The Only Thing We Have to Fear is Fear itself

The Only Thing We Have to Fear is Fear itself

Freeman Mbowe
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/2/14/makala3.php

KAMA ilivyo kawaida, ukiandika ukatoa hoja, tarajia maswali, pongezi na hata kejeli kutoka kwa wasomaji. Majibu yatategemea aliyeguswa kaguswa vipi.

Leo, nitajikita kwenye swali moja ambalo nimeulizwa.

Waungwana wamesema: "Mbowe tumekusikia na kukusoma hoja zako kuhusu mustakabali wa nchi yetu; sasa tufanye nini?"

Nashukuru kwa changamoto hii. Kama Mtanzania na zaidi kama kiongozi, nina wajibu wa kuweka fikra zangu wazi. Wenye hekima na busara wazitafakari. Wenye husuda wabeze!

Mawazo yangu si msaafu. Ni fikra mbadala ambazo zinakusudia kujenga hoja mjadala.

Ninaamini wako Watanzania wengi wenye uwezo mkubwa sana wa uongozi. Lakini mfumo wetu hauwapi fursa.

Sasa si siri, nchi yetu imekwama. Ni dhahiri Rais Jakaya Kikwete amelemewa. Yeye hataki au pengine hana ujasiri wa kukiri kuwa chama anachokiongoza hakina jibu la umaskini wa Watanzania.

Taifa lolote lililokwama linahitaji mabadiliko. Mabadiliko hayo huweza kuja kwa njia mbili. Ama kwa mtindo wa kutumia nguvu, yaani mapinduzi (revolution), au kwa mtindo wa amani, yaani mageuzi (reforms).

Ni dhahiri kuwa Watanzania wanapendelea mabadiliko kwa njia ya amani, yaani ‘reforms'. Tangu tumepata uhuru, Tanzania imefanyiwa ‘majaribio' mengi sana ya kisiasa, kijamii na hata ya kiuchumi, lakini ‘majaribio' haya hayakutukwamua. Bado tumekwama.

Yako maeneo machache tuliyopiga hatua kama taifa. Lakini mafanikio machache tuliyopata hayalingani na utajiri wa asili wa nchi yetu. Aidha, hayalingani kabisa na umri wa miaka 46 ya uhuru wetu.

Ni kweli subira huvuta heri, lakini subira inapoendelea kutumbukiza taifa kwenye lindi la umaskini, subira hii hukaribisha shari!

Ni rahisi kufikiria kuwa kukwama kwetu leo ni tunda la ufisadi wa viongozi. Ni kweli hili linachangia. Tukumbushane historia kidogo.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliongoza taifa hili kwa miaka 25. Alikuwa kiongozi aliyependwa sana na watu. Hakuwa fisadi na wala serikali ya awamu yake haikuwa ya kifisadi. Pamoja na uadilifu wa Mwalimu, bado nchi hii, ilikwama sana kiuchumi na hivyo kimaendeleo!

Kama taifa, tuna wajibu wa kutafakari tumekwama wapi? Ni dhahiri kuwa kutokomeza ufisadi pekee si suluhisho pekee la kuipeleka nchi yetu kwenye neema. Na wakati mwingine nimekuwa nikihoji: ‘Je, inawezekana amani yetu tunayojivunia ndiyo sababu ya kukwama kwetu?'

Sihitaji kujadili utajiri wa Tanzania. Wote tunaujua.

Katika kujadili kukwama kwetu na kupendekeza suluhisho, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, nilizungumza kwa nguvu kubwa mambo kadhaa.

Leo nitaanza kujadili machache ya msingi kama changamoto kwa Watanzania. Nilijenga hoja:

Kwamba mfumo wetu wa utawala ndiyo chimbuko la umaskini na kukwama kwetu.

Kwamba hata ukimleta ‘malaika' ukamweka Ikulu awe Rais wa Tanzania, kwa mfumo wetu wa utawala uliopo, lazima atakwama!

Kwamba utajiri wetu wa asili ndio utatumika kama chanzo cha kubomoa mshikamano wa taifa.

Kwamba, kwa matendo ya watawala wetu, ni wazi kwamba wamemsahau Mungu!

Kwamba amani yetu ni tete!

Sera iliyosikika sana wakati wa uchaguzi ni ile ijulikanayo kama sera ya majimbo. Sera hii ilikusudia (na inakusudia) kujibu hoja na hofu yetu kuwa mfumo wetu wa utawala ndio msingi wa kukwama kwetu.

Mada hii ni ndefu. Nakusudia kuijadili kwa kina na kwa mapana yake katika mfululizo wa makala kadhaa.

Niliamini niliyozungumza wakati ule. Bado nayaamini. Hatimaye, nitayaandikia kitabu, ili dira yangu ibaki kama kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.

Kama ilivyotarajiwa kwenye ushindani wa kisiasa, wapinzani wangu wakiongozwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, walipotosha kisha wakabeza hoja zangu, tena kwa kejeli kubwa!

Kikwete aliponda asichokielewa. Alichokuwa anawaeleza wananchi si sera ya majimbo bali ni uzushi wa CCM. Natumaini naye sasa atasoma na aelewe. Kama ninavyosema siku zote, jamaa hawa kwa propaganda ni hatari!

