Tukibaki Hai, Tutasimulia

Tukibaki Hai, Tutasimulia

Habari zenu wapendwa? Samahani kwa kuwa kimya kwa kitambo kidogo, sasa narejea na kama nilivyoapa, story hii nitaimalizia hapahapa.

Kuanzia kesho nitarejea kwenye ratiba yangu ya awali.
Karibu tena Steve
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - BONUS


Na Steve B.S.M





Usiku haukuwa umeisha, ndo' kwanza ilikuwa saa nne ya dakika za mapema. Richie alitoka kuoga akiwa anajifutafuta na taulo, amevalia nguo ya ndani rangi ya machungwa, miguu yake myembamba ipo wazi ikipuyanga na vinyweleo.

Alipomaliza kujifuta alitupia taulo kitandani kisha akaenendea mafuta ya ngozi, alichovya kidole lakini kabla hajajipakaa simu ikaita. Hakujua simu ipo wapi, alisahau alipoiweka, akarusha macho yake hapa na pale bahati akaiona, ilikuwa kwenye kona ya kitanda, shida nguo zilikuwa zimetanda sana kana kwamba kitanda kimechapwa na bomu, akainyaka simu hiyo na kuitazama, alah! Alikuwa ni Jamal, akastaajabu ni nini muda huu?

"Hello!" Akasema akiketi kitandani, "... Saa hii? ... Serious? ..." Simu ikakata, akatahamaki kwa sekunde, upesi akajivika suruali na shati, nguo zote hizo aliziokota kwenye kile kifurushi kilichokuwepo kitandani kwake, sijui kama nguo hizi zilikuwa safi au lah, alishuka chini upesi na alipofika nje ya ghorofa hili analokaa aliangaza na kidogo tu akamwona Jamal, mwanaume huyo alikuwa amesimama akiegemea moja ya gari, kwa namna alivyoegema hapo unaweza kudhani huo usafiri ni wake, alipomwona Richie anamjia akasimama.

"Ni nini hiko muda huu?" Aliuliza Richie, Jamal kabla hajaongea akatazama kwanza pembeni yake kana kwamba mtu anayehofia usalama wake kisha akasema,

"Richie, najua hili litakuwa 'too much' kwako lakini naomba unisaidie, tafadhali."

Wakati huo wa mazungumzo yakiwa yanaendelea, kuna mtu fulani alikuwa akiwatazama ndani ya gari.

Mtu huyo alitazama vinywa vya watu hawa na kwa kuutumia mkono wake wa kushoto akawa ananakili jambo kwenye 'notebook' yake, alilifanya zoezi hilo kwa sekunde kadhaa kisha akaifunga notebook na kuiweka kwenye 'dashboard'.

Muda mchache ulofuatia, kama dakika zisizozidi tatu, Jamal akamwona mtu fulani akiwa anaingia ndani ya jengo hili la ghorofa, mtu huyo alikuwa mrefu amevalia 'hood' nyeusi iliyofunika kichwa chake, mikono yake ameizamisha kwenye hood hiyo, mwendo wake wa kasi ya wastani, kichwa amekiinamishia chini.

Jamal hakumjali sana bwana huyo kwani hapa wanaishi watu wengi sana, ni ghorofa yenye 'floors' nyingi na vyumba vingi pia, akamchukulia kama mkazi tu wa eneo hili, akapuuza na kuendelea na maongezi yao kama kawaida, baada ya dakika mbili maongezi yakasimama kwa Richie kusema,

"Ningoje hapa, simu yangu niliiacha ndani."

Bwana huyo akatoka zake kuelekea ndani, alikwea ngazi upesiupesi, akashika korido na kuimaliza haraka, kidogo tu huyu hapa mlangoni mwake, chumba namba 43, akachomoa ufunguo mfukoni mwake na kuuchomeka kwenye kitasa, mara mlango ukafunguka wenyewe! Akahamaki, ina maana sikuufunga mlango kwa funguo? Alisema na nafsi yake, akausukuma mlango na kuingia ndani, akatazamatazama, akajiaminisha kila kitu kipo shwari, akaelekea chumbani kwake kuichukua simu iliyomleta huku.

Aliufungua mlango akayatupia macho yake kitandani, akaiona simu, lakini nyuma ya mlango kulikuwapo na mtu amesimama hapo na yeye hakuwa anafahamu jambo, akaichukua simu yake na kuiweka mfukoni, kugeuka, kabla hajaondoka hapa, akashuku kitu mlangoni.

Aliutazama mlango kwa sekunde tano, kuna kivuli kilikuwapo hapo, kivuli kisichoeleweka, moyo ukaguta, haraka akili yake ikamkumbusha yale ya mlango kuwa wazi, hofu ikamvaa, alihisi mwili mwake umepitwa na baridi fulani jepesi ambalo halieleweki, akaupiga moyo konde, mimi ni mwanaume, alisema na nafsi yake, akausogelea mlango taratibu, alipoufikia, katika kiza cha kivuli kile, akaona kiatu cha mtu, buti kubwa jeusi, moyo ukaita pah!


....


Jamal alitazama saa yake ya mkononi, muda ulikuwa umeenda, toka Richie amemuaga kwenda kuchukua simu sasa yapata nusu saa, akajiuliza bwana huyo anafanya nini muda wote huo? Alingoja kidogo, mwishowe akakata shauri kwenda kumwona.

Aliingia ndani akashika ngazi, alizikwea haraka akiziruka mbilimbili, muda si mrefu akawa ameishika korido ya kumpeleka kwa Richie, alipopiga hatua nne akamwona bwana yule aliyevalia hood nyeusi, bwana huyo alikuwa anamjia, uso wake, kama kawaida, ulikuwa unatazama chini, mikono yake ipo ndani ya nguo yake hiyo.

Jamal alimzingatia bwana huyu lakini hakuambulia kitu, hakumwona uso wala hakujua ngozi yake, alichoambulia ni harufu tu wakati akipishana naye, alimsindikiza kwa macho mpaka alipokata kona na kutokomea zake.

Alipofika kwenye mlango wa makazi ya Richie akagonga, kimya, akagonga tena lakini mara hii mlango ukafunguka wenyewe, akashangaa, akausukuma mlango huo na kuingia ndani, akaangaza, hamna kitu, akaita lakini napo kimya, akarudia kuita mara tatu, bado kimya, akaanza kuingiwa na hofu, kutazama mlango wa chumbani upo wazi, taratibu akaujongea na kuusukuma, lah! Akamwona Richie akiwa amelala chini!

"Richie!" Aliita lakini bwana huyo hakuonyesha dalili ya uhai, alikuwa ametulia tuli kana kwamba maiti ndani ya jeneza, upesi akamsogelea na kumtikisa, akampima mapigo yake ya moyo kwa masikio, akabaini bwana huyo alikuwa hai ila ni ufahamu amepoteza, basi upesi akatoa simu yake mfukoni na kupiga 911 kwaajili ya kuomba msaada wa dharura.


......


"Hallo!" Redio ndogo ilitamka ndani ya gari, "kuna mtu amezirai hapa, na mapigo yake ya moyo yako chini sana!" Redio iliendelea kutamka, na bwana aliyevalia hood alikuwa akiskiza kila jambo, ametulia kwenye kiti cha dereva alichokilaza chini kiasi.

Maongezi yaliendelea kidogo katika redio kisha kukawa kimya, baada ya dakika chache sana sauti ya king'ora ikaita kwa mbali, sauti hiyo ikawa inaongezeka kadiri na muda unavyozidi kwenda, kidogo tu eneo hili likaanza kuwakawaka kwa rangi nyekundu na bluu, mara 'ambulance' hii hapa, watu wawili wakashuka upesi na kwenda ndani ya ghorofa hili.

Wakati haya yanatokea, bwana yule mwenye hood alikuwa anatazama kila kitu. Muda si mrefu wale watu waliongia ndani wakatoka na mwili katika 'machela' yao, nyuma wakifuatwa na Jamal. Ilipofikia hapo, bwana huyu ndani ya hood akawasha gari yake na kuondoka zake, akiwa anaenda, Jamal akalikodolea gari hilo ambalo lilikatiza kwa ukaribu kwa kasi yake ya wastani lakini hakuambulia kitu, gari lilikuwa na vioo vyeusi ti, alichobaini ni gari hilo halikuwa na namba zozote za usajili.


***


Uwanja wa Kimataifa wa New York, saa tano asubuhi.


Taksi yenye rangi nyeupe iliingia katika eneo la uwanja wa ndeges ehemu mahususi kwaajili ya kupakulia wateja. Taksi hiyo ilisimama akashuka mwanamke fulani aliyevalia mithili ya walimbwende, nywele zake ni ndefu na ni nyeupe pe, miwani yake ya jua iliziba karibia robo ya uso wake, 'lips' zake zilikuwa zinang'aa na zimelowana, hakika alivutia.

Mwanamke huyu ambaye mwonekano wake ni mpya kabisa machoni petu alikuwa na mwendo mithili ya twiga mwenye kufuata maji ya mtoni, alitembea pasipo papara, kila hatua akiihesabu, kila alipokatiza kati ya watu alionekana wa tofauti kwa namna alivyonawiri, na yeye ni kama vile alilitambua hilo, akaringa.

Mkoba wake wa thamani uliokuwapo begani ulitetemeka, akaufungua na kutoa simu yake, akaitazama kwa kusimama, akatazama nyuma na pembeni yake kisha akapokea simu hiyo,

"Naam," alisema kisha akaendelea na mwendo, mwendo wa madaha kama kawaida, alizungumza na simu hiyo kwa hatua kama tano hivi kisha akasimama, akauliza,

"Umetuma saa ngapi?"

"Tazama kwenye barua pepe yako, utaona," sauti ilimjibu upande wa pili kisha simu ikakata, kabla hajapiga hatua nyingine akafungua 'inbox' ya barua pepe yake, huko akakutana na 'links' mbili za mtandao, akapiga simu.

"Nimeona," alisema kisha akakata simu yake na kuirejesha kwenye mkoba alafu akaendelea na safari yake, baada ya mlolongo mfupi wa abiria akawa sehemu ya ukaguzi, hapo alikuwapo mwanamke mmoja wa makamo ya miaka arobaini, amevalia miwani ambayo ameishusha chini ya pua, macho yake ni kuyarembua lakini kayakaza kuwatazama abiria, ukimtazama vibaya waweza sema anatazama kwa madharau.

Aliipokea 'passport' ya mwanamke huyu kisha akaikagua kwa macho yake, alipomaliza akamtazama mwanamke huyu na kumwamrisha avue miwani yake, mwanamke akatii, akaivua na kumtazama, alikuwa na macho ya kijani, sawa sawia na picha ilokuwepo kwenye 'passport' yake, basi mkaguzi alipojiridhisha akamruhusu aende zake, mwanamke huyo akatabasamu akirudishia miwani yake usoni kisha akasema,

"Tchao!"

Akaenda zake kwa mwendo wake wa madaha, mkononi mwake alikuwa amebebelea tiketi ya ndege kubwa ya Uchina, ndege zao la Boeing yenye uwezo wa kubeba abiria lukuki, humo alijikalia katika kiti cha dirishani na safari ikaanza si muda, ndege ilipong'oa nanga kuidaka anga mwanamke huyu alishusha pumzi ndefu, hatimaye aliiacha ardhi ya Marekani.

Baada ya masaa na masaa ya kudumu angani, hatimaye ndege hii kubwa ilitua salama ndani ya Taiwan katika uwanja wa kimataifa wa Taoyuan, kutokana na utofauti wa ukanda wa muda ulokuwepo baina ya pande hizi mbili, yaani New York na Taipei, Taiwan, ndege hii ilifika katika muda salama kabisa, jua linaangaza vya kutosha, mwanamke huyu akapokelewa na mwanaume aliyekuwa anamngoja muda wote huo, mwanaume huyo alikuwa ameegamia gari kubwa nyeusi, modeli ya Alphard, alipomwona mwanamke huyu alimtambua upesi akampungia mkono, mwanamke akamjia.

"Muda mrefu hatujaonana!" Mwanaume huyo alimpokea mgeni wake kwa kumkumbatia, hapa kwa karibu ndo' akaonekana vema, alikuwa ni Taiwan, mwanamke alipoingia ndani ya gari akavua wigi lake na kunyofoa sura bandia alokuwa amebandika, hapo akawa mtu mpya kabisa! Usingeweza sema ni mwanamke yule tuliyemwona kule New York, walikuwa watu wawili tofauti, wa kule ni mwanamke mgeni machoni petu ila huyu wa sasa ni mwanamke tunayemfahamu, mwanamke tuliyemwona si mara moja ama mbili, alikuwa ni Mitchelle!

Aliuliza,

"Kila kitu kipo sawa?"

Taiwan akamjibu, "sawa sawia."

Mitchelle akasema,

"Nataka kuwaona Truce na Kiellin. Tunyookee huko saa hii."

Taiwan akakaa kimya.

"Umenisikia?" Mitchelle akauliza.


***
Tawan hatoamini macho yake
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 31


Na Steve B.S.M





SUV nyeusi iliposimama, mwanaume aliyevalia suti na tai nyeusi alishuka upesi akafuata mlango wa nyuma na kuufungua, akatoka bwana mkubwa. Kidogo mlango mwingine ukafunguka akatoka mwanaume maridadi ndani ya suti, alikuwa ni Babyface, na yule bwana mkubwa aliyefunguliwa hapo mwanzo alikuwa ni mkubwa wake wa kazi, mkubwa ambaye huwa anakuwa naye mara kwa mara, bwana huyo kwa sifa ni mtulivu na asiyeongea maneno mengi, pengine hekima za uzee zilimzidia, hutanguliza akili kuliko mdomo, hamna anayejua.

Bwana Babyface pamoja na bwana huyo waliingia ndani ya jengo ambalo kwa nje walipokelewa na maafisa wengine wa usalama, kwa haraka kama watano hivi, walikuwa wako 'alerted, wanatazama huku na kule kutazama na kuhakikisha usalama wa jengo hili, na hawakuwa wenyewe, kwa mbali pia walikuwapo wengine ambao ukiwatazama tu kwa jicho la umakini utabaini ni wana usalama, wanarandaranda huku na kule.

