[wandishi Wetu]
Alifanyiwa uchunguzi wa afya majuzi, New York
Baadhi wajiuliza: Atamudu kampeni mwakani?
Profesa Semboja: Urais ni asasi, si mtu binafsi
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akiendelea kuzingatia ushauri wa wataalamu wake wa afya kuhusu kujipumzisha na kupunguziwa kazi, mjadala kuhusu afya ya kiongozi huyo umepamba moto sehemu mbalimbali nchini.
Mjadala kuhusu afya yake umezidi kutanuka kwa njia mbalimbali; huku baadhi ya wananchi wakimwna kama mtu aliyekusudia kuwavua lawama wasaidizi wake, lakini pia wengine wakihoji kuhusu ufanisi wake katika pilikapilika za Uchaguzi Mkuu wa mwakani, akitarajiwa kuwa mgombea urais kwa awamu ya pili.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, Kikwete akiwa mgombea urais wa CCM, alizunguka nchi nzima kwa kutumia gari katika kampeni ambazo ziliongezwa muda kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea mwenza wa CHADEMA, Rajabu Jumbe, na ni katika kampeni hizo Kikwete alipata misukosuko kadhaa, ikiwamo ya kuvamiwa jukwaani, jijini Mwanza na kuanguka jukwaani jijini Dar es Salaam.
Jumapili iliyopita, Oktoba 4, Kikwete aliishiwa nguvu akiwa jukwaani katika uwanja wa Nyamagana, Mwanza alikoshiriki shughuli za uchangishaji fedha katika Kanisa la AICT. Mara baada ya tukio hilo lililodumu kwa dakika kadhaa na kuzua hofu miongoni mwa wananchi walioshuhudia, Rais Kikwete alijitokeza na kuendelea na shughuli.
Alipojitokeza aliwaeleza wananchi hao kuwa nguvu imerejea, na kwamba alikuwa akipuuza ushauri wa wasaidizi wake kumtaka apumzike mara baada ya kurejea kutoka Marekani na kuahidi kuanza kuzingatia ushauri huo.
Baadaye, taarifa zilizotolewa kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu zilibainisha kuwa kuishiwa nguvu kwa Rais Kikwete kulitokana na uchovu wa safari na kwamba alisafiri kwa mwendo wa saa 19 kutoka New York, Marekani na kuwasili nchini usiku wa saa saba, na asubuhi ya siku hiyo alikwenda Arusha, kufungua mkutano wa 55 wa Chama Cha Mabunge ya Madola (CPA) na kisha kwenda Mwanza kushiriki shughuli ya Kanisa la AICT.
Hata hivyo, katika safari hizo Rais amekuwa akitumia usafiri wa ndege, na hasa kwenye safari yake ndefu iliyodumu kwa saa 19 ya kutoka New York. Mtaalamu wa masuala ya uchovu unaotokana na safari za ndege (
Jet Lag au
desynchronosis), Dk. John P. Cunha, anaeleza mambo anayoweza kukabiliwa nayo mtu aliyekabiliwa na uchovu wa aina hiyo.
Kwa mujibu wa Dk. Cunha, mtu huyo anaweza kukumbwa na hali ya wasiwasi (
anxiety), kutopata choo (
constipation), kuharisha, hali ya kuchanganyikiwa, kukaukiwa maji mwilini, kuumwa kichwa, kuwashwa, kutoka jasho, hitilafu katika mfumo wa mawasiliano mwilini na wakati mwingine kupoteza kumbukumbu, na baadhi hufikia hatua ya mapigo ya moyo kwenda katika mdundo usio wa kawaida.
Dk. Cunha kupitia mitandao mbalimbali ya kompyuta anaeleza kuwa mtu mwenye uchovu unaotokana na ndege anaweza kukabiliwa na mojawapo ya matatizo hayo kama alivyoorodhesha katika mtandao maarufu duniani wa Yahoo.
