Kwa muda wa miongo miwili sasa China imeendelea kuwa mmoja wa wawekezaji wakubwa nchini Tanzania, na takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa mwaka 2023 peke yake uwekezaji wa moja kwa moja (FDI) kutoka China kwenda Tanzania ulifikia dola za Marekani milioni 60.15, ambao uliongezeka kutoka karibu dola milioni 52 za mwaka 2022. Licha ya takwimu hizo za kuridhisha, Tanzania bado inafanya juhudi kuendelea kuvutia uwekezaji zaidi kutoka China.
Moja ya juhudi hizo ni kuzinduliwa kwa jukwaa maalumu la kuwezesha uwekezaji katika Mkoa wa Hunan, China, ili kuvutia angalau dola za Marekani bilioni 3 za uwekezaji kutoka China. Mpango huu ni matokeo ya ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba mjini Beijing, ambapo Rais Xi Jinping wa China alitoa ahadi ya uwekezaji wa dola bilioni 10 barani Afrika kupitia mipango mbalimbali.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alikiagiza kituo cha uwekezaji cha Tanzania (TIC) kupata angalau theluthi moja ya fedha hizo, ambazo ni sawa na dola za Marekani bilioni 3, kwa ajili ya uwekezaji nchini Tanzania. Ili kuitikia na kutekeleza agizo la Profesa Kitila, TIC imeanzisha kituo cha kuwezesha uwekezaji katika Mkoa wa Hunan, China, kilichoteuliwa kuwa lango la kutangaza fursa za uwekezaji nchini Tanzania kwa wafanyabiashara wa China. Kituo hicho kinalenga kutangaza zaidi fursa za uwekezaji za Tanzania katika sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na viwanda, madini na miundombinu, kwa kushirikiana moja kwa moja na wafanyabiashara na wawekezaji wa China.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo hicho ulioshirikisha zaidi ya makampuni 150 kutoka sekta mbalimbali nchini China, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania TIC Bw. Gilead Teri, alisisitiza umuhimu wa mpango huo ni hatua nyingine ya juhudi za Tanzania kuvutia uwekezaji kutoka China, na Tanzania inatarajia ongezeko kubwa la wawekezaji, hata baada ya uzinduzi viongozi kadhaa waandamizi wa Tanzania walitembelea viwanda vikubwa nchini China ili kuhamasisha kuanzisha shughuli za uzalishaji nchini Tanzania.
Umuhimu wa uwekezaji wa China nchini Tanzania umekuwa na manufaa anuai, ikiwa ni pamoja na kuchochea uzalishaji wa ndani, kuongeza mapato ya kodi kwa serikali, na hata kuleta ajira kwa vijana. Hadi kufikia Februari 2024, kulikuwa na miradi 1,274 ya China iliyosajiliwa Tanzania, ikiwa na thamani ya takriban dola za Marekani bilioni 11.4, na kuleta nafasi 149,759 za ajira katika sekta za viwanda, kilimo na huduma. Tanzania pia ni mdau muhimu wa kimkakati kwenye pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia moja” (BRI), ambalo ni la kimataifa kuhusu miundombinu na maendeleo ya uchumi lililozinduliwa na China ili kuimarisha mawasiliano na biashara duniani.
Mwezi Mei mwaka jana Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa Nje ya Tanzania (EPZA) ilialika ujumbe kutoka mkoani Hunan, uliongozwa na Naibu Meya wa mji wa Luodi wa mkoa huyo Bw. Yangwei, mji wenye wawekezaji wengi wenye nia ya kutafuta fursa za uwekezaji barani Afrika. Ziara hiyo ilionyesha moyo wa ushirikiano na maslahi ya pande zote mbili, na ililenga kuangalia njia za uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Tanzania. Ziara ya ujumbe huo kutoka na mjini Luodi na na Tanzania kufungua kituo hicho cha kuvutia uwekezaji, vinaonesha kuwa utekelezaji wa hatua mbalimbali za ushirikiano unapiga hatua.