Ahsante sana kwa shule ya gesi
Meneja Wa Makampuni meneja wa makampuni,
Kuna hawa wachina wa Anric gas company CNG hapo awali waliingia mkataba na DIT( Dar Institute of Technology) kutengeneza na kufanya installation ya mifumo ya gesi ya CNG kweny magari, je, serikali haiwezi kutumia makampuni yake kufanya hizo installation na kusaidia kupunguza gharama za maisha kwa wananchi hata kwa magari ya serikali na umma?
Je, ile kampuni ya pan Africa energy pale ubungo maziwa ni ya nani inahusika na kujaza CNG?
Nimeona magari ya Dangote yamefungwa mifumo ya gesi CNG je anapata wapi gesi asilia? Anamiliki mitambo yake mwenyewe?
Kwanini vituo vya gesi ni kimoja tu kipo ubungo tu? Kwanini visiwepo sehemu nyingine mikoani n.k?
Je, miradi mikubwa kama hiyo kwa nini wasipewe taasisi Kama JWTZ kwa mikakati kutokana na credibility ya taasisi zetu?
Ukiacha EWURA na mamlaka zingine, idara yetu ya usalama wa Taifa ( TISS) ina nguvu gani au uelewa gani na mamlaka na uwezo wa kushauri mambo muhimu ya rasilimali Kama gesi? Je, kuna au tuna vijana wangapi mpaka sasa katika Taifa letu waliosoma ndani na nje ya nchi na kubobea kwenye taaluma ya gesi?
Serikali inakwama wapi kubadilisha mifumo yote ya mafuta na kuweka iwe ya gesi mpaka pikipiki Kama gharama za mafuta ni kubwa?
Kwanini gesi isitumike kuzalisha umeme kurahisisha kukua kwa uchumi wa viwanda?
Ahsante sana nitaendelea kuuliza na kijifunza hapa.
Ahsante sana kwa maswali mazuri na yenye kuongeza ufahamu.
Tatizo kubwa lililopo kwenye uwekezaji katika fursa zilizopo kwenye sekta ya gesi asilia ni mtaji, ujuzi, uzoefu na utaalamu. Hapa ndipo penye tatizo, sasa ili kuweza kutatua hilo mara nyingi kampuni au taasisi zetu za wazawa zimekua zikiingia mikataba na makampuni ya kigeni ili kuunganisha nguvu ya kifedha, ujuzi, uzoefu na utaalamu. Lengo kubwa ni kupata uzoefu alafu baadaye wanajitegemea wenyewe. Ni kweli tunao mafundi wenye uwezo wa kuzibadili injini za petroli na dizeli zitumie gesi asilia na wanaofanya hiyo kazi sana sana ni wataalamu wa DIT. DIT pia wanatoa mafunzo kwa watanzania wanaotaka kujifunza fani hiyo ya kubadili injini zitumie gesi.
PanAfrican Energy Tanzania (PAET) ni kampuni tanzu ya Orca Energy. Orca Energy ni kampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi iliyowekeza Tanzania. Kampuni inajishughulisha na uendelezaji na usambazaji wa gesi asilia nchini Tanzania kupitia kampuni tanzu ya PanAfrican Energy Tanzania Limited. Hivyo ndio kampuni inayo miliki na kuendesha kitalu cha gesi cha Songo Songo.
PAET iliwekeza zaidi ya TZS 14.3 bilioni kabla ya gesi ya kwanza kuuzwa, na zaidi ya TZS 219 bilioni katika uchimbaji visima, miundombinu na miradi ya mitaji tangu wakati huo. PAET inasambaza gesi inayotumika kufua umeme Tanzania na kuendeleza viwanda vikubwa jijini Dar es Salaam. Kampuni pia inasambaza gesi asilia iliyokandamizwa au shindiliwa (CNG) kwaajili ya kutumia kwenye magari.
Ni kweli kabisa magari ya Dangote yamefungwa mifumo ya CNG.
Dangote anamiliki kituo cha CNG kinachogharimu Sh billioni 21 kilichopo maeneo ya kijiji cha Hiyari Mkoani Mtwara. Imejengwa ndani ya eneo la kiwanda cha Saruji cha Dangote na ina uwezo wa kuhudumia magari 250.
Hiki kituo cha CNG cha Dangote kilijengwa mahsusi kwa ajili ya kuhudumia magari yanayomilikiwa na kiwanda cha Saruji cha Dangote. Kampuni hiyo inamiliki magari zaidi ya 2,000, mengi yakiwa ni malori yanayotumika kusambaza saruji kutoka kiwandani kwenda mikoa mbalimbali. Hivyo wanatumia CNG kama nishati ya kuendesha magari hayo.