Katika demokrasia ya mfumo wa vyama vingi, chama cha siasa kina wajibu wa kutoa dira ya nchi. Chama kinakuwa chimbuko la fikra. Fikra hizo zinatekelezwa na serikali. Chama kinaweka misingi ya kiitikadi, serikali inatengeneza sera na kuzitekeleza.

Mageuzi yanayolikwamua taifa lolote huanzia kwenye mageuzi ya kifikra. Mageuzi ya kifikra hupatikana tu pale walio kwenye madaraka wanapotambua kwamba uongozi wa nchi ni dhamana na si miliki yao.

Ni pale tu wanapokubali ukweli kuwa rais na hata viongozi wengine wa juu peke yao hawawezi kuliletea taifa neema.


Ni pale tu watakapoheshimu kuweka mifumo mizuri itakayotoa fursa kwa wote wenye uwezo wa uongozi kupata nafasi hizo kwa misingi ya chaguzi zilizo huru na za haki.

Kikwete na timu yake waliingia madarakani bila fikra wala dira. Ndiyo sababu alikiri kuwa wale wanaotegemea mabadiliko wasahau, kwani anataka kufuata yale ya waliomtangulia kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya! Waingereza wanasema ‘business as usual!' Yaani, mambo yaleyale!

Kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya, si dira! Si itikadi! Si sera! Ni kaulimbiu. Ni vibwagizo vya uchaguzi! Ni mbwembwe! Ni sanaa.

Watu waliopewa au kujinyakulia dhamana dhidi ya watu wao wanapokosa fikra na dira zao wanazoziamini, huwa watawala, na hivyo kusababisha utupu (vacuum) wa dira.

Wanapokuwa na fikra zao wanazoziamini huwa na dira, nao huwa viongozi. Huongoza watu wao kuelekea kule wanakokuamini, hata kama ni kubaya.

Panapotokea utupu (vacuum) wa fikra za wenye dhamana, fikra za nje huziba utupu huo.

Katika mazingira haya wanajitokeza wengi kujaza utupu huu kwa kuwa madalali wa watawala.

Wanageuza Ikulu kuwa gulio. Hili ndilo linaloisibu nchi yetu. Tangu Baba wa Taifa aondoke madarakani, nchi imekosa fikra na dira. Viongozi wameacha kufikiri au hawana uwezo wa kufikiri?

Utupu huu wa kukosa fikra mbadala za ndani, unawafanya viongozi wetu kila kukicha kutimkia nje ya nchi kusaka mawazo na fikra mpya.

Ni dhahiri watu wa nje wakijaza utupu wetu, watajifaidisha kwanza wao!

Tahadhari! Katika historia ya dunia, hakuna taifa lililoendelezwa na fikra za taifa jingine. Kila taifa huvutia kwake kwa kuchuma kwa wengine.

Fikra zitakazokomboa taifa hili lazima zitoke huku huku. Watu wapo! Vichwa vipo! Vimebanwa na mfumo.

Nieleweke hapa! Sikatai wawekezaji. Ila sikubali kuwa ufumbuzi wa matatizo yetu ya umaskini utaletwa na wawekezaji na wafadhili wa nje. Sasa narejea kwenye hoja!

Chimbuko la fikra ya hoja ya sera ya majimbo

Naam! Baada ya kutafiti kwa kina, kwa upande mmoja nilibaini kuwa ukubwa wa nchi yetu na utajiri wake wa asili vimelemaza taifa letu.

Kwa upande wa pili, nilibaini na hivyo kuamini kuwa mfumo wetu wa utawala umeshindwa kutumia rasilimali watu na maliasili yetu kwa maendeleo ya taifa.

Kwanza, nilishangazwa na idadi ya Watanzania wasiojua ukubwa wa kijiografia wa nchi yao. Ni idadi ndogo sana ya Watanzania wanaojua kuwa nchi yetu yenye ukubwa wa kilometa za mraba laki tisa na arobaini na tano elfu (945,000 km2) ni zaidi ya ukubwa wa nchi za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Lesotho na Swaziland zikichanganywa!

Tanzania kwa idadi ya watu (milioni 3 ni nchi ya 38 kati ya nchi 195 za dunia. Katika Afrika, Tanzania ni ya saba ikizidiwa na Nigeria (milioni 132), Misri (milioni 79), Ethiopia (milioni 75), Kongo (milioni 63), Afrika Kusini (milioni 44) na Sudan (milioni 41).

Ni dhahiri basi kuwa Tanzania ni nchi kubwa ya kutisha, huku ikiwa yenye rasilimali za kupindukia.

Ukubwa na utajiri huu kama hautawekewa mkakati, unaweza kuwa kikwazo kikubwa ambacho watawala wetu hawajaweza kukiona.