Babyface alipanda lifti ya jengo hili pamoja na mkuu wake, walikuwa wawili tu ndani ya lifti na huu ukawa wasaa wao mzuri wa kuzungumza baadhi ya mambo.

"Nategemea kila kitu kitaenda sawa," Mkuu akasema akivutavuta koti lake kwa kulitengenezea, "Kama jambo hili likikoma, basi nitastaafu kwa heshima, nikilishindwa itabaki kuwa fedheha maishani mwangu."

Aliposema hayo akamtazama Babyface na kumuuliza,

"Unadhani nitafanikiwa?"

Babyface hakujibu kwa kinywa, badala yake akainamisha kichwa chini, Mkuu akashusha pumzi ndefu na mara mlango wa lifti ukafunguka, wakatoka, wakaongozana mpaka kwenye chumba maalum, chumba kikubwa cha kufanyia mkutano, humo wakakuta kuna watu wawili waliovalia kombati za kiofisa wa jeshi, muda si mrefu baada ya kufika hapa, chumba hicho kikajawa na watu kadha wa kadha wenye wadhifu mkubwa katika mambo ya usalama, watu hao walikuwa wamekaa kuizingira meza kubwa lakini kiti cha mkubwa wa kikao hiki bado kilikuwa wazi.

Kidogo king'ora kikalia, gari lilimleta mtu, ndani ya muda mfupi mtu huyo akawa amefika, alikuwa ndo' mkubwa wa kikao hiki, waziri wa ulinzi wa taifa hili, bwana Logan Diff, mwanaume mrefu shupavu, nywele zake mchanganyiko wa rangi nyeupe na nyeusi, mwili wake mkakamavu na umenyooka kimazoezi, hatua zake ni kamilifu akitembea kuonyesha amepitia mafunzo ya jeshi, kisigino ndo' kinaanza kugusa chini kisha mguu mzima, amevalia shati la bluu bahari, amelikunja mikono yake.

Bwana huyo alipoingia katika ukumbi huu, wote wakasimama, ni mpaka alipoketi yeye ndipo na wengine wakaketi kisha kikao kikaanza, muhtasari wa kikao ulitajwa na mada iliyowakutanisha hapo.

Bwana Logan Diff alikabidhiwa faili lenye nyaraka za siri, faili lenye jalada la jeusi huku likiwa na chapa nyekundu ya neno CONFIDENTIAL, akalipitia faili hilo kwa umakini, uso mkavu, kwa dakika mbili, kisha akaliweka faili hilo pembeni na kumtazama bwana yule aliyekuja akiongozana na Babyface, kwenye meza yake kulikuwa na kijibao kilichoandikwa jina lake, na ilikuwa hivyo kwa kila mtu aliyeketi hapa, mbele yake kilisimama kibao kinachomtambulisha jina kamili, kwa mkuu wa kazi wa Babyface kibao chake kilisoma Brendan Garret, afisa mwandamizi wa taasisi ya CIA.

"Garret," Logan aliita kisha taratibu akaanza kuaeleza mambo yahusuyo oparesheni ambayo ilipatiwa jina la oparesheni BALTIKA.

"Bwana Garret, kwa sahihi yako mwenyewe mnamo mwaka 2005, ulihitaji serikali iidhinishe mkakati wako wa kuwatengeneza binadamu bora zaidi kwaajili ya mapambano ya nje ya nchi, kwa maelezo uliyoyatoa, watu hao watatumika kama mbadala wa taifa letu kupoteza wanajeshi lukuki katika uwanja wa mapambano, mkakati kabambe kabisa, serikali ikaidhinisha na kuupitisha mkakati huo baada ya mapitio, mabilioni ya dola yakatolewa kwaajili ya kuufadhili, lakini baada ya vita tano kubwa, huko Iraq, Afghanistan, Syria, Sudan na Somalia mkakati wako ukashindwa kuonyesha matunda baada ya watu wako kubadilika, haukuweza kuwamudu tena kama hapo mwanzo, ikabidi wateketezwe, sio?"

Garret akatikisa kichwa kukubali maelezo hayo yote, Waziri Logan akaendelea kutoa taarifa kwa kutumia kumbukumbu ya kichwa chake,

"Jambo hili ni la siri, Garret, lazima kila kitu kisafishwe huku chini, laiti nisingefanya hisani ya kiubinadamu basi unajua mambo yangekuwa magumu zaidi lakini shida ni kwamba unanifanya niwe katika wakati mgumu, wa kujutia hisani yangu ...."

Alipofikia hapo akaweka kituo kikubwa, akanyanyua glasi ya maji iliyokuwapo pembeni yake na kunywa mafundo mawili makubwa kutibu koo lake kavu, alipofanya hivyo akaendeleza maneno yake kwa utaratibu kabla ya kwenda kwenye hukumu,

"Katika vita ya mwisho, kwa maelezo ambayo taasisi yako iliyatoa, Bwana Garret, hao watu waliuawawa wote, hakuna aliyebaki, chanzo kikiwa milipuko mikubwa ya mabomu, lakini ...."

Akavuta faili jingine na kutazama, faili hilo lilikuwa limetokea upande wa kitengo cha Polisi, akafungua moja kwa moja ukurasa nambari sitini na mbili, hapo kulikuwa na picha kadhaa pamoja pia na maelezo, hakuyasoma, yalishakuwa kichwani, alishajua kilichopo hapo, akalisogeza faili hilo kwa Garret kisha akaendeleza maneno Garret akiwa anatazama faili alilosogezewa karibu,

"Sidhani kama maelezo yako yalikuwa sawa, Garret, kwa mujibu wa picha hiyo katika faili za polisi, mwanamke huyo yuko hai na yuko mtaani, nadhani unamfahamu sivyo?"

"Ndio."

Logan akaongezea, "huyo ni 00/89/31/12 CKM. Imekuaje bado yuko hai?"

"Tulibaini hili jambo si muda mrefu," Garret aliteta, "tulistaajabu yupo mtaani na ..."

"Na akawa tayari ameshaua!" Logan akamkatisha. "Si ndivyo?"

Garret hakujibu, alinyamaza akitazama meza.

"Alafu mnaleta hapa maelezo ambayo hayajitoshelezi kabisa, Garret, unafahamu wazi kuwa watu hawa ni hatari, kama mlishindwa kuwamudu, raia wa kawaida huko mitaani wataweza? Haya maafa tutambebesha nani lawama? Nani anayejua kitakachofuatia baada ya hiki? Na nani anayejua kama kuna wengine zaidi ya mwanamke huyu huko mtaani?"

Logan alifungua faili jingine toka polisi, akalipitia kwa ufupi kisha akampatia bwana Garret kwa kulitupia mezani, faili hilo lilijawa na picha nyingi sana, picha za mauaji kadha wa kadha, picha ya maiti ya Ronelle, Travis, pamoja pia na picha ya ajali mbaya iliyommaliza Mpelelezi huko San Fransisco, hapo Logan Diff akasema,

"Mpelelezi huyo alikuwa anafuatilia mauaji yaliyotokea The DL, mauaji aliyoyafanya 00/89/31/12 CKM. Huyo mwanamke Ronelle alikuwa katika orodha yake ya upelelezi, akaishia kufa, huyo Travis kwa mujibu wa maelezo yake ya mwisho ya simu, aliongea na Mpelelezi, bila shaka ni kuhusu kesi hiyo ya The DL, naye akafa, na mwisho wa siku Mpelelezi mwenyewe akapata ajali, hit and run, una lolote la kutuambia kuhusu haya? Huu ni mkakati wenu wa kuzuia taarifa zenu kwenda kwa umma? Kwahiyo watu wenu wanaua na nyie pia mnaua?"

Garret aliipotaka kufungua mdomo wake kujitetea Logan alibamiza meza kwanguvu kumkatiza kisha akamkodolea macho ya ukali na kusema, "ulifanya kazi kubwa sana, Garret, hamna asiyefahamu hilo katika nchi hii, lakini kwa hili, unaenda kufuta 'legacy' yako yote uliyoijenga kwa damu na jasho!"

Baada ya kitambo kidogo ya kikao kumalizika, Bwana Garret alikuwa kwenye gari lake akiwa amezama ndani ya fikra, kichwa chake alikiegamiza kwenye dirisha macho yake yakitazama nje, pembeni yake Babyface aliketi akimtazama, alifahamu muda ule haukuwa sahihi kumwongelesha mkuu wake wa kazi ijapokuwa alitamani sana, basi akaishia kujihifadhi kifuani.

Gari lilienda kwa mwendo wa kilomita chache, liliposimama kupisha taa nyekundu ya barabarani, bwana Garret akaongea akiwa bado amelaza kichwa chake kwenye dirisha,

"Unafahamu chochote kuhusu mauaji ya wale watu?"

Garret aliuliza akilenga vifo vya Travis, Ronelle pamoja na Mpelelezi, kuna jambo alikuwa analipambanua kichwani mwake, jambo ambalo bado lilikuwa na kiza kinene, kabla Babyface hajajibu swali hilo akanyanyuka upesi na kumtazama kwa kuyakaza macho, akaongezea swali,

"Ulishiriki kwenye hayo mauaji?"

Babyface akajikuta anayakodoa macho yake kwa mshangao, hakutarajia swali hilo ghafla kiasi hiko.


***


Metropolitan Hospital, New York, asubuhi ya saa nne.


"Unaweza kumwona hivi sasa, amesharuhusiwa," mhudumu aliposema hivyo Hilda akashika zake njia lakini kabla hajafika popote akamwona Richie akiwa anakuja, mwanaume huyo alikuwa amekunja sura yake kana kwamba ametoka kulamba ndimu kali, mwendo wake pia ulikuwa wa taratibu akijikongoja, basi Hilda akamfuata na kumshika mkono ili apate kumsaidia, Richie akamshukuru kwa kuja kumjulia hali, wakaongozana mpaka nje ya hospitali ambapo walisimamisha taksi kwaajili ya safari, walipokwea na kuondoka, Hilda alimtazama Richie kwa macho ya huruma akauliza,

"Richie, kwani nini kilitokea?"

Kabla Richie hajajibu, Hilda akaongeza, "Jamal alinipigia simu amekukuta umezidiwa, nini kilikukumba, Richie? Mbona imekuwa ghafla hivyo?"

Richie akatikisa kichwa, akahisi maumivu makali, haraka akatuliza kichwa chake akisonya mithili ya mtu anayeita paka, alafu akasema,

"Nikikwambia sijui unaweza kuniamini?"

"Hujui nini?"

"Sijui kilichotokea."

"Hujui kilichotokea?"

"Sikumbuki kitu chochote kile, nastaajabu sana, naweza kukumbuka vitu vya juzi ama juma lililopita lakini sikumbuki kitu chochote kuhusu jana usiku, kitu pekee ninachokumbuka ni kukutana na Jamal."

"Serious?"

"Serious, nakwambia kweli, lakini nahisi maumivu ya kichwa kweli, kadiri niongeavyo nahisi kuyatibua."

Baada ya hapo Hilda akajiepusha kumuuliza maswali bwana huyu kwa kuhofia kumsababishia maumivu, walipofika nyumbani wakamkuta Jamal akiwa hapo anawangoja, wakasaidizana kumpeleka Richie chumbani kwake kwaajili ya mapumziko kisha wakasogea kando kwaajili ya mazungumzo mafupi.

"Anasema hakumbuki kitu?"

"Ndio, nimemuuliza anasema hamna anachokumbuka, lakini wewe ulikuwa naye hapa jana, uliona nini?"

"Alikuwa vizuri kabisa, nilifanya naye mazungumzo kabla hajaniaga kwenda kuichukua simu yake, ajabu nilipomfuata baada ya kuona anakawia ndo' nikamkuta amelala chini, hana fahamu!"

"Hakuona dalili yoyote?"

"Hapana ... lakini kuna mtu fulani nilimwona, hisia zangu zinapata kumshuku sana kuwa si mtu mwema, huenda akawa alimfanyia kitu Richie."

"Nani huyo?"

"Simjui, alivalia nguo za kujificha hata gari lake halikuwa na namba za usajili!"

"Atakuwa anataka nini kwa Richie? Kuna kipi cha kumfanya awindwe na mtu?"

"Sijajua ... lakini nilikuja hapa kumwona Richie sababu ya matatizo yangu binafsi, kwasababu yupo katika hali ya kutokumbuka si mbaya nikakushirikisha wewe, pengine unaweza kunisaidia."

"Nini hiko?"

Jamal akaleza kinachomsibu, wakati huo wakiwa hawana hili wala lile, palikuwa na mtu aliyekuwa anawatazama kwa umakini akiwa ndani ya gari, mtu huyo alikuwa ameshikilia kalamu mkono wake wa kushoto na alikuwa anaandika kila alichokitambua kwa kupitia kusoma 'lips' za wahusika. Bwana huyu alikuwapo hapa kwa muda, na hakuwa mwingine bali yuleyule aliyekuwapo hapa jana yake na kumvamia Richie.


***
Duh! Huku watu wanatafutana, kumbe kuna watu wanajua nini kinaendelea![emoji3166][emoji2962][emoji15]
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA -- 32



Na Steve, B.S.M







Taipei, Taiwan, majira ya saa kumi na mbili jioni.


Mitchelle alifuta chozi jicho lake la kushoto akishuhudia jeneza linashuka ardhini, alishindwa kuvumilia, alijikuta anahisi uchungu mkali katika moyo wake punde alipoona mwili unashushwa, aliweza kuhimili muda wote huo lakini si hapa.

Mwanamke huyo alikuwa amevalia gauni jeusi, kofia nyeusi yenye nyavu nyepesi zilizofunika robo ya uso wake, 'gloves' ndefu nyeusi mikononi na viatu vyeusi vyenye visigino virefu, nyuma yake walikuwapo wanaume wawili, wote walivalia suti nyeusi na miwani meusi, mmoja alikuwa ni bwana Taiwan na mwingine ni Yu, nywele zao wamezitengeneza vema, zinang'aa na zimelala kana kwamba zimelambwa na mbwa, wamevalia nyuso za mawe wakiwa wamesimama kama wanasesere, mbali na watu hao alikuwapo bwana mmoja aliyekuwa anahusika na shughuli za mazishi, bwana huyo alikuwa mzee mwenye asili ya Uchina, makamo yake miaka ya hamsini za mwisho ama sitini za mwanzo, alikuwa amevalia shati jeusi yenye chapa ndogo nyeupe mfukoni mwake ikisomeka FAREWELL FUNERAL SERVICES.

