Tusitegemee chochote kipya toka serikali hii ya kifisadi katika kuivunja mikataba iliyopitishwa kifisadi.
Date::7/8/2008
Serikali yajikoroga kuhusu mkataba TICTS
*Ikulu yasema ulipitishwa na Baraza la Mawaziri
*Yadai ulifuata taratibu zote za kiserikali
*Zambi asema Baraza lilikiuka sheria ya manunuzi
*Cheyo adai haamini kauli ya Ikulu
Na Muhibu Said, Dodoma
Mwananchi
WAKATI Spika wa Bunge, Samuel Sitta, akimsafisha Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi (CCM), kuhusu kauli yake kwamba uamuzi wa kuongewa muda wa mkataba kati ya serikali na Kitengo cha Upakiaji na Upakuaji Makontena Bandarini (TICTS) unaopingwa na Bunge, ulitolewa na Baraza la Mawaziri, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), amesema uamuzi huo wa Baraza hilo ulikiuka sheria.
Zambi alisema hayo katika mahojiano maalum na Mwananchi nje ya ukumbi wa Bunge mjini
hapa jana, muda mfupi baada ya Sitta kutamka kwamba, Karamagi hakusema uongo kuhusu kauli yake hiyo kwa vile Ikulu imethibitisha suala hilo.
Karamagi ambaye alijiuzulu Uwaziri wa Nishati na Madini kutokana na kashfa ya Richmond, ni mmiliki wa Kampuni ya Harbours Investment Limited (HIL) inayomiliki asilimia 30 ya hisa katika TICTS, huku Kampuni ya Hutchison Port Holdings (HPH) ya Hong Kong, China, ikimiliki asilimia 70 ya hisa katika TICTS.
Zambi ambaye Aprili 24, mwaka huu, aliwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu utendaji usioridhisha wa TICTS na kutaka mkataba huo usitishwe na Bunge kupitisha azimio kuhusu hoja hiyo, alisema kauli ya Spika juu ya kauli ya Karamagi haimaanishi kwamba Baraza la Mawaziri halifayi makosa.
Alisema kama kweli Baraza hilo liliamua kuhusu mkataba huo, basi lilikiuka Sheria ya Manunuzi Serikalini namba 21 ya mwaka 2004.
''Kauli ya Spika si kwamba, Baraza la Mawaziri halifanyi makosa. Lilikiuka Sheria ya Manunuzi Serikalini,'' alisema Zambi.
Alisema hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali katika taarifa yake ya ukaguzi ulioishia Juni 30, mwaka 2007, ilitaja kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi serikalini katika mkataba wa TICTS.
''Hivyo, hoja yangu bado iko valid (ina maana) na maamuzi ya Bunge hayafutwi na kauli ya Spika kwani ni mali ya Bunge,'' alisema Zambi.
Naye Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, alisema hawezi kulumbana na Spika katika jambo ambalo amekwishalitolea maamuzi, lakini akasema hakuna anayeweza kuyathibitisha majibu hayo ya Ikulu.
Awali, akitoa uamuzi kuhusu ushahidi uliowasilishwa na Karamagi ofisini kwake kuthibitisha kauli hiyo, Spika Sitta alisema baada ya kuwasiliana na Ikulu, iliwasilisha majibu ofisini kwake yanayoeleza kuwa mkataba wa TICTS ulifuata taratibu zote za kiserikali.
''Mheshimiwa Karamagi alileta barua, lakini hazikutosheleza sana, hivyo, nikawasiliana na Ikulu. Majibu yaliyokuja ni kwamba mkataba wa TICTS ulifuata taratibu zote za kiserikali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Karamagi hakusema uongo, bali alisema ukweli,'' alisema Spika Sitta.
Karamagi alilazimika kuwasilisha ushahidi huo baada ya kutakiwa na Spika Sitta kufanya hivyo kutokana na kauli kwamba, mkataba huo wa TICTS uliongezwa kwa kufuata sheria na kwamba, uliamuliwa na Baraza la Mawaziri kutokana na ufanisi mzuri wa kitengo hicho. Alitoa kauli hiyo katika Mkutano wa 11 wa Bunge, Aprili 24, mwaka huu.