Aidha, kama hautadhibitiwa mapema, unaweza kuwa chanzo cha migongano ya ndani kwa ndani, kwani kuna utupu wa kutisha. Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea kila kitu kutoka Dar es Salaam!
Chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere, chini ya mfumo wa utawala wa kijamaa, nchi yetu ilitawaliwa kutoka kati, yaani kutoka makao makuu ya serikali. Serikali ilisimamia na kumiliki njia zote kuu za uchumi (command economy), ambazo ni pamoja na ardhi, maliasili zote, biashara, viwanda, mabenki, majengo n.k.

Hata mfumo wetu wa kiutawala ulipata maagizo kutoka Dar es Salaam na hivyo kufanya makao makuu ya nchi na kiongozi mkuu kuwa na mzigo mkubwa sana wa kusimamia rasilimali za asili za taifa.

Ujamaa ulikwama. CCM, tangu enzi za Mzee Ali Hassan Mwinyi, ikautelekeza kisirisiri. Jambo la ajabu! Itikadi kuu ya nchi inatelekezwa kisirisiri bila wananchi kujua. Hii ndiyo fedheha ya watawala wasio viongozi.

Kwa upande wa siasa, nchi nayo ikaingizwa kichwa kichwa kwenye mfumo wa vyama vingi. Balaa likaanzia hapa!

Tangu wakati huo, mserereko wa uchumi wetu umekuwa wa soko (market economy). Ujamaa umebakia kuwa usanii wa kuombea kura kwa wananchi.

Sera za ubinafsishaji sasa zikaanza na baadaye kushamiri chini ya utawala wa Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin William Mkapa. Nchi yetu nayo haikusalimika na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi na kisiasa ya dunia.

Hii ilitokana na kufa kwa vita baridi kati ya mataifa ya mashariki ya kijamaa na yale ya Magharibi ya kibepari.

Nchi yetu hapa iliingia kwenye mfumo wa uchumi wa soko kwa kushinikizwa bila maandalizi ya kutosha yaliyosababishwa na kukosekana kwa fikra za ndani.

Rasilimali za taifa ghafla zikawa kama hazina mwenyewe. Viongozi wetu wakaanza kuzigawa kwa wageni bila kuweka mkakati wa ndani wa kuwezesha wazawa.

Kupitia ubinafsishaji na sera za uwekezaji, viongozi wetu nao wakaanza ‘kujikatia' mapande yao. Familia zao, wapambe wao nao hawakucheza mbali. Wawekezaji wa sampuli mbalimbali nao wakaingia ulingoni.

Kama nilivyokwisha kusema, nchi sasa ikageuzwa shamba la babu, ambapo kila mwenye kapu huvuna, na babu hana nguvu ya kuzuia. Uongozi wa nchi sasa ukawa biashara. Ufisadi wa kutisha ukazaliwa rasmi.

Kazi ya kugawa rasilimali ya taifa ikaendelea kufanyikia Dar es Salaam. Bunge likageuzwa kituko. Likawa idara ya CCM, na likatumika kupitisha maagizo ya wakubwa, si matakwa ya wananchi.

Mali za nchi zikawa zinagawanywa na kikundi kidogo cha watu chini ya Rais, huku kikidhani kina akili kuliko Watanzania wote.

Watanzania tukaendelea kupewa matumaini ya neema. Kila kukicha zinatolewa takwimu tamu tamu za kuonyesha uchumi unakua. Ni kweli, pato la taifa lilikua! Lakini cha kujiuliza, lilikua kwa faida ya nani ilhali wananchi waliendelea na wanaendelea kuwa maskini?

Sasa, hebu tuchambue bila woga ufisadi uliofanyika chini ya utawala wa Awamu ya Tatu, na ambao Rais Kikwete ameahidi kuuenzi na kuulinda! Mwanzo wa kuelemewa kwake.
 
Mh. Mbowe
Nakuunga mkono lakini naomba tu unidhibitishie mapato yatakayopatikana toka kwenye rasilimali yataingia kwenye pato la taifa siyo jimbo na yatatolewa kulingana na mahitaji ya sehemu husika bila upendeleo. Nakuhakikishia baada ya hapo I am in your team. Shule njema.
 
Naomba kuuliza swali kwa Mnyika : Hivi mheshimiwa unatumia strategy gani kuongoza hasa ukiangalia siasa za tz zilivyokuwa na majungu ? unafanya nini ku-overcome hayo majungu ?
 
Mimi naona nisubiri majibu ya Mnyika hapa kabla ya kutoa hukumu au maoni yangu!


Ngoja nii-diggest hiii kichwa ya mada kwanza halafu nitatoa maoni yangu!
 
Mimi naona nisubiri majibu ya Mnyika hapa kabla ya kutoa hukumu au maoni yangu!

Unaweza ukaendelea tu mzee kujibu huku tukisubiri jibu toka kwa mheshimiwa ! si unajua tena we save the good 4 last ! haya mzee nakuachia ukumbi...............
 
Kada Mpinzani:

Umeniuliza natumia strategy gani kuongoza hasa ukizingatia kuna majungu kwenye siasa za Bongo:

" Nami nikuulize swali- mtu akiwa katika mabafu ya uswahili anaoga,ghafla akatokea chizi akachukua nguo zake na kukimbia nazo. Atatumia strategy gani kukabiliana na hali hiyo?".

UKWELI....ni suluhisho la yote!

