TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA - 28
Na Steve B.S.M
"Namba unayopiga haipatikani ..."
Ilikuwa ni mara ya tatu sasa Mpelelezi anausikia ujumbe huu lakini bado hakuamini masikio yake, akapiga tena na tena, bado majibu ni yaleyale, namba unayopiga haipatikani kwa sasa.
Akasonya akishika kiuno, majira sasa ni saa tatu asubuhi, amesimama nje ya hoteli alofikia akiwa anatazama barabara kuu inayokatiza hapo, barabara hiyo ilikuwa na wingi wa magari pia na wingi wa watu wanaoenda na kurudi.
Alisimama hapo akiwa anatazama huku na kule, akili yake ipo mbali sana japo macho yake yanaangaza hapa, kichwani alikuwa anatafakari ni nini kimetokea na muda mwingine akiwa anadhani pengine anaota.
Alifungua simu yake akaingia mtandaoni, moja kwa moja akaelekea kwenye tovuti ya kupata habari za jiji la New York, si kwamba hakuingia huko hapo mwanzo, hapana, alishaingia kama mara nane sasa, na si tu sehemu moja, bali tovuti mbalimbali lakini bado hakuwa ameridhika.
Akajaribu tena kupiga simu, yaleyale, simu haipatikani, akang'ata meno yake kwa hasira, kidogo tu akiwa hapohapo, kabla hajafanya kingine, akahisi kitu kimegusa mguu wake wa kushoto, upesi akageuka.
Kumbe ilikuwa ni fimbo, fimbo ya mtu mlemavu asiyeona, fimbo ndefu rangi yake nyeupe.
Kutazama uso, akamwona bwana yule mlemavu ambaye anaishi naye hotelini hapa, bwana huyo alikuwa amevalia suruali nyeusi ya kitambaa, chini ana raba za kawaida sana, hata shati lake la juu halikuwa limenyooshwa, limejikunjakunja kana kwamba limekamuliwa na baunsa, usoni mwake, kama kawaida, alikuwa amevalia miwani meusi.
Bwana huyo alikuwa akitembea akiwa ametanguliza fimbo yake mbele kama macho, lakini alipogusa mtu alihisi kitu akasema upesi,
"Samahani sana, bwana."
Kisha akatabasamu kiwepesi na kuendelea na safari yake kana kwamba hakuna kilichotokea, Mpelelezi akabaki akimtazama bwana huyo namna akienda zake, hakukoma kumtazama mpaka anaishilia akijiuliza mtu huyu ni wa wapi na huku San Fransisco alipokuja hana ndugu kiasi amefikia hotelini? Na kama ni biashara basi ni biashara gani hiyo?
Kwa muda kidogo bwana huyo akawa amemsahaulisha mawazo yake ya awali, mawazo ya kuwaza kifo cha kutatanisha cha Travis, bwana yule alipoishia, akasimamisha taksi iliyokuwa inakatiza, akakwea na safari ikaanza.
Akiwa katika gari hilo, kando ya dirisha, alifungua simu yake akanyookea moja kwa moja kwenye kategoria ya picha, huko akatafuta kidogo na kuangukia kwenye fali alilolutunza kwa jina 'diary'.
Akalifungua na kuanza kutazama ...
Humo kulijaa picha za diary ile alopatiwa na yule mama ambaye mwanaye alifariki, diary ambayo ilikuwa na matukio ya yule mwanamke ambaye picha yake inatumika kwenye kitambulisho cha mtuhumiwa wa mauaji ya The DL.
Mpaka safari inakoma, Mpelelezi alikuwa anasoma diary hiyo kwakupitia picha za simu yake, alikuwa anazipitia kwa umakini kana kwamba anazifanyia mtihani baadae.
Aliposhuka, aliweka simu yake mfukoni akatazama nyumba iliyosimama mbele yake, ilikuwa ni ghorofa ya sakafu kadhaa, rangi yake dhahabu iliyopauka.
