*Wakosoa jibu la Waziri kuondoa shutuma
*Wanasiasa wasema Zitto ameibuka shujaa
*Mwenyewe asema hatakubali, atakata rufaa
Na Waandishi Wetu
SIKU moja tu baada ya kukabiliwa na adhabu ya kusimamishwa kuhuduria vikao vya Bunge kwa takribani miezi mitano, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) amejizolea umaarufu mkubwa na baadhi ya wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaifa wamemchukulia kama shujaa kutokana na msimamo wake.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wananchi mbalimbali, mmoja mmoja, taasisi na vyama vya siasa, wameelezea kutoridhishwa na hatua iliyochukuliwa dhidi ya mbunge huyo na kusema hatua hiyo haikuwa ya haki na inakandamiza uhuru na demokrasia Tanzania.
Profesa Mwesiga Baregu, mhadhiri mwandamizi wa masuala ya siasa na ushirikiano wa kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema uamuzi wa Bunge kumsimamisha Kabwe kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge haujamtendea haki.
Akizungumza na Mwananchi, ofisini kwake jana, Profesa Baregu alisema kwa kitendo hicho, Bunge halikumtendea haki Kabwe, halikutenda haki kwa demokrasia na pia halikutenda haki kwa wananchi.
Alisema kumwadhibu mbunge huyo hakujaweza kuondoa ukweli kwamba kuna mikataba mibovu inayoingiwa na serikali na suala la Buzwagi ni mfano tu kati ya mikataba mingi mibovu iliyoingiwa, hasa ya madini.
Wabunge wengi wanaonyesha kuwa hawana utashi wa kulinda maslahi ya wananchi na ndiyo maana wakakataa kuunda kamati kujadili suala lile muhimu,? alisema Profesa Baregu.
Alisema kuzimwa kwa jambo lile bungeni si dawa na wala kumuadhibu Kabwe kwa kuonyesha uzalendo wake hakusaidii kuliziba tatizo bali kilichofanyika ni kudhihirisha tu kwamba Bunge limetumika kuisigina demokrasia.
Profesa Baregu alisema kimsingi maswali ya Kabwe hayajajibiwa kwani jibu la kuwa kulikuwa na ulazima wa kuharakisha mkataba si jibu lenye mantiki.
Naye Dk Mohamed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema alichofanya Kabwe ni kutoa shutuma na njia muafaka ni anayeshutumiwa kutoa hoja mbadala na kuonyesha kwamba shutuma zilizotolewa si za kweli.
Alisema hilo ni jambo la kawaida hata katika uvumbuzi wa kisayansi, kinachoanza ni kuwa na wasiwasi na kitu, dhana ndiyo huzaa ukweli, sasa hakukuwa na ubaya wowote kuiacha dhana kujadiliwa ili hatimaye ukweli upatikane.
?Jibu la Waziri peke yake halijatosha kuondoa shutuma na kwa kweli kilichotendeka ni sawa na kuwazuia watu kusema. Kitendo kilichotendwa dhidi ya Kabwe ni cha aibu kwa Spika na hata kwa Bunge,? alisema Dk Bakari.
Umoja wa vyama vya upinzani mkoa wa Arusha, umempongeza Kabwe kwa kutoa hoja binafsi ya kutaka kuundwa kamati ya kuchunguza kusainiwa mkataba wa mradi wa madini ya Buzwagi wilayani Kahama na umemkaribisha mkoani Arusha kuzungumza na wananchi.
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amepinga hatua iliyochukuliwa na Bunge kumsimamisha Kabwe na kudai kuwa adhabu hiyo ni ya ukandamizaji wa demokrasia nchini.
Mbatia alisema pia kuwa hiyo ni picha halisi kuwa Bunge chini ya Spika Samwel Sitta, limekuwa ni la kuwaburuza wapinzani na pia kumlaumu Spika kwa kuruhusu kuingiza mjadala wa kiitikadi katika Bunge, suala ambalo alisema si sahihi.
