Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dk Baghayo Saqware amesema kutokana na utekelezaji wa Sera nzuri chini ya uongozi mahiri wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Sekta ya Bima imeendelea kuimarika na kupata mafanikio katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, ikiwa pamoja na kuongezeka kwa watoa huduma, ongezeko la ajira, wanufaika wa huduma, mali na mitaji ya bima.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Agosti 18, 2025 jijini Dar es Salaam, Dk Saqware amesema katika idadi ya watoa huduma za bima imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi kufikia 2,425 Juni 2025, sawa na ongezeko la jumla la asilimia 144.2. Ongezeko hilo ni sawa na wastani wa asilimia 22.1 kwa mwaka.
“Aidha, katika kipindi hicho, Mamlaka imeongeza aina mpya ya watoa huduma ikiwa ni pamoja na watoa huduma za afya (HSPs), warekebishaji na watengenezaji magari (ARMs) na Watoa Huduma Kidijitali. Vilevile, kampuni za bima mtawanyo nchini zimeongezeka kutoka kampuni moja (1) mwaka 2021 hadi kampuni nne (4) mwaka 2025,” amesema.
Kuhusu ongezeko la wanufaika wa huduma, Dk Saqware amesemawameongezeka kutoka milioni 14.2 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 25.9 mwaka 2024, sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 82.4 katika kipindi cha miaka minne, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 22.2 kwa mwaka.
Katika ajira rasmi amesema katika soko la bima zimeongezeka kutoka wafanyakazi 3,527 mwaka 2021 hadi kufikia wafanyakazi 6,916 tarehe 30 Juni 2025 sawa na ongezeko la asilimia 96.1. Ongezeko hilo ni sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 18.3 kwa mwaka.
Kuhusu mali za bima amesema thamani ya mali katika soko la bima imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.277 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 2.340 mwaka 2024, sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 83.3, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 16.3 kwa mwaka. Kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2025 (Januari – Juni), thamani ya mali katika soko la bima iliongezeka kutoka shilingi trilioni 2.340 mwishoni mwa mwaka 2024 hadi kufikia shilingi trilioni 2.495 kufikia tarehe 30 Juni 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 6.6.
“Aidha, thamani ya mitaji katika soko la bima imeimarika kutoka shilingi bilioni 416.0 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 847.3 mwaka 2024, sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 103.7, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 26.3 kwa mwaka. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, thamani ya mitaji katika soko la bima iliongezeka kutoka shilingi bilioni 906 mwaka 2024 hadi bilioni 993 kufikia Juni 30, 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.5;”
Dk Saqware pia amezungumzia uandikishaji wa ada za bima katika soko la bima nchini akisema umeongezeka kutoka shilingi bilioni 911.5 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 1.418 mwaka 2024, sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 55.6 katika kipindi cha miaka minne, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 11.7 kwa mwaka.
“Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Juni 2025, uandikishaji wa ada za bima umefikia shilingi bilioni 831.8,” amesema.
Katika kipindi hicho pia amesema mchango wa bima katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 2.01 mwaka 2023 na unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 3 ifikapo mwaka 2030;
Amesema pia katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, kumekuwa na ongezeko la bidhaa mpya za bima, ambapo kwa wastani bidhaa 15 mpya zimekuwa zikipewa idhini na Mamlaka kila mwaka kwa ajili ya kuuzwa katika soko la bima nchini. Katika kipindi cha Januari hadi Juni 2025, jumla ya bidhaa 10 mpya za bima zimepewa idhini na Mamlaka kuingia sokoni zikiwemo bidhaa za bima za kilimo na ufugaji;
“Kiwango cha ubakizaji bima nchini kwa Bima za Kawaida kimeongezeka kutoka asilimia 55.9 mwaka 2021 hadi asilimia 58.5 mwaka 2024. Aidha, kiwango cha ubakizaji bima kwa Bima za Maisha kimeongezeka pia kutoka asilimia 85.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 86.2 mwaka 2024;
“Ulipaji wa madai ya bima umeongezeka kutoka shilingi bilioni 397.6 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 592.1 mwaka 2024, sawa na jumla ya ongezeko la asilimia 48.9 katika kipindi cha miaka minne, ikiwa ni wastani wa ongezeko la asilimia 10.5 kwa mwaka. Aidha, wastani wa muda unaotumika na kampuni za bima kulipa madai ya bima yasiyo na utata umeimarika kutoka wastani wa siku 73 hadi ndani ya wastani wa siku 45,” amesema.
