Tanzania yatumia UNCCD COP17 kutafuta teknolojia na uwekezaji wa kurejesha ardhi

Tanzania yatumia UNCCD COP17 kutafuta teknolojia na uwekezaji wa kurejesha ardhi

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252
cece0efa-1b22-43f3-971c-905303ae1a17.jpg


Tanzania imesema ushiriki wake katika Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD COP17) unalenga kuimarisha juhudi za kurejesha ardhi iliyoharibika, kuhifadhi malisho na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya ukame.

Tanzania inashiriki mkutano huo unaofanyika katika Jiji la Ulaanbaatar, Mongolia, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akiongoza ujumbe wa Tanzania, alishiriki ufunguzi wa mkutano huo uliofanywa na Rais wa Mongolia, Khurelsukh Ukhnaa, Agosti 24, 2026.


Akizungumza katika mkutano huo, Mhandisi Masauni alisema kaulimbiu ya UNCCD COP17, “Restore Land, Restore Hope” (Rejesha Ardhi, Rejesha Matumaini), inasisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika urejeshaji wa ardhi, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame, pamoja na usimamizi endelevu wa maeneo ya malisho.

Aidha, alisema mwaka 2026 umetangazwa kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Wafugaji na Nyanda za Malisho, jambo linaloifanya ajenda ya Tanzania kuhusu uhifadhi wa malisho na ustawi wa wafugaji kuwa muhimu zaidi katika mkutano huo.

Mhandisi Masauni alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa ardhi kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo ukataji na uharibifu wa misitu, upanuzi wa mashamba kwa ajili ya kilimo, uchomaji moto usiodhibitiwa, mmomonyoko wa udongo, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi na upanuzi wa makazi.

“Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unatoa fursa ya kupata uzoefu, teknolojia, ushirikiano na rasilimali za kifedha kwa ajili ya kuimarisha usimamizi endelevu wa malisho, urejeshaji wa ardhi iliyoharibika, uhifadhi wa misitu, vyanzo vya maji na bioanuwai,” alisema Masauni.

Aliongeza kuwa hatua hizo pia zitasaidia kuongeza ustahimilivu wa jamii za wakulima na wafugaji katika kukabiliana na changamoto za kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.

Kwa upande wake, Afisa Kiungo wa Mkataba huo kutoka Tanzania, Thimoth Mande, alisema ushirikiano chini ya UNCCD unawezesha Tanzania kushughulikia kwa pamoja changamoto za uharibifu wa ardhi, upotevu wa bioanuwai na mabadiliko ya tabianchi badala ya kuzitazama kama changamoto zinazojitegemea.

Mande alisema ushiriki wa Tanzania katika COP17 si wa kuhudhuria mkutano pekee, bali pia ni fursa ya kuonyesha hatua ambazo nchi tayari imechukua katika kupambana na uharibifu wa ardhi, huku ikitafuta uwekezaji zaidi na teknolojia za kukabiliana na changamoto hiyo.

Alisema Tanzania inaweza kutumia matokeo ya mkutano huo kuhamasisha rasilimali kutoka katika mifuko mbalimbali ya mazingira na taasisi za kimataifa, zikiwemo GEF, IFAD, UNDP, FAO na UNEP, pamoja na sekta binafsi na mifumo bunifu ya fedha, ili kupanua miradi ya uhifadhi na urejeshaji wa ardhi kutoka maeneo maalum hadi maeneo makubwa zaidi.

Naye Meneja wa Kanda ya Mashariki na Kusini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Aminata Kirama, alisema baraza hilo lina jukumu la kufanya tathmini na tafiti katika maeneo yaliyobainishwa kuwa yanakabiliwa na changamoto za mazingira.

Mkutano wa UNCCD COP17 unatarajiwa kujadili hatua za kuimarisha urejeshaji wa ardhi, usimamizi wa malisho na kukabiliana na athari za ukame, huku Tanzania ikitumia jukwaa hilo kutafuta ushirikiano, teknolojia na rasilimali za kifedha kwa ajili ya kulinda mazingira na kuongeza ustahimilivu wa jamii.
 

Attachments

  • cece0efa-1b22-43f3-971c-905303ae1a17.jpg
    cece0efa-1b22-43f3-971c-905303ae1a17.jpg
    781.3 KB · Views: 7
Back
Top Bottom