1
TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU KUIMARISHA ULINZI
NA USALAMA WA ANGA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
ILIYOTOLEWA NA WAZIRI WA MAWASILIANO NA UCHUKUZI, MHE.
PROF. M.J. MWANDOSYA(MB.) KWA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 29 JANUARI 2002 Mheshimiwa Spika Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 39(1), naomba kutoa taarifa ya Serikali kwa Bunge lako tukufu kuhusu uimarishaji wa ulinzi na usalama wa anga ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika Kufuatia hatua ya Serikali ya Uingereza kutoa leseni kwa Kampuni ya British Aerospace (Bae) kuiuzia Tanzania mitambo ya kisasa ya rada, pamezuka hoja mbalimbali, ndani na nje ya nchi, zikishutumu kwa nguvu na wakati mwingine kwa jazba, uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kutumia karibu Pauni za Kiingereza milioni 28 kununulia vifaa vya rada. Hoja zote zimelenga katika maeneo yafuatayo:
i. Uhalali wa nchi maskini kama Tanzania kutumia fedha nyingi kwa
kitu ambacho wanadai eti hakitaleta faida yeyote kwa Taifa.
ii. Mitambo ya rada inayoagizwa eti ni ghali mno na ya aina ya teknolojia ya juu mno kuliko mahitaji yetu.
iii. Ipo hofu ya kuwepo mizengwe katika uagizaji huo inayotoa hisia za rushwa.
iv. Baadhi ya maafisa wa mashirika ya fedha wanasema eti mitambo inayoagizwa ni kwa ajili ya shughuli za kijeshi na siyo kuongoza ndege za kiraia.
Kutokana na vuguvugu la mjadala huo Serikali inapenda kutoa maelezo yafuatayo kwa azma ya kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuhusu ununuzi na umuhimu wa mitambo hiyo ya rada.
2. UMUHIMU WA RADA
2.1 Tanzania, kama nchi nyingine zote duniani, tajiri na masikini, inahitaji mitambo ya uchunguzi na uangalizi wa anga pamoja na uongozaji wa safari za ndege ambayo kwa lugha ya kitaalam, inaitwa rada. Kazi kubwa ya rada ni kuziwezesha Idara za Ulinzi wa Anga na Usalama wa Usafiri wa Anga kutambua ndege zinazotumia anga yetu ili kuimarisha ulinzi na kudhibiti usalama. Ukichukua safari za ndege mwezi mzima au kwa saa 24 kuna vilele ambapo ndege huwa nyingi. Mchanganyiko wa ndege kubwa na ndogo hufanya uongozaji wa ndege katika vipindi hivi kuwa mgumu sana. Hali hii husababisha ucheleweshaji na hisia ya anga yetu kutokuwa na usalama wa kutosha.
2.2 Rada za kuongozea ndege hapa nchini hazifanyi kazi na zile za ulinzi ni za zamani. Viwanja muhimu kama Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam (DIA), Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na Mwanza hapa nchini
havina rada kabisa. Uangalizi unategemea waongoza ndege kufuatilia safari kutegemea taarifa za muda wa kuondoka, kasi ya mwendo na ripoti za Marubani kuhusu mahali walipo. Hakika aina hii ya uongozaji ndege inategemea sana uaminifu wa Marubani.
Kwa sababu hiyo:
a) Kuna uwezekano mkubwa wa ajali za ndege kutokea kwa vile Idara ya Usalama wa Usafiri wa Anga inatumia, kwa kiwango kikubwa, uwezo wa binadamu na mawasiliano ya redio. Hali ya hewa ikiwa mbaya mawasiliano huwa si ya uhakika.
b) Upo uwezekano wa ndege kupita juu ya anga ya Tanzania kinyemela.
c) Kubwa zaidi ni suala la usalama wa nchi yetu na kunusuru maisha ya binadamu kwa kuepuka majanga ya ajali.
2.3 Zaidi ya anga yetu, tunadhibiti anga ya Rwanda na Burundi kwa ndege zinazopita zaidi ya futi 24,500. Jukumu hilo tulipewa na Shirika la Kimataifa la Usalama wa Usafiri wa Anga (ICAO) mwaka 1978. Kabla ya 1977 kazi hiyo ilikuwa inafanywa na iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
3. UNUNUZI WA RADA
Mheshimiwa Spika
3.1 Zipo njia mbili mbadala (options) kwa Tanzania kurekebisha hali ya udhaifu katika suala la usalama wa anga ulioelezewa. Njia ya kwanza ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania kununua rada zake na Idara ya Usalama wa Usafiri wa Anga kununua
rada zake. Njia ya pili ni kuwa na mfumo unaounganisha rada hizi.
