Mr Chopa,
Umefanya sivyo kumtukana.
Siwezi kukuhukumu lakini nadhani umeghadhibishwa na kule kuona kama vila kamdharau marehemu.
Si kitu.
Lakini kwako ilikuwa ni kumfahamisha kuwa marehemu alikuwa mama na mwalimu wetu ambae mfanowe haujapata kutokea Dar es Salaam na iitachukua miaka mingi kutokea mwalimu kama Bi. Bahia kwani ana wanafunzi katika familia moja kuanzia mume na mkewe na watoto wao na familia nzima wakawa wamesomeshwa Qur'an na yeye tofauti ikiwa ni miaka tu.
Baba na mama wamesomeshwa miaka ya 1950 na watoto miaka ya 1980 na wajukuu miaka ya 2000.
Madrasa ni ile ile na mwalimu ni yule yule na akisomesha bure.
Mwalimu Bahia ana wanafunzi kila pande ya dunia kuanzia Arabuni, Ulaya na Marekani.
Rambirambi nyingi zimepokelewa kutoka kwa wanafunzi wake kila pembe ya dunia na sasa hawa wanafunzi ni watu wazima na wamestaafu kazi.
Hakuna mtu aliyezaliwa Dar es Salaam ile ya 1950s na akakulia katika mazingira yale ambae hakuwa anamjua Mwalimu Bahia.
Mwalimu Bahia alikuwa anaingia katika nyumba za wakazi wa Kariakoo na kwengineko ama kwenye maulid au hakika ya mtoto au kwenye kufiwa.
Bi. Chiku mjukuu wa Bi. Chiku bint Said Kisusa kanitumia ujumbe ananambia kuwa, ''Mwalimu Bahia alikwenda hija na bibi yangu na waliporudi Mwalimu Bahia alikuja nyumbani kuniletea maji ya Zam Zam.
Kabla ya kunipa kunywa alinisomea dua ndefu sana na siku zote nikimpigia simu kuwa naumwa haipiti dakika teksi ishasimama nje ya nyumba yangu anakuja kunitazama basi hapo atanifanyia dua kisha ndiyo aniage.''
(Bi. Chiku bint Said Kisusa nimeweka paicha yake hapa akiwa uwanja wa ndege yeye na Bi, Tatu bint Mzee na Bi. Titi Mohamed wakimsindikiza Mwalimu Nyerere safari ya kwanza UNO 1955).
Hivi kwa mukhtasari hivi ndivyo alivyokuwa Mwalimu Bahia hadi umauti ulivyomfika.
Ndugu yetu hakuwa anamjua mwalimu na mama yetu Bi. Bahia na ndiyo fedhuli na dharau ile.
Tusimlaumu kwani Dar es Salaam ile si hii ya leo na si kila mtu kapitia malezi tuliyofunzwa sisi ya kuwa na subra, staha kwa umjuaye na usiyemjua.