UANDISHI WA HABARI ZA UCHUNGUZI
Hakuna burudani mwanana zaidi kwa mtu mwenye kupenda kusoma kama mikono yake kufanikiwa kunasa andiko la muandishi aliyeandika habari kuhusu masuala yaliyotokea au yanayotokea nyuma ya pazia, habari za uchunguzi… hakuna burudani tamu zaidi ya hii.
Lakini kama ukisoma kwa makini makala hizi unaweza kuhisi maumivu ya muandishi, woga na hatari anayochukua kufumbua masuala kama hayo. Jambo gumu zaidi kuandika habari uchunguzi kuhusu masuala ya siri sio mchakato ule wa kupata siri hizo bali ni ule uthubutu wa kuinua kalamu na kuandika kile ambacho umekikusudia. Hakuna hatari kubwa zaidi ya hii.
Nchini Myanmar kuna sakata ambalo mpaka sasa limechukua sura ya kimataifa likiakisi kabisa hiki ambacho ninakisema, uandishi wa habari ya uchunguzi.
Waandishi wawili wa habari za uchunguzi wa shirika la Reuters wanakabiliwa na mashitaka ambayo yanaweza kuwafanya wakatupwa jela kwa miaka 14 kama wakikutwa na hatia. Kosa lao ni nini hasa? Waliandika habari ambayo serikali ya Myanmar wanadai ushahidi uliotumika kuandika habari hiyi unahusisha nyaraka za siri za serikali na ni kosa nchini Myanmar kuanika hadharani siri za nchi.
Ni kwamba… kwa miaka mingi sana nchini Myanmar kumekuwa na kashikashi na mapigano ya kidini baina ya watu wa imani ya Kibudha dhidi ya imani nyingine hasa hasa wale wa imani ya kiislamu. Waislamu hawa wengi wao ni wale wa asili ('kabila') la Rohingya. Kuna nadharia ulimwenguni kwamba watu wa asili ya Rohingya ndio watu wanaonyanyasika zaidi kuzidi jamii yoyote ile duniani kutokana na kuishi kwa woga na mateso kwa karibia karne nzima sasa. Ubaya zaidi ni kwamba mara zote serikali ya Myanmar watawala wake ni watu wa imani ya Kibudha kutokana na wao kuwa ndio sehumu kubwa zaidi ya idadi ya watu nchini Myanmar.
Mara kadhaa kumekuwa na majaribio ya wapiganaji wa kibudha wanaofadhiliwa na serikali kutaka kuifuta jamii ya warohingya ndani ya nchi ya Myanmar kwa kuwauwa wote. Majaribio haya ya kuwafuta yamekuwa yakifanyika tangu miaka ya sabini kipindi Myanmar iko chini ya uongozi wa kidekteta. Lakini tukio la karibu zaidi ni lile ambalo limetokea mwaka jana 2017.
Tarehe 30 August Mwaka jana wanajeshi wenye silaha wapatao 90 waliingia kwenye kijiji cha Tula Toli kinachokaliwa na watu wa asili ya Rohingya na kuwakusanya wakazi wote kwenye upande mmoja wa eneo la kijiji ambalo wenyewe wanakijiji hupendelea kuliita "the sands" kutokana na kutokuwa na uoto wowote wa asili na kame. Wakiwa upande huo wa pili wa kijiji kamanda wa wanajeshi hao aliamuru kwamba wanakijiji waendelee na shughuli za uvuvi na kulima lakini wasithubutu kukimbia na atakaye jaribu kukimbia basi atatandikwa risasi.
Wanajeshi hawa ambao awali walizunguka kijiji na kutoa hizi amri walikuwa na asili ya Burma. Lakini kesho yake vikosi zaidi vya jeshi viliwasili na safari walikuwa ni wanajeshi wa Myanmar. Hawakuwa wamekuja kuokoa wananchi wao, hapana… walifika kutekeleza agizo la kuhakikisha hakuna mwanakijiji wa Tula Toli anatoka akiwa hai.
Baada ya wanajeshi wa Myanmar kuwasili wananchi walikusanywa wote sehemu moja ya wazi. Kwanza nyumba zao zote zilianza kuchomwa moto. Kisha wanajeshi waliwagawanya wanawake na watoto sehemu yao na wanaume sehemu yao. Kisha wanajeshi wakajipanga mstari mmoja huku mikononi wameshikilia silaha za moto. Wanawake na watoto wakaambiwa wakimbie kutoka mahali hapo. Lakini wakiwa wanakimbia walipigwa risasi nyuma ya mgongo na vichwani. Upande huu wa kijiji walipokusanywa upo karibu na mto, hivyo baadhi ya wanawake walikimbia na kupiga mbizi ili kuokoa uhai wao. Lakini wengi waliishia kupoteza maisha kwenye maji kutokana na maji ya mto kuwa na mkondo wenye kasi na hivyo kusababisha wengi kushindwa kuogelea na kuvuka upande wa pili. Inakadiriwa ni takribani wanawake thelathini tu katika kijiji kizima ambao walifanikiwa kupiga mbizi baada ya kutokea upande wa pili na kukimbilia milimani na kisha kukimbilia nchini Bangladesh.
