Taasisi na Serikali ziwekeze katika mafunzo ya watoa huduma kwa wenye changamoto ya kusikia

Taasisi na Serikali ziwekeze katika mafunzo ya watoa huduma kwa wenye changamoto ya kusikia

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Katika mfululizo wa makala hizi, tunaona ukubwa wa tatizo na ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vya matibabu vya Jiji la Mbeya, na athari zake za kisheria na kiafya kwa watu wenye ulemavu wa kusikia. Swali la msingi: Nini kifanyike ili kupata suluhisho la tatizo hili?

Sehemu ya kwanza ~ Mbeya: Wenye changamoto ya kusikia wanapitia wakati mgumu katika Vituo vya Afya

Sehemu ya pili ~ Mbeya: Baadhi ya Mifumo ya utoaji huduma kwa viziwi inakiuka Sheria za nchi na Mikataba ya Kimataifa


Ili kutii matakwa ya Kifungu cha 38(1)(a) na Kifungu cha 43(1)(a) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2010, pamoja na Sera ya Afya ya mwaka 2007, wadau wanatoa suluhisho la kudumu kumaliza tatizo hili. Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dr. Aika Temu, anapendekeza mabadiliko ya kimfumo kwenye ajira za wataalamu wa sekta ya afya.
20260416_123300.jpg
Dr. Aika Temu: "Tunaona umuhimu wa wao pia kuwa sehemu ya ajira kwenye serikali. Kwa hiyo tunahisi serikali pia kuona umuhimu wa kuwa na ikama of course ya hawa watu wakalimani wa lugha za alama kwenye taasisi mbalimbali ili hawa viziwi waweze kupata huduma stahiki moja kwa moja.

"Kwa sasa, kwa hospitali wetu ya Kanda wao wameweza kumwajiri kwa mkataba, kwa hiyo anawasaidia pia katika kurahisisha mawasiliano anapokutana na kundi la hawa viziwi, kama wenzetu wa Hospitali ya Zono au Hospitali ya Rufaa ya Kanda walivyofanya kuwajiri kwa mkataba.

"Nafikiri kwenye vituo vyetu vya afya, nafikiri ni jambo jema kuanza kufikiria hivyo kuwajiri hawa wakalimani hata kwenye hospitali hizi za mkoa, hospitali za wilaya, kuanza na hizi hospitali kubwa kubwa ambazo tunajua kwa namna moja au nyingine kundi hilo la viziwi huwa wanafika katika kupata huduma.

"Kwa hiyo ni ni kitu ambacho ni cha muhimu. Kama halmashauri kufikiria kuwajiri kwa mkataba hawa wakalimani."

Kwa upande wake, Afisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Lucas Kinyunyu, anaona suluhisho lingine la haraka ni watoa huduma wenyewe kupata mafunzo ya lugha ya alama.

Lucas Kinyunyu: "Kwanza Jamii itambue kwamba kuna hawa viziwi ambao wanahitaji huduma kama binadamu mwingine yeyote, pili, taasisi au serikali ziwekeze basi kwenye hayo mafunzo ili huyu hawa watoa huduma sasa waweze kupata mafunzo ili waweze kuwasiliana vizuri, vyema na hawa wateja ili mteja akifika akute wahudumu wapo.

"Kufanya hivyo maana yake tayari itahamasisha watoa huduma kwenda kusoma, pia kitakuwa kimesababisha pia hata jamii kuona kwamba kumbe hata mtu mwenye ulemavu kama hawa viziwi basi wanapata huduma zilizo nzuri.

"Kwa kweli kuna changamoto kubwa sana na na ninashauri tu taasisi pia viongozi basi waone kwamba kuna umuhimu wa kuwa na na mkalimani wa hizo lugha za alama ili kuweza kuwasiliana vizuri na na hawa viziwi.

