TUKIBAKI HAI, TUTASIMULIA
Na Steve B.S.M
Sehemu ya Tatu
"Mitchelle! ... Hey! ... Mitchelle! ... Kimbia! ... Kimbia Mitchelle, kimbia!"
Mitchelle alijaribu kunyanyuka. Mwili wake ulikuwa mzito. Viungo vyake vilikuwa vinauma. Alitazama mkono wake wa kushoto akaona unatiririka damu nyingi. Ni hapo ndipo akabaini ana jeraha kubwa begani.
Jeraha la risasi.
Alijaribu kuelewa kinachoendelea lakini hakufanikiwa abadani. Alikuwa anasikia sauti nyingi kwa wakati mmoja: huku mitutu ya bunduki ikitapika risasi kwa fujo, kule makelele ya watu wazima wakipayuka mithili ya wendawazimu, hapa kelele kali za magari asiyojua yanaelekea wapi na huku juu ndege zikikatiza karibu kana kwamba zinanyunyuzia dawa kwenye mshamba makubwa ya zabibu.
Ilikuwa ni tafarani!
Akiwa anabung'aa hapo, asijue lipi la kufanya wala wapi pa kukimbilia, alimwona mtu akimjia kwa kasi. Alitambua mtu huyo ni mwanaume kwasababu ya umbo lake lakini hakuweza kumjua ni nani hasa.
Kila alipojitahidi kumtazama usoni hakufanikiwa. Macho yake yalikua yamepooza. Yameishiwa nguvu. Kila alichokiona kilikuwa hafifu.
Alifumba macho kwanguvu. Aliamini pengine yatakuwa sawa akiyafungua. Alipoyafungua alimwona yule mwanaume amemfikia, ameinama akimpa mkono.
"Amka tuondoke!" sauti ilimwamuru. "Haraka, Mitchelle, hatuna muda. Amka, utakufa hapa!"
Mitchelle alijitahidi lakini jitihada zake hazikumridhisha mwanaume yule. Kufumba na kufumbua, alijikuta amenyanyuliwa kama mzigo wa kuni! Aliwekwa begani mwanaume yule akaanza mbio.
Mbio! Mbio! Mbio!
Alitupa miguu yake kwa kasi. Ni kama vile hakuwa amebeba kitu. Alienda kushoto, akarudi kulia. Alienda kulia, akarudi kushoto. Yote katika kukwepa mashambulizi ya risasi.
Mwanaume huyu alikuwa mwepesi ajabu. Na vipi kuhusu nguvu zake? Hakika alikuwa ni shupavu.
Alikimbia kwa kama mita mia mbili bila kupumzika lakini punde hivi, akasimama ghafla!
Ghafla sana.
"Nisamehe, Mitchelle."
Bwana yule alisema kwa utulivu. Sijui aliona nini lakini sauti yake haikuwa na matumaini tena ndani yake. Alisimama kama mshumaa. Mshumaa unaoteketea katika moto.
Haikupita hata sekunde tatu hapo, sauti kubwa ya mlipuko ikaita .. BOOOOOM!! ... Kufumba na kufumbua, yeye na Mitchelle walipotea katika vumbi na moshi mzito.
Moshi huo ulitawala kwa kama dakika tatu hivi kabla ya taswira ya Mitchelle, amelala kifudifudi, kuonekana kwa mbali, hatua kama thelathini toka eneo la tukio. Ni bayana alikuwa ametupwa na nguvu ya bomu. Kheri ni kwamba alikuwa mzima wa mwili.
Upande wa pili, yule mwanaume hakuwa amebakia kitu. Ni vipande vya nyama ndo' vilisambaa huku na kule. Kama ungevikusanya vipande hivi visingetoshea hata kwenye rambo.
Masikini alikanyaga mtaro wa mabomu bila kujua.
Mitchelle alinyanyua uso wake uliojawa udongo na vumbi, akatazama. Hakuona kitu. Ni kama vile mambo yalikuwa yanatukia ndani ya mvuke hivi.
