Taarifa ya Hali ya Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini Tanzania 2015/16-2019/20

Taarifa ya Hali ya Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini Tanzania 2015/16-2019/20

Suley2019

JF-Expert Member
Joined
Oct 7, 2019
Posts
2,203
Reaction score
5,628
Taarifa ya Hali ya Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini Tanzania 2015/16-2019/20 na Mheshimiwa Ummy A Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Wadau na Watoa Huduma za Afya, Jijini Dodoma, Tarehe 19 Agosti, 2020
  • Ndugu Viongozi wa Sekta ya Afya,
  • Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Wajumbe wa RHMT/CHMT
  • Ndugu Wadau Wetu wa maendeleo na
  • Watoa Huduma za afya,
  • Mabibi na Mabwana

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana tena ili kupeana habari kuhusu maendeleo ya sekta ya afya nchini na leo nikilenga hali ya afya ya uzazi nchini Tanzania kufikia mwaka huu 2020.

Kipekee ninawashukuru wadau na watoa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ambao mmekutana hapa ili kutimiza jukumu hili muhimu la kitaifa la kujadili namna ya kuendeleza mapambano ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto. Ninapenda kuwashukuru sana kwa michango yenu na ushirikiano wa dhati katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia watanzania hususani akina mama, watoto na vijana wetu.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Toka mwaka 2015/16 hadi 2020 Tanzania imeendelea kupiga hatua katika utoaji wa huduma za afya hususani Afya ya Uzazi na Mtoto. Hatua hizi ni 2 pamoja na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma. Tumeshuhudia katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mh. Dk John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Juni 2020 ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Katika kipindi hiki jumla ya vituo vya kutolea huduma 1,797 vimejengwa (Zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Halmashauri 99, Hospitali za Mikoa 10 ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Mara ya Mwalimu Nyerere Memorial Hospital ambayo ujenzi wake uliasisiwa na mwalimu J. K. Nyerere zaidi ya miaka 40 iliyopita (1977).

Aidha, Serikali imejenga na kufanya upanuzi wa Hospitali 3 za Rufaa za Kanda; Hospitali ya Mtwara, Hospitali ya Burigi (Ujenzi mpya) na upanuzi mkubwa wa Hospitali ya kanda ya Nyanda za Juu Kusini-Mbeya ambapo jingo kubwa la ghorofa 5 lenye uwezo wa vitanda 223 Maalumu kwa ajili ya huduma za mama na mtoto ikiwemo vyumba 3 vya upasuaji ambapo tangu 1950 haijawahi kujengwa jengo la kulaza wagonjwa la namna hiyo.

Uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya tano kwenye miundombinu ya utoaji wa huduma za afya umeongeza vituo vya huduma za afya ngazi ya msingi vinavyotoa huduma za upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni kutoka vituo 192 (Vituo vya afya 115 na Hospitali za halmashauri 77) mwaka 2015 hadi vituo 586 (Hospitali za Halmashauri 99 na Vituo vya Afya 487) mwaka 2020, sawa na ongezeko la vituo 394. Serikali imeongeza idadi ya Vituo vya huduma kwa ajili ya watoto wachanga wanaozaliwa wakiwa na shida ya kupumua, uzito pungufu na maambukizo ya bakteria (Neonatal Care Units) kutoka vituo 14 mwaka 2015 hadi vituo 104 mwaka 2020 sawa na ongezeko la vituo 90. Vituo vinavyotoa huduma ya Kangaroo (KMC) ikiwa ni njia ya kiasili ya kumtunza mtoto aliyezaliwa njiti vimeongezeka kutoka 80 mwaka 2015 hadi 104 mwaka 2020.

Aidha, Serikali imeongeza upatikanaji wa huduma kwa ajili ya watoto wagonjwa mahututi (Paediatric ICU) katika hospitali za rufaa za kanda 2 mwaka 2015 hadi hospitali za kanda 6 ambazo ni Muhimbili, Bugando, KCMC, Mbeya, Benjamin Mkapa na Mloganzila. Pia Serikali imeongeza vituo vya upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi kutoka vituo 176 mwaka 2015 hadi kufikia 650 mwaka 2020 sawa na ongezeko la vituo 474 ambapo tumeweka vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi pamoja na kuwajengea uwezo watumishi Ujenzi na Upanuzi huu umesogeza huduma muhimu kwa ajili ya dharura ya uzazi na watoto karibu na wananchi kupitia uimarishaji wa vituo vyetu vya afya ya msingi, hivyo kuwaondolea kero na gharama kubwa walizokuwa wanazitumia kufuata huduma hizi mbali na maeneo yao na hivyo kuboresha maisha yao.