Wa Lone and Kyaw Soe Oo wakiwa mikonini mwa polisi
Wanaume wote ambao walibakia pale kijijini walipangwa mstari mmoja na kisha kutandika risasi wote.
Unaweza kujiuliza serikali inawezaje kufanya unyama mkubwa namna hii kwa wananchi wake wenyewe.
Nimeeleza kwamba wananchi wengi wa Myanmar ni wa dini ya Buddha na hata viongozi karibia wote serikalini ni wa dini ya Budha wakati ambapo wananchi mfano wa kijiji cha Tula Toli ni wa jamii ya Rohingya ambao ni Waislamu.
Binafsi sidhani kama viongozi wale wa serikali wanachukia sana waislamu au ni waumini watiifu sana wa dini ya buddha bali ninachokiona ni kwamba wanatumia tofauti hiyo na mtafaruku huu wa kidini wa wananchi kati ya buddha na waislamu na wanatumia kama turufu ili waendelee kutawala. Yaani wanatumia kanuni ile ile ya kale, "wagawanye na kisha watawale"… unawagawa wananchi kutokana na tofauti zao na kisha unajifanya kuwaunga mkono wale ambao ni wengi na kisha mnawapiga vita wale wachache. Hii ndio kanuni ya viongozi dhalimu duniani kote tangu tupate kuishi juu ya hii dunia.
Ukatili huu uliofanyika Tula Toli umekuwa ukifichwa mno kutokana na hata wale ambao walifanikiwa kukimbilia Bangladeshi walipojaribu kusema serikali imekuwa ikikanusha na vikali. Mbaya zaidi maeneo ambayo watu wa jamii ya Rohingya wanapoishi serikali imeweka marufuku kali kwa watu wa nchi za nje kuyatembelea hasa waandishi wa habari na mara chache mno vibali vinatolewa kwa watu wa nje kutembelea na hata wakitembelea wanakuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la Myanmar na hata maeneo watakayoyatembelea yanachaguliwa na maafisa wa serikali kwamba ni wapi wapelekwe.
Ushahidi pekee ambao tulikuwa nao kwa kipindi chote hiki tangu August mwaka jana ni picha za satelaiti ambazo shirika la Amnesty walifanikiwa kuzipata ambazo zinaonyesha dhahiri kabisa kijiji cha Tula Toli kikiteketea kwa moto lakini imekuwa ngumu kupata picha za kuonyesha watu wakipigwa risasi.
Ndipo hapa ambapo waandishi wawili wa habari wa shirika la Reuters Bw. Wa Lone na Bw. Kyaw Soe Oo wa shirika la Reuters walijitoa muhanga na kuamua kuchunguaza kwa makini sakata hili. Katika uchunguzi wao walifanikiwa kupata nyaraka mbali mbali za kijeshi na kiserikali ambazo zinaainisha namna ambavyo amri zilitolewa na viongozi wa juu serikali kwenda kwa jeshi na polisi ili kutekeleza tukio lile. Si hivyo tu waandishi hawa walifanikiwa pia kunasa mkanda wa video ambao ulirekodiwa siku ambayo wale wanaume wa asili ya Rohingya kijijini Tula Toli walivyopigwa risasi (tazama hapo chini).
Huu ulikuwa ni ushahidi mwanana zaidi ambao ulimwengu ulikuwa unasubiri na umesaidia jamii ya kimataifa kujua kwa usahihi zaidi kile ambacho kinaendelea nchini Myanmar dhidi ya jamii ya Warohingya na hivyo kuleta mwamko kwa jamii ya kimataifa kuweka mashinikizo kwa serikali ya Myanmar.
Lakini tofauti na ambavyo ulimwengu mzima tunawaona Wa Lone na mwenzie Kyaw Soe Oo ni mashujaa kwa uthubutu wao wa kutufumbulia yale yaliyo nyuma ya pazia nchini Myanmar ajabu ni kwamba huko nchini mwao wanaonekana ni wasaliti na wahaini. Hivi ninanvyoandika Wa Leo na Kyaw Soe Oo wako gerezani na kesi yao ikiendelea kuunguruma na kuna kila dalili kwamba watakutwa na hatia.
Kosa lao ni nini? Kutoka 'siri' za nchi…
Nchini Myanmar kabla ya uhuru mwaka 1923 wakoloni waliunda sheria ambayo ilipiga marufuku kwa raia wa kawaida kusambaza taarifa ambayo inahesabika ni 'siri' za serikali. Hata baada ya uhuru viongozi wa Myanmar wameiacha sheria hii mpaka leo na inatumika kuwaadhibu wale wote ambao wanajifanya 'vilimilimi' wa kufukunyua madudu ambayo yanafanywa na serikali.
Hii ndio dunia ya hatari ambayo waandishi wa habari za uchunguzi wanaishi… vitisho, makatazo na kupigiwa mstari ambao hautakiwi kuvuka.
