SoC02 Tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, tumefikaje hapa? Tunatokaje hapa?

SoC02 Tatizo kubwa la ukosefu wa ajira, tumefikaje hapa? Tunatokaje hapa?

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Jan 22, 2020
Posts
27
Reaction score
35
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekua na changamoto kubwa sana ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa elimu ya vyuo mbalimbali, iwe elimu ya juu au elimu ya ufundi. Vilevile kumekua na changamoto hii kwa vijana ambao kwa namna moja au nyingine, kutokana na sababu mbalimbali za kimaisha wameshindwa kupata nafasi ya kupata elimu ya juu au ufundi. Kwa bahati mbaya sana, tatizo hili la ukosefu wa ajira limekua likikua kila kukicha na hakuna matumaini ya hali kubadilika katika siku za usoni.

Tumefikaje hapa? Kwa ufupi kabisa, sababu mojawapo iliyotufikisha hapa ni kushindwa kubadilika na kuendana na mabadiliko ya nyakati/dunia. Ukisoma katika historia ya dunia na binadamu kwa ujumla, utagundua mabadiliko kutoka nyakati za mawe (stone age), nyakati za viwanda/mapinduzi ya viwanda (industrial age/industrial revolution), na nyakati za kidijitali (information age/computer age/digital age/new media age) ambazo ndio nyakati tulizopo sasa hivi.

Kimsingi, kila nyakati zilihitaji mwanadamu awe na maarifa sahihi kwa wakati huo ili aweze kufanikiwa kwenye nyakati hizo. Kwa mfano nyakati za mawe (stone age) mwadamu alilazimika kuwa na maarifa ya kuweza kutengeneza vifaa mbalimbali kwa kutumia mawe, ili kurahisisha maisha yake kwa wakati huo. Zikafika nyakati za viwanda/mapinduzi ya viwanda ambapo binadamu alilazimika kuwa na elimu ili kujipatia maarifa/elimu ya kuendesha viwanda.

Hivyo alilazimika kwenda shule ili kupata elimu/maarifa ya kuendesha viwanda hivyo. Na hizi ndio nyakati zilizoleta mfumo wa kusoma, kwa sababu wakati huo watu walipelekwa shuleni kusoma ili wapate maarifa ya kufanya kazi viwandani. Baada ya nyakati za mapinduzi ya viwanda, zikaja nyakati za kompyuta na kidijitali (digital age/computer age/ new media age/internet age). Kimsingi hizi ndio nyakati ambazo tupo sasa hivi, nyakati ambazo ili kufanikiwa unahitaji kuwa na taarifa/maarifa sahihi kwa wakati sahihi.

Tumefika hapa kwa sababu dunia ipo nyakati za intaneti/kompyuta, ila sisi bado tupo kwenye nyakati za viwanda. Nyakati za kusoma ili ukimaliza uajiriwe. Hasahasa, hili linaonekana wazi kwenye mitaala yetu ya elimu, ambayo ndio msingi wa mafanikio ya mwanadamu yoyote.

Tunasoma mambo yaleyale kwa mfumo uleule wa nyakati za mapinduzi ya viwanda. Matokeo yake ni mfumo wetu wa elimu unazalisha watu ambayo dunia haiwahitaji kwa nyakati za sasa. Ni wazi kabisa serikali na sekta binafsi haziwezi kuwaajiri wahitimu wote.

Lakini kama wahitimu hawa wangekuwa na maarifa sahihi yanayoendana na mahitaji ya dunia ya sasa, wangeweza kutumia fursa mbalimbali zilizopo duniani, kujikwamua na kuwa na machaguo mbalimbali, badala ya kutegemea ajira peke yake kutoka serikalini na sekta binafsi.

Tumefika hapa pia kwa sababu hatujawekeza kwenye ubunifu. Kumekua na vijana mbalimbali wamekua wakibuni vitu mbalimbali, hasa kwenye eneo la teknolojia, lakini vijana hawa wanakosa muongozo, usimamizi na uwezeshwaji ili kuendeleza ubunifu wao. Tumefika hapa pia kwa sababu hatujawekeza inavyotakiwa kwenye kilimo, sekta ambayo ina uwezo wa kuajiri vijana wengi sana.

Pia hatujawekeza kabisa kwenye vipaji, nikiwa na maana ya vipaji kama muziki, mpira wa miguu, ucheshi n.k. Hatuna mfumo maalum wa kutambua, kukuza na kulea vipaji mbalimbali, na hatimaye vikawa vikubwa na kuwa chanzo kikubwa cha ajira.