Baada ya mazishi kukoma, Taiwan pamoja na mwenzake, Yu, walitoka eneo hilo wakalifuata gari lililowaleta hapa, gari kubwa aina ya Alphard rangi yake nyeusi, gari hilo lilikuwa jipya likiwakawaka, hapo wakajiegamiza wakiwa wanamtazama Mitchelle kwa mbali.

Taiwan alivua miwani yake kubwa uso wake ukabaki uchi, jicho lake la kushoto lilikuwa limevilia damu na ana ngeu mbichi pembeni yake, alijisogeza kidogo apate kuegama vizuri lakini akajikuta anaugulia maumivu makali kiasi cha kubweka kama mbwa, nyonga ilimvuta akaushika mguu kama mtoto mdogo.

"Hak'ya Mungu!" Akaapia akiukunja uso, "Haya maumivu utayalipia, Mitchelle!"

Bwana Yu alimtazama kwa macho ya huruma akimshika bega kumpa pole, mbaya napo alipomshika alikuwa na maumivu pia, akabweka tena.

"Samahani, sikujua. Sasa wapi hapaumi?"

"Kila sehemu panauma."

"Ni kheri unahema, nilihofia unaweza kupoteza uhai wako kwa hasira za mwanamke yule."

"Hata mimi pia nilihofu na hilo, sikutegemea kama ningeliona jua la leo, shukrani ziende kwa yule daktari, pesa nilizomhonga zimeokoa nafsi yangu, laiti angelijua mtoto alikwishafariki muda mwingi ulopita nikawa nakula pesa yake basi leo hii ungekuwa kwenye mazishi yangu."

Alisimama akijikaza, akaupindisha mdomo wake na kusema, "lakini namsikitikia, kuniacha hai ni kosa ambalo atakuja kulijutia siku za usoni," alafu akatabasamu mwenyewe. Bado walikuwa wamesimama wakimtazama Mitchelle kwa mbali, mwanamke huyo alikuwa amesimama kaburini kwa utulivu.

"Kesho ni siku ya kutajirika, kesho ni siku ya neema juu ya neema!" Taiwan alisema kisha akaendelea kutabasamu, kwa muda kidogo aliyasahau maumivu yake pale alipowaza pesa, pesa nono atakazozipata si muda mrefu, hata mate yalimjaa mdomoni.

"Unadhani tutafanikiwa?" Yu akauliza, papohapo Taiwan akamtazama kwa macho ya hasira, akamwambia, "Kama huniamini unaweza ukajitoa hivi sasa, bado muda unao."

Yu akanyamaza, mwenzake akaendelea kumtazama kwa macho ya maulizo, ikambidi aongee, "sawa, nimekuelewa!" Taiwan akaurejesha mgongo wake kwenye gari kisha akamwambia, "Kila kitu kipo tayari, hata asubuhi ya leo nimetoka kuwasiliana na wale jamaa nao wako tayari, sasa wewe jukumu lako ni moja tu, kazi yako ni moja na nyepesi ..."

"Ipi hiyo?" Yu akauliza kwa hamu, Taiwan akamshika mkono, "tulia, haina haraka."

Baada ya kuhiji vyakutosha, Mitchelle aliungana na wakina Taiwan tayari kwaajili ya kuondoka. Yu alishika usukani, nyuma ya gari wakiketi Taiwan na Mitchelle, gari ilikuwa kimya sana kiasi kwamba ungeisikia namna AC inavyopuliza, hakuna aliyemwongelesha mwenzake, Mitchelle alikuwa yu mbali kimawazo ingali hawa wengine walikuwa wanaigiza kana kwamba hamna mtu hapa karibu, walitazama mbele kwa nyuso za malaika asokuwa na kosa.

Baada ya muda mfupi, wakawa wamefikia kwenye nyumba fulani iliyojitenga, ukubwa wake ghorofa mbili, imepakana na bahari kwa ukaribu sana, mwonekano wake ni maridadi sana, humo gari likazama chini mpaka eneo maalum la kujiegesha, hapo wakashuka na kuendea mlango wakaingia kisha wakaelekea upande wa kushoto, huko kulikuwapo na mlango uliofanania na wa lifti, pembeni yake palikuwapo na kifaa chenye tarakimu kadhaa.

Mitchelle alibonyeza baadhi ya tarakimu na mara mlango ukafunguka, wakazama ndani. Walinyooka na korido wakapishana na milango miwili, mlango wa tatu ndo' wakaingia, humo palikuwa mithili ya maabara ama hospitali ndogo, walikutana na bwana mmoja aliyevalia koti jeupe, mzee aliyekula chumvi, kichwa chake cheupe na kibaraza chake kinang'aa.

Alimsalimia Mitchelle kwa adabu kubwa alafu akampatia muhtasari wa leo wa afya ya mhusika wake.

"Maendeleo ni mazuri, hali yake si haba, leo hii mapigo yake ya moyo yametengemaa."

Waliongozana na Mitchelle kufuata pazia kubwa la kijani, wakalisogeza na kutazamana na mwili uliolala kitandani. Mwili huo ulikuwa umejazwa mabomba sehemu kadha wa kadha, ulifunikwa sehemu za siri huku kwengine kukiwa wazi, kichwa cha mwili huu kilikuwa cheupe pe, mabega yake mapana, kifua chake kipana, uso wake unafanania na wa Mitchelle lakini umekomaa kiume kwa kushupaza fuvu za mashavu.

Mwili huo ulikuwa umetulia tuli, kama isingekuwa kupanuka na kusinyaa kwa kifua kwasababu ya kuhema basi tungedhani amekwishakufa, mashine ya kunakili mienendo ya mapigo ya moyo ilikuwa inaita kwa milio yake, kwasababu ya ukimya wa hapa mashine hiyo ikawa inasikika vema.

Mitchelle aliutazama mwili ule kwa macho ya kujali, akaushika kwa mikono yake mpaka pale aliporidhika, akajikuta anadondosha chozi, hakukaa hapo muda mrefu akaongozana na daktari kwenda nje ya kijichumba hiki, wakapata kuteta baadhi ya mambo.

"Zile kazi zote ulizon'tumia nimezipata, taratibu naziingiza kwenye mfumo wa bwana huyu, nadhani zitakapokamilika ataweza kunyanyuka kitandani na kuwa mtu kamili ... Hata kama sio kamili lakini atakuwa sasa binadamu mbele ya macho ya watu," daktari alijipambanua, Mitchelle akatikisa kichwa kumwitikia kisha akamuuliza, "mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia ngapi kukamilika?"

"Asilimia arobaini," daktari akajibu na kuongeza, "nadhani unafahamu, huyu mwanao ni hybrid, mfumo wake wa mwili si sawa na wewe, pia si sawa na mimi, yu katikati, namna mwili wake unavyojijenga ni taratibu sana lakini punde utakapokomaa basi yawezekana ukawa bora zaidi kuliko mimi na wewe."

"Na kwanini ni wa baridi sana?" Mitchelle akauliza, "nimemshika nikahisi baridi la ajabu. Huwa anakuwa hivyo?"

"Ndio," Daktari akajibu, "mwili wake ni wa baridi, lakini leo alikuwa wa baridi zaidi sababu alitoka kwenye jokofu si muda mrefu, nilibaini kufanya hivyo humsaidia kwenye 'recovery' ya upesi ya misuli na tishu zake za mwili."

"Kuna chochote unahitaji, Dr. Gates?" Mitchelle alisimama akauliza, hapa Dokta akatabasamu kwa mbali kisha akasema, "Ninachohitaji zaidi ni nyaraka toka kwenye chanzo, zile nyaraka hunisaidia zaidi kufanya kazi yangu, kama isingalikuwa kukawia kwa nyaraka hizo basi ningeweza kuokoa hata uhai wa Kiellin. Hayo mengine nashukuru maana natimiziwa ndani ya wakati."

Mitchelle akamuahidi Dr. Gates kwamba mradi wake utakapokamilika kama vile alivyopanga basi atamlipa kiasi kikubwa sana cha pesa kiasi kwamba hata akiacha kazi hatokuwa masikini kamwe, yeye mpaka uzao wake wa tatu, dokta akashukuru sana kisha wakaagana.

Mitchelle alienda sehemu ya kupumzika, hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano, huko akajiandikisha kwa kutumia kitambulisho bandia, kitambulisho kilekile akitumiacho sehemu zingine, akajipatia chumba kikubwa chenye kila kitu anachokihitaji mtu mwenye pesa zake, hapo akatulia tuli, aliona hapa ni patulivu zaidi ya kule kwenye jengo lake kubwa, alitaka kuwa mwenyewe apate kuyapanga mambo yake kwa ufasaha, mambo ya pesa kubwa.

Akiwa ametulia katika kitanda kikubwa chenye hadhi iliyojitosheleza, mara simu yake ikaita, kutazama ni namba tupu pasipo na jina, alipoikagua namba hiyo vema akaigundua ni ya nani, akaipokea akisema, "Fenty."

Mtu wa upande wa pili akampokea kwa kumpatia taarifa,

"Hakuna taarifa ya siri tena."

"Unamaanisha nini?" Mitchelle akauliza upesi, bwana yule kwenye simu akamwambia aingie kwenye 'inbox' ya email yake, ataelewa anachomwambia, upesi Mitchelle akaingia kwenye inbox yake na huko akakutana na 'links' mbili alizozibofya zikampeleka moja kwa moja kwenye 'audio' fulani ya kuskiliza, audio hiyo ikampa sauti ya yale yaliyokuwa yanaendelea ndani ya makazi ya Hilda, Richie pamoja na Jamal, lakini hakuskiza sana, aliyaacha mambo haya ili apate kufanya kusudi lililomleta hapa, atakapolimaliza hilo, basi yatafuatia mengine.

Akiwa anayafanya hayo, akaona ni vema aendelee kujiburudisha na kahawa aipendayo, muda huu hakutaka kubaki nyuma, alimwambia Jennifer amwandalie kahawa hiyo ili aendelee kuinywa atakapokuwapo safarini.

Alijimiminia unga wa kahawa kwenye kikombe kisha akajichanganyia na maji moto na sukari kwa mbali, akanywa fundo moja, akahisi mwili mwake umetetemeka kwa raha, hakika alihisi unafuu mkubwa, hamu tamu isiyoelezeka, sasa akaamini yuko tayari kwa kazi.


*****


Taipei, Taiwan, majira ya asubuhi ya saa mbili, masaa kumi na mbili kabla ya mnada mkubwa kufanyika.


Bwana Yu alikuwa pembezoni mwa jiji la Taipei akiwa ameegamia gari dogo jeusi kandokando ya barabara ndogo, hapo alikuwa anangoja jambo.

Bwana huyo alikuwa amevalia jeans nyembamba na buti kubwa la ngozi, usoni amevalia miwani kubwa ya jua mdomoni akitafuna 'bubblegum', mikono ameeka mfukoni akitazama huku na kule barabarani.

Kidogo akaliona gari fulani likiwa linakuja kwa mbali, rangi yake ya maziwa, modeli yake ni van, linakuja kwa kasi kufuata uelekeo wake, si punde gari hilo likasimama kwa upande wa pili, Bwana Yu akavuka barabara kulifuata gari hilo, Yu akazama ndani humo akawakuta watu watatu walioketi.

Watu hao walikuwa wamevalia nguo nyeusi, wote wamebana nywele zao nyuma, na kama ukiwatazama kwa harakaharaka utawaona wamefanana nyuso, tofauti zilikuwa za mbali sana kama vile sharubu changa ama upana na wembamba wa nyuso.

Baada ya Yu kuingia ndani ya gari hilo, mlango ukafungwa na mazungumzo yakaanza, hayakuwa marefu, la hasha, yalikuwa ni namna gani ya kuwezesha utekaji wa gari litakalobeba mzigo wa thamani ya mabilioni kabla ya kufika katika uwanja wa mnada, kazi ya Bwana Yu ikawa ni kusema ruti zote zitakazotumika kupitishia gari hilo, na baada ya kusema sasa kazi ikaachwa kwa genge hilo nao kusema juu ya mipango yao, kazi ilipokwisha, ndani ya dakika sita tu za maongezi, Bwana Yu akashuka toka kwenye gari akiwa na kila kitu kichwani kwake.

Alipofika kwenye gari akampigia simu Taiwan na kumweleza yaliyojiri, kisha akamalizia kwa kusema,

"Nadhani kazi yangu imeshakwisha."

"Hapana, Yu," Taiwan akamkatiza, "kazi yako itaisha usiku wa leo hii, uwe tajiri ama uwe maiti."


***
Hahaha uwe tajiri ama uwe maiti[emoji1782][emoji1787][emoji1787][emoji1787]
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA -- 33



Na Steve B.S.M






New York Police Department, New York, Saa mbili asubuhi.




Bwana alifungua mlango akaingia ndani ya ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, akasalimu na kuketi, mkononi mwake alikuwa amebebelea faili moja aliloliweka mezani na kusema,

"Nimefanikiwa kupata mwanya mdogo."

Bwana huyo alikuwa ndo' yule aliyepewa kazi ya kufuatilia mauaji ya Travis, bwana aliyeuawa muda mfupi baada ya kuwasiliana na Mpelelezi kisha gari lake likaandikwa kwa maandishi ya damu, jina lake Michael Summer, ilikuwa rahisi kumtambua sababu alibebelea kijibao kidogo kinachomtambulisha jina kifuani mwake.

"Nini umepata?" Mkuu aliuliza akijaribu kulifungua faili aliloletewa mezani, bwana Michael akamwambia,

"Usajili wa gari ile iliyombeba muuaji ni ya kampuni moja ya usafi inayoitwa RICKY & PAT CLEANING', nilifuatilia katika kampuni hiyo kuhusu gari lao wakaniambia hawana taarifa, gari hilo ni miongoni mwa magari yao chakavu ambayo huifadhiwa kabla ya muda wa kwenda kuharibiwa moja kwa moja."

