Watanzania wengi wa leo siyo kama wale wa mwaka 47!! Wengi wana uwezo wa kuchanganua mambo kwa urefu na mapana na ndiyo maana Sitta pamoja na kuwa aliongea kwa dakika chache tu, lakini hotuba yake imewagusa Watanzania wengi kuliko ile ya mheshimiwa ya masaa matatu na nusu. Kama kaongea pumba lazima aambiwe kwamba mheshimiwa umechemsha!
Ingekuwa ni amri ya Watanzania wengi tungekwambia uachie ngazi sasa badala ya kusubiri 2010 maana nchi imekushinda! Hakuna haki ya binadamu wanaofanya ufisadi wa kuiba mabilioni ya shilingi. Hawa hawaombwi wala kubembelezwa ili warudishe kile walichoiba bali ni kupewa mkong'oto kama ikibidi waseme na kuwekwa mahabusi wakati wanaisaidia polisi katika uchunguzi wake. Haihitaji kuwa na Phd ili kuweza kuanalyse kwamba JK kwa mara nyingine tena ameongea pumba na kushindwa tena kuitumia vizuri nafasi hiyo ili kurudisha credibility yake pamoja na ya serikali yake kwa Watanzania
Date::8/23/2008
Kauli ya Spika Sitta yazidi kupongezwa kuhusu wahujumu uchumi
Na Waandishi Wetu
Mwananchi
WANANCHI mbalimbali wameipongeza kauli ya Spika wa Bunge Samuel Sitta kuwa wahujumu uchumi hawatakiwi kuonewa huruma na kuielezea kuwa imeifunika hotuba nzima ya rais Jakaya Kikwete.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesaema maneno machache aliyoyasema Sitta wakati wa kumshukuru Rais Kikwete, yameifunika hotuba nzima ya Rais huyo.
Wakati baadhi yao, wakiwamo wakulima wanampongeza rais kwa kuwakumbuka na kuwamegea fedha za EPA, wengine mmesema Sitta ndiye ameeleweka zaidi kwa kuwa kauli yake imekwenda sawa na matarajio yao.
Kwa mujibuj wa wananchi hao kauli yake ilipendekeza njia ya mkato ya kumaliza ufisadi kwa kuweka kando haki za binadamu, wakati ile ya Kikwete ilionyesha huruma kuwapa nafasi watuhumiwa wa EPA kupumua kwa kuongezewa muda kurudisha fedha walizoiba.
Kauli hizo za wananchi na ile ya Spika zimekuja baada ya Rais kulihutubia bunge Alhamisi wiki hii ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo tangu aingie madarakani.
Kwa ufupi wananchi wamemtaka Rais Kikwete kukumbuka usemi wa "Ukitaka kumuua nyani usimtazame usoni,".
Akitoa maoni yake jana, Shahib Bakari wa jijini Mwanza, alisema Rais alipaswa kutoa ufafanuzi unaoeleweka katika suala la EPA kama alivyofanya katika suala la muungano.
Alisema anashindwa kuelewa kwanini watuhumiwa hao wanabembelezwa badala ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani?
Mariam Simon alisema amefurahisha zaidi na spika wa bunge kwa maelezo yake kutokana na kumwambia Rais kuwa mkali kwa vile hicho ndicho alichotarajia katika hotuba yake lakini hakukipata.
"Kwa kitendo chake kusema kuwa amewaongezea muda nimebaini kuwa rais ameonyesha udhaifu katika kushughulikia ufisadi.
"Yapo ambayo naweza kusema nimefurahishwa nayo lakini si katika mafisadi wa EPA, hapa naungana na spika na ninampongeza kwani ametuwakilisha kwa kutoa mawazo yetu," alieleza.
Naye Jumbe Magati alisema kuwa maefurahishwa na maneno machache ya spika kuliko hotuba nzima ya Rais kutokana na kushindwa kwake kuwachukulia hatua mafisadi hao.
Magati alisema kitendo cha Rais kushindwa hata kuwataja kinakwenda sambamba na hatua yake ya kushindwa kuwachukulia hatua, na kitendo chake cha kuwapa muda wa kurejesha fedha walizoiba kinachochea na kukuza wizi wa mali za umma.
Kwa upande wake, Charles Kibangu alisema kuwa ameridhika na hotuba hiyo kwa rais lakini kumtaka kufanyia kazi maneno ya spika wa bunge Samwel Sitta kwa vile hiyo ndiyo kiu ya wananchi wengi.
"Sina taabu na hotuba yake lakini naomba tu Rais aifanyie kazi maneno ya spika wa bunge ambayo ameyatoa jana, kwani hiyo ndiyo kiu ya wengi na hasa wanapotaka kusikia" alieleza.
Wengine ambao hawakupenda kutajwa majina yao walipiga simu kwenye chumba cha habari kuwa Spika amesema ukweli, kwani suala la haki kwa wahujumu uchumi halileti maana huku wezi wadogo wadogo wakichukuliwa hatua za kisheria na kufungwa.
"Je, hawa hawana na haki kama za hao watuhumiwa wa EPA?" alihoji mwananchi mmoja aliyepiga simu.
Mwingine aliyetoa maoni yake kwa njia ya mtandao, amemtaka Rais atambue kuwa watuhumiwa wa EPA pia wana haki ya kushitakiwa huku wakihoji nini kinachoshondikana kwa Rais kuwauma mafisadi hao.
Alihoji haki za binaadamu alizoziongelea Rais ni haki gani, kama siyo kuwapa uhuru mafisadi wa kutumia walichoiba hao huku wakiendelea kudunda na tai shingoni.
Mwananchi huyo ahoji kuna shida gani kuwataja wahujumu uchumi wa EPA wakati enzi za Edward Sokoine wahujumu uchumi walifahamika na kuminywa.