Tunatokaje hapa? Tunalazimika kubadilisha mitaala yetu ya elimu ili iendane na mahitaji ya dunia ya sasa, dunia inayobadilika haraka sana. Nitaelezea maeneo matatu ambayo kwa mtazamo wangu yanahitaji kutiliwa mkazo. Eneo la kwanza ni elimu ya ujasiriamali na biashara. Kama kuna eneo ambalo tunahitaji kuwapatia wanafunzi wetu maarifa ni hili.

Ili kuleta uhalisia, elimu hii inatakiwa ifundishwe na wafanyabiashara wakubwa ambao wanafanya kwa vitendo. Kuna tofauti kubwa sana ya kujifunza kutoka kwa mtu anayefanya kwa vitendo na asiyefanya kwa vitendo (nadharia). Hii itawasaidia wahitimu kumaliza na maarifa sahihi ya ujasiriamali na biashara, hivyo kuwa rahisi kwao kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine. Eneo lingine ni elimu ya fedha (financial education/literacy).

Nakuhakikishia ndugu msomaji, kuna elimu ya fedha ambayo watu waliofanikiwa kifedha wanayo ila wengi sana hatunayo. Kuna umuhimu sana wa kufahamu namna fedha inavyofanya kazi. Hii itasaidia sana upande wa kufanya maamuzi sahihi juu ya fedha kwenye eneo la biashara na uwekezaji. Nashauri pia elimu hii itolewe na watu waliofankiwa kifedha, kwa sababu kuna mengi ya kujifunza kutokana na uzoefu wao. Eneo lingine ni eneo la elimu na maarifa ya kompyuta na kidijitali (computer and digital skills).

Tunaishi kwenye dunia ambayo unachofahamu (taarifa/maarifa) ndio kitaamua ufanikiwe kwa kiwango gani. Bila maarifa ya kidijitali na kompyuta ni ngumu kufikia vyanzo vya taarifa na maarifa sahihi. Katika kufanikisha hili kwa ufanisi, tunalazimika kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wetu elimu ya maarifa ya kidijitali na kompyuta kuanzia ngazi ya elimu ya msingi kabisa. Hii itawasaidia kuhitimu wakiwa na maarifa ya kutosha yatakayowasaidia kutafuta taarifa na maarifa mbalimbali yatakayoweza kuwakwamua kiuchumi. Pia tunalazimika kuwawezesha vijana wabunifu kukuza ubunifu wao mbalimbali.

Ubunifu huu ukikuzwa na kuendelezwa utakua chanzo cha ajira kwa wabunifu wenyewe na pia kwa vijana wengine. Vilevile tuna haja ya kuchukua hatua za makusudi kuwekeza kwenye kilimo, hapa nchini kilimo kinadharaulika na kuonekana kama shughuli ya kimaskini, lakini kwa wenzetu wakulima ni matajiri sana. Tuna ardhi, vyanzo vya maji, tunahitaji tu uwekezaji wa kutosha kiteknolojia na kutafuta masoko ili kufaidika na sekta hii. Lakini pia tunalazimika kuweka mfumo maalumu wa kutambua, kukuza na kulea vipaji mbalimbali.

Hili ni eneo ambalo tunapaswa kulitazama kwa jicho la tofauti kabisa, kwa sababu ni eneo ambalo linaweza kuajiri vijana wengi sana bila kujali kiwango cha elimu. Tuna vijana wengi sana wenye vipaji mbalimbali, hasa muziki na mpira wa miguu. Ni vipaji ambavyo kama vitakuzwa na kulelewa vitawafikisha mbali sana na kutengeneza ajira kwa wao na vijana wengine wengi.

Tuna mifano michache hapa kwetu, msanii Diamond Platmumz kupitia muziki wake amefanikiwa kuwashika mikono wasanii wengine na kuwafanikisha, pia ametengeneza ajira kwa msururu wa watu. Kuna Mbwana Samatta ambaye kupitia mpira wa miguu, amefaniwa kimaisha. Tujiulize, kuna akina Diamond Platnumz na Mbwana Samatta wangapi huko mtaani? Mimi ninaamini wapo wengi sana, wanahitaji tu kusaidiwa kutambua vipaji vyao, kukuzwa na kulelewa ili wafike hatua walizofika hawa niliowataja na pengine kupiga hatua zaidi yao.

Serikali kama mdau wa kwanza wa maendeleo ya nchi na watu wake, ina nafasi kubwa na wajibu wa kutekeleza niliyoeleza ili kupunguza tatizo hili, kwa kadiri itakavyoona inafaa. Nawasilisha!
 
Upvote 0
Back
Top Bottom