Ingawa macho hayo yalimpatia tabu ya kuona, alifahamu fika kilichotokea. Yule mwanaume aliyemsaidia hakuwapo tena. Mlipuko ule ulienda naye.
Alilia kwa uchungu sana.
Alipiga yowe aliloamka nalo kitandani alipokuwa amejilaza kwa masaa kadhaa tangu alipodungwa sindano na Ferdinand.
Alitazama kushoto na kulia. Alikuwa anahema kwanguvu. Alizika uso wake kwenye viganja vyake vidogo akijaribu kufikiria kile alichokiota, kidogo mlango ukafunguliwa.
Alikuwa ni Jennifer, mwanamama mfanyakazi. Aliwasha taa upesi, kwa kupiga makofi mawili tu, kisha akamsogelea Mitchelle kitandani.
Japo mwanga wa taa hii ya chumbani ulikuwa ni hafifu, ulitosha kabisa kuonyesha uzuri uliokuwemo humu ndani. Kitanda kikubwa cha glasi, godoro lenye inchi zake za kutosha, shuka jeupe na mito laini ni baadhi tu ya vingi vilivyokuwamo.
Jennifer alipanda kitandani akaketi kando ya Mitchelle.
"Nini shida?"
Alimshika mwanamke huyo kama mwanaye, akamlaza kifuani kwake.
"Umewaota tena? ... Pole. Usijali, mimi nipo hapa ... usijali, Mitchelle."
Mitchelle alitanua mikono yake akamkumbatia mwanamama Jennifer. Macho yake yalilenga chozi. Alipojibandua kwenye mwili wa mwanake huyo, alivuta vikamasi vyepesi puani akauliza, "Nimelala kwa muda gani?"
"Si muda mrefu sana," Jennifer akamjibu. Alikuwa anamtazama Mitchelle kwa macho ya mama zaidi kuliko yale ya mfanyakazi kwa 'boss' wake.
Mitchelle alisukumia shuka kando akatoka kitandani. Hakutaka kulala tena. Alitwaa taulo jeupe toka kabatini, akamtazama Jennifer ambaye bado alikuwa kitandani, akamuuliza,
"Ferdinand alikuja tena?"
"Hapana," Jennifer alijibu akitikisa kichwa. Alinyanyuka toka kitandani akaongezea, "Alipiga simu majira fulani kuulizia hali yako, nikamwambia umelala."
"Ok. Mimi natoka, siwezi kulala tena. Usingizi wote umeniisha. Tafadhali niandalie nguo yangu ya kutokea."
"Haina shida."
"Nguo ya usiku tafadhali."
"Sawa."
Jennifer alielekea kabatini kutimiza zoezi aliloagizwa wakati Mitchelle akijivesha taulo baada ya kuvua nguo yake ya kulalia ili apate kuoga.
Aliingia kwenye bafu lake kubwa, akaenda mahali mahususi kwa ajili ya 'shower'. Hapo akatundika taulo lake kando kisha taratibu akaanza kuupooza mwili wake na maji ya baridi ili kuondoa mang'amung'amu ya usingizi.
Mwili wake mwembamba ulikuwa na uwiano sahihi katika kila upande. Wakati huu akiwa anaoga ilikuwa ni fursa nzuri ya kushuhudia hilo. Alielekezea sura yake bombani maji yakitiririka toka kichwani mpaka miguuni.
Alishika nywele zake nyeusi, ndefu kwa wastani, akazipindulia begani kuja kifuani. Hapo akaaacha shingo yake kwa nyuma ikiwa wazi.
Chini kidogo ya shingo hiyo, kwenye makutano ya shingo na mgongo, kulikuwa na 'tattoo' ndogo ya mistari midogomidogo iliyosimama. Chini ya mistari hiyo kulikuwa na tarakimu kadhaa na herufi tatu;
00/89/31/12-CKM.
