TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - BONUS
Na Steve B.S.M
Usiku haukuwa umeisha, ndo' kwanza ilikuwa saa nne ya dakika za mapema. Richie alitoka kuoga akiwa anajifutafuta na taulo, amevalia nguo ya ndani rangi ya machungwa, miguu yake myembamba ipo wazi ikipuyanga na vinyweleo.
Alipomaliza kujifuta alitupia taulo kitandani kisha akaenendea mafuta ya ngozi, alichovya kidole lakini kabla hajajipakaa simu ikaita. Hakujua simu ipo wapi, alisahau alipoiweka, akarusha macho yake hapa na pale bahati akaiona, ilikuwa kwenye kona ya kitanda, shida nguo zilikuwa zimetanda sana kana kwamba kitanda kimechapwa na bomu, akainyaka simu hiyo na kuitazama, alah! Alikuwa ni Jamal, akastaajabu ni nini muda huu?
"Hello!" Akasema akiketi kitandani, "... Saa hii? ... Serious? ..." Simu ikakata, akatahamaki kwa sekunde, upesi akajivika suruali na shati, nguo zote hizo aliziokota kwenye kile kifurushi kilichokuwepo kitandani kwake, sijui kama nguo hizi zilikuwa safi au lah, alishuka chini upesi na alipofika nje ya ghorofa hili analokaa aliangaza na kidogo tu akamwona Jamal, mwanaume huyo alikuwa amesimama akiegemea moja ya gari, kwa namna alivyoegema hapo unaweza kudhani huo usafiri ni wake, alipomwona Richie anamjia akasimama.
"Ni nini hiko muda huu?" Aliuliza Richie, Jamal kabla hajaongea akatazama kwanza pembeni yake kana kwamba mtu anayehofia usalama wake kisha akasema,
"Richie, najua hili litakuwa 'too much' kwako lakini naomba unisaidie, tafadhali."
Wakati huo wa mazungumzo yakiwa yanaendelea, kuna mtu fulani alikuwa akiwatazama ndani ya gari.
Mtu huyo alitazama vinywa vya watu hawa na kwa kuutumia mkono wake wa kushoto akawa ananakili jambo kwenye 'notebook' yake, alilifanya zoezi hilo kwa sekunde kadhaa kisha akaifunga notebook na kuiweka kwenye 'dashboard'.
Muda mchache ulofuatia, kama dakika zisizozidi tatu, Jamal akamwona mtu fulani akiwa anaingia ndani ya jengo hili la ghorofa, mtu huyo alikuwa mrefu amevalia 'hood' nyeusi iliyofunika kichwa chake, mikono yake ameizamisha kwenye hood hiyo, mwendo wake wa kasi ya wastani, kichwa amekiinamishia chini.
Jamal hakumjali sana bwana huyo kwani hapa wanaishi watu wengi sana, ni ghorofa yenye 'floors' nyingi na vyumba vingi pia, akamchukulia kama mkazi tu wa eneo hili, akapuuza na kuendelea na maongezi yao kama kawaida, baada ya dakika mbili maongezi yakasimama kwa Richie kusema,
"Ningoje hapa, simu yangu niliiacha ndani."
Bwana huyo akatoka zake kuelekea ndani, alikwea ngazi upesiupesi, akashika korido na kuimaliza haraka, kidogo tu huyu hapa mlangoni mwake, chumba namba 43, akachomoa ufunguo mfukoni mwake na kuuchomeka kwenye kitasa, mara mlango ukafunguka wenyewe! Akahamaki, ina maana sikuufunga mlango kwa funguo? Alisema na nafsi yake, akausukuma mlango na kuingia ndani, akatazamatazama, akajiaminisha kila kitu kipo shwari, akaelekea chumbani kwake kuichukua simu iliyomleta huku.
Aliufungua mlango akayatupia macho yake kitandani, akaiona simu, lakini nyuma ya mlango kulikuwapo na mtu amesimama hapo na yeye hakuwa anafahamu jambo, akaichukua simu yake na kuiweka mfukoni, kugeuka, kabla hajaondoka hapa, akashuku kitu mlangoni.