Daktari huyo anaeleza chanzo cha mtu kupata uchovu wa safari kuwa ni pamoja na mwili wake wakati fulani kushindwa kuhimili mabadiliko ya kijiografia ambayo msingi wake ni tofauti ya hali ya hewa kati ya eneo moja na jingine. Kwa mfano, tofauti ya muda na majira ya maeneo mbalimbali, ambako ndege itapita (
time zone).
Kwa mfano, msafiri wa ndege kutoka Jiji la New York, Marekani anapofika Paris Ufaransa, usiku wa manane kwa saa za Paris, mwili huendelea kubaki katika mazingira ya majira ya New York, anasema Dk. Cunha na kuongeza kuwa;
Wakati mwili wa mhusika ukipigana kuzoea hali ya hewa ya Paris, ghalfa na kwa muda fulani anaweza kujikuta katika hali ya uchovu au kuwashwa na hatimaye hali hiyo inaweza kumfikisha katika kuharisha au kutopata choo na akili huweza kuchanganyikiwa na kushindwa kutambua baadhi ya mambo yanayoendelea. Lakini wakati wote wa matukio hayo hufanyika na kutoa nafasi kwa mwili kujitahidi kumudu hali ya hewa ya eneo husika.
Anasema katika ubongo wa mwanadamu kuna kitu kinachoitwa hypothalamus ambacho hufanya kazi kama saa iliyotegwa muda, ni kitu ambacho kiko tayari kutoa taarifa za haraka sehemu mbalimbali za mwili kuhusu mambo mbalimbali kama njaa, kiu na usingizi. Kwamba mtu hujisikia njaa, kiu au usingizi baada ya hypothalamus kutimiza wajibu wake.
Mbali na jukumu hilo, hypothalamus pia huthibiti hali ya joto la mwili, msukumo wa damu na kiwango cha homoni na glukosi ndani ya mkondo wa damu, bila kusahau kuwezesha mwili kutambua nyakati mfano, asubuhi, mchana na jioni kwa njia mbalimbali, mfano kuruhusu macho kutambua giza na mwanga.
Lakini wakati mtazamo wa kitabibu ukiwa hivyo na taarifa kutoka Ikulu ikiweka bayana kuwa sasa itaanza kumpunguzia kazi Rais Kikwete, mmoja wa wasomi maarufu nchini, Profesa Haji Semboja, anasema tatizo kubwa lililojitokeza ni uhalisia kwamba urais umekuwa ukitafsiriwa kama mtu badala ya taasisi.
Kwa mujibu wa Semboja, kama urais ungekuwa ukitafasiriwa na kufanyiwa kama kazi kama taasisi ni dhahiri kuwa Rais Kikwete angekuwa na ratiba inayomtosheleza kulingana na uwezo wake kama mtu binafsi.
Urais si Kikwete binafsi, ni mfumo wa kitaasisi. Ni wazi kuwa Rais amesema yeye ndiye hakuzingatia ushauri wa wataalamu wake kutokana na kuwaondolea lawama. Ameamua kuwalinda kwa kubeba lawama, lakini ukitazama jambo hili kwa upana wake wasaidizi wake walipaswa kutambua tangu awali kuwa urais ni system nzima Ikulu hata mlinzi wa getini. Kwa hiyo, wasaidizi ndiyo wenye kuamua na si kila kitu kifanywe na Rais kama ambavyo wanasema sasa watajaribu kumpunguzia ratiba, anasema Profesa Semboja na kusisitiza kuwa;
Sidhani kama ni sahihi kukubali kuwa Rais ndiye alikataa ushauri, kwa taratibu za kimfumo Rais anapangiwa kila kitu ni kama anaamriwa hivi. Kwa tukio hili ameamua tu kuwa na nidhamu ya kuwalinda wasaidizi wake, namwombea afya njema lakini ni muhimu tuzingatie kuwa wengi walioamua kufanya kila kitu wenyewe walipata matatizo, Ikulu sasa ifanye kazi kama Ikulu.