Kuhusu mchango wa Sekta ya bima kwenye mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali ikiwemo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Kampuni (corporate tax) pekee, umeongezeka kutoka shilingi bilioni 137.7 mwaka 2022 hadi kufikia shilingi bilioni 18m3.1 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 32.97.
Katika hatua hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Mwenyekiti wa Bodi ambaye ameendelea kutoa dira, ushauri na miongozo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Sekta ya Bima nchin.
Hatua nyingine ni kufanyika kwa matamasha ya kibiashara, ambappo Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi, imeendelea kuratibu na kushiriki kwenye matamasha ya kibiashara ya bima ndani na nje ya nchi.
“Matamasha hayo yamelenga kuhamasisha Umma kuhusu dhana na umuhimu wa bima, kujenga mahusiano ya kibiashara, na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika Sekta ya Bima,” amesema.
Katika kipindi hicho, Serikali imeboresha sera na sheria hali iliyoongeza wawekezaji.
“Idadi ya kampuni za bima na kampuni za bima mtawanyo (reinsurance) zimeongezeka nchini. Wawekezaji wapya wamevutiwa na mazingira bora ya ufanyaji wa biashara ya bima na uthabiti wa kiuchumi,” amesema.
Pia, Dk Saqware ametaja kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 na Kanuni zake kuwa ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusainiwa na Mheshimiwa Rais, ikiwa ni hatua ya kihistoria inayolenga kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za afya kupitia mfumo wa bima.
“Aidha, mwaka 2024, Serikali kupitia Wizara ya Afya iliandaa na kupitisha Kanuni za Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha utekelezaji wa Sheria hiyo muhimu. Kanuni hizo zimeweka misingi ya utekelezaji, usimamizi, na ushirikishwaji wa wadau katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya bima ya afya kwa kila Mtanzania,” amesema.
Ametaja pia maboresho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 akisema yameongeza wigo wa bima za lazima katika maeneo muhimu ikiwemo bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi (imported goods) kuwa na bima za kampuni za ndani, majengo ya Umma na biashara kuwa na bima, vivuko na pantoni kuwa na bima.
“Kupitia ushirikiano na wadau, Serikali imeanzisha Konsotia ya Bima ya Kilimo kwa lengo la kuwahudumia wakulima, kupunguza athari za majanga ya asili, na kuongeza tija katika sekta ya kilimo. Hii ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa wakulima wanakuwa na uhakika wa kipato hata wanapokumbwa na majanga.”
Mbali na kilimo, ametaja pia kuanzishwa kwa konsotia ya mafuta na gesi ikiwa ni eneo la kimkakati kwa uchumi wa nchi, kwa lengo la kusimamia hatari na kulinda uwekezaji katika maeneo haya muhimu kwa uchumi wa nchi.
Amesema pia Serikali imefanikisha hatua kubwa ya kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na taasisi nyingine muhimu za Serikali.
“Miongoni mwa taasisi zilizounganishwa ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Mamlaka ya Usafiri Baharini (TASAC), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), na taasisi nyinginezo,” amesema.
Mikakati mingine iliyotajwa ni pamoja na kuimarisha matumizi ya kidigitali katika mfumo wa kidijitali wa usajili unaowawezesha wananchi na wawekezaji wanaotaka kutoa huduma za bima nchini kuweza kujisajili mahali popote walipo.
Aidha, amezungumzia uanzishwaji wa wa huduma ya bima ya Takaful ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaofuata misingi ya Kiislamu nao wanapata huduma za bima zinazozingatia imani zao.
“Hatua hii imepanua wigo wa ujumuishaji wa kifedha katika jamii kwa kuwa aina hiyo ya bima inawezesha makundi mbalimbali ya wananchi kutumia aina hiyo ya bima kulinda mali zao,” amesema.