Aliutazama mlango kwa sekunde tano, kuna kivuli kilikuwapo hapo, kivuli kisichoeleweka, moyo ukaguta, haraka akili yake ikamkumbusha yale ya mlango kuwa wazi, hofu ikamvaa, alihisi mwili mwake umepitwa na baridi fulani jepesi ambalo halieleweki, akaupiga moyo konde, mimi ni mwanaume, alisema na nafsi yake, akausogelea mlango taratibu, alipoufikia, katika kiza cha kivuli kile, akaona kiatu cha mtu, buti kubwa jeusi, moyo ukaita pah!
....
Jamal alitazama saa yake ya mkononi, muda ulikuwa umeenda, toka Richie amemuaga kwenda kuchukua simu sasa yapata nusu saa, akajiuliza bwana huyo anafanya nini muda wote huo? Alingoja kidogo, mwishowe akakata shauri kwenda kumwona.
Aliingia ndani akashika ngazi, alizikwea haraka akiziruka mbilimbili, muda si mrefu akawa ameishika korido ya kumpeleka kwa Richie, alipopiga hatua nne akamwona bwana yule aliyevalia hood nyeusi, bwana huyo alikuwa anamjia, uso wake, kama kawaida, ulikuwa unatazama chini, mikono yake ipo ndani ya nguo yake hiyo.
Jamal alimzingatia bwana huyu lakini hakuambulia kitu, hakumwona uso wala hakujua ngozi yake, alichoambulia ni harufu tu wakati akipishana naye, alimsindikiza kwa macho mpaka alipokata kona na kutokomea zake.
Alipofika kwenye mlango wa makazi ya Richie akagonga, kimya, akagonga tena lakini mara hii mlango ukafunguka wenyewe, akashangaa, akausukuma mlango huo na kuingia ndani, akaangaza, hamna kitu, akaita lakini napo kimya, akarudia kuita mara tatu, bado kimya, akaanza kuingiwa na hofu, kutazama mlango wa chumbani upo wazi, taratibu akaujongea na kuusukuma, lah! Akamwona Richie akiwa amelala chini!
"Richie!" Aliita lakini bwana huyo hakuonyesha dalili ya uhai, alikuwa ametulia tuli kana kwamba maiti ndani ya jeneza, upesi akamsogelea na kumtikisa, akampima mapigo yake ya moyo kwa masikio, akabaini bwana huyo alikuwa hai ila ni ufahamu amepoteza, basi upesi akatoa simu yake mfukoni na kupiga 911 kwaajili ya kuomba msaada wa dharura.
......
"Hallo!" Redio ndogo ilitamka ndani ya gari, "kuna mtu amezirai hapa, na mapigo yake ya moyo yako chini sana!" Redio iliendelea kutamka, na bwana aliyevalia hood alikuwa akiskiza kila jambo, ametulia kwenye kiti cha dereva alichokilaza chini kiasi.
Maongezi yaliendelea kidogo katika redio kisha kukawa kimya, baada ya dakika chache sana sauti ya king'ora ikaita kwa mbali, sauti hiyo ikawa inaongezeka kadiri na muda unavyozidi kwenda, kidogo tu eneo hili likaanza kuwakawaka kwa rangi nyekundu na bluu, mara 'ambulance' hii hapa, watu wawili wakashuka upesi na kwenda ndani ya ghorofa hili.
Wakati haya yanatokea, bwana yule mwenye hood alikuwa anatazama kila kitu. Muda si mrefu wale watu waliongia ndani wakatoka na mwili katika 'machela' yao, nyuma wakifuatwa na Jamal. Ilipofikia hapo, bwana huyu ndani ya hood akawasha gari yake na kuondoka zake, akiwa anaenda, Jamal akalikodolea gari hilo ambalo lilikatiza kwa ukaribu kwa kasi yake ya wastani lakini hakuambulia kitu, gari lilikuwa na vioo vyeusi ti, alichobaini ni gari hilo halikuwa na namba zozote za usajili.
***
Uwanja wa Kimataifa wa New York, saa tano asubuhi.
Taksi yenye rangi nyeupe iliingia katika eneo la uwanja wa ndeges ehemu mahususi kwaajili ya kupakulia wateja. Taksi hiyo ilisimama akashuka mwanamke fulani aliyevalia mithili ya walimbwende, nywele zake ni ndefu na ni nyeupe pe, miwani yake ya jua iliziba karibia robo ya uso wake, 'lips' zake zilikuwa zinang'aa na zimelowana, hakika alivutia.
