Mangula, ambaye alishika nafasi ya katibu mkuu wa CCM kwa kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa serikali ya awamu ya tatu, alitahadharisha kuwa iwapo mambo hayo hayatarekebishwa kwa haraka na kwa kipaumbele kinachostahili, taifa litaelekea pabaya zaidi.
"Utawala wa sasa umetofautiana na tawala nyingine kwa kupungukiwa na mambo matatu ya msingi ambayo ni ubinafsi, kufanyika maamuzi kabla ya kuelimisha wananchi pamoja na kutokuwepo kwa wigo mpana wa majadiliano kuhusu masuala mbalimbali ya mustakabali wa taifa," alisema Mangula.
Mangula alisema hali hiyo imesababishwa na watu wengi wanaopewa uongozi kutokuwa sifa za kuongoza na kwamba wamepata nafasi hizo kwa njia za urafiki.
"Hata utaratibu mzima wa kuwapata viongozi wanaostahili kwa sifa haupo, badala yake mambo yanafanywa kwa urafiki," alisema Mangula ambaye amekuwa kimya kwa muda mrefu. Akifafanua hoja zake hizo, Mangula alisema katika utawala wa sasa ubinafsi ndio umeonekana kuchukua kipaumbele katika kutatua mambo muhimu ya kitaifa.
Mangula aliweka bayana kwamba katika utawala uliopita ubinafsi haukupewa nafasi kwa kuwa kabla kiongozi hajazungumzia jambo lolote, alilazimika kupata mawazo ya chama tawala na wanachama kuhusu anachotaka kuzungumza. Aliongeza kwamba kutotumika kwa mfumo huo ndio sababu ya kupishana kwa kauli za viongozi kunakoendelea kutamba kwenye safu za mbele za vyombo vya habari kwa sasa.
" Tabia ya kutaka kuonekana kuwa wewe ni bora kuliko mwingine ipo, ndio maana leo viongozi, tena wa kutoka chama kimoja, wanapishana kauli kuhusu jambo moja," alifafanua.
Akizungumzia kufanyika kwa maamuzi kabla ya kuwaelimisha wananchi, Mangula alisema hilo ni tatizo linaloendelea kulalamikiwa na Watanzania.
Mangula alisema katika utawala uliopita watu walielimishwa kwanza kabla ya kufikiwa kwa maamuzi.
"Utaratibu wa kuelimisha kwanza kabla ya kufikiwa kwa maamuzi ndio uliokuwa ukitumika, lakini hali sasa inaonekana kuwa tofauti," aliongeza.
Kuhusu kutokuwepo kwa wigo mpana wa majadiliano katika masuala ya kitaifa, Mangula alisema hiyo inatokana na viongozi wachache waliopewa dhamana na wananchi kuamini kuwa mawazo yao yanajitosheleza.
Hoja za Mangula, ambaye kwa sasa anajishughulisha na masuala ya kilimo, zinashabihiana na zile zilizowahi kutolewa na mawaziri wakuu wawili wastaafu, Dk Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba kuhusu mustakabali wa taifa.
Source: Mwanachi