SoC01 Tatizo kubwa katika Elimu yetu ni Elimu ya Msingi na Awali

SoC01 Tatizo kubwa katika Elimu yetu ni Elimu ya Msingi na Awali

Stories of Change - 2021 Competition

ego

JF-Expert Member
Joined
Apr 10, 2013
Posts
1,620
Reaction score
1,407
Katika lugha ya Kiswahili cha mitaani kitu kuoza maana yake ni kupitiliza mda wake wa matumizi au kupitwa na wakati. Katika makala hii mwandishi ametumia neno “elimu yetu imeoza” kuonyesha elimu yetu imepitwa na wakati na inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa sana.

Kwa historia elimu yetu iliasisiwa zamani sana kabla ya kuja kwa wakoloni katika jamii yetu. Enzi hizo taifa la Tanzania wala Tanganyika havikuwepo. Jamii zetu zilikuwa zikijitawala katika mfumo wa makabila kwa kila jamii kuwa na mtawala wake wa kikabila. Makabila mengi yalikuwa na utawala wao wa ki chifu na walikuwa na utaratibu wao wa kutoka mtawala mmoja na kuingia mtawala mwingine.

Katika zama hizo jamii nyingi zilikuwa na mfumo wao wa elimu uliohakikisha wanajamii wanapeana elimu hasa kwa vijana iliyowawezesha kufahamu majukumu yao katika jamii zao. Jamii nyingi zilitumia mifumo ya nyimbo, hadithi kwa watoto, jando na unyago kutoa maarifa katika jamii. Elimu iliyotolewa katika jamii katika zama hizo ambazo tunaweza kuziita kabla ya kuja kwa wamisionari ilitolewa katika madarasa maalumu yaliyoandaliwa kulingana na mazingira ya enzi hizo. Madarasa haya yalikuwa ni kama kuota moto jioni huku watoto wakisikiliza hadithi kutoka kwa bibi yao, mikusanyiko maalumu maporini ya jando na unyago.

Wamisionari walipoingia katika jamii yetu walileta elimu tofauti na elimu yetu ya jadi na elimu hii ilifundishwa katika madarasa maalumu yaliyojengwa. Wakoloni walipokuja waliendeleza elimu iliyoasisiwa na wamisionari na elimu hii ilitolewa kwa baadhi ya wanajamii kwa viupembele vya kikoloni. Elimu hiyo ililenga kutengeneza makarani na watumishi katika serikali ya kikoloni. Misingi mikuu ya elimu ya kikoloni ilikuwa ni mambo makuu matatu ambayo ni kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Enzi za ukoloni elimu yetu ya jadi iliendelea kuwepo katika jamii kama elimu isiyo rasmi iliyotolewa katika madarasa yasiyokuwa rasmi lakini ilikuwa na mchango mkubwa sana katika jamii kwani maarifa yake ndiyo yailiyosimamia mambo kama maadili ya wanajamii na mahusiano katika jamii. Wanajamii waliheshimiana kwa rika tofauti kutokana na elimu ya jadi tuliyorithi katika jamii zetu. Mahusiano na mapenzi yalisimamiwa sana na elimu ya jadi katika jamii.

Miaka ya sitini tulipopata uhuru tuliifanyia mabadiriko makubwa elimu yetu tuliyoirithi kutoka kwa wakoloni ili kuipa sura ya uhuru. Mitaala ilibadirishwa ili na kuingizwa elimu ya uhuru iliyolenga kulinda uhuru wetu. Elimu ya uhuru ilikuwa ni pamoja na elimu ya ujamaa na kujigemea iliyolenga katika kuwapatia watu wetu ujuzi wa kujigemea na kuondokana na fikra za kutegemea wakoloni, elimu ya historia ya ukoloni iliyolenga katika kuwafahamisha vijana madhira waliyoyapitia wazazi wao enzi za utawala wa kikoloni.

