SHUTI LILIKOKIUKA KANUNI ZA MWENDO ZA KISAYANSI
Kuelekea Kombe la Dunia la 1998, wenyeji Ufaransa waliandaa mashindano maalumu ya kupima maandalizi yao.
Wakati huo Kombe la Mabara lilikuwa halijaanza kutumika kupima maandalizi ya Kombe la Dunia. Lilikuja kuanza 2001.
Mashindano hayo yaliyoitwa Tournoi de France yalifanyika 1997 na kushirikisha timu 4; wenyeji Ufaransa, Brazil, England na Italia.
Mechi zilichezwa kwa mtindo wa ligi, kwamba mwenye pointi nyingi ndiyo bingwa. England wakawa Mabingwa.
Mechi ya ufunguzi ilifanyika Juni 3, 1997 dimbani Stade de Gerland mjini Lyon, na kuwakutanisha wenyeji na Brazil.
Ni kupitia mchezo huu uliomalizika kwa sare ya 1-1, ndipo Roberto Carlos alifunga bao la mkwaju wa adhabu ndogo, linalosemekana kukiuka kanuni za mwendo za kisayansi na hadi sasa wanasayansi duniani bado wanaendelea na utafiti kujua mpira uliwezaje kwenda kama ulivyoenda.
Wanasayansi wanne wa Ufaransa; Guillaume Dupeux, Anne Le Goff, David Quere na Christophe Clanet wa taasisi ya utafiti wa kisayansi ya Ecole Polytechnique, walifanya utafiti ambao matokeo yake yalichapishwa kwenye jarida la New Journal of Physics la Septemba 2010.
Wanasayansi hawa walifanya uchambuzi wa majaribio kadhaa ya kimaabara yaliyozaa mlinganyo unaofafanua mwendo wa mpira na nguvu zilizokuwemo ndani yake katika muda wa kitendo.
Wakahitimisha kwa kusema endapo hesabu zitapigwa vizuri, katika umbali ule ule na nguvu ile ile ya shuti, mtu yeyote anaweza kurudia na mpira ukaenda vile vile.
Lakini mwanasayansi wa Brazil, Prof. Luis Fernando Fontanari anasema hiyo haiwezekani. "Hali ya wakati wa tukio kama nguvu ya upigaji, kishindo cha makutano ya mguu wa Roberto Carlos na mpira, na umbali hadi golini, vilikuwa vya nadra sana kiasi kwamba tunaweza kuita miujiza", anasema Profesa huyo wa chuo kikuu cha Sao Paulo -- kinachoheshimiwa zaidi Brazil.
Fontanari ni mmoja wa wahariri wa majarida ya "Physics of Life Reviews" na "Theory in Biosciences," ambayo ni miongoni mwa majarida muhimu zaidi ya kisayansi duniani.
Mwanasayansi mwingine kutoka Israel, Erez Garty, alifanya utafiti wake na kuhitimisha kwa kusema alichofanya Roberto Carlos ni mazingaombwe. Kazi yake iko YouTube.
Sent using
Jamii Forums mobile app