Mkuu aliendelea kutazama faili, bwana Michael akaweka kituo kifupi katika maelezo yake akimtazama, zikapita kama sekunde sita hivi za ukimya. Mkuu akasafisha koo lake, kuna picha aliiona katika faili hilo, picha ya mwanaume aliyekuwa ndani ya gari, mwanaume mwenye asili ya bara la Ashia, akauliza,

"Na huyu ni nani?"

Bwana Michael akamwambia ni mkurugenzi wa kampuni hiyo, kwa jina anaitwa Ricky Wang, nimejaribu kuonana naye lakini sijabahatika, nimeambiwa amesafiri kwenda kwao, pengine ningeonana naye ningepata taarifa zaidi maana walisema baadhi ya taarifa ni 'confidential' kwa mkurugenzi."

"Kingine?" Mkuu akauliza akiwa anaendelea kutazama faili.

"Kingine ni kuhusu bwana huyo, Ricky Wang," bwana Michael akajibu, "nimetazama usahili wake kwenye 'database', ana nyaraka zote rasmi za kufanya kazi nchini hapa lakini si raia wa Marekani, kama ni hivyo natilia mashaka umiliki wa kampuni yake labda tu kama kuna Mmarekani ambaye yupo naye ubia."

"Naye ni nani?" Mkuu akauliza, macho yake ameyabandua toka kwenye faili.

"Sijamjua, na hilo ni moja ya kitu ambacho ningetaka kumuuliza bwana huyo lakini hayupo, pengine ingeweza kutoa 'lead' fulani."

"Sawa, kuna la ziada?" Mkuu akauliza.

"Nadhani nitalipata n'takapofanikiwa kumpata mlinzi wa zamu, yeye anaweza kutusaidia kujua gari hilo lilitokaje katika yadi kwenda kutekeleza mauaji."

"Gari hilo limeonekana tena?"

"Halikurudi tena yadi lakini ukifungua huko mbele," akasimama kuonyeshea ndani ya faili, "gari hilo limenaswa na kamera za barabarani likiwa linaelekea Pennsylvania."

Mkuu akatazama picha hiyo kwa umakini, gari hilo lilionekana kwa mbali kiasi cha kutoweza kupata taarifa nyingi, akafunga faili na kulirejesha kwa bwana Michael.

"Kazi nzuri, Michael. Fuatilia gari hilo kwa kuwasiliana na mamlaka ya Pennsylvania, utanijuza kila utakachopata."

Michael akanyanyuka na kwenda zake.


****


Taiwan, masaa manne kabla ya Mnada mkubwa kufanyika.



Mitchelle alitazama nguo yake iliyokuwa inametameta ikiwa inaning'inia kwenye enga. Nguo hiyo ilimvutia machoni na aliamini atakapoiweka mwilini basi kila mtu atapata kuona uzuri wake, gauni lilikuwa maridadi sana, mtindo wake wa kipekee na namna litakavyokuwa linahakisi taa zile zinazomulika mnadani vinaweza kukupatia picha kichwani juu ya namna mambo yatakavyofana.

Alishatengeneza nywele zake vema, na vitu kama vile usafiri, mavazi na mzigo unaotakiwa kwenda kuuzwa mnadani ulikuwapo kitandani, upo tayari kabisa, upo ndani ya 'safe' ya chuma yenye kufunguliwa kwa tarakimu za siri, tarakimu anazozifahamu Mitchelle pekee.

Kila kitu kilikuwa vema, naam, lakini si kwamba kila kitu kilikuwa kimekamilika, la hasha, Mitchelle alitazama saa mkononi mwake, ilikuwa ni saa moja kamili ya usiku, muda muafaka, aliponyanyua tu kichwa chake akasikia kengele ya mlangoni, akajikuta anatabasamu kwa mbali, akaelekea mlangoni huko akakutana na bwana mmoja akiwa amebebelea mkoba, bwana huyo alikuwa amevalia kofia nyeusi na ni kana kwamba alilenga kutojulikana kwani alikuwa anatazama chini.

"Kila kitu kipo humo!" Akasema akikabidhi mkoba, Mitchelle akaufungua mkoba kuhakiki, akaona kila kitu kipo vema, basi akamkabidhi bwana huyo begi alilopokea na kufungua kutazama, alipoona kila kitu kipo sawa alishukuru kwa kutikisa kichwa kisha akaenda zake, hakuteta mengi, alijipakia katika pikipiki kubwa alokuja nayo akatia moto, hapo nje akakutana na gari linalotaka kuingia, gari hilo lilikuwa limewabebelea Bwana Taiwan pamoja na Yu, watu hao waliangalia pikipiki hiyo ikipita na kuishia zake wasimtambue hata aliyekuwa anaendesha maana alivalia helmet nyeusi yenye kioo cheusi.

"Ni nani huyu?" Taiwan akauliza, lakini hakuna aliyekuwa anajua kati yao, waliishia kumtazama bwana huyo akienda mwishowe wakaendelea na yaliyowaleta hapa, kuonana na Mitchelle.

Waliingia ndani moja kwa moja wakaketi sebuleni, kidogo tu Mitchelle akatoka akiwa ameng'aa ndani ya gauni lake maridadi, gauni lililofunika kifua na mikono yake huku likiacha mgongo ukiwa wazi kwa kiasi fulani, chini amevalia viatu vyenye visigino virefu, viatu ambavyo ukimtazama unaweza kujiuliza anatembeaje, mkononi amebebelea mkoba, mkoba wenye mali ya pesa ndefu ikiwa ndani ya 'safe' ya chuma.

"Hello, boys!" Alisalimu kisha akatabasamu, Taiwan na mwenzake wakastaajabu kwa uzuri wa mwanamke huyo, hakika alipendeza na alivutia kuendelea kumtazama, wakampa sifa zake.

"Ahsanteni sana, leo ni siku muhimu kwetu, na tuifanye ikawe hivyo!"

Wakatoka kulifuata gari, wakakwea na safari ya kuelekea mnadani ikaanza, ilikuwa ni mapema lakini ndo' utaratibu wenyewe haswa kwa wale ambao walitakiwa kukabidhi mizigo kwaajili ya mauzo, mizigo hiyo ilibidi ifike mapema ili kutoathiri ratiba ya mnada ukizingatia mahudhurio yalikuwa ni ya watu wazito, si vema kuwapotezea muda wao.

Mitchelle aliketi nyuma ya gari pamoja na Taiwan kulia kwake, katikati yao kuna mzigo wa thamani, huku Yu akiushikilia usukani kuelekeza chombo, kila kitu kilikuwa vema, gari lilienda katika mwendo wa usalama na kwa makadirio ya mwendo huo basi ingewapata lisaa limoja kuwasili wanapoelekea.

Baada ya muda mchache wa kuwa barabarani, kama dakika kumi na tano kupita, gari likakwama kwenye foleni, ilikuwa ni foleni kubwa iliyotembea mita kadhaa, magari yamesimama hamna linalosogea wala kujigusa, Taiwan akang'aka,

"Hili foleni limetokea wapi tena?"

"Huwa kuna foleni majira haya?" Mitchelle akauliza.

"Hapana," Taiwan akamjibu, "nashangaa hili limetokea wapi!"

"Pengine kuna ajali mbele," Yu akachangia akigeuza shingo yake kuwatazama walioketi nyuma, "na kama ni kweli basi tutakaa muda mrefu sana hapa."

Taiwan akashusha kioo na kuchungulia mbele, kidogo akaufungua mlango akatoka ndani kwenda kutazama, alitembea hatua kadhaa mbele kisha akarejea na kusema foleni ni kubwa na ameambiwa sasa yapata robo saa foleni hilo halijasogea hata inchi moja, kuna ajali mbaya imetokea hapo mbele ikihusisha magari makubwa, hapo Yu akashauri,

"Vipi tukitumia njia mbadala? Hamna anayejua hapa tutakaa kwa muda gani, huenda tukachelewa."

Mitchelle akaunga mkono hoja, hakutaka kupoteza muda wake hapo, upesi gari likachekechwa kutoka hapo kwenye foleni alafu likageuza kurudi lilipotokea, mwendo wa kama dakika tatu gari likashika njia ndogo kuelekea mashariki mwa jiji, barabara hiyo ilikuwa ni 'one-way' na ilikuwa nyeupe kiasi cha kuruhusu mwendo wa kujiachia, wakatembea huko mpaka mahala fulani walipokuta njia panda, wakakata kushoto, kidogo uso kwa uso na gari kubwa linalobeba taka, gari hilo lilikuwa limejiegesha katika namna ambayo gari lingine lisingeweza kukatiza, lilimeza barabara nzima likikaa kiubapa.

RICKY & PAT CLEANING Co.

Lilisomeka mbavuni, maneno makubwa meupe yanayoonekana vema.

"Shit!" Yu akabamiza usukani, akageuza shingo kutazama nyuma akaona ni kweupe, akaweka 'reverse' gari likaanza rudi nyuma, halijafika popote likatokea gari jingine na kuliweka gari hili kati, gari hilo lilikuwa kubwa jeusi lenye ngao kubwa ya chuma, tairi zake ni nene na ndefu kama trekta, lipo hewani sana wakilitazama gari la wakina Mitchelle kwa chini.

Milango ikafunguka wakashuka watu watano, watu hao walikuwa wamevalia kombati na kapelo nyeusi, kisha nyuso zao zikafunikwa na 'mask' zinazoziba kidevu, mashavu mpaka pua yakabakia macho tu, macho yenyewe hayakuonekana vema sababu ya kushushwa kwa kofia mpaka chini, watu hao walikuwa wamebebelea bunduki nzito nzito zilizoshikiliwa na mikono yote miwili miwili, wakanyooshea bunduki hizo kwenye gari alilomo Mitchelle kisha wakaamuru kila mmoja atoke ndani upesi!

"Ukifanya janja yoyote huu ndo' utakuwa mwisho wa maisha yenu, hatupo hapa kuleta matani!" Mmoja alifoka, Yu akatoka kwenye gari akiwa ameweka mikono yake kichwani, kidogo naye Taiwan akatoka akiwa ameiweka mikono yake juu, nyuso zao zinatweta kwa hofu, naye Mitchelle akatoka akiwa amefanya hivyohivyo, mikono yake iko juu.

"Mzigo uko wapi?" Mmoja akafoka, kabla hajajibiwa akalisogelea gari na kutazama, akauona mzigo kwenye kochi, akaunyaka na kumtupia mwenzake wa nyuma kwaajili ya kuukagua, yeye akanyoosha mdomo wa bunduki kwa mateka wao, yule bwana aliyetupiwa mzigo akaufungua upesi na kukutana na 'safe' ya chuma, hakuweza kuifungua, akapayuka,

"Nahitaji passcode!"

Basi bwana yule aliyekaribu na Mitchelle alimtazama mwanamke huyo akamwonyeshea mdomo wa bunduki usoni na kumwambia,

"Sema passcode upesi."

Mitchelle akamuuliza,

"Aliyekutuma anajua mimi ni nani?"

"Sema Passcode!" Bwana akafoka, saa hii akasogea karibu zaidi na mhusika wake, bunduki yake tayari ameshaikoki kwaajili ya shambulizi, Mitchelle akamtazama Taiwan, macho yake yalikuwa makali yakibanwa na ndita. Aliurejesha uso wake kwa mvamizi aliyemwonyeshea bunduki alafu akamtajia Passcode, yule mwenye mzigo akaweka passcode hizo na mara kukawa kimya, 'safe' haikufunguka.

"Nahesabu mpaka tatu, toa passcode!" Bwana yule akafoka tena, sauti yake haikuwa na utani na kidole chake kilikuwa kinakaribia kufyatua 'trigger' ya bunduki, Mitchelle akarudia tena passcode, ikaingizwa lakini 'safe' haikufunguka, bwana aliyemnyooshea bunduki akampa nafasi ya mwisho,

"Taja passcode!"

Saa hii aliuweka mdomo wa bunduki kwenye paji la uso la mwanamke huyo, na macho yake yakagongana ana kwa ana na macho ya Mitchelle, Mitchelle akarudia tena passcode, ilikuwa ni ileile alosema mwanzo, akasema,

"Weka tena!"

Passcode ikawekwa, mara hii 'safe' ikafunguka, lakini walichokutana nacho hakikuwa kile walichotaraji, halikuwa jiwe la thamani kama walivyodhani, la hasha, ilikuwa ni bomu ambalo muda wake umebakia sekunde mbili tu lipate kulipuka, swala la kufumba na kufumbua, bomu likaparachuka kwa mlipuko mkali!

Mabwana wanne walisambaratika hovyohovyo, vipande vya mwili vilishindana kuacha mwili, sehemu yote ikatapakaa damu.

Bwana yule aliyekuwa anamnyooshea bunduki Mitchelle alikuwa chini akiugulia maumivu, kichwa chake kilikuwa kinavuja damu, kofia yake ilirukia pembeni kichwa chake kikaachwa mavumbini, alijaribu kunyanyuka lakini hakuweza, kwa mbali alimwona mtu anamjia, hakumtambua vema, macho yake yalikuwa na ukungu, mtu huyo alipomsogelea karibu ndipo akamjua kuwa ni Mitchelle, akajitahidi haraka kuisogelea bunduki yake lakini hakufanikiwa, alipigwa risasi mbili akatulia hapohapo chini akigugumia maumivu.

"Nilikuuliza, aliyekutuma ananijua mimi ni nani?" Mitchelle alisema akisogea kwa madaha, "maana laiti angelinijua basi asingelituma watu watano, angelituma jeshi zima."

Baada ya kusema hayo alkfumua kichwa cha bwana huyo kwa risasi alafu akapokea simu yake iliyokuwa inaita kwenye mkoba,

"Mzigo ushafika tayari," sauti ya kiume ilisema, aliyekuwa anaongea upande wa pili alikuwa ni yule bwana aliyeondoka na pikipiki majira yale akipishana na wakina Taiwan mlangoni, alimalizia, "na mnada utaanza si punde, wahi." Kisha simu ikakata.

Mitchelle akaruka maiti zilizokuwapo hapo chini, akawafuata Taiwan na Yu, walikuwa wamelala wakijishika panapouma, akawamalizia risasi zake zote kisha akashika njia kwenda zake mnadani.