***
Masaa Mawili Mbele: Eneo la Manhattan, mbele ya baa ya kisasa ya The DL.
Mitchelle alishuka toka kwenye 'uber' iliyomleta punde tu baada ya kufanya malipo. Mara nyingi anapotoka nyakati za usiku, hupendelea kutumia usafiri wa kukodi kama wa namna hii.
Alikuwa amevalia suruali nyeusi ya jeans iliyombana, koti jeusi la ngozi lenye kola ndefu, ndani blauzi nyekundu yenye kumetameta, kapelo nyeusi na viatu vilivyopanda karibia na magoti.
Alitembea kufuata milango mipana ya kioo ya baa ya The DL huku akibofya simu yake kubwa. Alipoingia ndani alinyookea kwenye viti vinavyowakarimu wageni, haswa wanywaji, hapo akakutana na Ferdinand.
Mazingira ya hapa yalikuwa ni hafifu sana kwa mwanga. Inajulikana walevi hawapendi mwanga mkali wakiwa kwenye starehe zao hivyo taa zilizokuwepo hapa zilikuwa ni zile za urembo tu, nyekundu na bluu, zakuwafanya watu wasigongane kwa kutoonana kabisa.
"Umejuaje nipo hapa?" Ferdinand aliuliza baada ya kushusha glasi yake ya kinywaji chini. Mezani kulikuwa na chupa kubwa yenye kinywaji robo ujazo.
"Kwani wewe ni mgeni kwangu, Ferdy?" Mitchelle aliuliza. Kidogo naye aliletewa ulabu akaungana na Ferdinand kwenye unywaji.
"Nimeshindwa kulala. Kama ningebaki nyumbani huu usiku ungekuwa mrefu sana."
"Umeota tena?"
"Ndio."
"Ilikuwa mbaya kiasi gani?"
"Mbaya tu."
"Pengine unafikiria sana yaliyopita. Kuna muda inabidi uache yaende, Mitchelle. Ukifikiria sana, hautapata wasaa wa ya sasa."
Mitchelle alinyamaza. Aliacha kwanza mdomo wake unywe na kichwa chake kifikiri. Kwa muda wa kama dakika sita hivi kukawa na ukimya.
Ferdinand alimaliza ile chupa yame ya ulabu, akaagiza aletewe nyingine.
"Ferdy, hiyo ni ya ngapi? Huoni inatosha sasa?"
"Ndo' kwanza ya pili," alijibu mwanaume huyo akimtazama Mitchelle. Uso wake ulikuwa mchangamfu, macho yake yanang'aa na mwaga mwekundu wa baa.
Mitchelle hakutaka kubishana naye. Aliamua kuamini kile alichoambiwa. Lakini akifanya hilo kwa tahadhari.
"Vipi kwenye uchapishaji, kazi imeshaanza?"
"Ndio. Nilivyokuacha tu nyumbani nilipeleka ule mzigo akaanze nao ... lakini, Mitchelle?"
"Nini?"
"Kwanini uliamua hili jambo? Huoni ni hatarishi?"
"Jambo gani?"
"La kupeleka taarifa kama hizo sehemu kama ile?"
"Ferdinand, kanuni ya kuficha kitu inasemaje? ... ficha pale ambapo hamna anayepadhania. Unadhani kila kitu kikienda kombo, kuna sehemu yoyote ndani ya makazi yangu itakuwa salama? ... nilihitaji sehemu na watu ambao hawatafikiriwa KABISA hata pale adui yangu atakapowaza mara mia moja. Vitu hivyo vinapatikana nje ya mduara wangu wa maisha ya kila siku."
"Lakini mimi huwa naenda pale Olympus?"
"Ndiyo maana nilikuambia utafute njia mbadala. Weka mzigo mahali, mhusika aupitie. Makutano ya mara kwa mara yanaweza leta shuku."
"Lakini vipi kama taarifa hizi tungezitunza kwenye vyombo alafu tukavifukia ama kuviweka mahali pa mbali ambapo mtu hawezi fika kwa urahisi mfano kama vile visiwani huko au baharini au ..."
