Tukibaki Hai, Tutasimulia

Kimeumana
 
Aisee
 
Patam
 
Naendelea
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 29




Na Steve B.S.M





Dereva taksi alipoona mtu amepunga mkono, haraka akasogea eneo la tukio kumkwapua mteja, alisimamisha gari kisha mtu akaingia, naye akamtazama kwenye kioo juu ya kichwa chake, rear mirror, na kuuliza,

"Tunaelekea wapi?"

Bwana huyo aliyempakia alikuwa ni Mpelelezi, amebebelea kamkoba kadogo mkononi, ameketi anamtazama, majira yalikuwa ya saa mbili ya usiku.

"La Palma Hotel tafadhali," Mpelelezi alisema kisha dereva akaondosha chombo chake maramoja, kidogo tu wakawa wapo katika msitu wa magari lukuki, barabara imejaa magari yakienda na kurudi, wakati huo Mpelelezi akawa amebanwa na shughuli zake.

Alikuwa yu 'busy' ameweka 'earphone' masikioni anaskiza jambo, na huku kwenye simu yake akiwa anatazama jambo, alikuwa amemezwa kweli, hakuelewa hata safari iliendaje, akili yake yote ilikuwapo pale alipokuwa ameweka mazingatio.

Basi gari likaenda, mara kadhaa likasimama kwasababu ya foleni za hapa na pale lakini halikuchukua muda sana likaendelea zake na safari.

"Muda huu kuna folenifoleni sana," dereva akazungumza, wakati huo gari limesimama kungoja mataa yaruhusu, aliongea akiwa anamtazama Mpelelezi kama atamsikia lakini haikuwa hivyo, bwana huyo hakuwa na habari naye kabisa, yupo peke yake katika ulimwengu wa pekee.

Walipotoka hapo kwenye mataa, dereva akaongea tena kuhusu msongamano wa barabara na magari yake lakini kama alivyoongea hapo mwanzo, hakuna aliyemsikiza, aliongea mwenyewe, naye hakukoma akaendelea kuongea tena na tena.

Safari ikasonga, mara dereva alipopata nafasi akawa anamtazama Mpelelezi kwenye kioo, safari ilipotumia kama dakika kumi na tano hapo ndo' kitu cha kushangaza kikaanza kujiri.

Dereva alimtazama Mpelelezi kwa kioo, kama kawaida akamwona ametingwa, akakata kona toka barabara kuu na kushika njia ndogo, Mpelelezi hakutambua kitu, gari ikaendelea na safari.

Dakika mbili, tatu, nne, tano, kufumba na kufumbua, dereva akafungua mlango na kurukia nje! Ilikuwa ni kama utani lakini kweli. Mpelelezi alistaajabu kumwona dereva akiwa anabiringita chini, kutazama mbele anaona kiti kikiwa kitupu na gari likienda kasi ya kilomita themanini kwa saa, hajafanya kitu chochote, mara anaona gari kubwa kushoto kwake, limewasha taa na linakuja kwa kasi sana, kufumbua na kufumbua gari hilo likabamiza taksi na kulirusha maili na maili mbali!

Liliruka na kujigeuzageuza angani kabla halijatua kwenye jengo kubwa lilipojipondapomda na kuwa mithili ya karatasi lililofinyangwafinyangwa na kiganja cha mkono.

Gari lile kubwa halikubaki abadan, likatokomea lisijulikane limeenda wapi, kasi yake ilikuwa kubwa mno na ukilitazama mbelez huwezi jua kama limekumbana na shurba yoyote.

Kabla watu hawajajaa katika eneo la tukio, gari moja ndogo ikasimama kwa umbali wa mita kadhaa, mtu mmoja akashuka na kusimama akitazama gari lile lililogongwa, mtu huyu hakuwaa anaonekana maana aliposimamia hapakuwa na mwanga wa kutosha, ni baada ya kitambo kidogo ndipo gari likakatiza na kummulika usoni, alikuwa ni yule mwanamke, Evelyne.

Alisimama akiwa ameyatumbua macho yake kana kwamba haamini anachoona au mboni zake zinamdanganya, mkono wake wa kuume alokuwa ameshika nao mlango wa gari ulikuwa unatetemeka vidole, hakukaa hapo muda mrefu, akaingia kwenye gari na kuondoka zake.

Baada ya dakika chache watu wakawa wamejaa hapo kustaajabu ya ajali hiyo mbaya kupata kutokea karibuni, muda si mrefu gari la kubebea wagonjwa na pia polisi kadhaa wakawa wamewasili eneo la tukio, eneo hilo dogo likawa limesongwa kwa kiasi chake, watu wakitaka kushuhudia na huku wengine wakigeuka wasimuliaji kuelezea namna ajali hiyo ilivyotokea.