Mbali na matumizi ya gesi kwenye malori, kiwanda hicho pia kinatumia mfumo wa gesi kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ya kuzalisha saruji na kuzalisha umeme wa wati 750. Gesi inayonunuliwa na Dangote inatoka kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba kilichopo Mtwara. Kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba ni kiwanda kinachochakata gesi kutoka kitalu cha gesi cha Mnazi Bay.
Ni kweli kabisa vituo vya kujaza gesi asilia ni vichache. Sababu kubwa ni ukosefu wa fedha za kujenga vituo vingine. Lakini Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linampango wa kujenga vituo vitano zaidi vya kujaza Gesi Asilia iliyokandamizwa (CNG) jijini Dar es Salaam. Ahadi ya TPDC ya kuongeza vituo vya kujaza gesi hadi saba, imekuja wakati nchi ilikuwa inakabiliwa na mahitaji makubwa ya vituo kutokana na kuongezeka kwa magari yanayotumia mfumo wa gesi. Vituo vipya vya kujaza gesi asilia vinavyotarajiwa kuchochea na kuongeza upatikanaji wa CNG itakayotumiwa na magari vitajengwa kando ya Barabara ya Sam Nujoma, Feri, Muhimbili, Kibaha na Ubungo.
Serikali kupitia TPDC imewakaribisha watu wa sekta binafsi ikiwemo nawewe kuwekeza katika ujenzi wa vituo vingi vya gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza usambazaji wa gesi na ili watanzania waweze kunufaika na sekta ya gesi asilia katika mikoa yote ya Tanzania.
Lakini pia katika kituo kipya cha kujaza gesi cha Ubungo, serikali kupitia TPDC imepanga kujenga karakana itakayofanya kazi ya kubadilisha magari kutumia mfumo wa gesi.
Kwa sasa, ubadilishaji wa magari kutumia mfumo wa gesi unafanywa na DIT pekee. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kiasi cha zaidi ya Sh.bilioni 100 kwa ajili ya kuiwezesha DIT kujenga vituo vya umahiri ambavyo vitakuwa chachu ya kupika watalaamu wa kada mbalimbali wakiwemo watalaamu wa kufunga mifumo ya gesi kwenye magari yanayotumia mafuta ya petroli na dizeli.
Changamoto kubwa inayosababisha watu taasisi za ulinzi na usalama wasitumike nadhani ni ukosefu wataalamu wa mafuta na gesi kwenye hizo taasisi hizo. Kwasasa taasisi za TPDC, PURA na EWURA ndizo zilizopewa mamalaka kikatiba kushughurika na masuala ya mafuta na gesi kwasababu ya uwepo wa wataalamu wenye ujuzi na uzoefu katika taasisi hizo.
Kuhusiana na TISS sina taarifa kiukweli kwasababu hii ni taasisi nyeti ya serikali inayofanya kazi zake kwa siri.
Kuhusu vijana waliosomea fani za mafuta na gesi Tanzania na nje ya nchi. Sina data za idadi ya waliosomea fani hizi kwasasa. Ila kuna vijana waliosomea uhandisi wa mafuta na gesi, uhandisi wa petroli, jiolojia ya petroli, kemia ya petroli, kemia ya mafuta na gesi, uchumi wa petroli, usimamizi wa mafuta na gesi, sheria ya mafuta na gesi na uhasibu wa mafuta na gesi. Na naweza kusema kwasasa idadi ya wasomi wa mafuta na gesi Tanzania ni kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma hivyo tunategemea watafanya mapinduzi makubwa katika sekta hii mpya.
Kiukweli ili magari yote ya watanzania yatumie gesi asilia tunatakiwa kutengeneza miundo mbinu ya kusafirisha gesi kwenda mikoa yote ya Tanzania na pia vituo vya kujaza gesi asilia vijenjwe maeneo yote ya Tanzania ili watu wenye magari waweze kujaza gesi pale wanapoishiwa. Swala la kubadilisha magari yatumie gesi lilisharuhusiwa na tayari yapo magari yaliyobadilishwa na yanatumia gesi asilia.
Kwa upande wa gesi kutumika kuzalishia umeme. Asilimia 63 (63%) ya umeme tunao tumia Tanzania kwasasa unazalishwa kwa kutumia gesi iliyo gunduliwa Tanzania. Unaweza kuona jinsi gesi asilia ilivyo saidia sekta ya nishati nchini na kupunguza matatizo ya umeme katika taifa letu.
Ahsante sana na karibu sana boss.