"Ferdy, umelewa?"
"Mie? Akha!"
"Mara ngapi tushawahi ongea hili? Hii ndo njia rahisi na salama ya kunakilisha taarifa nyeti. Haiwezi kufuatiliwa wala kuathiriwa na virusi maalum waliotengenezwa. Kwa muda wote huo Olympus itakuwa ni ghala letu la siri lisilodhaniwa, zoezi likikamilika tutakua tuna data kwenye kila mfumo wa uwasilishaji na kwenye lugha tatu za dunia. Hapo ndo tutaanza mapambano rasmi."
"Vipi kuhusu wale watu wa Olympus na unyeti wa taarifa zetu?"
"Unamaanisha Bryson?"
"Ndio."
"Ferdy, ni wewe ndiye uliyefanya utafiti wa kina kumhusu Bryson na kampuni yake. Sivyo?"
"Ndio, najua kila kitu kumhusu yeye. Njia anayopitia kutokea na kurudia nyumbani, anakula nini asubuhi mpaka jioni, mahali anapoishi, madeni aliyonayo, anapofanyia kazi mkewe, anapoishi mama yake, anapopenda kwenda kustarehe, mpaka hospitali na dozi ambayo watoto wake wanaitumia. Najua kila kitu."
"Na hivyo vyote unavyovijua ndo' dhamana ya kazi yetu. Hakikisha anajua hilo. Na punde kazi yetu itakapokwisha, kila mmoja aliyehusika nayo hakikisha anaiga dunia."
"Usijali."
Ferdinand alimalizia kisha akainyanyua chupa yake ya kilevi na kuinywa kwa mtindo wa tarumbeta. Aliona glasi inamchelewesha. Alibeua mara tatu alafu akanyanyuka.
"Naenda maliwato, nakuja," aliaga akaenda zake.
Mitchelle akamsindikiza kwa macho yake madogo mpaka alipotokomea. Kichwani mwake kuna mambo kadhaa alikuwa anayawazua.
"Sio kila kitu ni cha kujua kwa undani, Ferdy," alisema kifuani mwake. "Mengine acha yawe surprise. Maisha bila surprise yanaboa."
Alitabasamu mwenyewe mithili ya mtu anayejitazama kwenye kioo kisha akanyanyua glasi yake ya kilevi kikali akalipasha koo.
Kwasababu ya upweke huu wa dakika kadhaa, alipiga mikupuo mingi ya kileo. Alipokunywa kama glasi nne hivi bila ya Ferdinand kurudi, akapata walakini.
Alitazama njia aliyoendea nayo mwanaume huyo lakini hakumwona. Ni watu wengine tu ndo' walikuwa wanapita huku na kule wakiendelea na yao.
Alimalizia kinywaji chake akasimama. Kabla hajaenda popote, akaita 'uber' kisha akaiweka simu yake mfukoni.
--
Choo cha wanaume
Mlangoni kulikuwa na kibao cheupe kilichoandikwa 'occupied' kumaanisha kuna mtu ndani, lakini kama ungelisimama hapo, kwa mbali, ungelisikia maongezi yanayoendelea ni ya zaidi ya mtu mmoja. Moja ya sauti ilikuwa ni ya Ferdinand.
"Hauna mzigo mwingine?" Ferdinand aliuliza. Macho yake yalikuwa yamelegea mno. Pombe sasa ilikuwa imefika penyewe.
Mbele yake walikuwa wamesimama wanaume wawili waliovalia suti bubu; koti tu na mashati tofauti ndani. Mmoja alikuwa mwenye upara na masharubu makubwa, mwili wake mpana. Mwingine alikuwa mwembamba mfupi, nywele nyingi nyeusi, mwenye kujawa na michoro mingi shingoni.
Yule mwenye upara aliguna kwa kebehi.