"Zitto Kabwe ni shujaa, ninavyomjua mimi si mropokaji hata siku moja, lakini amedhihirisha pia ushujaa kwa kusimamia lile analoliamini mpaka dakika ya mwisho, adhabu aliyopewa haikufuata kanuni na misingi ya haki za binadamu kujitetea, ni maonevu ambayo yameweka kovu lisilofutika kwa makundi ya demokrasia," alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji Christopher Mtikila pia ameungana na wenzake akisema Zitto hana kosa, adhabu aliyopewa ni uharamia wa demokrasia na suala ambalo kila Mtanzania anatakiwa kulitambua na kutotakubali kukaa kimya.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kutokea Mwanza, Mchungaji Mtikila alisema tayari ameshazungumza na mwanasheria wake aliyeko Dar es Salaam ambaye anaandaa kusudio la kupinga adhabu hiyo ili kulifikisha Mahakama Kuu mapema iwezekanavyo.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Wilaya ya Arusha, Calist Lazaro, alisema licha ya kumwalika Kabwe kwenda Arusha kuzungumza na wananchi, juu ya hoja hiyo na watamuandalia mapokezi makubwa. ?Tayari tunajipanga kumpokea aje Arusha kwani wabunge wa CCM hawajamvua ubunge, sisi tutaendelea kumpa heshma yake.
Kwa upande wa Asasi za kiraia zimesema utaratibu uliotumika kumwadhibu Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, ni batili kwa maelezo kuwa haukufuata maadili wala kanuni za Bunge.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa taasisi hizo jana, Wakili wa Kujitegemea, Tundu Lissu, alisema adhabu iliyotolewa kwa Kabwe sio halali, huku akitaka mbunge huyo aruhusiwe kuendelea na vikao vyote vya Bunge.
Lissu alisema ni bora Bunge likaeleza mbunge huyo amepewa adhabu ya ngapi ili wananchi walinganishe na kufahamu adhabu ambayo ilikuwa inastahili kulingana na kosa, kama analo.
Naye Gema Akilimali wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), alisema Bunge sasa limegeuka kuwa serikali na siyo mhimili wa tatu wa serikali kama ilivyokuwa hapo mwanzo.
Spika aueleze umma, je Bunge lipo au halipo kwani, linatetea serikali badala ya wananchi hii ni ajabu!? alisema Akilimali.
Pia alipendekeza Bunge lielewe kuwa adhabu ya Zitto ni dhidi ya wananchi wa Kigoma Kaskazini kwani, kutokuwa na mwakilishi katika vikao viwili vya bunge ni hasara kubwa kwao.
Mbali na mahojiano na makundi hayo ya wanazuoni na viongozi wa kisiasa, wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, wametuma barua pepe na wengine kupiga simu chumba cha habari, wote wakilaani kusimamishwa kwa Mbunge huyo.
Wakati huo huo Kabwe ametangaza azma ya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga adhabu ya kusimamishwa kujishughulisha na shughuli zote za Bunge hadi Januari mwakani kwa madai kwamba ameonewa.
Akizungumza na Mwananchi jana, Zitto alisema anawasiliana na mwanasheria wa chama chake, Tundu Lissu, pamoja na wanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuiomba mahakama uwezekano wa kuipitia upya hukumu aliyopewa na Bunge.
Alisema adhabu aliyopewa ni ya uonevu kwa kuwa kanuni ya Bunge namba 59 iliyotumiwa kumpa adhabu hiyo, haihusiani na masuala ya adhabu, badala yake ilipindishwa makusudi ili kumkomoa.
Zitto alisema kanuni hiyo inahusu masuala ya amani na usalama bungeni tofauti na ilivyotumiwa na Bunge kumuadhibu.
"Walipindisha kanuni kunikomoa, wameshindwa kuthibitisha uongo wangu, najua nafsi zao zimejuta kwa sababu nimeibua uozo unaofanywa. Nitashtaki pia kwa wananchi, waamue la kufanya," alisema Zitto.
Alisema adhabu hiyo pia haikutokana na Spika bali na Bunge, kinyume na kanuni za Bunge.
Hata hivyo, Zitto alisema pamoja na adhabu aliyopewa, moyo wake ni mweupe kwa kuwa ametimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha analinda raslimali za nchi.
"Nimefanya kazi ambayo Mbunge anatakiwa kuifanya. Wengi walikuwa hawajui kama kuna mkataba uliosainiwa kimya kimya na serikali London. Hata wabunge walioshinikiza niadhibiwe pia walikuwa hawajui hilo," alisema Zitto.