3.2 Serikali ilianza kulidadisi suala la rada tangu mwaka 1987, na hasa baada ya mitambo ya DIA na KIA kuharibika miaka ya 90. Kwa kuzingatia hali hiyo tarehe 5 Agosti, 1992 Serikali iliteua Kamati ya Wataalam ya kutafiti suala hili na kubuni mfumo wa rada ambao ungekidhi mahitaji ya Tanzania.
3.3 Kamati ya Wataalam ilipendekeza kwa Serikali ujenzi wa mfumo wa rada wa mtandao wa pamoja. Ilidhihirika kwamba mfumo wa aina hii ndio pia uliojengwa kwenye nchi nyingine za Ki-Afrika na ni wenye ufanisi zaidi. Aidha gharama zake ni pungufu ukilinganishwa na njia ya mwanzo ya kila Idara kuwa na rada zake.
3.4 Kufuatia mapendekezo ya Kamati hiyo, mwezi Oktoba/Novemba, 1992 Serikali ilialika zabuni kwa kutumia selective bidding. Katika zabuni masharti yafuatayo
yaliwekwa:
a) Uwezo wa Kampuni wa kutoa mitambo hiyo;
b) Gharama yake;
c) Huduma baada ya mauzo;
d) Utaratibu wa kupata fedha za kununulia mitambo hiyo;
e) Mitambo ambayo itakidhi mahitaji ya ulinzi na ya kiraia.
f) Wazabuni wote walitakiwa kuhakikisha kwamba mitambo inayoletwa, inayohusu usalama wa anga, inazingatia kanuni, taratibu na mahitaji yote kama yalivyobainishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usalama wa Anga (the International Civil Aviation Organisation).
3.5 Makampuni manne ya kimataifa yalialikwa kutoa mapendekezo:
a) Marconi Radar System ya Uingereza;
b) Thomson CSF ya Ufaransa;
c) Westinghouse ya Marekani;
d) Siemens Plessey SPS, ambayo hivi sasa inaitwa British Aerospace, (BAe) ya Uingereza. Kampuni moja ya Canada, Reytheon, ilileta pendekezo baada ya muda wa zabuni kupita, na nje ya utaratibu. Pendekezo hilo halikukubaliwa.
4. UCHAGUZI WA RADA BORA
4.1 Baada ya uchambuzi wa kitaalam uliofanywa, SPS ilionekana kukidhi masharti yote muhimu. Rada za aina ya Watchman na Rada Kuu za Kampuni hiyo, zilichaguliwa.
4.2 Mwezi Julai 1993 SPS iliwasilisha rasmi mpango mzima wa utengenezaji wa mitambo na utaratibu wa ununuzi.
4.3 Baada ya kuchambua mapendekezo yao, Serikali, mwezi Novemba, 1993 iliiarifu SPS kukubali mitambo iliyopendekezwa pamoja na taratibu za ununuzi.
5. GHARAMA ZA MRADI
Mheshimiwa Spika
5.1 Baada ya majadiliano marefu, mwezi June 1994 Serikali na Kampuni tulikubaliana utaratibu wa kununua mitambo. Mapendekezo ya awali ya Kamati ya wataalam yalionyesha thamani ya mitambo hiyo ilifikia kiasi cha USD 88 milioni.
5.2 Tarehe 11 Februari, 1995 Serikali iliamua kimsingi mradi huo utekelezwe baada ya
kujadili taarifa ya Kamati ya Wataalam. HAZINA na BENKI KUU walithibitisha kwamba mradi huu usingekiuka masharti yaliyokuwa katika mikataba ya Enhanced Structural Adjustment Facility na Policy Framework Paper (ESAF/PFP) kati yetu na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB).
5.3 Baada ya kutafakari zaidi kuhusu gharama ya mradi, Serikali ya Awamu ya Tatu, mapema mwaka 1996, iliona ipo haja ya kupitia tena mradi huo na kuamua kuutekeleza kwa awamu, na kutaka marekebisho yafanywe kwenye muundo wa gharama na ulipiaji wa mradi.