Alimtazama Ferdinand kwa macho ya dharau kisha akamtazama mwenzake wakatabasamu pamoja.
"Toa pesa. Si unajua huu mzigo ni gharama kubwa?"
"Si nimeshawapa?" Ferdinand alifoka. Mbali na kwamba macho yake yalikuwa legevu, mwili wake haukuwa na nguvu tena. Alisimama akiyumba, mdomo ameuachama.
"Mnataka mamilioni ama? Enh! Mnataka mamilioniii?"
Puani, upande wake wa kushoto, alikuwa na mabakimabaki ya unga uliochora alama ya 'nike'. Sasa ilikuwa bayana kumbe mbali na pombe alokunywa, alikuwa pia yupo kwenye ulevi mwingine.
"Toa pesa. Kama huna acha kutusumbua, sawa?" Yule mwanaume mwembamba alifoka akimnyooshea kidole. "Hatuna muda wa kupoteza hapa. Ni aidha tufanye biashara au twende zetu. Tuna wateja wanatungoja!"
Yule bwana mwenye upara alitoa kifuko kidogo cha 'nylon' chenye unga mweupe, akamwonyeshea Ferdinand bila kusema jambo. Alitabasamu tu akiyakodoa macho. Aliutikisatikisa mkono wake wenye dawa kama bwana amfanyiavyo mbwa wake.
Ferdinand alitazama mkono huo kwa hamu. Alijipapasapapasa mifukoni lakini hakuwa na kitu tena. Pesa yote imeshakwisha.
Hawajakaa sawa, mlango ukagongwa kwanguvu, BAM-BAM-BAM! Wote wakatazama kwa hamaki.
"Huoni kuna watu!" Bwana upara alifokea mlangoni. "Nenda vyoo vingine kabla sijaja hapo kukung'oa meno!"
Ajabu mlango uligongwa tena. Mara hii aliyekuwa anagonga alifanya hivyo mfululizo bila kukoma!
Bwana upara alimtazama mwenzie akampa ishara ya kichwa. Yule mwenzake akasonga mbele kuufuata mlango. Aliposhika tu kitasa, hakujua nini kilichojiri. Kitu pekee alichokumbuka ni kuruka juu baada ya kugongwa na kitu kizito kifuani.
Alijitambua yuko chini hajiwezi. Kichwa chake kinavuja damu.
"Alaa!!" Bwana upara alistaajabu. Aliyatumbua macho yake haswa. Alirudisha macho yake mlangoni akamwona mwanamke akiwa amesimama papo. Alikuwa ni Mitchelle.
Mlango ulibakia nusu, kipande kingine kinaning'inia kando.
Ilikuwa ni ajabu kuona mwanamke, tena wa umbo lile dogo, ndiye aliyefanya hayo. Hata bwana upara hakuamini hilo. Alidhani pengine kuna watu wa ziada pamoja naye lakini haikuwa hivyo.
Kilichofuata baada ya dakika tano ni yeye kuungana na mwenzie chini. Hajielewi. Kichwa chake kimekuwa chekundu.
"Ferdinand, tulikubaliana nini kuhusu madawa?" Mitchelle aliuliza kwa ukali. Macho yake madogo yalimezwa na ndita za usoni. Kwa muda wote huo Ferdinand alikuwa amesimama akinyoosha mikono juu kama mtu aliyenyooshewa bunduki.
Kwa kumtazama tu, ungembaini sio mzima.
Muda mfupi mbele Mitchelle na Ferdinand wakawa wako ndani ya 'uber' wakielekea nyumbani. Sura ya Mitchelle ilikuwa imefura. Alikuwa akitazama nje kupitia dirishani.
Ferdinand yeye hakuwa na hili wala lile kwani ufahamu haukuwa pamoja naye.
Ndani ya muda mfupi polisi wakawa wamefika katika eneo la The DL. Magari mawili yanayowaka taa nyekundu na bluu yalitema polisi watatu kwa idadi, wakazama ndani kuhakiki taarifa walizopewa kuhusu mashambulizi.
