16 Novemba 2020
Rais Magufuli: Cheo cha Waziri Mkuu hakina ‘uhakika’
OFISI YA WAZIRI MKUU, TANZANIA: OFISI YA WAZIRI MKUU, TZ
Rais wa Tanzania John Magufuli hii leo tarehe 16 November 2020 amemuapisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa awamu ya pili na
kumtahadharisha kuwa nafasi yake haina uhakika wa kuwa nayo kwa miaka mitano.
Rais Magufuli amemsifia Majaliwa akisema ni mchapakazi na muadilifu na anastahili nafasi hiyo, japo si sahihi kwa watu kuhesabu kuwa atasalia kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo.
“Baada tu ya kumchagua kuwa Waziri Mkuu naona kuna watu wanasherehekea na baadhi ya magazeti yanaandika kuwa atakuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10. Hilo si sahihi.”
Rais Magufuli ameeleza kuwa ni Waziri Mkuu mmoja tu Fredrick Sumaye (1995-2005) ambaye amedumu katika wadhifa huo kwa miaka mitano na wengine wote walikaa kwa vipi fi vifupi zaidi.
Majaliwa alihudumu kama Waziri Mkuu katika miaka mitano ilopita ya awamu ya kwanza ya Magufuli.
''Guarantee (uhakika) pekee alokuwa nao (Majaliwa) ni wa miaka mitano ilopita.
Miaka mitano ijayo linaweza kutokea lolote...Huo ndio ukweli. Kitu pekee kitakachomfanya abaki hapo ni utendaji kazi wake...Majaliwa ni mtendaji mzuri na ndio maana sikupata shida kumchagua tena,'' ameelezea rais Magufuli.
Kwa upande wake, baada ya kula kiapo katika ya Ikulu Chamwino, Waziri mkuu Majaliwa amesema:
''Namshukuru sana rais kwa kunipa nafasi tena, Mh. Rais utaunda Baraza la Mawaziri muda mfupi ujao jukumu langu ni kusimamia utendaji kazi wao, nitapita kila wizara na kuwataka waweke mpango kazi wa yale yaliyoanzishwa kwenye Ilani na kwenye hotuba yako''.
Bwana Majaliwa ameonesha atakayoyapa kipaumbele ikiwemo kupanda kwa bei ya saruji na kuahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
''Tulipokuwa kwenye kampeni, kumeibuka kupanda kwa bei ya saruji bila sababu ya msingi, hatutarajii saruji kuwa na bei kubwa...sasa naanza na hili la saruji'', amesema Bwana Majaliwa.