(Soma kitabu cha The New Prince cha Dick Morris uone jinsi ambavyo siasa za Machiavelli zilizomo kwenye The prince zinavyoweza kuepukwa!)

JJ
 
J.J Mnyika,
Ama kweli na wewe sasa umeiva ktk siasa za Kibongo maanake siku zote swali hurudishwa kwa swali!..

Na imekuwaje uwe ktk choo cha kiswahili?...
Kama wewe mswahili nadhani utaelewa kuwa hatuendi chooni kuoga na nguo bali msuli, kisha choo cha kiswahili kipo uani sio rahisi kukifikia bila kupitia nyumba kubwa.
Kwa hiyo moja kuna mtu ndani ya nyumba kamfungulia mwizi!...Na kama msuli ndio umeibiwa mwite mama akupe khanga uhifadhi nyanga!... aibu itabaki ndani ya nyumba!.. heee hee hee!

Hizi ni strategety za kiswahili uswahilini tupe zako za Chadema mkuu! vitabu vingine bob havizungumzii uswahilini.
 
Mkandara,

Teh teh teh! Huishiwi maneno.....

Unaweza kuwepo choo cha uswahili kwa kuwa ama wewe ni mkazi wa uswahili au umekwenda kuwatembelea jamaa wa uswahilini.

Kwani Msuli sio nguo?

Uswahilini kuna mabafu ya kupita nyumba kubwa na kuna yale ukikata tu kona ya kichochoro unakutana nayo! haya ndio nayazungumzia...

Sio Mwizi..Huyu ni Chizi.....

Umejibu vyema-ni lazima umwite mama akupe Khanga.....maana ukitoka weye ukafukuzia nguo..Chizi atakuwa mbele, wewe nyuma ukiwa mtupu...watakaoshuhudia watasema wewe uliye mtupu ndiye chizi wamfukuza mwenye mavazi....teh teh teh

Ndio siasa za bongo...ukitukanwa, nawe ukatukana..yatakukuta ya huyu jamaa ama.

Ndio njia pekee ya kukabiliana na siasa za majungu- KUSEMA na KUSIMAMIA UKWELI......

Wataka za CHADEMA weye, ngoja kada mpinzani anichokonoe kwa maneno...nitarejea....

teh teh teh...

JJ

PS: In a light touch!
 
Sasa J.J hiyo ni nyumba ya Mlalahoi!... haina mswahili tena maanake nyumba hizi ziko kibao ktk vitongoji vya mji - Tandale, Temeke n.k
Huko mzee lazima nawe uwe chizi vile vile maanake choo chenyewe kipo wazi, tobo kibao sasa ukiacha kumfukuza chizi sijui utakuwa naficha nini?... heee heee hee! hizo nyanga watu walisha ziona siku nyingi!...
Unajua tena upigaji bodi ndio sinema ya bure!
 
heshima mkuu, mnyika !

nimeuliza swali na jibu nililopata ni kuulizwa swali ! ok, am good with that critical thinking question, lakini sitaki kujibu ninavyofikiria mimi nataka ujibu kutokana na mtazamo wako, naweza nikafikiria tofauti na hivyo unavyofikiria wewe, huo mfano wako just shows how narrow ur thinking skills are ! eti chizi kaiba nguo kakimbia, kama ye chizi kweli na anajua meiba kwanini akimbie ? ebu naomba unijibu mheshimiwa !!
 
KadaMpinzani,
wee mhuni sana! chizi kakimbia sio? na kweli huyu hawezi kuwa chizi maanake chizi hajui alichokifanya!.....akimbie nini?
 
Mzee Mnyika,

Heshima yako ndugu yangu, lakini huyo Dick Morris ni yule jamaaa wa Clinton au mwingine?

Maana kama ni yeye, then we have some issues to talk kutokana na reffernce yako kwake? Kwa sababu lazima tujue message inatoka kwa nani na hasa ya vitabu!
 
mhm mnyika una matatizo wewe, eti ngoja kadampinzani anichokonoe kwa maneno kisha utarejea, kwanza vipi kuhusu hiyo philosophy unayotumia ? ujue kwamba kama ukiangalia kwa ukaribu haina tofauti na ile anayotumia muungwana inayosema "ari mpya, kasi mpya, nguvu mpya " maana naamini ukiwa na hivi vitu vipya (i.e ari, kasi na nguvu ) basi dhahiri utapata kizazi kipya na maisha mapya ! sasa sijui kwa nini usikubaliane na muungwana tu kwa hilo ?? nakushauri hiyo ufute maana chadema wenzako watadhani unaenda "undercover" kwao. Kuna tetesi wewe ni ccm damu damu !!!! stei tyun-di !! nakuletea tetesi mwenyewe kada mwana wa mpinzani.............


SHUKRANI NA HESHIMA MBELE MZEE !!
 
Kada Mpinzani,

Kizazi Kipya, Maisha Mapya si sawa na Ari, Kasi na Nguvu(ANGUKA).....falsafa ya kizazi kipya imejikita katika harakati za vizazi(generation struggle)!. Ingawa mtu anaweza kusema kwamba kizazi cha baada ya uhuru ambao wengi wao ni vijana wanapaswa kuwa na ari, kazi na nguvu. Lakini huwezi kusema kwamba KIZAZI KIPYA=ARI, KASI+ NGUVU MPYA.

