elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
SERIKALI ya awamu ya tano, imeleta mchango mkubwa katika kukamilisha na kuleta mafanikio katika sekta ya reli nchini. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa uongozi wa Rais John Magufuli umekuwa wa kipekee kutokana na mafanikio na malengo aliyoyafikia katika sekta ya reli.
Kwa mujibu wa Kadogosa, serikali imesaidia kuunganisha TRC iwe moja ambapo awali kulikuwa na mashirika mawili RAHACO na TRL ambayo yameungana na kutengenea bodi moja ya TRC inayosaidia katika usafirishaji ukizingatia kabla njia na uendeshaji vilikuwa na wamiliki tofauti.
Aidha, uwezo wa treni za kubeba mizigo kwa mwaka umeongezeka, na kwa takwimu zilizopo mwaka 2016-2017 treni ilibeba jumla ya tani 293,000, mwaka 2017-2018 ilibeba tani 366,000 na kwa mwaka 2018-2019 treni imebeba jumla ya tani za mizigo 426,000 na kuongeza kuwa treni za kubeba abiria kwa mwaka huu zimebeba abiria 556,000 ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2015, ambapo kwa mwaka kulikuwa na abiria 385,000.
Kadogosa alisema serikali ya awamu ya tano pia imeongeza mapato yake kupitia TRC kutoka Sh. bilioni 15 iliyokusanywa mwaka 2015 hadi Sh. bilioni 45.5 ambazo zimekusanywa mwaka huu. Alisema Shirika la Reli limeamua kuongeza safari kutoka Dar es Salaam mpaka Moshi ambazo zitaanza kuanzia wiki ijayo, hivyo treni itakuwa ikisafirisha abiria mara tatu kwa wiki.
Kadogosa alisema kuna mradi mikubwa miwili inayoendelea ambayo ni ujenzi wa njia ya kati ambao umekamilika kwa asilimia 70 na mpaka sasa, ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Isaka utakaosaidia kuzihudumia nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Aidha, alieleza juu ya ujenzi wa reli ya kisasa ambao ni mradi wa pili umekamilika kwa zaidi ya asilimia 70 mpaka hivi sasa na muda si mrefu mradi huo utakamilika, na kuongeza kuwa reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ambayo imegharimu Sh. bilioni 2.7 mpaka sasa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 72, huku ujenzi wa reli kutoka Morogoro-Makutupora ukikamilika kwa asilimia 42.
Alisema miradi hiyo imeleta fursa na kutoa ajira kwa watu wengi nchini ikiwamo wafanyakazi zaidi ya 14,000 ambao asilimia 88 ni Watanzania pamoja na makandarasi ambao asilimia 52 pia ni Watanzania, asilimia 48 wakiwa wa kutoka nje.