Baada ya kutoa kauli hiyo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah, aliomba mwongozo wa Spika na kumtaka Karamagi athibitishe kama mkataba huo uliamuliwa na Baraza la Mawaziri kwa vile anavyoelewa yeye (Anna) wakati huo Karamagi hakuwa waziri.
Hata hivyo, Anna Abdallah alipoulizwa na Mwananchi nje ya ukumbi wa Bunge jana, alisema ameridhika na majibu ya Ikulu kwa vile taratibu za kiserikali ni nyingi na kwamba hakukuwa na ulazima majibu yatolewe kama alivyofikiria yeye.
''Mimi nilichohitaji ni ushahidi kama kweli Baraza la Mawaziri liliamua kuhusu mkataba ule. Sasa kama Ikulu imesema mkataba ule ulifuata taratibu zote, full stop (mwisho).Taratibu ziko nyingi, nimeridhika na majibu hayo na siyo lazima iwe kama nilivyofikiria,'' alisema Anna.
Aprili 25, mwaka huu Bunge lilipitisha azimio la kuitaka serikali isitishe mara moja nyongeza ya mkataba wa miaka 15 uliofikiwa kati yake na TICTS kwa maelezo kwamba ulikiuka sheria.
Mkataba huo uliongezwa na serikali Desemba 30, mwaka 2005 na kufikia miaka 25 badala ya miaka 10 ambao ulikuwa unaisha mwaka 2010.
Azimio hilo lilipitishwa na karibu wabunge wote isipokuwa Karamagi, aliyetoa sauti bungeni ya 'siyo' baada ya Spika kuhoji wabunge wanaoafiki na wasioafiki azimio hilo lipite.
Azimio hilo lilipitishwa na Bunge baada ya Zambi kuwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu utendaji usioridhisha wa TICTS.
Katika maelezo kuhusu hoja yake, Zambi alisema mkataba huo uliongezwa kinyume cha sheria kwa kuwa tayari utendaji wa TICTS ulikwishashuka na kushindwa kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkataba huo.
Pia alisema ripoti ya CAG), ambayo iliweka bayana kuwa mkataba huo ulikuwa batili.
''Mheshimiwa Spika, katika taarifa yake ya ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya Umma kwa mwaka ulioishia 30/06/2007, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) pia amebaini upungufu mkubwa sana kwa upande wa TICTS. Ametaja pia kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi serikalini, kukiukwa kwa mkataba wenyewe wa TICTS na serikali. Kwa ujumla amesema nyongeza hiyo ya mkataba ni mbaya na haifai. Kwa ujumla ni kwamba
mkataba hauna nguvu kisheria,'' alikaririwa Zambi akisema.
Alisema kwa mfano, nyongeza ya mkataba kwa miaka 15, ilifanywa kupitia barua Na. TYC/R/160/32 ya Septemba, 2005, iliyoandikwa na kutiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Basil Mramba, ambayo pamoja na mambo mengine, ilimtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ahakikishe muda wa mkataba unaongezwa kuwa wa miaka 25.
Zambi alisema miongoni mwa mambo ambayo hayakutekelezwa kama mkataba ulivyotaka, ni pamoja na TICTS kuongeza ufanisi, matengenezo ya vifaa na malipo ya mrahaba.
Alisema msongamano wa makontena katika bandari ya Dar es Salaam uliongezeka kwa kiwango kikubwa na hivyo, kufanya baadhi ya meli kuacha kuja nchini.
Alitoa mfano kuwa mwaka jana msongamano uliongezeka na kufikia asilimia 88.7 ikilinganishwa na kiwango cha kimataifa cha asilimia kati ya 50 na 60.
''Mheshimiwa Spika, kimsingi mambo yote hapo juu yanaonyesha upungufu mkubwa uliopo serikalini na hususan katika suala hili. Hivyo, ni wajibu wa Bunge lako tukufu kuisimamia serikali kikamilifu ili isiendelee kuvunja kwa makusudi sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ambazo zipo kwa mujibu wa sheria,'' alisema Zambi.
Kutokana na hali hiyo, aliliomba Bunge kupitisha azimio la kusitisha mkataba wa TICTS ili upitiwe upya kwa maslahi ya taifa.