Zitto kupokelewa Dar kama shujaa
2007-08-16 10:00:05
Na Richard Makore, Lucy Lyatuu na Raymond Kaminyoge, Dodoma
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeandaa mapokezi makubwa kwa ajili ya kumpokea �shujaa� wao, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe aliyesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge.
Hali kadhalika wanaharakati kutoka mashirika 60 yasiyokuwa ya kiserikali na viongozi wa vyama vya siasa wamesema Bw. Zitto ni shujaa anayestahili kupongezwa kutokana na kusimamishwa kwa kile wanachoamini kwamba alikuwa anatetea maslahi ya taifa.
Mbunge huyo alisimamishwa kazi juzi na kutakiwa kutojihusisha na shughuli za Bunge hadi Januari 2008 kwa kile kilichodaiwa kuwa alilidanganya Bunge kutokana na kauli yake dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi kuwa aliingia mkataba wa madini nje ya nchi kinyume cha taratibu.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, Bw. John Mnyika alisema, Bw. Zitto anastahili pongezi kwa kuwa ni watu wachache wa aina yake wenye ujasiri wa kusema maneno kama aliyoyasema kwa ajili ya maslahi ya taifa.
``Na mimi naungana na Bw. Zitto kwamba Waziri Karamagi alilidanganya Bunge na kusaini mkataba wa madini bila maelezo ya kueleweka,`` alidai.
``Tukiwa kama viongozi vijana wa CHADEMA tunaandaa utaratibu wa kumpokea mbunge huyo pindi atakaporejea jijini kwa shangwe kubwa kutokana na uhodari wake wa kutetea maslahi ya taifa,`` alisema Bw. Mnyika.
Aliongeza kuwa watautangazia umma juu ya utaratibu utakaotumika katika mapokezi hayo ili kumpa moyo na kumtaka kuendelea kupambana na maovu mbalimbali yanayofanywa na serikali bila kukatishwa tamaa.
Aidha, Bw. Mnyika alisema, Sekretarieti ya chama hicho ilikutana kuanzia jana kujadili adhabu aliyopewa mbunge wao ili baadaye waweze kuitolea tamko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi Bw. James Mbatia alimtaka Bw. Zitto kutokata tamaa kwani ipo siku ukweli utajulikana kwa kuwa serikali haiwezi kuwadanganya wananchi wanaofahamu ukweli siku zote.
Unaweza ukawadanganya watu kwa muda tu lakini huwezi kuendelea kuwadanganya siku zote, alisema
Bw. Mbatia alilitaka Bunge kuzungumzia maslahi ya wananchi badala ya kujiingiza katika itikadi za kisiasa.
Aliwashutumu wabunge wa CCM kwa madai kuwa walimkandamiza Bw. Zitto bila sababu za msingi na kwamba hiyo imeonyesha picha halisi ya wabunge wa CCM kwa jinsi wanavyolindana badala ya kulinda maslahi ya taifa.
Aliwataka Watanzania kuwahukumu wabunge hao kwani hawajali maslahi ya waliwaochagua bali wanatekeleza matakwa ya itikadi za chama chao.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) Bw. Wilfred Lwakatare alisema, hiyo ni changamoto kwa Watanzania kuona walipeleka watu wa aina gani kuwawakilisha huko Bungeni.
Aliongeza kuwa hiyo ni changamoto pia kwa CCM kusoma alama za nyakati na kujiuliza wanayoyafanya kama ndiyo waliyotumwa kwenda kuyafanya bungeni.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mashirika 60 yasiyokuwa ya kiserikali, Bw. Tundu Lissu alisema, utaratibu uliotumika kumuadhibu umekwenda kinyume na kanuni za Bunge.
Alisema uhuru wa kuzungumza uliotolewa na Katiba uheshimiwe na Bunge litekeleze wajibu wake kikatiba wa kusimamia na kuhoji serikali.
Hata hivyo alilitaka Bunge kukomesha ushabiki wa kisiasa katika kujadili maslahi ya umma na vikao viendeshwe kwa ustaarabu na kuheshimiana.
Alidai kwamba utaratibu uliotumika kumuadhibu Bw. Zitto ulikuwa batili na kwamba adhabu hiyo sio halali na hivyo akalitaka Bunge kumruhusu mara moja kuendelea na vikao vyote vya Bunge.
Wakati huo huo, baadhi ya Wabunge wamesema haki haikutendeka kumsimamisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, bali walikuwa na nia ya kuidhoofisha kambi ya upinzani.
Wakizungumza na Nipashe jana, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Gando (CUF), Bw. Khalifa Khalifa, alisema kitendo hicho kina lengo la kuua demokrasia.
``Walikuwa na nia ya kuwanyamazisha wapinzani wasihoji mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali,`` alidai.
Alisema Bw. Kabwe alitaka kuundwa kwa kamati teule baada ya kuona kuna utata katika mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi lakini badala ya kamati teule kuundwa wameamua kumsimamisha.
``Utajuaje nani mwongo kati ya Zitto na Waziri wa Nishati na Bw. Nazir Karamagi, wakati amewasilisha hoja binafsi kutaka uchunguzi ufanyike, lakini badala ya kuunda kamati unamsimamisha, hapo bado kuna utata,`` alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Bi. Suzan Lyimo, alisema Mbunge huyo ameponzwa na kuibua hoja inayolenga maslahi ya taifa.
Alifafanua kuwa kinachosikitisha wabunge wengi wako Bungeni kwa itikadi ya vyama vyao badala ya kusimamia maslahi ya wananchi.
Aliongeza kuwa uamuzi wa Bw. Zitto kuwasilisha hoja hiyo alikuwa anataka iundwe tume ili ajiridhishe yeye na Watanzania wengine kuhusu utata anauona katika mkataba huo.
Alisema bila ya kuwa na wapinzani wengi Bungeni hali itaendelea kuwa mbaya kwa sababu itikadi ya vyama imetawala Bunge.
Alisema hakukuwa na uharaka wowote kwa Waziri Karamagi kuifuata kampuni ya Barrick nchini Uingereza ili kusaini mkataba wa Buzwagi.
Aliendelea kusema hata kama hakuna sheria inayokataza kusainia mkataba nje ya nchi, bado suala zima limezungukwa na mazingira ya utata.
``Kama suala la kumsimamisha Mbunge huyo kwa kusema uongo ilitakiwa kamati iundwe ili wote wawili wachunguzwe na ukweli ungepatikana, lakini wameona bora wamnyamazishe kwa kumsimamisha,`` alilalamika kwa masikitiko.
Mbunge wa Bukene (CCM), Bi. Teddy Kasela Bantu, alisema kwa kufuata kanuni za Bunge zilizopo, Mbunge huyo alistahili adhabu aliyopata.
Alisema hata kama idadi ya wabunge wa upinzani na wa chama tawala ingekuwa sawa kanuni zingefuata na angepata adhabu aliyopewa.
Akichangia juzi jioni, Mbunge wa Mtera (CCM), Bw. Samwel Malecela alisema Bw. Zitto ni lazima apewe adhabu kali kwa kumvunjia heshima Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwita mwongo na kwamba mdharau mwiba mguu huota tende.
Alisema wale wote watakaoiga tabia za mbunge huyo nao watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.