Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salaam za rambirambi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Kufuatia kifo cha Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani aliyefariki dunia leo katika hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam.
Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani amefariki dunia leo saa 2:05 Asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Rais Magufuli amempigia simu Jaji Mkuu wa Tanzania na kumpa pole baada ya kupata taarifa ya kifo cha Jaji Mkuu huyo Mstaafu.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Jaji Mkuu Mstafu Augustino Ramadhani, napenda kutoa pole kwako, familia ya marehemu, waheshimiwa Majaji wote pamoja na watumishi wa Mahakama ya Tanzania”, alisema Rais Magufuli.
Marehemu Jaji Augustino Ramadhani aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania mwaka 2007 mpaka mwaka 2010 alipostaafu.
Miongoni mwa nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu mwaka 2010 lakini pia mwaka 2014 aliteuliwa kuwa Rais wa Mahakama hiyo, wadhifa alioushika kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mwaka 2016 alipomaliza muda wake.
Marehemu Jaji Ramadhani pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais wa Awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Julai 4, 2012.
Mipango ya mazishi itajulikana baadaye.
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA BWANA LIHIMIDIWE.
Sent using
Jamii Forums mobile app