5.4 Tarehe 5 Machi 1997 Serikali iliagiza Mamlaka zinazohusika kukamilisha suala hili kwa mtazamo wa kupunguza gharama za mradi.
5.5 Mwezi Septemba 1997 Serikali ilikubaliana na Kampuni kuhusu idadi ya mitambo ya rada na kujenga mfumo wa uwiano. Thamani ya mradi inajumuisha mitambo, huduma, mafunzo, akiba ya vipuri vya mitambo ya rada, na mishahara ya wahandisi wa muda wa kigeni, kwenye Mkataba wa Mauzo.
5.6 Kufuatia taarifa ya awali ya Mtaalam Mwelekezi ambayo ilikubaliana na mpango wa Tanzania wa kununua rada za kisasa, tarehe 16-17 Oktoba, 1997 Serikali ya Tanzania ilikuwa na mazungumzo na Barclays Bank kuhusu Mkataba wa mkopo.
Kwa mujibu wa Mkataba huo Barclays Bank walikubali kutoa mkopo wa masharti nafuu. Mkopo huo umezingatia masharti ya IMF/WB kwa Tanzania kuhusu vigezo vya unafuu.
5.7 Aidha, mkopo huo ulizingatiwa kwenye mazungumzo ya Serikali na Mashirika ya Fedha ya IMF/WB kuhusu nchi yetu kuwa na uwezo wa kulipa madeni yake na pia kuendelea na mfumo/utaratibu wa kufutiwa madeni hayo (Debt sustainability analysis of the HIPC process).
5.8 Hadi sasa Serikali imeshafanya malipo ya awali ya USD 5.4 milioni. Malipo hayo yalihitajika ili Kampuni iweze kuanza matengenezo ya mitambo kwani haipatikani katika hali iliyo tayari kwenye maduka au bohari za viwanda. Kwa kawaida
hutengenezwa kukidhi mahitaji maalum na baada ya Mikataba kusainiwa.
6. MAONI YA WATAALAM WAELEKEZI
6.1 Katika jitihada za kuwa na muafaka na wahisani na taasisi za fedha za Kimataifa, Serikali iliridhia pendekezo la Benki ya Dunia kuteua mtaalam wa safari za anga kufanya uchunguzi kuhusu uamuzi wa Serikali ya Tanzania kununua mfumo huo wa rada.
6.2 Benki ya Dunia ilimteua mtaalam wa safari za anga kutoka Shirika la TECN-ECON la Uingereza kufanya kazi hiyo. Mtaalam katika uchunguzi wake, alitembelea Tanzania na kufanya mahojiano na wataalam wa safari za anga hapa nchini. Mtaalam huyo aliunga mkono na kusisitiza umuhimu wa uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kununua rada.
6.3 Ili kupata maoni ya ziada kuhusu mradi huu, Benki ya Dunia iliteua mtaalam wa pili kutoka kundi la makampuni ya Aerotech ya Marekani kufanya uchunguzi mwingine. Hata hivyo, tofauti na wa kwanza, mtaalam huyu wa pili hakufanya mazungumzo na wataalam wa Tanzania. Aidha, katika taarifa yake, badala ya kuzungumzia umuhimu au la wa Tanzania kutekeleza mradi huu wa rada, alipendekeza Tanzania inunue aina tofauti ya rada kutoka Marekani, badala ya Uingereza. Kutokana na mapungufu hayo ya taarifa ya mtaalam huyu wa pili, Serikali iliamua kuendelea na utekelezaji wa mradi wake wa Rada kwa mujibu wa mahitaji yetu.
7. FAIDA ZA MRADI
Kukamilika kwa mradi huu kutaiwezesha Tanzania:
7.1 Kuziona na kuzitambua idadi ya ndege zinazotumia anga ya Tanzania.
7.2 Kupunguza uwezekano wa ndege zinazopita bila kutambuliwa.
7.3 Kudhibiti vitendo vya ujangili na biashara haramu kupitia ndege na viwanja binafsi vya ndege.
7.4 Kutambua na kuongoza safari za ndege za kiraia kwa ufanisi na hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea ajali za ndege hapa nchini.
