Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amemkosoa hasimu wake Jose Mourinho kocha wa United na kuimwagia sifa tele Tottenham.
City wanaongoza kwenye msimamo wa ligi ya Uingereza kwa tofauti ya alama 11 baada ya kushinda mechi 16 kati ya 17, ikiwa ni pamoja na mechi ya Jumapili jijini Manchester.
Timu ya Guardiola itaikaribisha Tottenham Jumamosi na ushindi mwingine utawawezesha kuwa mbele ya Spurs kwa tofauti ya pointi 21.
Akiwasifia wachezaji wa Mauricio Pochettino na Chelsea, Guardiola alionekana kumchambua tena Mourinho na United.
"Nadhani Tottenham na Chelsea ni timu nzuri zinazotaka kucheza mpira," Muhispania huyo alisema, akinukuliwa na Mirror.
"Hawawategemei wengine [kucheza], wanataka kutengeneza mchezo wao wenyewe, na ni mtihani mwingine kwetu siku tatu baada ya kucheza Swansea.
"Baada ya hapo, tutaikabili Leicester Kombe la Carabao. Hakuna muda mwingi wa kupumzika lakini tupo tayari kuikabili Tottenham na kuendeleza kiwango ambacho tumeonyesha mara ya mwisho."
City wamefunga magoli 52 kwenye mechi 17 msimu huu, wakipewa sifa tele kwa mfumo wao, wakati United ya Mourinho inakosolewa kwa namna ya uchezaji wa timu yake licha ya kushika nafasi ya pili.