JK alitwambia miezi michache iliyopita ili kurudisha maadili mema ya Watendaji ndani ya serikali, watendaji watatakiwa wachague siasa au biashara. Sasa kulikoni tena mbona wanapigana vikumbo kufanya ufisadi mwingine? Ile kauli ya JK ilikuwa ni usanii tu?
Vikumbo vya vigogo tenda ya vitambulisho
Mwandishi Wetu Juni 25, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo
HOFU imetanda mchakato wa mradi tata wa Vitambulisho vya Taifa unaokadiriwa kugharimu karibu shilingi bilioni 200 unaanza tena leo kwa makampuni mbalimbali ya ndani na nje kuugombea huku baadhi yakihofia mchezo mchafu kutokea.
Hofu hiyo inagubikwa zaidi na kutajwa tajwa kwa watun mashuhuri ndani ya serikali kuhusika na mradi huo kwa namna moja ama nyingine kwa kuwa na uhusiano ama mawasiliano na baadhi ya makampuni yanayowania zabuni hiyo.
Taarifa ambazo Raia Mwema imepata wiki hii zinasema kiasi cha kampuni 104 zimejitokeza kuwania mradi huo mkubwa. Hizo ni pamoja na tatu za Malaysia za Iris, Data Sonic na Malaysia Microelectronics Solutions.
Mengine ni Infotech (T) Limited, Raha.com, Simba Technology, Business Connection, Softnet, Digisec, Etcon na NEC.
Kampuni nyingine ni Agumba, Transnational, Tata, Rubianes, Technobrain, GI, Necordata, IBM (South Africa), Copycat (Tz), BT Connect, SXmart, ZECGroup Computor Mart, Otiglobal na Jaba Trading.
Mradi huu wa Vitambulisho vya Taifa una historia ndefu ukiwa umebuniwa mwaka 1972, kiasi cha miaka 35 iliyopita kwa kupitisha bungeni Sheria ya Vitambulisho na Uraia ya 1972.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha
Tangu wakati huo mawaziri wengi waliopita katika Wizara ya Mambo ya Ndani waliukuta na kuuacha kutokana na sababu mbalimbali, za karibuni zaidi zikiwa ni mgongano wa kimaslahi, ya umma na ya binafsi.
Sasa ni mara ya nne kwa mradi huo kutangazwa kuanza. Oktoba 1995 ulitangazwa na kampuni zipapatazo 27 za nje na ndani ziliomba kazi hiyo. Kutokana na mizengwe, urasimu na hila za kifisadi makampuni 22 yalijitoa kwenye kinyanganyiro hicho na zabuni ikafutwa katika mazingira ya kutatanisha.
Mwaka 1998 zabuni zilitangazwa tena, waombaji wakajitokeza, lakini Serikali ikaifuta zabuni hiyo na kuahidi kuitangaza upya huku ikiacha kiwingu cha utata.
Mwaka 2007, Serikali ilikaribisha tena wazabuni kadhaa kupitia utaratibu wa Request for Proposal (RFP) ili wawasilishe maombi yao. Kampuni kutoka Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Afrika Kusini na Malaysia zilijitokeza, nyingi zikiwa na ushirikiano na kampuni za kizalendo za nchini.
Mchakato wa kupitia maombi uliashiria matumaini kuwa safari hii Serikali ilidhamiria kwa dhati kukamilisha zoezi hili. Katika hatua ya kushangaza na kwa sababu ambazo hazikuwahi kutajwa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Joseph Mungai ghafla alisitisha zoezi zima la mradi huo.
Tangu mwanzo maamuzi yaliyohusu mradi huu yaligubikwa na usiri mkubwa. Kwa mfano, uteuzi wa mshauri wa mradi uliendeshwa kwa upendeleo ambao wafuatiliaji wa mambo wanasema umekiuka sheria za nchi.
Serikali iliipa kazi hiyo ngumu kampuni ya Gotham International Ltd inayomilikiwa na Jack Gotham aliyekuwa akishirikiana na afisa wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) John Kyaruzi, ambaye alisaidia kuiunganisha kampuni hiyo na Business Connections ya Afrika Kusini na kwa pamoja wakashughulikia mchanganuo wa mradi huo.
Katika utangulizi wa mchanganuo wao, Gothan na Kyaruzi, ambao wote wakati wanabuni mradi huo walikuwa watumishi serikalini walitaja washirika wao katika ubunifu huo kuwa ni Profesa Damas Muna, Jaffar Buyogera, Dickson Maimu, Salum Mpugusi, Donald Carriere, Coen Kleihans, Kenneth Roko, Robert Alexander, Richard Butler, Anthony Githua, Rama Mwikalo na Robert Stewart.
Japokuwa mambo hayakuwekwa wazi sana, baadhi ya wanaotajwa katika safu hii ya wabunifu wa mradi wana mahusiano ya karibu na kampuni ya Business Connection iliyomo katika mchakato na Facet Technologies ya Afrika Kusini ambayo inaweza kuingia katika hatua za baadaye.
