutahadharisha watu kuwa tohara peke yake haitoshi kudhibiti ukimwi, bali ni lazima itumike sambamba na njia nyingine ikiwamo kuacha ngono, uaminifu katika ndoa na matumizi ya mipira ya kiume (kondomu). Katika swali lake la msingi, mbunge huyo alitaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuhamasisha wanaume wengi nchini kutahiriwa ili kupunguza kasi ya kuenea kwa VVU