Alitembea kwa madaha kana kwamba ametoka tafrija.



****
Duh!
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA -- 35


Na Steve B.S.M




Mitchelle aliirejesha simu yake kwenye mkoba lakini bado hakujua afanye nini, alipatwa na butwaa lililomshika miguu akasimama hapo alipo kana kwamba sanamu, akiwaza na kuwazua, mambo kama mia moja katika kichwa chake yakienda na kurudi, yakijiuliza na kujipatia majibu yenyewe, kwa mara ya kwanza alijikuta katika hali ya kutoelewa chochote kinachoendelea, ubaya hakuwa na muda wa kujadili zaidi na nafsi yake, akakata shauri kurudi ndani, alipoingia tu mlangoni akakutana na wanaume wawili waliovalia nguo za wahudumu, mikononi wamebebelea bunduki, nyuso zao ngumu kama roho zao, wakamchukua na kuongozana naye mpaka ukumbini ambapo mnada ulikuwa unafanyikia, huko akakuta watu wote ukumbi mzima wamewekwa chini ya ulinzi mkali, wale waliokuwa wahudumu ndo' hao wamebebelea bunduki badala ya trey za vinywaji.

Mbele ya ukumbi alikuwapo bwana yule mnene, kipande cha mtu, mikono yake iko mifukoni, pembeni yake wamesimama wanaume wawili waliobebelea bunduki nzito, mwanaume huyo alikuwa anamtazama Mitchelle akiwa ameupinda mdomo wake mdogo, Mitchelle aliposogezwa karibu naye aligunia puani kwa kebehi alafu akasema, "Ndio wewe!" Kisha akacheka.

"Leo ni siku ya namna gani!" Akasema, "Leo ni siku ambayo nchi ya Taiwan haitakuja kusahau kamwe!"

Akamsogelea Mitchelle kwa mwendo wa taratibu, Mitchelle akamtazama kwa macho ya hasira alafu akamuuliza, " wako wapi watu wangu?"

Bwana huyu mnene akacheka, akacheka tena, akacheka mpaka kifua chake kikamuuma akipaliwa na mate, alipotulia akauliza huku akiwa na macho yanayolengwalengwa na machozi ya furaha, "watu wako? Watu gani?" Akaigiza kama mtu anayefikiri alafu akasema, "watu wako? Oh! Unamaanisha Dr. Lambert na Jennifer?" Akatabasamu, "hao ndo' watu wako?" Akauliza kwa kebehi, punde wakatokea Jennifer na Dr. Lambert wakitokea nyuma ya jukwaa, walikuwa wamevalia nadhifu, Jennifer alikuwa yu ndani ya suti ya kahawia wakati Lambert akiwa amevalia suti nyeusi isiyokuwa na tai, watu hao walisimama kando ya bwana huyu mnene wakamtazama Mitchelle kama mtu mgeni mbele ya macho yao.

"Jennifer!" Mitchelle aliita, na pasipo Jennifer kusema jambo Mitchelle akawa ametambua ya kwamba mwanamke huyo hakuwa upande wake, vilevile Dr. Lambert, lakini kwanini? Hakuwa anajua chochote, kila kitu kilikuwa 'surprise' hapa, Jennifer akampungia mkono akitabasamu akajikuta anapatwa na hasira za ajabu, hasira za usaliti, akataka kujifaragua lakini bwana Lambert akamsihi asifanye hivyo kwani atajiumiza mwenyewe, hapa Mitchelle akatabasamu alafu akasema,

"Dokta, umenisahau? Unadhani hawa wanaweza kunizuia mimi?"

"Najua hawawezi," Dokta akajibu na kuongezea, "ndo' maana mimi nipo hapa." Akatoa kifaa fulani mfukoni mwake na kusema, "huu ndo' mwisho wako, Mitchelle, ni muda wa kulipia dhambi zote ulizozifanya."

Dokta akaenda mbele kwa kumweleza ni namna gani alikuwa anapandikiza vitu vyake katika 'antidote' alokuwa anampatia, na kama haitoshi namna gani walivyokula njama pamoja na Jennifer kwenye kumpandikizia vitu vya ziada katika kahawa yake.

"Vitu vyote ulivyokuwa unatumia na kukusababishia uraibu vilikuwa ni zao la mikono yangu, hiyo ndo' ilikuwa kazi yangu, na kwasababu ulikuwa ni kiumbe kisichokuwa na madhaifu, ilikuwa ni jukumu langu kukutengenezea udhaifu tutakaoweza kuutumia kwenye kukupata na kukumudu."

Mitchelle alijaribu kufurukuta, Dr. Lambert akabonyeza kifaa chake, mara moja akajihisi shoti ya umeme mwili mzima! Kufumba na kufumba alijikuta chini akiwa hajiwezi, hana nguvu kabisa, anahema kama mbwa wa mashindano, hakuwahi kujihisi mdhaifu kiasi hiko maisha yake yote.

"Haikuwa kazi rahisi kufanya hili," Dokta akasema akimkaribia, "na nilijua kwa mwenendo wa kukupatia dawa ingalichukua muda mrefu sana kukamilisha mpango wangu, hapo ndo' kukajenga hitaji la kahawa tamu, kahawa ambayo najua bila shaka umeinywa hata asubuhi ya leo, kwa pamoja vimeleta mafanikio haya."

Dokta alitazama kifaa alichokishikilia mkononi mwake alafu akasema, "huwezi kuishi bila antidote, mwili wako umeshakuwa 'addicted', hautavuka juma moja, vilevile hautaweza kuishi siku zaidi ya tatu bila ya kupata kahawa yako tamu, utapoteza nguvu na kutokomea, mbaya ni kwamba vitu hivi vipo kwenye mikono ya adui yako, sasa yapasa kuwa mtiifu."

Dokta alimkabidhi bwana yule mnene kifaa hicho alafu akamwambia kwa sauti ya chini kuwa kifaa hicho hufanya kazi ndani ya mita kadhaa karibu na mlengwa wao, hivyo muda wote kiwapo karibu kwaajili ya kuongeza ufanisi wake, baada ya maelezo hayo yeye pamoja na Jennifer wakaondoka zao wakimwacha Mitchelle akiwa chini hajiwezi, pamoja naye wapo wanaume lukuki walioshikilia bunduki nzito nzito, kidogo tu bwana yule mnene akabofya kifaa alichopewa na dokta, Mitchelle akatetemeka mpaka kupoteza fahamu zake!

Alipotelea kwenye kiza kinene kisicho na ukomo.


***


Taipei, Taiwan, majira ya saa nne asubuhi ...


Bwana mmoja aliingia ndani ya sebule nzuri, alikuwa amevalia suti nyeusi, nywele zake maridadi amezilazia nyuma, mwendo wake wa ukakamavu, akatazama na kumwona Dr. Lambert pamoja na Jennifer, watu hao walikuwa wamekaa kwa utulivu katika makochi makubwa malaini, mbele zao kuna vistuli vidogo vya kioo, vistuli hivyo vilikuwa vimebebelea glasi zenye vinywaji.

Bwana huyo aliyeingia akasema, "yupo tayari." Basi Dr. Lambert na Jennifer wakasimama na kuongozana na bwana huyo kidogo wakaingia ndani ya ofisi walimokutana na bwana mmoja aliyeketi akiwapa mgongo, pembezoni ya bwana huyo alikuwapo mwanaume yule mnene, mtu wa miraba, amesimama kama sanamu akitazama kwa macho yaliyofungwa na ndita kana kwamba ametoka kugombana na mtu.

Bwana yule alowaleta wakina Jennifer ofisini hapa akanena kwa lugha yake anayoijua kisha akaondoka zake kutoa faragha, bosi mkubwa alokuwa amekaa kitini akajigeuza na kukutana uso kwa uso na wageni wake, mara moja Dr. Lambert akatabasamu, sijui nini kilimfurahisha.

Bosi huyo alikuwa mwingi wa mashavu na uso mweupe pe usokuwa na tone hata moja la ndevu, kidevu chake kidogo kimechongoka, macho yake ni madogo, asili ya Ashia, lakini makali yakikutazama, alitabasamu kidogo alipowatazama wageni wake alafu akasema,

"Kazi yenu imekuwa njema sana!" Kisha akavuta droo ya meza yake, humo akatazama na kutoa macho yake upesi, mkono wake wa kushoto ukatoa bahasha ndogo ya kaki, bahasha hiyo ilikuwa imejaa almanusura kupasuka, akamkabidhi Dr. Lambert,

"Mimi ni mtu wa kupenda cash, samahani kama n'takuwa nimekukwaza," alisema akijiegemeza kwenye kiti chake, naye Dr. Lambert akatazama ndani ya bahasha hiyo, kulikuwa na fedha kedekede, akashindwa kujizuia kutabasamu, akamtazama Jennifer alafu akamtikisia kichwa.

"Huo ni mwanzo kama tulivyokubaliana," akasema bosi mkubwa, "lakini kadiri mtakavyokuwa na manufaa kwangu ndivyo n'takavyozidi kutoa, nadhani mnajua mimi na nyie biashara yetu haijakoma."

"Ndio," Dr. Lambert akaitikia kwa furaha na hawakukaa tena hapo kwa muda, bwana aliyewaleta akaja kuwachukua tayari kwaajili ya kuwapeleka hotelini kwa mapumziko. Bosi mkubwa aliwatazama wakiwa wanaenda zao, amesimama kando ya dirisha kubwa la kioo lililopo katika ofisi yake, mikono yake imo mifukoni, gari lilipopotea mbele ya macho yake akageuka kumtazama bwana yule wa miraba minne, akamwambia,

"Siku ya leo haitakuja kusahaulika milele katika ardhi ya Taiwan. Siku halisi ya ukombozi."

Bwana yule wa miraba hakusema jambo, alikuwa anatazama tu akisimama pasipo kupepesuka, ni kana kwamba alikuwa amesimikwa hapo na programu maalumu, bosi akaendelea kusema,

"Kaka yangu huko alipo atakuwa na furaha isiyokuwa na kifani, hatimaye haki yake imefuata mkondo na hakika atafurahi zaidi haja yetu itakapokamilika!"

Akasimama akiutazama ukuta kana kwamba kuna kitu anakiona, kitu kinachomfurahisha, akatikisa kichwa chake kisha akaketi kwa kujibwaga kwenye kiti.

"Na vipi kuhusu wale mabwana?" Kwa mara ya kwanza bwana yule wa miraba minne akazungumza, bado alikuwa amesimama akitazama mbele huku akiwa ametulia tuli, bosi mkubwa akafyonza meno yake chonge akiwa anatazama kwa uyakinifu, alikuwa anapanga jambo kichwani mwake, baada ya sekunde chache akasema,

"Nina mpango nao. Ngoja tuone mambo yatakavyowiwa."

"Mpango huo ni pamoja na kuwamaliza?" Bwana wa miraba minne akawahi kuuliza, alikuwa anafurahia sana hilo jambo, pengine alikuwa anapenda kuua watu kuliko hata kula, bosi mkubwa akamtazama pasipo kumjibu, naye akakaa kimya kana kwamba hakuna kilichotokea.


***


Taiwan, majira ya saa sita usiku...



"Bado hataki kula," bwana alisema akisimama, mbele yake alikuwapo mwenzake aliyeketi kwenye kiti kisichokuwa na meza, wote wamevalia kombati jeusi 'plain'.

"Kile chakula cha asubuhi kipo mpaka saa hii, hajagusa kabisa."

Bwana aliyeketi akatikisa kichwa chake akisonya, akasema,

"Jana hajala pia, sijui anataka kufa?"

Alisimama akanyoosha mgongo wake, mgongo ukalia kah-kah, akalalama kwa uchovu, kidogo akapiga mhayo akijiendea.

"Ngoja nikamtazame, kama hataki kula basi mimi nile chakula chake, nishachoka kumbembeleza." Kidogo akasimama, akageuka na kumtazama mwenzake kwa sura ya kubung'aa, akasema,

"Hiviii!" Akamsogelea mwenzake karibu, "kweli mkuu amelenga kumuua huyu?"

"Kwanini unauliza?" Mwenzake akahamaki.

"Kama wamelenga kumuua kwanini wanahangaika kumhudumia kiasi hiki?"

Wakatazamana kama matapeli wanaopanga 'kumpiga' mtu kisha kidogo bwana huyo akaendelea akisema,

"Anapewa chakula kizuri kuliko sisi. Bado mkuu amesema kuna daktari atakuja kumtazama na kumfanyia vipimo. Wewe unaona kawaida? Au wewe unaonaje?"

"Sitaki matatizo," mwenzake akamkatiza, "niliyonayo yananitosha, bwana, we nenda kamtazame alafu urudishe viungo vyako vya siri hapa. Acha kiherehere."

Bwana akamsonya alafu akaenda zake kumtazama mlengwa, kiunoni amening'iniza kadi inayotumika kufungulia milango, akaambaambaa na korido na si muda akawa mbele ya mlango mzito wa chuma ambao ilikuwa na dirisha la kioo, kioo kigumu, hapo akachungulia kwa ndani, akamwona mwanamke amesimama akiwa amempatia mgongo, anatazama ukutani, kutazama pembeni akaona sahani ya chakula na chakula chake kikamilifu, hakikuguswa hata tone, akaita,

"Wewe! Weweee!"

Mwanamke yule hakugeuka, akamuuliza,

"Kwanini hauli?"

Hakujibu wala hakumtazama, akasema,

"Wewe usile, unataka kufa kama yule mama enh?"

Mwanamke yule kusikia hivyo akageuka, alikuwa ni Mitchelle, nywele zake zilikuwa hovyo na sura yake imefura, akatazama mlangoni na kuuliza, "mwanamke gani?"

Yule bwana akatabasamu, hatimaye alipata 'attention' ya mtu wake, akajivuna kwa raha kabla hajajibu, "si yule Jennifer!"

"Jennifer?" Mitchelle akauliza akisogelea mlango.

"Ndio, kwani hawajakupa taarifa amefariki jana usiku?" Bwana akahamaki.

"Nini kimemuua?" Mitchelle akauliza.

