SoC02 Tanzania inavyoweza kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana

SoC02 Tanzania inavyoweza kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Jul 18, 2022
Posts
49
Reaction score
57
Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambayo imekuwa na changamoto ya vijana kukosa ajira mara baada ya kuhitimu masomo. Kumekuwa na mitazamo mingi juu ya tatizo hili ambapo wengine wamefikia hatua ya kusema ni bomu linalojiandaa kulipuka.

Kwa vyovyote vile kuna haja ya kulipa kipaumbele suala la ajira kwa vijana. Itakumbukwa kwamba sehemu kubwa ya watu katika nchi yetu ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa. Ni kweli kwamba serikali haiwezi kuajiri vijana wote wanaohitimu masomo yao lakini pamoja na hivyo ni lazima kuwe na mkakati endelevu wa namna ya kutengeneza fursa za ajira.

Kwa kufanya hivyo kila mwananchi na raia wa Tanzania kwa nafasi yake kulitumikia taifa kwa juhudi na maarifa yake yote kwa maendeleo ya taifa lake. Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa kufanyika kuhakikisha Tanzania inaondokana na tatizo la ajira na kupata maendeleo yatakayonufaisha walio wengi katika zama hizi;

Serikali ianzishe bodi ya mikopo kwa vijana kama ilivyo bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Bodi hii itapokea na kuchakata maombi yote ya mikopo pamoja na maandiko ya miradi ya wahusika kabla ya mkopo kutolewa. Taratibu za uombaji hazitatofautiana sana na zile za bodi ya mkopo, isipokuwa tu muombaji atahitajika kuambatanisha andiko la mradi na baadaye ataunganishwa na wataalamu katika eneo husika kwa ushauri wa kitaalamu wa wazo analotaka kufanya.

Mfano kama andiko linahusu kilimo basi ataunganishwa na afisa kilimo wa eneo husika kwa ajili ya kusimamiwa kitaalamu kwa matokeo chanya zaidi. Fedha zote za halmashauri ambazo hupaswa kutolewa kuwawezesha vijana zikusanywe katika bodi hii. Hii itaondoa msongamano na malalamiko kwa waombaji ikiwa mikopo itatolewa kwa njia ya halmashauri ambapo utoaji wa mikopo imekaa kisiasa zaidi.

Sambamba na hilo tupitie upya mfumo wote wa elimu ili uweze kuwaanda wanafunzi kujiajiri pindi wamalizapo masomo ikiwa ni pamoja na kuongeza masomo kwa vitendo ili kuzalisha wabunifu na wajasiriamali. Hapa natamani kila kata iwe na chuo cha ufundi hata cha wastani ili kufundisha kwa vitendo.

Kwa tafsiri isiyo rasmi “elimu ni uhamishaji wa maarifa, ujuzi na uwezo kutoka kwa mtu au kizazi kimoja na kingine hivyo basi tutaondokana na utaratibu wa kuwafundisha wanafunzi kujibu mitihani badala yake wapate maarifa. Ndio maana tuna A nyingi za darasani halafu tuna 0 nyingi za kuziishi mtaani.

Kuendana na hilo hapo juu. Kila kiwanda na sehemu nyingine za uzalishaji wa kiufundi nchini zitakiwe kuwa na mfumo wa mafunzo vitendo (hata gereji za Kiboroloni). Viwanda hivi vitachukua idadi stahili ya wanafunzi wa vyuo na kuwafanyisha kazi kwa nguvu sana na masaa ya kutosha na kuwafunza ustadi za kazi - wastani wa gharama za kufanya hivyo upunguzwe kwenye kodi ya mapato.

Pia tuweke utaratibu wa kutambua kipaji cha mwanafunzi kuanzia elimu ya awali ili hata atakapokuwa anaendelea na masomo ajue kipaji chake na iwe rahisi kukiendeleza na hata akifika ngazi za juu aweze kuchagua masomo yatakayoendana na kipaji chake badala ya kujikita katika kutoa vyeti vya nadharia. Kuna baadhi ya walimu na wazazi huwalazimisha wanafunzi kuchagua masomo ambayo hayaendani na vipaji pamoja na matakwa yao hivyo hupelekea kuua ndoto za wengi.