"Naona nafikiri kama ambavyo tumesema, nafikiri tukiwekeza kwenye watoa huduma tunaweza kusaidia jamii. Yaani huwa wanasema mteja mmoja akija, hata dukani mtu akifungua duka, akija mteja mmoja akapata huduma ambayo anaitaka hata kama ni yeye pekee yake ndani hata ya wiki au mwezi mzima, ataenda kutangaza na kwingine kwamba sehemu fulani kuna huduma hii na hii na hii.

"Tukipata hata kiziwi akapata huduma sehemu iliyo nzuri, hata akipata changamoto yaani ajifili tunasema inferiority yaani kwamba mimi nimebaguliwa, siwezi kupata huduma, naumwa nitamweleza nani, kwa hiyo anakuwa yuko huru kwamba sehemu fulani nikienda nitapata huduma. Lakini tunatamani ziwe ni sehemu za karibu, mtu anatoka kijijini kabisa mbali kule yaani mpaka afikirie kupanga safari, kwanza anapata anapata changamoto ya kuwasiliana kwenye usafiri.

"Akifika anapata changamoto ya kuwasiliana na mtoa huduma, kwa hiyo huyu mtu bado anajiona kama yaani yeye sio sehemu ya jamii. Kwa hiyo nasisitiza tu kwamba tuone taasisi au serikali iwekeze basi kwenye hawa watoa huduma ili hata viziwi pia waweze kupata huduma ambazo wanastahili kama kama wateja wengine."

Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Mbeya (CHAVITA), Tusajigwe Mwalwega anatoa ushauri wa kimkakati wa kila kituo cha afya.

Tusajigwe Mwalwega: "Mimi ni nini kifanyike, naona ni vizuri serikali itoe tamko kwenye vituo vya afya kwamba kila nesi au mwanafunzi aende kusoma ajifunze lugha ya alama. Ni lazima, yaani sio hiyari, iwe ni lazima. Pili, angalau vituo vya afya viwe na kitengo lengo lengo la kufundisha mkalimani lugha ya msingi.

"Hawa wataweza kusaidia kutoa huduma ndogo ndogo. Lengo kumchukua mkalimani wa nje kumlipa gharama ni kubwa, ni mara mbili hapo. Wito wangu mimi, vituo vya afya vingine wapate mfano wa Mkurugenzi wa Rufaa alivyoweka mkalimani. Kama wanashindwa, wamwaite nesi tumfundishe lugha ya alama kwa gharama ndogo."

Amani Gideon kutoka Shirika la TWF anasisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati ya muda mrefu inayolinda haki za viziwi kupata huduma muhimu za kijamii.

Amani Gideon: "Anapendekeza kwamba serikali ijitahidi kutenga bajeti ambayo inaweza kuwasaidia watu wengine wapate mafunzo ya kujifunza hii lugha kwa sababu ni lugha kama zingine. Kwa hiyo watakapojifunza hii lugha itawasaidia watu wengi kuwasiliana na watu na watajiona hawajatengwa na watapata huduma ambazo zinastahili kwao kama kawaida."

Diwani wa Kata ya Nsalaga, Clemence Mwandembwa, anaahidi kuchukua hatua za kiushawishi na kiutendaji kupitia baraza la madiwani.

Clemence Mwandembwa "Of course hiyo iko wazi kwamba ni muhimu sasa kuwa na wakalimani kwenye vituo vyetu hivi vya afya pamoja na zahanati na sehemu mbalimbali ambapo wanatoa huduma za afya.

"Ni muhimu sana kuwepo hawa watu. Kwa sababu uwepo wa wale watu kwanza utatoa haraka kupata huduma kwa wale watu, hata kuwajali. Anapokuja na karatasi, maanake ndugu yake anakuwa amemwandikia au mtu anayemlea kwamba ana shida hii na hii msikilizeni. Itakuwa rahisi sasa unazungumza na mtu ambaye labda anaweza akawa labda ni daktari au nesi au mtu yeyote yule anaye pamoja na kwamba ni daktari au ana nafasi fulani anakaa elimu ka maalum wako.

