Suley2019
JF-Expert Member
- Oct 7, 2019
- 2,203
- 5,610
JUNI 10, 2020 |
TAKUKURU MAKAO MAKUU KUHOJI WABUNGE 69 MATUMIZI YA FEDHA ZA CHADEMA
Kwa taarifa hii, tunapenda kuuthibitishia umma kwamba ni kweli kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU Makao Makuu, imewaita Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA na waliowahi kuwa wabunge wa chama hicho kwa ajili ya mahojiano.
Hatua hii inafanyika ikiwa ni mwendelezo wa uchunguzi unaoendeshwa na TAKUKURU Makao Makuu wa malalamiko dhidi ya matumizi ya fedha za Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA ambapo hatua iliyopo sasa ni ya kuwahoji Wabunge sitini na tisa (69) – wanachama na waliowahi kuwa wanachama wa chama hicho.
Fedha hizi ni zile ambazo zililalamikiwa na waliokuwa Wabunge wa chama hicho ambao walitangaza kukihama chama chao ambapo katika malalamiko yao walidai kwamba walikuwa wakikatwa fedha katika mishahara yao kila mwezi kuanzia mwezi Juni 2016.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo kila mwezi – Wabunge wa Viti Maalum walikuwa wakikatwa kiasi cha shilingi 1,560,000 na Wabunge wa kuchaguliwa kwenye Majimbo walikuwa wakikatwa shilingi 520,000 na kwamba hawakuwa wakifahamu namna ambavyo fedha hizo zimekuwa zikitumika.
Kwahiyo, tunapenda kuujulisha umma kwamba, kama ambavyo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo alivyoviambia vyombo vya habari Mei 27, 2020 ni kwamba uchunguzi dhidi ya tuhuma hii tayari ulisha anzishwa na baadhi ya wahusika walishaanza kuhojiwa.
Tunafanya hivi kwakuwa yawezekana katika tuhuma hii kukapatikana makosa yafuatayo:
- Ubadhirifu na ufujaji wa fedha za chama
- Matumizi mabaya ya mamlaka
Mpaka sasa tayari tumeshafanya mahojiano na:
- Viongozi wa CHADEMA
- Viongozi waliowahi kuwa CHADEMA
- Wabunge waliotoa taarifa
- Maafisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
- Viongozi wa Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na sasa tunawahoji
- Wabunge wanachama wa CHADEMA pamoja na
- Wabunge waliowahi kuwa wanachama wa CHADEMA.
Mahojiano haya ambayo yanafanyika katika Ofisi za TAKUKURU Makao Makuu – Dodoma kuanzia leo - yanatarajiwa kukamilika wiki ijayo.
IMETOLEWA NA:
Doreen J. Kapwani
AFISA UHUSIANO – TAKUKURU MAKAO MAKUU