Muda si mrefu polisi hao waliungana na polisi wengine wa nyongeza walioambatana na wanakitengo cha habari walioharakisha kuchukua taarifa za picha mnato kwaajili ya kusaidia upelelezi.
Miongoni mwa polisi hao waliofika hapa, alikuwa ni bwana huyu mrefu, mwili mpana, aliyevalia shati maridadi jeupe la mistari, kachomekea vema ndani ya suruali yake nyeusi na mgongo wake umefunikwa na koti refu kwa wastani, rangi ya kahawia iliyokoza, kifuani amening'iniza beji ya nembo ya polisi kilichoandikwa:
NEW YORK POLICE DEPARTMENT (KITENGO CHA POLISI NEW YORK)
DETECTIVE (MPELELEZI)
005789.
Tayari eneo la tukio lilishazungushiwa utepe wa polisi. Hakuruhusiwa raia kuingia eneo hilo isipokuwa wanausalama pekee.
Bwana huyo alisogea eneo hilo kwa hatua zake za wima. Alingia moja kwa moja mpaka maafa yalipojiri, akatazama miili miwili iliyokuwa imelala mfu.
Aliikagua miili hiyo kwa kitambo kidogo kisha akamuuliza moja wa mapolisi waliowahi eneo la tukio.
"Umesema ni mtu mmoja ameyafanya haya?"
"Ndio, afande. Ni mwanamke mmoja."
"Mwanamke?"
"Ndio. Kamera za koridoni zilimwonyesha mtu mwenye umbo la kike akija upande huu wa vyoo."
"Zimekamata sura yake?"
"Hapana. Alikuwa amevaa kofia."
"Usafiri?"
"Hakuja na usafiri. Kamera zinamwonyesha aliingia na gari ya kukodi."
"Mmelitambua gari hilo?"
"Hapana. Alishukia mbali kwa kamera kukamata picha vema."
"Hapana!" Bwana yule aling'aka akitoka katika eneo la tukio. Polisi aliyekuwa anaongea naye akamfuata nyuma kama mkia. "Haiwezekani, lazima kuwe na kitu!"
Walifika nje, hapo wakasimama bwana yule akiyakagua mazingira.
"Shida mwanga ulikuwa hafifu sana alipokaa," aliongezea yule polisi. "Ni ngumu sana kuona sura ya mtu vizuri, na kwa vielelezo vile inaonekana ulikuwa ni ugomvi wa madawa ya kulevya."
Mara yule bwana mpelelezi alinyooshea kidole barabarani. "Kule hakuna kamera iliyonasa gari hilo?"
"Hapana, mkuu," polisi aliwahi kujibu. "Kamera inayofanya kazi ipo kilomita tatu kutoka hapa. Kutambua gari itachukua muda kidogo."
"Shit!"
"Lakini kuna mtu alinaswa na kamera."
Bwana mpelelezi alimtazama mwenziwe kwa macho ya hamu, akamuuliza;
"Nani huyo?"
"Mwanaume fulani aliyekuwa na mwanamke huyo."
"Kwanini hukuniambia mapema yote?"
"Niliona ina msaada kidogo."
"Unamaanisha nini?"
"Picha ya bwana huyo ilishatumwa makao kwaajili ya utambuzi lakini hamna kilichopatikana."
"Kivipi?"
"Picha yake imeingizwa katika mfumo wa kutambua vitambulisho vya taifa na vyote vile vilivyo rasmi lakini hakuna rekodi yeyote ile inayomhusu. Hakuna taarifa yake yoyote rasmi. Si anwani, taaluma, kazi wala miamala!"
Bwana mpelelezi akatabasamu asijue hata cha kufurahisha ni nini. Alitafakari hapo kwa muda kidogo kabla hajaamua kurudi tena ndani. Kule sehemu lilipojiri tukio.
"Naomba kila kitu! .. kila kitu kinachohusu kesi hii!"
Alipayuka.