Sijui kama unanielewa! Ndio maana natumia Kizazi Kipya, Maisha Mapya sambamba na kauli mbiu ya CHADEMA ya Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli.

Ari, Kasi na Nguvu Mpya isiyokuwa na falsafa, itikadi na fikra mbadala ni sawa na ANGUKA(soma anguko!) na ndivyo tunavyoendeshwa sasa.

Lakini kwa upande mwingine, Kizazi Kipya, Maisha Mapya nilianza kuitumia kabla hata ya Kikwete kuteuliwa na kuja na kauli mbiu ya Ari, Kasi na Nguvu Mpya. Kwa hiyo ni makosa kusema kwamba nimeiga kwa Kikwete au nimeamua kufanana na Kikwete.(rejea maandiko yangu ya miaka ya nyuma).

Siwezi kukubaliana na Muungwana katika Ari,Kasi na Nguvu mpya bila Kizazi Kipya, Maisha, Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli na NGUVU YA UMMA!

CHADEMA wananielewa kwa kuwa ni chama cha KIZAZI KIPYA.

Tetesi ni kitu cha kawaida katika jamii. Ila ukweli unabaki kuwa sijawahi kuwa mwanachama wa CCM tangu kuzaliwa kwangu!

Ila ni vyema ukazileta hizo tetesi kama ulivyoahidi
 
Mkandara:

Ni yule wa Clinton. Is nothing good that can come from Jerusalem? Dick Morris kama binadamu ana mapungufu mengi lakini walau katika The New Prince ametoa mbadala wa The Prince ambayo kwa karne nyingi imekuwa ikifanya siasa za dunia ziwe za Kimakaveli!

Ila bado namsoma tena tena na tena. Kuna hoja za Msingi za Nicolla bado kitabu chake hakijazijibu!.

Kada Mpinzani,

Ukiona majibu kama yale ujue nimekosa wasaa wa saa wa kujibu kwa kirefu na soma vizuri utaona kwamba niliamua kuchanganya na mizaha. Naomba nisijibu hili swali lako la nafanyaje siasa katika Tanzania yenye majungu. Naomba kwamba nipate muda wa kuchangia hoja ya katiba kule aliyoifungua Mkandala. Niko naandika kitabu kuhusu Uchaguzi wa Ubungo-naamini kitabu hiki kitatoa majibu ya jinsi ya mwanasiasa wa kizazi kipya anavyoweza kufanya siasa katika mazingira ya Tanzania yenye siasa chafu!

Hivi hujawahi kuoana chizi akipora kitu anachojua unakipenda na kukimbia nacho huku akicheka?(Joke).

JJ
 
ndugu yangu mnyika ufahamu kamwe hutaweza kujibanza kokote katika kupinga kauli mbiu yako kufanana na ile ya muungwana,kwanini nasema hivyo ? hahihitaji kwenda darasani kwani muungwana katika kauli mbiu yake anasema ari mpya,nguvu mpya na kasi mpya na wewe katika kutetea unasema kauli yako ina mtazamo zaidi katika kutumika kwa kizazi kipya,lakini ebu angalia ili ya muungawana utaona wazi kwamba kimantiki ameijenga kiufundi zaidi na kuweza kuchukuwa dhana ndefu kwa maneo machache,nafahamu unajua kwamba uwezi kupata ari mpya kama hutakuwa na maisha mapya aidha kijamii ama kifikira,pili uwezi kupata nguvu mpya kama idadi kubwa ya waliochoka katika masuala mbalimbali hawataondoka na tatu uwezi kupata kasi mpya kama hutakuwa na damu mpya ambayo ni vijana na wazee wacache ambao kifikra watakuwa wamebadilika

twende kazi
 
BigMan,

Nakubaliana nawe kiasi. Ndio maana wakati wa kampeni Ubungo utakumbuka nilikuwa nikisema huwezi kuwa na Ari, Kasi na Nguvu mpya ukiwa na mbunge kama Keenja. Yakatokea, yaliyotokea. Sasa jiulize kuna wakina Keenja wangapi katika mfumo wetu wa utawala hivi sasa? So are were just paying lip service?

JJ
 
Habari Gani!! Sasa Ndesamburo jino kwa jino na CCM! Kulikonii!!! Soma Zaidi

Hatujamkashfu Ndesamburo - CCM

1256.jpg

Ndugu Philemon Ndesamburo

Kutoka gazeti la 'wapinzani wetu' Tanzania Daima,
na Mwandishi Wao


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro, kimesema hakijawahi kumtuhumu Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, kwa kusambaza rushwa kwa watendaji wa chama hicho na kwa waandishi wa habari.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na Mlezi wa chama hicho Wilaya ya Moshi Mjini, Mildred Kisamo, jana aliiambia Tanzania Daima kuwa taarifa hizo zimekishitua chama hicho mkoani humo.