7.5 Ukosefu wa rada ya kisasa unatunyima fursa ya kuongeza mapato ya ada ya ndege zinazopita juu ya anga ya Tanzania, ambayo hivi sasa hufikia USD 7 milioni kwa mwaka kwa safari za ndege 114,404. Ni wazi mapato yataongezeka kutokana na
uwezo wa rada kubaini ndege zaidi zinazopita.
7.6 Kujenga imani ya wasafiri wa kawaida, wafanyabiashara, na watalii na hivyo kuwavutia wengi zaidi na kuongeza mapato ya nchi. Mashirika mengi ya ndege yanasita kuja Tanzania kutokana na ukosefu wa vifaa vya usalama wa anga yetu.
7.7 Faida kubwa zaidi ni kwamba mradi huu utatuwezesha kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa.
8. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika
8.1 Kumekuwa na maoni mengi na yanayotofautiana kuhusu Mradi huu. Wapinzani wa mradi wanasema, badala ya kununua rada, Serikali ya Tanzania itumie fedha za mradi huu kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji, afya na elimu. Ni kweli Tanzania ni nchi masikini. Wananchi wa Tanzania tunahitaji maji, hospitali na shule. Suala hili Serikali inaendelea na daima itaendelea kulishughulikia.
8.2 Hata hivyo, ingefaa ikumbukwe kwamba, pamoja na maji safi na salama, shule na huduma za afya, wananchi wana haki ya kuhakikishiwa ulinzi na usalama wa Taifa lao ili waendelee kushiriki katika shughuli za maendeleo yao na Taifa kwa jumla.
8.3 Suala la kuwepo kwa rada ya matumizi ya kiraia tu limezungumzwa sana. Katika usalama wa anga huwezi ukatenganisha ule wa kiraia tu na ule wa ulinzi wa nchi. Hata kama tungeamua kununua rada ya matumizi ya kiraia tu, tungefanya hivyo
katika mpango mzima wa tathmini ya usalama na ulinzi wa anga yetu. Hivi ndivyo inavyofanyika duniani kote. Taratibu za ununuzi wa rada yetu zimezingatia ukweli huo na hali hii halisi. Ikumbukwe pia kwamba teknolojia zote za usalama wa anga, hata zinazotumiwa kuongoza ndege za kiraia, zimebuniwa, zimeendelezwa na zimetolewa chini ya leseni maalum na Idara za Ulinzi.
8.4 Kumekuwa na maoni kwamba Tanzania inaweza kununua mfumo wa rada ya kuongozea ndege za kiraia kwa bei nafuu kutoka kwenye makampuni mengine duniani. Uchambuzi wa bei za mifumo ya rada inayozingatia mahitaji ya ulinzi na usalama wa anga umedhihirisha kwamba Tanzania ingetumia fedha nyingi zaidi iwapo ingeamua kununua rada za mifumo tofauti, moja kwa ajili ya kutambua na kuongoza ndege za kiraia na nyingine kwa ajili ya shughuli za ulinzi wa Taifa letu. Ndio maana, kwa makusudi kabisa Serikali imeamua kununua aina ya rada yenye mtandao wenye uwiano.
8.5 Aidha kumekuwa na hoja inayorejewa mara kwa mara kuwa ipo rada ya USD 10 milioni, ambayo ingefaa kuongozea ndege. Ni budi ieleweke kwamba rada ya aina hiyo imo katika mfumo wa mitambo iliyoagizwa. Rada hiyo hutumika katika kuongoza ndege kwenye sehemu ya mwisho ya safari yake kuelekea kutua kwenye uwanja wa ndege. Kwa hiyo ni dhahiri rada hii pekee haiwezi kukidhi mahitaji kama tulivyoyaainisha.
8.6 Ipo hoja kuwa malipo ya awali ya USD 5.4 milioni yamefanywa bila kupitishwa rasmi Bungeni. Malipo hayo yamefanyika kwa mujibu wa Mkataba wa Mkopo baina ya Serikali, BAe na Barclays Bank. Kuhusu hili tunapenda kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa malipo yamezingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha za Serikali.