**
Queens, New York. Olympus Printing Press
Saa nne asubuhi.
"Hildaa!" Sauti ya Bryson iliitia ndani. "Njoo upesi, tafadhali."
Hilda aliyekuwa amekalia kazi yake ya kuchapa alinyanyuka upesi kwenda kuonana na mkuu wake wa kazi. Kama ilivyo ada, alikuwa nadhifu kwa sketi zake fupi na viatu vyake visivyo na purukushani.
Kwa ufupi mwanamke huyo alishajijua aende vipi na mwili wake wenye utajiri wa nyama. Kipi aonyeshe, kipi afiche. Kipi avae, kipi aache.
Aliingia ofisini akasimama kwa nidhamu kabla hajaruhusiwa kuketi kitini.
Bryson alikuwa amevalia shati alilofungua vifungo viwili vya juu. Uso wake ulikuwa mzito na macho yake mekundu kama nyanya zilizooza. Kila saa alikuwa akipiga mihayo akitazama kwa huruma.
Hilda alimtazama 'boss' wake namna alivyokuwa anapangilia mafaili kivivu. Alitamani kumuuliza nini kimemsibu lakini alikosa pa kuanzia.
"Hilda, katika siku ambazo nimeteseka, jana ilikuwa mojawapo!" Bryson aliongea kidogo kisha akafikicha macho yake. Yalikuwa yanamuuma kwa kujawa na usingizi.
"Usiku mzima sijalala kabisa, nipo huku na kule natafuta nilipoweka flash ya watu ya kazi. Aisee! Mungu tu ndo' anajua."
"Pole, boss. Kwani ilikuaje?" Hilda alipata pa kuanzia kuikata kiu yake.
"We acha tu! Hizi sigara zitakuja kuniua siku. Kutafuta koooote hukoo, unajua nikaja kuipatia wapi? ... nashangaa natoa sigara nivute, naiona kwenye pakti. Sijui hata ilifikaje? Yani sijui!'
Hilda alitamani kweli kutabasamu lakini alivumilia.
"Pole sana, boss."
"Laiti nisingeipata," Bryson aliendeleza maneno, "sijui ningekuja kuwaambia nini wale mabwana?"
"Ni wale ulioniambia?"
"Ndio. Yani wale sitaki nao mchezo kabisaa. Anyways, shika hii flash, sijaifungua hata kidogo. Najua hamna kazi nitakayoifanya humo. Nimechoka mno. Sasa fanya kuandika yaliyomo humo, sawa? ... achana na kazi zote fanya hiyo!"
Hilda alipokea flash akasimama.
"Utakapomaliza, utanambia. Pesa yako nzuri sana ipo. We hakikisha unaifanya kazi kwa stadi na siri."
"Haina shida, boss."
Hilda alitoka akaekelekea kwenye kiti chake. Cha kwanza kabisa alichomeka flash aliyopewa, akaifungua. Mbali na kwamba ilikuwa ni kazi, alikuwa na hamu kubwa ya kujua yaliyomo ndani.
Taarifa alizopewa na boss wake kuhusu kazi hiyo hakika zilimpatia hari kubwa ya udadisi. Kwake ilikuwa ni kazi ya kipekee.
Alitengenezea miwani, akatumbua macho akisoma kila jambo aliloliona. Taratibu na kwa umakini. Akili yake yote ilizamia humo. Hakusikia wala kuona kingine chochote nje ya tarakilishi ya kazi yake. Alikuwa yupo kwenye ulimwengu wa peke yake.
Lakini ghafla alisikia sauti inamnong'oneza;
"Ni ... nni ...n ... nini hiki, Hilda?"
Alikurupuka mithili ya mbwa aliyeona chatu! Kutazama ni Richie. Upesi akafunga tarakilishi yake.
"Umeona chochote?" Alimuuliza Richie akiwa ameyatoa macho yake ndani ya miwani.
Richie akatikisa kichwa kukubali.
"Ndio."
***