Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Dar es Salaam. Tanzania imefungua rasmi Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi, unaolenga kujadili hatua za pamoja za kulinda mazingira ya bahari na maeneo ya pwani katika ukanda wa Bahari ya Hindi Magharibi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 6, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Masauni, amesema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaowakutanisha zaidi ya wajumbe 500 kutoka nchi za ukanda huo na washirika wa kimataifa.
Masauni amesema mkutano huo una umuhimu wa kipekee kwa kuwa pia unaadhimisha miaka 40 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Nairobi mwaka 1985, ambao amesema umeendelea kuwa mfumo muhimu wa kikanda katika usimamizi wa mazingira ya bahari na pwani.
Amesema ushirikiano wa nchi wanachama unahitajika zaidi kutokana na changamoto zinazokabili bahari, zikiwamo mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la joto na tindikali baharini, uchafuzi wa plastiki, uvuvi usio endelevu na uharibifu wa makazi ya viumbe vya baharini.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania katika kipindi cha uongozi wake imesimamia hatua mbalimbali za kikanda, zikiwamo kukamilishwa kwa Itifaki ya Bioanuwai za Bahari na Pwani pamoja na Maeneo Yanayolindwa, Mpango wa Kikanda wa Kukabiliana na Mafuta Baharini na Mkakati wa Kikanda wa Plastiki na Kemikali Zinazohusiana nayo.
Masauni amewataka wajumbe kuhakikisha ripoti zinazojadiliwa zinazingatia ushahidi, huku maamuzi yatakayopitishwa yakiwa machache, yanayoeleweka na yanayotekelezeka.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maisha ya wananchi, usalama wa chakula, miundombinu yenye ustahimilivu na maendeleo ya uchumi wa buluu.
Amewataka pia washiriki kuhakikisha jamii za pwani, wanawake na vijana wanashirikishwa katika utungaji wa sera na uwekezaji unaohusu mazingira ya bahari.
Masauni amesema maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano wa 12 wa Mkataba wa Nairobi yatakuwa na athari katika afya ya bahari na ustawi wa wananchi kwa miongo ijayo.