"Sijui. Ninachofahamu ni kuwa amekufa. Hayo mengine sijui ... haya utakula ama utanipa hiko chakula?"



***
Ohooo! Duh!
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 36



Ingawa Jennifer alimsaliti, akimuuza kwa watesi wake kama alivyofanya Yuda kwa Yesu, lakini bado alisikia kitu ndani yake, hakikuwa kingine bali hisia ya uchungu, akasogelea kwa ukaribu zaidi kuta hii iliyomtenganisha yeye na mlinzi, macho yake yanametameta lakini ndita amezikunja, akauliza,

"Alikuwa na nani?"

"Nani?" Mlinzi akauliza, macho yake yalikuwa yapo juu ya ile sahani ya chakula alokuwa anaitamani, hata akili yake ilikuwapo huko, masikio yakafa ganzi.

"Jennifer!" Mitchelle akarudia kwa sauti ya mkazo. "Mara yake ya mwisho alikuwa na nani?"

Mlinzi akamtazama.

"Sasa mimi najuaje? Nipo na wewe hapa kutwa nzima, najuaje ya huko duniani?"

"Mbona umefahamu kuwa amekufa?"

"Nimesikia wenzangu wanaongea, wale majamaa walokuja hapa asubuhi. Amekutwa amekufa ndani ya chumba chake cha hoteli, mlango unaotazamana na chumba cha daktari."

Mitchelle aliendea sahani ya chakula akaitwaa na kurejea nayo alipokuwa amesimama, akamwonyeshea mlinzi akisema,

"Nipo tayari kukupatia, sio tu leo hata siku zote n'takazokuwamo humu, ninachotaka ni taarifa tu toka kwako."

Mlinzi akamtazama kwa macho ya mashaka kisha akaitazama sahani ile ilokuwamo mkononi mwa mfungwa wake, akauliza,

"Nitakuaminije?"

"Una rimoti, si ndio?" Mitchelle akamuuliza na kuongezea swali juu yake, "nitafanya nini ukiwa na rimoti hiyo? Unajua kabisa kuwa ukibonyeza kitufe hiko basi sitakuwa na tija tena."

Mlinzi akajipapasa mfukoni, kweli hakuwa na kitu chochote isipokuwa 'mafunguo' na kadi, rimoti haikuwa pamoja naye lakini hakutaka kuukubali unyonge huo, akasema kwa kujiamini,

"Ukileta janja janja yoyote nitabonyeza kitufe hiko kwa nusu saa nzima, nadhani utakuwa ushakauka kwa umauti!"

Mitchelle akatikisa kichwa, mlinzi akatazama kando na mbali yake, hakika alikuwa mwenyewe, alipohakikisha hilo akamgeukia tena Mitchelle na kumuuliza,

"Unataka taarifa gani?"

Mitchelle akamwambia kile anakihitaji, bwana mlinzi akamsikiliza kwa umakini, alipomaliza akampatia chakula kwa kupitia kidirisha kidogo kilichokuwapo langoni, mlinzi akakitwaa na kumuahidi atamrejea baadae.

Akaenda zake.


****


Alipoweka sigara yake kubwa chini, boss mkubwa alimtazama mwenziwe aliyekuwa ameketi katika meza hii, sigara yake akaisiginia kwenye kisosi kisha akatemea moshi pembeni, moshi mzito, alafu akasema, "Tuna miezi miwili tu, kila kitu inabidi kiwe kimeshakamilika, unajua kuna mkutano mkubwa wa UN mbele yetu na huo ndo' 'target' yetu kubwa."

Kando ya bwana huyo alokuwa anaongea naye walikuwapo wanaume wengine wawili, wote walikuwa wamevalia suti nyeusi, macho yao yanatazama kiti kikubwa kilichokaliwa na boss mkubwa, nyuso zao zina umakini kana kwamba waliambiwa kinachoongelewa hapa basi kinajiri kwenye mtihani hapo baadae, mbali na hao wanaume alikuwapo mwingine alosimama, bwana yule wa miraba minne, alikuwa amesimama kwa utulivu, hatikisiki wala kuyumba, kidevu amekinyanyua juu, mikono ameikutanisha kwenye kiuno chake.

"... Kabla ya mkutano huo inabidi tuwe tumeshageuza adui yetu kuwa silaha yetu kubwa. Kila mtu hapa anajua ni namna gani mwanamke yule ana uwezo wa ajabu, tunakumbuka vema namna gani alivyofanikiwa kutokomeza kabisa jeshi letu kabla hatujaja kusimama upya, namna gani tulivyopoteza wanaume mamia kwa mamia kwenye mikono yake, laiti akiwa mikononi mwetu basi hatutazuilika na mtu yeyote!"

"Lakini ..." Bwana mmoja akasema kwa shaka, "tutafanikiwa vipi katika hilo? Tutamwamini vipi mtu yule hata sasa kiasi cha kumtwika majukumu yetu nyeti?"

Boss mkubwa akagunia puani alafu akaegemea kiti chake kikubwa, macho yake yakamtazama mwanaume mwingine kwa namna ya kumpa ruhusa, naye mwanaume huyo akaongea akisema kuwa Mitchelle si binadamu wa kawaida, mbali na kwamba nje ana umbo la binadamu na hata matendo pia lakini ana mfumo kamili unaomwendesha, mfumo unaojitegemea, endapo watakapoweza kuumudu mfumo huo basi wataweza kumtumia kama mtumwa wao kama vile alivyotumika kuwaangamiza hapo kabla.

"Hatujajua ni nini kilitokea hapo nyuma lakini huenda mwanamke huyo aliharibu mfumo wake wa kiuendeshaji hivyo akaanza kujitegemea, kwa mujibu wa Dr. Lambert, tunaweza kumtengenezea upya mfumo wa kummudu japo ni zoezi kubwa lakini linawezekana."

"Na hilo ndo' linafanya daktari yule anaendelea kuwa hai hata sasa," akasema boss mkubwa, "yeye alishiriki katika kumtengeneza mwanamke huyu, japo si kwenye zoezi zima lakini angalau anajua wapi pa kuanzia na nani wa kuanza naye kulikamilisha hili."

"Tutaweza kweli kuuwahi mkutano huo ndani ya miezi miwili?" Bwana yule akauliza, boss akamtazama na kumwambia hiyo ndo' sababu ya yeye kuwaita hapo, kuharikisha mpango huo kadiri itakavyowezekana.

"Mtaongozana na Dr. Lambert kwenda US, huko mtafanya naye kila kitu kws ukaribu, kwa hap tulopofikia hatuwezi kumwamini yeye tu asilimia zote, nataka muwe naye karibu mno. Yeye atawaelekeza chakufanya, wapi pa kwenda na nani wa kumwona, pesa zitakazokuwa zinatumwa zitawafikia ninyi kabla ya mikono yake, na ninyi ndo' mtakaonipa taarifa ya kila jambo."

Baada ya kusema hayo, alitoa angalizo,

"Kuweni makini na yule bwana, nadhani mnajua kilichotokea juzi yake?"

Mabwana wakatikisa vichwa vyao kuonyesha wameelewa, boss mkubwa akasimama kuondoka zake.



Hiyo Juzi yake, majira ya saa za usiku, Kianjin Hotel, Taiwan. Majira ya usiku mzito.


Baada ya mhudumu kukatiza, mlango ukafunguka na kichwa cha Dr. Lambert kikachomoza nje, akatazama korido ndefu ya hoteli, pande zote mbili, hakukuwa na mtu isipokuwa mhudumu aliyekuwa anaishilia, akatoka ndani ya chumba chake na kuufuata mlango uliokuwa unatazamana naye, alikuwa amevalia nguo maalum wanayovaa watu watokapo kuoga, nguo yenye 'material' ya taulo ikiwa imebanwa na kamba kiunoni, akabisha hodi kwa kubonyeza kitufe cha kengele na muda si mrefu mlango ukafunguliwa na mwanamke aliyevalia taulo kifuani, ana tabasamu usoni mwake, si mwingine bali Jennifer, Dokta akaingia ndani na mlango ukafungwa upesi.

"Aah! Hata sasa bado hujalala?" Alisema Dr. Lambert akijimwaga kwenye kiti kama mzigo uliomzidia kuli, Jennifer akatabasamu kisha naye akaketi pembeni yake.

"Usiku huu ni mwanana sana," Dokta akasema akiupeleka mkono wake kiunoni mwa Jennifer, Jennifer akashtuka kidogo kisha akatabasamu na kuupokea mkono huo kwa mkono wake wa kushoto, dokta akaendelea akisema namna gani usiku huo ulivyokuwa bora, mosi wamepata fedha nyingi sana na pili wapo pamoja baada ya muda mrefu wa kutengana.

"Nilikuwa naingojea siku hii kwa muda mrefu sana, kuna muda nilidhani haitaweza kutokea lakini kweli hakuna lisilowezekana chini ya jua, sasa mtesi wetu yupo ndani na sisi tupo huru, kisasi cha aina gani hiki?"

Dokta akamkumbatia Jennifer kwa nyuma, akauliza, "au kuna lolote unalonidai, mpenzi?" Kwa kutumia ishara, Jennifer akamjibu hamna analodai kisha akatabasamu na kumgeukia dokta, akambusu mdomoni.

"Nisamehe sana," akasema kwa mikono, "kuna muda nilikuwa nakutilia mashaka juu ya hili, nilistaajabu kwanini haukutaka kutumia sumu nikammaliza upesi kumbe ulikuwa na mpango kabambe, mpango wa kuishi ya kifahari mpaka kufa kwetu."

Dokta akatabasamu, tabasamu la majivuno, alijiona yupo juu ya dunia hii, anapaa pasipo mipaka, akamtazama Jennifer machoni na kumwambia, "unaweza kuamini kuwa mpango huo haujaisha?"

Baada ya hapo kilichofuata kilikuwa ni kuonyeshana mapenzi mazito kinyume kabisa na umri wao, huenda walijiandaa sana kwenye kila mazingira, mithili ya watoto wenye damu changa wakakabiliana na kiu zao, baada ya dakika thelathini wakawa wamejilaza kitandani wanatazama dari, miili yao imefunikwa na shuka, kila mtu anahema kwa purukushani, dokta anavuja jasho jingi sana, Jennifer akamgeukia na kumpa ishara ya mikono ikisema,

"Niambie basi kuhusu mpango wako, au sipaswi kuusikia?"

Kisha akauweka mkono wake kwenye kifua kongofu cha dokta, naye dokta akatasamu, akamgeukia mwanamke huyo na kumuuliza, "unahamu kubwa ya kuujua?"

Jennifer akajibu kwa kichwa, uso wake umejawa na hamu ya udadisi, punde dokta akauvuta mto ulokuwapo pembeni yake na kumfunika nao Jennifer usoni, kwa haraka akanyanyuka na kumkalia Jennifer kwa juu yake, akatumia nguvu zake zote kumziba mwanamke huyo asipate pumzi, mwanzo Jennifer alidhani ni mchezo lakini kadiri muda ulivyoenda akabaini haikuwa mzaha, ulikuwa ni mpambano wa kutetea uhai wake, lakini alikuwa ameshachelewa, hakujiweza tena kujinasua, alitapatapa kwa kadiri yake lakini hakufua dafu, dokta alimng'ang'ania kama ruba, haikupita muda akaishiwa na nguvu, mikono yake iliyokuwa inapambana ikalegea na kujitupia kando, dokta akajua kashamaliza kazi.

"Sehemu yako katika mpango wangu imeshakwisha," alisema dokta, mwili wake unavuja jasho maradufu ya awali kwa kazi alotoka kuifanya, akafuta paji lake la uso kwa kiganja kisha akajimwagia pembeni ya kitanda, akautazama mwili wa Jennifer, ulikuwa umelala mfu, akafuata nguo alokuja nayo humo mfukoni akatoa chupa ndogo akammiminia mwanamke huyo mdomoni na pembeni yake kidogo, alipomaliza akachukua kichupa cha pili toka mfukoni akakifungua na kujipakaza mikononi kisha kwa uangalifu akatoka katika chumba hiki baada ya kujihakikishia usalama koridoni, akarejea chumbani mwake alipofunga kwa 'lock' na kuzima taa kuwa kiza totoro.

Kidogo, baada ya kama dakika tano, mabwana mawili wakashika korido ya hoteli hii wakiwa wanatembea mwendo wa dharura, bwana mmoja alikuwa mrefu mwembamba na mwingine akiwa mfupi ila mwembamba pia, wote wamevalia suti nadhifu rangi yake nyeusi, mabwana hao walikomea kwenye mlango wa chumba kimoja wakatazamana usoni, bwana mrefu akatikisa kichwa, yule mfupi akaufungua mlango kwa kusogeza tu kitasa, mlango ukafunguka wakazama ndani, si punde wakawa wamesimama kando ya mwili wa Jennifer, mwili uliolala chini ukiwa hauna pumzi ndani yake, hapo yule bwana mrefu akaitoa simu yake mfukoni na kuipiga, punde simu ikapokelewa akasema,

"Amekufa. Amekwishamuua."

Baada ya hapo kukawa na ukimya mfupi kisha akauliza, "tufanye nini?" Punde kidogo akakata simu na kumwambia mwenzake, "tuondoke."

"Tunafanyaje?" Mwenzake akauliza, akamjibu huku akiutazama mwili wa Jennifer, "boss amesema haituhusu, tuache kama ilivyo."

"Hivyo tu?"

"Ndio. Ametusihi kazi yetu hapa ni kutazama tu. Hili lipo nje ya maslahi yetu."

Baada ya maongezi hayo mafupi, walichomoa vifaa vyao walivyovipachika, vifaa vya kunasia sauti, kisha wakaondoka zao.


***
Duuh!
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA -- 37

Na Steve B.S.M



Pennyslavia, Marekani. Majira ya saa nane mchana.

AFISA Michael Summer alivua miwani yake ya jua akaiweka juu ya ‘dashboard’, alifanya hivyo baada ya kuzima gari lake kwani sasa hakuhitaji miwani hiyo maana ameshatoka juani na safari yake imekomea hapo, akafungua mlango na kutoka ndani kisha akaunyoosha mgongo wake, mgongo ukalia ka-ka-kaa! Akashusha pumzi ndefu ya uchovu kisha akalijongea jengo moja lililopo mbele yake, jengo lenye bango kubwa linalosomeka: THE SMITHS. Jengo hilo lilikuwa linahusika na mauzo ya vipuri vya magari, mlango na kuta ya jengo hilo kwa mbele ilikuwa ni ya kioo kitupu.