Akaingia humo na kunyookea mlango nambari 64, akagonga hapo, sauti ya kike ikaitikia, kidogo mlango ukafunguka akachungulia msichana mwenye makamo ya miaka ishirini hivi, nywele zake ndefu rangi ya bia, macho yake gololi na 'lips' zake nyembamba sana, akamuuliza Mpelelezi,
"Naweza kukusaidia?"
Mpelelezi akaeleza adhma yake. Alionyeshea picha ya kijana fulani katika simu yake kisha akasema anahitaji maongezi machache kuhusu kifo cha mtu huyo.
Alipofanya hivyo, msichana yule akakodoa, uso wake ukapara kwa hofu, akatazama kama Mpelelezi yu na watu wengine, akaona yu mwenyewe, basi upesi akaufunga mlango wake lakini kabla hajafanikiwa, Mpelelezi akauzuia kwa mkono.
"Naomba tuongee tafadhali!"
Msichana yule akakataa katakata, hakutaka kusikia lolote toka kwa Mpelelezi bali kuondoka kwake tu, akalazimisha kufunga mlango kwanguvu zake zote Mpelelezi akimzuia, ilikuwa ni kama igizo la futuhi.
Msichana huyo alipoona hana uwezo wa kumshinda nguvu Mpelelezi, akapaza sauti ya kuomba msaada, sauti yake ilikuwa kali na nyembamba yenye kuumiza sikio, Mpelelezi aliposikia hayo akaachia mlango upesi kutazama mazingira yake ya usalama.
Hakutaka kuleta zengwe hapa, anafahamu fika hakuwa na kitambulisho wala chochote cha kumtambulisha kama yeye ni mwanausalama, hivyo hakuwa na uhalali wowote wa kuwa hapo.
Akatoka hapo haraka akielekea chini lakini wakati huo baadhi ya majirani walishatoka kwenye viota vyao kutazama kinachoendelea, walimtazama Mpelelezi akienda zake na Mpelelezi kama asiyejua kilichoendelea hapa, akatembea kama mtu aliye katikati ya jiji, hakujali watu, ni kama vile hakuwa anawaona, alipofika chini akaitisha taksi na kuketi kitako.
Akiwa ndani ya gari alitazama anwani nyingine ya kuitembelea kisha akampatia dereva maelekezo na gari likaelekea huko.
Njiani akaendelea kusoma ile 'diary' kwenye simu yake, hakutaka kuwaza kitu kingine kabisa, mawazo yake yalikuwa hapo kwa asilimia zote, na kweli baada ya muda mawazo yake yakalipa, kuna jambo akaona humo, jambo la muhimu kuliandika chini, akafanya hivyo katika simu yake hiyohiyo ...
Alitazama orodha ya anwani za kutembelea akaona imesheheni, alikuwa na sehemu nyingi za kwenda na watu wengi wa kuongea nao, kazi ndo' kwanza ilikuwa inaanza, tena katika kipindi chake kibaya kazini.
Alichoomba ni huko kwengine kusilete matata kama hapa alipotoka, la sivyo ... Akatikisa kichwa, lakini alijikuta akitabasamu pale alipokumbuka mkasa wa yule msichana, namna walivyokuwa wanagombania mlango ilikuwa kituko haswa, lakini kila kitu kina sababu, aliamini msichana yule alikuwa na sababu ya kukataa kuongea naye na ni jukumu lake kujua sababu hiyo ni ipi ...
Basi gari likatokomea katika barabara yake ...
***
"Umepata taarifa?" Aliuliza bwana akiwa anaketi chini, mkononi alikuwa amebebelea glasi yenye kinywaji rangi ya dhahabu, glasi inachuruza kwa baridi.
Bwana huyu si mgeni machoni petu, la hasha, alikuwa ni yule mwanaume ambaye alitambulishwa kama mume kwa yule mwanamke ambaye alikutana na Mpelelezi katika uwanja wa kuchezea kamari, yaani Casino.
Mwanaume huyu ambaye tulimwona siku ile akiwa ameukunja uso kumkuta Mpelelezi pamoja na Mwanamke yule ndani, hapa alikuwa na uso wa binadamu wa kawaida kama mimi na wewe, alipoketi alimpatia mtu aliyekaa naye mkabala glasi hiyo alokuja nayo kisha yeye akawa mtupu isipokuwa chupa yake ya maji mezani.