Hali kadhalika, tupunguze miaka ya kusoma kuanzia shule ya msingi iwe miaka 6 ya kukaa darasani na mmoja kwa ajili ya ufundi mfano ufundi gereji, useremala na ushonaji kulingana na umahiri wa mwanafunzi. Pia kwa upande wa sekondari tuanzishe masomo ya ufundi na shule zote ziwe “technical school” kwa ajili ya kuimarisha elimu ya kujitegemea (EK) pamoja na ufundi kuelekea uchumi wa viwanda.

Turejeshe utaratibu wa hapo awali wa elimu ya kujitegemea ambapo wanafunzi walikuwa wanapatiwa elimu hali kadhalika wakipewa mafunzo maalumu ya kujitegemea kwenye kazi za mikono mfano uzalishaji mali kupitia kilimo na bustani. Hii itawasaidia wanafunzi kufanya kwa vitendo siyo kusoma tu kwenye vitabu, lakini pia kutenda. Tutakuwa tunawasaidia kujitegemea pindi wamalizapo masomo yao mashuleni.

Tukiwapa vijana ujuzi wa kutosha tuwashauri wazazi wote wenye uwezo wa kifedha kuwapa mitaji watoto wao ili wafungue karakana (workshops) na viwanda vidogo (SMEs) baada ya kuhitimu na waliobaki wasaidiwe na serikali kupitia bodi ya mikopo.

Serikali ianzishe progamu ya kufanya Intership kwa vijana wanaosoma fani za sayansi na teknolojia mfano uhandisi wa barabara wapelekwe kwenye miradi yote inayofanyika nchini hadi zile za Wachina mpaka zitakapo kamilika. Hii itawafanya vijana kujifunza kwa vitendo na hivyo kubaki na ujuzi pindi miradi inapofika mwisho. Kwa miaka ijayo badala ya kuwatumia wageni pekee kwenye miradi mikubwa tutaanza kuwaajiri kupitia makampuni ya watu wetu.

Tuingie ubia na makampuni yenye kuuza pikipiki na bajaji kuwakopesha bodaboda vijana au wakakopa kupitia bodi ya mkopo (na wakarejesha kila jioni kama wafanyavyo sasa kwa mabosi wao). Hii itasaidia kuwa na pikipiki na bajaji nyingi mtaani na hivyo kutatua tatizo la ajira na kuongeza mapato ya serikali na matumizi ya mafuta/gesi.

Kupitia wingi huu wa vifaa hivi tufikirie kuanzisha mpango wa matumizi ya gesi kwenye bajaji, pikipiki, na magari ili gesi yetu ya Mtwara ipate wateja na hivyo kuinua maisha ya watu na kuchochea uchumi.
Kwa kuhitimisha nipende kusema kuwa binafsi naamini kuwa kama tukitekeleza mambo haya yote niliyoyaeleza basi tatizo la ajira kwa vijana linawezekana kutatuliwa kabisa.

Cha msingi ni kuweka nia na kuhimizana kufanya kazi kwa bidii pasipo kuhujumu mali za umma na mali za wanyonge. Wakati tukiishi hapa duniani ni vyema tutambue kuwa tuna wajibu wa kuzitumia fursa zote tulizojaliwa na mwenyezi Mungu zitusaidie kutatua changamoto na kututimizia mahitaji yetu muhimu.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa ili tufanikiwe tunahitaji ardhi, watu na uongozi safi (bora) na ni vitu ambavyo tayari tunavyo kumbe tunahitaji kiongozi/viongozi wa kuwaonyesha njia wananchi ili Tanzania ipate maendeleo yatakayonufaisha walio wengi katika zama hizi.
 
Upvote 6
Tatizo la ajira nchini ni la kujitakia kwa maana ni kushindwa kwa sera zetu au ukosefu wa ubunifu na uwajibikaji wa viongozi wetu kuweza kuunganisha raslimali tele zilizopo na kuzigeuza tija kwa vijana
 
Tatizo la ajira nchini ni la kujitakia kwa maana ni kushindwa kwa sera zetu au ukosefu wa ubunifu na uwajibikaji wa viongozi wetu kuweza kuunganisha raslimali tele zilizopo na kuzigeuza tija kwa vijana
Naomba na mimi unipigie kura au utoe maoni lwenye makala zangu
 
Back
Top Bottom