Aidha, Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuimarisha vituo 7 vya kanda vya damu salama na kuongeza vituo vidogo 14 (satelites) vya damu salama ambapo vituo 5 ujenzi wake unakamilishwa. Hii ni pamoja na kujengea uwezo timu za Halmashauri 184 katika ukusanyaji wa damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na mtoto pamoja na wagonjwa wengine. Hivyo, upatikanaji wa damu salama kwa ajili ya akinamama na watoto kama kundi lenye uhitaji mkubwa umeongezeka kutoka chupa 196,735 mwaka 2015 hadi chupa 309,376 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 57.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Katika kipindi cha mwaka 2016 - 2020 jumla ya Watoa huduma za afya 14,479 wenye ujuzi waliajiriwa na kufikia watumishi 100,631 mwaka 2020 ikilinganishwa na watumishi 86,152 mwaka 2015. Watumishi hawa ni pamoja na madaktari, wauguzi na wakunga, wafamasia, wataalamu wa maabara, n.k. Watumishi hawa walipelekwa katika vituo mbalimbali vya utoaji huduma nchi nzima kulingana na mahitaji ya mikoa na wilaya na kuwezesha kuimarika kwa utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi na mtoto. Ni dhahiri kuwa uwepo wa watumishi hao umewezesha kuongezeka kwa akinamama wanaozalishwa na watoa huduma wenye ujuzi kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi asilimia 80 mwaka 2020, hivyo kufikia lengo la utekelezaji tulilojiwekea katika mpango mkakati wa pili wa kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga, mtoto chini ya miaka mitano na kijana (One Plan II) wa mwaka 2016 - 2020.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa Dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ajili ya huduma za afya nchini ambapo kumekuwa na ongezeko la bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi bilioni 270 mwaka 2019/20. Ongezeko hilo limewezesha kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwa ajili ya afya ya uzazi na mtoto kutoka asilimia 53 mwaka 2015 hadi asilimia 96 Juni 2020. Dawa hizo ni pamoja na dawa ya kuzuia kuvuja kwa damu baada ya kujifungua aina ya Oxytocin, dawa za kudhibiti kifafa cha mimba zinazotolewa kwa sindano aina ya magnesium sulphate, dawa za kuongeza damu aina ya Fefo na pia upatikanaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Katika kipindi cha mwaka 2015/16 - Juni 2020; Serikali imeendelea kuimarisha huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto kwa kununua magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) 152 ambayo yamesambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini. Magari hayo yamewezesha kuokoa Maisha ya akina mama wengi pindi wanapotakiwa kufikishwa kwa haraka katika vituo vya kutolea huduma.

Aidha, katika kuimarisha upatikanaji, uhifadhi na usambazaji wa Chanjo, Serikali imeendelea kutoa fedha za kununulia chanjo pamoja na ukarabati wa maghala ya kuhifadhia chanjo eneo la Mabibo Dar es Salaam, ununuzi wa magari 74 ya kubebea chanjo, ununuzi majokofu 1,385 yanayotumia nguvu za jua ambapo Magari hayo na Majokofu yalisambazwa ngazi ya Halmashauri na Taifa. Kuwepo kwa majokofu haya sio tu kumeimarisha mnyororo baridi wa chanjo lakini pia kumewezesha vituo vya afya hususani zahanati na vituo vya afya kupunguza gharama za uendeshaji kwa ni awali walikuwa wananunua mitungi ya LP gas takribani kila mwezi.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, viashiria vikuu vya mwenendo wa huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, vimeendelea kuimarika kama ifuatavyo
  • Idadi ya wanawake wanaotumia huduma za afya ya uzazi kabla ya ujauzito na baada ya kujifungua imeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2015/16 hadi asilimia 43 mwaka 2020.
  • Aidha, kuimarishwa kwa ubora wa huduma za kliniki kwa wajawazito na watoto kumeleta ongezeko kubwa la akinamama wanaohudhuria 6 mara nne au zaidi kwenye kliniki ya wajawazito kutoka akinamama 747,524 (asilimia 39) mpaka akinamama 1,758,191(asilimia 81) Juni 2020.
  • Kiwango cha wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka kutoka akinamama 1,226,707 (asilimia 64) mwaka 2015 mpaka akinamama 1,801,603 (asilimia 83) Juni 2020, ambapo tumevuka lengo la asilimia 80 tulilokuwa tumejiwekea katika Mpango Mkakati wa Afya ya Uzazi na Mtoto (2016-2020).
    1597844804355.png

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Kwa kutumia takwimu za mfumo wa kufuatilia vifo vitokanavyo na uzazi, tumeshuhudia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa zaidi ya asilimia 71 ukilinganisha na vifo vilivyotolewa taarifa kupitia utafiti mwaka 2015/2016 (TDHS). Hali hii inaashiria kuwa tutakapofanya utafiti wa hali ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini ifikapo mwaka 2021, kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi nchini Tanzania kitakuwa kuwa chini ya vifo 190 kwa vizazi hai 100,000 ukilinganisha na vifo 556 kwa vizazi hai 100,000 kama ilivyotolewa taarifa kwenye utafiti wa mwaka 2015/16.

