Timu za Taifa za Tanzania na Kenya zimetolewa kwenye hatua ya kufuzu kombe la dunia nchini Urusi-2018 kwa kufungwa ugenini kwenye mechi za marudiano. Taifa Stars ya Tanzania iliingia uwanjani jana dhidi ya Algeria wakiwa na akiba ya sare ya 2-2 kwenye mechi ya awali.
Taifa Stars ilizabwa mabao 7-0 katika mechi ya jana na kutupwa nje kwa jumla ya mabao 9-2. Kati ya sababu zilizowapoteza Taifa Stars ni kuimarika kwa kikosi cha Algeria,kwa kuwepo kwa Yacine Brahimi wa Porto ya Ureno,pamoja na kucheza pungufu baada ya Mudathir Yahya kulimwa kadi nyekundu. Pungufu kwa Algeria!? Algeria pia walipewa penati mbili nyepesi sana-za kupendelewa.
Kwa upande wa jirani zetu Harambee Stars ya Kenya,waliingia uwanjani kurudiana na Cape Verde wakiwa wameshinda bao 1-0 nyumbani. Jana walitandikwa mabao 2-0 na kusukumwa nje kwa jumla ya mabao 2-1. Harambee Stars imeponzwa na kucheza kwa kujihami na kutokuwa na msaidizi wa kueleweka wa Victor Wanyama kwenye kiungo. Cape Verde walicheza kwa nguvu kubwa.
Hayo yameisha, tugange yajayo