Punde, kama baada ya dakika mbili tangu watu wasongamane, mtu fulani akaja upesi katika eneo hilo, alikuwa akikimbia kwa kutupa mikupuo mikubwa ya hatua, alipokaribia msongamano wa watu, akapiga kelele akisema,

"Derevaa! Dereva yupo kule, dereva yupo kule! ..."

Kelele zake zilifanya kila mtu amtazame, upesi pasipo kupoteza muda askari mmoja akachoropoka kwenda naye eneo la tukio. Nyuma yake alifuatwa na mtu wa huduma ya kwanza toka kwenye 'ambulance' iliyofikia hapo.

Walipofika huko wakamkuta Dereva akiwa chini, ana majeraha kadhaa na haonekani kujitambua, upesi akachukuliwa na kupelekwa kwenye gari la huduma, haikuwa mbali na mahali ajali ilipotokea, hapo akapewa huduma ya kwanza na si muda akawa amerejea kwenye fahamu zake, hali yake haikuwa mbaya kiasi cha kumkimbiza hospitalini upesi.

Alihojiwa kwa muda chache na polisi kisha gari ndo' likambeba kumpeleka hospitali kwaajili ya matibabu zaidi, pamoja naye akaongozana na polisi mmoja.

Kwa maelezo ya dereva huyo ni kwamba breki zilifeli akiwa katika mwendokasi, na kwasababu ya kunusuru uhai wake akajitupa nje ya chombo, pia kumnusuru mteja wake aliyekuwa amembeba kwenye gari, akamshauri arukie nje kwani hakukuwa na njia mbadala, hata kama angetumia 'handbrake' bado asingefanikiwa kuisimamisha gari upesi kiasi cha kutoikuta barabara kubwa inayokatiza mbele yao.

Baada ya hapo ikabidi mahojiano yahitimishwe kwasababu ya hali ya mtuhumiwa, nafasi itakapopatikana basi yataendelea siku za usoni.

Wakati gari hilo la wagonjwa likiwa linaendelea na safari yake, dereva aliyekuwa amelazwa kitandani, alipata kuuliza kuhusu hali ya yule bwana aliyembeba, alitaka kujua kama amesalimika ama lah. Wakati anauliza macho yake yalikuwa mekundu yaliyojawa maji.

Mhudu akamjibu,

"Kwa hali ile tuliyoiona, hamna anayeweza kubaki na uhai. Gari limeharibika sana kiasi kwamba tumeshindwa kutoa chochote kile. Kama mwili upo ndani, basi ni mpaka gari litakapokatwakatwa, la sivyo haitawezekana kuutoa."

Dereva aliposikia hayo, akachuruza chozi akirejesha kichwa chake kitandani, baada ya hapo pakawa kimya safari ikiendelea.

Mbali na hapo, lile gari kubwa lililosababisha ajali lilisimama mahali baada ya mwendo wake mkali wa madakika kadhaa. Hapo lilipotuama mazingira yalikuwa tulivu na mwanga hafifu lakini bado ubavu wake uling'aa sababu ya maneno yaliyoandikwa hapo yalikuwa ya rangi nyeupe inayometa, yakisomeka;

'RICKY & PAT CLEANING'

Baada ya muda kidogo, ndani ya gari hilo sauti ya kiume ikavuma, sauti iliyoashiria anaongea na simu. Sauti hiyo ilisema,

"Kila kitu kimeenda sawa," kisha kukawa kimya, kidogo akaongezea, "sawa, majira ya saa sita usiku." Baada ya hapo kikafuatia kimya cha muda mrefu, kimya kilichoashiria kuisha kwa maongezi.


... La PALMA Hotel ... Saa sita usiku ...


Baada ya mteja kwenda zake, mhudumu alinakili taarifa kwenye tarakilishi yake ya mezani kisha akainama kuchukua kitu chini ya meza yake kubwa, aliponyanyuka uso kwa uso akakutana na mtu amesimama hapo kama mstimu, akashtuka! Moyo ulimpasua damu ikaenda mbio.

"Aah! Kumbe ni wewe!"

Mbele yake alikuwa amesimama mwanaume mweusi mwenye miwani, mkononi mwake ameshikilia fimbo ya kumsaidia kutembea.

Mhudumu alitabasamu kiuongo sababu ya taaluma yake kisha akashusha pumzi kuiondoa hofu kifuani mwake, alafu akamuuliza bwana huyo amsaidie na nini, bwana akasema,

"Nimekuja kurejesha funguo."