Si kwamba Wa Lone na Kyaw Soe hawakuwa wanajua hatari ambayo walikuwa wanajiingiza kwa kuandika kile ambacho walikuwa wanakiandika… walijua. Lakini kuna muda unapaswa kujitoa muhanga ili kuanika ukweli. Unapaswa kujitoa muhanga ili historia ikae sawia na umma ujua yale yanayoendelea nyuma ya pazia.
Juu: Wanaume wa Kirohingya wakiwa wamepigishwa magoti tayari kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Myanmar
Chini: Maiti zao zikiwa zimetupwa kwenye shimo (tazama mmoja mmoja picha ya juu kisha linganisha na hawa wa chini... (uso na mavazi ))
Binafsi ni mshabiki mkubwa wa mchoraji wa kihispanyola anayeitwa Goya y Lucientes aliyeishi mwishoni mwa karne ya 19. Goya ni moja wa wachoraji mahiri kuwahi kuishi na 'amewa-inspire' hata wachoraji wengine wakubwa kama kina Picasso n.k. Lakini Michoro yake mingi imejaa "violence"… picha za miili ya watu isiyo na vichwa ikitafunwa na wanyama wakali ambao hawajawahi kuonekana kwenye maisha halisi. Mingine ina michiro ya wapiganaji ambao wamepigishwa magoti na kuzibwa macho kwa vitambaa vyeusi wakiwa mbele ya 'firing squad' na michoro mingine mingi yenye ukatili wa hali ya juu.
Watu wengi hawaelewi na wengine wanashangaa kwa nini Goya aweze kuwa hamasa ya manguli kama kina Picasso na kwa nini tuko watu tunaopenda kazi zake.
Nimekuwa nikiamini kwamba kazi yoyote ya sanaa (uchoraji na uandishi hasa hasa) kitu cha muhimu zaidi ni uwezo wako wa kufanya utambuzi wa ufahamu wa mchoraji/muandishi, ujumbe anaojaribu kuutoa, dhumuni analojaribu kulifikia na anachotanabaisha kuhusu yeye na kile kilichomo nafsini mwake kikimfurukuta. Lakini pia 'artist' hawa wanajaribu kuacha alama ya kumbukumbu kwenye historia juu ya uhalisia wa maisha halisi na madhila yaliyokuwemo katika kipindi chao. Wanajaribu kuacha kumbukumbu ya kudumu kwa ulimwengu usisahau juu ya udhalimu unaorindima kila uchwao. Pengine kwa kutukumbusha huku tunaweza kuepuka kesho kutukuza udhalimu na ukatili ule ule kama wa karne ulizopita. Binafsi nikiangalia michoro ya Goye hiki ndicho ninachokiona kwenye akili yangu ya ndani ya akili. Sioni "violence" naona alama katika historia, naona tafasiri ya zama na kizazi. Sijui wengine wanaona nini lakini binafsi hii ndio sababu ya kuwa shabiki wake.
Kwa hiyo muhimu zaidi si kile unachokiona bali ni yale yasiyoonekana kwenye mchoro au simulizi. Hicho ndicho kinachipa thamani kazi hiyo na kutukuka.
Ndio sababu kwa nini watu wanashindwa kuelewa mchoro kama Monalisa wa mchoraji wa nguli Da Vinci unakuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 800 au mchoro wake mwingine maarufu wa 'Salvator mundi' kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 500. Thamani hii inatokana na si kile unachokiona kwenye mchoro bali kile ambacho macho yako hayakioni. Ujumbe na Siri iliyofichwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na alama manguli hawa waliyoiacha ili kutafasiri kizazi ambacho wao waliishi.
Ni sababu hii hii pia waandishi wa habari za uchunguzi wakiishi kwa falsafa hii… licha ya hatari iliyodhahiri mbele lakini huwezi kuzuia kuwiwa moyoni mwako kwamba kila pande ya dunia iko na akina 'da vinci' wao. Na pengine ndio kazi hii tunayoifanya. Kuweka alama katika historia kutafasiri kizazi tunachokiishi. Kuacha ujumbe na siri kwa ajili ya vizazi vijavyo. Ndio maana licha ya hatari zote, lakini ni lazima kuchunguza na kuandika… na kisha kuandika tena.
Siku kadhaa zilizopita kuna mtu aliniuliza…"unaandika mno, kwa nini?" Kipande hiki kifupi cha andiko hapo juu ni jibu ambalo sikumuambia kwa kukosa muda wa kutosha wa kumfafanulia lakini ndicho ambacho nilitamani kumjibu. Nilimjibu kwa sentensi chache ambazo sina hakika kama alinielewa hasa;
"…natamani kutafasiri kizazi chetu. Natamani kuacha ujumbe na siri za zama hizi kwa ajili ya vizazi vijavyo… naandika kwa sababu nataka kuishi maisha yote mawili. Haya ya sasa na siku nisipokuwepo.."
Jioni njema wakuu,
Habib - 0718 096 811
To Infinity and Beyond