Alisema katika kikao cha viongozi wa mkoa huo na waandishi wa habari kilichofanyika ofisi ya CCM, mkoani Kilimanjaro, walizungumzia kauli iliyotolewa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwamba Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kudhibiti rushwa.

Mkutano huo wa CHADEMA wa hadhara, ulifanyika Januari 20 katika Kata ya Pasua, mjini Moshi.

‘Katika mkutano wao, viongozi wa CHADEMA walisema Rais Kikwete ameshindwa kupambana na rushwa …. nilichosema mimi kujibu kauli hiyo ni kwamba rais hajashindwa kudhibiti rushwa na kwamba haiwezi kudhibitiwa na rais peke yake,” alisema.

Aliongeza kuwa aliwajibu wapinzani hao kuwa rushwa ni suala la jamii nzima ya Tanzania pamoja na viongozi wa chama hicho, na kwamba wanapaswa kwa pamoja kushirikiana kupambana na rushwa.

‘Sikuwahi kutamka kuwa Ndesamburo anasambaza rushwa, nashangaa hayo maneno yametokea wapi… nilisisitiza kuwa rushwa haiwezi kumalizwa bila ushirikiano wa pamoja,” alisisitiza.

Januari 22 mwaka huu, Tanzania Daima ilimkariri kimakosa mlezi huyo akidai kuwa Ndesamburo anasambaza rushwa kwa watendaji wa chama hicho tawala na waandishi wa habari.

Kutokana na kauli hiyo, Ndesamburo kupitia kwa waikili wake, Shayo Jonathan, alikusudia kwenda mahakamani kuishitaki CCM, mlezi huyo pamoja na Tanzania Daima.
 
Waraka wa kwanza wa Mbowe kwa Kikwete

Freeman Mbowe

MHESHIMIWA rais,

Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba kakujalia afya njema tangu ubebe jukumu kubwa la kutawala taifa hili. Naendelea kumwomba aendelee kukujalia afya njema na akupe busara za kukabiliana na vikwazo mbalimbali vya kulijenga taifa la Tanzania na akuepushe na nguvu yoyote ya giza yenye azma ya kulibomoa.

Mheshimiwa rais,
Leo nimeamua kukuandikia waraka huu. Pengine utashangaa kama watakavyoshangaa wananchi wako wengi unaowaongoza. Najua wengine watahoji, iweje nikuandikie kupitia gazetini na isiwe moja kwa moja. Sababu ni rahisi. Kwa kuandika gazetini, nina hakika itakufikia.

Wengine wanaweza kuona ni utovu wa nidhamu kuweka hadharani barua kwenda kwa mtawala mkuu wa nchi. Katika mazingira ya kawaida, hii yaweza kuwa kweli, lakini kwa mazingira na utamaduni uliojengwa na ofisi yako sambamba na chama chako, rais wetu, unayeitwa “mtu wa watu”, uko radhi kuonana kikazi au hata kistarehe na watu wengine wote isipokuwa viongozi wenzako wa vyama vya siasa.

Hata hivyo nikiri, serikali yako, kama ilivyokuwa iliyokutangulia, hukumbuka viongozi wa vyama vya siasa pale panapokuwepo ugeni wa kimataifa, jambo lenye kawaida ya kuambatana na hafla ya ulaji na unywaji Ikulu. Hapo, wapinzani huitwa kwa zamu kwenye ulaji na unywaji.

Aidha, unapokuwa kwenye ziara zako nje ya nchi, serikali yako imejijengea utamaduni wa kuwabeba “msukule” wabunge wa upinzani.

Wapinzani wanaoambatana na wewe hawana jukumu lolote wanalopewa zaidi ya kuwa sehemu ya kundi kubwa la “watalii” wenye jukumu moja tu, la kuhalalisha matumizi ya kodi za wananchi, kutambulishwa kwenye kila kikao au mikutano kwa lengo la kujenga taswira chanya ya serikali yako.

Wengi hubebwa bila hata kujua madhumuni ya safari ni nini! Na wakirejea, biashara huishia pale uwanja wa ndege! Yatokeapo maazimisho ya sherehe za kitaifa, wapinzani hukumbukwa. Hapa ni kuwahadaa wananchi wakiwemo waandishi wa habari. Tutaonana Uwanja wa Taifa kukuona ukikagua gwaride, kisha tutaachana pale, kusubiri sikukuu nyingine ya kitaifa.

Ninaamini wengi wa viongozi na wabunge wa upinzani hukubali kushiriki mambo haya kama ishara ya utayari wao na vyama vyao katika kujenga utaifa wetu na si kwa ajili ya kingine chochote. Hata hivyo nikiri, upande wa pili wa mchezo huu mchafu, ghafla umedhoofisha wapinzani dhaifu na wabinafsi na umejenga taswira ya rushwa ya kisiasa na kimaslahi. Mwaliko mmoja tu wa Ikulu au safari moja na msafara wako au waziri mkuu, vimeweza ghafla kubadilisha misimamo ya baadhi ya watu walioonekana awali kuwa makini katika kutetea maslahi ya taifa.