Akiwa anasogelea mlango, amebakiza kama hatua nne hivi, mara bwana mmoja aliyevalia ‘overall’ ya bluu na kapelo nyeusi alitoka ndani ya jengo hilo akiwa anatembea kwa upesi. Bwana huyo alikuwa anatazama chini akitembea, kidogo akampisha bwana Michael lakini kabla hajaenda popote alihamaki mkono wake wa kushoto umedakwa, kutazama akaona uso wa Michael ukimwangazia na kwenye mkono wa kushoto bwana huyo ameshikilia ‘beji’ ya polisi aliyokuwa anamwonyeshea.

Michael akasema, “bila shaka wewe ni Anthony Sandlers,” kabla bwana yule hajajibu, akaongezea: “mimi ni mpelelezi, nina maongezi kidogo na wewe.”

Maneno hayo yakamshtua bwana yule ndani ya overall. Alimtazama afisa Michael kwa macho ya shaka kisha akatikisa kichwa kuridhia alichoambiwa lakini ajabu ni kwamba punde mkono wa bwana huyo ulipoachiwa, alitimka mbio kama mwendawazimu!

Alitupa miguu yake kadiri alivyoweza akielekea mashariki mwa jengo lile, bwana Michael naye asiwe nyuma, akatimka kumfukuzia. Mbio mbio mbio! Bwana yule alivuka barabara akiyakwepa magari, naye Michael akafanya hivyo! Bwana yule aliwavuka watu na kuwasukuma huku na kule, naye Michael akafanya hivyo! Walikimbizana kwa kama dakika tano pasipo yoyote kufanikiwa.

Ni kama bahati, pikipiki moja ilitokea kusikojulikana ikamsukumia mbali bwana yule mwenye overall. Aliruka juu kiasi chake kisha akabamiza kwenye moja ya kuta ya duka, alipoanguka hapo akawa hana tena jipya, alitulia chini kuugulia maumivu. Bwana Michael Summer, akiwa anahema juu juu, akamsogelea bwana huyo huku akiwa ameshikilia kiuno chake. Alipomfikia akachuchumaa na kumtazama bwana huyo na mbio zake za sakafuni, akamwambia:

“Sasa naona tunaweza kuongea.”

Baada ya muda mchache watu hao wawili wakawa wamo ndani ya gari la Afisa Michael Summer, bwana yule wa overall, Anthony Sandlers kwa jina, akiwa yu kifungoni kwa pingu mikono yake ipo nyuma ya mgongo.

“Kama haufahamu kitu kwanini ulikuwa unakimbia?” Michael alifoka akimtazama Anthony. Macho yake yalikuwa makali, uso wake haukuwa na lepe la utani. “Nakuuliza wewe. Kwanini ulinikimbia?”

“Kwasababu niliogopa!” Anthony akafoka kwa ‘panick’. “Nilikimbia kwasababu niliogopa!” akarudia tena jibu lake. Afisa Michael akaingia mfukoni mwake na kutoa simu, aliifungua akamwonyesha bwana Anthony. Katika simu hiyo kulikuwa na picha kadhaa zinazoonyesha tukio la mauaji ya Travis. Picha ya mwisho ilikuwa ni ile iloandikwa kwa maandishi ya damu ya Travis ‘SUITS AND TIE’.

Anthony akasema kwa mkazo, “van uliyoitoa yard siku hiyo, ndo’ limehusika na mauaji ya afisa huyu wa polisi. Wewe ulikuwa zamu, nataka kujua nani alichukua usafiri huo.”

Kabla Anthony hajajibu, Michael akamwonyesha picha ya van hiyo, picha ambazo zilidakwa na CCTV camera, akasema: “Bila shaka sio gari ngeni machoni pako. Sasa naomba kujua, gari lilitokaje yard ukiwa unalinda na ni nani aliyelichukua.”

Anthony akamtazama Michael usoni, macho yake yalikuwa yanasema jambo lakini hakufungua mdomo kutamka, Michael akamsihi kama hatoonesha ushirikiano basi na yeye atajumuishwa kama mshirika wa mauaji, ‘an accomplice in murder’, kusikia hivyo bwana Anthony akashuku na kujitetea:

“Sijui nani alichukua hilo gari. Lilibiwa tu! … liliibiwa na mtu ambaye sikumwona.”

“Liliibiwa?” Michael akauliza kwa kejeli. “na ulinzi wote ule niliouona pale kwenye yard, gari liliibiwa vipi? Liliwezaje kupita kwenye mageti matatu mpaka nje pasipo kugundulika wakati wewe ndo’ mtu pekee unayetoa ruhusa ya kitu chochote kukatiza getini? Ina maana hukuliona au ulishiriki katika wizi huo?”

Anthony akashusha pumzi, hakuwa na cha kujibu. Alifikiria njia ya kujinasua na kikombe hiki lakini hakupata cha maana kichwani mwake. Michael aliendelea kumhimiza aseme ukweli ili ajiepushe na kesi ya mauaji, alimuahidi bwana huyo kuwa atamlinda na kumsaidia endapo tu akitoa ushirikiano kamili.

“Naamini kuna mtu nyuma ya maamuzi yako, Anthony. Niambie. Unaweza kuniamini.”

Anthony alifikiri. Akakumbuka familia yake nyumbani, mke na mtoto, chozi likamshuka. Aliisikia sauti ikisema kichwani mwake kumkumbusha maagano yake yake ya kazi ya kuwa uhai wa familia yake utakuwa rehani kama akienenda kinyume, akajikuta anatoa chozi zaidi.

Kabla hajasema kitu kingine, risasi ilipasua kioo cha nyuma ya gari kisha ikatua kichwani mwake na kumfumua ubongo! Yani ndani ya sekunde tu, bwana huyo akawa maiti ndani ya gari akimwaga damu pomoni. Afisa Michael akabaki ameduwaa. Hakukaa vema, mdunguaji aliyetoka kufanya tukio la mauaji, akamweka afisa huyo katika ‘target’ yake.

Kisha akavuta pumzi moja ndefu.


******

Kwenye Majira ya Saa tano usiku:

Hilda alijigeuza kitandani akalala chali, mikononi mwake ameshikilia tablet anatazama filamu humo ndani. Mwanamke huyo aliyekuwa amevalia nguo nyepesi ya kulalia, macho yake yalikuwa yamepwaya kwa uchovu wa usingizi lakini hakutaka kusalimu amri, alichokuwa anakifanya ni kubadilisha tu mapozi lakini tablet haiachii mkononi.

Katika chumba hiki hakukuwa na mwanga mwingine isipokuwa mwanga wa tablet pekee. Vitu vingine humu ndani havikuwa vinaonekana vema isipokuwa uso wa Hilda tu ambao ulikuwa unaangazwa na mwanga wa chombo hicho.

Mwanamke huyo akitazama filamu yake, alijisemea: “Nikifika katikati nalala. Nimechoka sasa.” Kisha akapiga mihayo miwili kwa mkupuo. Anapambana na macho asilale.

Katika dirisha la chumba hiko, kwa chini kabisa kuna gari lilionekana likisogea karibu na maeneo haya. Gari hilo lilikuwa ni van nyeusi isiyokuwa na maandishi, vioo vyake vyote ni tinted kiasi cha kutokuona aliyekuwemo ndani ama dereva anayeendesha.

Gari hilo lilisonga na lilipofika karibu na malango ambayo yanatumika kuingilia ndani ya makazi ambamo Hilda yumo, lilijiegesha na kuzima taa, kisha kidogo likazima na injini, kukawa kimya kama vile hakuna kitu.

Hilda alijitahidi kutazama filamu yake lakini kadiri alivyokuwa anasonga mbele akawa anazidiwa, usingizi ulimzidi nguvu mno, ilifikia kipindi aliachia tablet yake ikamwangukia usoni akashtuka kama mbwa aliyetupiwa jiwe, hapo ndo’ akakata shauri, acha tu alale.

Alizima kifaa chake akajilaza lakini kabla hajapotelea usingizini, alisikia mlango wake ukiita kengele keng-keng-keng-keng-keng! Akashtuka, akajiuliza ni kweli amesikia kengele ama ni mang’amung’amu yake ya usingizi, basi akakaa kusikiliza kwa umakini, kidogo kengele ikaita tena, kumbe si mang’amung’amu bali ni uhalisia, mlangoni pake kulikuwa na mgeni. Mgeni katika majira haya ya usiku.

“Nani huyu saa hii?” alilalamika akinyanyuka kitandani, akauendea mlango wake wa sebuleni na kabla hajafungua akachungulia nje kwa kupitia kitundu kilichopo mlangoni hapo, nje akaona sura ya mtu, mtu anayemjua, lakini hakujua kwanini mtu huyo yupo hapo muda kama huo, alitafakari upesi kama kuna jambo lililoenda kombo lakini hakulipata. Alifungua mlango wake akisema, “Karibu.”

Lakini uso wake, dhahiri shahiri, haukuonyesha kumaanisha kile alichokitamka ila hilo halimkuzuia mgeni wake kuingia ndani, aliingia na mlango ukafungwa. Korido ikabakia tupu na kimya.


****

East Hampton, New York. Saa saba usiku.


Bryson alizima gari lake kisha akatulia humo ndani kwa dakika kadhaa. Kuna jambo alikuwa analiwaza. Aliegemea kiti akitafakari, kidogo akashusha pumzi ndefu kisha akaufungua mlango wa gari na kwenda nje. Alihakikisha ame-lock gari yake kwanza ndipo akaelekea ndani. Alipofika mlangoni, alitaka kuweka ‘codes’ za kufungua mlango wake lakini akabaini kuna kitu hakipo sawa.

Taa ya sebuleni ilikuwa inawaka.

Akajiuliza kifuani mwake ni nani aliyekuwapo hapo, basi upesi akaweka codes na alipoingia alitembea upesi mpaka sebuleni, hapo akastaajabu kumwona mke wake amejilaza kwenye kochi. Mwanamke huyo amejikunyata akijifunika shuka.

Kabla hajasema jambo, mwanamke huyo alifungua macho yake na katikati ya giza jepesi la sebuleni akamwona mume wake amesimama kama mnara, akamuuliza: “Umetoka wapi muda huu, Bryson?”

Bryson akaketi, naye mke wake akanyanyuka na kukaa kitako.

“Umerudi saa ngapi kutoka hospitali?” Bryson aliuliza na kuongezea, “mbona hukuniambia kama unarudi nyumbani? Mtoto vipi?”

Mke wake aliguna kwanza alafu akamtaka mumewe atazame simu yake, Bryson akaitoa na kutazama, kwenye kioo kulikuwa na ‘missed calls’ takribani kumi toka kwa mkewe, tena na ‘messages’ kadhaa.

“Ulitaka nikuambiaje, Bryson kama hupokei simu zangu wala kujibu messages zangu?” mke akauliza. “nimejaribu sana kukutafuta, napiga na natuma ujumbe lakini kimya, ulitegemea ningefanya nini kama sio kuja nyumbani? Ajabu nakuja nyumbani haupo na unarejea majira haya? Ina maana huu ndo’ muda wako unaorudi nyumbani mimi nikiwa hospitali kumuuguza mtoto? Bryson!”

Bryson alikaa kimya, mke akaendelea kuongea akilalamika ya kwamba amemkuta mtoto aliyebakia nyumbani akiwa na njaa na amelala peke yake majira hayo ya usiku, alipomaliza kulalamika hayo akarejea kwenye swali lake, Bryson alikuwa ametokea wapi muda huo? Na akaongezea, kwanini hakuwa hapokei simu yake wala kujibu messages zake?

Bryson alikosa cha kujibu kwa muda huo, aliona kama kichwa chake kinafanya ziiiiii – ziiiiii- ziiiiii asielewe hata cha kufanya, upesi mke wake akanyanyuka kama radi na kumwendea kwenye kochi alilokaa, akampokonya simu na kuifungua, moja kwa moja akaenda kwenye ‘call logs’, huko akakuta mtu wa mwisho mwanaume huyo kuwasiliana naye alikuwa ni Hilda!

Mwanamke huyo akaanza kudondosha machozi kama mito ya baraka. Aliitupa simu ya mume wake kwenye kochi kisha akaenda zake chumbani. Korido nzima anavuta makamasi ya kilio. Aliamini kabisa kuwa Hilda ashamchukulia mwanaume wake. Moyo wake ulisinyaa kwa maumivu.

Bryson aliketi pale sebuleni kwa muda kidogo akiwaza mambo haya yanayojiri mbele ya macho yake. Alitaka kusimama kumwendea mke wake lakini akienda huko atamwambia nini akamwelewa? Hakuona jibu. Alikaa hapohapo sebuleni na nguo alizotoka nazo kazini mpaka usingizi ukamsomba, akakoroma kama nguruwe mdomo akiuacha wazi.

Jua linapokucha, aliamka akijikuta hapohapo kwenye kochi, akakurupuka kana kwamba amemwona mwizi. Alipotazama saa yake akashangaa kuona ni saa mbili kasoro asubuhi, upesi akanyanyuka kwenda kumtazama mke wake chumbani, hakumkuta! Akaenda pia kwenye chumba cha mtoto wake lakini pia vilevile hakumkuta, nyumba nzima alikuwa mwenyewe, mke hayupo na pia mtoto aliyekuwa amebakia naye hapa nyumbani hayupo. Akahisi kuchanganyikiwa.

Alipiga simu ya mkewe ikaita lakini haikupokelewa, akawaza kwenda hospitali lakini akienda huko itakuwa nini? Baada ya kufikiria kwa kina akaona ni stara kwenda kazini kuendelea na majukumu yake alafu akitoka huko, majira ya jioni, apitie hospitali kuungana na familia yake, pengine mke wake atakuwa amepunguza jazba. Akajiandaa na muda si mrefu, kama dakika arobaini na tano, akawa amefika kazini.