Mwenendo huu unaendana na takwimu za utafiti uliofanywa Mkoa wa Kigoma kwa Kushirikiana na Taasisi ya Thamini Uhai kwa ufadhili wa CDC mwaka 2018 ambapo kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi kilikuwa ni 174 kwa kila vizazi hai 100,000.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Taarifa za mapitio ya vifo hivi zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya vifo vitokanavyo na uzazi vinazuilika. Kwani, sababu zake ni pamoja na kupoteza damu wakati wa uchungu, kujifungua na baada ya kujifungua na kifafa cha mimba ambavyo huchangia asilimia 50 ya vifo vyote. Sababu zingine zinazopelekea vifo vitokanavyo na uzazi ni pamoja na upungufu wa damu unaotokana zaidi na lishe duni na ukosefu wa madini chuma mwilini hasa wakati wa ujauzito, maambukizi ya bakteria baada ya kujifungua, uchungu kinzani, kupasuka mfuko wa uzazi n.k.

8 Ndugu Wadau na Watoa Huduma Serikali imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kulinda afya ya mtoto ikiwa ni pamoja na utoaji wa chanjo mbalimbali, udhibiti wa Magonjwa mbalimbali, Afya ya Usafi wa Mazingira, Mafunzo ya IMCI kwa watoa huduma za afya nchini, Kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu za watoto kwa zaidi ya asilimia 96, ujenzi na ukarabati wa wodi za watoto wachanga na utoaji wa elimu kwa wazazi juu ya unyonyeshaji katika kipindi cha miaka miwili kumechangia kupungua zaidi kwa vifo vya watoto nchini.

Kwa kutumia mfumo wa ufuatiliaji wa utoaji huduma za afya unaonesha kuwa vifo vya watoto wa umri chini ya mwaka mmoja vilikuwa vifo 9 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2019/20. Takwimu hizi zinaonesha mafanikio makubwa ukilinganisha na Takwimu za utafiti wa Viashiria vya Afya wa mwaka 2015/16 ambapo vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja ilikuwa vifo 43 kati ya vizazi hai 1000

Takwimu zetu za mwaka 2019/20 vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa vifo 11 kati ya vizazi hai 1,000, ambapo takwimu za utafiti wa
mwaka 2015/16 ilikuwa vifo 67 kati ya vizazi hai 1000.

Takwimu zetu za mwaka 2019/20 vifo vya watoto wachanga vilikuwa vifo 7 kati ya vizazi hai 1,000, ambapo takwimu za utafiti wa mwaka 2015/16
ilikuwa vifo 25 kati ya vizazi hai 1000.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma, haya ndio mafanikio ya uwekezaji kwenye afya uliofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kulinda afya ya mtoto. Ongezeko la vituo vya kutolea huduma za Afya ya Uzazi na mtoto nchini na ubora wa huduma zitolewazo umechangiwa na 9 uongozi imara wa Serikali ya Awamu ya Tano, utashi thabiti wa kisiasa na ushiriki mzuri wa wananchi katika kujiletea maendeleo.

Wito wangu kwa wananchi, Viongozi wa Kijamii, Viongozi wa dini, Watoa huduma za Afya, na Wadau wetu wa maendeleo: Tuendeleze mshikamano katika kuzuia vifo hivi kwa kuhimiza wanawake kuwahi kliniki mapema pindi wanapojihisi kuwa ni wajawazito, kuzingatia maelekezo yanayotolewa kwenye kliniki na watoa huduma za Afya na kuwasaidia wajawazito ili wajifungulie katika vituo vyetu vya huduma hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ya awamu ya tano imewekeza karibu na wananchi
huduma za Afya ya mama na mtoto.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Naomba kuwashukuru watoa huduma za afya nchini tena na nawaomba tusichoke kuwahudumia ipasavyo akina mama wajawazito na watoto wetu
na tuendelee kushirikiana na Serikali yetu katika mapambano haya ya kuimarisha huduma za afya hususani za afya ya uzazi na mtoto. Nawashukuru kwa dhati wadau wetu wa maendeleo tunaosaidiana nao katika kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto. Hivyo ni matarajio yangu kuwa taarifa hii itawafikia wananchi kwa ufasaha ili kuongeza uelewa wa juhudi za Serikali yao katika kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Ndugu Wadau na Watoa Huduma
Tuendelee kushirikiana katika mapambano dhidi ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto nchini ili ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwe ni miongoni mwa nchi chache duniani kufikia malengo endelevu ya maendeleo kama tulivyoweza kufikia malengo ya millennia kwenye kushusha vifo vya watoto.

Ahsanteni sana​
 
Back
Top Bottom