Kila baya lina jema, utamaduni huu kwa upande mwingine unasaidia taifa hili kujua mchele ni upi na pumba ni zipi. Naamini kwa dhati kabisa, nia ya serikali yako si njema, kwani ina kusudio la kuwatumia wapinzani kama chambo, hasa mbele ya macho ya viongozi wenzako wa nje, kujenga sura ya kinafiki kuwa ndani ya nchi yetu, tuna mshikamano wa kisiasa.

Mheshimiwa rais,
Waraka wangu kwako leo unakusudia kukukumbusha jambo moja la muhimu sana, ambalo napenda kuamini unalijua. Cha ajabu ni kwamba, kama ungekuwa hulijui nisingesikitika. Lakini nasikitika kwa sababu naamini unalijua, lakini pengine unalidharau.

Nikiri jambo moja. Kama kuna kitu kinaniweka kwenye siasa, si chuki binafsi, si ajira na wala si cheo, bali ni ndoto yangu ya siku moja kuona nimeshiriki mchakato wa kuistawisha nchi yangu, kwa pamoja na mambo mengine, kujenga umoja wa kitaifa.

Hakuna jambo lolote la “neema” linalowezekana katika taifa lililogawanyika. Si rahisi wote kuwa na fikra sawa, lakini ni rahisi kwa asilimia zaidi ya 80 ya wananchi kuupenda, kujivunia na hivyo kuuulinda utaifa wao. Hii haijalishi kama nchi ni maskini au tajiri. Hali hii hata hivyo, haizuki. Hufanyiwa kazi, tena kimkakati.

Nasisitiza, sifa ya kwanza ya taifa lolote ni umoja wa utaifa wake. Umoja wa kitaifa kamwe haujengwi na kundi lolote la kijamii ndani ya nchi kama vile chama, dini au kabila. Hujengwa pale dhamira ya mtawala inapowaongoza watu wake kuweka kama agenda kuu ya uongozi na dira ya nchi msingi wa kuunganisha taifa bila kujali mipaka ya kiitikadi, kidini, kikabila, kijiografia, kijinsia au rangi.

Baada ya kiongozi kujidhihirisha kwa fikra zake, huzitafsiri kuwa dhamira ambayo huitoa kama kauli, si mara moja, bali kila fursa itokeapo, kwani kwake ni sawa na sala. Ni uumini. Naye hatimaye hukamilisha uumini wake kwa vitendo, tabia na mienendo yake ya kila siku.

Ndiyo, watu na hususan viongozi watapingana kwa mengi ikiwemo mitazamo, lakini yote haya hayawi mapenzi yao kwa taifa lao.

Watalipenda, watajivunia na kamwe hawatalikimbia!

Mheshimiwa rais,
Dhuluma, nguvu na rushwa vinaweza kushinda uchaguzi, lakini haviwezi kujenga umoja wa kitaifa. Umoja wa kitaifa kamwe haujengwi na fedha, majeshi au mifumo ya kiusalama. Mifumo hii hujenga hofu na ukondoo!

Penye dhamira nzuri, kila jambo lililo kikwazo cha umoja wa taifa huwa ajenda yenye kipaumbele kwa kiongozi yeyote anayestahili sifa ya kuwa mtu wa watu kama ambavyo naamini ungependa. Kwa vyovyote vile, hutafurahisha wote, lakini wenye kupenda haki katika maisha haya ni wengi kuliko wenye kudhulumu na kuichukia haki.

Utawala ni kazi ngumu. Inahitaji uwezo wa kufikiri na kutafakari, ambao nina hakika unao. Penye umoja wa kitaifa, hata baadhi ya maamuzi magumu ambayo hayapendwi na wananchi huridhiwa.

Kiongozi makini lazima akubali lawama pale anaposimamia jambo ambalo anaamini lina maslahi kwa taifa. Hali hii inamfanya kiongozi awe mkweli, muwazi na asiyefanya mambo kwa kificho. Kiongozi mzuri ni lazima basi kwa kiwango kikubwa atende yale anayoyahubiri.

Mheshimiwa rais,
Niruhusu nikukumbushe jambo moja, ambalo kwa mara nyingine, naamini unalijua, lakini bado napata wakati mgumu kujua unalitafakari vipi. Hili linamhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye baadhi ya wananchi wako wameamua kukuita JK kama yeye.

Sikusudii kufungua ukurasa wa somo la Mwalimu, ila nakumbuka wakati wa kampeni, wapiga debe wako wakuu, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na Mzee Stephen Wassira – ambao vilevile leo ni mawaziri wako, walifanya mkutano na waandishi wa habari wakidai sina haki ya kumzungumza Mwalimu kwenye kampeni zangu, kwani wewe unamjua Mwalimu kuliko mimi!!

Dhamira nyoofu na kauli, vilivyoshabihiana na matendo, ndivyo viliyompa Mwalimu jeuri, kujiamini, kupendwa, kuheshimika, kuogopwa, kusamehewa, kuombewa na hatimaye leo, wengine (ndani ya imani yake) wanatafakari uwezekano wa kumfanya mwenye heri na hatimaye mtakatifu.

MWALIMU ALIJENGA TAIFA!
Mwalimu, kama binadamu, alikuwa na makosa kadhaa ya kisera na hasa ya kimaamuzi, hususan katika masuala ya baadhi ya sera za kiuchumi.

