Dr PL
JF-Expert Member
- Sep 13, 2024
- 327
- 537
Picha kwa hisani ya Google
Kuota matiti kwa mwanaume (Gynecomastia) ni kuongezeka ukubwa/ujazo wa matiti kwa mwanaume. Hutokana mabadiliko ya viwango vya homoni za kiume (Testosterone) na homoni ya kike (Estrogen) kwa mwanaume [hormonal imbalance] ambapo mwanaume anakuwa na viwango vya juu vya homoni ya Estrogen ambayo kazi yake ni kuchochea matiti kukua na kuongezeka ukubwa.
Tatizo hili huwapata watu wa jinsia ya kiume wa umri wowote. Mara nyingi huonekana utotoni, wakati wa kubalehe na uzeeni (miaka 50+).
Kuota matiti kwa mwanaume (Gynecomastia) inaweza isiwe na athari zozote kiafya lakini humfanya mwanaume kuwa na mwonekano wa tofauti na kukosa kujiamini kama mwanaume. Hata hivyo kuwa na uvimbe kwenye matiti huhitaji uchunguzi zaidi ili kutofautisha na saratani ya matiti. ( Saratani ya matiti kwa mwanaume ni nadra).
Visababishi:
(1). Visababishi vya asili (natural causes).
👉Viwango vya juu vya homoni ya Estrogen hufanya homoni ya kiume (testosterone) kuwa chini hivyo kusababisha kuota matiti.
Hii hutokea katika vipindi fulani vya maisha ya mwanaume kama vile:
(a). Wakati wa utoto: kuna baadhi ya watoto wa kiume ambao huzaliwa wakiwa na matiti makubwa, hii hutokana na kuingiliwa na homoni ya Estrogen akiwa tumboni mwa mama yake. Hali hii huisha yenyewe bila matibabu wiki chache baada ya kuzaliwa kutokana na kiasi cha homoni ya Estrogen kupungua na kuwa katika viwango sahihi.
(b). Wakati wa balehe: wakati wa kubalehe kwa mvulana kunakuwa na mabadiliko makubwa ya homoni mbalimbali. Mwanzoni mwa balehe baadhi ya wavulana hushuhudia kuongezeka ukubwa wa matiti kutokana na kupanda haraka kwa viwango vya homoni ya Estrogen ukilinganisha na testosterone. Hali hii pia huisha yenyewe kati ya miezi 6 hadi miaka miwili (2) baada ya kubalehe.
(c). Uzeeni: kuanzia miaka 50 na kuendelea baadhi ya wanaume huota matiti hasa kutokana na mwili kuzalisha kiwango kidogo cha homoni ya testosterone kutokana na umri mkubwa au kwa sababu ya matumizi ya aina fulani za dawa.
👉Unene uliopitiliza: kutokana na na unene uliopitiliza mafuta hujaa kwenye matiti na hivyo kuongezeka ukubwa.
(2). Visababishi vingine:
👉Magonjwa: kuota matiti kwa mwanaume inaweza kuwa dalili ya magonjwa fulani mwilini mfano: magonjwa ya ini, figo au korodani; uvimbe kwenye tezi fulani mwilini, viwango vya chini vya homoni ya kiume-testosterone (male hypogonadism), magonjwa ya dundumio (thyroid gland disorders). Hata hivyo hali hii huambatana na dalili zingine za magonjwa hayo.
👉Matumizi ya aina fulani za dawa na madawa ya kulevya. Kuna baadhi ya dawa ambazo mwanaume akitumia humsababishia maudhi madogomadogo kama kuota matiti (gynecomastia).
Matibabu:
Ili kutibu ni lazima kisababishi kijulikane na kukishughulikia.
Mfano kama kisababishi ni matumizi ya aina fulani za dawa basi ni vyema kuacha kutumia hiyo dawa husika au kupatiwa dawa mbadala ambayo haina athari kama hizo.
Kama ni unene uliopitiliza basi kupunguza uzito inaweza kusaidia kupunguza na kuepuka hali hiyo au kisababishi ni ugonjwa basi utibiwe.
Kuna baadhi ya wanaume ambao hali hii huisha yenyewe bila matibabu lakini wengine hasa wenye viwango vya chini sana vya homoni ya kiume-testosterone huhitaji matibabu zaidi. Kwa hiyo ni muhimu kufika hospitalini kwa daktari kwa ajili ya uchunguzi, vipimo na matibabu sahihi.