Jeshi la Julio laivaa Cameroon
Send to a friend Saturday, 09 April 2011 09:56 0diggsdigg
Mshambuliaji wa timu ya taifa U/23 Mrisho Ngasa akipita katikati ya mabeki wa timu hiyo wakati wa mazoezi jana jioni kwenye Uwanja ea Karume jijini Dar es salaam
Sosthenes Nyoni
TIMU ya Taifa ya Vijana ya Tanzania chini ya miaka 23, leo inatarajia kushusha ama kupandisha presha za Watanzania pale itakapovaana na Cameroon katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Olimpiki utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kushusha ama kupanda kwa presha za Watanzania kutategemeana na matokeo ya mchezo huo yatakayoamua timu hiyo kusonga mbele au kubaki.
Tanzania inashuka dimbani ikiwa na deni la bao moja tu baada ya ule wa awali ulifanyika nchini Cameroon kukubali kipigo cha mabao 2-1kutoka kwa wenyeji.
Tayari kocha Jamhuri Kihwelo'Julio' ameongeza baadhi ya wachezaji katika kikosi chake kitakachoikabili Camoroon leo akiwemo nyota wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mrisho Ngassa akisaidiana na washambuliaji chipukizi wenye kasi Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.
Hata hivyo vijana hao watamkosa nahodha wake Salum Telela aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa awali na tayari nafasi yake amepewa kipa Shaaban Kado akisaidiwa na Himid Mao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Julio alisema kuwa watalazimika kupigana kufa au kupona ili waweze kushinda mpambano huo huku akiwataka wachezaji wake wacheze kwa tahadhari.
"Tuna bao moja la ugenini, lakini hii haitoshi na kujiona tumeshinda kwa vile tunacheza nyumbani, zinahitajika jitihada za dhati ili tuwewe kupata mabao ikiwezekana mengi,"alisema Julio.
Kwa upande wa Ngasa mwenye thamani ya Sh 54m, alisema atajituma kwa uwezo wake wote kwa kushirikiana na wachezaji wenzake ili waweze kushinda mchezo huo dhidi ya Cameroon.
"Nipo hakuhakikisha tunaipeperusha vema bendera yetu, ni matumaini yangu kwa kushirikia wote na mashabiki wetu basi tutashinda na kusonga mbele."Naye kocha wa Cameroon, Dieudonne Nke alisema kuwa wamejiandaa vya kutosha kwaajili ya kukabiliana na wapinzania wao.
"Tuko vizuri sasa, hali ya hewa ya hapa haitusumbui kwasababu inafanana na ya kule kwetu hivyo kilichobaki ni kupigana uwanjani tu na nina hakika tutashinda,"alisema Nke.