Aliongoza Tanzania wakati mgumu sana, lakini pamoja na umaskini ule, kila alichofanya Mwalimu kililenga utaifa, Utanganyika na hatimaye Utanzania wetu!

Mheshimiwa rais,
Tangu umeingia Ikulu, umezungumza mengi. Ndani ya nchi na hata nje. Uzuri wa maendeleo ya kiteknologia, yanatusaidia sisi walalahoi kujua wewe rais wetu umezungumza nini popote duniani.

Nimeona nivunje itifaki zote, niweze kukupongeza bila kificho chochote mbele ya Watanzania wenzangu, kuhusu hotuba uliyoitoa bungeni Desemba 30 mwaka 2005, wakati ukizindua Bunge jipya baada ya uchaguzi.

Wengine wataendelea kushangaa! Mbona Mbowe anazungumzia mambo ya kale! Hapana!

Mheshimiwa rais,
Tangu umeingia Ikulu, hakuna maneno mazito, ya kizalendo, ya kiungwana na yenye kutia matumaini ambayo ulishawahi kuyazungumza kama yale. Sifa zote hizi nakupa kwa sababu moja tu: Hotuba ile ilijenga MATUMAINI YA UTAIFA.

Mheshimiwa rais,

Hotuba yako ya kufungua ilikuwa ya kujiamini mno. Ilifurahisha wengi, wakiwemo wa vyama vingine vya siasa. Uliamsha ari ya wananchi wako na wengine tuliamini angalao kwa kipindi cha wiki chache kuwa, sasa mambo huenda yatabadilika. Uliweza kuendelea kuwapagaisha wananchi na kuwafanya “misukule” angalao kwa wiki kadhaa.

Kwa kumbukumbu zangu na ufahamu wangu mdogo wa kisiasa, mara ya mwisho kusikia hotuba iliyogusa wengi kwa kiwango kile, ni wakati wa uhai wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Mwalimu alitania kwenye hotuba zake, lakini hukufanya utani, uzushi au masihara na kauli zake au yeyote atakayekwaza dhamira yake na TAIFA lake!

Kwangu, ile ilikuwa dira ya taifa. Ilijenga hoja za msingi za utaifa bila kujali zimetoka kwenye ilani ya CHADEMA, ya CCM au ya chama kingine chochote.

Tunajua kipindi kile, ulikuwa umetingwa na mambo mengi sana ikiwepo kushangaa, pengine kisirisiri, wingi wa kura zako pamoja na mshikemshike tuliokupatia kwenye kinyang’anyiro. Busara za kawaida zitajua kuwa ulikuwa unatafakari namna ya kuzawadia wale wote waliowezesha miujiza ile kutokea. Ni dhahiri ulikuwa unatafakari namna ya kuunda serikali yako. Naamini kipindi kile ulikuwa hujatulia na kupumzika.

Siku hiyo, nilikuwa ndani ya Ukumbi wa Bunge kama mwalikwa. Bado nilikuwa na mimi natibu majeraha. Nilikusikiliza kwa makini na kujisemea:

Hotuba ya mheshimiwa rais yaweza kuwa jibu la nchi yetu. Je, ameandika vipi hotuba nzuri kiasi hiki wakati ametingwa sana? Nikakumbuka rais wangu una wasaidizi! Lakini nikajiuliza tena; basi rais utakuwa na wasaidizi na washauri makini sana! Nikajiuliza umewapata wapi ghafla? Kwani nilijiaminisha hawawezi kuwa wale wazee walionikebehi bila haya eti “nisimtumie” Nyerere kwenye kampeni zangu!

Naam, hata kama umeandikiwa, kwa vyovyote umeipitia na kuikubali kwani hata ulipokuwa unaisoma, uliisoma kwa kujiamini na hata kuongezea mengine nje ya karatasi. Hivyo basi, lolote lililo ndani yake ni lako. Napenda kuamini ilikuwa ni dhamira yako! Ni hadidu ya rejea ya miaka mitano ya utawala wako!

Mheshimiwa rais,

Hotuba yako bado naiwaza na kuisoma mara kwa mara. Nina mengi ya kukupongeza ndani yake na waraka huu mmoja hautoshi. Najua nawe una majukumu mengi. Naomba uniruhusu niishie hapa kwa leo na wiki ijayo niingie kuijadili hotuba yako kama walivyofanya wabunge wetu kule Dodoma na mijadala yao ikabaki kwenye kumbukumbu za Bunge, ili zije kusomwa na vizazi vya mbele.

Niruhusu mheshimiwa nifanye kazi hiyo ya kukukumbusha kauli zako mwenyewe, kifungu kwa kifungu na namna ulivyotekeleza kwa vitendo, ahadi zako. Nitakuchosha, lakini ndiyo wajibu na heshima yangu kwa utaifa wetu!

Mheshimiwa rais,

Naomba kutoa hoja…

Tukutane wiki ijayo

Freeman@chadema.net

Tanzania Daima: Jumatano Aprili 4, 2007
 
Back
Top Bottom