Mgogoro wa TBL, SBL watinga bungeni
Thursday, 29 October 2009 16:42
Na John Daniel, Dodoma
MBUNGE wa Busega, Bw. Raphael Chegeni (CCM), amemtaka Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kueleza kama anatambua mvutano wa kibiashara uliopo kati ya kampuni mbili za bia, Serengeti Breweries (SBL) na Tanzania Breweries (TBL) unaotishia amani ya nchi.
Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni jana, Bw. Pinda alikiri kuwepo kwa mvutano huo na kwamba tayari amekutana na baadhi ya wahusika akiwemo Jaji Mark Bomani (Mwenyekiti wa Bodi ya Serengeti) na kuzungumzia tatizo hilo.
Katika swali lake la nyongeza Bw, Chegeni, alimtaka Bw. Pinda kuona umuhimu wa kushughulikia suala hilo kwa karibu na hatua zaidi kuchukuliwa haraka kwa kuwa moja ya washindani hao ameagiza kungolewa kwa mabango ya mshindani mwezake kwa kuyapiga mawe, jambo ambalo ni kinyume na ushindani wa kibiashara na hatari kwa amani
na utulivu wa nchi.
Bw. Pinda alisema serikali haiwezi kuingilia kati tatizo hilo moja kwa moja kwa kuwa ipo mamlaka iliyoundwa kisheria kwa lengo la kushughulikia ushindani wa haki katika biashara bali serikali inaweza kuingilia kati pale tu inapojiridhisha kwamba tume hiyo ya ushindani imeshindwa kumaliza tatizo hilo.
Mgogoro huo umekuwa wa muda mrefu na hivi karibuni iliripotiwa kuwa kampuni mojawapo imewahonga baadhi ya wamiliki wa baa ili wasiuze bia za washindani wao.
Source: Gazeti la Majira
My Take:
TBL wamechemka vibaya mno katika mbinu yao hii chafu ya kupambana na ushindani unaotolewa na SBL.Tutegemee haki itatendeka katika kulishughulikia suala hili.FCC waachwe wafanye kazi yao kwa uhuru maana inavyoelekea SIASA inaanza kuchukua mkondo wake kwenye hili(wanasiasa washavamia tayari).Tutegemee maamuzi ya HAKI kutoka FCC na si vinginevyo...TBL wamefulia mbaya zama hizi(kwa mtizamo wangu)