"Ambapo akija mgonjwa anazungumza naye moja kwa moja, shida ni nini hapa, yaani labda kichwa, hapa vipi, lakini pia wakiopo watu maalum itasaidia kwenye maswala mbalimbali. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwa na hawa wakalimani kwenye hospitali zetu.

"Niseme tu kwamba kwanza kupitia hii issue ya leo ya mambo ya afya kwa watu maalum au kwa watu mbalimbali kama viziwi na watu wengine, kwanza nimelichukua, nimelibeba kwa uzito sana. Kwa sababu wale unaowazungumzia viziwi ni binadamu kama sisi, nao wanastahili kupatiwa huduma kama sisi, wanastahili pia kusikilizwa kila ambacho wanakizungumza.

"Kwa hiyo nimelichukua kama kiongozi, lakini pia nitaenda kuliwasilisha kwenye vikao vyangu, na uzuri mimi ni mjumbe pia wa Kamati ya Uchumi, Afya na elimu Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Kwa hiyo kukutana na DMO, kukutana na watu mbalimbali wa afya ni very simple. Kaa tu useme bwana hili jambo limekaaje. Kwa hiyo naamini na wao wanaweza bakanifumbulia kwa upana zaidi ili mwisho wa siku tuone namna ya serikali inawasaidia hawa watu.

"Ndiyo maana nimesema ukienda hospitali wanapata huduma kama kawaida, lakini je kwa nini tusiweke wale wakalimani? Kwa hiyo mimi nimelichukua, nimelibeba kwa uzito, nitaenda kuliwasilisha vizuri.

"Hata kama wanapata huduma, tuongeze anayehudumiwa ajisikie raha anakutana na mtu anayemsikiliza yeye kuliko kuandikiwa kwenye karatasi na michakato mbalimbali ili ajione bwana na mimi wamenijali, wamenisikiliza, lakini nimepata huduma nimetabasamu kwa sababu nimepata kila ambacho nakihitaji."

Ushahidi ni kwamba inawezekana kuwa na wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vya matibabu, ukweli huu unadhahirishwa na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, kituo pekee mkoani hapa kinachofanikiwa kuwa na mkalimani wa mkataba.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dr. Godlove Mwanji, anaeleza chanzo cha uamuzi wao;

Dr. Godlove Mwanji: "Kuna siku walikuwa wamekuja hapa kuomba msaada kabla hatujapata yule mkalimani. Sasa sisi tunahangaika kuelewana hapa, ndio wazo likanijia: Hivi hawa sisi huwa wanaumwa, sasa huwa wanajielezaje? Kwa hiyo wazo likaanzia pale.

Sasa nakumbuka tulipokuwa tunaanza kwenye zile huduma za kuwa na mkalimani, cha kwanza nakumbuka ndani ya muda mfupi tuliweza kuwafanyia upasuaji mkubwa viziwi sita. Ambao walikuwa wameishi na uvimbe kwa miaka mingi.

Tulipowauliza baadaye kupitia sasa mkalimani, walisema walikuwa wakijieleza hapo hawaeleweki, kwa hiyo ni kama wanasusa wanaamua kuondoka. Tunashukuru Mungu haukuwa uvimbe wa kuwapotezea maisha.

Tulipata watu kama 20 baada ya kuendesha zoezi pia la kuwapima VVU wakaanza dawa. Nakumbuka 16 tuliweza kuwafanyia tohara watu wazima. Na kutoka hapo, wamekuwa na mahusiano mazuri sana na sisi kupitia huyu mkalimani."

Ufumbuzi upo, na mifano ya kuigwa ipo; kilichobaki ni utekelezaji wa dhati kutoka kwa mamlaka ili viziwi wa Mbeya nao wapate haki yao ya msingi ya afya bila vikwazo.

Andiko la: Mwanaisha Makumbuli
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 

Attachments

Back
Top Bottom