Mwanamke huyu ambaye mwonekano wake ni mpya kabisa machoni petu alikuwa na mwendo mithili ya twiga mwenye kufuata maji ya mtoni, alitembea pasipo papara, kila hatua akiihesabu, kila alipokatiza kati ya watu alionekana wa tofauti kwa namna alivyonawiri, na yeye ni kama vile alilitambua hilo, akaringa.
Mkoba wake wa thamani uliokuwapo begani ulitetemeka, akaufungua na kutoa simu yake, akaitazama kwa kusimama, akatazama nyuma na pembeni yake kisha akapokea simu hiyo,
"Naam," alisema kisha akaendelea na mwendo, mwendo wa madaha kama kawaida, alizungumza na simu hiyo kwa hatua kama tano hivi kisha akasimama, akauliza,
"Umetuma saa ngapi?"
"Tazama kwenye barua pepe yako, utaona," sauti ilimjibu upande wa pili kisha simu ikakata, kabla hajapiga hatua nyingine akafungua 'inbox' ya barua pepe yake, huko akakutana na 'links' mbili za mtandao, akapiga simu.
"Nimeona," alisema kisha akakata simu yake na kuirejesha kwenye mkoba alafu akaendelea na safari yake, baada ya mlolongo mfupi wa abiria akawa sehemu ya ukaguzi, hapo alikuwapo mwanamke mmoja wa makamo ya miaka arobaini, amevalia miwani ambayo ameishusha chini ya pua, macho yake ni kuyarembua lakini kayakaza kuwatazama abiria, ukimtazama vibaya waweza sema anatazama kwa madharau.
Aliipokea 'passport' ya mwanamke huyu kisha akaikagua kwa macho yake, alipomaliza akamtazama mwanamke huyu na kumwamrisha avue miwani yake, mwanamke akatii, akaivua na kumtazama, alikuwa na macho ya kijani, sawa sawia na picha ilokuwepo kwenye 'passport' yake, basi mkaguzi alipojiridhisha akamruhusu aende zake, mwanamke huyo akatabasamu akirudishia miwani yake usoni kisha akasema,
"Tchao!"
Akaenda zake kwa mwendo wake wa madaha, mkononi mwake alikuwa amebebelea tiketi ya ndege kubwa ya Uchina, ndege zao la Boeing yenye uwezo wa kubeba abiria lukuki, humo alijikalia katika kiti cha dirishani na safari ikaanza si muda, ndege ilipong'oa nanga kuidaka anga mwanamke huyu alishusha pumzi ndefu, hatimaye aliiacha ardhi ya Marekani.
Baada ya masaa na masaa ya kudumu angani, hatimaye ndege hii kubwa ilitua salama ndani ya Taiwan katika uwanja wa kimataifa wa Taoyuan, kutokana na utofauti wa ukanda wa muda ulokuwepo baina ya pande hizi mbili, yaani New York na Taipei, Taiwan, ndege hii ilifika katika muda salama kabisa, jua linaangaza vya kutosha, mwanamke huyu akapokelewa na mwanaume aliyekuwa anamngoja muda wote huo, mwanaume huyo alikuwa ameegamia gari kubwa nyeusi, modeli ya Alphard, alipomwona mwanamke huyu alimtambua upesi akampungia mkono, mwanamke akamjia.
"Muda mrefu hatujaonana!" Mwanaume huyo alimpokea mgeni wake kwa kumkumbatia, hapa kwa karibu ndo' akaonekana vema, alikuwa ni Taiwan, mwanamke alipoingia ndani ya gari akavua wigi lake na kunyofoa sura bandia alokuwa amebandika, hapo akawa mtu mpya kabisa! Usingeweza sema ni mwanamke yule tuliyemwona kule New York, walikuwa watu wawili tofauti, wa kule ni mwanamke mgeni machoni petu ila huyu wa sasa ni mwanamke tunayemfahamu, mwanamke tuliyemwona si mara moja ama mbili, alikuwa ni Mitchelle!
Aliuliza,
"Kila kitu kipo sawa?"
Taiwan akamjibu, "sawa sawia."
Mitchelle akasema,
"Nataka kuwaona Truce na Kiellin. Tunyookee huko saa hii."
Taiwan akakaa kimya.
"Umenisikia?" Mitchelle akauliza.
***