Enzi hizo mahitaji ya wasomi yalikuwa ni makubwa kuliko uwezo wetu wa kuzalisha wasomi na hii ilitupekea kuanzisha elimu ya watu wazima ikilenga katika kuzalisha watumishi wengi zaidi katika mda mfupi. Enzi hizo wahitimu wa elimu ya msingi walikuwa wakiingia makazini na kuajiriwa katika sekita mbalimbali. Haya yalitupeleka katika kuboresha mitaala ya elimu ya msingi ili iendane na mazingira hayo. Elimu ya msingi ilijumuisha masomo ya elimu za kati na juu ili kuwaandaa wahitimu kufanya kazi baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Wahitimu wa elimu hii ndiyo walioenda kufanya kazi na wengine kuwa walimu kurudi kufundisha wenzao na hili lilitengeneza mnyonyororo wa matatizo katika elimu yetu kwani wale waliotawakiwa kuboresha elimu hiyo nao walikuwa wameandaliwa katika mlolongo wa changamtoto.

Mda umebadirika, mambo mengi yamekwenda yakibadirika lakini jamii imebaki kugangania kufundisha mambo yaleyale ambayo yanaweza kuwa yamepitwa na wakati. Miaka kabla ya kuja kwa wakoloni jamii zetu waliwafundisha watoto wa kiume mbinu ya kulinda jamii pamoja na kuwinda, watoto wa kike walifundishwa jinsi ya kutunza familia, watoto wadogo walifundishwa historia ya jamii zao kupitia nyimbo na hadithi. Haya ndiyo mambo yaliyokuwa muhimu katika jamii enzi hizo.

Wakati wa ukoloni vijana walifundishwa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kuwa hayo ndiyo mambo ambayo mkoloni aliyahitaji. Baada ya uhuru vijana tuliwafundisha kusoma kuandika na kuhesabu kwa kuwa haya tuliendelea kuyahitaji, tuliwafundisha historia yetu ili wajue tulikotoka na kuwafundisha elimu ya ujamaa na kujitegemea kwa kuwa miaka hiyo tuliyahitaji hayo.

Miaka ya 2000 tumeendelea kuwafundisha watoto wetu mambo yale yale ambayo yalikuwa muhimu miaka ya 60, kujua kusoma, kunadika na kuhesabu kama ndiyo msingi mkuu wa maarifa ya elimu ya msingi. Katika haya tumejazia mambo mengine kutoka elimu ya kati na juu kutengeneza elimu ya msingi na matokeo yake ni tumejikuta tukitengeneza jamihi ya watu wazima wasiokuwa na maadili kwa kuwa hawakufundishwa misingi ya maadili, kuwa na jamii ya watu wazima wasiojua wale nini ili kulinda miili yao kwa kuwa elimu yao ya msingi haikuwafundisha misingi ya kula vizuri, hawajui umunimu wa kuchagua viongozi na njia sahihi za kuwachagua kwa kuwa hawana elimu ya msingi kuhusu uchaguzi.

Niliwahi kusoma makala moja ya afya katika mtandao wa BBC iliyosema “wakati vitambi ni ugonjwa unaowasumbua watu wasiosoma katika nchi za magharibi lakini kwa afrika vitambi imekuwa ni tatizo linalowakumba wasomi” kwamba elimu yetu inatengeneza maprofesa wasiojua waleje ili kulinda afya zao. Mtu mwingine alisema tunapokwenda katika siasa fikra zetu ziko sawa, iwe kuanzia kwa mhitimu wa darasa la saba mpaka maprofesa kama ni kulaumu viongozi sote tunalaumu yaleyale.