Mhudumu akamuuliza namba ya chumba chake kisha akatazama kwenye tarakilishi yake kuona rekodi, akaona bwana huyo bado alikuwa na siku tatu za makazi hapo, basi akauliza,

"Mbona unasitisha makazi yako, bwana?"

Bwana akamjibu amepata dharura hivyo hatobakia tena hapo, anapaswa kuondoka. Mhudumu akamweleza utaratibu wa fedha kwa wale wasiomaliza muda wao lakini bwana huyo hakujali, alisema yeye amekuja kutoa tu taarifa hana haja na fidia.

Baada ya kuuweka ufunguo mezani, bwana huyo akaenda zake, wakati akienda, dada wa mapokezi akamsindikiza kwa macho mpaka alipotoka, alikuwa anashangaa namna bwana huyo alivyokuwa anatumia fimbo yake kwa ustadi mkubwa, akaishia kutukuza uwezo wa Mungu.

Bwana yule alipofika zake nje, akapanda taksi na kumwambia dereva ampeleke moja kwa moja mpaka uwanja wa ndege, dereva akatii na kung'oa zake nanga.

Bila shaka bwana huyu alikuwa amelenga kukwea 'Red Eye Flights' - ndege zinazoruka usiku wa manane na kuwasili asubuhi ya mapema.

Muda si mrefu, gari likawa limepotea.


***


Baada ya kuoga, Mitchelle aliketi sebuleni kwa kazi fulani, mwili wake ulikuwa umelowana na hakujali kujikausha.

Alifunika kichwa chake kwa taulo dogo jeupe, taulo kubwa akalitumia kufunikia kiwiliwili chake lakini taulo hilo halikumziba vizuri hivyo sehemu kubwa ya mwili wake ikawa wazi, nalo hakujali, kwani kuna nani wa kumtazama hapa?

Alifungua tarakilishi yake akatazama mambo kadhaa humo, haswa juu ya mnada mkubwa unaotazamiwa kuendeshwa Taiwan siku za karibuni, mnada huo ulikuwa unahusika na mauzo ya vitu na vito vya thamani kubwa.

Baadhi ya mali kwaajili ya mauzo hayo makubwa zilikuwa tayari zishakabidhiwa katika mamlaka husika, na baadhi ya watu wakubwa kiuongozi na kipesa, walikuwa tayari washa-book nafasi zao katika mnada huo adhimu.

Mitchelle alitazama orodha hiyo na akajiridhisha haswa kuwa siku hiyo pesa ipo, tena si ndogo bali ya kutosha, cha muhimu ni kucheza karata zake vema.

Kidogo akiwa katika mafikirio hayo, akakumbuka jambo. Alichukua simu yake akaandika namba fulani toka kichwani kisha akapiga, simu ikaita na kitambo kidogo ikapokelewa na sauti ya kiume, Mitchelle akauliza,

"Vipi?"

Bwana huyo wa upande wa pili akamweleza kuwa kila kitu alichomuagiza amekwishafanikisha, na sasa alikuwa katika zoezi la kumtumia ujumbe kwa njia ya barua pepe.

Baada ya maongezi hayo mafupi, Mitchelle akakata simu kisha akatazama 'inbox' ya email yake, huko akakuta 'messages' mbili, kila moja ikiwa na kichwa chake cha habari, ujumbe wa kwanza uliandikwa RICHIE, wa pili ukaandikwa HILDA, akafungua ujumbe mmoja baada ya mwingine, kwenye kila ujumbe kulikuwa na picha pamoja na maelezo ya anwani ya makazi, akazisoma zote.

Kidogo ujumbe mwingine ukaingia, na mwingine tena ukaingia, jumla zikawa mbili. Akazifungua na kuzisoma, saa hii jumbe hizo zilikuwa zimeambatana na picha za watu wengine mbali na wale wa mwanzo, na picha hizo zikaambatana na anwani zake.

Akazipitia.

Alipomaliza akapiga simu kwenye namba ileile akasema,

"Nimezipata, pesa yako itaingia muda si mrefu." Kisha akakata simu.

Sasa akatulia akifikiria kidogo, mwishowe akajisemea,

"Nitajua ukweli kuhusu kazi yangu, Bryson, kama tupo ndani ya mkataba wetu au lah, bila shaka hatutakuwa maadui."

Alivyosema hayo akajipooza na kahawa yake mezani, kahawa iliyoletwa na Jennifer si punde.


***"
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…