Mtu huyo aliyekuwa naye mkabala si mwingine bali ni yule mwanamke ... mwanamke mrembo mwenye utashi wa kucheza kamari kiasi cha kumshtua Mpelelezi, alikuwa amekaa ndani ya blauzi na pensi fupi ya jeans, uso wake una 'make-up' ya kiasi.
Alikunywa kile alicholetewa kwa fundo moja kisha akaiweka glasi mezani, ndipo akauliza,
"Taarifa gani?"
"Yule bwana yupo San Fransisco," akasema yule mwanaume akiwa anamtazama Mwanamke huyo kwa macho ya mkazo, hata alipokunywa maji yake bado alikuwa anamtazama kwa kumkazia mboni.
"Oooh ..." Mwanamke akaitikia, lakini macho yake hayakuonyesha mshangao wowote kama ilivyokuwa kwenye kauli yake, alikuwa anatazama glasi yake ya kinywaji mezani kama mtu anayefikiria jambo.
Mwanaume akasema,
"Hii ndo' fursa yetu sasa ya kurekebisha makosa."
"Makosa yapi?" Mwanamke akauliza macho yake yakimtazama mwenziwe.
"Hujui makosa yapi?" Mwanaume akastaajabu. "Ulipata nafasi nzuri lakini hukufanya uliyotakiwa kufanya, nilistaajabu kumkuta bwana yule akiwa hai katika nyumba yako!"
"Najua ninachokifanya, Jerry!" Mwanamke akawaka. Aliyatoa macho yake kiasi kuonyesha msisitizo wa anachokisema, Mwanaume akatabasamu, halikuwa tabasamu la furaha.
"Ni kipi hiko? Tulipewa kazi moja tu, moja tu!"
"Na nitaifanya. Sawa?"
"Kama ulilenga hivyo, Evelyn, kwanini ulihitaji msaada wangu siku ile?"
Siku ile ...
Siku ile?
Siku ipi hiyo? ...
Ngoja kidogo,
Ilikuwa ni majuma kadhaa yaliyopita, siku ambayo Mwanamke huyu, Evelyne, alikuwa katika gari majira ya saa tatu usiku akiwa anatazama dirishani.
Hakuwa mwenyewe, pembeni yake alikuwapo huyu mwanaume, Jerry, akiwa ametulia kama chai ndani ya chupa, naye macho yake yalikuwa yanatazama nje, ni bayana kuna kitu walikuwa wanangojea hapa.
Baada ya muda kidogo, Jerry, yaani huyu mwanaume akauliza,
"Una uhakika atakuja hapa?"
Kisha akatazama saa yake ya mkononi.
Mwanamke yule, yaani Evelyne, akiwa anaendelea kutazama nje, akamtoa shaka mwenzake, bado aliamini mtu wake atakuja kama walivyokubaliana hata kama ni kwa kuchelewa.
"Kwa namna nilivyoongea naye mara ya mwisho, naamini kabisa atakuja."
Kweli, haikupita dakika kumi baada ya hiyo kauli, wakamwona mwanaume akiwa anatembea kwa kasi, Jerry alikuwa wa kwanza kumwona, akamnyooshea kidole akiuliza,
"Sio yule?"
Kutazama, ni Mpelelezi, bwana huyo alikuwa ameshuka toka kwenye gari la kukodi si muda, sasa anatazamia kuingia ndani ya Casino.
"Anajua amechelewa, unaweza ukaona tu mwendo wake," alisema Mwanamke ndani ya gari kisha akafungua mlango na kushuka, nyuma yake akifuatiwa na Jerry.
Waliingia ndani, wakasimama kwa mbali walipojihakikishia kumwona Mpelelezi, walikuwa wanamtazama kwa umakini kuhakikisha hapotei machoni mwao, kidogo wakamwona mhudumu akiwa na Mpelelezi, papohapo Evelyne akamtazama Jerry kwa kumpa ishara kisha akafungua pochi yake na kumkabidhi kitu mwanaume huyo, Jerry alipopokea, akaondoka kumfuata yule mhudumu aliyeongea na Mpelelezi, wakati huo Evelyne akiwa anatazama.