Katika hatua nyingine, gazeti hili la Raia Mwema lilitaka kufahamu mara ya mwisho Rais Kikwete alifanyiwa uchunguzi wa afya yake lini na kama kuna utaratibu unaojulikana wa kufanyiwa uchunguzi huo. Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema ya kuwa Rais Kikwete amekuwa akifanyiwa uchunguzi wa afya yake mara kwa mara.
Mheshimwa Rais huwa anafanyiwa uchunguzi wa afya yake mara kwa mara na hata majuzi mjini New York alifanyiwa uchunguzi, alisema Salva.
Alipoulizwa Rais ana kawaida ya kusafiri kwa ndege yake (
Gulf Stream) au ya mashirika ya biashara kwenda na kurejea kutoka Marekani, safari iliyodumu kwa saa 19 na kumsababishia uchovu mkubwa, alijibu kwamba haoni uhusiano wa ndege aliyotumia na tukio la Mwanza. Hata hivyo, wataalamu wa safari za anga wanasema kwamba, ili usichoke sana, safari ndefu kiasi hicho huhitaji ndege kubwa zenye nafasi kubwa inayomwezesha abiria kulala vizuri.
Kuhusu suala la Ofisi Binafsi ya Rais (OBR) kuangalia upya ratiba Rais, Rweyemamu alisema ofisi hiyo itatathmini upya ratiba ya shughuli za Rais. Ofisi hiyo ndiyo hupanga ratiba za Rais na baada ya tukio la Mwanza imetangaza kwamba itaangalia upya ratiba ya shughuli za Rais.
Mwaka 2005, alipoanguka jukwaani na kuchukuliwa na wasaidizi wake, aliwahishwa kwenda kupatiwa huduma na saa chache baada ya tukio hilo, Chama Cha Mapinduzi kilitoa taarifa kuwa afya ya mgombea wao wa urais ni shwari.
Baadaye alizungumza na waandishi wa habari usiku wa tukio hilo na kuwaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo la kuanguka ni mikikimikii ya kampeni iliyoongezewa ugumu na kitendo chake cha kufunga mfungo wa mwezi Ramadhani.
Haikuwahi kujitokeza tukio jingine la kushitua kuhusu afya yake, hadi hili la juzi la kuishiwa nguvu akiwa jukwaani na kushindwa kwa muda kuendelea kuhutubia ingawa pia amewahi kufanyiwa uchunguzi wa macho katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Ingawa masuala ya hali za afya za marais wengi wa Afrika huwa ni siri kubwa, baadhi ya wananchi wamenukuliwa wakitaka kuelezwa kwa kina kinachomsumbua Rais Kikwete kiafya.
Rais Kikwete
Baadhi waliozungumza na Raia Mwema walieleza kushangazwa kwao kwamba hata taarifa iliyotolewa na Ikulu ikielezea sababu ya tukio hilo kuwa ni uchovu, haikuwa na viambatanisho vyenye uthibitisho wa watalaamu wa afya, zaidi ya kuwa ni taarifa inayopandikiza mtazamo usio na utetezi wa kitaalamu.
Tayari baadhi ya watu wameanza kutazama ugumu wa kampeni za Kikwete mwakani kama hali ya afya yake haitatengemaa, na hasa pilikapilika za kampeni za kuzunguka nchi nzima kuomba kura na safari hii akiwa na majukumu ya kikazi kama Rais, tofauti na mwaka 2005, ambapo Rais aliyekuwa madarakani alikuwa Mkapa na Kikwete akibaki kuwa mgombea tu.
Hali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupatwa na mkasa wa kiafya, iliwahi pia kumpata Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyekuwa akisumbuliwa kwa maumivu katika mguu wa kushoto na kulazimika kufanyiwa upasuaji, mjini Zurich, Usiwi, Juni, 12, mwaka 2004, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya Kikwete kuingia madarakani.
Mkapa, ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 65, alikwenda katika Kliniki ya Hirslanden, Zurich, kwa ajili ya kutazamwa afya yake na hatimaye kufanyiwa upasuaji mguuni. Baada ya matibabu yake kwa muda wa wiki kadhaa, Mkapa alilazimika kutembea kwa msaada wa magongo
Source: Raia Mwema