Tanzania yawalenga wawekezaji wa Ujerumani kwa teknolojia, ajira

Tanzania yawalenga wawekezaji wa Ujerumani kwa teknolojia, ajira

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014

Serikali imesema uwekezaji kutoka kwa makampuni ya kigeni, hususan Ujerumani, haupaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa mtaji unaoingia nchini pekee, bali pia teknolojia, ajira na fursa kwa wafanyabiashara wadogo na vijana wanaojihusisha na teknolojia.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema hayo Septemba 16 jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na Waziri wa Shirikisho, Ulaya na Masuala ya Kimataifa wa jimbo la Hesse nchini Ujerumani, Manfred Pentz, aliyefika Tanzania akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka nchini humo.

Kapinga amesema ziara hiyo ni mwendelezo wa mkutano wa Invest Africa uliofanyika mwezi uliopita, ambapo Tanzania iliendelea kutafuta fursa za kuongeza biashara na uwekezaji.
Washiriki.png


Amesema katika kipindi hicho, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Ujerumani imeongezeka kwa asilimia 56, huku mauzo ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda nje yakiongezeka kwa asilimia 62.

“Tunachohamasisha ni biashara na viwanda. Tumezungumza masuala ya biashara, viwanda, dawa na fursa nyingine ambazo wafanyabiashara wa Ujerumani wanaweza kunufaika nazo,” amesema.

Kwa mujibu wa Kapinga, Tanzania tayari ina uwekezaji kutoka kampuni za Ujerumani, ikiwemo Knauf na Twiga Cement, hali ambayo amesema inaonyesha nafasi ya nchi hiyo katika uchumi wa Tanzania.

Amesema manufaa ya uwekezaji yanaonekana pia katika uhamishaji wa teknolojia, akitolea mfano sekta ya saruji ambako baadhi ya viwanda vinatumia teknolojia inayolenga kupunguza athari kwa mazingira.

“Capital investment, nini cha ziada tunanufaika sisi kwa wawekezaji hawa? Tunanufaika na mambo mbalimbali. La kwanza, teknolojia mpya ambazo zinatumika kwenye uwekezaji ambao uko ndani ya nchi,” amesema.

Ameeleza kuwa Twiga Cement, iliyopo Tanga, inatumia gesi asilia katika uzalishaji wa saruji badala ya makaa ya mawe yanayotumiwa na baadhi ya viwanda vingine.

“Kwa hiyo hata kuwa na teknolojia ambayo inatusaidia kutunza mazingira ni baadhi ya mambo ambayo tunanufaika nayo,” amesema.

Mbali na teknolojia, Kapinga amesema uwekezaji una mchango katika ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa kuwa kiwanda kinapozalisha bidhaa, huibua mnyororo mpana wa shughuli za kiuchumi.

Amesema mnyororo huo unahusisha usafirishaji, mawakala, wasambazaji na wafanyabiashara hadi bidhaa inapomfikia mlaji.

Vijana walengwa

Waziri huyo amesema Serikali pia inalenga kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanatumia fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo kupitia kampuni changa za teknolojia, maarufu kama startups.

Amesema biashara ya teknolojia imekuwa ikikua kwa kasi duniani na Serikali imekuwa ikiweka mazingira ya kuwawezesha vijana kuingia katika sekta hiyo.

“Tunapambana kwa ajili ya kufungua fursa kwenye mlengo huo na ndiyo maana suala la startup linapokuja. Tunaendelea ku-support startups kupitia initiatives mbalimbali,” amesema.

Kwa mujibu wa Kapinga, Serikali inashirikiana na wizara, taasisi mbalimbali pamoja na taasisi za fedha kufungua fursa kwa vijana ili teknolojia isitumiwe kwa mawasiliano pekee, bali pia kuwa chanzo cha kipato na ajira.

Ujerumani yalenga Afrika Mashariki


Kwa upande wake, Pentz amesema ujumbe wa wafanyabiashara wa Hesse umefika Tanzania kwa lengo la kujenga ushirikiano wa muda mrefu na wa kuaminika kati ya kampuni za Ujerumani, Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

Amesema Hesse ina nguvu katika sekta za dawa, digitalization, akili bandia (AI), fedha na usafirishaji, huku akieleza kuwa soko la Afrika lenye watu takribani milioni 350 katika eneo analolenga linaifanya Afrika Mashariki kuwa eneo lenye fursa.

Amesema moja ya maeneo wanayolenga ni ushirikiano katika teknolojia ya AI na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wawekezaji.png

“Tunataka kujenga ushirikiano wa muda mrefu na wa kuaminika, siyo kwa miradi binafsi pekee, bali na eneo zima kwa manufaa ya pande zote,” amesema.

Pentz amesema ziara hiyo inalenga pia kuifanya Hesse kuwa daraja la kuunganisha kampuni za Afrika Mashariki na soko la Ulaya.

Amesema baadhi ya kampuni za Hesse tayari zinafanya shughuli katika ukanda huo na ujumbe wa wafanyabiashara umeletwa ili kujenga juu ya mahusiano hayo.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni sehemu muhimu ya mafanikio ya pande zote, akisema Afrika ni bara lenye fursa nyingi na Ujerumani inalenga kuwa mshirika katika kuzitumia.

Tanzania: Soko la EAC, SADC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, amesema Tanzania ina nafasi ya kimkakati kwa wawekezaji kutokana na uanachama wake katika EAC na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema mwekezaji anayejenga kiwanda Tanzania anaweza kutumia nchi hiyo kama kituo cha kufikia masoko ya nchi nyingine za ukanda huo.

“Tanzania tupo EAC na tupo SADC. Ukiwekeza kiwanda Tanzania, kiwanda kinapeleka bidhaa mpaka South Sudan. Kuna nchi nyingi zinazotuzunguka,” amesema.

Amesema Serikali inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kutoka Ujerumani na nchi nyingine, akieleza kuwa mazingira ya diplomasia yaliyowekwa na Serikali yamechangia kuimarisha mahusiano ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Pentz amesema Tanzania ina soko linalokua na mazingira ya amani na usalama, mambo aliyoyataja kuwa miongoni mwa sababu zilizowavutia wawekezaji wa Ujerumani.

Ameeleza pia kuwa ziara yake ni sehemu ya safari ya kikanda inayohusisha majadiliano kuhusu AI, baada ya kutembelea Rwanda na Kenya.

Serikali yasisitiza sekta binafsi

Kapinga amesema Serikali inalenga kuhakikisha sehemu kubwa ya uwekezaji inatoka katika sekta binafsi, akieleza kuwa ndiyo sababu imeendelea kutumia mfumo wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).

Amesema katika kutathmini miradi, Serikali huangalia iwapo mradi una uwezo wa kupata fedha na kujiendesha kibiashara, au kama ni “bankable”.

Pia amesema Serikali imeendelea kuboresha sera na mazingira ya biashara, ikiwemo kuweka kalenda ya kodi ili kuongeza utabirika kwa wafanyabiashara.

Amesema changamoto za kodi bado zipo, lakini Rais Samia Suluhu Hassan ameunda kikosi kazi cha kushughulikia changamoto hizo.

Kapinga amesema Serikali haitaki kuvutia kampuni kubwa pekee, bali pia wawekezaji wadogo, huku ikilenga kupunguza urasimu katika masuala ya kodi na usajili wa biashara.
 
Back
Top Bottom