Hapa unachoweza kuona elimu yetu ina matatizo makubwa katika elimu ya awali na msingi. Huko ndiko tunatakiwa kujenga tabia za hulka kwani wataalamu wanaamini asilimia 90 ya tabia za mwanadamu hutokana na mafunzo na huku wataalamu wengine wakiamini samaki mkunje angali mbichi. Elimu ya msingi ndiko tunakotakiwa kujenga tabia na hulka za wanajamii wetu katika kutenda na kuwaza. Lakini kwa elimu yetu mambo ambayo kila mtanzania anatakiwa kuyajua hatuelezwi na tumerundikiwa elimu ya kitaalamu ya mambo ambayo si muhimu kwa kila mtu kuyajua ndiyo tumerundikiwa kama elimu ya msingi. Mfano tunamfundisha mtoto wetu mada ya chakula kuanzia darasa la kwanza lakini tunachowafundisha siyo waleje ili kulinda miili yao, siyo wale nini chenye afya kwao bali tangu darasa la kwanza tunawafundisha aina za makundi ya vyakula na kila kundi kutaja aina za vyakula husika. Tukienda katika mwili wa binadamu tunafundishwa kuchora figo, kuchora moyo na kuchora ubogo kwa kuweka sehemu zake zote vizuri katika mchoro lakini elimu ya kujua umuhimu wa viungo hivi katika miili yetu na je tufanye nini ili kuvitunza vizuri hatufundishwi na matokeo yake ni kuwa na wasomi wanaojua vizuri mambo katika taaluma zao lakini wanaoongoza kwa kuugua magonjwa ya Tabia. Unakuwa na mtoto aliyefundishwa masomo ya chakula tangu mdogo kabisa lakini bado anapendelea kula sana vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta mengi bila kuelezwa popote kuwa sukari na mafuta ni hatari kwa afya yake.

Hii ni mitaala ya elimu ya miaka ya 60 na 70 mpaka 80 ambako elimu ya msingi haikutumika sana kutoa elimu ya msingi “basic knowledge” bali ilitumika pia kutoa elimu ya kati na juu kwa kuwa ni wananchi wachache sana walifanikiwa kufikia elimu ya juu na hili ndilo limesababisha elimu hiyo kutolewa katika mika ya 2000 ambako wengi wanafikia elimu ya juu kunaonekana tunawalisha watoto wetu viporo vya elimu.

Nini kifanyike

  • Elimu ya jadi iliyokuwa ikitolewa katika jamii kutoa elimu ya maadili na mahusiano imetoweka kwa elimu isiyo rasmi kuchukuliwa na mitandao ya kijamii inayotoa elimu ya kigeni isiyojenga mambo haya. Ni wakati sasa wa mitaala ya elimu rasmi kuweka elimu ya mahusiano na maadili katika elimu rasmi ili kuchukua nafasi ya elimu ya jadi iliyotoweka.
  • Elimu imegawanyika katika makundi matatu, elimuya msingi, elimu ya kati na elimu yajuu. Ni wakati wa kuweka bayana malengo na majukumu ya kila elimu kwa kuweka elimu ya msingi kufundisha “basic knowledge” tu kwa kuondoa masomo ya elimu ya kati na juu katika mitaala ya msingi. Elimu ya watu wazima ambayo mpaka leo imebaki katika mitaala ya elimu ya msingi iondolewe kabisa na kurudishwa katika elimu za kati au juu tu.
  • Elimu isiyoaendana na wakati iondolewe kabisa katika mitaala. mfano moja ya athari za ukoloni ni kujenga kisaikolojia kuwa mtu mweupe ni bora kuliko mweusi. Miaka ya 60 na 70 tuliwafundisha watoto wetu historia ya ukoloni ili kukabiliana na tishio la ukoloni kurudi tena lakini kwa elimu ya ukoloni ilituletea shida ya vijana hata ambao hawakushuhudia utumwa kuendelea kuamini mtu mweupe ni bora kuliko mweusi kwa kuwa walisoma jinsi mtu mweupe alivyomtesa mtu mweusi wakiwa wadogo. Tishio la ukoloni wa nchi moja kuitawala nchi nyingine limeondoka ni wakati wa kuondoa elimu hii kwa watoto ili kutokuwajengea fikra za kujiona wao watu weusi ni duni ukilinganisha na watu weupe. Hakuna familia ambayo baba anachukua watoto wadogo na kuwaeleza jinsi alivyokuwa akipigwa na kuteswa na jirani na watoto wakamuona baba ni sawa na jiarani. Elimu hii wafundishwe watu wazima.
 
Upvote 2
Umenena vema, ni swala nyeti hili. Mabadiliko haya yakiambatana na mabadiliko ya mazingira ya utoaji wa elimu kusudiwa yatakuwa na tija zaidi
 
Back
Top Bottom