Baada ya muda kidogo, Jerry akarejea na kumwambia Evelyne kuwa kazi imekamilika, kila kitu kimeenda kama kilivyopangwa, Evelyne akampongeza, wakangoja kwa dakika kadhaa wakiwa wanamtazama Mpelelezi kwa mbali, muda ulipowadia, Evelyne akaaga na kwenda moja kwa moja kumfuata Mpelelezi.
Alipokuwepo huko, Jerry alikuwa anatazama kila kitu, macho yake hayakubanduka hata sekunde, aliangalia kila kinachoendelea.
Baada ya muda kidogo, akaona Mpelelezi anadondoka, hapo Evelyne akamtazama na upesi akasogea katika eneo la tukio, akambeba Mpelelezi wakijinasibu wapo naye pamoja kisha wakatoka zao kwenda nje.
Jerry akiwa amembebelea Mpelelezi begani, nyuma yake Evelyne akiwa anatembea kwa upesi, walinyookea kwenye gari lao wakampakia Mpelelezi humo na kuondoka.
Hawakwenda mbali, Jerry akashuka na kumwacha Evelyne peke yake kwenye gari, alimwambia kuna mahali anapaswa kwenda na asubuhi watapata kuonana, basi Mwanamke akiwa katika usukani, akaenda zake akiwa amembebelea Mpelelezi nyuma kana kwamba mzigo.
Lakini akiwa anaenda alikuwa akikaa kumbuka kauli ya Jerry, ya kwamba amtupie mwanaume huyo mahali salama baada ya dakika thelathini kupita kwani hatokuwa na uhai tena.
Kinyume na hapo akanyookea na mwanaume huyo nyumbani akiwa bado ni mzima, anahema japo hana fahamu, huko akamtua na kumpeleka moja kwa moja chumbani.
Kesho yake asubuhi, Jerry alipokuja, anastaajabu kumwona Mpelelezi sebuleni, na alipopata wasaa wa kuzoza na Evelyne kule chumbani aliuliza ni kivipi mwanaume yule alikuwa mzima ingali walimuwekea dawa kali kwenye kinywaji.
Majibu ya Evelyne hayakueleweka, Jerry akahitimisha kuwa dawa ilikuwa imebadilishwa, haikuwa ile waliyoipanga kwani kwa ukali wake uhai wa Mpelelezi ungekuwa historia hivi sasa.
Lakini kwanini Evelyne alifanya hivyo? Hakuna aliyejua bali yeye mwenyewe, sasa anapata nafasi ya pili, nafasi ya sasa hivi, nafasi ya leo hii, Jerry anamsisitiza lakini kama haitoshi simu inaita, anampatia Evelyne aongee nayo, ilikuwa ni simu ya kazi.
Mtu ambaye hakumjua ni nani mpaka pale aliposikia sauti yake.
Mtu huyo akamweleza kuwa hapo alipo yupo nyuma ya gari la kukodi alilomo Mpelelezi, anamfuatilia kwa kitambo sasa, na atakapopata wasaa basi ataimaliza kazi yake upesi bila kusita.
Kabla Evelyne hajaongezea neno, simu ikakatwa, akamtazam Jerry kwa mshangao.
"Hata mimi sikufahamu hilo!" Jerry akajitetea akiwa ameyatoa macho.
Evelyne akasema,
"Kwahyo hapa tuongeapo, kipofu muuaji yupo kazini?"
"Ndio," Jerry akajibu kwa kujiamini, "si umesikia mwenyewe?"
Evelyne akanyanyuka upesi na kwenda zake, hata kinywaji chake hakumaliza, Jerry akajribu kumwita lakini hakufua dafu, mwanamke alienda zake kana kwamba ni kiziwi, hakuna anachosikia.
***.
nini kinaendelea hapa?