Huko akakutana na Richie. Alikaa hapo ofisini kwa kama dakika kumi na tano pasipo Hilda kutokea, akamuuliza Richie kama ana habari yoyote kumhusu mwanamke huyo, Richie akasema aliwasiliana naye mara ya mwisho jana mapema, hakupata kuwasiliana naye tena hivyo hajui kinachoendelea, siku ikazidi kusonga, wanaume hawa wawili, wote, wakiwa katika maswali na mashaka. Kila mmoja katika muda wake alimtafuta Hilda pasipo mafanikio, simu ilikuwa inaita lakini haipokelewi.

Yalipofika majira ya mchana, wakati wa mapumziko ya kupata chakula cha mchana, Richie akautumia muda huo kwenda nyumbani kwa Hilda kumjulia hali. Hakuweza kuvumilia mpaka jioni wakati wa kutoka kazini. Kila dakika iliposogea alijikuta anazidiwa na hofu na anapaliwa na woga. Alipofika huko, akaukuta mlango wa Hilda ukiwa wazi pasipo kufungwa na funguo, alitegua kitasa akaingia ndani na punde kidogo akabaini jambo ambalo hakulitegemea.

Jambo la kutisha.

Aliukuta mwili wa Hilda ukiwa kitandani, hauna uhai, damu zimetapakaa kwenye godoro na shuka. Maiti ya mwanamke huyo imeachama mdomo na macho wazi!



***
Looh! Hiki kizaazaa kakileta richie yeye mwenyewe
 
TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 38.


Na Steve B.S.M



RICHIE aliishiwa nguvu za miguu akajikuta anaketi chini. Kwa muda kidogo hakujua afanye nini kwani akili yake ili-jam, haelewi anachokiona, ni baada ya dakika kadhaa ndipo alipata akili ya kutoa taarifa akapiga 911 na muda si mrefu gari ya wagonjwa ikafika ikiongozana na maafisa wa polisi. Richie akampa taarifa Bryson naye mwanaume huyo akafika katika eneo la tukio si muda mrefu, jasho linamtoka, moyo unamwenda mbio.

Alimkuta Richie yuko pembeni ya gari la polisi, akamfuata ampatie habari kwani yale aliyomweleza kwenye simu alihisi kutoelewa vema.

“Boss, kuna mtu amemuua, Hilda,” Richie alisema kwa uchungu. Macho yake mekundu na anatetemeka mwili mzima. Alimkumbatia Bryson akashindwa kujihimili, akajikuta analia kama mtoto, sasa kazi ya Bryson ikawa kumbembeleza.

Kidogo mwili wa Hilda ukatolewa ndani ukiwa juu ya machela, umefunikwa gubigubi, ukawekwa kwenye gari la wagonjwa alafu gari hilo likatimka, Bryson akalitazama mpaka linaishia, hakuamini ule ndo’ ulikuwa mwisho wa yeye kumwona Hilda. Punde afisa mmoja wa askari akawafuata na kuwataka wanaume hao wawili waelekee kituo cha polisi kwaajili ya kutoa maelezo kama watu wa karibu na mhanga wa mauaji.

Baada ya lisaa wakawa wapo ndani ya ofisi ya mpelelezi, wameketi nyuma ya meza kubwa nyeupe lakini kiti cha mpelelezi kipo tupu. Nje ya ofisi hiyo, koridoni kona ya pili, kulikuwa na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, ndani ya ofisi hiyo Mkuu alikuwa ameketi kwenye kiti chake jasho linamvuja, mkononi ameshikilia simu inayoita.

Simu iliita kidogo ikapokelewa, Mkuu akauliza moja kwa moja: “Umempata Michael?” mtu wa upande wa pili akamjibu hapana, akaghafirika mno. “Sasa yupo wapi? Anajua kabisa yu mwenyewe hivi sasa na simu hapatikani siku ya pili hii! Sasa kweli hizi kesi nitawapa hawa maafisa wachanga?” kidogo akakata simu, akatoka ofisini kwake kwenda kuonana na afisa mmoja, bwana mdogo ambaye alikuwa miongoni mwa wale maafisa waliofika kwenye eneo la tukio, akampatia maelekezo mafupi kisha bwana huyo mdogo ndo’ akaenda kujumuika na wakina Bryson katika kile chumba cha mpelelezi.

Aliwahoji wahusika wake, mmoja baada ya mwingine, akarekodi kila alichosikia na kila kilichosemwa, baada ya hapo akachukua mawasiliano yao kisha akawaachia. Aliwaambia kwa sasa hawatakiwi kutoka nje ya jiji la New York mpaka pale upelelezi utakapokamilika kwani wanaweza wakahitajika muda wowote, lakini pia aliwataka waongeze uangalifu zaidi kwenye nyendo zao maana hamna anayejua ni nani alihusika na mauaji na lengo lake haswa ni nini.

Wakatoka ndani ya kituo na Bryson akanyookea moja kwa moja kwenye gari yake, akafungua mlango lakini kabla ya kuingia ndani akageuka nyuma kutazama, akamwona Richie amesimama mbali naye akiwa anamtazama tu, hakuelewa bwana huyo anawaza nini ama anafanya nini hapo, akapaza sauti kumuuliza; “vipi kuna shida?”

Richie hakujibu, aliendelea kusimama akimtazama, akakata shauri kumfuata. Alipomfikia akamuuliza nini kimejiri, Richie kwa sauti ya upole akamwambia anataka kwenda nyumbani.

“Sawa,” Bryson akamjibu na kumwambia, “twende nikupeleke.”

Richie akatikisa kichwa na kusema, “Nitaenda mwenyewe.” Kisha akaondoka zake akimwacha boss wake kwenye butwaa.

“Ana nini huyu?” Bryson alijiuliza mwenyewe asiwepo wa kumjibu.



***

Haven of Peace Hotel, New York. Majira ya saa nane mchana.


Mkuu wa upelelezi alitazama barabarani kushoto na kulia akiwa mbele kabisa ya hoteli hii. Bwana huyo alikuwa amesimama hapo mwenyewe, amevalia suti ya kijivu na miwani ya jua.

Alitazama saa yake ya mkononi kisha akatazama tena kushoto na kulia barabarani, upande wa kulia akaliona gari moja ambalo lilimteka hisia zake, SUV nyeusi na maridadi, gari hilo halikuwa na ‘plate number’ na mwendo wake ulikuwa wa wastani. Katika magari yote ambayo yalikuwapo barabarani, hili ndo’ liliteka macho ya mkuu.

Kitambo kidogo gari hilo lilifika mbele ya hoteli, akashuka kijana Babyface. Kijana huyo alikuwa amevalia suti nyeusi maridadi, uso wake hauna matani, alimtazama mkuu wa upelelezi akamsalimu kisha akaendelea na mambo yake, mambo ya kutazama usalama wa hapa na pale. Alipojiridhisha akafungua mlango wa gari akashuka bwana mmoja upesi, bwana huyo alikuwa amevalia shati rangi ya ugoro na suruali nyeusi ya kitambaa, kichwani amejivesha kofia aina ya fedora, rangi yake nyeupe.

Bwana huyo pasipo kumsalimia Mkuu wa upelelezi akaingia ndani ya hoteli moja kwa moja nyuma yake akiwa anafuatwa na Babyface kisha mkuu wa upelelezi kwa nyuma kabisa.

Alitembea kwa ufupi akiwa ametupa mgongo, alipofika mahali anapoelekea, chumba kidogo cha makutano, ndipo akavua kofia yake na kumtazama mwenyeji wake hapa. Kumbe bwana huyo alikuwa ni Brendan Garret, mkuu wa shirika la ujasusi wa nje nchini Marekani, yaani CIA. Ni wazi hakuwa hapa kwa kikao maalum cha serikali, nguo alizovaa zilisema hivyo; hayupo eneo hili kiofisi.

Mhudumu, mwanamke aliyevalia sare nadhifu, alifika akawasikiliza wateja wake, wateja wakaagiza maji akaenda zake, hapo ndo’ maongezi rasmi yakaanza.

“Umefikia wapi kuhusu Mpelelezi?” Garret aliuliza akimtazama Mkuu wa upelelezi, kando yake ameketi Babyface, wote sura zao zimejifunga kwa umakini. Mabwana hawa walikuwa wanamtazama Mkuu huyu kana kwamba ‘drafti’ linalodai akili.

“Well …” Mkuu wa upelelezi akafungua kinywa, “nimefanya kila jitihada zilizopo ndani ya uwezo wangu na nimethibitisha kuwa kweli amekufa.”

“Kivipi?” Garret akauliza. “Umethibitishaje kuwa amekufa?”

Mkuu wa upelelezi akatoa mkoba wake ambao ulikuwa chini ya meza kwa muda wote huo, na hilo likathibitisha bwana huyu alikuwapo hapa kwa kitambo kidogo. Katika mkoba huo alitoa bahasha moja ya kaki, akamnyooshea bwana Garret, Babyface akaidaka kwanza na yeye ndo’ akaifungua kutazama ndani. Alitoa picha kadhaa akamkabidhi bwana Garret kisha akatoa na karatasi kadhaa zenye maelezo na mihuri, akamkabidhi pia bwana Garret.

Mkuu wa upelelezi akasema, “huo ni uthibitisho. Mahali ambapo mwili wake ulipokelewa na kuhifadhiwa, mpaka na vipimo vya DNA vya mabaki ambayo hayakuwa na uwezekano wa kutambulika kwa macho ya kawaida, vyote vinathibitisha alikuwa ni mpelelezi. Ni bayana ame---” akasita kumalizia, mhudumu alikuwa anaingia na yale alokuwa ameagizwa, alipoyaweka na kuweka kila kitu sawa aliondoka zake Mkuu wa upelelezi akaendelea habari yake, habari ya kuthibitisha kuwa mpelelezi amefariki kwenye ajali ile mbaya.

Maelezo yake pamoja na vielelezo alivyotoa vikamkosha bwana Garret, aliamini hamna shaka sasa kuhusu kifo cha mpelelezi. Alimkabidhi nyaraka zile Babyface, naye bwana huyo akazirejesha kwenye bahasha kisha akatulia nazo.

“Kitu pekee nilichokuwa nahofia ni kumbukumbu za mpelelezi,” akasema bwana Garret, “laiti angelikumbuka hata lepe ya yale yaliyotokea nyuma ambayo najua hata wewe unayafahamu vema basi tungekuwa katika matata makubwa. Nashukuru mpaka kifo chake hilo halikupata kutokea, sijilaumu kwanini nilingoja. Lakini pili nashukuru hakupata kitu chochote kumhusu yule mwanamke tunayemtafuta, hata kama alipata kitu basi hivi sasa hakina maana tena, mwili mfu hausimulii hadithi.”

Akaweka kituo anywe maji, alipofanya hivyo akaendelea kunena, mara hii uso wake ukionyesha kuzama kwenye fikra.

“Lakini kipya ninachowaza hivi sasa ni kwamba, unadhani ile ajali ya mpelelezi ilikuwa ni ajali asili? Kama sivyo, ni nani ambaye angetaka kumuua bwana yule na kwasababu zipi?” alipouliza hayo alimtazama Mkuu wa upelelezi akamuuliza, “au unajua lolote?”

Mkuu akamwambia hajui kitu kwani oparesheni ambayo alikuwa anaifanya mpelelezi ilikuwa nje ya utaratibu, alisimamishwa kazi kwa wakati huo kwasababu ya utovu wa nidhamu, haswa kukaidi kuwa mkabala na mshirika ambaye alipatiwa.

Alisema, “Kama kungekuwa na jambo la siri katika tukio lile basi ningelijua, ama nitalijua. Lakini kwa mazingira niliyoyakagua na vijana wangu mpaka sasa, sina budi kuamini ajali ile ilikuwa ni ya asili. Madereva wote wawili walikamatwa na mazingira yote ya ajali yakajieleza bayana, hitilafu ya gari.”

Basi baada ya maelezo hayo, waligongesha glasi zao za maji kwa kujipongeza kisha maongezi yalofuatia baada ya hapo yakawa maongezi mepesi, maongezi ya kusogezea muda zaidi kuliko ya kumaanisha.

Swali likiachwa kwetu, ni kumbukumbu gani ambayo iliwafanya wakuu hawa wawili kuogopa nyendo za Mpelelezi? Lakini je, kama hofu hiyo haikuhusika na ajali ile kwa vyovyote, basi ni nini kilikuwa nyuma ya ajali ile mbaya kupata kutokea?


***

Majira ya Saa kumi na mbili ya jioni:

“Nimeshafika, nipo hapa chini.” Alisema Jamal kwenye simu akiwa ameegamia gari, mbele yake kumesimama jengo kubwa analolitazama, jengo ambalo ndani yake ndimo Richie anapata kuishi.

Muda si mrefu, kama baada ya dakika tatu, Richie akatokea kujiunga na Jamal. Bwana huyo alikuwa amevalia tisheti kubwa na bukta fupi, miguu yake ameisitiri kwenye ‘crocs’. Macho yake ni mekundu sana, haikuhitaji shule kujua ametoka kumwaga machozi muda si mwingi ulopita.

Jamal alimkumbatia bwana huyo kumpa faraja kisha akamuuliza ni nini kimetokea kwani alimvyompigia simu hakumweleza mengi, lakini swala hilo likageuka kuwa mtihani mgumu sana kwa Richie. Kila alipojaribu kueleza alijikuta anakabwa na uchungu kooni, taswira ya mwili wa Hilda usokuwa na uhai haikumuacha akakaa salama.

Kama baada ya dakika kadhaa ndipo angalau aliweza kumudu kifua chake akafungua kinywa na kuongea:

"Jamal, Bryson amemuua Hilda."

Jamal akatoa macho kwa butwaa. Richie akaongezea,

"Nina uhakika aslimia mia, yeye ndo' kamuua Hilda."


***
Lah hallaullah! Rich ilitakiwa atangulie sio hilda pumbavu kabisa
 
Asante tivu mbona nahisi kama hilda ameuliwa na mke wa Bryson ngoja tuone
Hilda kaondolewa na alie taka kumuondoa richie ila alinusurika! Ila kama ni mke wa bryson basi itakua ni Brrrrrraking newz
 
Duh! Jamaa bado kakomaza fuvu[emoji849][emoji3517]
 
Back
Top Bottom