Lakini pengine utata mkubwa katika mchakato mzima ni unaowakilishwa na kuteuliwa kwa Maimu kuwa kwanza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Vitambulisho, japo sasa anatajwa kuwa Mratibu Mradi.
Kingine kinachoshangaza ni hatua ya Serikali kukubali kwamba baada ya kumaliza mchanganuo wa mradi kundi hili la kina Gotham ndilo liwe linasimamia mradi.
Ukiacha kundi hilo la Gotham, utata mwingine unaogubika mradi huo ni nafasi ya sasa ya Laurence Masha. Miaka kiasi 10 iliyopita Masha alikuwa wakili wa kampuni moja ya Malaysia, ambayo ilishinda zabuni kabla ya mradi kufutwa.
Kampuni hiyo, kimsingi ilishinda kesi na Raia Mwema haikuweza kupata kwa hakika kama ililipwa. Sasa inaaminika kwamba nayo imo katika kinyanganyiro hicho na Masha ndiye Waziri mhusika.
Huko nyuma mradi huo ulipotangazwa tena, kampuni hiyo ilikuwa inajipitishapitisha ikidai kwamba yenyewe ndiyo iliyostahili kupata zabuni kwa kuwa, na kweli, ilishinda wakati ule kabla ya mradi kufutwa.
Kwa upande mwingine, kuna mvutano ambao umedumu kwa muda mrefu sasa ukihusu aina ya teknolojia muafaka kwa mazingira ya Tanzania.
Mojawapo ni ile ya Micro Chip Smart Card ambayo wataalamu wanasema ni ghali mno na kwa kuwa Tanzania haina mtandao wa miundombinu ya mawasiliano ya kisasa, basi itakuwa ni kazi bure kuchagua teknolojia hiyo. Ushauri mzuri uliotolewa ni kuwa na aina ya Smart Card ya kawaida ambayo si ya kiwango cha juu na ambayo itakidhi matarajio ya mradi ili nchi iweze kumudu gharama zake.
Aidha, wachambuzi wa mambo wanashangazwa na mwelekeo wa Serikali kutaka kuendesha mradi huo nchi nzima kwa wakati mmoja jambo ambalo ni gumu.
Wanasema kitaalamu mradi wa ukubwa kama huo unaohusisha teknolojia ya kisasa hauwezi kutekelezwa bila ya majaribio au pilot project ambayo itawezesha marekebisho ya hitilafu na ufanisi kabla ya kueneza nchi nzima.
Wanasema ni dhahiri kuwa kwa mwenendo wanaotaka Wizara, wa nchi nzima mara moja, mradi huu lazima utakwama na kusababisha hasara kubwa kwa nchi.
Wataalamu pia wamekuwa wakihoji dhamira ya kuwa na vitambulisho vingi tofauti, kwa mfano, vitambulisho vya uchaguzi vinavyotolewa na Tume ya Uchaguzi, leseni za udereva zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA), pasi itolewayo na Idara ya Uhamiaji na sasa hivi vitambulisho vya uraia vya Wizara ya Mambo ya Ndani. Hii inadhihirisha namna idara za Serikali zinavyokosa ushirikiano na mipango endelevu kiasi cha kusababisha ubadhirifu usio wa lazima wa fedha za umma.
Vilevile Serikali hadi hivi sasa haijaamua kama mradi huu utajiendesha wenyewe au utagharamiwa na Serikali. Kuna habari kuwa kila raia atalipia kitambulisho chake, na kama hivyo ndivyo basi iko haja ya kuchukua tahadhari kubwa ili wananchi wasije kukamuliwa gharama kubwa zitakazosababishwa na maamuzi mabaya.
Lakini wachambuzi wanasema katika macho ya wanasiasa mradi huu ni bingo ya mwisho na ambayo haifai kuikosa. Ni vigumu kujua idadi kamili ya viongozi wenye tamaa wanaohusika na maslahi binafsi na Mradi huu wa Vitambulisho lakini jambo la uhakika ni kuwa kwa kasi hii umma ujiandae kmwenendo ambao Mhe. Wawa mradi mwingine wenye mauzauza.
Wachambuzi wanasema kwamba kwa kutoonyesha umakini wa mambo, kwa mfano, katika mahitaji ya mradi, kwenye kipengele cha mkataba ama Specific Contract Requirements; Type of Contract kumeandikwa TBD (To be Determined-mkataba utafahamika baadaye) ikiwa na maana kwamba kuna wazo la mradi na hesabu ya fedha inafahamika, lakini haijulikani ni aina gani ya mkataba utaingiwa. Kwamba seriali inategemes mzabuni ndiye aseme aina ya mkataba atakaoingia nayo.
Kwingine ni kwenye Method of Payment: Prices TBD. Kwamba haijulikani malipo yatafanyika kwa mfumo upi.
Kwingine ni kwenye General Supply Expeience, yaani huyo mshindi atatakiwa kuwa na kiasi gani cha fedha ili aweze kuruhusiwa kuendesha mradi huo nako kumean dikwa TBD, maana yake kwamba itamhuhitaji mzabuni ndiye ataje ana fedha kiasi gani za mradi na Serikali umuamini.