8.7 Kwa kuwa muda mrefu umepita tangu zoezi la ununuzi wa rada lianze, rada tutakayopata ni ya kisasa zaidi ambayo ni mfumo wa rada aina ya WATCHMAN na Rada Kuu. Rada za WATCHMAN zilianza kutumika mwaka 1984. Tangu hapo zaidi ya 100 zimeuzwa. Uingereza kwenyewe zimewekwa rada kama 15 hivi, katika viwanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na London Heathrow na Gatwick. Nchi nyingine zenye rada za WATCHMAN ni Bahrain, China, Dubai, Finland, Portugal, Spain, Switzerland, Marekani na Zimbabwe. Mfumo wa rada uliobuniwa una uwezo wa kutambua aina yoyote ya ndege, kujua umbali juu ya ardhi, na iko wapi. Uhai wa rada hizi kwa matengenezo ya kawaida ni zaidi ya miaka 20. Ni dhahiri kwamba katika muda wa uhai wa rada, gharama za mradi zitakuwa zimejilipa na tutakuwa na mapato ya ziada.
8.8 Matumizi ya teknolojia ya kisasa kabisa imeweka msingi na uwezekano wa kutumia mfumo mpya wa ICAO ujulikanao kama "S-Mode data link system". Mitambo itakayotumika imesanifiwa na kutengenezwa ili iweze kuwiana na matumizi yanayopendekezwa na ICAO kutumia satelaiti, bila kuifanyia mabadiliko makubwa.
8.9 Tanzania inahitaji kununua rada ya kisasa ili kuimarisha usalama wa anga kwa ajili ya ndege za kiraia na ulinzi wa taifa letu. Hivyo ndivyo walivyofanya wenzetu ambao wana mfumo wa rada za kisasa kabisa zinazokidhi mahitaji ya ulinzi wa mataifa yao na usalama wa safari za ndege za kiraia. Kupuuza hali mbaya ya usalama wa anga kama ilivyo sasa ni kukubali ongezeko la uwezekano mkubwa wa kutokea ajali kubwa katika anga yetu. Gharama za madai ya fidia na bima hakika zitazidi hata gharama za mradi wa rada.
8.10 Malalamiko mengi ya ndege za kimataifa kuhusu usalama wa anga Bara la Afrika yanahusu ndege kupewa kibali na mamlaka moja kupita katika njia, umbali juu ya ardhi na wakati ambapo ndege nyingine imepewa au zimepewa kibali au vibali kupita katika njia ile ile na mamlaka nyingine kutokana na kutokuwepo rada. Mara nyingi ndege zimekuwa karibu kugongana. Baa hili mara nyingi limeepukwa kutokana na umakini wa wanaoendesha ndege. Hata hivyo wanalalamika wanafanya kazi ya ukubwa wa zaidi ya mara 16 wakiwa anga ya Afrika ukilinganisha na anga ya Atlantiki ambako ndege ni nyingi zaidi. Yote haya yanatokana na ubovu wa vifaa vya usalama wa anga.
8.11 Hivyo Serikali imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Uingereza wa kutoa leseni kwa Kampuni ya British Aerospace (Bae) Systems kutuuzia rada. Tunaishukuru Serikali ya Uingereza kwa uamuzi wake huo. Ni uamuzi muafaka kwa wakati muafaka.
9
Mheshimiwa Spika, Thomas Paine, mwanasiasa maarufu wa zama za mapinduzi Marekani, siku moja alitamka "Wale wote wanaotegemea kuvuna baraka za uhuru, lazima …………….wabebe mzigo wa kuulinda". Nilikuwa napitia Jarida linalotolewa na Jeshi letu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Toleo la 4 la Januari 2002. Mhariri, kwa maandishi makubwa anasema "Hakuna Amani Isiyo na Gharama ….. Watanzania Tusifanye Mdhaha". Hili linasisitiza msemo wa wahenga "Gharama ya Uhuru ni kuwa macho siku zote, kuulinda". Mheshimiwa Spika, Naomba nimalizie kwa kumnukuu mmoja wa Wabunge wa Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Anna Kilango, ambaye katika kutafakari suala zima la umaskini na ununuzi wa Rada hii alisema "Hata nyumba ya maskini inafungwa mlango. Pamoja na umaskini wetu tunahitaji ulinzi na usalama. Hata katika umaskini wetu sisi ni Taifa huru". Mheshimiwa Spika, Jukumu la kuimarisha Ulinzi na Usalama wa Anga yetu na ulinzi na usalama wa nchi yetu kwa ujumla, daima litakuwa ni jukumu la Serikali, Bunge lako Tukufu na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Prof. M.J. Mwandosya (Mb.)
WAZIRI WA MAWASILIANO NA UCHUKUZI
DODOMA
29 Januari 2002